Nakala juu ya kilimo cha maharage

Uzalishaji wa mazao

Backgrounder

Utangulizi

Maharage ni zao maarufu zaidi duniani kati ya mazao mengine ya jamii ya mikunde. Maharage yalifika Tanzania miaka mia tatu (300) iliyopita. Nchini Tanzania na sehemu kubwa ya Afrika Mashariki, maharage yanazalishwa kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na kwa ajili ya kuuza. Wakulima wa Afrika mashariki wanazalisha zaidi ya nusu ya maharage yanayozalishwa barani Afrika. Nchini Tanzania, mara nyingi maharage yanapandwa pamoja na mahindi au na zao la kudumu kama ndizi au kahawa.

Kati ya robo moja hadi theluthi moja za kaya wanauza maharage, na yanauzika kirahisi Tanzania na nchi za jirani. Wenye mapato madogo mjini na asilimia themanini (80%) ya Watanzania waishio vijijini wanaotegemea kilimo, wanakula haya maharage yenye protini na vitamini kila siku.

Baada ya kuvuna, mizizi ya maharage hubakia kwenye udongo na ahuongeza kilo 20 – 60 zaidi za nitrojeni katiaka udongo kwa hekta moja, ambayo itatumika kwa zao litakalofuata. Hii ni sawa na mifuko ¾-2 zaidi ya urea, na inaweza kuongeza ustawi wa mazao yatakayofuata. Kwa kutumia mbinu sahihi za kilimo bora cha maharage mavuno ya maharage yanaweza kuwa zaidi ya kilo 800 kwa ekari.

Nakala hii inazungumzia namna ya kuzalisha maharage Tanzania, pia unaweza kuoanisha maelezo haya na nchi zingine zilizopo kusini mwa jangwa la Sahara ambako maharage haya hulimwa.

Je, kuna mambo ya kuzingatia?

  • Maharage haya yanauzika kirahisi nchini Tanzania na nchi zingine za Afrika Mashariki.
  • Maharage ni chanzo kikuu cha protini na vitamini kwa bei nafuu.
  • Kupanda mazao jamii ya mikunde kama maharage yanaweza kuongeza hadi mifuko miwili ya kirutubisho cha nitrojeni kwa hekta kwenye shamba lako.

Ni changamoto kubwa zipi zinazozuia uzalishaji wa maharage Tanzania?

  • Wadudu kama, inzi weupe na funza wa kwenye maharage.
  • Magonjwa, yakiwemo magonjwa yanayosababishwa na fangasi, evirusi na bakajani.
  • Kutokuwa na uhakika wa hali ya hewa, ukame pamoja na kuchelewa au kuwahi kwa mvua na kuisha haraka.
  • Upungufu wa rutuba kwenye udongo.
  • Uhaba wa mbegu bora.
  • Nafasi duni ya kupata taarifa juu ya masoko ya maharage.

Maswala ya jinsia katika uzalishaji wa maharage ya kawaida

  • Zao la maharage linahusishwa/linafanywa zaidi na wanawake. Lakini nguvu kazi katika uzalishaji wa maharage unatofautiana sehemu mbalimbali. Kwa mfano, mashariki mwa Kenya, kazi ya wanawake ni kupanda mbegu, kuvuna, kupiga, kusafrisha, na kuhifadhi. Wanaume wahahusika zaidi na kunyunyizia dawa na kudhibiti wadudu. Nchini Kenya kwenye bonde la ufa na pande za SNNPR kule Ethiopia, wanaume wanafanya kazi zote zinazohusu uzalishaji wa maharage ya kawaida.

Athari tarajiwa za mabadiliko ya hali ya hewa kwenye maharage ya kawaida

  • Utafiti wa hivi karibuni unaonyesha kuwa, mazao ya maharage ya kawaida yanaweza kushuka kwa asilimia 30-50 katikati ya karne na zaidi katika eneo la Sahel.
  • Watafiti wanafanya kazi ya kubuni aina ya maharage ya kawaida yanayoweza kuhimili ongezeko la joto Afrika Mashariki.

