Njia ya kupumnzisha Mashamba iliyoboreshwa kwa wakulima wa Afrika

AfyaMazingira na Mabadiliko ya TabianchiMiti na kilimo mseto

Backgrounder

Kuna tofauti gani kati ya njia ya asili ya kupumnzisha shamba na njia iliyoboreshwa ya kupumnzisha shamba?

Njia ya asili ya kupunzisha shamba ni kupumnzisha tu shamba kwa kutokulilima. Kawaida huachwa kwa mimea asilia kumea kwa muda mrefu ili kurejesha rutuba ya udongo. Njia iliyoboreshwa ya kupumnzisha shamba pia ni kupumnzisha shamba kwa shughuli za kilimo lakini mkulima anapanda miti jamii ya kunde, vichaka na/au mimea jamii ya kunde katika ardhi iliyopumnzishwa.

Njia zilizobereshwa za kupumnzisha shamba zinaweza kusaidiaje wakulima?

Njia zilizoboreshwa za kupumnzisha shamba zinasaidia wakulima kurejesha rutuba ya udongo katika mashamba yao haraka zaidi kuliko njia ya kawaida ya kupumnzisha shamba, kwahiyo zinasaidia wakati ambapo haiwezekani tena kupumnzisha shamba kwa muda mrefu. Zaidi ya hayo, udongo huwa na rutuba sana na mbolea kidogo inahitajika au haihitajiki ili kupata mavuno mengi.

Maendeleo ya njia zilizoboreshwa za kupumnzisha shamba

Moja ya changamoto kubwa kwa wakulima wote ni kudumisha rutuba ya udongo wao. Kwa jadi, wakulima wangerejesha rutuba ya udongo kwa kuacha sehemu ya ardhi yao bila kuilima kwa miaka mingi wakati ardhi mpya na yenye rutuba ililimwa na kupandwa mazao kwa ajili ya uzalishaji wa chakula. Hatahivyo, ongezeko la haraka la idadi ya watu, limepunguza kiwango cha ardhi inayopatikana kwa mkulima na kuunyong’onyeza mfumo huu wa asili wa kutunza rutuba ya udongo.

Kwa hivyo, kupumnzisha shamba kwa njia ya asili ambayo huchukua muda mrefu haiwezekani tena. Zimebadilishwa na zile njia za muda mfupi, zinazochukua msimu mmoja au miwili tu. Kuendelea kulima ardhi sasa pia ni njia ya kawaida ya kilimo. Kwa mfano, magharibi mwa Kenya, takribani nusu ya wakulima huacha 10% mpaka 25% ya ardhi yao ya kilimo ili kuipumnzisha wakati wa kipindi kifupi cha mvua, lakini kwasababu kipindi cha kupumnzisha mashamba hakichukui muda mrefu wa kutosha kuboresha rutuba ya udongo ya kutosha, mavuno ya mazao yanakuwa ya kiwango cha chini sana kama yale ya misimu iliyopita.

Ili kupunguza shida hii, njia zilizoboreshwa za kupumnzisha shamba zinaweza kuchukua nafasi ya njia za asili za kupumnzisha shamba. Hii inamaanisha kwamba, wakulima wanapanda miti jamii ya kunde na vichaka na/au mimea midogo midogo ya muda mfupi katika ardhi iliyopumnzishwa. Kwa muda mrefu kadri udongo ulivyo na fosforasi ya kutosha, aina hii ya kupumnzisha shamba inaweza kuwa njia stahiki ya kurejesha nitrojeni katika udongo pale yanapotumika kwa kubadilishana na mazao.

Faida ya njia zilizoboreshwa za kupumnzisha shamba

Utafiti katika sehemu zingine za Afrika umeonyesha kuwa miti na vichaka vilivyopandwa kama njia bora za kupumnzisha ardhi hujaza haraka rutuba ya udongo katika msimu mmoja au zaidi wa kilimo. Kwahiyo, zinapunguza muda unaohitajika kurejesha rutuba ya udongo. Pia inatoa malighafi nyingine kama vile kuni na vijiti kwa wakulima. Mbali na kuboresha rutuba ya udongo, mimea iliyopandwa kurutubisha ardhi, inaweza kutumika kudhibiti magugu aina ya striga (Striga hermonthica). Inaweza pia kudhibiti magugu mengine kama nyasi, hasa hasa kama mimea hii ya kurutubisha ardhi itarudiwa kupandwa mara kwa mara au imekaa kwa muda mrefu wa miezi 18 au zaidi. Kwa kuingiza biomasi kwenye udongo, muundo wa udongo pia unaboreshwa zaidi ambapo kwa mfano, uwezo wa utunzaji wa maji unaimarishwa.

