Matangazo ya Redio kuhusu kazi za utunzaji bila Malipo

Usawa wa kijinsia

Ujumbe kwa mtangazaji

Taarifa kwa Watangazaji

Kulingana na UN Women, kazi ya utunzaji “hujumuisha shughuli na mahusiano ili kukidhi mahitaji ya kimwili, kisaikolojia, na kihisia-moyo ya watu wazima na watoto, wazee kwa vijana, dhaifu na wenye uwezo. Inajumuisha shughuli za utunzaji wa moja kwa moja zinazohusiana na kutunza watoto, wazee, watu wenye magonjwa, na watu wenye ulemavu, pamoja na kazi zisizo za moja kwa moja au za nyumbani kama vile kupika, kusafisha, kuchota maji, kupika chakula na kukusanya kuni … Kazi za utunzaji zisizolipwa zinarejelea huduma zinazotolewa na watu binafsi ndani ya kaya au jumuiya bila kupokea fidia yoyote ya fedha kwa manufaa ya wanachama wake. Kazi nyingi za utunzaji zisizolipwa hufanyika ndani ya familia. Kazi za utunzaji bila malipo pia hutokea katika ngazi ya jamii kwa watu walio nnje ya nyumba (marafiki, majirani, na wanajamii).”

Kote ulimwenguni, majukumu ya ulezi huwa ya wanawake na wasichana. Katika Afŕika Kusini mwa Jangwa la Sahaŕa, wanawake wanafanya kazi za matunzo zisizolipwa mara 3.4 zaidi ya wanaume. Hii inazuia fursa za wanawake za elimu na ajira, na huathiri ushiriki wao wa kijamii na muda wa burudani, na hivyo kuathiri afya ya wanawake na viwango vya umaskini.

Katika matangazo haya, utajifunza zaidi kuhusu utunzaji ambao haujalipwa na ukosefu wa usawa wa kijinsia unaohusishwa nayo. Mada za matangazo ni pamoja na:

  • Haja ya kutambua na kuthamini kazi za utunzaji zisizolipwa za wanawake
  • Utunzaji usio na malipo ni kazi yenye tija
  • Haja ya kila mtu katika kaya kushiriki kazi ya utunzaji
  • Siku katika maisha ya mhudumu asiyelipwa
  • Athari zilizofichika za kazi ya utunzaji bila malipo kwa wanawake
  • Kufundisha watoto kuhusu kugawana majukumu ya nyumbani
  • Kuwawezesha wahudumu wasiolipwa ni juhudi za jamii
  • Kumsaidia mwenza wako kazi za matunzo 
  • Sema hapana kwa ukatili wa kijinsia dhidi ya wahudumu wasiolipwa
  • Waajiri wanaweza kusaidia wafanyakazi wa huduma wasiolipwa kusawazisha kazi na maisha
  • Kuboresha upatikanaji wa rasilimali za umma husaidia wafanyakazi wa huduma wasizolipwa
  • Jinsi vyombo vya habari vinaweza kubadilisha simulizi kuhusu kazi za utunzaji ambazo hazijalipwa

Matangazo hutofautiana kwa urefu kutoka takriban sekunde 45-60 na yanaweza kurushwa mara nyingi wakati wa programu za afya na usawa wa kijinsia, na programu zingine zinazofaa.

Majina ya matangazo yanalenga tu kutambua mada ya tangazo. Hazikusudiwi kusomwa kwa sauti kama sehemu ya tangazo.

Script

Tangazo #1: Kuthamini kazi ya utunzaji isiyolipwa ya wanawake

MSIMULIZI:
Wanaume! Hatimaye ni Ijumaa, na mwisho wa wiki nyingine ndefu ya kazi! Umefanya kazi kwa bidii!

Lakini unajua ni kitu gani muhimu kama kazi yako? Kazi ambayo mwenza wako hufanya nyumbani.

Baada ya siku ndefu, ngumu katika kazi, ni vizuri kurudi nyumbani kwenye kaya yenye furaha? Ili kujua kuwa watoto wako sawa? Nyumba inayofanya kazi vizuri hukupa amani ya akili ili kuweza kuzingatia vyema kazini.

Kwa hiyo leo, mthamini mwenza wako kwa kazi zote anazofanya nyumbani.

Tangazo #2: Kazi bila malipo bado ni kazi yenye tija

TUKIO:
KITUO CHA KUTAZAMA

SFX:
SAUTI, VICHEKO, MLIO WA CHUPA KUGONGANA

UMAR:
David! Ulikosa kipindi cha kwanza! Ulikuwa wapi?

