Wanawake wanajiwezesha: Mchezo kuhusu wanawake kulima na kuuuza maharage — Part 5

Usawa wa kijinsiaUzalishaji wa mazao

Ujumbe kwa mtangazaji

Nukuu kwa Waandishi wa Habari
Wakina dada wanafanya wenyewe haya ni maigizo yenye sehemu-tano inayoongelea kikundi cha wanawake wanaokabiliana na chagamoto za kujikwamua na kupata maendeleo. Wanawake hawa ni wanachama wa vikundi vya kuweka na kukopa au vicoba nchini Tanzania, na wote wanalima maharage. Wanawake wanafanya kazi nyingi zaidi katika shughuli za uzalishaji wa maharage. Lakini kwasababu ya utamaduni wao wa kimajukumu katika jamii, wanaume wanafanya maamuzi yote baada ya mavuno, ikiwemo kuuza maharage na kumiliki kipato.

Baathi ya wahusika katika maigizo, ni mama Farida na Mama Mjuni, ambao wameonekana kuongoza katika kujaribu kufanya tofauti. Wanawahimiza wanawake kufanya kazi pamoja katika mashamba yao, na mwishowe kuzalisha maharage pamoja na kutafuta masoko kama kikundi.

Soma wahusika wakuu

Maigizo yanapinga hali mbaya, ikiwemo ugomvi baina ya mwanamke na mwanaume: unyanyasaji wa nyumbani katika familia moja, na juhudi za jamii kuwatumia wanawake vibaya na kujipatia faida kutokana na shughuli za kijangili.

Kuna utani kidogo katika maigizo, ingawa inaongelea mandhari nzito. Ukitengeneza maigizo na kikundi, hakikisha kuwa sehemu zenye mada nzito zinaoanishwa na sehemu zenye mada nyepesi za kufurahisha, za marafiki wakinongoneza matukio mazuri na wakicheka.

Kila kipengele kina urefu wa kama dakika 20-25, ikiwemo muziki wa kianzia na kumalizia. Kwasababu vipengele ni virefu, unaweza kupanga kurusha vipengele (kipande kimoja wapo katika Igizo) viwili au vitatu tu katika kipindi chako. Kwa mara nyingi vipande viwili au vitatu vinachukua dakiak 6-8.

Unaweza kupata mrejesho wa maigizo kwa kuandaa kipondi kitakacho pokea simu ambazo wasikilizaji watajadili baathi ya mambo waliyoyasikia katika maigizo, waalike wataalamu wa kike na wakiume kujadili mada. Majadiliano yanaweza kujumuisha:

  • jinsi jamii inavyogawanya kazi za kuzalisha na kuuza maharage, au mazao mengine yanayolimwa katika eneo, na jinsi gani mgawanyo huu umetenga mahitaji ya wanawake, na hata inaweza kuathiri familia;
  • unyanyasaji majumbani na utamaduni au tabia za ukimya inayoruhusu hii kuendelea; na
  • aina ya msaada wanaume wanayoweza kuwapatia wanawake ambao wanahangaika kujisaidia wao na famila zao.

Script

1.
Scene 1
2. Sehemu:
Nje. Gala la Sigi. Asubuhi.
3. Utambulisho wa kipengele:
Mazingira ya gala.

4. Wahusika:
Sigi, Afande Kaifa, Afande Filipo, Mkulima.

5. SIGI:
Nakuhakikishia hautapata dili nzuri kama hii!
6. MKULIMA:
Acha hizo Sigi! Hiyo hela ndogo sana kwa magunia yote haya!
7. SIGI:
Hiyo ndio ofa yangu ya mwisho! Kwa hiyo unaweza kukubali au ukaacha.
8. SFX:
INJINI YA PIKIPIKI.
9. SIGI:
Oh! Afande Kaifa! Karibu bwana! Nikusaidie na nini? Usiniambie una mzigo mwingine wa maharage! (ANACHEKA)
10. AFANDE KAIFA:
Nahitaji uje na mimi kituoni.
11. SIGI:
(KWA MSHTUKO) Kituo cha polisi? Kufanya nini?
12. AFANDE FILIPO:
Usiulize maswali mengi; wewe fanya kama ulivyoambiwa.
13. SIGI:
Inabidi niulize kuna nini? Kwanza wewe nani kuniamrisha? Unajua unaongea na nani? Kwanza mimi naongea na bosi wako!
14. AFANDE KAIFA:
Ni kweli una haki ya kujua kwamba upo chini ya ulinzi kwa kujaribu kusababisha uharibifu wa shamba la wanawake wa vikoba.
15. SIGI:
(KWA MSHANGAO) Nini? Mbona sielewi?
16. AFANDE FILIPO:
Tunajua kuhusu mipango yako ya kutaka kuharibu shamba la wanawake wa vikoba.
17. SIGI:
Afande Kaifa, unajua kabisa huu ni uongo mtupu! Unanijua mimi, siwezi kufanya huo upuuzi! Najua watu wamenitengenezea tu ili kuchafua jina langu, watu wananionea wivu!
18. AFANDE KAIFA:
Twende Sigi! Utajitetea kituoni!
19. SIGI:
Kaifa ndugu yangu si unaona nipo kwenye mazungumzo ya kibiashara hapa. Nakuomba ndugu yangu, tumefanya biashara nyingi sana na tumejuana muda mrefu. Nakuomba nimalize mazungumzo yangu alafu nitakuja kituoni.
20. AFANDE KAIFA:
Haitawezekana Sigi.
21. SIGI:
(KWA HISIA) Nakuomba rafiki yangu, Mimi na wewe hatujaanza kujuana leo…Mara ngapi nimekupa ofa nzuri kwa maharage yako eh?
22. AFANDE KAIFA:
Mara nyingi nakubali. Lakini hili suala halihusiani na biashara! Lazima nifanye kazi yangu kwa sasa ambayo ni kukupeleka kituoni kwa ajili ya maswali.
23. SIGI:
(KWA USHAWISHI) Acha mambo yako Kaifa! Hakuna haja ya yote hayo; haya ni mambo madogo sana. (ANACHEKA) Mimi najua tutamaliza vipi.
24. AFANDE KAIFA:
Unajaribu kusemaje?
25. SIGI:
Si unajua ule msemo wa zamani unavyosema- nisaidie na mimi nikusaidie.
26. AFANDE KAIFA:
(KWA UKALI) Unajaribu kunipa hongo?
27. SIGI:
(KWA UOGA) Hapana! Hapana! Sio hivyo!
28. AFANDE KAIFA:
Unajua nitakuongezea kosa la kujaribu kumuhonga mkuu wa polisi.
29. SIGI:
(AKIOMBA KWA UPOLE) Hakuna haja ya yote hayo.
30. AFANDE KAIFA:
Haya twende kituoni mara moja la sivyo nitamwambia Afande Filipo hapa atumie nguvu.
31. SIGI:
(KWA UOGA) Hakuna haja ya kutumia nguvu sawa? Tunaenda.
32. AFANDE KAIFA:
Haya panda kwenye pikipiki.
33. SFX:
SIGI ANAPANDA KWENYE PIKIPIKI NA KUWASHA INJINI.
34. MKULIMA:
(KWA UOGA) Vipi kuhusu mimi kiongozi? Mnaondoka wakati hatujamaliza kuongea biashara.
35. AFANDE KAIFA:
Kutakuwa hakuna biashara hapa leo, labda kama unateka kuenda kumalizana nae kituo cha polisi.
36. MKULIMA:
(KWA UOGA) Hapana kiongozi.
37. SFX:
AFANDE KAIFA ANAWASHA PIKIPIKI NA KUONDOKA.
38. CONTROL:
fande Kaifa

