Ujumbe kwa mtangazaji
Taarifa kwa Watangazaji
Wakulima wengi katika kijiji cha Kisiwani, wilayani Same, kaskazini mwa Tanzania mkoani Kilimanjaro, huchagua na kuhifadhi mbegu kwa ajili ya msimu ujao, kwa kufuata mbinu za kilimo. Wakulima wa kijiji hiki wamekuwa wakitumia njia hizi kwa miaka kadhaa sasa, na wanasema kuwa wanapata matokeo bora zaidi kuliko kutumia mbegu bora kutoka kwenye maduka ya kilimo, kwani mbegu bora wakati mwingine hushindwa kuota kwasababu ya kuhifadhiwa kwa muda mrefu au sababu nyinginezo. Wakulima pia wanasema kwamba mbegu za kienyeji hustahimili wadudu, magonjwa, na mabadiliko ya hali ya hewa; kwamba hakuna mbolea, dawa za kuulia wadudu, au dawa za ukungu
zinazohitajika kwa mbegu za kienyeji; kwamba chakula kinachozalishwa kutokana na mbegu za kienyeji ni bora na kina virutubisho zaidi kuliko mbegu zilizoboreshwa; kwamba chakula kinachopikwa kwa mbegu za kienyeji ni bora zaidi; na kwamba mbegu za kienyeji huongeza bayoanuwai na uhifadhi wa asili. Wanaongeza kuwa mbegu wanazochagua na kuhifadhi zinaweza kutumika hata baada ya misimu mitatu ya upandaji ya kilimo zikihifadhiwa vizuri na haziharibiwi na wadudu na magonjwa.
Wakulima hawa wanakabiliwa na changamoto ya kuchagua na kuhifadhi mbegu, ikiwa ni pamoja na hali ya hewa na uhaba wa vifaa vya kuhifadhi mbegu, lakini wanaendelea kuhifadhi mbegu kienyeji. Katika andiko hili, tunasikia hatua ambazo wakulima wanachukua kuhifadhi na kuokoa mbegu, ikiwa ni pamoja na kulima, kuvuna, kuhifadhi na kulinda mbegu dhidi ya wadudu na magonjwa. Tunazungumza na Bwana Omary, Afisa Ugani wa Wilaya ya Same, jinsi anavyowasaidia wakulima, na pia tunazungumza na mkulima aitwaye Emmanuel Kakore, ambaye anaelezea kwa undani jinsi wakulima
wanavyochagua na kuhifadhi mbegu kwa msimu ujao, kwa kuzingatia mbinu ya kilimo.
Ikiwa ungependa kuzalisha programu sawa nah ii kuhusu kuchagua na kuhifadhi mbegu kwa kutumia maarifa na mbinu za kilimo-ikolojia, unaweza kutumia andiko hili kama mwongozo. Ukiamua kutumia andiko hili kwenye kipindi chako cha kawaida, unaweza kutumia waigizaji wa sauti au watangazaji wa redio kuwakilisha wahojiwa. Katika hali hii, tafadhali wajulishe hadhira yako mwanzoni mwa kipindi kwamba hizi ni sauti za waigizaji wa sauti na si wahojiwa halisi.
Ikiwa ungependa kutafiti na kuunda programu yako mwenyewe kuhusu mada hii, unaweza kuwauliza wakulima na wataalam wengine maswali yafuatayo:
- Kwa nini unapendelea kuchagua na kuhifadhi mbegu zako?
- Je, ni vigezo gani vya kuchagua na kuhifadhi mbegu fulani?
- Je, ni aina gani ya hifadhi na mbinu unazotumia kuhifadhi mbegu?
- Je, unalindaje mbegu zilizohifadhiwa dhidi ya wadudu na magonjwa?
Muda wa program, ikijumuisha utangulizi na ukamilishaji, dakika 15-20.
Script
SFX:
SAUTI YA JUU HALAFU YA CHINI
MTANGAZAJI:
Mabibi na mabwana, karibuni katika kipindi cha leo, ambapo tutakwenda kujifunza kuhusu kuchagua na kuhifadhi mbegu za msimu ujao kwa mbinu za kilimo.
Ili kulizungumzia hili, nilimtembelea Bwana Emmanuel Kakore, mkulima anayeishi kijiji cha Kisiwani, Wilaya ya Same katika Mkoa wa Kilimanjaro, kaskazini mwa Tanzania. Emmanuel Kakore amefanya kilimo cha ikolojia kwa takriban miaka tisa.
