Backgrounder
Katika wiki chache zilizopita, washirika wetu wa utangazaji walitutumia maswali yao ya kushinikiza kuhusu ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19). Ili kuwajibu, tuliunda maswali haya yanayoulizwa mara nyingi (FAQs), tukitumia mamlaka yenye sifa na vyanzo vya habari vilivyothibitishwa kama vile Shirika la Afya Duniani.
Hapa kuna majibu ya baadhi ya maswali yako yanayoulizwa mara nyingi (FAQs) kuhusu ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19).
Kanusho: Nakala hii haichukui nafasi ya ushauri wa kitaalam wa matibabu. Ikiwa una maswali maalum juu ya afya yako, wasiliana na mamlaka ya afya ya eneo lako mara moja.
Habari za msingi
Ugonjwa wa virusi vya Corona (COVID-19) ni nini?
Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni, ugonjwa wa virusi vya Corona (COVID-19) ni ugonjwa unaoambukiza unaosababishwa na virusi vipya vilivyogunduliwa. Virusi hivi ni familia ya virusi vya corona, ambavyo hujumuisha mafua.
Kwanini inaitwa COVID-19?
Jina COVID-19 linatokana na maneno “Virusi vya Corona” na “ugonjwa”, ambayo yamefupishwa na kuwa COVID. Namba 19 iliongezwa kuashiria kwamba virusi hivi vipya viligundulika mnamo mwaka 2019. COVID-19 pia huitwa virusi vya corona, virusi vipya vilivyogunduliwa vya corona na SARS-COV-2, ni jina lake la kisayansi.
Ugonjwa wa virusi vya Corona (COVID-19) ulitokea wapi?
Ugonjwa wa virusi vya Corona (COVID-19) uligunduliwa kwa mara ya kwanza huko Wuhan, China ambapo inawezekana ulitoka kwa mnyama. Tangu wakati huo, wanasayansi walifanya tafiti ambazo zinathibitisha kwamba virusi ni vya asili na havikutengenezwa katika maabara.
Kwa nini mlipuko wa sasa wa ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) unaitwa janga?
Mnamo mwezi Machi 2020, ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) ulitangazwa kuwa janga na Shirika la Afya Ulimwenguni kwa sababu unaathiri idadi kubwa ya watu katika eneo kubwa la ulimwengu.
Kila nchi imeathiriwa na ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19)?
Watu wameambukizwa na wamekufa kutokana na ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) katika nchi takribani 200 ulimwenguni, pamoja na zaidi ya nchi 40 za Kiafrika. Kwa habari mpya juu ya idadi ya kesi za ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) katika kila nchi na takwimu zinazohusiana, angalia: https://www.worldometers.info/coronavirus/#countries.
Kwanini ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) ni hatari?
Virusi hivi ni hatari kwasababu vinaenea kwa urahisi na vinaweza kuleta matatizo makubwa ya kiafya.
Kuna tofauti gani kati ya ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) na Ugonjwa sugu wa mfumo wa kupumua (SARS)?
Virusi ambavyo vilisababisha ugonjwa sugu wa mfumo wa kupumua (SARS) vipo katika familia moja ya virusi vya corona kama ilivyo kwa ugonjwa wa corona (COVID-19). Ni ngumu sana kueneza virusi vinavyosababisha SARS, lakini magonjwa kutokana na SARS kwa ujumla ni makubwa zaidi.
Maambukizi na mambo hatarishi
Ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) unaenea vipi?
Ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) husambazwa na matone au majimaji ambayo hutolewa hewani wakati mtu aliyeambukizwa anakohoa, kupiga chafya au anatoa hewa nnje wakati wa kupumua. Watu wanaweza kuambukizwa kwa kugusana na matone au majimaji haya hewani au kwa kugusa maeneo ambayo matone au majimaji haya yametua. Njia ya kawaida ambayo ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) unaenea ni kutoka kwa mtu mmoja hadi mtu mwingine.
Matone au majimaji yanayosababisha ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) yanaweza kuishi juu nyuso za vitu kwa muda gani?
Wanasayansi wanafikiria kwamba matone au majimaji yanayosababisha maambukizi ya ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) yanaweza kuishi kwenye ubao kama karatasi kwa chini ya masaa 24 na kwenye kitu cha plastiki au chuma kwa hadi siku mbili au tatu. Ili kusaidia kuzuia maambukizi kutoka katika nyuso za vitu vilivyoguswa mara kwa mara, safisha vitu hivyo mara kwa mara kwa maji na sabuni au kitu cha kutakasa chenye sabuni.
