Madeline na Musa: Kilimo cha maharage ya Soya kwa mazao bora na kipato

Uzalishaji wa mazao

Ujumbe kwa mtangazaji

Maelezo kwa mtangazaji

Kuna sababu nyingi za kulima maharage ya soya. Maharage ya soya yanavirutubisho vingi yakiwa na asilimia 40 ya protini. Maharage ya soya yanaweza kutumika kama chakula kwa familia na yanaweza kusindikwa kama maziwa ya soya, mafuta ya kupikia, na bidhaa mbalimbali ikiwemo kutengeneza chakula cha kulikiza kwa watoto. Pia ni chanzo kizuri cha protini katika vyakula vya wanyama.
Kuma uhitaji mkubwa wa maharage ya soya katika masoko na kwa bei nzuri zaidi. Hivyo kulima zao la maharage ya soya na kuuza inaweza kuongeza kipato kwa wakulima.

Na mwisho, mabaki ya zao la soya yana madini ya nitrojeni, hivyo kuongeza rutuba kwenye udongo. Lakini kama mazao mengine, maharage ya soya yanafanya vizuri zaidi kama mkulima akitumia utaalamu uliopendekezwa. Kwa mfano, wakipanda mbegu za kisasa au za asili kama ilivyopendekezwa na wataalamu wa kilimo na kuacha nafasi sahihi kati ya mimea kwenye mstari.

Igizo hili linaonesha kwamba, maarifa ya kilimo yanaweza kuja kwa kupitia vyanzo visivyotarajiwa. Kuna jamii inayopata wakati mugumu wa mavuno mabaya ya maharage ya soya na hawawezi kungudua chanzo cha tatizo lao. Mwisho wa siku wanaokolewa na chanzo ambacho hawakutarajia: Ni kijana mmoja kutoka kijiji cha jirani.

Unaweza kutumia igizo hili kuhamasisha kuandaa programu ya hatua zinazopendekezwa ili kuzalisha maharage ya soya katika eneo lako. Au unaweza kuchagua kuwasilisha igizo hili kama sehemu ya mpango wako katika kilimo, kwa kutumia wasanii wa sauti na kuwawakilisha wasemaji.

Unaweza kufuatilia igizo hili kwa kuwahoji wakulima na wataalamu wa maharage ya soya. Wakaribishe wasikilizaji kupiga simu au kuandika meseji za maswali na kutoa maoni yao. Mada kwa ajili ya majadiliano yanaweza kuwa kama:

  • Wazalishaji wa maharage ya soya wana fursa gani nzuri kwenye soko?
  • Ni changamoto gani endelevu au ugumu gani wakulima wa zao la soya wanapitia? Na nini suluhu za hizi changamoto?
  • Je kuna vikwazo vyovyote vinavyozuia kutumia suluhu hizi?

Kumbuka: Mwishoni mwa kila tukio, jina la mhusika mmoja limetajwa, sambamba na neno “Kudhibiti.” ” Mhusika mkuu” ni mhusika ambaye ni muhimu sana katika tukio, na anaongoza vitendo na mwelekeo wa shughuli. Mhusika mkuu lazima asimame karibu kidogo na kipaza sauti kwa ajili ya tukio hilo.

Igizo hili ni la dakika 25. Pamoja na muziki wa utambulisho na kumalizia.

Script

Sehemu ya kwanza
Eneo: Ndani: Nyumbani kwa Bibi Anase. Mchana.
Wahusika: Bibi Anase na Madelina
Kwa umbali SFX: Tunasikia kelele za mlango ukigongwa.

SFX:
TUNASIKIA KELELE ZA MLANGO UKIGONGWA NA BIBI ANASE.

BIBI ANASE:
(KARIBU NA MIC, ANAPAZA SAUTI) Mende! Mende! Wewe, Mendelina!

SFX:
BIBI ANASE ANAITA HUKU AKIENDELEA KUGONGA MLANGO.

BIBI ANASE:
Mende! Wewe Mende, kwani leo huendi shule?

MADELINA:
(SAUTI INATOKEA CHUMBANI, MBALI NA MIC) Nakuja bibi.

SFX:
MLANGO UNAFUNGULIWA

MADELINA:
(AKISOGELEA MIC) bibi, kila siku nakwambia jina langu halitamkwi Mendelina, ni Madelina! Shikamoo bibi.

BIBI ANASE:
Marahaba. Leo utachelewa shule!

MADELINA:
Nilikuwa namalizia kuvaa!

BIBI ANASE:
Unajua nini mjukuu wangu, unapenda sana kulala. basi malizia tufunge mlango; mimi pia nataka nitoke.

MADELINA:
(KWA MSHANGAO) Eeh! Kwani bibi unaenda wapi?

BIBI ANASE:
Tuna kikao cha wanakijiji wote leo na mkuu wa halmashauri ya wilaya. Tena nimeshachelewa!

MADELINA:
Kikao hicho kinahusu nini?

BIBI ANASE:
Tunaenda kujadili kuhusu mavuno ya maharage ya soya kwa mwaka huu.

Mhusika Mkuu:
Bibi Anase

 

Sehemu ya pili:
Eneo : Nje. Shambani kwa Mama John: Mchana.
Wahusika: Bibi Anase na Mama John
Kwa umbali SFX: Mama John analima

SFX:
MAMA JOHN ANALIMA

BIBI ANASE:
(AKISOGELEA MIC) Wewe Mama John, hauendi kwenye kikao?