 

39.
Scene 2
40. Sehemu:
Ndani. Kituo cha polisi. Asubuhi.
41. Utambulisho wa kipengele:
Mazingira ya kituo cha polisi.

42. Wahusika:
Sigi, Adam, Alex, Afande Kaifa, Afande Filipo, Mjuni.

43. SFX:
MLANGO UNAFUNGULIWA, SIGI, AFANDE KAIFA NA AFANDE FILIPO.
44. AFANDE KAIFA:
Kaa chini.
45. SFX:
SIGI ANAVUTA KITI NA KUKAA CHINI.
46. SIGI:
Haina haja ya mambo yote haya, eeh.
47. AFANDE KAIFA:
Ebu niambie kitu gani kilikufanya utake kusababisha uharibifu kwenye shamba la wanawake wa vikoba? Kwani wao walikufanya nini?
48. SIGI:
Sijui ni nani aliyekuambia huo upuuzi, lakini narudia tena… mimi sina hatia.
49. AFANDE KAIFA:
Kwa hiyo unataka kuniambia kwamba hukuwalipa watoto wa mama K kufanya hiyo kazi?
50. SIGI:
(KWA MSHANGAO) Nini? Unanipa shutuma gani hizo? Kusema kweli, nimesikitishwa sana na wewe, Kaifa.
51. AFANDE KAIFA:
Tuna mashahidi ambao wapo tayari kutoa ushahidi juu yako.
52. SIGI:
(KWA UKALI) Sijali kuhusu hao mashahidi wako! Nimeshakwambia sina hatia! Huku ni kupotezeana muda, nina vitu muhimu vya kufanya.
53. AFANDE KAIFA:
Kwa hiyo bado unakataa?
54. SIGI:
Ndio nakataa! Kwa hiyo unishtaki au uniachie.
55. AFANDE KAIFA:
Basi sina budi bali kuwaleta mashahidi wangu. (ANAMGEUKIA AFANDE FILIPO) Afande Filipo walete mashahidi.
56. AFANDE FILIPO:
Sawa bosi.
57. SFX:
AFANDE FILIPO ANATOKA NJE ILI KUWALETA MASHAHIDI.
58. AFANDE KAIFA:
Naona unafanya mambo yawe magumu! Unajiona mjanja sana eh? Hata mimi mjanja.
59. SFX:
MLANGO UNAFUNGULIWA NA AFANDE FILIPO ANAINGIA NA ADAM, ALEX NA MJUNI.
60. SIGI:
(KWA MSHTUKO) Adam?!…Alex!
61. AFANDE KAIFA:
Hukudhani kwamba ingekuwa wao sio? Vijana wako wameamua kukugeuka.
62. SIGI:
(KWA UKALI) Nyie wapuuzi!
63. SFX:
SIGI ANAJARIBU KUWARUKIA.
64. AFANDE KAIFA:
Afande Filipo ebu mkamate!
65. SFX:
AFANDE FILIPO ANAMKAMATA SIGI NA KUMKALISHA CHINI.
66. AFANDE FILIPO:
(KWA UKALI) Kaa chini!
67. SIGI:
Siamini kama mmeamu kufanya hivi- baada ya yote niliyowafanyia. Haya ndio malipo yangu? Kwa kunigeuka?
68. ADAM:
Tumechoka tabia yako ya kutupelekesha ovyo na kutuamrisha kila saa! Kwa hiyo tukafikiria kwamba ukiwajela hutoweza kufanya hivyo.
69. SIGI:
(ANAINUKA KWENYE KITI KWA HASIRA) Nyie wapuuzi! Nitawaua!
70. SFX:
AFANDE FILIPO ANAMZUIA SIGI.
71. AFANDE KAIFA:
(KWA HASIRA) Ebu kaa chini, bwana Sigi! Tayari upo kwenye matatizo makubwa. (ANAWAGEUKIA AKINA ADAM) Ebu niambieni vijana: ni nani aliwatuma kuenda kusababisha uharibifu kwenye shamba la wanawake wa vikoba?
72. WOTE:
(KWA PAMOJA) Ni Sigi!
73. AFANDE KAIFA:
Kwa hiyo uanona bwana Sigi, vijana wote wanasema wewe ndio uliyepanga mipango yote. Kazi nzuri sana vijana, nadhani sasa muda umefika kwenda kuwaambia wanawake wa vikoba.
74. CONTROL:
Afande Kaifa.

