Mwanamke Mkenya aliyejikita kwenye kilimo hifadhi na kuboresha maisha yake

Afya ya udongo

Ujumbe kwa mtangazaji

Ujumbe kwa watangazaji

Kilimo hifadhi ni kilimo kinachotumia mbinu maalum za kilimo zinazoboresha udongo na rasilimali nyingine za asili huku zikiboresha mavuno na uhakika wa chakula. Kinahusisha mbinu kama kufunika ardhi na mabaki ya mimea na mazao, kupokezana kwa mazao yanayopandwa na kutifua ardhi kwa kiasi kidogo-na kupunguza au kuepuka shughuli nyingine zinazosumbua uso wa ardhi. Magharibi mwa Kenya, kilimo hifadhi kinahusisha matumizi ya mbolea ya wanyama au mbolea kutokana na mimea ya asili inayopatikana kama vile Tithonia.

Magharibi mwa Kenya, Hali ngumu ya hewa na mbinu mbaya za kilimo zimechangia upotevu wa udongo na uoto wa asili. Hii inapunguza rutuba na kupelekea wakulima kutegemea sana mvua kwa sababu udongo hauwezi kuhifadhi maji. Bila kuwa na unyevu kwenye udongo, mazao yasiyoweza kustahimili ukame, hudhoofika na kupotea kabisa. Lakini hii inaweza kuzuiliwa kwa kutumia mbinu za kilimo kama kilimo hifadhi ambacho kwa kipindi cha miezi na miaka, kinaboresha udongo na kuongeza mavuno.

Nchini Kenya, 80% ya wakulima ni wakulima wadogowadogo na huandaa mashamba yao kwa mikono. Baada ya kufyeka mabaki ya mazao, baadhi ya wakulima huyachoma mabaki hayo kupunguza kazi, kisha wanalima kwa jembe la mikono mashamba yao. Familia nyingine baada kufyeka mabaki ya mazao wanalima kwa jembe la ng’ombe. Kisha wakulima hutumia jembe la mkono kuchimba mashimo ya kupandia na baadae kupalilia kwa kutumia jembe la mkono. Kulingana na kilimo hifadhi, hizi mbinu zinasumbua udongo na kuharibu uwezo wake wa kubeba rutuba na kuhifadhi maji kwa afya nzuri ya mimea.

Mwongozo huu wa kipindi unakuletea hadithi ya mjane aliyetengwa na jamii yake mpaka alipojiunga na kikundi cha wakulima. Wanakikundi walianza kwa kulima mazao ya chakula, mahindi halafu wakafahamishwa kuhusu kilimo hifadhi. Baada ya mjane kufahamishwa kilimo endelevu kupitia kikundi, alikifanya kilimo mseto na kupelekea kuboresha maisha yake kuwa mazuri.
Unaweza kuamua kutumia makala hii kama sehemu ya programu yako ya kilimo, kutumia wawakilishi kuwakilisha wahusika, ikibidi kufanya hivyo tafadhali wataarifu wasikilizaji mwanzoni kuwa sauti ni za waigizaji na sio za wahusika halisi waliofanyiwa mahojiano.
Pia unaweza kutumia makala hii kama zana ya utafitti, au kama msukumo wa kutegeneza mpangilio kuhusu kilimo hifadhi au mada sawa na hii nchini mwako.

Zungumza na wakulima na wataalam wanaotumia mbinu za kilimo rafiki wa mazingira au elimu kuhusu aina hii ya kilimo. Unaweza kuwauliza:

  • Ni matatizo gani ya kilimo cha kienyeji ambayo kilimo hifadhi kinaweza kuyabainisha?
  • Je wakulima wameweza kunufaika na kilimo hifadhi?
  • Ni vizuizi gani vipo dhidi ya kuiga njia za kutokukwatua ardhi yani kusumbua udongo kidogo inavyowezekana na mbinu nyingine za kilimo hifadhi, na namna zinavyoweza kuhainishwa?

Makadirio ya muda kuanzia utangulizi na muziki wa kumalizia ni kama dakika 20.