MAMA JOHN:
(KARIBU NA MIC) Kwani kikao ni leo jamani?

BIBI ANASE:
Ehee! Kumbe mwenzangu huna hata habari? Hujambo lakini?

MAMA JOHN:
(AKIHEMA KWA UCHOVU) Sijambo shikamoo, za huko?

BIBI ANASE:
Nzuri! Eeh! Naona tayari unaandaa shamba kwa ajili ya msimu ujao.

MAMA JOHN:
Ndugu yangu si umeona mwenyewe mavuno ya mwaka huu.

BIBI ANASE:
Sasa mama John jamani si ndio twende kwenye kikao tukajadili na wenzetu ili tupate suluhisho!

SFX:
MBUWA, TUNASIKIA SAUTI YA MLEVI KWA MBALI AKIWA ANAIMBA KWA SAUTI YA MTU ALIYELEWA

MAMA JOHN:
Subiri kwanza, si unamkumbuka yule mwanangu Erick?

MBUWA:
(AKIIMBA KWA SAUTI YA MLEVI) Ukisikia sauti ya mtu mzima analia, rafiki yangu! (ANABEUWA). Jua tu kuna tatizo.

MAMA JOHN:
(KWA MAMLAKA) Kuna nini tena Mbuwa? Mapema mapema hivi unatuvurugia amani!?

BIBI ANASE:
Ehhe Mama John! Kwani huoni kama amelewa?

MBUWA:
(AKIENDELEA KUIMBA HUKU AKILIA) Ukisikia sauti ya mtu mzima analia, rafiki yangu! Jua tu kuna tatizo.

MAMA JOHN:
(ANACHEKA) Mungu wangu! Maajabu ya dunia!

BIBI ANASE:
Mbuwa! Kwanini unalia?

MBUWA:
(ANALIA KWA HISIA) Swali gani hilo unaniuliza? Kwani hujaona mavuno ya maharage ya soya msimu huu?

BIBI ANASE:
Tumeona, na ndiyo maana tunaenda kwenye kikao cha kijiji ili tujadili haya mavuno mabaya!

MAMA JOHN:
(ANAMKATIZA) Kwanini unasikiliza upumbavu wake, Bibi Anase?! Kwani huoni kama kalewa?

MBUWA:
Nani kalewa? Mimi sijalewa.

MAMA JOHN:
(AKIWA AMEKASIRIKA) Endelea, Mbuwa, ondoka! Hebu tuondokee hapa!

MBUWA:
(ANAANZA KUONDOKA) Naondoka, lakini kumbuka kuwa nimeongea na mungu asubuhi na amesema ataleta mtume wa maharage ya soya kutusaidia kwenye uzalishaji.

BIBI ANASE:
(AKICHEKA) Rafiki yangu, hayo ndiyo madhara ya pombe.

MAMA JOHN:
(KWA MSHANGAO) Mbuwa ni msumbufu wakati mwingine.

BIBI ANASE:
Hata hivyo, tulikuwa tunazungumzia kitu kingine kabla Mbuwa hajaingilia mazungumzo yetu.

MAMA JOHN:
Ndiyo ndiyo, tulikuwa tunamzungumzia mwanagu Erick.

BIBI ANASE:
Si yule anayemfata John?

MAMA JOHN:
Ehee! Huyo huyo! Jana kaniletea mbolea ya kienyeji! Ndio hii najaribu kuweka kwenye udongo hapa. Kumbe mwenzangu tulikua tunakosea kutumia mbolea za kisasa yanauwa ardhi yetu!

BIBI ANASE:
Kwani unafikiri hizo mbolea ndio tatizo?

MAMA JOHN:
(KWA MSISITIZO) Sio tu mbolea lakini pia kaleta madawa ya kinga! Sasa wewe unafikiri chanzo cha kupata mavuno mabovu mwaka huu ni nini?

BIBI ANASE:
Nahisi pia ardhi imepoteza rutuba asilia, hebu angalia rangi yake!

MAMA JOHN:
Mimi nakwambia ni mbolea za kisasa tunazozitumia. Zina sumu!

BIBI ANASE:
Sawa Mama John kajiandae twende kwenye kikao. Tutajua vizuri sababu ni nini huko!

MAMA JOHN:
Subiri namalizia sasa hivi kuweka mbolea.

BIBI ANASE:
Mpaka umalize, kikao kimeisha. Fanya ukajiandae na wewe!

MAMA JOHN:
(ANAANZA KUONDOKA) Acha nikavae, naona ukiwepo sifanyi chochote hapa!

BIBI ANASE:
ANACHEKA) Habari ndiyo hiyo! twende bwana, umoja ni nguvu!

Mhusika Mkuu:
Bibi Anase

Sehemy ya tatu
Eneo: NJE. Shuleni. Mchana.
Wahusika: Madelina, Musa na Faraja
Kwa umbali SFX: Sauti ya kengele ya shule

SFX:
TUNASIKIA SAUTI YA KENGELE YA SHULE

SFX:
TUNASIKIA SAUTI ZA WATOTO WAKIKIMBIA NA KUCHEZA

FARAJA:
(KWA SHAUKU) Madee twende kwa mama Boni kabla mihogo haijaisha!

MADELINA:
Tumsubiri Musa.

FARAJA:
(ANAGUNA) Kwani Musa hapajui pale? atakuja mwenyewe?

MADELINA:
Hapana bwana alisema tumsubiri!

FARAJA:
Eeeh! Musa naye asitajwe! yule anakuja!