Lakini kabla sijazungumza naye nitazungumza na afisa ugani wa wilaya, Mheshimiwa Omary Mhina.
Habari za asubuhi, Bwana Omary, na asante kwa wakati wako. Niko hapa kukuuliza maswali machache kuhusu kuchagua mbegu na kuzihifadhi kwa msimu ujao kwa kutumia mbinu za kilimo.
Lakini kwanza, ni mazao gani yanayolimwa kwa wingi katika wilaya yako?
OMARY MHINA:
Wilaya ya Same imegawanywa katika kanda tatu za kilimo-ikolojia: nyanda za chini, nyanda za kati na nyanda za juu, na wakulima kwa kawaida hulima mahindi, maharagwe, alizeti, mtama, mihogo, viazi, miti ya matunda na mboga mboga. Kahawa hulimwa zaidi katika ukanda wa kati, na mpunga katika ukanda wa nyanda za chini.
MTANGAZAJI:
Ni wajkati gani mzuri wa kulima katika eneo lako?
OMARY MHINA:
Mara nyingi, msimu wa kilimo huanza mwezi wa Septemba na Oktoba, ingawa kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, msimu unaweza kuanza mwezi wa Novemba na Desemba. Kwa hivyo wakati wa kuvuna unaweza kuwa kutoka mwezi Aprili hadi Juni.
MTANGAZAJI:
Kilimo cha Ikolojia ni nini?
OMARY MHINA:
Kilimo cha ikolojia ni kilimo cha mfumo wa ikolojia ambapo wakulima hawatumii mbolea za viwandani wala dawa za kuulia wadudu. Ni kilimo ambacho kinahifadhi na kuheshimu uhusiano wa viumbe hai vyote na mazingira yao ili kupata matokeo mazuri. Badala ya pembejeo za viwandani, hutumika dawa za asili na/au za kuua wadudu na mbolea ya mimea inayotokana na kuoza kwa mimea na samadi ya wanyama. Hii ni rafiki wa mazingira kwani haidhuru udongo wala mazao, na ni salama kwa walaji na kwa viumbe hai wengine.
MTANGAZAJI:
Kuna tofauti gani kati ya kilimo cha ikolojia na kilimo cha kawaida linapokuja suala la kuchagua na kuhifadhi mbegu?
OMARY MHINA:
Wakulima wengi wanapendelea kutumia mbegu zilizochaguliwa kutoka kwenye kilimo cha ikolojia kwa msimu ujao. Katika hali hii, mtu ambaye hana mbegu anaweza kupata au kununua kutoka kwa jirani kwasababu wakulima kwa kawaida hubadilishana au hugawana mbegu. Mkulima mwenye ujuzi kwa kawaida huchagua mimea yenye afya zaidi kwa ajili ya mbegu, huiruhusu ikauke vizuri, na kisha kuipanga na kuichambua kabla ya kuhifadhi. Wale wanaopendelea aina ya mbegu zilizoboreshwa kawaida huzinunua kutoka kwenye maduka ya kilimo. Tofauti ni kwamba mbegu zilizochaguliwa na kuhifadhiwa kulingana na kanuni za kilimo cha ikolojia zinaweza kuhifadhiwa kwa muda mrefu na bado kuwa na manufaa, ikiwa zimehifadhiwa vizuri.
MTANGAZAJI:
Je, unawasaidiaje wakulima kuchagua na kuhifadhi mbegu?
OMARY MHINA:
Nawashauri wawe na eneo maalumu la shamba kwa ajili ya kuoteshea mbegu hasa mahindi na maharage. Mavuno yote kutoka kwa shamba hili huchaguliwa, kukaushwa, kuwekwa kwenye vifaa vya kuhifadhi, na kuhifadhiwa kama mbegu kwa ajili ya msimu ujao.
MTANGAZAJI:
Je, wakulima hutunzaje mbegu kwa ajili ya kuhifadhi?
OMARY MHINA:
Kwa maharage, mazao yanapokomaa vizuri na tayari kukaushwa shambani kwa maandalizi ya kuvunwa, majani yanageuka kutoka kijani kibichi hadi manjano au hudhurungi. Kisha wakulima hung’oa mimea hiyo na kueneza mazao yaliyovunwa kwenye sehemu tambarare kama vile sakafu, mwamba tambarare, au kwenye turubai. Wanaacha mazao kukauka kabisa kwenye jua kwa siku kadhaa, kulingana na jinsi mazao yalivyokuwa makavu yalipovunwa na hali ya hewa ya mahali hapo.