 

75.
Scene 3
76. Sehemu:
Nje. Shambani kwa Mama Mjuni. Jioni.
77. Utambulisho wa kipengele:
Wanawake wanalima shambani.

78. Wahusika:
Afande Kaifa, Mama Mjuni, Mama K, Grace, Doris, Afande Filipo.

79. SFX:
WANAWAKE WANAIMBA HUKU WAKIIMBA.
80. WOTE:
(WANAIMBA) Wanawake wenzangu tuungane kwa pamoja ili tulime mashambani! Tufanye kazi kwa pamoja ili tubadilishe maisha yetu nay a familia zetu.
81. SFX:
PIKIPIKI INAKARIBIA.
82. SFX:
WANAWAKE WANAACHA KUIMBA GHAFLA.
83. GRACE:
Sio Afande Kaifa yule?
84. MAMA MJUNI:
Ndio yeye. Sijui anakuja kufanya nini?
85. DORIS:
(KWA WASI WASI) Mungu wangu mama Mjuni! Farida hayupo! Tutamuambia nini?
86. MAMA MJUNI:
(KWA SAUTI YA CHINI) Nyie tulieni! Mimi nitaongea nae.
87. WOTE:
Sawa.
88. MAMA MJUNI:
(KWA SHAUKU) Za kwako Afande Kaifa! Tukusadie na nini?
89. AFANDE KAIFA:
(AKIKARIBIA KIC) Za mchana jamani.
90. WOTE:
Nzuri.
91. AFANDE KAIFA:
Nipo hapa kwa sababu nina habari nzuri na habari mbaya.
92. MAMA K:
(KWA SHAUKU) Kuna nini?
93. AFANDE KAIFA:
Habari mbaya ni kwamba kuna mtu alijaribu kusababisha uharibifu kwenye shamba lenu….
94. MAMA MJUNI:
(ANAMKATISHA) Kuharibu shamba letu? Nani?
95. DORIS:
(ANAINGILIA) Ndio, nani alitaka kufanya hivyo?
96. MAMA K:
(ANAINGILIA KATI) Itabidi utuambie…
97. AFANDE KAIFA:
(ANAJARIBU KUWATULIZA) Sawa basi akina mama naomba tusikilizane…
98. SFX:
UKIMYA.
99. AFANDE KAIFA:
Habari nzuri ni kwamba tumeshamkamata mtu mwenyewe.
100. GRACE:
(ANAINGILIA) Ni mwanaume?
101. MAMA MJUNI:
Kwani ni nani?
102. AFANDE KAIFA:
Ni Sigi!
103. MAMA K:
(ANASHTUKA) Sigi?!
104. GRACE:
(ANARUKA) Nilijua tu!
105. DORIS:
(KWA KUCHANGANYIKIWA) Nini?
106. MAMA MJUNI:
(KWA HASIRA) Yule mpuuzi! Subiri nimkamate! Nitamuua!
107. GRACE:
Kwani tusiende ofisini kwao?
108. AFANDE KAIFA:
Akina mama naomba msichukue sheria mikononi. Hivi tunavyoongea, yupo chini ya ulinzi kwa hiyo achene sheria ifuate mkondo wake.
109. MAMA MJUNI:
(KWA HISIA) Ndio mfungeni tu!
110. DORIS:
(KWA HASIRA) Anastahili kufungwa jela!
111. GRACE:
(ANAINGILIA KATI) Bila ya shaka atakuwa na hatia tu.
112. MAMA K:
(ANAINGILIA KATI) Hapana! Sidhani kama Sigi ana hatia! Ni mteja wangu mkubwa!
113. MAMA MJUNI:
(KWA MSHANGAO) Mama K, sitaki kuamini! Tupo hapa tukipewa habari na Afande Kaifa kuhusu Sigi kutaka kuharibu shamaba letu lakini wewe unafikiria bar yako tu?!
114. MAMA K:
Ndio, hana hatia! Kwanza kwanini aharibu shamba letu wakati amejaa mapesa yote yale! Kila akija kwangu huwa anafunga bar. (ANAANZA KULIA) Nani atanunua vinywaji?
115. GRACE:
Mama ebu acha utani! Sigi ana hatia; si umemsikia Afande Kaifa hapa.
116. MAMA MJUNI:
Mimi ninachojiuliza: Mmemkamata vipi?
117. AFANDE KAIFA:
Kuna vijana walitupa taarifa.
118. MAMA MJUNI:
Vijana gani?
119. AFANDE KAIFA:
Vijana wake mama K na mwanao.
120. MAMA MJUNI:
(KWA MSHTUKO) Nini? Mwanangu kaanza lini kukaa na wale wahuni?! We subiri nifike nyumbani leo! Atajuta siku aliyozaliwa.
121. MAMA K:
Kwa hiyo wanangu ndio wahuni eeh?
122. AFANDE KAIFA:
(INTERVENES) Akina mama! Nawaomba mtulie tafadhali! Inabidi mfurahi watoto wenu wameamua kufanya kitu kizuri kwa kutuletea taarifa kituoni. Sigi alijaribu kuwalipa ili wasababishe uharibifu shambani kwenu lakini wakamgeuka.
123. MAMA MJUNI:
Ni kweli lakini. Wamefanya kitu kizuri sana.
124. AFANDE KAIFA:
Unajua nimekuwa nikiangalia angalia, nikagundua Farida hayupo hapa.
125. MAMA MJUNI:
(KWA KUJISHTUKIA) Oh, alisema anarudi nyumbani kuangalia watoto.
126. AFANDE KAIFA:
(ANAHISI KITU) Ahaaa!
127. GRACE:
Ni kweli, alisema hivyo.
128. AFANDE KAIFA:
Sawa jamani endeleeni na kazi. Acha mimi niwaache.
129. MAMA MJUNI:
Asanteni sana kwa kumkamata yule jangiri.
130. AFANDE KAIFA:
Sawa, kwa heri!
131. WOTE:
Kwa heri.
132. SFX:
AFANDE KAIFA ANAWASHA PIKIPIKI NA KUONDOKA.
133. CONTROL:
Mama Mjuni

 

