Wanawake wanajiwezesha: Mchezo kuhusu wanawake kulima na kuuuza maharage — Part 2

Usawa wa kijinsiaUzalishaji wa mazao

Ujumbe kwa mtangazaji

Save and edit the full 5-part drama as a Word document. (300 KB)

Nukuu kwa Waandishi wa Habari
Wakina dada wanafanya wenyewe haya ni maigizo yenye sehemu-tano inayoongelea kikundi cha wanawake wanaokabiliana na chagamoto za kujikwamua na kupata maendeleo. Wanawake hawa ni wanachama wa vikundi vya kuweka na kukopa au vicoba nchini Tanzania, na wote wanalima maharage. Wanawake wanafanya kazi nyingi zaidi katika shughuli za uzalishaji wa maharage. Lakini kwasababu ya utamaduni wao wa kimajukumu katika jamii, wanaume wanafanya maamuzi yote baada ya mavuno, ikiwemo kuuza maharage na kumiliki kipato.

Baathi ya wahusika katika maigizo, ni mama Farida na Mama Mjuni, ambao wameonekana kuongoza katika kujaribu kufanya tofauti. Wanawahimiza wanawake kufanya kazi pamoja katika mashamba yao, na mwishowe kuzalisha maharage pamoja na kutafuta masoko kama kikundi.

Soma wahusika wakuu

Maigizo yanapinga hali mbaya, ikiwemo ugomvi baina ya mwanamke na mwanaume: unyanyasaji wa nyumbani katika familia moja, na juhudi za jamii kuwatumia wanawake vibaya na kujipatia faida kutokana na shughuli za kijangili.

Kuna utani kidogo katika maigizo, ingawa inaongelea mandhari nzito. Ukitengeneza maigizo na kikundi, hakikisha kuwa sehemu zenye mada nzito zinaoanishwa na sehemu zenye mada nyepesi za kufurahisha, za marafiki wakinongoneza matukio mazuri na wakicheka.

Kila kipengele kina urefu wa kama dakika 20-25, ikiwemo muziki wa kianzia na kumalizia. Kwasababu vipengele ni virefu, unaweza kupanga kurusha vipengele (kipande kimoja wapo katika Igizo) viwili au vitatu tu katika kipindi chako. Kwa mara nyingi vipande viwili au vitatu vinachukua dakiak 6-8.

Unaweza kupata mrejesho wa maigizo kwa kuandaa kipondi kitakacho pokea simu ambazo wasikilizaji watajadili baathi ya mambo waliyoyasikia katika maigizo, waalike wataalamu wa kike na wakiume kujadili mada. Majadiliano yanaweza kujumuisha:

  • jinsi jamii inavyogawanya kazi za kuzalisha na kuuza maharage, au mazao mengine yanayolimwa katika eneo, na jinsi gani mgawanyo huu umetenga mahitaji ya wanawake, na hata inaweza kuathiri familia;
  • unyanyasaji majumbani na utamaduni au tabia za ukimya inayoruhusu hii kuendelea; na
  • aina ya msaada wanaume wanayoweza kuwapatia wanawake ambao wanahangaika kujisaidia wao na famila zao.

Script

1.
Scene 1
2. Sehemu:
Ndani. Kituo cha polisi – Ofisi ya Afande Kaifa. Asubuhi.
3. Utambulisho wa kipengele:
Afande Kaifa anakoroma.