MUSA:
(AKIKARIBIA MIC) Mambo zenu?

ALL:
Poa!

FARAJA:
Tulikuwa tunakusubiria wewe twende tukale mihogo!

MADELINA:
Tuwahini bwana nina kipindi cha kemia baada ya mapumziko.

SFX:
WOTE WANAANZA KUTEMBEA.

FARAJA:
Eeh! Alafu mwalimu Kalimi anavyopenda sifa, ukichelewa kidogo tu msala!

MUSA:
(ANACHEKA) Hana shida ili mradi tu ufanye kazi zake!

MADELINA:
Ni rahisi kwako wewe kusema kwa sababu huwa unafaulu somo lake!

FARAJA:
(AKIINGILIA) Hebu tupe ubuyu!

MUSA:
Hapana kawaida tu, alafu Madee leo tukitoka si tutaenda wote nyumbani kudiscuss?

MADELINA:
Du nafikaje kwenu, Baba yako alivyokuwa mkali na ninavyomuogopa!

FARAJA:
Ndiyo kwanza…nimefeli mtihani wake wa mwisho nilifeli.

MUSA:
(KIUTANI) Mhm! Faraja tumeshakuzoea kila siku tu wewe unafeli geografia!

SFX:
WANACHEKA

MADELINA:
Musa kwenu mbali bwana, nikichelewa bibi atanimaindi!

MUSA:
Si utamwambia tulikuwa tunajisomomea!

MADELINA:
Faraja tutaenda wote?

FARAJA:
Haiwezekani! mimi nikitoka shule inabidi nikachote maji mtoni.

MUSA:
Madee unajua kabisa Faraja hapendi kusoma alafu unamuuliza!

SFX:
WOTE WANACHEKA

FARAJA:
Achana na mimi! Nani hapendi kusoma?

MUSA:
Si wewe?

MADELINA:
Poa Musa, tutaenda lakini itabidi niwahi kurudi nimsaidie bibi!

MUSA:
Freshi.

SFX:
KELELE ZA WANAFUNZI WAKIGOMBANIANA MIHOGO.

FARAJA:
Jamani tukiendekeza stori mwisho tutakosa mihogo!

Mhusika mkuu:
Madelina

Sehemu ya Nne
Eneo: NJE : Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya. Mchana
Wahusika: Bibi Anase, Mama John, Lugano, Mzee Mpalu, Ali na Monica
Sauti ya umbali SFX: Tunaona mandhari ya halmashauri ya wilaya

LUGANO:
Za asubuhi wajumbe.

ALL:
Nzuri.

LUGANO:
Nilitegemea tungeaza kikao mapema lakini naona watu bado wanaendelea kufika. Bibi Anase na Mama John nao ndio wanafika.

BIBI ANASE:
(WAKISOGELEA MIC) Habari zenu?

ALL:
Nzuri!

LUGANO:
Sawa! Naona tuanze kikao chetu sasa. Wengine wakija wataungana nasi. Mimi kama mkuu wa wilaya ya halmashauri ya Matopile nimeamua kuitisha kikao hiki hapa kijijini ili tuweze kujua nini tatizo yanayotokana na mavuno mabaya ya maharage ya soya kwa msimu huu.

MZEE MPALU:
(ANADAKIA) Ni misimu mitatu sasa!

LUGANO:
Unachosema ni kweli kabisa, ni misimu mitatu sasa hili tatizo limekuwepo. Sasa ningependa niwaulize nyie wajumbe wenzangu, mnafikiri tatizo ni nini?

SFX:
KILA MTU ANAJARIBU KUONGEA

LUGANO:
(AKIJARIBU KUWATULIZA) tusikilizane! Mmoja baada ya mwingine! Haya bwana Ali!

ALI:
Kwa kusema kweli mkuu sijui tatizo ni nini! Kwa sababu tumekuwa tukitumia mbegu za kisasa kwa kuzipanda kama mlivyotuelekeza!

LUGANO:
Samahani mkuu kwa kukukatisha lakini inabidi useme tatizo ni nini na suluhu kwa tatizo hilo. Mama John endelea.

MAMA JOHN:
Mimi naona tatizo ni mbolea tulizokuwa tukitumia, Hizi mbolea za kisasa zinaua mimea yetu!

MZEE MPALU:
(ANADAKIA) Mimi nakataa! Tatizo sio mbolea za kisasa, mbona mimi nimekuwa natumia mbolea za kienyeji lakini matokeo yake ni mavuno mabaya!

MAMA JOHN:
(ANAMKATISHA) Labda aina ya mbolea uliyotumia sio nzuri!

LUGANO:
(ANAWAKATISHA) Msibishane tafadhali, ni muhimu kukumbuka sababu ya kikao hiki. Tuko hapa kupata suluhu.

BIBI ANASE:
Mheshimiwa naomba niseme kitu.

LUGANO:
Haya, Bibi Anase.

BIBI ANASE:
Asante sana, najua tuko hapa kwa ajili ya kutafuta sababu ya mimea kuathirika. Lakini ningependa kukumbusha kwamba miongoni mwetu tungependa kuuza hata kidogo tulichovuna msimu huu. Sasa sijui utatusaidaje?

LUGANO:
Sawa, umeongea jambo la msingi sana bibi Anase. Kuhusu hilo, nimepanga kuongea na wakuu wa halmashauri za wilaya nyigine kuhusu masoko na kama tutaweza kupata masoko huko kwingine.

