Taarifa za awali: Usimamizi wa misitu kwa kushirikiana na jamii

Mazingira na Mabadiliko ya TabianchiMiti na kilimo mseto

Backgrounder

Utangulizi 

Usimamizi wa misitu ya jamii huanzishwa na jamii zinazoishi karibu na misitu, na/au na serikali au washirika wa maendeleo kama sehemu ya kukabiliana na uharibifu wa misitu. Pia unaweza kuitwa usimamizi shirikishi wa misitu, usimamizi wa misitu unaotegemea jamii, au usimamizi wa pamoja wa misitu. Katika usimamizi wa misitu ya jamii, jamii ina haki ya kufanya maamuzi muhimu kuhusu jinsi misitu na rasilimali zake zinavyotumika, kusimamiwa, na kuhifadhiwa, na mara nyingi hutumia haki hizo kupitia vyama vya misitu vya kijamii. Jamii zinazoshi karibu na misitu huhamasika kuilinda kwa sababu inachangia katika mahitaji yao ya Maisha ya kila siku. Usimamizi wa misitu ya jamii unaweza kutumika kusimamia misitu ya asili na maeneo yenye miti, pamoja na mashamba ya miti na vichaka vinavyomilikiwa na jamii.

Kwanini mada hii ni muhimu kwa wasikilizaji?

Kwasababu jamii zinazoishi maeneo yenye misitu katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara zinapaswa kujua.

  • Jinsi jamii zinazoishi karibu na misitu zinavyoweza kujipanga ili kuhifadhi misitu hiyo.
  • Faida ambazo jamii zinaweza kupata kwa kusimamia na kuhifadhi misitu kwa ufanisi.
  • Aina za sheria ndogo (by-laws) ambazo jamii zinapaswa kutunga na kuzifuata kusaidia kusimamia misitu yao.
  • Jinsi ya kutumia rasilimali za misitu kwa njia endelevu.
  • Jinsi ya kushirikiana na serikali na mashirika ya maendeleo ili kuanzisha shughuli endelevu za kuzalisha kipato—ndani au nje ya misitu—bila kuhatarisha misitu.
  • Jinsi ya kurejesha misitu iliyoharibiwa kwa kupanda miti, na jinsi ya kuchagua na kupanda miti bora na inayofaa kwa mazingira hayo.
  • Jinsi ya kuunda, kusimamia, na kudumisha vikundi vya usimamizi wa misitu ya kijamii.

 

Ni ukweli gani muhimu kuhusu usimamizi wa misitu ya kijamii?

  • Katika Afrika Mashariki na Magharibi, jamii zina uwezekano mkubwa wa kusimamia na kuhifadhi misitu ikiwa zinaweza kupata kipato na mahitaji yao ya maisha kutoka kwenye misitu hiyo.
  • Moja ya kazi muhimu za usimamizi wa misitu ya kijamii ni kuamua jinsi rasilimali za asili za msitu zinavyoweza kutumiwa—na matumizi yapi si endelevu. Jamii zinahitaji mafunzo juu ya jinsi ya kuvuna rasilimali za msitu kwa njia endelevu bila kuiharibu.
  • Usimamizi wa misitu ya kijamii hupunguza ujangili na matukio haramu ya ukataji miti.
  • Jamii zinazoishi karibu na misitu lazima zishirikishwe katika kuandaa mpango wa jinsi ardhi ya misitu itakavyotumika, kusimamiwa, na kulindwa. Mpango huo lazima ujumuishe ramani iliyotengenezwa na jamii inayoonyesha wapi na jinsi rasilimali za misitu kama mbao, asali, na kuni zitakavyovunwa.
  • Jamii zinahitaji kuandaa sheria ndogo (by-laws) za kusimamia jinsi misitu inavyotumika na kulindwa, na kujumuisha faini au adhabu nyingine zinazokubalika na jamii kwa wale wanaokiuka mipango ya usimamizi wa misitu.
  • Jitihada za kuhifadhi misitu zinapaswa kuunganishwa na kuboresha maisha ya jamii zinazoishi jirani na maeneo ya misitu. Utafiti uliofanyika Tanzania umeonyesha kuwa uharibifu wa rasilimali za asili unahusiana na viwango vya chini vya kipato katika jamii zinazoishi karibu na misitu.
  • Kuna njia nyingi ambazo jamii zinaweza kujiunga kwa ajili ya usimamizi wa misitu. Nchini Ghana, serikali imeanzisha Maeneo ya Usimamizi wa Rasilimali za Jamii (Community Resource Management Areas – CREMAs), ambayo huleta pamoja jamii zinazotumia rasilimali za aina moja ili kuzisimamia kwa pamoja rasilimali hizo bila ubaguzi. CREMAs hutumika kama eneo la akiba kwa ajili ya hifadhi na mbuga ambazo zina misitu iliyo hatarini.