Taarifa muhimu juu ya kuzalisha maharage

1. Ardhi inayofaa na maandalizi ya shamba

Maharage ya kawaida yanahitaji udongo wenye rutuba ya wastani au yenye rutuba nyingi. Na hayawezi kustawi kwenye udongo wa asidi au alkali/ tindikali ya chini au juu. Pale ambapo udongo una asidi wakulima wanaweza kupunguza asidi kwa kuongeza chokaa na mbolea za samadi.

Palilia ukiondoa magugu makubwa. Fukia magugu madogo ili kuongeza viumbe hai kwenye udongo. Vunja udongo ulioshikana hasa kwenye mstari wa kupanda. Mistari ya mwinuko au matuta yanafaa zaidi kwaajili ya kupanda maharage haya. Shamba lililo andaliwa vizuri maharage huota mapema na huweza kupunguza matatizo ya magugu kuwa mengi, wadudu, na magonjwa shamabani.

Kama shamba linakabiliwa na maji kujaa au kutuama, zingatia kulima shamaba kwa kutengeneza matuta katika/ili kupanda maharage haya.

Kwa maelezo zaidi: Angalia nakala namba 2, 4 (kwa Kiswahili na Kingereza) na 5 (kwa Kiswahili), kwenye orodha ya dibaji hapo chini.

2. Kuchagua aina mbalimbali

Kuna aina mbili za maharage: Yanayotambaa na yasiyotambaa. Hapa tunaongelea juu ya aina ya maharage yasiyotambaa.

Maharage yanayokomaa kwa muda mfupi:

  • Yanafaa kwenye maeneo yenye mvua chache.
  • Yanafaa kwa wakulima ambao watachelewa kupanda, kwa mfano, mvua haikunyesha, au mazao ya awali yaliathiriwa na wadudu au magonjwa.

Maharage yanayo komaa baada ya muda mrefu:

  • Mara nyingi yana mavuno mengi, lakini hayafai kwenye maeneo yenye ukame.
  • Yanaongeza madini ya nitrojeni na yanachangia rutuba kwenye udongo zaidi ya maharage ya muda mfupi.

Nchini Tanzania, yafuatayo hapo chini ni aina ya maharage ambayo yanastahimili magonjwa sugu ya maharage kama chule, bakapembe, kutu ya majani, kuvu nyeupe, uozo wa mizizi, bakajani na batobato maharage:

  • Jesca
  • Lyamungu 85
  • Selian 97
  • Lyamungu 90
  • Selian 94
  • Uyole Njano

Wakulima wanatakiwa kuchagua aina ya maharage ambayo tayari yana masoko na, yanakidhi matarajio ya familia kiladha na kimapishi. Kuchagua aina ya maharage, utahitaji utafiti wa mkulima au vikundi vya wakulima kwenye soko.

Kwa taarifa zaidi, angalia nakala namba 2 (kwa Kiingereza na kwa Kinyarwanda) nakala namba 4 (kwa Kingereza na Kiswahili) nakala namba 5 (kwa Kiswahili).

3. Ubora wa mbegu

Panda mbegu bora tu. Hakikisha mbegu hizo hazijaathiriwa na wadudu, magongwa, na hazina mbegu za magugu. Usitumie mbegu zilizoharibika au makunyanzi. Usitunze mbegu zitokanazo na mimea iliyoathiriwa na magonjwa, kwa sababu mbegu hizo zitakuwa zimeambukizwa magonjwa.

Mbegu zilizonunuliwa zinaweza kutunzwa musimu hadi musimu, lakini kwa mazao mengi na bora, nunua mbegu mpya baada ya kila misimu mitatu.

Ili kuhakikisha kwamba mbegu zinafaa, fanya majaribio ya kuotesha siku 10 kabla ya kupanda.

Kwa taarifa zaidi, angalia nakala namba 4 (kwa Kiingereza na Kiswahili).

4. Ubora wa udongo

Inashauriwa kupima udongo kabla ya kuweka mbolea. Vipimo vya udongo vinapatikana baadhi ya maeneo nchini Tanzania, na vinatoa majibu pamoja na ushauri. Baadhi ya wakulima wadogowadogo – lakini sio wote watakaoweza kumudu bei ya vipimo.