Ni nani aliye hatarini zaidi kwa ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19)?
Watu walio hatarini zaidi kwa ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) ni wazee na watu walio na hali za magonjwa kama vile ugonjwa wa kisukari, shinikizo la damu, shida ya moyo, na saratani, ambayo hupunguza uwezo wa mfumo wao wa kinga kupambana na virusi. Sababu za kijamii na kiuchumi kama vile umaskini pia huongeza hatari ya kuambukizwa ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19), kwa sehemu kwasababu ya ukosefu wa rasilimali ili kuhakikisha usafi sahihi. Wanawake wako hatarini zaidi kwasababu huwa na jukumu la kutunza wagonjwa katika familia au wanajamii na kwasababu wanawajibika kwa wafanyikazi wengi wa afya.
Kuna aina ya kundi la damu ambalo liko hatarini zaidi kwa ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19)?
Wanasayansi wanaotafiti hili hawajapata uhusiano wa wazi kati ya aina ya kundi la damu na maambukizo ya ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19).
Ni kweli kwamba ugonjwa wa virusi vya corona (COVID- 19) unaua tu wazee?
Wazee wana uwezekano mkubwa wa kuumwa sana na kufa wakati wameambukizwa ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19). Lakini watu wa rika zote, pamoja na wadogo, wanaweza kuambukizwa, kuugua sana, na kufa kutokana na ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19). Wanawake na makundi mengine yaliyo hatarini wanaweza kuwa na uwezo mdogo wa kufanya maamuzi ya kutafuta matibabu na wanaweza kuwa na uwezo mdogo wa kumudu huduma za afya, sababu zote hizi mbili zinaongeza hatari.
Maambukizi: Uongo na ukweli
Wanyama wa nyumbani wanaweza kuambukizwa ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) na kupitisha virusi kwa wanadamu?
Uchunguzi umeonyesha kuwa idadi ndogo sana ya wanyama wa nyumbani wameambukizwa ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19). Lakini hakuna ushahidi kwamba ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) unaweza kuenea kutoka kwa wanyama hadi kwa wanadamu.
Ninaweza kuambukizwa ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) kupitia kuumwa na mbu?
Hapana. Hakuna ushahidi kwamba kuumwa na mbu kunaweza kusambaza virusi kwa wanadamu.
Ninaweza kuambukizwa ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) kupitia ngono?
Kama aina zingine za migusano ya mwili, kuwa karibu zaidi ya mita moja na mtu yeyote aliyeambukizwa ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) kuna hatari ya kuambukizwa.
Ninaweza kuambukizwa ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) kupitia teknolojia ya 5G?
Hapana. Virusi haviwezi kuenea kupitia mtandao, au kwa redio au televisheni. Ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) unaenea kutoka kwa mtu aliyeambukizwa kwenda kwa mtu mwingine.
Kuelewa dalili
Dalili za ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) ni nini?
Dalili kuu ni homa, kukohoa, uchovu, na shida ya kupumua.
Shida ya kupumua ni nini?
Kukosa pumzi ni hali isiyotarajiwa ya kushindwa kupumua. Lakini ni muhimu kukumbuka kwamba hii ni moja tu ya dalili kuu za ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19). Ikiwa unapata shida katika kupumua bila dalili zingine za ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19), ugonjwa wako unaweza kuhusishwa na suala linguine tofauti la kiafya. Ikiwa shida ya kupumua inaendelea, piga simu kwa mamlaka za afya katika eneo lako.
Joto gani linachukuliwa kuwa la kawaida kwa mtu mwenye afya?
Joto la kawaida la mtu mwenye afya huanzia nyuzi joto 36- 37.
Ni lini watu walioambukizwa na ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) wanaanza kuonyesha dalili?
Wakati wa wastani kati ya kuambukizwa na kuanza kuonyesha dalili ni siku tano hadi saba. Katika idadi ndogo ya kesi za maambukizi, kipindi hicho kinaweza kufikia siku 14. Asilimia ndogo ya watu huwa hawaonyeshi dalili.
Ninajuaje ikiwa nina ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) na sio homa au mafua?