Ni changamoto zipi kubwa katika usimamizi wa misitu ya kijamii?

  • Jamii zenye kipato cha chini zinazotegemea misitu kwa matumizi ya kila siku haziwezi kutilia maanani au kuwa na uwezo wa kutekeleza mipango ya muda mrefu ya usimamizi wa misitu.
  • Kaskazini mwa Ghana na maeneo mengine, jamii zinazotegemea misitu kwa ajili ya Maisha yao ya kila siku mara nyingi hujikuta katika ugomvi na mamlaka zinazohusika na usimamizi wa misitu kuhusu matumizi ya rasilimali.
  • Nchini Kenya, jamii zinazosimamia misitu zinakosa nguvu ya kuwafikisha mahakamani wahalifu wa ukataji miti na wawindaji haramu wa wanyamapori wanaowakamata kwa makosa ya kutumia vibaya rasilimali.
  • Sera, sheria ndogo (by-laws), au mipango isiyo wazi kuhusu jinsi jamii zitakavyoshiriki kwa usawa rasilimali za misitu na mapato yoyote watakayoyapata.
  • Pale ambapo rasilimali za misitu kama mbao ni haba, zinaweza kutotosha kutumika na jamii iliyo karibu na msitu.
  • Jamii zilizopo karibu na misitu zinaweza kuwa na migogoro kati yao wenyewe kuhusu kugawana na kutumia rasilimali za misitu.
  • Hakuna misitu inayosimamiwa na jamii nchini Uganda kwasababu maamuzi mengi kuhusu shughuli za misitu hufanywa katika ngazi ya kaya.
  • Nchini Nigeria, licha ya kwamba idadi ya watu inaongezeka na rasilimali za misitu zinapungua, kuna usimamizi mdogo wa misitu ya kijamii ili kulinda na kurejesha rasilimali za misitu.

Kwa taarifa zaidi, tafadhali angalia nakala namba 1-25.

Vipengele vya kijinsia katika usimamizi wa misitu ya kijamii

  • Katika eneo la Tharaka Nithi, Kenya, wanawake hushiriki zaidi katika usimamizi wa misitu kuliko wanaume, kwani wanaume hufanya kazi mbali na nyumbani na mbali na msitu. Wanawake pia ndio wanaoathirika zaidi na uharibifu wa mazingira kwani ndio wenye jukumu la kuchota maji, kukusanya kuni, na vifaa vya ujenzi kutoka kwenye misitu.
  • Nchini Tanzania, ingawa wanawake wanayo maarifa na ujuzi kuhusu usimamizi wa rasilimali za asili, wanakuwa na majukumu madogo katika usimamizi wa misitu kutokana na mfumo wa kijinsia unaoweka vikwazo kwa ushiriki wao.
  • Nchini Afrika Magharibi, wanawake mara nyingi hawajui haki zao za kumiliki ardhi, misitu, na miti, na jinsi wanavyoweza kunufaika na bidhaa au huduma za misitu. Pia hawajui kwamba wanayo haki ya kufanya maamuzi kuhusu jinsi ya kusimamia misitu.
  • Nchini Cameroon, wanaume hupendelea kupanda miti inayoweza kuleta kipato kikubwa, wakati wanawake, ambao wanamajukumu ya kulea watoto na wanafamilia wengine, wanaweza kuchagua miti inayotoa matunda na malisho, inayokuwa na sifa za tiba, na inayoboresha rutuba ya udongo.
  • Nusu ya familia nchini Ghana na Burkina Faso, wanawake wana ushawishi juu ya maamuzi ya waume zao kuhusu ni miti gani ya shea ya kuhifadhiwa na katika nusu nyingine ya familia, wanaume wanachagua miti gani ya shea ya kuhifadhiwa.