DAVID:
(KULALAMIKA), Umar, hutaamini. Ni mke wangu kichaa

UMAR:
Ah, David. Abi amefanya nini sasa?

DAVID:
(AKIWA AMEKASIRIKA) Unaweza kufikiria, baada ya wiki ndefu ya kazi ngumu, mwanamke huyu alikuwa akinipa msongo wa mawazo. Yeye yuko nyumbani wiki nzima lakini anafanya kama vile yeye ndiye anayetoka kwenda kutafuta chakula cha familia. (ANAONYESHA KUTOKUBALIANA) Alisema nimsaidie kusogeza viti.

UMAR:
Tulia rafiki yangu. Nini kimetokea?

DAVID:
Nilihamisha viwili, kisha nikaondoka. Upuuzi. Hata Mungu alipumzika! Sio haki. Mimi ndiye ninaleta pesa zote, na yeye huleta tu usumbufu na msongo wa mawazo!

UMAR:
Ah David, unajua hiyo si kweli. Daima unazungumza kuhusu vyakula vitamu ambavyo Abi hutengeneza na jinsi mapacha wako walivyo nadhifu na wenye afya njema. Je, hilo si muhimu pia?

DAVID:
(AKITAFAKARI) Nadhani. Huenda haletei pesa, lakini kazi anayofanya kutuweka sote tukiwa na furaha na afya haina thamani!

UMAR:
Haswa. Kazi zake za nyumbani ni muhimu, na ina tija kama yako.

MSIMULIZI:
Kazi isiyolipwa NI kazi yenye tija! Bila hivyo, familia yako ingekuwa wapi?

 

Tangazo #3: Kazi ya utunzaji bila malipo ni jukumu la kila mtu

MSIMULIZI:
Wanawake hufanya kazi nyingi zaidi za kusafisha, kutunza watoto, na kazi zingine zisizo na malipo nyumbani na katika jamii.

Aina hii ya kazi mara nyingi huonekana kama jukumu la kifamilia ambalo ni la wanawake. Lakini wanawake hawapaswi kubeba jukumu lote la kazi hii isiyo na mwisho peke yao!

Kila mtu katika kaya—wanaume, wanawake, na hata watoto wakubwa wanaweza kusaidia katika kazi ya bila malipo. Mzigo unapaswa kugawanywa zaidi kwa usawa.

Kumbuka kwamba kaya inayofanya kazi haina tofauti na kiwanda, ofisi au sehemu ya uzalishaji-inahitaji mikono ya wote kufanya kazi.

Kwa hivyo wacha sote tushirikiane pamoja ili kuwa na kaya yenye mafanikio na yenye furaha.

 

Tangazo #4: Mahitaji ya kazi: Siku katika maisha ya mfanyakazi asiyelipwa

MARIYA: Wow, Zainab, angalia mahitaji ya kazi hii. Ni wazimu.

ZAINAB: Haiwezi kuwa mbaya hivyo, Mariya.

MARIYA: Mmmh, utaona. Sharti la kwanza ni “Lazima uwe kwenye simu 24/7, siku 365 kwa mwaka.”

ZAINAB: Nini? Hakuna likizo? Itakuwaje ikiwa wewe ni mgonjwa!

MARIYA: Unatarajiwa kujitokeza hata kama wewe ni mgonjwa. Oh na hakuna likizo ya uzazi. Inaonekana ni wakati pekee unapopata mapumziko kutokana na kazi hii isiyolipwa ni wakati unajifungua mtoto, na labda kuchukua muda kidogo kwa ajili ya kupona.

ZAINAB: Ndio, lakini sio kana kwamba kuzaa ni kitu cha mchezo. Maelezo hayo ya kazi hayafai kabisa. Lakini pesa ya malipo lazima iwe nzuri, sawa?

MARIYA: (KICHEKO) hela gani? Mshahara ni naira sifuri kwa mwezi, na naira sifuri kwa mwaka

 

ZAINAB: (MWENYE KUSHTUKA) Nini?

MARIYA: Unaweza kuongeza mapato yako na kazi zingine, lakini inasema lazima uzisawazishe na kuwa kwenye simu. Na kuna zaidi. Unahitaji kuwa na ujuzi ufuatao: kupikia, kushona, uhasibu, hesabu za msingi, ujuzi wa sayansi, ununuzi …

ZAINAB: (ANAINGILIA) Hapo hamna kitu. Ununuzi? Hii ni kazi ya aina gani? Jina la kazi ni nini?

MARIYA: Mama wa nyumbani na mfanyakazi asiyelipwa.