Njia pekee ya kujua ikiwa una ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) ni kupitia vipimo vya daktari. Lakini kama una dalili za ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) – homa, kukohoa, uchovu, shida ya kupumua – unapaswa ujitenge kwa siku 14.
Ikiwa nina dalili, lazima niende hospitalini au nipigie simu kwanza?
Piga simu kila wakati kabla ya kwenda hospitalini. Mipangilio maalumu ya kuwahudumia watu wenye dalili za ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) na uwezo wa mifumo ya kiafya inatofautiana kati ya nchi – na ndani ya nchi.
Mapendekezo ya kubaki salama na kuwa na afya
Ninajilindaje kutokana na ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19)?
Osha mikono yako mara kwa mara kwa kutumia maji na sabuni au kitakasishi cha kileo, kaa angalau mita moja mbali na watu walio nje ya familia yako, na epuka kugusa pua yako, mdomo, macho na masikio.
Kwa nini kunawa kwa maji na sabuni ni muhimu?
Sabuni inahitajika kwa ajili ya kuua virusi vya corona (COVID-19). Kitakasishi chenye angalau 60% ya kileo (pombe) kinaweza pia kutumika kuua virusi vya corona (COVID-19) katika mikono.
Kujitenga binafsi ni nini?
Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni, watu wanapaswa kujitenga kwa siku 14 ikiwa wana dalili za ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19), kama wamekutana na mtu ambaye ana au anaweza kuwa ameambukizwa ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19), au kama wameambiwa wajitenge na mamlaka ya afya ya umma. Kujitenga binafsi kunamaanisha kukaa nyumbani na kujiepusha na maeneo ya umma ili kuzuia kuwaambukiza wengine.
Ninajitengaje mimi binafsi?
Watu katika kujitenga wanapaswa kukaa nyumbani na kuhakikisha wanakaa angalau mita moja ya umbali kati yao na wengine, pamoja na familia, na kufuatilia dalili za ugonjwa. Ikiwa haiwezekani kukaa katika chumba tofauti na kutumia chumba tofauti cha choo, weka vitanda angalau mita moja kutoka kitanda kimoja hadi kingine. Safisha mara kwa mara maeneo ambayo yanaguswa kwa kutumia sabuni na maji au kitakasa chenye sabuni. Epuka kushirikiana na wengine vitu binafsi kama mswaki, vyombo vya kula, na taulo.
Endelea kufuata mapendekezo ya Shirika la Afya Ulimwenguni ya kubaki salama na afya. Osha mikono yako mara nyingi kwa maji na sabuni au kitakasishi cha kileo. Funika pua yako na mdomo kwa kiwiko chako wakati wa kukohoa au kupiga chafya.
Matibabu: Ukweli na uongo
Kuna matibabu au tiba ya ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19)?
Hapana. Hakuna matibabu au tiba ya ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19). Watu ambao wana dalili wanapaswa kujitenga ili kuzuia kuwaambukiza wengine. Hakuna ushahidi kwamba chochote kati ya yafuatayo yanaweza kutibu, kuponya, au kuzuia ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19):
- Dawa za mafua
- Pombe
- Supu ya pilipili
- Vitamini C
- Chumvi, vitunguu saumu, au limao
- Vinywaji vya moto kama vile chai ya rangi
- Mavazi ya joto
- Hali ya joto au kujianika kwenye mwanga wa jua
- Kuoga maji ya moto
- Hydroxychloroquine
- Kujipulizia pombe au klorini mwilini
- Kunywa dawa ya kuua viini vya maradhi
- Kujifukiza pua na mdomo
- Vikausha mikono
- Miale ya taa za ultaviolet
- Dawa za kuua vimelea (antibiotics)
- Chanjo ya nimonia
Kuna chanjo ya ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19)?
Ndiyo. Read more about COVID-19 vaccines here: https://www.who.int/emergencies/diseases/novel-coronavirus-2019/covid-19-vaccines
Barakoa na glovu
Ni wakati gani ninapaswa kuvaa barakoa?
Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni, mtu yeyote ambaye ana dalili zinazohusiana na ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) au aliyepimwa kuwa na ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) anaweza kuvaa barakoa ili kuzuia kueneza virusi kwa wengine. Watoa huduma za afya wanaowahudumia watu walioambukizwa ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) wanaweza kuvaa barakoa ili kupunguza uwezekano wa kuambukizwa.
