Maranda ya mbao yaongeza maisha ya ghala kwa viazi batata

Shughuli za baada ya mavuno

Ujumbe kwa mtangazaji

Save and edit this resource as a Word document.

Viazi vina nafasi muhimu katika usalama wa chakula na aushi kwa jamii za wakulima katika nchi nyingi zinazoendelea. Kulingana an Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), uzalizaji na matumizi ya viazi batata unaongezeka. Nchi zinazoendelea kwa sasa huzalisha zaidi ya nusu ya kiasi cha viazi batata kinachotolewa duniani kote

Uhifadhi hutoa changamoto kubwa kwa wakulima. Wakulima wa viazi batata huvuna zao lao lote kwa wakati mmoja. Jambo hili husababisha mafuriko katika soko na hii ina maana kuwa wakulima wanapokea malipo duni kwa mazao yao. Viazi batata huharibika endapo vitabaki kwa muda mrefu katika shamba kama vimekomaa. Huvamiwa na wadudu na havidumu kwa muda mrefu vinapohifadhiwa. Hii husababisha hasara kubwa kwa wakulima.

Hasara kama hii huwa na athari kubwa kwa usalama wa chakula na mapato ya wakulima. Inachangia pia katika kupanda kwa bei kwa watumiaji msimu wa zao unapopita.

Makala haya yanaangazia mtazamo mbunifu katika tatizo la uhifadhi wa viazi batata. Mkulima anatumia maranda ya mbao kuhifadhia viazi vyake kwa muda mrefu. Hadithi hii inakoleza uvumbuzi wa kimashinani ambao kwao, wakulima wanabuni njia za kukabiliana na changamoto zinazowakuba.
Makala haya yana misingi ya mahojiano halisi. Unaweza kutumia makala haya kama msukumo kutafiti na kuandika makala juu ya mada sawia katika eneo lako. Ama unaweza kuchagua kutoa makala haya katika kituo chako ukitumia waigizaji wa sauti kuwakilisha wazungumzaji. Endapo utafanya hivyo, tafadhali hakikisha unaiambia hadhira yako mwanzoni mwa kipindi kuwa sauti hizo ni za waigizaji na wala si wazungumzaji asilia walioshiriki katika mahojiano.

Script

Wimbo wa Kitambulisho: Uendelee kwa hadi nukta tano kisha ufifie chini ya sauti ya mtangazaji.

Mtangazaji:
Viazi batata ni zao la chakula muhimu nchini Kenya. Huwa vinakuzwa katika nyanda za juu za mikoa ya Kati, Bonde la Ufa na Magharibi. Hata hivyo, usalishaji na uuzaji wa viazi hutatizwa na hali duni ya uhifadhi ambayo hupunguza mapato ya wakulima pamoja na kuwavunja moyo.

Katika kipindi chetu cha leo, tunakutana na mkulima mmoja wa viazi batata ambaye amegundua njia ya ajabu ya kuhifadhi viazi batata vyake katika hali nzuri kwa muda mrefu baada ya kuvuna.

SFX:
Sauti za makelele ya sokoni. Zififie chini ya sauti ya mtangazaji.

Mtangazaji:
Tuko katika kituo cha biashara cha Kinungi kilichoko katika barabara yenye shughuli nyingi ya Nakuru-Naivasha. Ni asubuhi na mapema and soko la ina shughuli nyingi. Leo, wakulima wana viazi batata vichache vya kuuza sokoni. Mavuno ya mwisho yalikuwa miezi mitatu iliyopita. Zao mpya bado linaendelea kukua shambani.

Lakini mambo ni tofauti kwa Bw. Githenya Kariuki. Yeye amefika hapa kuuza viazi vyake kwa mnunuzi kutoka Nairobi, yapata kilomita 70 kutoka hapa. Yeye anasema kuwa ni msimu wa viazi batata kwake, haya yote yakitokana na mbinu yake mpya ya kuhifadhi viazi batata.

Githenya:
Unajua, mimi nategemea viazi kukidhi mahitaji ya familia yangu. Mimi hulisha na kusomesha watoto, na bado hubaki na pesa kiasi fulani kushughulikia nyakati ngumu. Nina watoto watatu katika shule za upili, na huo si mzaha. Karo inakuwa nyingi sana, hasa kwa mtu kama mimi anayetegemea kilimo tu.

SFX:
Sauti ya watu wanaotembea huku wakizungumza. Paaza na kuchanganya ukififiisha chini ya sauti ya mtangazaji na ile ya mtu anayelima.