4. Wahusika:
Afande Kaifa, Mzee Kaifa, Afande Filipo.

5. SFX:
AFANDE KAIFA ANAKOROMA USINGIZINI.
6. SFX:
MLANGO UNAGONGWA.
7. AFANDE KAIFA:
(ANASHTUKA KWA HASIRA) Nini tena?
8. AFANDE FILIPO:
(ANAFUNGUA MLANGO NA KUINGIA) Samahani mkuu lakini mzee wako amefika sasa hivi na anataka kukuona.
9. AFANDE KAIFA:
(GHAFLA ANAKURUPUKA) Mwambie aingie sasa! Unasubiria nini?
10. SFX:
MLANGO UNAFUNGULIWA NA MZEE KAIFA ANAINGIA.
11. SFX:
AFANDE KAIFA ANAINUKA NA KUENDA KUMSALIMIA MZEE KAIFA.
12. AFANDE KAIFA:
Shikamoo mzee.
13. MZEE KAIFA:
(ANAKARIBIA MIC) Siamini kama imefikia wakati inabidi nisubiri kwenye foleni kama watu wengine ili tu kumuona mwanangu!
14. AFANDE KAIFA:
(KWA UTULIVU) Sio hivyo mzee, sikujua kama ni wewe. Huwa nawaambia wasinisumbue nikiwa nimepumzika. Unaendeleaje?
15. SFX:
MZEE KAIFA ANAVUTA KITI NA KUKAA CHINI.
16. MZEE KAIFA:
Naendelea vizuri. Naona unalala wakati wa kazi.
17. AFANDE KAIFA:
(ANATOA KICHEKO KWA MBALI) Nimetingwa na kazi kiasi cha kwamba nashindwa kupumzika kabisa.
18. MZEE KAIFA:
(KWA UKALI) Wewe usiongee na mimi kama unavyoongea na raia wengine. Umesahau kwamba nilikuwa mkuu wa polisi kabla yako?
19. SFX:
UKIMYA.
20. MZEE KAIFA:
Mkeo na watoto wanaendeleaje?
21. AFANDE KAIFA:
Wanaendelea vizuri tu. Mama anaendeleaje?
22. MZEE KAIFA:
Ungekuwa unataka kujua mama yako anaendeleaje ungekuja kumuona badala ya kuniuliza maswali.
23. SFX:
UKIMYA.
24. MZEE KAIFA:
Mama yako hali yake sio nzuri sana. Miguu bado inamsumbua, kusema kweli hali imezidi kuwa mbaya.
25. AFANDE KAIFA:
Itakuwa kwa sababu ya uzito wake.
26. MZEE KAIFA:
Ndio na kuona bado kunamsumbua.
27. AFANDE KAIFA:
(KWA WASI WASI) Itabidi nije kumuona siku moja, najua atafurahi sana.
28. MZEE KAIFA:
Unataka kujua kitu kitakachomfurahisha mama yako? Siku utakayomzawadia mjukuu wa kiume!
29. AFANDE KAIFA:
(KWA SAUTI YA CHINI) Tunajitahidi mzee.
30. MZEE KAIFA:
Itabidi uongeze bidii kabla mama yako hajawa kipofu kabisa. Alafu kutakuwa na faida gani kama atashindwa kumuona mjukuu wake?
31. AFANDE KAIFA:
Mzee unashindwa kuelewa, sio rahisi kama unavyofikiria.
32. MZEE KAIFA:
Una maana gani nashindwa kuelewa? Kwani mimi sikukuzaa?
33. AFANDE KAIFA:
Sio hivyo mzee.
34. MZEE KAIFA:
Hilo ndio tatizo lako na mama yako ndiye aliyekuharibu. Ndio maana hata mkeo anakutawala na kila leo mnazaa wasichana tu.
35. AFANDE KAIFA:
Sio hivyo mzee.
36. MZEE KAIFA:
Sasa je? Unajua saa nyingine wanawake ni kama mbuzi na inabidi utumie nguvu ili wakuelewe.
37. AFANDE KAIFA:
Sawa nimekuelewa.
38. MZEE KAIFA:
Hapana huelewi, mambo yamebadilika siku hizi. Zamani ilikuwa tusipowapiga wake zetu, mashemeji zetu wanashangaa kwanini hawapati malalamiko.
39. AFANDE KAIFA:
Nakuahidi mjukuu hivi karibuni mzee.
40. MZEE KAIFA:
Ahadi! Ahadi! Ahadi! Basi! Ndio kazi yako. Sikiliza mwanangu unahitaji mrithi wako muda utakapofika kama wewe uliyokuwa mrithi wangu.
41. AFANDE KAIFA:
Sawa.
42. MZEE KAIFA:
Sawa, acha mimi niende sasa.
43. AFANDE KAIFA:
Acha nikutoe nje.
44. MZEE KAIFA:
Hapana usijali… Nitamfikishia mama yako salamu zako lakini hakikisha unakuja kumuona ukipata muda.
45. AFANDE KAIFA:
Nitakuja.
46. SFX:
MZEE KAIFA ANAFUNGUA MLANGO NA KUTOKA NJE.
47. CONTROL:
Mzee Kaifa

 

48.
Scene 2
49. Sehemu:
Nje. Shambani kwa Farida. Asubuhi.
50. Utambulisho wa kipengele:
Farida anajaza maharage kwenye magunia.

51.Wahusika:
Farida, Jenny.