ALI:
Kwanini? Tukizingatia maharage ya soya, ni zao ambalo linauzika sana.

BIBI ANASE:
Jamani, mimi nina wazo jamani. Mnaonaje tukichanganya hicho kidogo tulichopata msimu huu tukakiuza kwa pamoja kisha tukagawana pesa?

MONICA:
(ANAPAYUKA) Na hizo pesa tutagawana vipi?

MZEE MPALU:
(ANADAKIA) Haiwezekani!

SFX:
KELELE ZINAANZA TENA HUKU LUGANO AKIJARIBU KUWATULIZA.

Muhusika mkuu:
Lugano

Sehemu ya 5
Eneo: Nje: Nyumbani kwa. Mchana.
Wahusika: Madelina na Musa
Kwa umbali SFX:: Madelina na Musa wakitembea

SFX:
MADELINA NA MUSA WAKITEMBEA

MUSA:
Na hapa ndio shambani!

MADELINA:
Haya ni mazao gani?

MUSA:
Maharage ya soya.

MADELINA:
(Anashangaa) Unasema kweli?

MUSA:
Ndio. Kwani hujawahi kuona maharage ya soya yakiwa shambani?

MADELINA:
Nimewahi lakini sijawahi kuona maharage ya soya yamestawi kiasi hiki. Bibi yangu alipanda maharage msimu huu lakini mavuno hayakuwa mazuri.

MUSA:
Unasema kweli?

MADELINA:
Yaani kijiji kizima mavuno hayakuwa mazuri msimu huu.

MUSA:
Kwani tatizo ni nini?

MADELINA:
Kwakweli hatujui, kila mtu anaongea yake. Bibi anasema ardhi imepoteza rutuba yake.

MUSA:
Inawezekana.

MADELINA:
Nilipoondoka, nimemuacha bibi ameenda kwenye kikao kwa ajili ya kujadili jinsi ya kutatua tatizo la mavuno mabaya ya maharage ya soya pale kijijini.

MUSA:
Poleni sana jamani.

MADELINA:
Asante sana. Kwa hiyo nani amewasadia kupanda haya maharage ya soya mpaka yakafikia hapa?

MUSA:
Ni mimi na baba yangu tu.

MADELINA:
KWA MSHANGAO) Unasema kweli?

MUSA:
Ndio. Baba amenifundisha kila kitu kuhusiana na kilimo cha maharage ya soya.

MADELINA:
Unafikiri siku moja unaweza kuja kijijini kwetu kumuelekeza bibi yangu kuhusu kilimo cha maharage ya soya?

MUSA:
Sawa, nitafurahi kuja.

MADELINA:
(KWA FURAHA) Hiyo Itakuwa nzuri sana.

Mhusika mkuu:
Madelina

Sehemu ya sita
Eneo: Nje: Nyumbani kwa Bibi Anase. Jioni
Wahusika: Madelina na Bibi Anase
Kwa umbali SFX: Bibi Anase akiosha vyombo

SFX:
BIBI ANASE AKIOSHA VYOMBO

MADELINA:
(AKIKARIBIA MIC) Shikamoo bibi!

SFX:
MADELINA ANAFUNGUA MLANGO NA KUINGIA NDANI.

BIBI ANASE:
(KARIBU NA MIC) Wewe Mendelina ebu njoo hapa! (ANAPAZA SAUTI) Mende!

MADELINA:
Abee bibi.

BIBI ANASE:
Saa ngapi sasa hivi?

SFX:
MADELINA ANAKAA KIMYA

BIBI ANASE:
Si nakuuliza.

MADELINA:
Saa kumi na mbili bibi.

BIBI ANASE:
Saa hizi ndio mnatoka shule?

MADELINA:
Hapana.

BIBI ANASE:
Tatizo ni nini?

MADELINA:
Bibi nilipitia kwa rafiki yangu Musa, yule mtoto wa mwalimu wa geografia.

BIBI ANASE:
Ulipitia nyumbani kwa rafiki yako eeh? Mbona yeye asije kwenu?

MADELINA:
Amesema atakuja, alafu bibi nimekuta maharage ya soya nyumbani kwao yamestawi hadi raha! Akasema atakuja kutusaidia kupanda maharage ya soya!

BIBI ANASE:
Sijakataa kutembelea marafiki zako lakini kwanini usirudi nyumbani kwanza? Unanifanya nipate wasiwasi nikifikilia uko wapi.

MADELINA:
Samahani bibi, sitarudia tena.

BIBI ANASE:
Hebu nionee huruma, nimerudi nimekuta vyombo vichafu. Hivi kweli nimetoka kwenye kikao nianze kuosha vyombo tena jamani?!

MADELINA:
Nisamehe bibi, nimekukosea! Subiri nikusaidie kuviosha.

SFX:
MADELINA ANAMSAIDIA BIBI ANASE KUOSHA VYOMBO.

Sehemu ya saba
Eneo: Nje. Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya. Mchana.
Wahusika: Madelina, Bibi Anase, Musa, Lugano, Ali, Mzee Mpalu, Mama John na Monica
Kwa umbali SFX: Wanakijiji wanabishana

SFX:
WANAKIJIJI WANABISHANA.

MAMA JOHN:
(ANAPAZA SAUTI) Hizo mbolea za kisasa ni sumu na ndio zinasababisha mavuno mabaya.

ALI:
(ANAMKATISHA) Haiwezekani! Mimi nimetumia sana mbolea za kienyeji mbona sijaona mabadiliko yoyote.