Script

WAHUSIKA

Mtangazaji
Jenipher Awino, Mkulima

KIASHIRIA

MTANGAZAJI:
Salam, msikilizaji, karibu kwenye kipindi. Leo tutasikia hadithi ya mwanamke mkulima aliyebadilisha maisha yake kwa kujikita katika kilimo hifadhi. Mwanamke huyu anaitwa Jenipher Awino, na anaishi katika kijiji cha Bar Kite magharibi mwa Kenya.

Bi Awino amekua mjane miaka kumi na tano iliyopita na ni kama alikata tamaa katika maisha baada ya kuanguka katika umasikini uliokithiri. Lakini aliamua kujinasua katika kutengwa na jamii kwa kujiunga na wanajamii wengine kwenye vikundi vya kilimo vilivyojikita katika kilimo hifadhi na kubadilisha maisha yake. Ungana nami ninapotembelea shamba lake na kutueleza historia yake ya maisha.

KIASHIRIA KINASIKIKA ALAFU KINAPOTEA. PIKIPIKI INASIMAMA ALAFU SAUTI YA JEMBE LIKILIMA INASIKIKA.

MTANGAZAJI:
Ni saa nne asubuhi wakati nilipofika shambani mwa Awino baada ya kuwasiliana nae kupitia simu. Bado yuko shambani akipalilia nyanya zake.

(ANAITA) Siku ikatike

JENIPHER AWINO:
(AKIJA KWENYE MIC)Siku ikatike. Habari yako?

MTANGAZAJI:
Nzuri, Asante, Na wewe?

JENIPHER AWINO:
(AKIWA KWENYE MIC) Nzuri, asante pia. Karibu Nyumbani.

MTANGAZAJI:
Asante, lakini tafadhali sikiliza ombi langu kwamba uendelea kupalilia wakati tunazungumza.

JENIPHER AWINO:
Sawa.

MTANGAZAJI:
Unaweza kutuambia ulianzaje kilimo na ni mazao gani ulianza kulima kwa mara ya kwanza?

JENIPHER AWINO:
Nilianza kilimo wakati bado nikiishi na wazazi wangu, hivyo ni kipindi cha nyuma kidogo. Kipindi nilipoolewa, nilikua najua njia moja tu ya kilimo, njia niliyojifunza, kutoka kwa wazazi wangu.

Nilikua naandaa shamba kwa kufyeka magugu kidogo, halafu natifua ardhi kwa jembe ili kufanya udongo uwe laini na sawa kwa ajili ya kupandia. Baada ya hapo, nachimba mashimo ya kupandia na baadae napalilia shamba kwa kutumia jembe la mkono. Sikuwahi kupata mavuno mazuri kutokana na hizi mbinu ingawa niliweka nguvu zote uko.

Marehemu mume wangu alikua anajihusisha na kazi za kawaida, ukarabati wa magari. Lakini hatukua na uwezo wa kukidhi mahitaji ya familia yetu ndogo. Alipofariki miaka 15 iliyopita, mtoto wangu wa kwanza alikua na miaka 10 tu. Niliendelea kulima kwa kutumia mbinu zilezile baada ya kifo cha mume wangu kwa sababu sikujua mbinu nyingine tofauti zaidi ya zile nilizokua nazijua miaka ya nyuma.

MTANGAZAJI:
Ulikua unajihusisha na kilimo tu, au ulikua unajishughulisha na vitu vingine vilivyokua vinakupatia kipato kusaidia familia yako?

JENIPHER AWINO:
Pia nilikua natengeneza mifagio laini kwa ajili ya kuuza sokoni, nilianza kufanya hivi wakati bado mume wangu akiwa hai, pia nilifanya kazi za shambani.

MTANGAZAJI:
Jinsi gani hali yako iliathiri mahusiano yako na watu wanaokuzunguka?

JENIPHER AWINO:
Niliishi kwenye nyumba yenye eneo za mita mraba 3 kwa 3. Hii ilinipelekea kutokufikiri kuhusu kitu chochote chanya kinachotokea kwenye maisha yangu. Nilijitenga na wanajamii. Nilifikiri kwamba kwa juhudi zangu binafsi nitayamudu matatizo yangu.