52. SFX:
FARIDA ANAJAZA MAHARAGE KWENYE GUNIA.
53. JENNY:
(ANAKARIBIA MIC) Naona mambo sio mabaya. Utakuwa umevuna sana mwaka huu!
54. FARIDA:
(ANACHEKA) Kwanini unasema hivyo?
55. JENNY:
Sio naona unajaza maharage kwenye gunia mpaka yanataka kumwagika.
56. FARIDA:
(ANACHEKA) Natamani ingekuwa kweli mpendwa. Hapa yenyewe sina njia nyingine bali kujaza maharage ili kupata wateja kwa sababu nimevuna magunia machache sana mwaka huu.
57. JENNY:
Hauko peke yako, kila mtu analalamika mwaka huu. Umekuwa mwaka m’baya kwa kila mtu.
58. FARIDA:
Ehee kwanza niambie kumetokea nini leo? Gereji yako imewaka moto au?
59. JENNY:
(ANACHEKA) Unataka kusemaje?
60. FARIDA:
Si nakushangaa upo hapa badala ya kweye gereji yako.
61. JENNY:
Kwa hiyo unataka kusema huwa sikutembelei kabisa?
62. FARIDA:
Kunitembelea huwa unanitembelea lakini sio asubuhi hivi kama leo.
63. SFX:
FARIDA NA JENNY WANACHEKA.
64. JENNY:
Yaani Farida badala ya kunikaribisha Chai asubuhi yote hii, wewe ndio kwanza unanikejeli.
65. FARIDA:
(ANACHEKA) Kwa kweli leo sijabeba chai lakini kuna chupa ya uji hapo pembeni kama unataka.
66. SFX:
JENNY ANAFUNGUA CHUPA YA UJI NA KUMIMINA UJI KWENYE KIKOMBE.
67. JENNY:
Unaendeleaje lakini tangu tulivyoonana mara ya mwisho?
68. FARIDA:
Naendelea vizuri tu.
69. JENNY:
Unajua sikuwa na amani tangu tulivyoonana mara ya mwisho.
70. FARIDA:
Kwa sababu gani?
71. JENNY:
Ebu acha maigizo, unajua kabisa ninamaanisha nini.
72. SFX:
KUNAKUWA NA UKIMYA WA MUDA MFUPI WAKATI FARIDA AKIENDELEA NA KAZI.
73. JENNY:
Farida, najua Kaifa ameanza kukupiga tena.
74. FARIDA:
Sikilliza, kila kitu kipo sawa. Nimeongea na Kaifa na tumesuluhisha tofauti zetu.
75. JENNY:
Kweli eh?
76. FARIDA:
Ndio.
77. JENNY:
Kila kitu kinaonekana sawa sasa hivi kwa sababu unaweza kufanya kazi na kubeba magunia lakini nilivyokutembelea siku ile ulikuwa unashindwa hata kubeba kagunia kadogo ka mbolea.
78. FARIDA:
Sikiliza, mimi na Kaifa tulikuwa tuligombana kwa sababu nilimshauri aniache nitafute masoko kwa ajili maharage kwa sababu yeye anaonekana ametingwa sana na kazi.
79. JENNY:
Sasa je? Kuna shida gani?
80. FARIDA:
Aliona kama sijamheshimu kaka mwanaume. Alikasirika sana.
81. JENNY:
(KWA HASIRA) Nini? Ukisikia upuuzi ndio huo! Mbona simuoni kukusaidia kipindi cha kulima shambani kama yeye ni mwanaume kweli. Mbona hayupo hapa sasa hivi?
82. FARIDA:
Sikiliza Jenny nishakwambia yameisha, sitaki matatizo sasa hivi.
83. JENNY:
Farida, huwezi kuendelea kuishi hivi.
84. FARIDA:
Jenny si nimekwambia yameisha lakini. Haitatokea tena.
85. JENNY:
Kweli eeh? Mara ngapi umesema hivyo lakini mambo haya haya yanajirudia. Una uhakika gani haitatokea tena?
86. SFX:
UKIMYA
87. FARIDA:
Sikiliza saa nyingine Kaifa anapitiwa lakini haimaanishi kwamba ana nia mbaya. Anataka maisha bora kwetu sote.
88. JENNY:
Lakini haimaanishi ndio awe anakupiga. Sio sawa.
89. FARIDA:
Bwana wee! Mimi najua huwezi kuelewa, inavyoonekana Vumi amesharidhika kutokuwa na watoto.
90. SFX:
UKIMYA.
91. FARIDA:
(KWA UPOLE) Jenny naomba unisamehe! Sikumaanisha.
92. JENNY:
Kwa sababu mimi na Vumi hatugombani, haimaanishi kwamba kila kitu kiko sawa kati yetu.
93. SFX:
UKIMYA.
94. JENNY:
Unatakiwa kuelewa kwamba kisa Kaifa anakupiga haimaanishi kwamba ndio anakupenda au anakujali sana. Kwanza Kaifa anatakiwa kushukuru sana kwa kila kitu ulichompa pamoja na hao watoto uliomzalia. Sio kila mtu ana bahati kama mliyonayo.
95. SFX:
FARIDA ANAANZA KULIA.
96. JENNY:
(ANAM’BEMBLEZA) Farida acha kulia..ebu njoo.
97. SFX:
FARIDA ANAENDELEA KULIA.
98. FARIDA:
Saa nyingine najihisi mpweke sana. Kama vile niko shimoni na siwezi kutoka. Sijui nini cha kufanya.
99. JENNY:
Sikiliza Farida, inatakiwa ujikaze kwa ajili yako na wanao ndio kitu muhimu sasa hivi.
100. CONTROL:
Farida.

 