134.
Scene 4
135. Sehemu:
Ndani. Kituo cha polisi. Asubuhi.
136. Utambulisho wa kipengele:
Mazingira ya kituoni.

137. Wahusika:
Afande Kaifa, Mzee Ali, Afande Filipo.

138. SFX:
MLANGO UNAFUNGULIWA.
139. AFANDE FILIPO:
(MBALI NA MIC) Samahani bosi lakini.
140. AFANDE KAIFA:
(ANAMKATISHA) Nilikwambia nini tabia yako ya kuingia ofisini kwangu bila ya kugonga?
141. AFANDE FILIPO:
Samahani bosi lakini mwenyekiti wa serikali za mtaa anataka kukuona.
142. AFANDE KAIFA:
(ANAINUKA KUTOKA KWENYE KITI) Sawa, mwambie aingie basi!
143. SFX:
MZEE ALI ANAINGIA.
144. AFANDE KAIFA:
Mzee Ali, karibu sana! Habari yako?
145. MZEE ALI:
(AKIKARIBIA MIC) Nzuri tu; Samahani kama nakuvamia.
146. AFANDE KAIFA:
Hapana usijali, karibu kiti.
147. SFX:
MZEE ALI ANAVUTA KITI NA KUKAA CHINI.
148. AFANDE KAIFA:
Ehee niambie mzee Ali, tatizo gani limekuleta hapa leo?
149. MZEE ALI:
Sidhani kama ni tatizo kusema kweli…
150. AFANDE KAIFA:
(ANACHANGANYIKIWA KIDOGO) Oh..?
151. MZEE ALI:
Ndio.
152. AFANDE KAIFA:
Sawa, nakusikiliza.
153. MZEE ALI:
Unajua Kaifa, wanawake wako tofauti sana na wanaume.
154. AFANDE KAIFA:
(KWA SHAUKU) Ni kweli nakubaliana na wewe!
155. MZEE ALI:
Wako tofauti na sisi kwa namna wanavyopenda kuzungusha zungusha mambo. Wao hawako kama wanaume; sisi hatupindishi mambo.
156. AFANDE KAIFA:
Nakubaliana na wewe asilimia mia kabisa. Lakini bado sijaelewa unajaribu kuniambia nini?
157. MZEE ALI:
Ninachojaribu kukuambia…(ANASITA) Ninachojaribu kukuambia ni kwamba mkeo bado hajatulipa pesa aliyotukopa.
158. AFANDE KAIFA:
(KWA MSHANGAO) Pesa gani? Unaongelea nini?
159. MZEE ALI:
(BILA YA KUTEGEMEA) Una maana gani naongelea nini?! Si ulimuomba mkeo atukope pesa kwa ajili ya ada ya watoto?
160. AFANDE KAIFA:
Hata sijui unaongelea nini. Kwanza ndio mara ya kwanza nasikia yote haya.
161. SFX:
UKIMYA.
162. MZEE ALI:
Basi kutakuwa na shida.
163. AFANDE KAIFA:
Ni kweli. Alikopa shingapi?
164. MZEE ALI:
Laki nne.
165. AFANDE KAIFA:
(AKIFIKIRIA) Ahaa, kumbe!….itabidi niongee na mke wangu.
166. MZEE ALI:
(KWA KUJISHTUKIA) Basi, acha mimi niende.
167. AFANDE KAIFA:
Usijali; nitapata suluhisho juu ya hili jambo.
168. MZEE ALI:
Sawa, lakini jaribu kuwa muelewa ukiongea nae.
169. AFANDE KAIFA:
Usijali; kila kitu kitakuwa sawa tu.
170. MZEE ALI:
Sawa kwa heri.
171. AFANDE KAIFA:
Kwa heri.
172. SFX:
MZEE ALI ANAONDOKA.
173. AFANDE KAIFA:
Afande Filipo!
174. AFANDE FILIPO:
(ANAKUJA AKIKIMBIA) Ndio bosi.
175. AFANDE KAIFA:
Nina kazi kwa ajili yako.
176. AFANDE FILIPO:
Sawa nakusikiliza bosi.
177. AFANDE KAIFA:
Nataka uanza kumfuatilia mke wangu.
178. SFX:
UKIMYA.
179. AFANDE FILIPO:
(KIGUGUMIZI) Sija…sija…sijaelewa bosi.
180. AFANDE KAIFA:
(KWA UKALI) Ni kitu gani ambacho hujaelewa hapo?
181. AFANDE FILIPO:
(KWA KUSITA) Kwa hiyo unatakanimchunguze mkeo?
182. AFANDE KAIFA:
Kwani hujanielewa?
183. AFANDE FILIPO:
Nimekuelewa bosi.
184. AFANDE KAIFA:
Fanya kazi yako na uache kuuliza maswali. Utaniletea ripoti.
185. AFANDE FILIPO:
Sawa bosi.
186. SFX:
AFANDE FILIPO ANAMPIGIA SALUTI AFANDE KAIFA NA KUANZA KUTOKA NJE.
187. AFANDE KAIFA:
Oh! Na kitu kingine…Sitaki mtu yoyote ajue.
188. AFANDE FILIPO:
Sawa, bosi!
189. CONTROL:
Afande Kaifa

 

190.
Scene 5
191. Sehemu:
Nje. Kituo cha polisi. Mchana.
192. Utambulisho wa kipengele:
Mazingira ya kituoni.

193. Wahusika:
Afande Kaifa, Afande Filipo.

194. SFX:
MLANGO UNAGONGWA.
195. AFANDE KAIFA:
Pita!
196. SFX:
MLANGO UNAFUNGULIWA NA AFANDE FILIPO ANAINGIA.
197. AFANDE FILIPO:
Samahani bosi, nilidhani utakuwa umepumzika.
198. AFANDE KAIFA:
Ndio unasemaje?
199. AFANDE FILIPO:
(KWA KUSITA) Sasa bosi…Unajua bosi…nilifanya ile kazi uliyonituma.
200. AFANDE KAIFA:
Ehee imekuwaje?
201. AFANDE FILIPO:
(ANASITA) Kwa hiyo bosi…
202. AFANDE KAIFA:
Afande Filipo, Ebu ongea basi!
203. AFANDE FILIPO:
Nilimfuatilia mke wako kama ulivyoniambia, na nikamuona anakutana na kijana mmoja hivi.
204. AFANDE KAIFA:
(AKIONGEA PEKE YAKE) Umemuona akikutana na kijana?
205. AFANDE FILIPO:
Ndio bosi lakini sidhani ni kama unavyofikiria.
206. SFX:
UKIMYA KWA MUDA.
207. AFANDE FILIPO:
Nilimuona kama anamkabidhi pesa yule kijana. Nahisi walikuwa kama wanafanya biashara.
208. AFANDE KAIFA:
Basi, hakuna kingine?
209. AFANDE FILIPO:
Ndio bosi.
210. AFANDE KAIFA:
Sawa, inatosha kwa sasa.
211. AFANDE FILIPO:
Sawa bosi.
212. CONTROL:
Afande Filipo