MSIMULIZI: Kazi ya utunzaji bila malipo ni ngumu kuliko unavyofikiria. Wacha tuwaunge mkono wafanyakazi wa utunzaji wasiolipwa, tushiriki kazi nyumbani, na kushinikiza kuwepo kwa mipangilio iliyo sawa katika kaya zetu, jamii, na hata katika sekta ya kibinafsi.

 

Tangazo #5: Madhara yasiyo onekana ya kazi ya utunzaji isiyolipwa

MSIMULIZI:
Wanawake na wasichana hufanya kazi nyingi sana bila malipo—kusafisha, kutunza watoto, kufua nguo, kukusanya kuni na kuchota maji.

Wanawake hufanya mara tatu hadi nne ya kazi hii isiyolipwa kuliko wanaume katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Na hii ina madhara makubwa. Inaathiri wanawake kimwili na kisaikolojia. Lakini kuna athari zingine, zilizojificha zaidi pia.

Inazuia fursa za wanawake za kiuchumi na kielimu, na ushiriki wao katika shughuli za kijamii, kitamaduni na kisiasa.

Kwa hivyo wacha tusawazishe kazi za utunzaji zisizolipwa ili wanawake waweze kuwa na maisha na ndoto nnje ya kazi hizo.

Tangazo #6: Fundisha kizazi kijacho kuhusu kazi za utunzaji ambazo hazifanyiwi malipo

MSIMULIZI:
Tunahitaji kubadilisha mitazamo yetu kuhusu jukumu la wanawake la kufanya kazi ya matunzo bila malipo, ikiwa ni pamoja na kazi za nyumbani. Na wakati mzuri wa kuanza ni wakati watoto bado wakiwa wadogo.

Wafundishe watoto wako kwamba kazi ya utunzaji bila malipo ni muhimu na muhimu kwa kaya. Ni jukumu la kila mtu, na inapaswa kugawanywa kwa usawa kati ya wasichana na wavulana, na hata wanaume na wanawake.

Ujuzi wa kufanya kazi za nyumbani ni muhimu kwa kila mtu. Hakuna kazi ambazo kwa asili zimekusudiwa kuwa za wavulana au wasichana. Kwanini wavulana hawawezi kupika, au wasichana kuosha magari?

Anza kufundisha watoto wako sasa kwa maisha bora ya baadaye.

 

Tangazo #7: Kuwawezesha wahudumu wasiolipwa ni juhudi za jamii

MSIMULIZI:
Leo, watu wengi wanafahamu na kuonyesha huruma yao kwa matatizo ambayo wafanyakazi wa huduma zisizolipwa wanakabiliana nayo katika jamii yetu. Hawa ni wanawake ambao hufanya kazi za nyumbani bila kikomo na kazi zingine za utunzaji katika kaya na jamii, bila malipo na mara nyingi bila shukrani.

Lakini haitoshi kufanya tu mabadiliko katika kaya zetu wenyewe. Ni lazima tutengeneze jamii ambayo kazi ya utunzaji bila malipo na wafanyakazi wanaheshimiwa na kutendewa haki.

Na njia moja ya kufanya hivyo ni kuunga mkono sera na vuguvugu za kisiasa zinazowezesha na kulinda haki za wafanyakazi wa kutoa huduma.

Kwa hivyo piga kura kwa manufaa ya kaya yako!

 

Tangazo #8: Msaidie mwenza wako kufanya kazi za nyumbani

SFX:
SIMU INAITA

ENE:
(AKIWA NA FURAHA) Mwanangu, umenikumbuka leo. Habari yako?

JAMES:
(AKICHEKA) Mama, siwezi kukusahau kamwe. Niko sawa. Kwa kweli nilitaka kuomba ushauri wako kuhusu Lucy.

ENE:
Mkeo? Hajambo?

JAMES:
Sijui, nataka ushauri wako kuhusu namna ambavyo naweza kuzungumza naye. Tangu Junior azaliwe, amekuwa hana bidii ya kufanya kazi hata kidogo.

ENE:
Unamaanisha nini?

JAMES:
Jana tulialika marafiki fulani, na walipofika, alikuwa bado anasafisha nyumba—unaweza kufikiria hiyo hali? Wakati huo huo, hakukuwa na kitu cha kuwahudumia. Ilinibidi nikimbie na kununua kuku kwenye mgahawa ili kuepuka aibu kabisa. Sijui la kumwambia, lakini anahitaji kubadilika.

ENE:
(KWA UKALI) Mwanangu, sina furaha na wewe.

JAMES:
Ehn?

ENE:
Sijakulea hivyo. Alipokuwa anasafisha nyumba, wewe ulikuwa unafanya nini?