 

Kwa taarifa zaidi, tafadhali angalia nakala namba 2, 3, 10, na 11.  

Athari zinazotabiriwa za mabadiliko ya tabianchi kwa usimamizi wa misitu ya jamii

  • Katika wilaya ya Masindi, magharibi mwa Uganda, ukataji wa msitu unasababisha upungufu wa mvua na hufanya wanajamii kuwa hatarini kwa athari za mabadiliko ya tabianchi.
  • Uharibifu wa Msitu wa Mau nchini Kenya umechochea hatua za kuurejesha ili kuokoa maisha ya jamii zinazozunguka msitu huo na kuwawezesha kuwa na ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi.
  • Serikali ya Jimbo la Cross River la Nigeria (lenye asilimia 50 ya misitu yote ya nchi) inahusika katika juhudi za kuendelea kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kusaidia jamii kunufaika na shughuli za kujipatia kipato kutokana na misitu kwa kutumia rasilimali za misitu kwa njia endelevu.
  • Mabadiliko ya tabianchi yanatarajiwa kupunguza kiasi cha biomasi kinachopatikana katika misitu ya Burkina Faso (na sehemu zingine) na kusababisha kutoweka kwa baadhi ya spishi za mimea

Kwa taarifa zaidi, tafadhali angalia nakala namba 9, 13, na 23.

 

Lini usimamizi wa misitu ya jamii unahitajika?

Jamii huanza usimamizi wa misitu ya jamii kwasababu mbalimbali, ikiwemo:

  • When there is poaching of wild animals by communities living near the forests.
  • Uharibifu wa ardhi unaosababishwa na matumizi mabaya ya misitu na usimamizi wake.
  • Athari za mabadiliko ya tabianchi zinazosababisha kiangazi na kupotea kwa mimea.
  • Pale jamii inapotokuwa na upungufu wa ujuzi na uwezo wa kupambana na kupungua kwa rasilimali za asili zinazohatarisha maisha yao.
  • Pale jamii zenye kipato cha chini zilizokaribu na misitu zinapotumia rasilimali za asili kupita kiasi.
  • Pale jamii zinapotegemea misitu kwa chakula na rasilimali kama vile kuni.
  • Pale migogoro inapotokea katika jamii kuhusu ushirikiano usio sawa wa rasilimali za misitu au wakati kunapokuwa na ushindani mkali kuhusu rasilimali chache za asili zilizopo.
  • Pale amabapo kuna uwindaji haramu wa wanyamapori unaofanywa na jamii zilizokaribu na misitu.