 

213.
Scene 6
214. Sehemu:
Ndani. Nyumbani kwa Farida. Mchana.
215. Utambulisho wa kipengele:
Mazingira ya kwa Farida.

216. Wahusika:
Afande Kaifa, Farida, Zuhura, Jirani.

217. SFX:
MLANGO UNAFUNGULIWA.
218. SFX:
SIFA NA ZUHURA WANAMKIMBILIA BABA YAO.
219. SIFA/ZUHURA:
(KWA SHAUKU) Baba! Baba!
220. JIRANI:
Za kwako Kaifa?
221. AFANDE KAIFA:
Nzuri tu? Smahani kwani we ni nani?
222. JIRANI:
Oh! Mimi ni jirani wenu; naitwa Monica, nasihi hapo chini tu.
223. ZUHURA:
(ANAMKATISHA) Baba! Umetuletea zawadi? Ulisema tukilala utatuletea.
224. AFANDE KAIFA:
(KWA UKALI) Wewe kimya! (ANAMGEUKIA JIRANI) Mke wangu yuko wapi?
225. JIRANI:
Ametoka mara moja lakini amesema anarudi muda sio mrefu. Aliniomba niangalie watoto.
226. SFX:
MLANGO UNAFUNGULIWA.
227. SFX:
SIFA NA ZUHURA WANAMKIMBILIA MAMA YAO.
228. SIFA/ZUHURA:
Mama! Mama!
229. FARIDA:
(KWA MSHANGAO) Kaifa! Umesharudi kutoka kazini. Sikutegemea kukuta umerudi mapema yote hii.
230. AFANDE KAIFA:
Mimi nilikuwa naomba unikute.
231. FARIDA:
Una maanisha nini?
232. AFANDE KAIFA:
Ulikuwa wapi? Na usiniambie ulikuwa kwenye vikoba kwa sababu nilikuwa huko lakini haukuwepo.
233. SFX:
UKIMYA.
234. AFANDE KAIFA:
Hivi unajua shamba yenu ilikuwa livamiwe?
235. SFX:
UKIMYA.
236. JIRANI:
(ANAANZA KUINUKA) Mimi naona bora niende.
237. AFANDE KAIFA:
(KWA UKALI) Kaa chini!
238. JIRANI:
(KWA UOGA) Sawa.
239. AFANDE KAIFA:
(KWA HASIRA) Hakuna kuenda popote kwa sababu leo ndio siku ambayo natakakijiji kzima kijue nimeoa mwanamke wa aina gani.
240. FARIDA:
Una maana gani?
241. AFANDE KAIFA:
Nitakuuliza tena. Ulikuwa wapi?
242. FARIDA:
Sikiliza, kuna vitu ilibidi nifanye.
243. AFANDE KAIFA:
Wewe ni muongo! Usifikiri sijui kuhusu kuhusu mambo yako. Jinsi ulivyomdanganya mama Mjuni na mume wake – kwamba unahitaji mkopo ili kuwalipia ada watoto.
244. FARIDA:
(ANASHTUKA) Umejuaje kwamba…
245. AFANDE KAIFA:
Hukutugemea kama ningegundua sio? Najua kuliko unavyofikiria! Najua umekutana na kijana leo ambaye umemkabidhi pesa.
246. FARIDA:
(KWA UKALI) Kwa hiyo unanipeleleza?
247. AFANDE KAIFA:
(ANACHEKA KIDOGO) Utakuwa umesahau kwamba umeolewa na polisi!
248. JIRANI:
Jamani, acha niwapeleke watoto kulala. Haya twendeni. (AKIELEKEA CHUMBANI NA WATOTO)
249. AFANDE KAIFA:
Ebu niambie umekuwa ukifanya nini?
250. FARIDA:
Sifanyi chochote.
251. AFANDE KAIFA:
Wewe ni muongo tena muharibifu mkubwa! Utaniambia umefanyia nini hizo pesa!
252. FARIDA:
Haikuhusu nilichofanyia na pesa. Kwanza wewe hukunipa hizo pesa!
253. AFANDE KAIFA:
Kwa hiyo unajaribu kusemaje? (KWA UKALI) Ebu njoo hapa wewe panya mkubwa!
254. FARIDA:
(AKIPIGA KELELE) Ebu niachie!
255. SFX:
VITU VINASIKIKA VIKIDONDOKA WAKATI KAIFA NA FARIDA WAKIGOMBANA.
256. SFX:
WATOTO WANALIA KUTOKA CHUMBANI.
257. CONTROL:
Afande Kaifa

 

258.
Scene 7
259. Sehemu:
Nje. Nyumbani kwa mama Mjuni. Mchana.
260. Utambulisho wa kipengele:
Mazingira ya nyumbani kwa Mama Mjuni.