JAMES:
(MWENYE KUBABAIKA) Nilikuwa … lakini … mimi

ENE:
Kumbuka siku ya sherehe ya kuadhimisha kuzaliwa kwa baba yako, wewe na ndugu zako mlikuwa mnanisaidia. Hata yeye wakati mwingine alikuwa ananisaidia. Nyie ni timu! Kwa hivyo kwanini usimsaidie mke wako?

JAMES:
(KWA UKIMYA) Nilipaswa kumsaidia.

ENE:
Ndio, ulipaswa kufanya hivyo! Nyumba yako itakuwa na amani kama utakuwa unamsaidia mwenza wako.

 

Tangazo #9: Sema hapana kwa unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wahudumu wasiolipwa

DANJUMA:
Ooooh takataka. (AKIONYESHA KUTOKUBALI)

BULUS:
Ah Dan, Nini kimetokea?

DANJUMA:
Aisha ameunguza chakula changu tena. Nina hakika alikuwa akitazama filamu ya Kihindi na akasahau kuwa chakula kilikuwa jikoni.

BULUS:
(KICHEKO) Siku moja ataweka sukari badala ya chumvi kwenye supu yako!

DANJUMA:
Bulus, unaona? Wanaume wengine wangeweza hata kumpiga kwa hili alilofanya ili kumpa akili. Anapaswa kunishukuru kwani niliapa kutoweka mikono juu ya mwanamke… (ANAONYESHA KUTOKUBALIANA).

BULUS:
(AKIONESHA KUSHTUKA) Juu ya chakula? Dan, nina hakika lilikuwa kosa. Haupaswi hata kufikiria hivyo. Na kwanini daima ni wajibu wake kukufanyia kazi zote bila malipo kama vile kukupikia? Hiyo si haki!

DANJUMA:
Ndio, upo sahihi. (TULIA KIDOGO) Ah, Siendi kumpiga, nilikuwa nasema tu kwamba wanaume wengine wangefanya hivyo.

BULUS:
Najua, lakini bado ni wazimu tu. Kama … unaweza kufikiria ikiwa kila mara tulipofanya makosa kwenye shamba hili, Bw. Sule angekuwa anatupiga? Kama vile wakati ule haukufunga mlango na mbuzi sita walitoroka?

DANJUMA:
Acha kuleta mambo ya zamani

BULUS:
Ikiwa bosi wetu hakukupiga kwa kumgharimu pesa, basi nadhani pia unaweza msamehe mkeo kwa kuunguza chakula.

DANJUMA:
(AKIVUTA PUMZI) Nitasimamia. Nadhani itabidi niamke mapema ili kuandaa chakula changu cha mchana mwenyewe. Siwezi kupoteza uzito kama hivi.

MSIMULIZI:
Unyanyasaji wa kijinsia haupaswi kamwe kutokea kwa sababu yoyote, angalau kwa sababu mpenzi wako anatatizika na kazi za nyumbani.

 

Tangazo #10: Waajiri wanaweza kusaidia wafanyakazi wa huduma wasiolipwa kusawazisha kazi na maisha

MTANGAZAJI:
Karibu tena kwenye wasaa wa Biashara ya Wanawake kwenye Redio Yako, kituo nambari moja cha redio. Tuko pamoja na Yankat Frank kwenye biashara yake, Yankat Chips. Asante kwa kuwa nasi, Bi. Frank.

YANKAT:
Namefurahi.

MTANGAZAJI:
Nimekuwa nikiona chipsi zako za viazi katika eneo lote la jimbo. Unafanya vizuri sana.

YANKAT:
Ndio, tulipanua biashara yetu katika miaka michache iliyopita. Wakati naanza biashara ya chips, nilijua nitalazimika kufanya maamuzi magumu ya kupanua biashara. Nimebarikiwa kuwa na timu kubwa iliyo karibu yangu.

MTANGAZAJI:
Ninaona wanawake wengi wanafanya kazi hapa. Je, hiyo ilipangwa?

YANKAT:
Nimekuwa na ndoto ya kuwawezesha wanawake, na nilipoanza biashara hii ya usindikaji, ilikuwa fursa nzuri.

MTANGAZAJI:
Ni mpango mzuri

YANKAT:
Nilijifunza kuhusu changamoto ambazo akina mama vijana wanaofanya kazi hukabiliana nazo kusawazisha kazi na kazi za nyumbani kutokana na uzoefu wangu mwenyewe. Ndiyo sababu tunajaribu kuwa na saa zinazobadilika. Na mwaka ujao, natumai tutakuwa na nafasi kwa akina mama kuja na watoto wao wakati wa saa zao za kazi.

MTANGAZAJI:
Kweli unawasaidia.