Ni aina gani ya barakoa ninapaswa kuvaa?
Barakoa za matibabu aina ya N-95 zinapaswa kutumiwa tu na wahudumu wa afya. Kila mtu mwingine anaweza kuvaa barakoa za upasuaji ambazo zinatumika mara moja tu na kutupwa au barakoa za kitambaa ambazo zinaweza kutumika zaidi ya mara moja.
Ninatumiaje barakoa kwa usalama?
Kabla ya kuvaa barakoa, osha mikono yako kwa maji na sabuni kwa angalau sekunde 20. Funga barakoa yako nyuma ya kichwa chako au masikio ili iweze kufunika mdomo wako na pua kabisa. Katika pande zote, inapaswa kutoshea uso. Kamwe usiguse barakoa ukiwa umeivaa na usitumie tena barakoa ya kutupa ambayo imekwisha kutumika.
Wakati barakoa ya kuvaa na kutupa inaloa au inachafuka, toa na itupe kwenye mfuko wa taka au kontena mara tu baada ya kuivua, na ufunge mfuko wa taka au hilo kontena. Osha mikono yako kwa maji na sabuni kwa sekunde 20 kabla ya kugusa barakoa kavu na safi.
Watu ambao wanavaa barakoa lazima waendelee kuosha mikono yao mara kwa mara kwa maji na sabuni, kuendelea kukaa angalau mita moja ya umbali kati yao na wengine, na kuepuka kugusa pua, mdomo, macho na masikio.
Ninaweza kuosha na kutumia tena barakoa?
Barakoa aina ya N-95 na barakoa za upasuaji haziwezi kutumiwa tena baada ya kutumika. Barakoa zilizotengenezwa kwa kitambaa zinaweza kutumika tena na lazima zisafishwe kila siku kwa maji na sabuni na kukaushwa vizuri kabla ya kuvaa tena.
Ninapaswa kuvaa glovu?
Shirika la Afya Ulimwenguni halipendekezi mtu wa kawaida kuvaa glovu. Kuosha mikono yako mara kwa mara kwa maji na sabuni angalau sekunde 20 au kutumia kitakasishi cha kileo ndio njia bora zaidi ya kuzuia kuambukizwa kutoka katika nyuso za vitu unavyoweza kugusa mara kwa mara.
Ikiwa unachagua kuvaa glovu, endelea kuosha mikono yako mara kwa mara na epuka kugusa pua yako, mdomo, macho na masikio.
Barakoa na glovu zitanilinda kutokana na ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19)?
Hakuna uhakikisho kwamba kuvaa barakoa na/au glovu kutazuia maambukizi. Vifaa vya kujikinga kama barakoa huwa na ufanisi zaidi pale ambapo hatua zingine za kinga kama vile kunawa mikono na kusimama kwa umbali kati ya mtu na mtu zinaheshimiwa.
Kuelewa kupona
Ni kwa muda gani mtu aliyeambukizwa ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) anaweza kuendelea kuambukiza?
Watu walioambukizwa ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) wanaweza kuambukiza kabla ya kuanza kuonyesha dalili. Inawezekana kwamba watu wanaweza kuendelea kuambukiza hata baada ya kuacha kuwa na dalili zinazohusiana na ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19). Wanasayansi bado wanatafiti kipindi hiki kinaweza kuwa cha muda gani. Kabla ya kuondoka eneo ambalo umejitenga, wasiliana na mamlaka ya afya ya eneo lako.
Baada ya kutoka eneo la kujitenga, ni muhimu kuendelea kufuata mapendekezo ya Shirika la Afya Ulimwenguni ya kukaa salama na ya afya. Osha mikono yako mara nyingi kwa maji na sabuni au kitakasishi cha kileo, kaa angalau mita moja mbali na watu walio nje ya familia yako, na epuka kugusa pua yako, mdomo, macho na masikio.
Inachukua muda gani kupona kutokana na ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19)?
Watu walio na kesi ndogo ya ugonjwa wa corona (COVID-19) kawaida hupona katika wiki mbili hadi tatu. Kesi kali zaidi zinaweza kudumu hadi wiki sita au zaidi.
Mtu ambaye amepona kutokana na ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) anaweza kuambukizwa kama atakutana tena na maambukizi?
