Wakulima nchini Malawi wanatumia kinyesi cha wanyama kulinda mazao yao dhidi ya mbuzi wenye njaa

Ujumbe kwa mtangazaji

Save and edit this resource as a Word document.

Wakati mwingine mvua huwa hazitabiriki nchini Malawi, hivyo wakulima kushindwa kuvuna mazao ya kutosha kwa ajili ya famila zao. Mazao yanayolimwa wakati wa baridi yanaweza kusaidia. lakini, mara nyingi wakulima wanasita kulima wakati wa baridi, wakihofia mbuzi na kondoo wanaokuwa wakizurura hovyo kutafuta malisho hasa mazao yanapoanza kukua. Kama wakulima wanataka kulinda mazao yao, basi watalazimika kutumia muda wao mwingi wakiwa shambani, na wataendelea na zoezi hilo hadi wakati wa mavuno. Hali hii inamfanya mkulima kushindwa kufanya kazi zake nyingine wakati huo, kama vile kuandaa shamba kwa ajili ya kilimo wakati wa masika. Mambo hayo husababisha uhaba wa chakula kuendelea katika jamii husika.

Lakini wakulima kutoka katika sehemu ya wilaya ya Nkhotakota katikati ya nchi ya Malawi hivi sasa wana furaha. Wamekuwa wakitumia uvumbuzi waliovumbuliwa na mkulima mwenzao. Hivi sasa wanaweza kuendelea na shughuli zao nyingine bila kulazimika kulinda mazao yao wakati wa msimu wa baridi.

Muswada huu umeandikwa kutokana na mahojiano ya ukweli. Unalazimika kutumia muswada huu kuhamasisha utafiti na uandike muswada unaofanana na mazingira uliyopo. Au unaweza kutumia muswada huu katika kituo chako cha redio ukitumia sauti za waigizaji au watangazaji. Kama utafanya hivyo, hakikisha umewaeleza wasikilizaji wako mwanzo wa kipindi kuwa hizo ni sauti za waigizaji na wala sio za watu halisi waliohusika katika mahojiano hayo.

Script

Mtangazaji:
Habari ya asubuhi mpendwa mkulima. Ufuatao ni mfululizo wa kipindi kingine kiitwacho Nini kipya kinachokujia kupitia redio yako uipendayo. Leo tutabaini ni nini kipya katika kilimo cha msimu wa baridi. Uko nami, mtangazaji wako, Andrew Mahiyu.

Katika kipindi cha leo, ambatana nami katika katika wilaya ya Nkhotakota ili ujue uvumbuzi mpya. Je unaweza kuhisi ni kitu gani kimevumbuliwa katika eneo hilo?

Sauti ya pampu ya kusukuma maji

Mtangazaji:
Endelea kusikiliza wakati tukitafiti.

Muziki kwa sekunde tano,halafu utoe taratibu na kuingiza sauti za shambani –ndege, kwa mbali ng’ombe wakitembea, na sauti ya hatua zinazokanyaga majani makavu. Pandisha sauti ya maji yanayotiririka wakati mtangazaji akizungumza, halafu uicha sauti hiyo iendelee kwa chini.

Mtangazaji:
Karibu na kutana na mkulima mvumbuzi, ambaye amefanikiwa kulima mahindi katika msimu wa baridi, licha ya kuwepo mifugo inayozurura hovyo mashambani. Natembea nikishuka, kuelekea mtoni ili nikutane naye. Hebu tutafiti ni kwa nini ameamua kuchukua changamoto hii. Habari Bwana . Isaac Deko, Jina langu ni Andrew Mahiyu, mimi ni mtangazaji wa redio. Samahani nimekuja bila taarifa. Je unaweza kujitambulisha kwa wasikilizaji wetu na kuwaeleza ni nini unachokifanya hapa mtoni?