Mambo ya kuzingatia kabla ya kutekeleza mpango wa usimamizi wa misitu ya jamii

  • Jamii inahitaji kuelimishwa jinsi watakavyonufaika kwa kulinda na kuhifadhi msitu. Manufaa haya yanaweza kujumuisha upatikanaji wa miti na bidhaa zisizo za miti kutoka kwenye maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya madhumuni hayo.
  • Jamii lazima zihusishwe katika mifumo ya utawala na maamuzi tangu mwanzo wakati usimamizi wa misitu ya kijamii unapoanzishwa, ili wasihisi kwamba wanapoteza msitu wao na rasilimali zake kwa watu wa nnje ya jamii yao. Hii pia hupunguza upinzani wao kwa mawazo ya uhifadhi wa misitu yanayowasilishwa.
  • Ni muhimu kubaini spishi nadra za mimea, miti, na wanyamapori ambazo zinahitaji kulindwa na zisitumike kwa matumizi ya nyumbani.
  • Sheria ndogo zinapaswa kuandikwa ili kusimamia jinsi rasilimali za msitu zitakavyotumika kwa njia endelevu na jamii zinazozunguka.
  • Kuna haja ya kuzingatia muundo sahihi wa utawala kwa usimamizi wa rasilimali na ushiriki sawa wa manufaa.
  • Jamii zinahitaji kufanya utafiti ili kugundua jinsi jamii itakavyonufaika na usimamizi wa misitu, jinsi rasilimali za misitu zitavyohifadhiwa, na jinsi jamii itavyorejesha msitu ikiwa utapungua.
  • Ni muhimu kujadili jinsi rasilimali za misitu zitavyolindwa dhidi ya uharibifu wa mazingira, ukataji miti, na uwindaji haramu.
  • Jamii zinahitaji kuunda mchakato wa kutatua migogoro ya ndani, ambayo mara nyingi hutokea wakati rasilimali za misitu zinapokuwa chache kutokana na hali mbaya ya hewa na/au matumizi kupita kiasi.
  • Jamii zinapaswa kuzingatia umuhimu wa kuanzisha ubunifu wa nishati mbadala kwa jamii ili kupunguza utegemezi mkubwa wa rasilimali za misitu kama vyanzo vya nishati (kwa mfano, kuni) na kuzuia ukataji miti.
  • Kuna haja ya kuwaelimisha wanajamii kuhusu mbinu endelevu za matumizi ya misitu na ardhi wakati wanapotumia misitu kwa ajili ya kuendesha maisha yao. Jamii zitapaswa kufanya maamuzi kuhusu rasilimali zipi zinaweza kutumika, kutoka maeneo gani ya msitu, kwa kiasi gani, na mara ngapi.
  • Jamii zinapaswa kuzingatia mambo waliyojifunza kutoka kwenye miradi ya awali ili kuongeza nafasi za mafanikio wakati wa kutekeleza mpango mpya wa usimamizi wa misitu ya jamii.
  • Pia ni muhimu kuwa na mfumo wa sheria/sera unaowezesha usimamizi wa rasilimali za jamii katika ngazi ya kitaifa.

Kwa taarifa zaidi, tafadhali angalia nakala namba 1, 4-8, 14-19, 20-25.

Mifumo ya kilimo mseto

Moja ya mbinu zinazotumika mara kwa mara na vyama vya usimamizi wa misitu ya jamii ni kilimo-mseto. Kilimo-mseto ni mfumo wa matumizi ya ardhi ambapo miti au vichaka vinapandwa pamoja na mazao ya kilimo, au kwenye malisho ya mifugo. Inapofanywa kwa uangalifu, miti na vichaka havizuii ukuaji wa mazao, na miti ya aina ya mikunde huongeza virutubisho kama vile nitrojeni kwenye udongo, huku kivuli cha miti kikinufaisha mazao kama vile mahindi, maharagwe, mboga, na ndizi wakati wa joto. Miti na vichaka vinavyotumika mara nyingi katika mifumo ya kilimo-mseto ni pamoja na: Grevillea robusta, leucaena, Sesbania grandiflora, velvet bean, Gliricidia sepium, na Calliandra calothyrsus. Miti na vichaka pia huvutia nyuki na, kwa kuweka mizinga, jamii zinaweza kuvuna asali. Katika mifumo ya kilimo-mseto, miti na vichaka vinaweza pia kutoa malisho kwa mifugo kama vile mbuzi na ng’ombe.