Kupura huondoa mbegu za maharagwe kutoka kwenye maganda yakishakauka, na kunaweza kufanywa angalau kwa njia mbili tofauti. Kwanza, ikiwa kuna mazao machache tu, wakulima hushikilia tu mizizi na kuipiga mimea. Na pili, wakulima wanaweza kukusanya mazao yote yaliyokaushwa na kuyapiga kwa fimbo nzito.
Baada ya kupura, wakulima hupepeta maharagwe ili kuondoa mabaki yasiyotakiwa, uchafu, au makapi. Njia hii pia hutumiwa wakati wa kuchagua nafaka za mahindi.
Wakulima huanza kuchagua mbegu wakati mazao yanakua. Na uteuzi wa mbegu unaendelea hadi mbegu zilizochaguliwa zimehifadhiwa, kwa kuzingatia sifa fulani. Mbegu zilizohifadhiwa lazima ziwe kubwa, zionekane zenye afya zisizo na uharibifu wa wadudu na magonjwa, na kavu vya kutosha.
MTANGAZAJI:
Wakulima huchaguaje mbegu zilizo nzuri?
OMARY MHINA:
Wakati wa kupepeta mbegu kwenye upepo, mbegu zote zilizoharibika, zilizoshambuliwa na zilizoharibiwa huondolewa. Ikiwa zinabaki, zinaondolewa tu kwa mkono, na kisha mbegu zilizochaguliwa zinakuwa ziko tayari kwa kuhifadhiwa.
MTANGAZAJI:
Vipi kuhusu mahindi? Wakulima huchaguaje mbegu zilizo nzuri za mahindi?
OMARY MHINA:
Kama ilivyo kwa mazao mengine, uteuzi wa mbegu huanza wakati mazao yangali shambani. Mazao yanayopendekezwa zaidi ni yale ya katikati ya shamba ili kupunguza athari za uchavushaji mtambuka kutoka kwa mashamba ya mahindi yaliyo karibu. Inapendekezwa kuwa mahindi yahifadhiwe kama mbegu yavunwe yakishakomaa. Baada ya kuvuna, baadhi ya wakulima huchukua mmea mzima wa mahindi pamoja na majani, na kuuweka juu ya paa zao za jikoni. Kisha, wanapopika, moshi wa kuni unaua wadudu wanaoweza kuvamia nafaka za mahindi. Lakini wakulima wengi huvuna mahindi yakiwa yamekauka shambani na majani kuwa na rangi ya kahawia. Wanaondoa mabua na kuyakausha kwenye jua kwa muda wa siku tatu hivi, kulingana na hali ya hewa. Ninawafundisha kugawanya mhindi katika sehemu tatu: A, B, na C.
“A” ni sehemu ambayo imeunganishwa kwenye bua la mahindi. “B” ni sehemu ya kati na ile tunayopendekeza itumike kama mbegu, na “C” ni sehemu nyingine. Mbegu katika “B” inapaswa kuwa kubwa kama “A” na “C” kwa pamoja. Nafaka za sehemu A na C mara nyingi huwa ndogo kwa ukubwa, na kwa hivyo hazifai kuhifadhiwa kama mbegu. Lakini nafaka kwenye sehemu B ni kubwa na yenye afya na hivyo ni nzuri kwa kuhifadhiwa kama mbegu.
MTANGAZAJI:
Je, wakulima huhifadhi vipi mbegu wanazochagua kwa msimu ujao?
OMARY MHINA:
Kwa kawaida wakulima hutumia magunia ya kawaida ya kuhifadhi yanayouzwa kwenye maduka au maduka ya kilimo, yenye uwezo wa kubeba kilo 80 hadi 120. Wao hufunga mbegu za mahindi au maharagwe na kuhifadhi magunia katika chumba maalum cha kuhifadhia nyumbani—ama katika chumba tofauti na mazao yao yaliyohifadhiwa au katika sehemu tofauti ya chumba kimoja cha kuhifadhia. Ikiwa wanataka kuuza mbegu zilizohifadhiwa, wakulima huziweka kwenye gunia ambalo huhifadhi kilo 10 au 20. Hawauzi mahindi yaliyowekwa kwenye paa za jikoni.
MTANGAZAJI:
Je, mbegu zinaweza kuhifadhiwa kwa muda gani na bado zikaweza kutumika?