Wakati gani wakulima wanaweza kuanzisha njia zilizoboreshwa za kupumnzisha mashamba?

Miti na vichaka vinaweza kuoteshwa kwa nyakati tofauti kulingana na eneo. Kwa mfano nchini Kenya mazoea ya kawaida ni kupanda miti na vichaka katika msimu mrefu wa mvua (kawaida baada ya kupalilia kwa mara ya kwanza au kwa mara ya pili, kulingana na hali ya mvua ya eneo hilo).

Inaachwa ikue yenyewe katika msimu mfupi wa mvua na kukatwa mwaka uliofuata mwanzoni mwa msimu mrefu wa mvua. Katika nnchi za kusini kama vile Malawi na Zambia ambapo hawana misimu miwili ya mvua, watu hupanda miti na vichaka baada tu ya kupanda mahindi.

Mara tu wanapovuna mahindi huacha miti. Katika msimu wa pili, hakuna mazao yanayopandwa. Katika msimu wa tatu, miti hukatwa na majani yote na takataka huingizwa kwenye udongo wakati wa kuandaa ardhi na kuitengeneza – na kwa hivyo hutumika kama mbolea. Kwahiyo njia zilizoboreshwa kwa ajili ya kupumnzisha mashamba katika maeneo yenye msimu mmoja wa mvua huachwa kwa kipindi kirefu. Njia hii inashauriwa pia kwa mashamba yenye udongo wenye rutuba kidogo sana au mashamba yaliyomea magugu aina ya striga, nyasi au magugu mengine ambayo ni magumu kudhibiti.

Ni aina gani ya mimea ya kupumnzisha shamba mkulima anaweza kupanda ili kupumnzisha shamba?

Njia ya kupumnzisha shamba iliyoboreshwa inakuwa bora zaidi ya njia ya kupumnzisha shamba ya asili – pale tu ikiwa aina ya mimea iliyotumika ni bora zaidi ya mimea ya asili iliyopo – angalau katika kuboresha kemikali na hali ya udongo. Mmea mzuri wa kupumnzisha ardhi lazima uwe na sifa zifuatazo.

 • Inakua haraka na kufunga dari haraka, kutokomeza magugu na kudhibiti mmomonyoko.
 • Ina mizizi mirefu ili kuchukua virutubisho vilivyo ndani kabisa kwenye udongo.
 • Inarekebisha nitrojeni kibaiolojia kutoka angani, kwa ujumla hutengeneza virutubishi bora.
 • Inatoa bidhaa za ziada kama vile vijiti, nafaka na lishe.
 • Haitaenea kama magugu katika maeneo yaliyopandwa.
 • Inazaa kwa urahisi mbegu zenye uwezo wa kukaa muda mrefu.
 • Inazuia wadudu na magonjwa katika eneo hilo.

Njia zilizoboreshwa za kupumnzisha shamba zinafanyaje kazi?

Mwishoni mwa kipindi cha kupumnzisha shamba, miti, vichaka na mimea jamii ya kunde hukatwa na majani yaliyooza (majani na matawi) huingizwa kwenye udongo wakati ardhi inaandaliwa kwa ajili ya upandaji wa mazao kwa msimu unaofuata. Baada ya kupumnzisha shamba kwa kutumia mimea aina ya kunde, mavuno ya mahindi yanaweza kuwa makubwa zaidi ya mara 2-3 kuliko mahindi ambayo yamepandwa kwa muda mrefu bila kuongeza mbolea. Faida za ardhi iliyopumnzishwa kwa kipindi cha miezi 8 inaweza kubakia kwa kipindi cha msimu mmoja au zaidi kulingana na kiwango cha uharibifu wa udongo. Maelfu ya wakulima magharibi mwa Kenya, kwa sasa wanatekeleza mfumo wa njia zilizoboreshwa za kupumnzisha ardhi na wameongeza mazao yao kwa kiwango kikubwa. Wengi wa wakulima hawa hurudia tena kupanda katika ardhi iliyopumnzishwa kwa njia zilizoboreshwa kila mwaka, aidha katika shamba hilo hilo moja au kwa kubadilisha mashamba.