Wanasayansi wanatafiti hili, lakini hawajaamua ikiwa maambukizo yanaweza kutokea au la.
Mtu ambaye hana dalili anaweza kuwa mwambukizaji wa ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19)?
Ndio, inawezekana kwa mtu asiye na dalili kuwa mwambukizaji wa ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19).
Mimba, malaria, na hali ya awali ya kiafya
Wanawake wajawazito wanaweza kueneza ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) kwa mtoto wao kabla ya kuzaliwa?
Wanasayansi bado wanachunguza swali hili. Kufikia sasa, hakuna ushahidi kwamba mwanamke mjamzito anaweza kueneza ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) kwa mtoto wake kabla ya kuzaliwa.
Wanawake waliambukizwa ugonjwa wa corona (COVID-19) wenye watoto wanapaswa kunyonyesha?
Kufikia sasa, hakuna ushahidi kwamba ugonjwa wa corona (COVID-19) unaweza kusambazwa kwa watoto kupitia kunyonyesha. Lakini, kama aina zingine za mgusano, kunyonyesha kuna hatari ya kuambukizwa ikiwa mama ameambukizwa ugonjwa wa corona (COVID-19) kwasababu ya ukaribu wa mwili kati ya mama anayenyonyesha na mtoto wake. Wanasayansi wanapendekeza kwamba akina mama ambao wameambukizwa ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) waoshe mikono yao kwa maji na sabuni kabla ya kunyonyesha na kuvaa barakoa kufunika pua na midomo yao wakati wanafanya hivyo. Ikiwa hii haiwezekani, ruhusu mtu ambaye hajaambukizwa ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) kumlisha mtoto.
Wanawake wajawazito wanapaswa kuendelea kwenda hospitali kwa ajili ya kliniki ya ujauzito?
Ziara za wajawazito ni muhimu ili kuhakikisha afya ya mama na kichanga. Walakini, kwasababu ya ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19), wahudumu wa uzazi wengi aidha huongeza muda kati ya tarehe za kudhuru kliniki au kuhimiza wanawake wajawazito kupiga simu hospitalini. Ikiwa una wasiwasi wowote juu ya afya yako mwenyewe au afya ya mtoto wako, pigia mtoa huduma wako wa afya wa karibu.
Niendelee kwenda hospitalini kwa matibabu ya ugonjwa wa malaria au VVU?
Kwa wakati huu, ni bora kupiga simu kabla ya kwenda hospitalini kwa sababu yoyote. Waulize wafanyakazi wa afya katika eneo lako jinsi ya kusimamia masuala yoyote yanayohusiana na afya wakati huu.
Athari pana za ugonjwa wa virusi vya Corona (COVID-19)
Ninaweza kwenda kufanya kazi?
Shirika la Afya Ulimwenguni linapendekeza kukaa nyumbani kadri iwezekanavyo ili kuzuia uwezekano wa kuambukizwa. Kwa habari maalum za nchi yako, fuata miongozo kutoka katika mamlaka ya eneo lako na ya kitaifa.
Ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) utaathiri vipi kilimo?
Ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) unaweza kuathiri vibaya watu mbalimbali na aina ya shughuli katika kilimo. Kwanza kabisa, athari za vizuizi vya kukaa nyumbani vitapunguza kiwango na aina ya chakula kinachozalishwa na kuuzwa. Ili kubaki salama, wakulima wanapaswa kudumisha suala la kukaa umbali wa angalau mita moja kati yao na wengine wanapofanya kazi shambani na kuchukua hatua za usafi kama vile kunawa mikono mara kwa mara. Vizuizi vilivyowekwa kushughulikia ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) vitaathiri wazalishaji, wachuuzi, na wengine kwenye safu ya usambazaji wa chakula, lakini kwa viwango tofauti.
Kadiri athari za kilimo na chakula zinavyokuwa wazi kwa wakati, wakulima na wengine watahitajika kurekebisha mazoea yao. Kwa kuongezea mwongozo wa Shirika la Afya Ulimwenguni, fuata mapendekezo ya kitaifa ili uwe salama na na mwenye afya.
Je, ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) unaathiri tofauti wanawake?
Wanawake wapo kwenye hatari kubwa ya kuambukizwa ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) kwasababu mara nyingi huwajibika kwa kutunza wagonjwa katika familia na jamii, na kwa sababu wanawajibika kwa wafanyakazi wengi wa huduma ya afya.