OMARY MHINA:
Wakulima wengi huweka mbegu za kutosha kudumu kwa miezi sita tu hadi msimu ujao, lakini zinaweza kuhifadhiwa kwa miezi 24. Ikiwa hazijavamiwa na wadudu, mbegu zilizohifadhiwa zinaweza kuwa muhimu kwa misimu miwili ya kilimo.
MTANGAZAJI:
Je, unawashauri vipi wakulima kupambana na wadudu na magonjwa na kuweka mbegu zibaki salama?
OMARY MHINA:
Ninawashauri kutumia mbinu za kienyeji na rafiki kwa mazingira kama vile dawa za kuulia wadudu na magonjwa, kwa mfano, kumwaga majivu kwenye majani ya mazao ambayo yameshambuliwa na wadudu.
Pia, wakulima wanaweza kusaga majani kutoka kwenye mwarobaini (Azadirachta indica) na mmea wa pilipili na kuyatia maji. Hii inaweza kunyunyiziwa kwenye nafaka za mahindi na maharagwe kabla ya kuhifadhi ili kulinda dhidi ya wadudu. Lakini mbegu zilizonyunyiziwa lazima zikaushwe vizuri kabla ya kuzihifadhi.
MTANGAZAJI:
Je, ni changamoto zipi ambazo wakulima wanakutana nazo katika kuchagua na kuhifadhi mbegu?
OMARY MHINA:
Changamoto mojawapo ni ukosefu wa vifaa vya kuhifadhi dawa za kuua wadudu ambazo wanatengeneza. Wakulima hawana vifaa vinavyofaa vya kuhifadhia, kwa hivyo hutumia vifaa vinavyopatikana kama vile chupa za maji za kawaida. Pia, kwa ajili ya kutengeneza viuatilifu vya kienyeji, wakulima hawana vifaa vya kupima wingi wa viambatisho vya viuatilifu vinavyotengenezwa kienyeji. Kwa hivyo, wanakadiria tu idadi ya viungo vya dawa.
MTANGAZAJI:
Asante, Bwana Omary, kwa muda wako na mchango wako.
SFX:
KIPANDE KIFUPI CHA MZIKI, HALAFU FIFISHA.
MTANGAZAJI:
Wasikilizaji wapendwa, ni matarajio yangu kuwa mmejifunza mengi kutoka kwa Bw. Omary, afisa ugani. Hebu sasa nikupeleke kwa Emmanuel Kakore kwa zaidi kuhusu mitazamo ya wakulima kuhusu mifumo ya mbegu inayotumiwa na wakulima.
Emmanuel Kakore ni mkulima anayeishi katika kijiji cha Kisiwani, Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, kaskazini mwa Tanzania. Amefanya kilimo cha ikolojia kwa takriban miaka tisa.
Habari za asubuhi, Emmanuel Kakore. Ninataka kukuuliza maswali machache kuhusu kuchagua na kuhifadhi mbegu kwa ajili ya msimu ujao kwa njia za ikolojia ya kilimo.
Unalima mazao gani?
EMMANUEL KAKORE:
Nalima zaidi mahindi, maharagwe, mihogo na ndizi.
MTANGAZAJI:
Je, ni kwa namna gani unachagua na kuhifadhi mbegu kwa ajili ya msimu ujao?
EMMANUEL KAKORE:
Kwanza, nina shamba maalum la takriban nusu ekari ambalo ninalitumia kwa ajili ya kupanda mazao kwa ajili ya mbegu kwa msimu ujao. Kwa mahindi na maharagwe, wakati wa kuvuna na mbegu zimekauka shambani, tunavuna na kuzikausha kwenye jua. Zikiwa zimekauka vya kutosha, tunazichanganya na dawa za kienyeji ili kuzilinda dhidi ya wadudu, na tunazifunga na kuzihifadhi kwa usalama kwa ajili ya msimu ujao. Pia tunawauzia wakulima wengine wakati wa msimu wa kilimo.
MTANGAZAJI:
Ni wakati gani mzuri wa kulima shamba lako la mbegu?
EMMANUEL KAKORE:
Msimu mfupi wa mvua huanza mwishoni mwa Septemba au Oktoba, lakini kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, siku hizi msimu unaweza kuanza Novemba, Desemba, au Januari. Kwa hiyo, wakati mvua zinapoanza, wakulima hupanda na kisha kujiandaa kupalilia, kujazia pale ambapo hayajaota, kuweka udongo, kudhibiti wadudu na magonjwa, kumbuka kuwa pembejeo zote zinafuata kanuni za ikolojia ya kilimo.