261. Wahusika:
Mama Mjuni, Farida, Mzee Ali, Afande Kaifa

262. SFX:
FARIDA ANAHEMA KWA NGUVU HUKU AKIKIMBIA.
263. SFX:
FARIDA ANAGONGA MLANGO KWA NGUVU.
264. SFX:
MAMA MJUNI ANAFUNGUA MLANGO.
265. MAMA MJUNI:
(KWA MSHANGAO) Heeh! Farida kuna nini tena?
266. FARIDA:
(BADO AKIHEMA KWA NGUVU) Anataka kuniua! Anataka kuniua!
267. MAMA MJUNI:
(AKIONEKANA KUCHANGANYIKIWA) Una maanisha mumeo? Farida ebu tulia kwanza.
268. SFX:
FARIDA ANAANZA KULIA.
269. MZEE ALI:
(AKIKARIBIA MIC) Kuna nini hapa?
270. SFX:
FARIDA ANENDELEA KULIA.
271.
PUNGUZA SAUTI HATUA KWA HATUA
272.
ONGEZA SAUTI HATUA KWA HATUA
273. SFX:
FARIDA, MAMA MJUNI NA MZEE ALI WAKIKARIBIA MIC.
274. FARIDA:
Hapana! Hapana! Hapana! Siwezi kuingia humo! Ataniua!
275. MAMA MJUNI:
Farida ebu tulia, sawa? Sisi tutaongea nae.
276. SFX:
MLANGO UNAGONGWA.
277. SFX:
AFANDE KAIFA ANAFUNGUA MLANGO.
278. AFANDE KAIFA:
(KWA HASIRA) Anafanya nini hapa huyu? Eeeh?
279. MZEE ALI:
Kaifa ebu subiri kwanza. Tupo hapa kuongea.
280. AFANDE KAIFA:
Simtaki huyu mwanamke ndani ya nyumba yangu. Mmesikia?
281. MZEE ALI:
Inabidi make chini muongee na mkeo ili kusuluhisha matatizo yenu.
282. AFANDE KAIFA:
Kwani wewe ni kiziwi mzee? Nimesitaki kumuona tena huyu mwanamke! Muongo mkubwa!
283. MAMA MJUNI:
Kaifa ebu msikilize mkeo basi.
284. AFANDE KAIFA:
Sitaki kusikia upuuzi huo!
285. MAMA MJUNI:
Tafadhali Kaifa, kama utaki kumfikiria mkeo basi wafikirie wanao. Jaribuni kumaliza tofauti zenu kama wazazi…kwa sababu watoto wenu wanawahitaji. nI bora kukaa chini na kuongea.
286.
PUNGUZA SAUTI HATUA KWA HATUA
287.
ONGEZA SAUTI HATUA KWA HATUA
288. MZEE ALI:
Kwa hiyo ilikuwaje mpaka mkafika uku?
289. AFANDE KAIFA:
Yaani umekaa kabisa hapo unaniuliza hilo swali?
290. MZEE ALI:
Ndio ni lazima nikuuliza, mimi na mke wangu tulikuwa tumepumzika. Ghafla tunashtukia tunaamshwa na kelele za Farida akilia anasema unataka kumuuua.
291. AFANDE KAIFA:
Je alikwambia pia kama alichukua pesa uliyomkopesha kwa ajili ya ada ya watoto na kumkabidhi kijana mmoja.
292. MAMA MJUNI:
(ANAGUNA) We Farda, ya kweli hayo?
293. FARIDA:
(AKILIA) Ndio.
294. MAMA MJUNI:
Kwanini umefanya hivyo Farida? Ulikuja kwangu na shida nikakuamini kwa moyo wangu wote na mpaka nikakuombea pesa kwa mzee Ali.
295. SFX:
FARIDA ANENDELEA KULIA.
296. AFANDE AKIFA:
(KWA UKALI) Mjibu!
297. SFX:
FARIDA ANENDELEA KULIA.
298. AFANDE KAIFA:
(KWA SAUTI) Sema ukweli!
299. FARIDA:
(ANAACHA KULIA) Unataka kujua ukweli?
300. AFANDE KAIFA:
Ndio, nataka kujua.
301. FARIDA:
(KWA SAUTI KALI) Ukweli ni kwamba ilibidi nidanganye ili nipate pesa kutoka kwa Mama Mjuni niweze kununua shamba ambalo nitaweza kulima maharage na ambapo ningeweza kufanya maamuzi ya kuamua wapi nitauza maharage yangu – kwa sababu nimetamani kwa muda mrefu hata mara moja nijisikie kama mtu muhimu! Nimechoka tabia ya kunifanya mimi kama vile si kitu kila ninapokuja kwako kuongea masuala yetu ya maisha.
302. AFANDE KAIFA:
Kwa kweli…
303. FARIDA:
(ANAMKATISHA) Bado sijamaliza! Ukweli ni kwamba nataka nijisikie kama mwanamke anayeheshimiwa na ambaye anajaliwa na sio mashine ambayo kazi yake ni kutumikishwa tu bila ya kuuliza maswali.
304. SFX:
UKIMYA.
305. MZEE ALI:
Kwa jinsi ninavyoona, nyie wawili mna tatizo la kutoweza kukaa chini na kuongea. Kama mngekuwa mna tabia ya kuongea, haya yote yasingetokea.
306. FARIDA:
Tatizo la mume wangu hataki kuongea.
307. AFANDE KAIFA:
Kwa hiyo ni sawa na wewe kudanganya?
308. FARIDA:
Je ni sawa na wewe kunipiga?
309. MZEE ALI:
(ANAINGILIA KATI) Haina haya kuanza kubishana juu ya mambo ambayo yameshapita. Kitu ambacho mnatakiwa kufanya sasa ni kuanza upya kujenga upya ndoa yenu.
310. SFX:
FARIDA ANAANZA KULIA.
311. FARIDA:
(AKILIA) Mama Mjuni hujui tu jinsi gani mambo yalivyokuwa magumu hii miaka michache iliyopita. Nimemvumilia sana huyu mwanaume.
312. MAMA MJUNI:
(KWA UKALI) Kaifa unayasikia hayo lakini? Ni kweli wewe ndio kichwa cha nyumba lakini mkeo ndio moyo wa hii nyumba, kwa sababu yeye ndiye anayekujali wewe huku akiwalea watoto; Anafua, anapika na anafanya kazi shambani. Kitu anachohitaji kutoka kwako ni kumheshimu na kumsikiliza tu. Farida amedanganya kwa sababu anajua hata kama angekwambia ukweli ingekuwa kazi bure tu kwa sababu asingepata msaada wowote kutoka kwako.
313. MZEE ALI:
Unajua wanawake wengi wanapitia mambo kama haya hapa kijijini. Wanawake wengi wanakosa msaada kutoka kwa waume zao. Chukua mfano suala la maharage, nimejaribu kuongea na wanaume wengi na wengine wapo tayari kubadilika kuanza kushirikiana na wake zao kufanya maamuzi kama ya wapi wanauza hayo maharage na kwa kiasi gani. Lakini kwa wengi wao itachukua muda sana.Kwa hiyo Kaifa nadhani ni vizuri kama utaanza kushirikiana na mkeo kwa sababu mmebarikiwa na familia nzuri na watoto wazuri. Inabidi muanze kuishi kwa amani na furaha sasa.
314. AFANDE KAIFA:
(KWA KUSITA) Kwa kweli…kwa kweli, ningependa nimuombe msamaha mke wangu na namuahidi nitaanza kumsikiliza na kushirikiana nae siku za usoni.
315. SFX:
UKIMYA.
316. MAMA MJUNI:
Farida, si umemsikia mumeo alichosema? Wewe unasemaje kuhusu hilo?
317. FARIDA:
Sidhani kama anaweza kubadilika huyu.
318. MZEE ALI:
Farida, nadhani ni ishara nzuri kama Kaifa ametambua makosa yake.
319. FARIDA:
Kutambua makosa peke yake haitoshi. Inatakiwa aoneshe kweli kama amebadilika. Kuongea siku zote ni rahisi lakini vitendo ndio muhimu.
320. CONTROL:
Farida

