Ondoa magugu kwa uangalifu shambani kwako

Uzalishaji wa mazao

Ujumbe kwa mtangazaji

Wanawake wakulima wanaokusikiliza watafurahishwa na kipindi hiki kinachoelezea jinsi ya kudhibiti mbigili shambani. Magugu aina ya mbigili ni moja kati ya shughuli zinazowamalizia wanawake muda mwingi shambani, ambapo mamilioni ya wanawake wa kiafrika hulazimika kushinda shambani wakifanya kazi hii.

Moja kati ya mbinu za kudhibiti mbigili shambani ni kuzing’oa. Hata hivyo, kwa sababu mbegu za mbigili ni ndogo sana, zinasambaa na kuongezeka kwa haraka. Njia madhubuti ya kuyadhibiti magugu haya ni kwa wakulima kuelewa jinsi magugu hayo yanavyojizalisha na kusambaa shambani. Muswada huu utaelezea umuhimu wa kung’oa magugu aina ya mbigili shambani na kuyaondoa shambani ili kupunguza uwezekano wa kuyafanya yasambae na kuwa kero. Hakikisha unakitangaza kipindi hiki wakati ambapo wanawake wanakuwa tayari wamesharejea nyumbani. Unaweza ukabadilisha jina hili la mbigili, kwa jina la magugu yanayofahamika vizuri katika eneo lako.

Muswada huu unaweza kuwa wakufikirika kama vile mchezo mdogo wa kuigiza. Unaweza kutumia muswada huu kuhamasisha utafiti na kuandika muswada unaofanana na mazingira uliyopo. Unaweza pia kuamua kuutumia muswada huu katika kituo chako cha redio, ukitumia sauti za waigizaji kuwakilisha wazungumzaji wakuu.

 

Script

Washiriki:
Mtangazaji
wakulima wawili wanawake

Mtangazaji:
Wakulima wengi wanaonisikiliza leo, hasa wanawake, bila shaka watafurahia mjadala wetu wa leo wa jinsi ya kudhibiti mbigili shambani. Mbigili ni magugu yanayosababisha uharibifu mkubwa kwa mazao hasa mahindi, mtama, ufuta na hata mpunga. Magugu haya yana tabia ya kunyonya maji ardhi pamoja na virutubisho vingine na kuyaacha mazao yakiwa hayana kitu. Wakulima wanatumia muda mwingi kuyang’oa magugu haya shambani, lakini kama ukijifunza mbinu bora ya kudhibiti mbigili, hutakuwa na sababu ya kutumia muda mwingi kuzing’oa shambani. Kwa taarifa zaidi endelea kusikiliza…

Muziki wa ala (sekunde tatu)

Mwanamke mkulima 1:
Habari rafiki. Ni mshangao ulioje! Sijakuona siku nyingi … Nilikuwa nimeanza kuwa na wasiwasi …

Mwanamke mkulima 2:
Oh! Huna sababu ya kuwa na wasiwasi. Tatizo ni kwamba sina muda wa kutosha kutoka nje siku hizi. Hivi sasa ninaishi na watoto wa dada yangu, na katika kipindi hiki cha mwaka kuna magugu mengi sana ambayo ni lazima nipambane nayo shambani! Wakati mwingine nalazimika kutumia siku nzima niking’oa mbigili katika shamba langu la mahindi!

Mwanamke mkulima 1:
(Mguno) Ohhh! Naelewa. Mbigili ni magugu yanayosumbua sana!

Mwanamke mkulima 2:
Kwa maana hiyo una tatizo kama la kwangu?

Mwanamke mkulima 1:
Zamani nilikuwa nalo. Lakini hivi sasa limekwisha. Nilijifunza mbinu za kufanya magugu hayo yasisambae shambani. Hivi hukumbuki wakati ule wale mawakala wa kilimo walipokuja hapa kuzungumza nasi kuhusiana na magugu?

Mwanamke mkulima 2:
Ndiyo. Nilifuata maelekezo ya Yule wakala. Lakini … bado magugu yako kila mahali.

Mwanamke mkulima 1:
Hmmm. Vizuri, nitakueleza kile mimi ninachofanya. Lakini, kwa nini usinieleze kwanza mbinu unazotumia?

Mwanamke mkulima 2:
Kwanza nayang’oa magugu kwa mikono, halafu nayachoma moto.

Mwanamke mkulima 1:
Kung’oa mbigili kwa mikono ni vizuri tena ni muhimu. Lakini unafanyaje baada ya kung’oa mbigili na kuzichoma moto?

Mwanamke mkulima 2:
Huwa ninazilaza kwenye mistari ya mahindi yangu shambani.