YANKAT:
Ninaamini ni muhimu kwa waajiri kuwasaidia wafanyakazi wao kuzalisha kilicho bora zaidi. Ni haki yao kutendewa mema! Na kwa kuwasaidia wafanyakazi wangu, wanaweza kutoa mchango wa kifedha katika nyumba zao huku wakiendesha Maisha yao kwa mafanikio!

Tangazo #11: Kuboresha upatikanaji wa rasilimali za umma husaidia wafanyakazi wa huduma wasizolipwa

MALKIA:
Mume wangu, hao wanawake waliokuja ikulu jana ni kina nani? Walizungumza nawe kwa muda mrefu.

CHIFU:
Hm? Oh hao walikuwa baadhi ya wanawake wenyeji wanaoishi katika mjini kwasasa. Walikuja kunishukuru, na walitaka kujua kama kuna lolote wangeweza kufanya kwa ajili ya jamii yetu. Walikuwa wakiomba ruhusa na udhini yangu kama chifu kwa ajili ya wao kutekeleza mipango yao.

MALKIA:
(AKIWA NA FURAHA) Hicho ni kitu kizuri. Natamani watu wengi zaidi wangetukumbuka hivyo. Ulisema wanataka kukushukuru? Kivipi?

CHIFU:
Unakumbuka tulipotaka kujenga kisima kipya, na ulipendekeza kwamba tukijenge karibu na mji?

MALKIA:
Ndio, watu walipinga kwa sababu maji yalikuwa umbali mrefu sana chini ya ardhi kuliko sehemu nyingine, lakini sehemu nyingine ilikuwa mbali sana.

CHIFU:
(AKIONYESHA MSISIMKO) Hivyo ndivyo wanawake walivyosema. Walisema kuwa kujenga kisima hicho karibu na mji kuliwapunguzia muda wa Kwenda kuchota maji hivyo kupata muda mwingi wa kwenda shule na kusoma.

MALKIA:
Sishangai—safari hiyo ya kuchota maji haikuwa mzaha. Mara mbili kwa siku! Baada ya kisima kujengwa, kiwango cha ufaulu katika mitihani ya mwisho wa shule kilipanda. Si ajabu wasichana hao walikuja kukushukuru.

CHIFU:
Sikujua kwamba kuweka tu kisima mahali pazuri zaidi kunaweza kufanya hivyo

MALKIA:
Kwa hivyo unachosema ni mke wako, Malkia, ana busara sana. (WOTE WANACHEKA)

MSIMULIZI:
Unapofikiria juu ya ujenzi wa miundombinu, zungumza na wafanya kazi za utunzaji bila malipo! Waulize wanachotaka na wanachohitaji, na uwajumuishe katika kufanya uamuzi. Unapozingatia mahitaji yao, unaweza kuangaza siku nyingi zijazo!

 

Tangazo #12: Jinsi vyombo vya habari vinaweza kubadilisha simulizi kuhusu kazi za utunzaji ambazo hazijalipwa

MSIMULIZI:
Kuna njia nyingi za kuboresha hali kwa wafanyikazi wa utunzaji ambao hawalipwi. Njia moja ni kwa watu wanaofanya kazi katika vyombo vya habari na wenye ushawishi kutumia majukwaa yao kupinga na kubadilisha simulizi iliyopo kwamba wanawake wanawajibika kwa kazi zote za utunzaji.

Tunaweza kurekebisha mfumo dume na kuonyesha kwamba wanaume wanaweza pia kuwa walezi wazuri na wenye uwezo wa kufanya kazi za matunzo.

Tunaweza kukuza sauti za wafanyikazi wa utunzaji wasiolipwa na kusikiliza sauti na maoni yao.

Wataalamu wa vyombo vya habari, hebu tutumie jukwaa letu kuleta mabadiliko katika maisha ya wahudumu wasiolipwa.

Acknowledgements

Shukrani:

Imechangiwa na: Ted Phido, Mwandishi huru, Lagos, Nigeria

Imehaririwa na: Zahra Sheikh Ahmed, Program analyst Women’s Economic Empowerment, UN Women East and Southern Africa Regional Office, Nairobi.

Rasilimali hii imeandaliwa kupitia  mpango wa ‘UCARE – Unpaid Care in sub-Saharan Africa‘, ambao inalenga kuongeza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake kupitia dhamira ya kugawana zaidi haki na usawa wa matunzo yasiyolipwa na kazi za nyumbani ndani ya kaya na familia katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Mradi huu unatekelezwa kwa ushirikiano wa Farm Radio International (FRI), UN Women, na The African Women’s Development and Communications Network (FEMNET) kutokana na ufadhili wa Global Affairs Canada.