Kwa taarifa zaidi, tafadhali angalia nakala namba 12.

 

Simulizi mbili za mafanikio katika usimamizi wa misitu ya jamii

  1. Mradi wa uhifadhi wa msitu wa Ekuri, Nigeria

Mnamo mwaka wa 1991, Hifadhi ya Taifa ya Cross River ilianzishwa na serikali ya jimbo la Cross River nchini Nigeria. Karibu na hifadhi hiyo kulikuwa na msitu wa ekari 33,600 ambao ulizingatiwa kuwa sehemu ya hifadhi hiyo, na jamii ya wakulima ya Ekuri yenye wanachama 600 ilianza kuhifadhi msitu huo tangu miaka ya 1980 ili kuzuia shughuli za ukataji miti zilizopendekezwa katika hifadhi ya taifa. Msitu huo unajumuisha vijiji vya zamani na vipya vya Ekuri, ambavyo viko umbali wa kilomita saba. Baada ya hifadhi hiyo kuanzishwa, jamii iliiomba mamlaka ya hifadhi hiyo ruhusa ya kusimamia msitu huo wao wenyewe. Ombi lao lilikubaliwa na walipatiwa afisa wa msitu wa jamii ambaye aliwasaidia kujenga mfumo wa usimamizi wa msitu wa jamii ambao ulikuwa wa kwanza na wa aina yake nchini Nigeria

Kama fidia ya kuhifadhi msitu, jamii ya Ekuri inanufaika na msitu kupitia kilimo, kuvuna bidhaa zisizo za miti kutoka msituni, kutengeneza bidhaa za mikono, biashara ndogo ndogo ya majani ya msitu yanayoliwa na maembe pori, pamoja na uwindaji na uvuvi. Maeneo mawili ya ekari 50 yametengwa kwa ajili ya jamii kuvuna miti ya mbao na bidhaa zisizo za miti ya mbao wanazohitaji.

Mnamo mwaka wa 1992, kikundi la jamii ya Ekuri kilianzishwa kama Mpango wa Ekuri, umoja rasmi. Mpango wa Ekuri unajumuisha watu wa Ekuri (Wote kwa ujumla- Mkutano mkuu), bodi ya wadhamini, mratibu wa mradi, na wafanyakazi wa kusaidia kama walinzi wa mitaani wanaozunguka kwenye msitu kufanya doria. Bodi ya wadhamini ina wanachama kumi, wakiwemo wanawake wanne, ambao huchaguliwa kutoka vijiji vyote viwili. Uongozi hubadilika kila baada ya miaka minne au mitano. Katika vikundi vya mikopo- midogo vya mpango huu, wanawake ni wengi zaidi kuliko wanaume.

Mwanzoni mwa kila mwaka, vijiji vya jamii ya Ekuri hukutana na kupanga shughuli za mwaka na kutenga fedha zinazohitajika. Wakati wa mikutano hiyo, maamuzi kuhusu jinsi fedha zitavyotumika lazima yathibitishwe na vijiji vyote vya Ekuri na ripoti ya mwaka inawasilishwa kwa jamii kwa ajili ya tathmini, uwajibikaji, na maoni. Rasimu ya sera zinawasilishwa kwa mkutano mkuu kabla ya kutathminiwa na bodi inayosimamia Mpango wa Ekuri. Bodi hii hufanya maamuzi kulingana na vipaumbele vya jamii ya Ekuri. Wanajamii wanakuwa tayari zaidi kufuata maamuzi kwani wanahusishwa katika kuyafanya; hayajachochewa na mamlaka za nje.

Wanawake wanahusishwa katika kufanya maamuzi katika ngazi zote na katika shughuli zote, ikiwemo usimamizi wa misitu, maendeleo ya jamii, na shughuli za kupunguza umaskini. Maamuzi yanazingatia usawa kati ya matumizi ya rasilimali za misitu na shughuli za uhifadhi.