Mtangazaji:
Tunatembea mita mia tatu kutoka barabara kuu na kufika katika shamba la Githenya. Bi. Githenya analima kisehemu cha ardhi ambacho bwana yake anasema kitapandwa viazi.

SFX:
Sauti ya mlango ukifunguka.

Githenya:
Hili ni ghala langu ambamo naweka mengi ya mazao yangu.

Mhojaji:
Ghala lenyewe ni kubwa. Lazima ulitumia kiasi kikubwa cha mbao kulijenga. Naona kitu kama rundo la nyasi kule pembeni. Je, kile ni chakula cha ng’ombe wako?

Githenya:
Hatimaye mimi huitumia kama chakula cha ng’ombe. Lakini nyasi ile huzuia maranda ya mbao yasipeperushwe na upepo mkali wa asubuhi. Hilo likifanyika, viazi vyangu vitapata mwangaza na haitachukua muda mrefu kabla havijazaanza kubadilika rangi. Vinapoanza kubadilika rangi, basi vinakuwa havifai kama chakula cha binadamu.

Mhojaji:
Je, umekuwa na tatizo hapo mbeleni?

Githenya:
Nimekuwa nikitamani kuhifadhi viazi batata kwa muda mrefu zaidi. Kwa kawaida, niliviweka katika pembe moja ya ghala langu. Lakini baada ya muda, yalikuwa yakigeuka kijani kibichi na hivyo kuwa havifai kuuzwa. Kwa hivyo, nililazimika kuviuza vyote mara tu baada ya kuuza. Kwa vile soko huwa na viazi batata kwa wingi baada ya mavuno, bei yake huwa chini. Viazi vinapoharibika, naweza kuvitumia kama mbegu, lakini haiwezekani nikatumia vyote vilivyoharibika.

Mhojaji:
Uligunduaje maranda ya mbao?

Githenya:
Huwa natumia maranda ya mbao kama matandiko kwa kuku wangu. Siku moja, nilienda kwenye taka ambapo seremala hutupa machunjo ya mbao. Nilipokuwa naokota maranda, niliona viazi vilivyokuwa vimetupwa. Vilionekana kuwa katika hali nzuri. Jambo hili lilinipatia wazo la kutumia maranda ya mbao badala ya nyasi kufunikia viazi batata vyangu. Nilitumia safu mbadala za pumba na viazi, nikianza na kumalizia na safu ya maranda.

Mhojaji:
Kiazi batata ni kama kitu kingine cho chote chenye uhai. Huishi na kupumua. Ukikiweka katika sehemu yenye joto, kitakua. Ukikifunga katika mfuko wa mpira, kitanyongwa. Kikiugua, kitaharibika. Na turejee kwa mahojiano na Bw. Githenya.

Mhojaji:
Ulijifunza nini katika majaribio haya?

Githenya:
Jambo moja nililojifunza ni kuwa maranda hayo ya mbao lazima yawe yamelowa kwa kiasi fulani. Ikiwa yamekauaka sana, basi ubora wa viazi vile utapungua kwa kasi kwa kuwa vitakauka na kuvamiwa na wadudu. Kwa upande mwingine, ikiwa yamelowa zaidi, basi viazi vitaoza baada ya muda mfupi.

SFX:
Sauti ya nyasi ikigeuzwa na kuwekwa kando.

Mhojaji:
Ni kilo ngapi za viazi batata vilivyoko katika rundo hili?

Githenya:
Rundo hili lina kilo 400. Hili lingine lina kilo 300. Nilizipanga hivi kwamba nimetumia nafasi iliyoko kikamilifu. Kumbuka kuwa hili ni ghala ambamo mimi huweka vitu vingine pia.

Mhojaji:
Ni changamoto gani ulizokumbana nazo katika kujaribu mbinu hii?

Githenya:
(Akicheka) Mara kwa mara watu hawaamini kitu mpaka waone kikifanikiwa. Nilipomwambia mke wangu kuwa nilitaka kujaribu njia mbadala ya uhifadhi, aliteta kuwa hii ingechukua nafasi kubwa sana katika ghala. Nilimwambia tungejaribu mara moja tu na kama haikufanikiwa, basi tungeiacha. Kwa hivyo, akakubali.

Lakini nilikuwa na tatizo lingine. Mwanzoni, seremala walinipa maranda ya mbao bure. Lakini baada ya muda mfupi, wakanitaka kuilipia. Sikuwa na pesa kama hizo. Kwa hivyo, tukaafikiana kwamba wangenipa maranda nami niwape viazi vya thamani kama sawia.