MZEE MPALU:
(ANAPAYUKA) Mimi nawaambia ardhi yetu imelaaniwa!

SFX:
LUGANO ANAGONGA JIWE KWENYE MEZA ILI KUWATULIZA WANAKIJIJI.

LUGANO:
(AKIJARIBU KUWATULIZA) Naomba tusikilizane! Tusikilizane jamani!

SFX:
WATU WANANYAMAZA KIMYA.

LUGANO:
Naomba tusikiklizane jamani, hatujaja hapa kubishana. Hiki ni kikao chetu cha pili lakini bado hatujapata suluhu ya suala letu la kilimo cha maharage ya soya.

SFX:
MADELINA NA MUSA WANATOKEA NA GHAFLA KUNAKUWA NA UKIMYA.

MADELINA/MUSA:
(WAKIKARIBIA MIC) Shikamoo!

SFX:
WANAKIJIJI WANANYAMAZA KIMYA

MONICA:
Hawa watoto wamekuja kufanya nini jamani.

BIBI ANASE:
(KWA UKALI) Wewe Mendelina! Umekuja kufanya nini huku?

MADELINA:
Nimemleta rafiki yangu, anaitwa Musa.

MUSA:
Shikamoni!

SFX:
KILA MTU ANABAKI KIMYA.

BIBI ANASE:
Kwanini hamjaenda shule?

MADELINA:
Hatuna vipindi leo tumefanya mtihani tu!

ALI:
(ANADAKIA) Aise mimi naona hawa watoto wanatupotezea muda tu.

MONICA:
Ni kweli kama wanataka kuongea na bibi yao si wamsubiri huko huko nyumbani!

MAMA JOHN:
Kweli kabisa, Bibi Anase waambie warudi nyumbani!

MZEE MPALU:
(KWA HASIRA) Nyie watoto tabia gani hiyo? Mnakuta watu wazima wanaongea alafu mnakuja kuingilia maongezi yetu. Hivi ndivyo unavyowafundisha watoto wako?

BIBI ANASE:
Ni wajukuu zangu!

MZEE MPALU:
(KWA UKALI) Haijalishi! Hawana adabu kabisa!

ALI:
Mhm! watoto wa siku hizi.

LUGANO:
(ANAINGILIA KATI) Inatosha! Inatosha jamani! haina haja ya kulalamika sana. Bibi Anase hebu waambie wajukuu zako wakakusubirie huko nyumbani!

BIBI ANASE:
Haya Mendelina nendeni nyumbani!

MADELINA:
(ANAPAYUKA) Musa anaweza kuwaelekeza jinsi ya kupanda maharage ya soya vizuri!

LUGANO:
Unasemaje?

SFX:
WANAKIJIJI WOTE WANACHEKA

ALI:
(AKIENDELEA KUCHEKA) Hawa watoto wa siku hizi wanajifanya wajuaji sana!

MONICA:
Eti atatusaidia kupanda maharage ya soya! Hawa watoto wanaweza kutufundisha nini sisi?!

MZEE MPALU:
Bibi Anase, waambie wajukuu zako waenda wakalale.

MADELINA:
(ANAPAYUKA) Ninachokisema ni kweli! Yeye na baba yake wamevuna maharage mengi ya soya mwaka huu na baba yake ndio kamfundisha! Kwahiyo anaweza kutusaidia.

ALI:
(ANAMKATISHA) Wewe mtoto ebu shika adabu yako! Amsaidie nani?!

LUGANO:
Hebu Subiri kwanza! Eti bibi Anase mjukuu wako anasema kweli?

BIBI ANASE:
Siku moja aliwahi kuniambia kuwa ana rafiki yake ambaye kwao wamefanikiwa kuvuna maharage mengi ya soya. Lakini sina uhakika kama ni kweli.

LUGANO:
Basi tuwape nafasi jamani, kama ni kweli wanayosema. Bwana mdogo upo tayari kutupa darasa?

MUSA:
(KWA SAUTI YA CHINI) Ndiyo

LUGANO:
Kwahiyo lini utapa muda wa kuje kutufundisha?

MUSA:
Jumamosii hii kwasababu sitaenda shule,

LUGANO:
Sawa haina shida, jamani tumesikia? Tutapata somo hili siku ya Jumamosi

Mhusika mkuu:
Madelina

Sehemu ya 8
Eneo: Nje. Shambani kjwa Bibi Anase. Mchana.
Wahusika: Bibi Anase, Madelina, Musa, Lugano, Monica, Mzee Mpalu, Ali, Mama John na Baba Musa
Kwa umbali SFX: Tunaona mandhari ya shamba la bibi Anase

SFX:
WANAKIJIJI WAKINUNG’UNIKA

MZEE MPALU:
(KWA UKALI) Nilijua hapa tunapotezeana muda tu.

MONICA:
Haswa! Toka lini mtoto mdogo kama Yule awafundishe watu wazima kama sisi kuhusu kilimo?!

ALI:
Hiki ni kichekesho kabisa, Yule anajua nini kuhusu kilimo cha maharage ya soya?

MAMA JOHN:
(ANAINGILIA) Alifundishwa na baba yake ambaye ni mwalimu ya jiografia. Lazima atakuwa na maarifa mengi kuhusu kilimo zaidi ya wengi wetu hapa!

MZEE MPALU:
(KWA HASIRA) Huu ni upuuzi

BIBI ANASE:
Unamaanisha nini ukisema huu ni upuuzi? Ungekuwa unajua, tusingekuwa na hili tatizo, kwani uongo?