Lakini hii haikusaidia. Nilitambulishwa na rafiki yangu katika kikundi cha wanajumuiya kiitwacho Tego Yie (Editor’s note: a Luo phrase meaning strengthening faith). Huu ndio ulikua mwanzo wa mabadiliko yangu. Ni miaka mitano imepita tangu nijiunge na kikundi cha wanajumuiya. Kikundi kilikua na ndoto za kubadilisha maisha kupitia kilimo.

MTANGAZAJI:
Ilikua rahisi kwa rafiki yako kukushawishi kujiunga na kikundi?

JENIPHER AWINO:
Wanawake wengi kijijini wamejiunga na vikundi ambapo wanajifunza shughuli mbalimbali kama merry-go-round kujipatia kipato (Zingatio la mhariri:Merry go round ni msemo wa kilugha unaomaanisha Chama cha kuweka na Kukopa). Lakini nilijihisi nimeachwa nyuma; Nilihisi sitaweza kuendana na mfumo wao kwa sababu hali yao ya kiuchumi ilikua juu kuliko yangu.

MTANGAZAJI:
Kitu gani kilibadilisha mtazamo wako?

JENIPHER AWINO:
Nilianza kuhudhuria sio tu mikutano ya kikundi ila pia mikutano ya jumuiya iliyoitishwa na utawala wa ndani-chifu na msaidizi wa chifu. Kwenye mikutano ya jumuiya, nilisikia kuhusu mradi unaosimamiwa na Wizara ya Kilimo na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali kujifunza husuhu Kilimo hifadhi pamoja na vikundi vya wakulima. Kikundi chetu ni miongoni mwa vikundi vilivyoshiriki.

MTANGAZAJI:
Mafunzo ya Kilimo hifadhi yalihusu nini haswa?

JENIPHER AWINO:
Nilipojiunga na kikundi, mafunzo yalihusu kilimo mseto cha mahindi na jamii za maharage. Nilikua tayari kujifunza kitu chochote kipya ambacho kinaweza kufanya maisha yangu kua mazuri.

Tulikua tunapata mafunzo kutoka wizarani kwa msimu ambayo ni miezi mitatu na wiki mbili. Kulikua na eneo la maonyesho lenye sehemu nne tofauti. Sehemu ya kwanza ilikua na mseto wa mahindi na dengu, nyingine ilikua mseto wa ahindi na maharage, nyingine ilikua na Dolichos lab-lab, nyingine ilikua na kunde.

Wakati wa mafunzo, tuliiacha ardhi bila kuisumbua kwa kutifua udongo ila kwa kung’olea tu magugu. Mara nyingine tulitumia jembe kutoa magugu kwenye udongo. Lakini hatukubandua uso wa ardhi, hivyo udongo ulibaki na rutuba na uwezo wake wa kuhifadhi maji. Pia, mizizi ya mazao haikutolewa nje ya ardhi na kuisababishia mazingira mabaya kutokana na upepo.

Kama kikundi, tulikua tunarekodi taarifa zote kuanzia kupanda hadi kuvuna. Wiki moja baada ya kupanda tuliangalia idadi ya majani ya muhindi kwa kila mmea, urefu wa mmea na mmea na urefu kila jani. Tulifanya ivi tena wiki ya pili, ya tatu, ya nne, na tuliendelea mpaka maindi yalipokomaa.

Mahindi yalikomaa na kuwa tayari kuvunwa baada ya siku 105. Nilipenda kila hatua ya tuliyokua tunafanya na huu ndio ulikua ufunguo wa macho yangu.

MTANGAZAJI:
Hii ilikuaje ufunguo wa macho yako?

JENIPHER AWINO:
Baada ya kujifunza kwenye maeneo ya maonyesho, kila mmoja wetu alifanya jaribio lilelile kwenye shamba lake, nilichagua mseto wa mahindi na maharage. Niliweza kumudu kufyeka magugu tu na nilishindwa kumudu mashine ya kupandia. Nilipalilia kwa kung’oa mimea isiyohitajika na kupalilia juu juu kwa jembe dogo ambalo halikusumbua udongo. Tulikubaliana kama kundi kutembelea kila shamba la mmoja wetu kuhamasishana na kuona jinsi tulivyokua tunafanya. Hii ilinipelekea mimi kufanya vizuri zaidi.