101.
Scene 3
102. Sehemu:
Nje. Kiwandani. Asubuhi.
103. Utambulisho wa kipengele:
Lori la Sigi linawasili.

104. Wahusika:
Sigi, Mr Patel, Stella.

105. SFX:
LORI LA SIGI LINAINGIA KIWANDANI.
106. SFX:
INJINI YA LORI INAZIMWA.
107. SIGI:
(ANASHUKA KUTOKA KWENYE LORI KWA SHAUKU) Haya vijana! Anzeni kushusha magunia! Twende kazi! Twende kazi!
108. STELLA:
(ANAKARIBIA MIC) Samahani, mimi naitwa Stella.
109. SIGI:
(KWA MBWEMBWE) Mambo! Mbona sijawahi kukuona hapa kiwandani? Sikujua kiwanda kina wasichana warembo kama wewe!
110. STELLA:
(KWA AIBU) Asante….Nipo hapa kwa ajili ya kusimamia malipo na…
111. SIGI:
(ANAMKATISHA) Umesema unaitwa nanivile?
112. STELLA:
Stella.
113. SIGI:
Oh! Ndio Stella. Niambie umeolewa?
114. STELLA:
Sioni umuhimu wa hilo swali hapa sasa hivi.
115. MR PATEL:
(ANAKARIBIA MIC) Ahaa! Naona mmeshakutana.
116. SIGI:
Ndio Mr. Patel! Unaendeleaje?
117. MR PATEL:
Naendelea vizuri sasaumewasili. Umechelewa tena.
118. SIGI:
Ndio mzee tulipata tatizo kidogo.
119. MR PATEL:
Sikiliza Sigi nategemea kupata faida ya pesa ninayokulipa. Na hiyo inamaanisha maharage yenye ubora wa juu kwa muda unaofaa.
120. SIGI:
Naelewa mzee, ndio maana nilitaka nihakikishe Napata maharage ya kiwango bora kabisa. Unajua msimu huu mavuno yamekuwa ya shida.
121. MR PATEL:
Unajua tumeingia mkataba na nategemea utauheshimu. Mimi nina kiwanda cha kuendesha.
122. SIGI:
Nakuahidi haitatokea tena mzee.
123. MR PATEL:
Sawa, nategemea hutoniangusha, Naona umeshakutana na Stella hapa.
124. SIGI:
Ndio.
125. MR PATEL:
Kuanzia sasa yeye ndio atasimamia malipo yote. Kwa hiyo ina maana ukiwa unakuja itabidi uwe unamuona yeye.
126. SIGI:
Kwani wewe unasafiri?
127. MR PATEL:
Hapana nitakuwepo.
128. SIGI:
Kwa hiyo huu utaratibu ni kwa muda au?
129. MR PATEL:
Hapana kuanzia sasa ndio itakuwa hivyo. Ukileta maharage hutaripoti kwangu tena lakini utaripoti kwa Stella.
130. SIGI:
Samahani Mr Patel, tunaweza kuongea pembeni kidogo?
131. MR PATEL:
Haina shida unaweza kuongea mbele ya Stella kwa sababu yeye ndio atakuwa anasimamia malipo.
132. SIGI:
Ni kwamba tu sijazoea utaratibu huu mzee.
133. MR PATEL:
Unamaanisha kuripoti kwa mwanamke?
134. SIGI:
Ndio, maisha yangu yote sijawahi kuripoti kwa mwanamke.
135. MR PATEL:
(ANACHEKA KIDOGO) Subiri nikwambie kitu. Siku chache zilizopita nilikutana na mwanamke aliyekuwa mekanika aliyenisaidia kutengeneza gari yangu. Lakini nilichogundua ni kwamba hakuwa mekanika tu lakini yeye ndiye aliyekuwa mmiliki wa gereji na ameajiri wanaume wanaomfanyia kazi.
136. SIGI:
Ndio lakini hii sio gereji.
137. MR PATEL:
Lakini ni biashara. Nilijifunza kitu kikubwa sana siku ile, kwamba wanawake nao wana uwezo wa kufanya kazi kama wanazofanya wanaume kama wakipata fursa. Na ndio sababu nimemuajiri Stella kwa sababu naamini anaiweza kazi.
138. SIGI:
Sielewi kwanini unataka kubadilisha mfumo mzuri tuliokuwa tumeuzoea ili mradi tu kumuajiri mwanamke.
139. MR PATEL:
Ndio nimeshafanya uamuzi bwana Sigi na kuanzia sasa utaripoti kwa Stella. Natumaini mtafanya kazi vizuri tu, siku njema.
140. SFX:
MR PATEL ANAONDOKA.
141. STELLA:
(ANAJIWEKA SAWA) Mimi naona tunaweza tukaendelea kwa sababu tushajua jinsi mambo yalivyo!
142. SFX:
UKIMYA.
143. STELLA:
Bwana Sigi nitahitaji ushirikiano wako wa hali na mali na hiyo ina maana kuripoti kwangu mara kwa mara. Haijalishi una mawazo gani juu yangu lakini ili tufanikiwe nitahitaji ushirikiano wako. Sawa, kwa hiyo tuanze kwa kunionehs huo mziogo wa maharage ulioleta leo.
144. SIGI:
(KWA SAUTI YA CHINI) Nifuate.
145. SFX:
SIGI NA STELLA WANAONDOKA.
146. CONTROL:
Mr Patel

 