ALI:
Sasa ona, mpakata sasa hajafika kama alivyoahidi?

LUGANO:
Tafadhali wajumbe, achene kulalamika sana, lazima atakuwa amepatwa na dharula. Tunaomba tuwe wavumilivu kwa dakika chache zijazo.

ALI:
Nitasubiri kwa dakika tano tu. Asipotokea mimi naondoka, Ninamambo mengine muhimu zaidi za kufanya!

MONICA:
Hata mimi pia!

MZEE MPALU:
Huyu mtoto anatabia gani? kuwaweka watu wazima mpaka sasa hivi?

SFX:
TUNASIKIA SAUTI YA PIKIPIKI

BIBI ANASE:
Anaweza kuwa ndiyo huyo kwenye pikipiki?

LUGANO:
Ndiyo, hata mimi nafikiri ndiyo yeye.

SFX:
PIKIPIKI INAFIKA KISHA INASIMAMA

BABA MUSA:
Habari zenu!

ALL:
Nzuri!

MUSA:
Shikamoni!

ALL:
Marahaba!

MONICA:
Huyu ni nani?

BABA MUSA:
Mimi ni baba yake Musa, naitwa Mzee Shamte!

BIBI ANASE:
(KWA FURAHA) Oooh! Ni mwalimu wa Jiografia!

LUGANO:
(KWA FURAHA) Hivyo! Karibu sana! Karibu kijijini kwetu! Kwa jina naitwa Lugano, Ni mkuu wa halmashauli ya wilaya hapa. Nimefurahi sana kukuona!

BABA MUSA:
Nimefura pia. Musa aliniambia kuwa leo atakuja kijijini kwenu kufundisha juu ya mavuno bora ya maharage ya soya. Sikuamini! Nilijua ananitania tu. Hivyo nimeamua kumleta ili nijionee mwenyewe.

LUGANO:
Kusema kweli, wote tulikuwa tunamsubiri tu yeye!

MZEE MPALU:
(ANADAKIA) Na tumemsibiri kwa muda mrefu sana!

BABA MUSA:
Kumbe ni kweli!

BIBI ANASE:
Musa alituambia kuwa mlipata mavuno mengi ya maharage ya soya kijijini kwenu!

MAMA JOHN:
Ni kweli alituambia! Unaweza kutupa maarifa uliyotumia ili kupata mavuno mengi ya maharage ya soya?

MONICA:
(KWA MSISIMKO) Tafadhali tuelekeze!

ALL:
(KWA PAMOJA) Tafadhali tuelekeze!

LUGANO:
(AKIWATULIZA WANAKIJIJI) Tafadhali naomba ukimya wenu, tumpe bwana Shamte nafasi ya kuongea.

BABA MUSA:
Sawa, mimi na kijana wangu, tutafurahia sana kuwafundisha mbinu mbalimbali za kufuata ili kupata mavuno mengi na bora ya maharage ya soya.

SFX:
WOTE WANASHANGILIA

BABA MUSA:
Lakini kabla ya yote, ningependa kuwauliza – mnafikiri ni tatizo gani linapelekea kupata mavuno machache ya maharage ya soya?

MAMA JOHN:
(ANAINGILIA) Mimi nafikiri ni mbolea za kisasa ambazo tunazitumia. Zinapoteza rutuba ya udongo!

MONICA:
Sawa kabisa, na hizo dawa tunazo nyunyizia pia!

BABA MUSA:
Sidhani kama hilo ndilo tatizo, Mimi natumia mbolea za kisasa na nanyunyizia dawa za kiasasa.

ALI:
(ANADAKIA) Mmeona! Niliwaambia tatizo sio mbolea za kisasa!

BABA MUSA:
Itakuwa ni kitu kingine!

LUGANO:
(MSHANGAO) Unahisi inaweza kuwa ni nini??

BABA MUSA:
Inaweza kuwa upaliliaji mmbaya!

MAMA JOHN:
Unafikiri hilo linaweza kuwa ni tatizo?

BABA MUSA:
Lazima ufuate mbinu bora za upaliliaji. Upaliliaji wa awali lazima ufanyike ndani ya wiki mbili baada ya kupanda, hii inategemea na kiwango cha magugu. Upaliliaji wa awamu ya pili ni baada ya wiki tano hadi sita baada ya kupanda.

BIBI ANASE:
Sijui kuhusu wenzangu lakini mimi huwa nahakikisha napalilia magugu yote kwasababu huwa yananichefua.

BABA MUSA:
Au basi inaweza kuwa tu ni aina ya udongo… kama unahistoria ya chemichemi na uwingi wa madini kwenye maji!

MZEE MPALU:
(ANAINGILIA) Nilijua tu! Ardhi hii inalaana! Nilijua tu!

LUGANO:
(ANAINGILIA) Sasa naomba tuelewane! Bwana Shamte! Umeona? Hakuna mtu anayejua chanzo cha hili tatizo. Sisi sote tunabahatisha tu, lakini hakuna anaejua.Tumejaribu kufuata mbinu za kisasa na kupanda mbegu za kisasa mara kwa mara lakini bado tunapata mavuno mabaya. Tumetumia mbegu za kisasa kwa misimu saba sasa.