Wakati cha mavuno, ulikua wa kutabasamu. Kutoka kwenye hekta moja ile ile ambayo sijawahi kupata zaidi ya kilo 190, Nilivuna kilo 1290.

Huu ndio ulikua mwanzo wa safari yangu ya mafanikio. Ilikua mara yangu ya kwanza maishani mwangu kuuza mazao ya shamba langu sokoni na bado kubakiwa na chakula kwa ajili ya familia yangu. Hii ndio iliyonihamasisha na niliapa kutokurudi kwenye umasikini uliokithiri na ulioathiri utu wangu kijijini.

MTANGAZAJI:
Ndio kitu ulichojifunza tu?

JENIPHER AWINO:
Baada ya shughuli hii ya kwanza na kundi, mashirika yasiyo ya kiserikali kuwasiliana na sisi kupitia utawala wa ndani. Shirika moja lisilo la kiserikali lijulikanalo kama Farm Inputs Promotions Africa ilitupatia mafunzo ya jinsi ya kupanda mboga asilia. Nilipanda aina tofauti za mboga za kienyeji, sana sana kwa ajili ya kuuza. Pia shirika lilitupa mafunzo ya kufuga kuku na kututambulisha kwenye kitengo cha kuku na msingi wa usimamizi wa kuku. Nilijenga nyumba ya kuku ambapo walikua wanahifadhiwa, na kulindwa dhidi ya wanyama hatarishi kwa uzio wa wavu. Kuku wamekua wakiwapa mayai wakulima. Wakulima wanawapa kuku mayai kuyaatamia na kutotoa.

Pia nilijiunga na makampuni tofauti ya kilimo. Shirika la Kenya la Utafiti wa Kilimo na Shirika lisilo la Kiserikali linaloitwa Nishati vijijini na Usalama wa chakula lilitufundisha kupanda migomba kwa kutumia mapandikizi yaliyokua yamepandikizwa kwenye mazingira safi kwenye vitalu vianavyoitwa tissue culture.

Pia, nilipata mbuzi mmoja kutoka Shirika la Heifer, na ninauza maziwa. Pia nina mradi mpya wa kusindika wa machungwa na viazi vitamu, na kuuza krips na chips kwenye shule za msingi zilizo karibu. Natengeneza unga wa uji, kwa kutumia nyama za ndani za machungwa na viazi vitamu na maharage na mtama.

MTANGAZAJI:
Unaweza kutaja faida za kilimo hifadhi?

JENIPHER AWINO:
Baada ya kujihusisha na kilimo hifadhi, ndio ulikua mwisho wa kununua mahindi sokoni kwa sababu ninazalisha chakula cha kutosha kwaajili ya family yangu. Kilimo hifadhi kinahusisha kazi kidogo na muda kidogo, mavuno mengi, muundo wa udongo unaimarishwa na kinazuia mazao kusinyaa kwa sababu ya ukame.

Kwasababu kilimo rafiki wa mazingira kinahusisha kwa kiwango cha chini cha ukwatuaji wa ardhi, hakuna mmomonyoko wa udongo, na hii inaongeza uwezo wa udongo kuhifidhi maji.

Lakini kilimo hifadhi ni kirahisi kwa wale tu wenye uvumilivu wa kufanya kazi zao za shamba; Matokeo hayaji kwa usiku mmoja. Katika kilimo rafiki wa mazingira, ni muhimu kufunika udongo kila wakati. Hivyo nilitandaza shamba kwa kutumia mabua ya mahindi au Tithonia ambayo pia inaongeza nitrojen kwenye udongo. Pia nilitumia samadi ya mimea iliyooza kama mbolea.

MTANGAZAJI:
Kazi zako ziliwahamasisha wanakijiji wengine au ndugu zako?