Mhojaji:
Githenya hakuachia hapo. Aliwaeleza wakulima katika kundi lake mafanikio ya mbinu hii mpya.

Githenya:
Wakulima walipojaribu mbinu hii, walisema kuwa viazi batata vyao vilikaa vizima kwa muda mrefu zaidi kuliko kutumia mbinu nyinginezo. Hii ndiyo sababu kwa muda wa miaka mitatu iliyopita, wanachama wa kundi langu la kilimo wamekuwa wakitumia mbinu ya maranda ya mbao. Matumizi ya maranda ya mbao ni yenye ufanisi hivi kwamba sasa tunaweza kuhifadhi viazi batata vyetu kwa hadi miezi minne baada ya mavuno.

Mhojaji:
Bw. Samuel Njiru ni Afisa Kilimo wa Wilaya katika wilaya ya Kinangop. Anasema kuwa njia duni za uvunaji zinaweza kusababisha hasara kubwa katika uhifadhi wa viazi batata.

Bw. Njiru:
Uhifadhi bora huanza kwa uvunaji wenye uangalifu. Majira ya mavuno ni suala nyeti. Lazima wakulima wawe waangalifu sana ili wasivune mapema sana au wachelewe. Baadhi ya maambukizi yanayovamia viazi batata kwenye ghala huanza wakati wa kuvuna. Ili kuepukana na haya, inatakikana kuvuna viazi batata kama viazi vyenyewe vimekomaa kikamilifu. Hii hupunguza kuchunua ngozi yake ambako kunaweza kupelekea maambukizi. Kwa upande mwingine, iwapo viazi hivi vitachelewa kuvunwa, kuna uwezekano mkubwa kuwa vitakuwa tayari vimeambukizwa.

Mhojaji:
Unazuiaje kuchunuliwa kwa viazi?

Bw. Njiru:
Ili kuepuka uharibifu, ni vizuri kukata sehemu ya juu ya ardhi ya mimea hii siku 10 kabla ya kuvuna viazi batata. Jambo hili hupatia viazi muda wa kuunda ngozi iiyokomaa na ngumu. Lazima wakulima wahakikishe pia kuwa hawavuni wakati wa mvua. Ikiwa huwezi kuepuka kuvanya hivyo, lazima uviache viazi kukauka katika matuta kwa muda wa takriban siku 10 katika sehemu baridi.

Mtangazaji:
Asante Bw. Njiru. Hebu tuwaeleze kwa kifupi wasikilizaji wetu mambo muhimu tuliyozungumzia. Kwanza, vuna viazi wakati ngozi yake imekuwa ngumu lakini usichelewe. Pili, chagua viazi ambavyo havina alama ya kudhulika. Tatu, tumia safu mbadala za maranda ya mbao katika uhifadhi. Na mwisho, chagua na uondoe viazi vyo vyote vilivyoharibika.

SFX:
Sauti ya pikipiki ya magurudumu matatu inayoongezeka na kisha kulainika chini ya mtangazaji.

Mtangazaji:
Naondoka huku nikiwaacha Kinungi na Githeya wakipakia mzigo wao wa mwisho wa viazi batata. Anaweza kufunga safari nyingine kuelekea sokoni kwa sababu ya mbinu yake mpya ya kutumia maranda ya mbao kuhifadhi viazi batata vyake.

SFX:
Sauti ya pikipiki ya magurudumu matatu inayoongezeka na kisha kulainika chini ya mtangazaji.

Mtangazaji:
Endapo una swali lo lote kuhusu mada ya leo ama hata wasiwasi kuhusu jambo lo lote katika shamba lako, tuma ujumbe mfupi kupitia nambari 0715 916 136. The Organic Farmer atakupigia simu au akutumie barua. Hadi wiki ijayo saa kama hizi, jina langu ni ……….. nikikutakia usiku wenye baraka.

Muziki wa kumalizia, hadi nukta nne kisha ufifie na kutoweka.

Acknowledgements

Yamechangiwa na: John Cheburet, The Organic Farmer, Nairobi.
Yamehaririwa na: Dr. Victor Mares, production systems agronomist and post-harvest expert, the International Potato Center (CIP).

Information sources

Mahojiano na mkulima na afisa kilimo wa wilaya, October 12, 2009.
Mtandao wa FAO: Storage and Processing of Roots and Tubers in the Tropics.
http://www.fao.org/DOCREP/X5415E/x5415e04.htm
Infonet-Biovision, undated. Potato. http://www.infonet-biovision.org/default/ct/139/crops