Isaac Deko:
Awali ya yote, napenda nikushukuru kwa kunitembelea. Jina langu ni Isaac Deko, mwanachama wa jumuiya ya wakulima wa Nkhunga. Hivi sasa, ninamwagilia mahindi yangu niliyoyalima wakati wa msimu wa baridi. Hiki ni kipindi cha kiangazi kama unavyofahamu. Ninatumia pampu yangu hii ya mkono kumwagilia mazao yangu. Nimepanda mahindi robo heka.

Sauti ya pambu ya maji

Mtangazaji:
Hatuwezi kuyaona mazao yake kwa vile yako urefu wa mita mbili kutoka mahali ambapo tumesimama, hapa mtoni. Mmomonyoko wa udongo umechukua udongo katika eneo ambalo liko karibu na mto, kwa hiyo inabidi tukwee kidogo ili twende tukayaone mahindi. Bwana. Deko, hatuna hakika kama maji yanayosukumwa na h ii pampu yanakwenda katika eneo lililokusudiwa. Je tunaweza kwenda kuangalia?

Isaac Deko:
Ndio tunaweza. Twende.

Sauti ya hatua zinazokanyaga kwenye majani makavu. Punguza sauti ya maji yanayotiririka.

Mtangazaji:
Oh! Hapa kuna shamba zuri la mahindi.

Isaac Deko:
Ndiyo ni zuri.

Mtangazaji:
Lakini, Bwana. Deko, nafurahi kuona shamba lingine la mahindi hapa karibu. Inaonekana kama vile kulikuwa na mtu aliyekuwa akikata na kupunguza mazao katika shamba hili. Ni nini kilitokea kwa mahindi haya?

Isaac Deko:
Hapana, hakuna mtu aliyefyeka mahindi haya. Kuna mbuzi na kondoo wanaokuja kula hayo mahindi. Wakati mwingine hata ng’ombe huwa wanayala, pale vijana wanaowachunga wanapokuwa sio makini. Katika kipindi hiki cha kiangazi, kwa kawaida huwa tunaacha mbuzi wetu na kondoo kuchunga mahali popote wanapoweza kwenda. Kutokana na hali hiyo huwa tunaacha mifugo yetu, ilishe tu hadi tunapoanza kulima mazao ya wakati wa masika.

Mtangazaji:
Lakini si mashamba yao wala uzio wao unaolindwa. Je unakaa hapa ili uwafukuze mbuzi na kondoo wasile mazao?

Isaac Deko:
Hapana, siri ni kwamba, unachukua kinmyesi cha mbuzi na kondo na kukiroweka ndani ya maji kwa siku nzima, halafu nakivuruga vizuri, kuhakikisha kuwa kimechanganyika vizuri. Baada ya hapo unachukua mchanganyiko huo na kuunyunyizia kwenye miche ya mahindi.

Mara mifugo hii inaponusa mazao yangu, haiwezi kuyala. Nafikiri kwamba, huenda mifugo hii inafikiri kuwa inapokuwa ikila mimea yenye harufu ya kinyesi chao, inahisi kuwa inakula kinyesi chao wenyewe! Kwa hiyo huwa wanaacha mazao yangu na kwenda mahali pengine, ambapo mazao hayana harufu ya kinyesi cha mifugo. Huyu mmiliki wa shamba hili la mahindi lililo jirani na mimi, hafanyi kama mimi ninavyofanya. Yeye huwa anafikiria kuwa mimi natumia ushirikina katika shamba langu. Lakini kuna siku Fulani nilimweleza kuhusu siri yangu. Alifuata maelekezo niliyompatia siku mbili zilizopita. Sidhani kama mbuzi watakula mahindi yake tena.

Mtangazaji:
Wewe binafsi ulivumbuaje ujanja huu?

Isaac Deko:
Vizuri, mkulima ni lazima awe kama mtafiti. Inatubidi tutafute mbinu za kawaida za kukabiliana na matatizo tunayokumbana nayo kila siku katika shughuli zetu za kilimo. Hatulazimiki daima kusubiri mtu Fulani afanye utafiti kwa ajili yetu.