Mwanamke mkulima 1:
Aha! Nadhani hilo ndio tatizo lako la kwanza. Unapozilaza mbigili katika mistari ya mahindi shambani, zinakuwa zikidondosha mbegu kwenye udongo. Mwaka unaofuata zinakuwa zimezaliana kwa wingi, hivyo tatizo linakuwa kubwa zaidi.

Mwanamke mkulima 2:
Unamaanisha nising’oe magugu?

Mwanamke mkulima 1:
Hapana, simaanishi hivyo – kwanza unatakiwa ung’oe mbigili zote. Lakini ni vizuri kuzing’oa mara unapoona zimetoa maua – kabla hazijatoa mbegu. Kama utazing’oa mapema kabla hata hazijatoa maua, zitaanza kuzaliana na unaweza ukajikuta una magugu mengi shambani kuliko yale ya kwanza.

Zivute kwa uangalifu ili shina lisikatike. Usizilaze kwenye ardhi. Mara unapozing’oa, zitie kwenye mfuko wa plastiki, halafu nenda ukazichomee nje ya shamba. Kama utaziweka ardhini, mbegu zake zitaanguka kwenye udongo na kuendelea kuzaliana.

Mwanamke mkulima 2:
Napenda kukiri kuwa hata sjawahi kuona mbegu zake!

Mwanamke mkulima 1:
Najua … mbegu zake ni ndogo sana, kiasi kwamba inakuwa vigumu kuziona. Ni ndogo kama mavumbi. Lakini zina madhara ya ajabu, ndio maana inabidi uwe makini. Zinaweza kutulia ardhini kwa miaka mingi. Baadaye, kwa muda ambao hukutarajia – mbegu zinaanza kutoka. Mara nyingi zina tabia ya kujizalisha zinapoona kuwa ziko karibu na mizizi ya mazao shambani ili ziweze kujilisha hapo. Hasa katika mazao kama ufuta, mtama na mahindi. Mbigili zina tabia ya kujitengenezea mizizi mirefu inayokwenda ardhini na kunyonya virutubisho vyote ikiwa ni pamoja na maji. Hii ndiyo sababu mahindi yako, ufuta na mtama inakonda na kushindwa kutoa mazao bora.

Mwanamke mkulima 2:
Vizuri, nafurahi nimekimbilia kwako leo! Kuanzia leo litazing’oa mbigili kwa uangalifu – na mwisho nitaachana na adha hiyo…

Ingiza muziki uache uendelee kucheza

Mtangazaji:
kung’oa magugu kwa mkono ni moja kati ya hatua muhimu za kudhibiti mbigili shambani. Hakikisha unang’oa mbigili shambani mara zinapoanza kutoa maua – la sivyo zitazalisha mbegu nyingi zaidi. Kama utafuata utaratibu huu magugu hayawezi kuenea hovyo shambani kwako. Vuta kwa uangalifu na hakikisha haikatiki. Weka mbigili kwenye mfuko wa plastiki, zitoe nje ya shamba na kuzichoma mara moja.

Napenda kukumbusha kuwa, hata kama ukifuata hatua hizi, usije ukashangaa kuona kuwa msimu ujao bado ukawa na mbigili shambani kwako. Hii ni kwa sababu mbegu za mbigili zinaweza kulala usingizini ndani ya ardhi kwa miaka mingi bila kuota, halafu zikaota baadaye. Kwa hiyo ni vizuri kuendelea kuzing’oa, kama utaacha kuzing’oa hata kwa msimu mmoja, basi itakubidi kuanza tena upya zoezi hili.

Jambo la kuzingatia ni kwamba, zoezi la kung’oa mbigili peke yake halitoshi kuangamiza magugu haya shambani. Njia bora ni kutumia njia mchanganyiko za kuyadhibiti ikiwa ni pamoja na kilimo mchanganyiko na tabia ya kubadilisha mazao shambani ikiwa ni mazao yanayoweza kuhimili hali zote. Ni vema pia ukatumia mbolea kurutubisha mazao yako. Mazao yenye afya yanaweza kuhimili magugu. Tutaendelea kuzungumzia mbinu hizi katika vipindi vyetu vijavyo (kesho, wiki ijayo, _________). Asante kwa kutusikiliza.

Acknowledgements

Wachangiaji: Jennifer Pittet, Mtafiti/Mwandishi, Thornbury, Canada.

Imepitiwa na : Aad van Ast, Idara ya Sayansi Mimea, mazao na kikundi cha uoto wa magugu na mazao, Chuo kikuu cha , Haarweg 333, 6709 RZ Wageningen, Uholanzi

Information sources

Macpherson, George. “kupambana na magugu kwa kutumia elimu.” Ulimwengu wa Kilimo. Number 1815, Feb. 1994.

Pittet, Jennifer. Mbinu mchanganyiko za kupambana na mbigili. Toronto: nchi zinazoendelea, mtandao wa Farm Radio, Package 32, Script 5, April 1994.