Kwa miaka mingi, jamii mbili za Ekuri zimeanzisha hatua za kuhakikisha kwamba uhifadhi wa msitu wa muda mrefu unapewa kipaumbele zaidi kuliko mahitaji yao ya haraka ya maisha. Mpango wa Ekuri unahusika na utekelezaji wa ukataji miti kwa udhibiti na kuuza miti kwa manufaa ya jamii, ambapo mapato yanatengwa kulipa walinzi wa misitu wa eneo hilo. Ukataji miti unafanyika katika maeneo yaliyotengwa na kwa miti ambayo ina kipenyo cha angalau sentimeta 70 kwa urefu, huku miti midogo ikiachwa ikue na kutoa mbegu.

Miti kwenye ardhi au viwanja binafsi inamilikiwa na jamii. Wanajamii wanaruhusiwa kuvuna miti kwa matumizi ya nyumbani, kwa mfano, kujenga nyumba au fanicha, lakini si kwa madhumuni ya kibiashara. Hakuna mtu mwingine yeyote isipokuwa wanajamii wa Ekuri anaye ruhusiwa kuvuna na kuuza bidhaa zisizo za miti kutoka msituni, na wanajamii wanaweza kuuza tu kwa wafanyabiashara waliosajiliwa na Mpango wa Ekuri.

Jamii hutumia ardhi za msitu kulingana na taratibu zilizowekwa. Wanajamii wanawajibika kukamata wakataji miti haramu. Kwa miaka mingi, wanajamii ambao wamevuna miti kiharamu wamefunguliwa mashtaka mahakamani.

Ingawa Mpango wa Ekuri unachukuliwa kama mfano wa usimamizi wa misitu ya jamii nchini Nigeria, bado kuna changamoto. Jamii ya Ekuri inahofia kwamba ruzuku za ukataji miti zilizotolewa na serikali ya jimbo na mipango ya kujenga barabara kuu itazidisha matumizi ya rasilimali za msitu na kusababisha kuporwa kwa ardhi yao. Kwa mujibu wa Edwin Ogar, mwanachama mwanzilishi wa Mpango wa Ekuri, Matumizi hayo kupita kiasi yataangamiza makazi ya spishi 350 za ndege pamoja na Nyati wa Afrika, tembo, nyani, kima na spishi nyingine za wanyama, mimea, na miti zinazokaribia kutoweka.

Mpango wa Ekuri umepokea misaada mingi na tuzo za kimazingira kwa miaka mingi. Mnamo mwaka wa 1997, Ford Foundation ilitoa fedha kwa ajili ya kuainisha mipaka ya ardhi ya jamii baada ya mazungumzo na jamii jirani. Fedha hizo pia zilitumika kwa mafunzo ya jinsi ya kuandaa orodha ya miti na mipango ya awali ya matumizi ya ardhi ya msitu. Mnamo mwaka wa 2004, Mpango wa Ekuri ulishinda tuzo ya Equator ya $5,000.

Kwa taarifa zaidi, tafadhali angalia nakala namba 4-6, 17, 18, 22, na 24.

  1. Uhifadhi wa Msitu wa Arabuko Sokoke

Mnamo mwaka wa 1993, Makumbusho ya Taifa ya Kenya na Asili (Nature) Kenya walianzisha Mradi wa Kipepeo kwa jamii zenye kipato cha chini zinazokaa karibu na Msitu wa Arabuko Sokoke wenye ukubwa wa ekari 41,600 katika pwani ya Kenya. Mradi wa Kipepeo unahusisha wanajamii katika kulea vipepeo na kuwauza katika hifadhi za  wadudu huko Ulaya na Marekani ambapo hukua na kuvutia wageni katika maisha yao ya siku 12.