BABA JOHN:
(ISHARA YA MSHANGAO) Ahaa! Sasa hii ndiyo chanzo cha tatizo lenu. Msirudie kupanda mbegu za kisasa zaidi ya mara mbili au tatu. Ndiyo sababu mmekuwa mkipata mavuno mabaya.

LUGANO:
Hatukujua! tulijua inatakiwa kuwa hivyo.

BABA JOHN:
Nataka kuwaonyesha kitu hapa. Naweza kupata jembe, kamba na rula?

LUGANO:
Bibi Anase, tunaweza kupata hivyo vifaa?

BIBI ANASE:
Ndiyo! Mendelina! Hebu kimbia na Musa mkatuletee, jembe, kamba na rula. Fanya haraka!

MADELINA:
Sawa bibi! Musa, twende!

BIBI ANASE:
Kimbieni!

SFX:
MADELINA NA MUSA WANAENDA KUFUATA VIFAA

BABA MUSA:
Kabla sijasahau, kitu kingine unachotakiwa kufanya, unapaswa kujaribu kuotesha mbegu chache kwanza ili kuhakikisha kwamba asilimia 70 hadi 80 ya hizo mbegu zimeota. Kama hazikuota, itakubidi ubadilishe mbegu nyingine

SFX:
MADELINA NA MUSA WANARUDI WANAKIMBIA

MADELINA:
Hizi hapa bibi!

SFX:
MADELINA NA MUSA WANAKABIDHI VIFAA

ALI:
(KWA KEJELI) Wote tunajua kazi ya jembe ni nini- sasa na hiyo kamba na rula? Ni matumaini yangu hutufindishi somo la jiografia!

SFX:
WOTE WANACHEKA

LUGANO:
Tafadhali, naomba tuwe wastaarabu. Bwana Shamte anapoteza muda na nguvu zake kutufundisha mbinu zote hizi.

BABA MUSA:
Aha! Bila shaka, Mr. Lugano, yuko sahihi kabisa. Hili ni darasa la jiografia. Kitu cha kwanza lazima ujue kabla ya kupanda ni nafasi kati ya mistari na mitaro. Musa, hebu chukuwa rula na uanze kupima.

SFX:
MUSA ANAPIMA UMBALI KWA KUTUMIA RULA

BABA MUSA:
Umbali kati ya kila mstari ni sentimita 45. Na lazima kuwe na umbali wa sentimita tano kati ya mmea kwenye mstari. Na kama umbali kati ya kila mitaro ni sentimita sitini au zaidi, weka mistari miwili kwenye kila tuta. Kwa mbegu fupi, acha nafasi ya sentimita tano kati ya mimea. Lakini kwa mbegu ndefu na yenye majani mengi, acha nafasi ya sentimita kumi na tano.

ALI:
Sasa hihi inasaidia nini?

MUSA:
(ANAINGILIA) Inasaidia mimea kukua vizuri na pia kuzipa nafasi ya kuweza kuchepua vizuri.

MONICA:
Aha kumbe Bwana. Shamte?

BABA MUSA:
Sawa sawa! Musa, sasa unaweza kuanza kupanda mbegu.

MUSA:
Sawa baba.

SFX:
MUSA ANAANZA KUPANDA MBEGU

LUGANO:
Umemlea mtoto wako vizuri sana.

MAMA JOHN:
Ni kweli, na inapendeza sana.

BABA MUSA:
Asante sana.

MONICA:
Ndiyo, Sasa tunamatumaini ya kupata bahati hiyo msimu huu.

BABA MUSA:
Ninauhakika, hakikisha tu mnanafuata kanuni vizuri ambazo nimewaelekesha leo.

Mhusika mkuu:
Baba Musa

Sehemu ya tisa
Eneo: Nje. shambani kwa Bibi. Jioni.
Wahusika: Madelina, Musa, Bibi Anase, Lugano, Ali, Mama John, Monica na Mzee Mpalu.
Kwa umbali SFX: Sauti ya mziki

SFX:
TUNASIKIA SAUTI YA MZIKI HUKU WATU WAKICHEZA

MUSA:
(AKIKARIBIA MIC) Madelina kuna nini tena?

MADELINA:
Kuna sherehe ya mavuno leo hapa kijijini!

SFX:
MZIKI UNAENDELEA KUSIKIKA.

MUSA:
Lakini sitakaa muda mrefu inabidi niende nyumbani kamsaidia baba kazi za nyumbani.

MADELINA:
Kwani baba yako haji?

MUSA:
Hapana alisema anakazi za kufanya.

MADELINA:
Niliambiwa nikulete leo, (KWA FURAHA) Yaani Musa wanakijiji wote wanataka wakuone!

MONICA:
(KWA FURAHA) Eeeh! Musa amekuja!

SFX:
WATU WANAANZA KUMSHANGILIA MUSA KWA KELELE.

LUGANO:
(KWA SHAUKU) Musa! Karibu! Karibu sana unakunywa kinywaji gani?

MUSA:
Asante! Nitakunywa soda.

MZEE MPALU:
Aise! mpe rafiki yangu bia.

MAMA JOHN:
Aaah! Mzee Mpalu usifundishe mtoto wa watu kuwa mlevi! Musa! Baba yako yuko wapi?

MUSA:
Hakuweza kufika kwasababu alikuwa na kazi.

MONICA:
Ahaa jamani!

MAMA JOHN:
Utamfikishia salamu zetu maana bila yeye tusigeweza kupata mavuno mengi msimu huu.

SFX:
WANAKIJIJI WOTE WANAITIKIA

MUSA:
Sawa nitamwambia.