147.
Scene 4
148. Sehemu:
Nje. Gereji ya Jenny. Asubuhi.
149. Utambulisho wa kipengele:
Mazingira ya gereji.

150. Wahusika:
Jenny, Stella, mekanika 1, mekanika 2.

151. SFX:
KELELE ZA GEREJI.
152. JENNY:
Ongeza mafuta kwenye injini. Itasaidia kuondoa misuguano na kuifanya injini idumu.
153. SFX:
MAFUTA YANAMIMINWA KWENYE INJINI.
154. MEKANIKA1:
Inatosha?
155. JENNY:
Ongeza kidogo.
156. MEKANIKA2:
Samahani dada Jenny lakini kuna gari imeiingia sasa hivi.
157. JENNY:
Sasa unasubiri nini? Nenda ukamsikilize mteja.
158. MEKANIKA2:
Nimemsikiliza lakini anakuulizia wewe.
159. JENNY:
Amekwambia jina lake?
160. MEKANIKA2:
Hapana.
161. JENNY:
Sawa, acha nikamsikilize. Msaidie Juma kutengeneza hiyo corolla ya blue ina tatizo la injini.
162. MEKANIKA2:
Sawa.
163. SFX:
JENNY ANAENDA KUMUONA MTEJA.
164. STELLA:
(MBALI NA MIC, KWA UTANI) Naona unaringa sana siku hizi tangu uwe bosi. Yaani unashindwa hata kuja kumsalimia rafiki yako wa siku nyingi.
165. JENNY:
(KWA MSHANGAO) Ebu subiri kwanza! Ni macho yangu au?
166. STELLA:
(ANACHEKA) Hapana sio macho yako.
167. JENNY:
Stella?! Ni wewe?
168. STELLA:
Ndio na nimejaa tele.
169. JENNY:
Mungu wangu! Hata siamini!
170. SFX:
JENNY NA STELLA WANAKUMBATIANA KWA FURAHA.
171. JENNY:
Yaani! Ni miaka! Unafanya nini kijijini?
172. STELLA:
Nimepata kazi huku.
173. JENNY:
Hivi ni miaka mingapi imepita?
174. STELLA:
Sina uhakika…kama miaka kumi hivi.
175. JENNY:
Kabisa! Naona mambo sio mabaya kabisa Hiyo gari sio mchezo shoga angu.
176. STELLA:
(ANACHEKA) Asante! Lakini mimi nimeajiriwa tu, wewe ndio mmiliki wa gereji. Mambo yako yatakuwa mazuri zaidi yangu.
177. SFX:
JENNY NA STELLA WANACHEKA.
178. JENNY:
Unajua sikuwahi kufikiri kama nitakuona tena. Bado siamini macho yangu kama umerudi.
179. STELLA:
Nimechoka maisha ya mjini ndio maana nimerudi. Nimepata kazi kiwandani kama supervisor.
180. JENNY:
Hongera sana kipenzi! Hayo ndio maneno sasa. Kwa hiyo ina maana utakuwepo?
181. STELLA:
Ndio. Niambie…maisha yanasemaje?
182. JENNY:
Sio mbaya… nimeolewa.
183. STELLA:
(KWA SHAUKU) Achaa! Kwa nani?
184. JENNY:
Amini usiamini lakini nimeoelewa na Vumi.
185. STELLA:
(ANACHEKA) Usiniambie! Nilijua tu! Alafu ulikuwa uanjifanya humpendi. Kwa hiyo mna watoto wangapi?
186. JENNY:
(KWA SAUTI YA CHINI) Kwa kweli Mwenyezi Mungu bado hajatubariki.
187. STELLA:
(BILA KUTEGEMEA) Oh!
188. JENNY:
Vipi wewe? Umeolewa?
189. STELLA:
Hapana mpendwa. Sijui nyie hapa kijijini lakini mjini hakuna wanaume, au labda wanaume wazuri wote wameshaoa.
190. JENNY:
Ebu acha utani! Unataka kuniambia miaka yote hiyo na umeshindwa kupata mchumba?
191. STELLA:
Jenny, sio rahisi kama unavyofikiria. Saa nyingine nahisi kama maisha ya ndoa sitayaweza, bora tu nikazane na kazi yangu.
192. JENNY:
(ANATOA KICHEKO) Kweli hubadiliki. Wewe muda wote unawaza kazi tu.
193. STELLA:
Ehee! Na vipi kuhusu Farida? Yupo?
194. JENNY:
Huwezi amini Stella, Farida ameolewa na ana watoto watatu wa kike.
195. STELLA:
Achaa! Jamani hongera zake. Itabidi nimtembelee siku.
196. JENNY:
Itabidi ufanye hivyo. Najua atafurahi sana kukuona.
197. STELLA:
Nimefurahi sana kukuona. Niliwamiss wote sana.
198. JENNY:
Hata sisi tulikumiss mpendwa. Hivi lakini ulijuaje utanipata hapa?
199. STELLA:
Leo asubuhi nilimsikia bosi wangu akimuambia mtu kwamba alikutana na mwanamke mekanika aliyetengeneza gari yake. Nikajua kuna mwanamke mmoja tu hapa kijijini aliyekuwa anapenda magari tangu mdogo.
200. SFX:
JENNY NA STELLA WANACHEKA.
201. JENNY:
Kwa hiyo ulimsikia bosi wako akinitaja ndio ukanikumbuka.
202. STELLA:
Sio hivyo Jenny jamani, unajua nimerudi kijijini juzi juzi tu hapa na nilikuwa bado siajtulia kabisa. Kwa hiyo ilibidi niweke mambo sawa kabla ya kuja kukuona.
203. JENNY:
Nimefurahi umekuja shoga angu. Nasubiri kwa hamu kumuambia Farida kuhusu hii siku ya leo.
204. STELLA:
Hata mimi nasubiria kwa hamu hiyo siku tutakaa pamoja. Najua tuna mengi ya kuongea.
205. JENNY:
Ndio, itabidi tupange siku moja.
206. STELLA:
Hilo nalo neno. Jenny mpendwa nimependa sana ulivyoitengeneza gereji, najua mzee wako angekuwepo angefurahi sana.
207. JENNY:
Asante sana kipenzi.
208. CONTROL:
Jenny