Mradi huu ulianzishwa kutoa mbinu mbadala za kujipatia kipato kwa wanajamii ambao walikuwa wakitegemea ukataji miti haramu na uwindaji wa wanyama pori kutoka msituni. Kwa miaka mingi, msitu ulizidi kuharibika kutokana na zaidi ya wanajamii 100,000 kutoka vijiji 50 waliokuwa wakitumia rasilimali zake. Wengi wao ni wakulima wanaolima mazao kama mahindi, viazi vikuu, na maharage, pamoja na mazao ya biashara kama nazi na korosho. Walikuwa wakikata miti kwa ajili ya ujenzi, kuni, uzalishaji wa mkaa, na uchongaji wa vinyago. Kulikuwa pia na uwindaji haramu wa swala, panya, ndege, na spishi nadra za wanyama pori, kama vile Nunga (Aders duikier), Pungu/sange wenye rangi ya dhahabu (golden-rumped elephant shrew) na Nguchiro (Sosoke bushy-tailed mongoose), kwa ajili ya nyama ya pori. Kuhifadhi msitu huu ilikuwa muhimu kwasababu msitu wa Arabuko Sokoke una utajiri wa bayoanuwai na pia ni sehemu kubwa zaidi ya msitu wa asili wa pwani ulio salia Afrika Mashariki, ukiwa na mkusanyiko mkubwa wa mimea na wanyama wa asili walio hatarini na wanaokaribia kutoweka.

Wakati wa upembuzi yakinifu wa mradi, ambapo wazo la kupata riziki kwa kuuza mazalia ya vipepeo lilipendekezwa kwa jamii zinazokaa karibu na Msitu wa Arabuko Sokoke, wengi walilikataa kwasababu ya imani za kitamaduni kwamba ilikuwa ni kinyume na maadili. Wanajamii wachache walikubaliana kulijaribu, huku wengine wakichukua mtindo wa kusubiri na kuona. Wanajamii waliokubali walipoanza kupata kipato kutokana na kuuza vipepeo, baada ya miaka michache, kulikuwa na ongezeko la watu kujiandikisha kwenye mradi huu. Baadaye, Huduma za Misitu ya Kenya ilikagua Sheria ya Misitu na kuanzisha kifungu kilichoweka usimamizi wa pamoja wa misitu, na kuwapa wanajamii wanaoishi karibu na misitu nafasi ya kushiriki katika usimamizi wa rasilimali za misitu. Hii hatimaye ilisababisha kuundwa kwa vyama vya usimamizi wa misitu ya jamii.

Asili (Nature) Kenya na Makumbusho ya Taifa ya Kenya walianzisha kampeni za uhamasishaji ili kuwafahamisha wanajamii wanaoishi karibu na msitu kuhusu umuhimu wa kuhifadhi msitu huo. Wanajamii walitakiwa kuachana na ukataji miti haramu na uwindaji wa nyama  pori na kukubaliana na mfano endelevu wa kutumia rasilimali kama vile mbao na mimea inayotumika katika tiba za asili. Mwanzo wa mradi, wakazi walihamasishwa kupanda miti majumbani mwao ili kupunguza utegemezi wao kwa msitu.

Huduma ya Misitu ya Kenya ilizuia wanajamii walio karibu na misitu na mali asili kuingia maeneo hayo umbali wa kilometa tatu za kwanza ndani ya msitu. Waliruhusiwa kukusanya fito katika kilometa ya kwanza na kuni katika kilometa ya pili. Kilometa ya tatu ilitengwa kwa uhifadhi wa viumbe hai, ambapo shughuli zisizo za kuvuna rasilimali, kama vile kutazama ndege na kuendesha baiskeli, ziliruhusiwa.

Asili (Nature) Kenya, Marafiki wa msitu wa Arabuko-Sokoke, na A-Rocha Kenya walinunua na kugawa miche ya miti na miti ya matunda kwa jamii ili wapande mashambani mwao. Miti hii hutoa majani yanayovutia wadudu kama vile vipepeo. Ili kuhakikisha kwamba jamii itafaidika haraka, spishi zilizotolewa zilikuwa zinakua haraka kama Casuarina, Azadirachta indica (mchaichai), na Gmelina arborea. Ufugaji wa nyuki pia ulianzishwa.

