Maswali Yanayoulizwa Mara kwa Mara kuhusu kazi za matunzo bila malipo

Masuala ya jamii

Script

Nini maana ya kazi za utunzaji bila malipo, na kwanini ni muhimu?

Kazi za utunzaji bila malipo inajumuisha usaidizi na huduma ambazo watu binafsi hutoa bila fidia ya kifedha. Hizi ni pamoja na, kwa mfano, utunzaji, kazi za nyumbani, msaada wa kihisia, na kukata kuni na kuchota maji. Kimsingi inahusisha kazi zinazowanufaisha wanafamilia, lakini inahusu kuwasaidia watu binafsi nje ya nyumba ya mtu, kama vile marafiki, majirani na wanajamii. Kazi ambazo hazina malipo mara nyingi huwa kwenye kaya na jamii, haswa kwa wanawake na wasichana.

Kwanini kazi za utunzaji bila malipo zinapaswa kutambuliwa na kuthaminiwa kama kazi?

Kazi za utunzaji bila malipo hutoa huduma ambazo haziwanufaishi tu wale wanaopokea huduma moja kwa moja, lakini jamii kwa ujumla. Kazi hizi zinaweza kufanywa na mtu, kwa mfano, mfanyakazi wa ndani. Kazi hizi zinahitaji nguvu za kimwili na kiakili ili kuzifanya, na zina gharama kubwa katika suala la muda na rasilimali. Kazi ambazo hazifanyiwi malipo mara nyingi husababisha vikwazo vya muda na kuzuia ushiriki katika kazi ya kulipwa, nafasi za uongozi, na elimu. Kutambua umuhimu wa kazi ambazo hazifanyiwi malipo katika uchumi na jamii, kungewezesha kazi hizi kuzingatiwa kama suala muhimu la sera za kiuchumi na kijamii.

Je, kazi za utunzaji bila malipo zinachangia vipi maendeleo ya kijamii na kiuchumi?

Kazi zisizo na malipo una jukumu muhimu katika kusaidia watu binafsi, familia, na jamii, na kuchangia ustawi wa jumla wa jamii. Huwezesha shughuli za kiuchumi kwa kudumisha idadi ya watu wenye afya na utendaji kazi, kukuza uwiano wa kijamii, na kuwezesha watu binafsi kushiriki katika nguvu kazi.

Kina nani wanahusika na kazi za utunzaji bila malipo?

Ulimwenguni na Afika, kusini mwa jagwa la Sahara, wanawake wana jukumu kuu la kufanya kazi ambazo hazina malipo. Kusini mwa jagwa la sahara, inakadiriwa kuwa wanawake wanatumia muda mara 3.4 zaidi ya wanaume kufanya kazi ambazo hazina malipo. Kazi za wanawake ambazo hazina malipo, mara nyingi huwa hazitambuliwi na hazithaminiwi na hii inazuia fursa za wanawake kujihusisha na shughuli za kuzalisha kipato na shughuli nyinginezo.

Je, ni matatizo gani yanayohusiana na kazi bila malipo, hasa Afrika, kusini mwa Jangwa la Sahara?

Kazi bila malipo ni tatizo kubwa katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na kwingineko kutokana na kutokuwepo kwa usawa wa kijinsia. Wale wanaofanya kazi bila malipo, wengi wao wakiwa wanawake na wasichana, mara nyingi wanakabiliwa na changamoto kama vile ufinyu wa muda, upatikanaji mdogo wa huduma za usaidizi, na kutokutambuliwa kwa kazi zao. Hii inaweza kusababisha mfadhaiko, uchovu, kutengwa, na hatari ya kiuchumi.

Wanawake ambao hawana rasilimali za kifedha mara nyingi hukabiliwa na majukumu magumu ya nyumbani yenye kuchosha na yanayochukuwa muda wao. Kazi ambazo hazina malipo mara nyingi huhusishwa na kiwango cha juu cha msongo wa Mawazo, masuala ya afya ya akili, Maisha duni, umasikini, kushindwa kutoka sehemu moja kwenda nyingine, afya duni na kuwa mtu wa hadhi ya chini. Kulingana na utafiti fulani, wahudumu wa nyumbani wa umri wa makamo na wanaofanya kazi wakati wote wana uwezekano mara tano zaidi wa kuwa na matatizo ya kiakili kuliko wanawake walio katika kazi nyinginezo, huku “kutokutambulika” kukifafanuliwa kuwa “shida ya kukumbuka, kujifunza mambo mapya, kuzingatia, au kufanya maamuzi yanayoathiri. maisha yao ya kila siku.”

Kazi sizizo na malipo zinaweza kuchochea kutokuwa na usawa wa kijinsia kwa kupunguza fursa za wanawake za elimu, ajira, na maendeleo ya binafsi, mara nyingi na kuwafanya kufanya kazi zenye ujuzi mdogo, kazi zisizo za kawaida au zisizo rasmi. Ingawa kazi bila malipo zinazuia ushiriki wa wanawake katika soko la ajira, katika ngazi ya kijamii, pia huathiri uzalishaji, ukuaji wa uchumi, na juhudi za kupunguza umaskini.

Je, suluhisho la kukosekana kwa usawa wa kijinsia katika kazi za utunzaji bila malipo ni nini?