Kama ulivyoona, hii ni njia rahisi. Lakini, inafanya kazi! Je huu si utafiti? Kwa mara ya kwanza nilipakaza kinyesi cha wanyama katika sehemu moja ya mti, ambayo mbuzi walikuwa wakipenda sana kuila. Nilichogundua ni kwamba, wale mbuzi walikuwa wakipita katika lile eneo bila kuusogolea ule mti. Baadaye nikaamua kujaribu utaalamu huu kwenye mahindi yangu. Nilichogundua ni kwamba, mbuzi walikuwa hawali mahindi yangu. Hivi ndivyo livyobaini jambo hili.

Mtangazaji:
Je ni kwa muda gani harufu ya kinyesi cha wanyama inaendelea kukaa kwenye mmea?

Mtangazaji:
Hiyo ni habari njema. Je unatarajia kupata maguni mangapi ya mahindi kutoka katika eneo hili ulilolima?

Isaac Deko:
Naamini nitapata maguni tisa ya mahindi ambayo tayari yamepukuchuliwa, yenye uzito wa kilo hamsini kila gunia.

Hatuwezi kufa kwa njaa kutokana na mifugo hii inayozurura hovyo, huo ndio ufumbuzi wake. Kwa yeyote ambaye anadhani kuwa mbinu hii haiwezi kufanya kazi, niko tayari kumsaidia bila malipo yoyote.

Mtangazaji:
Hali ilikuwaje, ulipokuwa bado hujafahamu mbinu hii?

Isaac Deko:
Ilikuwa inachosha sana. Mke wangu alilazimika kushinda siku nzima shambani, wakati mimi nililazimika kubaki nyumbani nikifanya kazi nyingine. Hiyo ilikuwa mwaka 2005 na 2006. Alilazimika kupika na kula chakula chake hapa hapa shambani, na kurejea nyumbani jioni. Alilazimika kufanya zoezi hili kila siku hadi tunapovuna. Unajua kuwa, hiki ndio kipindi cha mwaka ambapo huwa tunaandaa mashamba yetu kwa ajili ya mazao ya msimu wa masika. Lakini hatukuweza kujishughulisha zaidi na utayarishaji wa mashamba, hadi pale tunapokuwa tumemaliza kuvuna. Muda wote tulikuwa tukichelewa kuandaa mashamba yetu, hali kadhalika tulikuwa tukichelewa kupanda mbegu. Hali hiyo iliathiri shamba. Lakini hivi sasa tunaweza kufanya kazi zetu kama kawaida.

Mtangazaji:
Je kuna wakulima wengine hapa karibu tunaoweza kuwatembelea ambao wamefuata utaratibu kama huu wa kwako?

Isaac Deko:
Ndio, Yupo Bwana. Levison Kasakula Mwale. Ana shamba la mahindi hapa karibu. Alifuata kile ninachofanya. Alipata mavuno mazuri ya mahindi. Mazao yake hayakuliwa na mbuzi. Tunaweza kwenda kuzungumza naye. Bila shaka yuko shmabani kwake.

Sauti za hatua zinazokanyaga majani makavu

Mtangazaji:
Habari za mchana, mama (angalizo: mwanamke au mama).

Sauti ya mbuzi kwa mbali

Florida Kasakula:
Oh, Kumbe nina wageni leo. Karibuni.

Mtangazaji:
Asante sana. Jina langu ni Andrew Mahiyu. Tumekuja hapa kujifunza jinsi unavyoweza kuyalinda mazao yako dhidi ya mifugo inayozurura hovyo. Tulidhani, tungeweza kumkuta mume wako. Lakini kwa vile upo, bila shaka unajua jinsi ya kulinda mazao yako dhidi ya wanyama. Je unaweza kujitambulisha?