Maharage yana uwezo wa kujitengenezea kirutubisho cha naitrojeni – lakini sio virutubisho vingine. Kwa hiyo ni vizuri kutumia mbolea iliyo na kirutubisho cha phosphorus wakati wa kuapanda, kama vile TSP, SSP, DAP, NPK, au Minjingu mazao. Lakini kwasababu baadhi ya udongo wa Tanzania una phosphorus na hauhitaji mbolea ya phosphorus, kupima udongo ni muhimu.

Samadi pia husaidia kuongeza mavuno. Weka tani 2 – 4 kwa ekari moja wakati wa kupanda na ongezea na kati ya DAP, NPK au Minjingu mazao. Tumia mfuko moja wa kilo 50 za DAP kwa kila ekari, au mfuko mmoja wa kilo 50 za NPK (10:30:10) kwa ekari.

Kwenye udongo usio na rutuba, ni muhimu kuongeza kirutubisho cha nitrojeni kwa ajili ya kukuza maharage. Wakulima wanaweza kutumia mbolea za kupandia kama DAP, Minjingu mazao, au Yara Legume. Hauhitaji vitu vingine vyakuongezea. Tahadhari kwamba, naitrojeni inaongeza ukuaji wa majani, na ukizidisha, itasababisha kuwa na mimea mikubwa lakini mavuno machache.

Mbolea (iwe ya viwandani au ya samadi) pia husaidia kuzuia magonjwa kuenea na kufanya mimea kurudi katika hali yake nzuri.

Kwa maelezo zaidi, angalia nakala namba 2, na 4 (kwa Kingereza) na 5 (kwa Kiswahili).

5. Kupanda kwa kuacha nafasi

Kupanda mazao kwenye mistari iliyopendekezwa inachukua muda mwingi mwanzoni, lakini itadhibiti baadhi ya magonjwa kama kuvu nyeupe itakanayo na msongamano wa mimea shamabani inaokoa muda baadae wakati wa kupalilia na kuvuna na inasaidia kupata mavuno mengi kwa ekari.

Ukipanda maharage yasiyotambaa, kama zao pekee, unashauriwa kuacha nafasi zifuatazo:

  • Panda mistari umbali wa sentimita 50 kati ya mstari na mtari.
  • Ndani ya mistari: Panda mbegu mbili kila sentimita 20. Au panda mbegu moja kila sentimita 10 ili kupunguza ushindani.

Kilimo mseto:

  • Ukipanda na nafaka nyingine, na kuzuia maharage kuathiriwa na kivuli, panda mistari miwili ya nafaka halafu mstari mmoja wa maharage.

Kilimo mseto, maharage na mahindi:

  • Panda mahindi kwa sentimita 75 kati ya mistari. Panga mstari mmoja wa maharage katikati ya mistari wa mahindi.
  • Katika kuboresha nafasi, (inayojulikana kama mfumo wa namba 2) panda mahindi katika sentimita 25 kati ya mistari na acha mita 1 kati ya mistari ya mahindi na mistari miwili ya mahindi acha umbali wa sentimita 50. (Mifumo hii ya kuacha nafasi inaleta idadi sawa na namba ya mahindi kwa hekta, kwahiyo mavuno huwa ni sawa.

Kama hauna tepumesha/futi kamba au kipimio, funga vifuniko vya chupa ya soda kwenye kamba kwa umbali unaohitajika au weka alama na makapeni au kwa kufunga vijitambaa katika kila baada ya sentimeta 20.

Kwa maelezo zaidi, angalia nakala namba 2, na 4 (kwa kingereza na kiswahili) na 5 (kwa Kiswahili).

6. Palizi
Kuondoa magugu kunapunguza ushindani kati ya mazao na magugu kwa ajili ya virutumisho, maji, jua, na nafasi. Magugu pia ni vivutio kwa baadhi ya wadudu. Unaweza kudhibiti magugug kwa kutumia mikono au kwa kutumia dawa za viwandani, au unaweza kutumia mbinu zote mbili.

Njia asili za kuthibiti magugu:

  • Panda maharage kwenye udongo ambao hauna magugu, uliolimwa na kusawazishwa vizuri (kubaki bila mabonge mabonge).
  • Palilia magugu wiki mbili baada ya kupanda.
  • Palilia mara ya pili wiki 5-6 baada ya kupanda.