Zaidi ya watu 10,000 wa maeneo ya karibu wanahusika katika mradi wa vipepeo na shughuli nyingine za uzalishaji wa kipato ambazo zilianzishwa pamoja nao, ikiwa ni pamoja na ufugaji wa nyuki, kilimo mseto, na kilimo cha alovera na uyoga. Mradi wa vipepeo unaweza kumuwezesha kila mshiriki kupata kati ya dola 100 na 200 za Marekani kwa wiki. Jamii pia ina juhudi za kupanda tena miti ya asili, ambayo imeongeza ukubwa wa msitu.

Msanzu Karisa ni mfugaji wa vipepeo mwenye umri wa miaka 40 na baba wa watoto watatu. Tangu alipojiunga na Mradi wa Vipepeo mwaka 2006, ameona manufaa ya kiuchumi. Anapata kati ya shilingi 40,000 hadi 50,000 za Kenya ($300-385 za Marekani) kwa mwezi kutokana na kuuza vipepeo 200-400. Kwa mapato haya, ameweza kuwasomesha ndugu zake na kununua ekari moja ya ardhi ambapo anapanga kujenga nyumba. Bwana Karisa ni mshiriki wa kikundi cha kufuga vipepeo chenye wanachama 70. Wanachama hufuga vipepeo kila mmoja kivyake, lakini kila kundi lina mwakilishi ambaye hukusanya vipepeo na kuvipeleka kwenye kituo cha Mradi wa Kipepeo. Mradi unawalipa wanajamii kwa ajili ya vipepeo hao, kisha huviuza kwa wanunuzi wa kimataifa. Wawakilishi pia hukutana na wafanyakazi wa usimamizi wa mradi kujadili uzalishaji, masoko, na masuala yanayohusiana na vikundi vya kulea vipepeo. Kila mwanachama binafsi analipwa kwa vipepeo anavyovileta. Vipepeo ambavyo havipelekwi nje ya nchi hukuzwa kwenye kituo cha Mradi wa Kipepeo. Wageni wanaotembelea kituo hutozwa ada ili kuona vipepeo, na pesa zinazopatikana huzungushwa miongoni mwa wafugaji wa vipepeo mwishoni mwa mwaka.

Bwana Karisa anasema kuwa mafanikio ya mradi wa vipepeo yamehamasisha wanajamii kuhifadhi Msitu wa Arabuko Sokoke na kuwa macho katika kuripoti wawindaji haramu au wauzaji wa magogo haramu kwa Huduma ya Misitu ya Kenya, jambo ambalo limepunguza makosa kama hayo.

Kwa miaka mingi, Mradi wa Kipepeo umepokea ufadhili kutoka kwa mashirika ya wafadhili. Kwa mfano, mwaka 2003, USAID ilitoa dola milioni 1.2 kwa shughuli za uhifadhi kama vile upandaji miti na mradi wa kulea vipepeo.

Kwa taarifa zaidi, tafadhali angalia nakala namba 1, 7, 8, 14, 16, 19, and 21.

Acknowledgements

Imechangiwa na: James Karuga, Mwandishi wa kilimo, Kenya

Imehaririwa na: Elijah Yaw Danso, Mshauri wa maendeleo ya jamii na usimamizi wa rasilimali asili, Ghana

Information sources

Martins Egot, Ekuri Msemaji wa jamii na Mwenyekiti, Bodi ya udhamini ya Mpango wa Ekuri, Nigeria, alihojiwa May 30, 2024.

Edwin Ogar, Mratibu wa zamani  Mpango wa Ekuri, Nigeria, alihojiwa June 1, 2024.

Msanzu Karisa, mfugaji wa vipepeo, Mradi wa Kipepeo, Kaunti ya Kilifi, Kenya, interviewed on June 10, 2024.