Florida Kasakula:
Napenda kuanza kwa kusema kuwa mume wangu hayupo anajishughulisha na kazi nyingine. Jina langu ni Florida Kasakula. Tulijifunza mbinu hii toka kwa Bwana Isaac Deko. Alitufundisha jinsi ya kuloweka mavi ya mbuzi na yale ya kondoo pamoja na kuyachanganya vizuri, na kisha kuunyunyizia mchanganyiko huo kwenye miche ya mahindi. Kwanza tulijaribu kunyunyizia katika sehemu ndogo ili tuone kama inafanya kazi. Kweli, ilifanya kazi. Mbuzi walikuwa wakija na kunusa, kisha wakaondoka. Kwa hali hiyo tukagundua kuwa mfumo huu ni wa ukweli.

Mtangazaji:
Hivi una hakika kabisa kwamba mbuzi hawawezi kula haya mahindi?

Florida Kasakula:
Hawawezi. Wao wanakuja kujificha jua tu, na baadaye kwenda zao bila kula hata jani moja. Njia hii ni ya uhakika.

Mtangazaji:
Ulikuwa ukifanya nini kabla hujagundua mbinu hii?

Florida Kasakula:
Hali ilikuwa inatisha. Tulilazimika kujenga kibanda cha muda cha kupumzikia wakati tukiwasubiri hawa mbuzi. Tulitumia siku nzima hapa, tukipika na kula na hatimaye kulazimika kuondoka baada ya jua kuzama. Kama ningethubutu kwenda nyumbani hata kwa dakika tano tu, basi ningekuta sehemu kubwa ya mahindi imeshaliwa.

Lakini hivi sasa hatufi kwa njaa kwa ajili ya mbuzi. Tutakuwa na chakula karibu mwaka mzima.

Mtangazaji:
Bila shaka familia za Kasakula na Deko hazitakufa kwa njaa. Karibu mwaka mzima familia hizi zitakuwa na mahindi. Na hakuna sababu ya kulinda mazao shambani. Wanaweza kuendelea na shughuli zao za kilimo katika shamba lao kubwa na wakawa tayari kupanda mazao ya msimu ya mvua kwa wakati. Hii ni kwa sababu ya mbinu mpya iliyogunduliwa na mkulima mmoja na akwaambia wakulima wenzake, ili waweze kukabiliana na njaa katika eneo lao. Kama na wewe ulikuwa na tatizo kama hilo, bila shaka umejifunza kutoka kwa Isaac Deko na Florida Kasakula.

Hadi wakati mwingine, kutoka katika kipindi cha Nini kipya, mimi ni Andrew Mahiyu.

Pandisha muziki na halafu upunguze taratibu

Acknowledgements

Washiriki: Andrew Mahiyu, Jumuiya ya chama cha kitaifa cha wakulima nchini Malawi (NASFAM), ushirika wa kimataifa wa redio ya Farm.
Imepitiwa na: Dilip Bhandari, Afisa mipango wa Asia/South Pacific, Makamu wa rais wa uhamasishaji katika Heifer International, & Terry Wollen, , Heifer International.

Information sources

Mahojiano na wakulima kutoka katika moja ya jumuiya za NASFAM katika wilaya ya Nkhotakota nchini Malawi, yaliyofanyika Septemba 10, 2009.

Shukrani za dhati kwa Commonwealth of Learning (COL), shirika la Umoja wa mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na utamaduni (UNESCO), tShirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), serikali ya Canada kupitia shirika lake la misaada la (CIDA), Taasisi ya misaada ya Canada, chama cha watangazaji wa redio za Kanda duniani (AMARC), Shirika la habari la Afrika (IPS) , na kituo cha Ufundi cha kilimo na ushirika vijijini (CTA), kwa kufadhili uandishi wa mashindano ya miswada ya redio kuhusiana na uvumbuzi wa wakulima wadogo.