 

321.
Scene 8
322. Sehemu:
Nje. Shambani kwa wanawake wa vikoba. Mchana.
323. Utambulisho wa kipengele:
Wanawake wanaimba.

324. Wahusika:
Mama Mjuni, Wanawake, Mr. Patel.

325. SFX:
WANAWAKE WANAIMBA.
326. WOTE:
Wanawake, tumeonesha kuwa tunaweza! Sio kulima maharage tu mashambani, Lakini pia kufanya bioashara na kuuza masokoni. Tumeonesha kuwa umoja ni nguvu. Wanawake tumeonesha kuwa inawezekanana na tumeweza.
327. SFX:
MAKOFI YANAPIGWA.
328. MAMA MJUNI:
Asanteni wapendwa kwa hiyo nyimbo nzuri inayoonesha tulichoweza kufanikisha siku ya leo hapa! Hii ni hatua kubwa sana kwa wanawake wote kijijini. Tumeweza kufanikisha malengo tuliyojiwekea miezi michache iliyopita. Inabidi wote tufurahie kuweza kufanikisha kulima mahindi ambayo leo hii tunayuza kiwandani.
329. SFX:
WANAWAKE WANASHANGILIA.
330. MAMA MJUNI:
Sawa basi, bila ya kupoteza muda ningependa kumkaribisha mgeni wetu rasmi aliyetutembelea shamabani kwetu siku ya leo.
331. SFX:
WANAWAKE WANAPIGA MAKOFI.
332. MR PATEL:
Asanteni sana akina mama! Ningependa kumshukuru pia mkuu wetu wa operesheni kiwandani, bi. Stella ambaye ndiye aliyekuwa wa kwanza kuniambia juu ya kikundi chenu cha Vikoba…Nimefurahi sana kwa sababu nyie si wakulima wazuri tu bali hata waimbaji wazuri pia.
333. SFX:
WANAWAKE WANASHANGILIA KWA VIGEREGERE NA MAKOFI.
334. MR PATEL:
Mimi sio muongeaji sana lakini ningependa kuwaambia tu kwamba mmeweza kufanikisha kitu kikubwa sana hapa leo. Nikitazaama haya maharage yaliyonawili vizuri, Napata furaha kubwa sana moyoni. Na ndio maana nimeamu kuingia mkataba na kikundi chenu cha vikoba kutuuzia maharage kuanzia mwezi ujao.
335. SFX:
WANAWAKE WANASHANGILIA KWA MAKELELE.
336. CONTROL:
Mr. Patel.

 

337.
Scene 9
338. Sehemu:
Nje. Nyumbani kwa mama K. Asubuhi.
339. Utambulisho wa kipengele:
Mazingira ya kwa Mama K.

340. Wahusika:
Grace, Mama K.

341. SFX:
JOGOO ANAWIKA.
342. SFX:
GRACE ANAFUNGUA MLANGO NA KUTOKA NJE.
343. MAMA K:
(KWA MSHANGAO) Wewe Grace unaenda wapi hivyo umevaa kama mwanafunzi?
344. GRACE:
Shikamoo mama. Sikudhani utakuwa macho asubuhi yote hii.
345. MAMA K:
Nakuuliza: Unaenda wapi umevaa hivyo?
346. GRACE:
Nimeamua kurudi shule ili jimalize masomo yangu ya A level.
347. MAMA K:
Kwa pesa ya nani?
348. GARCE:
Una maana gani kwa pesa ya nani. Mama unajua kabisa tutangeneza pesa nyingi sana kwa kuuza maharage kiwandani, na pia nimeshatengeneza pesa nyingi kwa kuuza maharage yangu. Niliweka akiba ili niweze kulipia ada ya shule. Na leo ndio siku naanza masomo.
349. MAMA K:
(ANACHEKA) Masomo?! Wewe si mtu mzima sana kurudi shule?
350. GRACE:
Mama unajua wanavyosema…elimu haina mwisho.
351. MAMA K:
Na vipi kuhusu majukumu yako hapa nyumbani? Nani atasaidia na kazi za hapa nyumbani?
352. GRACE:
Nitasaidia na kazi za nyumbani kama kawaida, lakini hio haitanizuia kuacha kuenda shule – kwa sababu ni lazima niende shule.
353. MAMA K:
Na vipi kuhusu bar? Nani atakuwa ananisaidia na bar hapa nyumbani kama utakuwa uanondoka kila asubuhi?
354. GRACE:
Kuhusu bar, itabidi ujitahidi mwenyewe tu hivyo hivyo.
355. MAMA K:
Siku zote nilijua tu kuwa wewe mtoto ni mbinafsi na huwa humfikirii mtu mwingine yoyote bali peke yako.
356. GRACE:
Mimi sio mbinafsi, na ndio maana nimeamua kurudi shule ili nipate elimu nije kukusaidia hapo baadae! Kwa heri mama!
357. SFX:
GRACE ANAONDOKA.
358. CONTROL:
Grace

 