Kuthibiti magugu kwa kutumia dawa za viwandani:
Madawa ya kuua magugu yanapatikana na kwa bei nafuu. Lakini kuna changamoto: 1) wakulima hawana uzoefu na madawa na huenda wasitumie vipimo kama inavyotakiwa au kufuata taratibu zake; 2) wakulima wanaweza wasichukue tahadhari za usalama kama vile kuvaa mavazi yaliyopendekezwa.

Kama unataka kutumia dawa za viwandani, pata ushauri kutoka kwa wataalam.

Kwa maelezo zaidi, angalia nakala namba 2, na 4 (kwa Kiingereza na Kiswahili).

7. Kudhibiti wadudu na magonjwa

Kagua shamba lako mara kwa mara kuwachunguza wadudu ambao wanaweza kuathiri maharage yako shamabani. Wadudu wanao athiri sana maharage nchini Tanzania ni kama vile, funza, buu/ funza inzi maharage, funza wa miche ya maharage, inzi mweupe, vidukuri, mbawa kavu wa majani, mbawakavu wa maua na, funza wa vitumba vya maharage na wadudud wanaofyonza mifuko ya maharage.

Kubadilisha maharage na mazao mengine yasiyo jamii ya mikunde kunasaidia kuzuia ongezeko la wadudu wapatikanao kwenye maharage.

Kilimo mseto kinaachia mwanya ambao wadudu hawawezi kustawi.

Kulima baada ya mavuno huanika mayai ya wadudu wa maharage juani na kuwaua, huku iki punguza wadudu kuendelea msimo ujao.

Kuchanganya maharage na mahindi kunasaidia kupunguza mdudu aina ya bruchid, ambae anapatikana wakati wa kuhifadhi mazao shambani.

Ili kuthibiti magonjwa ya maharage:

  • Tumia mbegu safi.
  • Pishanisha mazao,
  • Palilia vizuri, na
  • Kulima baada ya mavuno.

Usitumie mbegu kutoka kwenye mimea ambazo zina magonjwa kwa sababu zitakuwa zimeathirika. Kwa magonjwa yatokanayo na virusi, ng’oa mimea na zika mbali na shamba.

mosaic-disease
Ukoma au batobato kwenye mmea wa maharage

Kwa maelezo zaidi, angalia nakala namba 1, 2, 3 (kwa Kiswajili), 4 (kwa Kiingereza na Kiswahili), na 5 (kwa Kiswahili).

8. Kuvuna

Vuna wakati majani na mbegu ni kavu na zinarangi kati ya njano na kahawia. Ucheleweshaji wa kuvuna unasababisha kupoteza mazao. Vuna asubuhi ili kupunguza kusambaratika kwa mbegu.

Kwa maelezo zaidi, angalia nakala namba 3, 4 (kwa Kingereza na Kiswahili), na 5 (kwa Kiswahili).

9. Taratibu ya kukabiliana na matatizo ya unyevu unyevu na udongo usio na fosiforasi ya kutosha

Katika sehemu kubwa ya ardhi zinazozalisha maharage Africa, kuna mapungufu ya madini ya fosiforusi kwa matumizi ya mimea. Pia kuna upungufu wa unyevu nyevu kwenye ardhi. Vitu hivi viwili vinaweza kupunguza mavuno ya maharage.

Ili kupambana na matatizo haya, taratibu zifuatazo zinashauriwa:

  • Tumia mbolea ya samadi ili kuongeza viumbe hai kwenye udongo, mbolea hizi zinatunza unyevunyevu na kusaidia kutengeneza phosphorus kwenye udongo.
  • Tandaza mabaki ya mimea shambani na majani mengine ili kuhifadhi unyevu unyevu kwenye udongo.
  • Fanya kilimo mzunguko na punguza kulima kwenye mistari ya mazao ili kuhifadhi unyevu unyevu wakati wa msimu, kiangazi na ukame.

Kwa maelezo mengine, angalia nakala namba 7.

Ni wapi naweza kupata taarifa zaidi kuhusu mada hii?