Kazi ambazo hazina malipo zinapaswa kushughulikiwa na wahusika wengi, ikijumuisha serikali, mashirika yasiyo yasiyo ya kutengeneza faida, huduma za mashirika binafsi na familia.

Kutambua na kuthamini kazi ambazo hazina malipo

  • Serikali zinaweza kuweka sera na programu za kutambua na kuthamini kazi ambazo hazina malipo. Hii inaweza kujumuisha kampeni za kukuza ufahamu, programu za mafunzo kwa walezi wa familia, na vyeti maalum au diploma za kazi za utunzaji. Nyumbani, wanafamilia wanaweza pia kutambua na kusaidia wale wanaofanya kazi za utunzaji bila malipo.

Sawazisha kazi na maisha ya familia

  • Serikali zinaweza kupitisha sera zinazohimiza upatikanaji wa miundombinu ya msingi na huduma muhimu za umma kama vile umeme, huduma za afya, maji, malezi ya watoto, shule na usafiri. Uboreshaji lazima uhakikishe kwamba huduma zinaendelea kupatikana na watu wote wanamudu.

Boresha vifaa viwe vya kisasa ili kupunguza mzigo wa kazi za utunzaji

  • Majiko ya kisasa, vifaa vya kuosha, mashine ambazo zinaweza kufikiwa kwa urahisi, na aina nyingine za vifaa vinaweza kupunguza muda na nguvu zinazotumika kufanya kazi kama vile kuchota maji, kusindika mavuno ya familia, na kukusanya kuni. Utafiti katika maeneo ya vijijini, Senegal uligundua kuwa kuwekeza katika mifumo midogo ya mabomba ya maji uliokoa muda wa wanawake ambapo walitumia muda huo kuanzisha biashara mpya za ufugaji na bustani.

Chochea Mawazo chanya kuhusu uanaume – ondoa taswira hasi kuhusu kazi za utunzaji

  • Mabalozi wa kujitolea na viongozi wa kimila wanaweza kueneza ujumbe wa kubadilisha mawazo hasi na kuacha kazi ambazo hazina malipo kufanywa na wanawake tu. Hii inahusisha kuongeza ufahamu wa umma juu ya dhana potofu za kibaguzi zinazoendeleza ukosefu wa usawa katika kazi za utunzaji, na kuwachochea wanaume, wavulana, wanafamilia wengine, wafanyabiashara, wanasiasa na serikali, wazee, viongozi wa kidini na vyombo vya habari kuchochea hatua zenye kuleta mawazo chanya kuhusu uanaume.
  • Wanaume wana uwezekano mkubwa wa kushiriki katika kazi za matunzo pale ambapo watafahamu thamani yake na uwekezaji wa muda na ujuzi unaohitajika. Ikiwa mtazamo wa pamoja wa kazi za utunzaji ni chanya zaidi, na haswa ikiwa hili linaungwa mkono na kiongozi anayeheshimiwa, wanaume wana uwezekano mkubwa wa kushiriki.
  • Fikra potofu nyingi huendelezwa na kudumishwa ndani ya familia. Vipindi vya redio na mikakati ya mawasiliano vinaweza kutoa maono mbadala na kukuza uwajibikaji wa pamoja wa kazi za matunzo kwa kuchochea majadiliano na kubadilisha mitazamo, mienendo na maadili.

Kuza utamaduni wa kuwajibika kwa pamoja

  • Kupunguza kiasi cha kazi za matunzo zisizolipwa na kushiriki kazi za nyumbani ndani ya kaya, na pia miongoni mwa sekta binafsi na serikali, kutawawezesha wanawake kiuchumi kwasababu watakuwa na muda mwingi wa kujishughulisha wenyewe, familia zao, na kazi za kulipwa. Kampeni ya Umoja wa Mataifa ya Wanawake ya HeforShe inatoa njia kwa wanaume kusimama katika mshikamano na wanawake kwa usawa wa kijinsia, na kujumuisha Mawazo chanya kuhusu uanaume kwa kufanya kazi na wanawake na kila mmoja kujenga biashara, kulea familia, na kurudisha kwa jamii zao.

Tangaza Siku ya Kimataifa ya Utunzaji na Usaidizi

  • Mnamo Julai 2023, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilitangaza Oktoba 29 kuwa Siku ya Kimataifa ya Utunzaji na Usaidizi ili kutambua na kuangazia matatizo yanayohusiana na kazi za utunzaji bila malipo na kuangazia haja ya kushughulikia vikwazo vya kimfumo vinavyoendeleza kazi za utunzaji bila malipo kwa kuzingatia jinsia.

Acknowledgements

Rasilimali hii imeandaliwa kupitia  mpango wa ‘UCARE – Unpaid Care in sub-Saharan Africa‘, ambao inalenga kuongeza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake kupitia dhamira ya kugawana zaidi haki na usawa wa matunzo yasiyolipwa na kazi za nyumbani ndani ya kaya na familia katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Mradi huu unatekelezwa kwa ushirikiano wa Farm Radio International (FRI), UN Women, na The African Women’s Development and Communications Network (FEMNET) kutokana na ufadhili wa Global Affairs Canada.