 

209.
Scene 5
210. Sehemu:
Ndani. Bar ya mama K. Mchana.
211. Utambulisho wa kipengele:
Ambience Mama K’s bar.

212. Wahusika:
Mama K, Grace, Sigi, Mlevi, Mwajuma.

213. SFX:
KELELE ZA MZIKI NA MAONGEZI YA WATU.
214. MLEVI:
(KWA SAUTI YA KILEVI) Mama K hii konyagi au gongo?
215. MAMA K:
Kwa nini?
216. MLEVI:
(ANACHEUA) Najiona kama nimelewa zaidi ya kawaida leo!
217. MAMA K:
Lamwai umeshaanza mambo yako! Tena naomba uniache kwa sababu leo sijisikii kabisa yaani! Kwani hio chupa inaonekana kama chupa ya gongo?
218. MLEVI:
Sijui! Wewe ndio inabidi uniambie kama umeniwekea gongo. Mbona ina ladha kama ya gongo?
219. MAMA K:
Naomba usinichezee kabisa! Kwanza hujanilipa hela ninayokudai ya wiki mbili zilizopita!
220. MLEVI:
Kwani wewe sijui tabia yako ya kunichanganyishia gongo kwenye konyagvi ili nilewe! Tena inabidi uache mara moja!
221. MAMA K:
Wewe endelea kubwabwaja tu alafu uone!
222. MLEVI:
(ANACHEUA) Itakuwa nimelewa kwa sababu leo Mwajuma anaonekana mrembo hatari!
223. MWAJUMA:
(KWA HASIRA) Lamwai! Nakuonya uniache. Nitainuka hapa nikutandike sasa hivi.
224. MAMA K:
(ANAINGILIA KATI) Hakuna kupigana kwenye bar yangu!
225. SIGI:
(ANAKARIBIA MIC) Tajiri wa kijiji ndio naingia! Tajiri wa kijiji ndio naingia!
226. SFX:
WATU WANAANZA KUSHANGILIA.
227. MAMA K:
(ANAMKARIBISHA) Karibu Sigi! Karibu sana! (ANAMGEUKIA MLEVI) Wewe ebu inuka ili Sigi akae!
228. MLEVI:
Kwa nini unapenda kunisumbua mama K lakini wakati unaona kabisa bado nina kinywaji kwenye glasi yangu eeh?
229. MAMA K:
Aaagh! Ebu inuka bwana! (ANAMUINUA MLEVI KWENY KITI) Kwanza unakunywa kwa mkopo alafu bado unapiga kelele. (ANAMGEUKIA SIGI) Hiki hapa kiti Sigi.
230. SIGI:
Kwanza kabla sijakaa nina tangazo! (KWA MBWE MBWE NYINGI) Mimi kama Sigi, tajiri wa kijiji! Mutu mukubwa! Natangaza kufunga baa rasmi! Hakuna mtu yoyote anaeruhusiwa kununua kinywaji chochote na kila mtu atakunywa kwa bili yangu.
231. MLEVI:
Eeeh! Kama ndio hivyo basi kaa tu baba!
232. SFX:
WATU WANASHANGILIA HUKU WAKIMUIMBA SIGI.
233. SIGI:
Mama K ebu mpe kila mtu kinywaji anachotaka! Vinywaji juu yangu leo!
234. SFX:
WATU NDANI YA BAR WANAMZINGIRA MAMA KA NA KUANZA KUMSUMBUA.
235. MAMA K:
(KWA HASIRA) Aaagh! Ebu subirini kwanza na nyie wapenda vya bure! (ANAMGEUKIA SIGI) Sigi utakunywa nini?
236. SIGI:
Kama kawaida- niletee bia ya baridi! Alafu yule mwanao mrembo yuko wapi?
237. MAMA K:
(KWA SHAUKU)Nani -Grace? Atakuwa ndani, subiri nikuitie alafu nitakuletea na bia yako.
238. SFX:
MAMA K ANAINGIA NDANI KWA HARAKA.
239. MLEVI:
(ANAMGEUKIA SIGI) Hicho kiti vipi mkuu? Kiko vizuri au?
240. SIGI:
Kiko vizuri kabisa.
241. SFX:
MLEVI ANAKUNYWA POMBE KUTOIKA KWENYE CHUPA YAKE.
242. MLEVI:
Nataka uelewe kwamba kuanzia leo hicho kiti ni chako kila utakapokuja hapa.
243. SFX:
MAMA K ANARUDI AKIMSEMA GRACE.
244. MAMA K:
Wewe kazi yako kukaa ndani tu! Kuna mtu anataka kukuona hapa. (ANAMGEUKIA SIGI) Huyu hapa Sigi, na bia yako hiyo! Karibu!
245. SIGI:
Asante! Grace karibu kiti.
246. GRACE:
Asante lakini hapana.
247. MAMA K:
Unaona! Hilo ndio tatizo lako, ndioo maana mpaka leo bado hujaolewa.
248. GRACE:
Lakini nina kazi za kufanya ndani alafu mimi sinywi pombe.
249. SIGI:
Sio lazima unywe pombe, unaweza kunywa soda kama unataka.
250. MAMA K:
Ebu kaa na wewe! Hujui hata anataka kuzungumza nini na wewe.
251. SFX:
GRACE ANAVUTA KITI NA KUKAA.
252. SIGI:
Ehee! Namna hiyo bwana. Hakuna ubaya kukaa chini na kuongea.
253. MAMA K:
Sawa basi acha niwaache.
254. SFX:
MAMA K ANAONDOKA.
255. SIGI:
Kwanza kabisa naomba unisamehe kwa jinsi nilivyokuwa siku ile ulivyonitembelea na Doris. Sikufanya vizuri, naomba unisamehe.
256. GRACE:
Ndio maana umeniita hapa? Ili uniombe msamaha?
257. SIGI:
Ndio. Nimegundua sikuwatendea haki siku ile.
258. GRACE:
Sawa.
259. SIGI:
Kwa hiyo ina maana umenisamehe?
260. GRACE:
Ndio.
261. SIGI:
Una cha kusema?
262. GRACE:
Sasa unataka niseme nini jamani?
263. SIGI:
Sikiliza niko tayari kufanya biashara na wewe. Nitakupa tenda.
264. GRACE:
Sio lazima kwa kweli.
265. SIGI:
Hapana nataka…Lakini sidhani hii ni sehemu nzuri ya kuongelea biashara.
266. GRACE:
Kwani ina tatizo gani?
267. SIGI:
Unajua…sio sehemu nzuri kwa maongezi ya muhimu. Kuna makelele na vurugu sana. Kama vipi twende ofisini kwangu.
268. GRACE:
Sijui bwana…sidhani kama hilo ni wazo zuri.
269. SIGI:
Kwa nini? Nakuahidi tutaongea biashara tu. Ndio maana tunaenda huko.
270. GRACE:
Sijisikii vizuri kuenda huko baada ya kilichotokea mara ya mwisho nilivyokuwa huko.
271. SIGI:
Sikiliza najua nilikukosea lakini sio kawaida yangu. Nakuahidi sipo hivyo.
272. GRACE:
(KWA KUSITA) Sawa…
273. CONTROL:
Sigi