Kupumnzisha shamba kwa aina moja ya mmea

Kupumnzisha shamba kwa kutumia aina moja tu ya mmea hufanyika kwa kupanda aina moja ya mmea katika shamba lote. Kawaida, mfumo huu unapendekezwa kwa aina ya mmea ambao hukua haraka na kutengeneza dari zito ambalo linafunika na kuua magugu. Aina ya mimea hiyo ni Crotalaria grahamiana, Crotalaria paulina na Colopogonium mucunoides (mucuna).

Kupumnzisha shamba kwa mchanganyiko wa aina mbalimbali ya mimea

Inawezekana na inafaa pia kupumnzisha shamba kwa njia zilizoboreshwa kwa kupanda safu mbadala mbili au zaidi za aina tofauti ya mimea ya kupumnzisha ardhi. Aina hii ya mimea hukua pamoja pasipo kuathiriana. Njia hii ni nzuri hasa kwa aina ya mimea inayokua polepole ambayo haitakuwa inashindana yenyewe kwa yenyewe. Kupumnzisha shamba kwa kutumia mchanganyiko wa aina mbalimbali za mimea inaweza kutoa moja au zaidi ya faida zifuatazo.

 • Aina tofauti za mimea zinaweza kutoa bidhaa anuwai, kama vile kuni, miti au majani yaliyooza na ikiwa aina moja itashindwa kuota au itaota vibaya, aina nyingine inaweza kufanya vizuri.
 • Kulingana na eneo na muda wa kupumnzisha shamba, huwa zinaongeza muda wa faida ya kupumnzisha shamba kwasababu hufanya virutubishi vya mmea kupatikana kwa muda mrefu.
 • Inafanya matumizi bora ya rasilimali zinazopatikana kama vile mwanga na nafasi.

Ifuatayo ni baadhi ya muunganiko wenye mafanikio wa aina ya mimea mchanganyiko:

Sesbania (Sesbania sesban) + siratro

Sesbania + groundnut

Sesbania + Tephrosia vogelii or Tephrosia candida

Sesbania + Crotalaria (Crotalaria grahamiana)

Tephrosia + Crotalaria

Uanzishaji wa aina ya mimea ya kupumnzisha shamba

Kwa aina ya mimea ya kupumnzisha shamba kufaidisha mazao, lazima iwe na wakati wa kutosha shambani kukua, kujilimbikizia virutubishi vingi na kutoa biomasi nyingi. Njia nyingi zinaweza kutumika kuanzisha njia bora za kupumnzisha shamba.

 • Tandaza mbegu katika shamba kati ya mazao yaliyopo, kwa mfano, na mahindi baada ya aidha palizi ya kwanza au palizi ya pili. Ikiwa unapanda maharagwe na mahindi sehemu moja, vuna maharagwe kwanza kisha panda mbegu za mmea wa kupumnzisha shamba. Mbinu hii inafaa zaidi kwa aina ya mimea iliyo na mbegu kubwa kama mucuna.
 • Panda katika safu. Panda mbegu za miti, vichaka na mimea aina ya mikunde kwa ajili ya kupumnzisha na kurutubisha shamba katikati ya safu za mazao ya chakula baada ya palizi ya kwanza au baada tu ya mazao ya chakula kuota na fukia mbegu kwa udongo. Kwa mahindi, kwa mfano, panda kwenye mitaro kati ya safu baada ya aidha palizi ya kwanza au ya pili.
 • Panda miti kama njia iliyoboreshwa kwa ajili ya kupumnzisha na kurutubisha ardhi katika njia ya asili ya kupumnzisha ardhi iliyopo. Njia mojawapo ya kufanya haya ni kwa kuchimba mashimo katika ardhi asilia na kupanda mbegu moja kwa moja ama kupanda miche. Kama magugu katika shamba ni mengi na yamesongamana na kuleta kizuizi wakati wa uchimbaji wa mashimo, yafyeke kwanza. Crotalaria grahamiana na Tephrosiavogelii zinaweza kupandwa moja kwa moja katika ardhi asilia. Kwa aina ya mimea kama Sesbania sesban ambayo ina mbegu ndogo au haikui kwa urahisi kutoka katika mbegu, kuza miche na ipande aidha katika mazao yaliyopo au katika ardhi asilia.