  1. Africa Soil Health Consortium (ASHC), 2015. Crop pests and diseases. CABI, Nairobi. http://africasoilhealth.cabi.org/materials/legumes-crop-pests-and-diseases/ (479 KB, kwa Kingereza)
  2. Africa Soil Health Consortium (ASHC), undated. Better beans through good agricultural practices: for farmers in Rwanda. http://africasoilhealth.cabi.org/wpcms/wp-content/uploads/2014/10/361-N2Africa-Rwanda-common-beans-booklet.pdf (1,901 KB, kwa Kiingereza tu)
  3. Africa Soil Health Consortium (ASHC), undated. Mbinu endelevu za kuthibiti magonjwa na wadudu wa maharage (Common bean pests and diseases). http://africasoilhealth.cabi.org/wpcms/wp-content/uploads/2016/11/534-Bean-pests-and-diseases-leaflet.pdf (2,054 KB, kwa Kiswahili)
  4. Africa Soil Health Consortium (ASHC), undated. Radio transcripts on various aspects of bean production. Available for download at https://africasoilhealth.cabi.org/materials/ (Kwa Kiingereza na Kiswahili)
  5. Africa Soil Health Consortium (ASHC), undated. Tupande Maharage Bingwa (Common bean manual). http://africasoilhealth.cabi.org/wpcms/wp-content/uploads/2016/11/521-Common-bean-manual-Kiswahili-.pdf (12,849 KB, kwa Kiswahili)
  6. Ramirez-Villegas, J, Thornton, P.K., 2015. Climate change impacts on African crop production. CCAFS Working Paper no. 119. CGIAR Research Program on Climate Change, Agriculture and Food Security (CCAFS). Copenhagen, Denmark. https://cgspace.cgiar.org/bitstream/handle/10568/66560/WP119_FINAL.pdf (3,011 KB, kwa Kingereza tu)
  7. Namugwanya Margaret, Tenywa, J.S., Otabbong, E., Mubiru, D.N., Basamba, T.S., 2014. Development of Common Bean (Phaseolus Vulgaris L.) Production Under Low Soil Phosphorus and Drought in Sub-Saharan Africa: A Review. Journal of Sustainable Development; Vol. 7, No. 5; 2014. Downloadable at www.ccsenet.org/journal/index.php/jsd/article/download/38006/22352 (219 KB, kwa KiIngereza tu)

Maana ya maneno muhimu:

  • Mazao jamii ya kunde: Ni mmea jamii ya mikunde Fabaceae au Leguminosae, tunda au mbegu ya mmea huo wajamii ya mikunde hupandwa mbegu zake, ambayo inatuma na mbegu hiyo hutumika kwa chakula pulse, majani/masalia hutumika kwaajili ya mifugo, na samadi. Kwa mfano, mazao jamii ya mikunde yanayolika ni kama: njegere, maharage, karanga, maharage ya soya, dengu, mbaazi, kunde.
  • Wingi wa asidi na alkali kwenye udongo: Kipimo cha asidi na alkali kwenye udongo. Udongo wenye kipimo chini ya tindikali pH 7 una asidi nyingi na udongo wenye kipimo zaidi ya tindikali 7 una alkali nyingi. Mimea mingi inastawi kwenye tindikali pH kati ya 5.5 hadi 7.0.
  • Ubora wa udongo: Hii ni hali halisi ya udongo hasa wakati wa kupanda. Mambo yanayochangia ubora wa udongo ni pamoja na muundo na uimara wa chembechembe za udongo, kiwango cha unyevuunyevu, kiwango cha hewa, upenyaji wa maji na mkondo.

Acknowledgements

Imechangiwa na: Vijay Cuddeford, Mhariri mkuu, Farm Radio International, kwa kunukuu nakala ya CABI, Technology and messaging brief for the Legume Alliance campaign: Notes for Northern Tanzania common bean growing, unpublished document.

Kazi hii imewezeshwa kwa masaada wa Shirika la utafiti, lililopo Ottawa, Canada (International Development Research Centre, Ottawa, Canada) www.idrc.ca, na msaada wa kifedha kutoka serikali ya Canada, kupitia idara ya msuala ya kimataifa Kanada, ( Global Affairs Canada) www.international.gc.ca

canadaidrc