 

274.
Scene 6
275. Sehemu:
Ndani. Nyumbani kwa Farida. Mchana.
276. Utambulisho wa kipengele:
Mziki wa taarab unasikika kwenye redio.

277. Wahusika:
Farida, Afande Kaifa, Zuhura.

278. SFX:
TAARAB INASIKIKA KWENYE RADIO.
279. SFX:
AFANDE KAIFA ANAFUNGUA MLANGO NA KUINGIA.
280. AFANDE KAIFA:
(KWA SAUTI) Farida! Farida!
281. FARIDA:
(ANAKARIBIA MIC) Abee! Nakuja!
282. SFX:
AFANDE KAIFA ANAZIMA REDIO.
283. FARIDA:
Umeita muda mrefu sana? Sikukuzikia, nilikuwa chumbani napanga nguo.
284. AFANDE KAIFA:
Utanisikia vipi na kelele zote hizi za mziki?
285. ZUHURA:
(ANAKIMBIA KARIBU NA MIC) Baba amerudi! Baba amerudi! Baba amerudi! Shikamoo!
286. AFANDE KAIFA:
Marahaba!
287. ZUHURA:
Baba nikuoneshe matokeo ya mtihani wangu wa hesabu?
288. AFANDE KAIFA:
Baadae sawa?
289. ZUHURA:
Lakini jimefaulu.
290. FARIDA:
Farida, baba yako amechoka sasa hivi. Mwache apumzike alafu baadae utamuonesha mtihani wako sawa?
291. ZUHURA:
Sawa.
292. FARIDA:
Vipi unajisikiaje?
293. AFANDE KAIFA:
Nataka nipumzike tu nikirudi nyumbani bila ya makelele ya mziki na watu kunisumbua.
294. FARIDA:
Sawa, nikuletee chakula?
295. AFANDE KAIFA:
Ndio.
296. SFX:
FARIDA ANAMUANDALIA AFANDE KAIFA CHAKULA.
297. FARIDA:
Unajua kuna kitu nilitaka tuongee.
298. AFANDE KAIFA:
Si nimekwambia nataka kupumzika?
299. FARIDA:
Lakini si tunaongea tu jamani?
300. AFANDE KAIFA:
Sikiliza Farida hapa nilipo nimechoka sana sawa?
301. FARIDA:
Lakini unajua mara nyingi hatupati muda wa kuongea kwa sababu huwa unarudi usiku sana au saa nyingine unakuwa umetingwa.
302. SFX:
UKIMYA.
303. FARIDA:
Nilikuwa nafikiria kutafuta wateja wapya kwa ajili ya kununua maharage yetu. Nahisi watanunua kwa bei nzuri, mama Mjuni kuna wateja amewapata.
304. AFANDE KAIFA:
Kwa hiyo hauamini uamuzi wangu?
305. FARIDA:
Una maana gani jamani? Mimi nilidhani itakuwa vizuri kujadili kwa pamoja kuhusu kuuza maharage yetu.
306. AFANDE KAIFA:
(ANAGUNA) Nadhani unasahau sehemu yako kama mwanamke wa nyumba hii.
307. FARIDA:
Mimi sioni tatizo lolote kwa mume na mke kukaa chini na kujadili maisha yao. Mbona Mama Mjuni na mzee Ali huwa wanajadili hayo mambo.
308. AFANDE KAIFA:
Nini kitafuata baada ya hapo? Utaniloga kama Mama Mjuni alivyomloga mzee Ali au?
309. FARIDA:
Heee! Una maana gani?
310. AFANDE KAIFA:
Kwani nani asiyejua kwamba mama Mjuni amemloga mzee Kaifa, ndio maana anapika na kumfulia mkewe nguo. Wewe unafikiri kwa nini mzee Ali huwa anafanya chochote mke wake anamuambia? Weweunafikiri mwanaume mzima na akili zake atpika na kufua nguo?
311. FARIDA:
Mimi sina hata cha kusema! Kwa kweli sijui tumefika vipi huko wakati nilikua najaribu kukupa ushauri tu.
312. AFANDE KAIFA:
(KWA HASIRA) Sikukuoa ili uwe unanipa ushauri; Nimekuoa ili unizalie watoto. Unataka kunisaidia? Nizalie mtoto wa kiume!
313. SFX:
AFANDE KAIFA ANATOKA NJE NA KUBAMIZA MLANGO KWA HASIRA.
314. ZUHURA:
Mama kwanini baba amekasirika?
315. FARIDA:
Usijali mwanangu.
316. ZUHURA:
Amekasirika kwa sababu sisi ni wasichana?
317. FARIDA:
Hapana mwanangu, anataka watoto wa kiume ili muwe mnacheza wote sawa.
318. CONTROL:
Farida