MBUWA:
(AKIONGEA KAMA MLEVI) Ndiyo! Mpe bia! Nabii! Nabii ambae nilikuwa namuongelea!

MONICA:
(KWA MSHANGAO) Mbona simuelewi Mbuwa.

ALI:
Hivi karibu atachizi.

MBUWA:
(AKIENDELEA) Ni yule ambae ametusaidia kupata mavuno mengi ya maharage ya soya! Karibu sana, nabii wangu! Karibu!

MUSA:
Shikamoo!

MBUWA:
(ANADAKIA) Hapana! Hapana! Hapana! Mimi ndiyo nilitakiwa nikusalimie, nabii wangu! Mhm! Nilijua utakuwa mfupi sana kutokana na stori za watu. Mwanafunzi mmoja mdogo ameelimisha kijiji kizima kuhusu uzalishaji wa maharage ya soya!

SFX:
MBUWA ANAANZA KUCHEKA

MUSA:
(KWA AIBU) Sio mimi niliyewafundisha, ni baba yangu.

MBUWA:
(AKIWA AMELEWA) Kweli? Unaweza kunifundisha vitu ambavyo baba yako amewafundisha wanakijiji, mimi sikuwepo.

MADELINA:
(ANADAKIA) Mbuwa, Umelewa!

MBUWA:
(KWA UKALI) Wewe! Wewe mtoto mdogo kuwa makini na unachosema! Nani kalewa?

MUSA:
Ni sawa tu Madelina, Naweza kumfundisha tena.

MBUWA:
(KWA FURAHA) Haswaa! Mtu wangu! Ndo maana unaakili sana (KWA MSISIMKO). Nifundishe kuhusu vipimo kwanza! Nimesikia ulileta mashine kubwa na kila kitu kwa ajili ya kufanya vipimo!

MUSA:
Tulitumia tu rula na kamba!

MBUWA:
(KWA MSHANGAO) Rula tu?! Poa endelea!

MUSA:
Kwanza unatakiwa kupima umbali kati ya kila mstari, mtaro na mimea.

MBUWA:
Sawa! Umesema umbali kati ya mistari, matuta na mimea.

MUSA:
Ni mitaro sio matuta.

MBUWA:
Unasema kweli?

MADELINA:
Mbuwa, Musa atashidwa kumaliza kukuelezea kama utakuwa unamkatisha kila muda.

MUSA:
Sawa, umbali kati ya kila mstari ni sentimita arobaini na tano. Na mwisho kuwe na umbali wa sentimita tano kati ya mmea na mstari ili kusaidia mmea kukuwa na kuota vizuri.

MBUWA:
(ANASHANGAA) Haya mahesabu ni magumu sana kwangu!

MADELINA:
Musa, tuondoke!

MBUWA:
(ANALUKIA) Subiri, subiri kidogo! Na hizi mbegu za kisasa?

MUSA:
Usitumie mbegu za kisasa zaidi ya mara mbili au tatu ili kuhakikisha unapata mazao bora na mengi zaidi.

MBUWA:
Sawa! asante sana kijana wangu, kunywa bia moja kwa kazi yako nzuri.

MUSA:
Samahani sana, lakini mimi situmii bia.

MBUWA:
(AKILAZIMISHA) Acha hizo bwana mdogo kunywa bia.

MADELINA:
(KWA HASIRA) Mbuwa, amekwambia hatumii bia. Kwanini hutaki kumuelewa?

BIBI ANASE:
(KWA SAUTI KUBWA) Wewe Mbuwa! Achana na hawa watoto. Mendelina, njoo na musa mchukue chakula.

MADELINA:
Sawa bibi, Musa, twende.

MUSA:
Shikamo bibi.

BIBI ANASE:
Marahaba baba! Asante sana mjukuu wangu, tangu utuoneshe mbinu za upandaji wa maharage ya soya mavuno yamekuwa mazuri sana!

MUSA:
Asante bibi.

BIBI ANASE:
Hivi baba yako anaendeleaje?

MUSA:
Anaendelea vizuri tu.

BIBI ANASE:
Je anakuja kwenye sherehe?

MUSA:
Anadharura hatoweza kufika lakini anawasalimia.

BIBI ANASE:
Sawa mjukuu wangu wangu, chakula chako hiki hapa.

MUSA:
Asante bibi.

BIBI ANASE:
Mende!

MADELINA:
Abee bibi.

BIBI ANASE:
Usisahau kuosha vuombo.

MADELINA:
Sawa bibi!

MUSA:
Bibi yako anakuita Mende?

MADELINA:
Hawezi kutamka Madelina, kwahiyo ananiita Mendelina.

MUSA:
(ANACHEKA) Kila mtu shuleni atajua jina lako la “Mende.”

MADELINA:
(ANACHEKA) Musa, umeanza masiara, nitakubutua!

MUSA:
Chukuwa kipande cha kuku, Mende.

MADELINA:
Musa, nitakuchapa

SFX:
MADELINA ANAANZA KUMPIMBIZA MUSA HUKU WAKIWA WANACHEKA

Mhusika mkuu:
Madelina.

Acknowledgements

Imechangiwa na: Kheri Mkali, mwandishi wa mswaada, Dar es Salaam, Tanzania

Farm Radio International inawashukuru Catholic Relief Services (CRS) kwa ufadhili wa kuandaa mswaada huu.

gac-logoMradi unaendeshwa kwa ufadhili wa serikali ya Kanada kupitia idara ya masual