MTANGAZAJI:
Je, ni muda gani mzuri wa kuvuna na kuchagua mbegu?
EMMANUEL KAKORE:
Kwanza mimi huzingatia hali ya hewa, kwasababu wakati mvua zinaisha, hufuatia wakati wa baridi, na hakuna jua la kutosha kwa ajili ya kukausha mazao. Kwa mahindi, huwa nainamisha mimea ya mahindi ili kuzuia nafaka zisioze kutokana na mvua.
Kwahiyo hali ya hewa inapokuwa nzuri na vipindi vya jua vya kutosha kwa siku, mimi huvuna mazao yangu na kuyakausha kwa siku tatu hadi tano, kulingana na jua ni kiasi gani kwa siku.
MTANGAZAJI:
Je, taratibu za uvunaji wa mbegu hasa mahindi ni zipi?
EMMANUEL KAKORE:
Wakati mahindi yamekauka shambani na majani yanageuka na kuwa kahawia, hii ni ishara kwamba ni wakati wa kuvuna. Ninakata masuke, na kuacha mimea ya mahindi shambani, kisha napeleka mavuno nyumbani. Tunaondoa maganda na, ikiwa hali ya hewa ni nzuri, tunakausha kwenye jua kwenye turubai kwa siku kadhaa.
MTANGAZAJI:
Je, unatunzaje mbegu kwa ajili ya kuzihifadhi?
EMMANUEL KAKORE:
Wakati mahindi yamekauka vya kutosha, mimi hutoa maganda na kutenganisha yale yenye nafaka kubwa na yale yenye nafaka ndogo. Ninapanga mbegu za mahindi kwa kugawanya kila mhindi katika sehemu tatu, kwa maneno mengine, kuondoa sehemu ndogo za juu na za chini. Ninachukua sehemu ya kati, ambayo mara nyingi ina nafaka kubwa na bora kuliko sehemu nyingine mbili, na hizi ni mbegu ninazohifadhi kwa ajili ya msimu ujao.
MTANGAZAJI:
Unajuaje wakati ambapo mbegu zimekauka vya kutosha kwa ajili ya kuhifadhiwa?
EMMANUEL KAKORE:
Mara nyingi sisi hutumia njia kama vile kumwaga nafaka kwenye sakafu na kusikiliza sauti inayotoa. Pale ambapo nafaka zimekauka vya kutosha kuhifadhi, hutoa sauti tofauti na kutawanyika sehemu kubwa. Mbali na hayo, mtu anaweza kuuma kwa meno nafaka fulani na kugundua ikiwa zimekauka vya kutosha. Sisi pia huweka kiasi kidogo cha chumvi katika chupa yenye kuonyesha ndani na mbegu na kuiacha chupa kwa saa kumi na mbili. Ikiwa chumvi inayeyuka, inamaanisha kuwa mbegu hazijakauka vya kutosha. Lakini ikiwa chumvi haijayeyuka, basi tunajua kwamba mbegu ni kavu na tayari kwa ajili ya kuhifadhiwa.
MTANGAZAJI:
Ni aina gani ya vifaa vya kuhifadhia ambavyo wewe unatumia?
EMMANUEL KAKORE:
Ni changamoto sana kwani hatuna vifaa maalum vya uhifadhi wa hali ya juu. Badala yake, tunatumia vyombo vya kienyeji kama magunia. Tunaweka mbegu kwenye magunia, tunapanga vipande vya mbao kwenye sakafu, na kisha tunaweka magunia juu ya mbao. Hii husaidia kulinda mbegu kutokana na kunyonya unyevu kutoka kwenye sakafu.
Pia nanunua magunia madogo yanayohifadhi kilo 10 au 20, na ninahifadhi mbegu ninazokusudia kuziuza kwenye magunia haya. Pia mimi hutumia vyombo vya kuhifadhia vya plastiki kama ndoo.
MTANGAZAJI:
Vyombo vya kuhifadhia unavyotumia vina ufanisi gani?
EMMANUEL KAKORE:
Kwa kweli, vinafaa – tunaweza kuhifadhi mbegu kwa muda mrefu bila shida yoyote. Kinachohitajika ni kulinda mbegu kutokana na unyevu. Kwa hivyo ninahakikisha kuwa chumba ninachohifadhi mbegu kimefungwa kila wakati na sakafu haitoi unyevu, haswa ninapohifadhi mbegu kwenye magunia.