359.
Scene 10
360. Sehemu:
Ndani. Banda la kuku la Farida. Jioni.
361. Utambulisho wa kipengele:
Farida analisha kuku.

362. Wahusika:
Farida, Jenny.

363. JENNY:
(MBALI NA MIC) Farida upo wapi?
364. FARIDA:
(KARIBU NA MIC) Nipo huku! Kwenye banda la kuku!
365. JENNY:
(KWA UTANI) Nilijua tu nitakukuta huku! Mama na kuku zake.
366. FARIDA:
(ANACHEKA) Sasa niende wapi tena jamani?
367. JENNY:
(KWA MSHANGAO) Heeh! Kuku wako wamekuwa wakubwa! Unawalisha nini?
368. FARIDA:
Lishe ya kawaida tu, pumba basi.
369. JENNY:
Mungu wangu! Wana wiki ngapi?
370. FARIDA:
Kama wiki tatu hivi. Ndhani kuanzia wiki ijayo nitaanza kuwauza.
371. JENNY:
Honge kipenzi. Uko peke yako? Watoto wako wapi?
372. FARIDA:
Wapo shuleni, nahisi wana kama tamasha leo. Bonanza Sijui.
373. JENNY:
Na baba yao?
374. FARIDA:
Yupo kazini.
375. JENNY:
(KWA UPOLE) Kwa hiyo mnaendeleaje sasa hivi?
376. FARIDA:
(KWA KUSITA) Kusema kweli anajitahidi sana sasa hivi…japo ni ngumu kuwa nae sehemu moja. Akini Naona anajaribu kuwa mtu tofauti siku hizi.
377. JENNY:
Basi sio mbaya. Lakini kusema kweli: sasa hivi unaonekana una furaha zaidi tofauti na kipindi kile cha mabalaa.
378. FARIDA:
Ni kweli, nahisi tunajitahidi.
379. JENNY:
Ebu tuachane na hayo! Vipi hawa kuku? Maana siondoki hapa mpaka nipate mmoja ya hao kuku!
380. FARIDA:
Nilijua tu!
381. JENNY:
Yaani nitaandamana kabisa kama sitopata kuku!
382. SFX:
WOTE WANACHEKA.
383. CONTROL:
Farida.

 

384.
Scene 11
385. Sehemu:
Nje. Kiwandani. Asubuhi.
386. Wahusika:
Jenny, Farida, Grace, Mama Mjuni, Mama K, Stella, Mr. Patel.
387. Utambulisho wa kipengele:
Lori linawasili.

388. SFX:
LORI LINAWASILI.
389. SFX:
WANAWAKE WANASHANGILIA.
390. SFX:
HONI YA LORI.
391. STELLA:
Huyo sio Jenny anaendesha lori?
392. FARIDA:
Nani mwingine? (ANACHEKA)
393. STELLA:
(ANACHEKA) Hawezi kuacha mambo yake!
394. SFX:
INJINI YA LORI INAZIMWA NA JENNY ANASHUKA KUTOKA KWENYE LORI.
395. JENNY:
(KWA SHAUKU) Tumefanikisha jamani! Tumefanikisha!
396. FARIDA:
(KWA FURAHA) Yaani siamini mach yangu!
397. GRACE:
Nahisi kama vile niko ndotoni.
398. MAMA MJUNI:
Sio ndoto tena kipenzi bali ndio ukweli! Hivi unajua nimeongea na baadhi ya wanawake na wanasema kuwa waume zao wapo tayari kushirikiana nao kwenye maamuzi ya kuuza maharage.
399. FARIDA:
Ndio hivyo, hao wanaume wameshagundua umuhimu wetu.
400. SFX:
WOTE WANACHEKA.
401. STELLA:
Kwa hiyo umeleta magunia mangapi Jenny?
402. JENNY:
Magunia 92.
403. STELLA:
Hongera sana wanawake wenzangu kwani Mmefanikiwa kuleta mzigo wenu wa kwanza.
404. SFX:
WANAWAKE WANASHANGILIA KWA KWA KELELE NA VIGEREGERE.
405. STELLA:
Jamani naomba mtusaidie kushusha mzigo.
406. WAFANYAKAZI:
Sawa.
407. SFX:
WAFANYAKAZI WANASHUSHA MZIGO KWENYE LORI.
408. GRACE:
Angalia, bwana Patel anakuja.
409. MR. PATEL:
(AKIKARIBIA MIC) Akina mama, nimefurahi sana kwamba hamjavunja ahadi yenu na mmetuletea maharage kama mlivyoahidi. Saa mbili kamili juu ya mshale! Inanioensha kuwa huo ndio mwanzo wa ushirikiano mzuri kati yenu na sisi.
410. SFX:
WANAWAKE WANASHANGILIA.
411. MAMA MJUNI:
Na sisi tunakushiukuru Mr. Patel kwa kutupa nafasi hii. Tunakuahidi ya kuwa tutafanya kazi kwa bidii na tutaheshimu mkataba wetu pia.
412. MR. PATEL:
Nafurahi sana akina mama! Sina mengi ya kusema…lakini endeleeni! hongera sana na kila la heri.
413. SFX:
WANAWAKE WANASHANGILIA.
414. FARIDA:
(KWA FURAHA) Ndio! Tumeweza na tumefanikisha!
415. MAMA K:
Jamani lazima tusherehekee leo! Sherehe kwenye bar yangu tukiondoka. Vinywaji bure kwa watu! Ndani ya nyumba!
416. JENNY:
Mama K leo anatoa ofa ya vinywaji?
417. MAMA MJUNI:
Kweli leo ni siku muhimu sana.
418. CONTROL:
Mama Mjuni

Acknowledgements

Imechangiwa na: Kheri Mkali, mwandishi wa muongozo, Dar es Salaam, Tanzania.
Imepitiwa na: Frederick Baijukya, mtaalamu wa kilimo na mratibu wa shirika la N2Africa Tanzania, Shirika la kilimo kwa nchi kitropiki (IITA), East Africa Hub, Dar es Salaam, Tanzania.

Kazi hii imewezeshwa kwa masaada wa Shirika la utafiti, lililopo Ottawa, Kanada (International Development Research Centre, Ottawa, Canada) www.idrc.ca, na msaada wa kifedha kutoka serikali ya Kanada, kupitia idara ya masuala ya kimataifa, (Global Affairs Canada) www.international.gc.ca.
gaclogoidrc