Baada ya kuvuna mazao ya chakula, acha miti kwa ajili ya kupumnzisha na kurutubisha ardhi ikue shambani. Ndani ya miezi 6 mpaka 8, itajifunga kwa juu na kutoa kivuli kizito chini, ambacho husaidia kuzuia ukuaji wa magugu. Kwa aina ya mimea inayokua haraka kama vile crotalaria na tephrosia, sio lazima kupalilia ardhi. Kisha panda mazao mwanzoni mwa msimu ujao.

Kupumnzisha shamba na fosforasi

Katika hatua hii, mara nyingi inahitajika kuongeza mbolea ya fosforasi, haswa katika udongo wenye upungufu wa fosforasi. Weka mbolea ya fosforasi katika shimo la kupandia au isambaze kwenye udongo. Kiasi cha fosforasi iliyotumika itategemea mazao yatakayopandwa baada ya kipindi cha kupumnzisha shamba.

Wakulima wanaweza wakatumia mbolea isiyo ya kaboni aina ya triple superphosphate (TSP) au diammonium phosphate (DAP), au fosfati ya mwamba kama Minjingu kutoka kaskazini mwa Tanzania, ambayo inaanza kupatikana magharibi mwa Kenya.

Mbolea ya Minjingu (Minjingu phosphate rock – MPR) ni unga laini wa ardhini ulio na fosforasi 13% (au theluthi mbili ya asilimia ya TSP). Inaweza kutumika kwa kuieneza sawasawa juu ya shamba lote na kuiingiza ndani ya udongo pamoja na majani kutoka kwa mimea ya kupumnzisha na kurutubisha ardhi wakati ardhi inaandaliwa kwa ajili ya kupanda mazao. Inaweza pia kuwekwa katika shimo la kupandia. Wakati wa kuitumia kulima mahindi, tumia viwango ambavyo vitatoa kilo 22 hadi 25 ya fosforasi kwa hekta kwa msimu, haswa kwenye udongo wenye fosforasi kidogo. Baadhi ya miti na vichaka kama tithonia na sesbania hujilimbikizia potasiamu katika biomasi ya majani yake. Wakati biomasi hii inapooza, potasiamu inapatikana kwa mazao. Kwa kutumia aina hii ya miti kama mfumo wa kupumnzisha na kurutubisha ardhi iliyoboreshwa, inaweza ikapunguza upungufu wa potasiamu kwa ajili ya mazao yatakayofuata kupandwa.

Toleo kamili la waraka huu lina habari zaidi kuhusu:

Watangazaji wanaweza kupata wapi habari zaidi kuhusu kilimo mseto (agroforestry) na njia za kupumnzisha mashamba zilizoboreshwa?

Kwa habari zaidi, au kupata mbegu au miche, wasiliana na:

National Agroforestry Research Centre

S.L.P 5199

Otonglo, Kisumu

Kenya

Simu: (035) 51163, 51164, 21918 and 21234

Barua pepe: icrafksm@africaonline.co.ke na kefrimas@africaonline.co.ke

World Agroforestry Centre (ICRAF)

United Nations Avenue, Gigiri

S.L.P 30677-00100 GPO

Nairobi

Kenya

Simu: +254 20 722 4000

Fax: +254 20 722 4001

Barua pepe: ICRAF@cgiar.org

Tovuti: http://www.worldagroforestrycentre.org

Au wasiliana na huduma za ugavi za kilimo katika eneo lako ambao wanaweza kukuelekeza kwa mashirika yanayojishughulisha na Kilimo mseto (agroforestry)

Acknowledgements

Mpango uliotelekezwa kwa msaada wa kifedha kutoka serikali ya Canada uliotolewa kupitia Wakala wa Kimataifa wa Maendeleo wa Canada (CIDA)

 

Toleo la Kiswahili la jarida hili limeandaliwa kwa ufadhili wa Justdiggit kupitia mradi wake wa Kisiki Hai (Farmer Managed Natural Regeneration – FMNR) ulioko mjini Dodoma.