MTANGAZAJI:
Je, mbegu zinaweza kuhifadhiwa kwa muda gani na bado zikafaa kutumika?
EMMANUEL KAKORE:
Ikiwa zimehifadhiwa vizuri na kwa usalama, na hakuna wadudu na wanyama wadogo kama panya huvamia, mbegu zinaweza kuwa na manufaa kwa takriban misimu mitatu bila tatizo lolote. Lakini ninapohifadhi mbegu kila baada ya mavuno, mimi hutumia mbegu hizi kwa msimu ujao na kuuza mbegu zozote za ziada.
MTANGAZAJI:
Je, unazilindaje mbegu ili kuhakikisha kuwa zinafaa kwa msimu ujao?
EMMANUEL KAKORE:
Jambo muhimu ni kulinda mbegu dhidi ya wadudu kama vile wadudu waharibifu wa mahindi, wadudu kama vile panya na unyevunyevu. Kwa hivyo tunatengeneza dawa za kienyeji ambazo tunanyunyizia kwenye mbegu kabla ya kuhifadhi ili kuzilinda dhidi ya wadudu. Ninahakikisha kwamba chumba ninachohifadhi mbegu hakina unyevu, na kwamba sakafu na dirisha hairuhusu unyevu kufikia mbegu.
MTANGAZAJI:
Je, ni dawa gani za kienyeji unazotumia kudhibiti wadudu waharibifu wa mbegu?
EMMANUEL KAKORE:
Mimi hutumia majani ya mwarobaini, pilipili, alizeti mwitu, kitunguu saumu, na mkojo wa ng’ombe.
MTANGAZAJI:
Je, unaandaje dawa zako za kuua wadudu?
EMMANUEL KAKORE:
Kwa mkojo wa ng’ombe, tunaikusanya na kuihifadhi kwenye ndoo kwa siku ishirini na moja. Kisha tunasaga alizeti pori na vitunguu saumu na kuvitia maji na kukoroga pamoja na mkojo wa ng’ombe ambao umehifadhiwa kwa siku 21, kisha tunautumia kama dawa ya kuua wadudu.
Kando na hayo, tunasaga majani ya mwarobaini na alizeti mwitu, na kuchanganya na maji kisha hukoroga, na kutumia kitu cha kunyunyizia kama dawa ya kuua wadudu.
Pia tunatayarisha dawa za wadudu katika fomu ya poda. Viambatanisho hivyo ni majivu ya kinyesi cha ng’ombe kilichochomwa kilichochanganywa na mahindi au nafaka nyinginezo, unga wa pilipili na unga wa majani ya mwarobaini. Unachanganya kwa uwiano wa 1: 1: 1. Kisha unachanganya gram 250 za unga na kilo 20 za mbegu.
SFX:
SAUTI AU MZIKI, HALAFU FIFISHA
MTANGAZAJI:
Mabibi na mabwana, huu ndio mwisho wa programu yetu. Tumesikia jinsi wakulima wanavyochagua na kuhifadhi mbegu za msimu ujao katika kilimo cha ikolojia katika wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, kaskazini mwa Tanzania.
Tulimsikia Bw. Omary Mhina, afisa ugani na mtaalamu wa kilimo katika eneo hili, na tulimsikia Bw. Emmanuel Kakore, mkulima anayechagua na kuhifadhi mbegu zake kwa ajili ya msimu ujao katika shughuli zake za kilimo cha ikolojia.
Tunatumahi kuwa umejifunza mambo mengi wakati wa programu hii. Asante na uwe na siku njema.
Acknowledgements
Shukrani
Imechangiwa na: Enos Mathias Lufungulo, mwandishi wa habari wa kujitegemea
Imehaririwa na: Eliud M. A. Letungaa. Ofisi ya Kilimo na Mifugo, Mtandao wa Vikundi vya Wakulima na wafugaji Mkoa wa Arusha (MVIWAARUSHA).
Information sources
Vyanzo vya taarifa
Mahojiano:
Omary Mhina, afisa ugani, Wilaya ya Same
Emanuel Savopo Kakore, mkulima, Kijiji cha Kisiwani
Leticia Emmanuel, mkulima, Kijiji cha Kisiwani
Yusuph John, mkulima, Kijiji cha Kisiwani
Ester Philipo, mkulima, Kijiji cha Kisiwani
Mahojiano yote yalifanyika mwezi tarehe 26 June, 2022.
Rasilimali hii imeandaliwa kwa msaada wa kifedha kutoka kwa taasisi ya Biovision Foundation.