Katika hali ya dharura, mzigo wa kazi kwa wanawake unaweza kuongezeka. Wana jukumu la kufanya kazi na kutunza watoto wenye umri wa kwenda shule wakati shule / huduma za utunzaji wa watoto zimefungwa, na pia kuwatunza watu wagonjwa. Kama wafanyakazi wa afya, wanaweza kufanya kazi kwa muda mrefu, wakati bado wanawajibika kwa shughuli za nyumbani.
Kuna kuongezeka kwa kiwango cha unyanyasaji wa kijinsia, ikijumuisha unyanyasaji majumbani, wakati wa shida, wakati huduma za ulinzi zinaweza kuingiliwa na pale ambapo vizuizi vya harakati na sera za kubaki nyumbani zinaweza kutengeneza mazingira hatari zaidi ya nyumbani kwa wanawake walio katika hatari ya unyanyasaji wa majumbani.
Athari za kiuchumi za ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) zinaweza kuwaangukia wanawake bila mpangilio. Kwa mfano, upotezaji wa ajira unaweza kusababisha maamuzi kama vile kutokupeleka wasichana shuleni au ndoa za watoto.
Huduma muhimu za kiafya kwa wanawake, ikiwamo huduma za kijinsia na uzazi, zinaweza kuathiriwa wakati wa shida, ambayo inaweza kusababisha kuongezeka kwa athari mbaya za kiafya na vifo wakati wa kuzaliwa kwa mtoto.
Kwa maelezo zaidi
Ninaweza kupata wapi habari zaidi kuhusu ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19)?
Unaweza kupata habari za kuaminika na za leo kwenye tovuti ya Shirika la Afya Ulimwenguni kupitia: https://www.who.int/health-topics/coronavirus.
Ninawezaje kuepuka habari za kughushi na uwongo kuhusu ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19)?
Wakati wa kufanya utafiti na kutoa ripoti juu ya ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19), tumia habari kutoka kwa mashirika yenye kuaminika kama vile Shirika la Afya Ulimwenguni. Daima angalia tarehe ya chanzo ili kuhakikisha kuwa habari hiyo ni ya sasa na haijapitwa na wakati. Ikiwa hauna hakika juu ya habari hiyo, angalia mara mbili kutoka katika chanzo kingine. Kwa habari zaidi juu ya kuangalia ukweli na haswa kuangalia ukwel wa hababari kuhusiana na ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19), tembelea: https://africacheck.org/reports/live-guide-all-our-coronavirus-fact-checks-in-one-place/.
Acknowledgements
This resource is undertaken with the financial support of the Government of Canada provided through Global Affairs Canada.
Information sources
Centers for Disease Control and Prevention, 2020. Clinical Questions about COVID-19: Questions and Answers. https://www.cdc.gov/coronavirus/2019-ncov/hcp/faq.html
Centers for Disease Control and Prevention, 2020. Discontinuation of Isolation for Persons with COVID-19 Not in Healthcare Settings (Interim Guidance). https://www.cdc.gov/coronavirus/2019-ncov/hcp/disposition-in-home-patients.html
Harvard Health Publishing, 2020. COVID-19 basics. https://www.health.harvard.edu/diseases-and-conditions/covid-19-basics
Farid, H., 2020. Intimacy, sex, and COVID-19. Harvard Health Publishing. https://www.health.harvard.edu/blog/intimacy-sex-and-covid-19-2020041519550
Farid, H., and Memon, B., 2020. Pregnant and worried about the new coronavirus? Harvard Health Publishing. https://www.health.harvard.edu/blog/pregnant-and-worried-about-the-new-coronavirus-2020031619212#q2
Wenham, C., Smith, J., and Morgan, R., on behalf of the Gender and COVID-19 Working Group, 2020. COVID-19: the gendered impacts of the outbreak. The Lancet: Vol 395.
World Health Organization, 2020. Coronavirus disease (COVID-19) advice for the public: When and how to use masks. https://www.who.int/emergencies/diseases/novel-coronavirus-2019/advice-for-public/when-and-how-to-use-masks
World Health Organization, 2020. Q&A on coronaviruses (COVID-19). https://www.who.int/news-room/q-a-detail/q-a-coronaviruses.