JENIPHER AWINO:
Kwa sasa mimi ni mshauri wa kijiji wa masuala ya kilimo na ni mkufunzi wa wakufunzi. Nimekifanya mseto kilimo changu ambapo nalima mazao tofauti, na hii inanipatia kipato kikubwa. Nimehama kutoka kwenye nyumba ya futi kumi kwa kumi iliyoezekwa kwa majani ambayo kuhamia kwenye nyumba ya hali ya wastani.

Nimepata heshima kwenye jamii, ambayo imenihamasisha sio tukufanya kazi kwa bidii ila kwa umakini zaidi. Kupitia elimu na ujuzi nilioupata, watu wananitembelea kutoka ndani ya jamii na kutoka maeneo mengine mbalimbali. Wananiita profesa licha ya elimu yangu ya shule ya msingi.

MTANGAZAJI:
Je una hadithi nyingine ya mafanikio ukiachana na mavuno mengi, kufikia masoko, na kujenga nyumba?

JENIPHER AWINO:
Kutokana na mapato yangu ya shambani,nilimpeleka mwanangu wa kwanza wa kiume kujifunza ufundi. Anaishi mji wa mbali kidogo akifanyia mazoezi alichojifunza. Alikuja nyumbani siku moja na kuona nauza kichane cha ndizi kwa shilingi 1500 ya Kenya na fungu la mboga kwa shilingi 500. Alichokua anakifanya kilikua hakimpatii kipato kizuri, hivo aliamua kurudi nyumbani na kujifunza kilimo kama mimi.

Kutokana na kipato ninachokipata kupitia kilimo, nilimnunulia pikipiki kwa ajili ya biashara. Kupitia uchapakazi wake, aliweza kununua pikipiki mbili na ana eneo la kufanyia mazoezi lenye vifaa vyote. Biashara zake zinafanya vizuri na amejenga nyumba yake baada ya kuishi kwenye nyumba isiyokua ya kudumu kwa mda mrefu.

MTANGAZAJI:
Una ndoto gani?

JENIPHER AWINO:
Ndoto yangu ni kuona watoto wangu wanasoma adi hatua wanayoitaka. Pia nina ndoto ya kununua gari kwa ajili ya kupelekea mazao yangu sokoni. Pia ninatamani kujenga nyumba nzuri zaidi kuliko hii ninayoishi sasa.

MTANGAZAJI:
Asante, Jenipher Awino, kwa kutupitisha kwenye safari yako ya uchapaji kazi na malengo.

Na,msikilizaji, unaweza kufanya ivi pia! Jenipher alianza kidogo na umesikiliza ndoto zake kubwa.

Leo, tulitembea pamoja shambani mwa Jenipher na tumesikia hadithi ya mwanamke aliyekua analima kilimo mseto, mahindi pamoja na maharage, na kutokukatua ardhi, pia ana shamba la migomba na kuuza mayai.

Unaweza kuanza kwa kutumia mbinu zilezile: kutokukatua ardhi, kutumia nafasi sahii kati ya mimea, kupalilia kwa usahii na wakati sahihi wa kupalilia, njia sahihi za uvunaji, na kutokuisumbua ardhi-yote ni kwa ajili ya mavuno mazuri na maisha bora.

Kwaheri hadi wakati mwingine tutakapokutana katika kipindi cha mkulima. Mimi ni mtangazaji wako, (jina la mtangazaji).

Acknowledgements

Imeandaliwa na: Rachel Adipo, Program Officer, Adaptive Research and Information Technology Program, Ugunja Community Resource Centre.
Imehakikiwa na: Getrude Kambauwa ,Chief Land Resources Conservation officer, Land Conservation Department Headquarters, Malawi Ministry Of Agriculture, Water and Irrigation Department; Wycliff Kumwenda, Farm Services Manager, National Smallholder Farmers’ Association of Malawi; Peter Kuria, Programme Officer for African Conservation Tillage Network, Kenya

Vyanzo vya taarifa

Mahojiano na Jenipher Awino, mkulima na mshauri wa kijiji masuala ya kilimo, Octoba 16, 2014

This script was translated with the support of Canadian Foodgrains Bank as part of the project, “Conservation Agriculture for building resilience, a climate smart agriculture approach.” This work is funded by the Government of Canada, through Global Affairs Canada, www.international.gc.ca