 

319.
Scene 7
320. Sehemu:
Nje/Ndani. Gala la Sigi. Mchana.
321. Utambulisho wa kipengele:
Gari ya Sigi inawasili.

322. Wahusika:
Sigi, Grace.

323. SFX:
GARI YA SIGI.
324. SFX:
SIGI ANAZIMA INJINI.
325. SIGI:
Haya tumefika.
326. SFX:
SIGI ANASHUKA KUTOKA KWENYE GARI NA KUMFUNGULIA MLANGO GRACE.
327. GRACE:
(KWA UOGA) Mimi naona bora tuongee kwenye gari, haina haja ya kuenda ofisini kwako.
328. SIGI:
(ANACHEKA KIDOGO) Sasa maana yake itakuwa nini? Yaani tumekuja kote huku ili kubaki nje?
329. SFX:
UKIMYA.
330. SIGI:
(KWA MSISITIZO) Twende tu bwana. Alafu kule ofisini kumetulia hakuna kelele kama huku nje. Hakuna usmbufu.
331. GRACE:
(KWA KUSITA) Sawa.
332. SFX:
SIGI NA GRACE WANASHUKA KUTOKA KWENYE GARI NA KUELEKEA OFISINI.
333.
PUNGUZA SAUTI HATUA KWA HATUA
334.
ONGEZA SAUTI HATUA KWA HATUA
335. SFX:
SIGI ANAFUNGUA MLANGO.
336. SIGI:
Karibu sana ofisini kwangu. Vuta kiti ukae tu.
337. SFX:
SIGI ANAVUTA KITI NA KUKAA.
338. SFX:
GRACE NAE ANAKAA.
339. GRACE:
Asante.
340. SIGI:
Unatumia kinywaji gani? (KWA UTANI) Nikupe bia au? (ANACHEKA)
341. GRACE:
Hapana asante. (ANABADILISHA MAZUNGUMZO) Nilikuwa nakwambia mwaka huu ulikuwa m’baya sana upande wa mavuno lakini nimefanikiwa kupata magunia kadhaa ya maharage.
342. SIGI:
Aaah! Haraka ya nini? Kwanini tukimbilie kuongea biashara?
343. GRACE:
Lakini si ndio sababu tuko hapa au?
344. SIGI:
Tuna muda mwingi sana, hakuna haraka. Alafu unajua nimekununulia zawadi.
345. GRACE:
(KWA MSHANGAO) Zawadi?!
346. SIGI:
Ndio, nilitaka iwe kama ishara ya kuomba msamaha kwako kwa makosa yangu tulivyokutana mara ya mwisho.
347. GRACE:
(ANACHEKA KWA UOGA) Hapana kulikuwa hakuna haja kwa kweli.
348. SIGI:
(KWA SHAUKU) Usijali, siburi nikupe.
349. SFX:
SIGI ANAFUNGUA DROO NA KUTOA ZAWADI.
350. SIGI:
Hii hapa.
351. SFX:
SIGI ANAMPA GRACE ZAWADI.
352. GRACE:
(ANAJIFANYA KUFURAHIA) Aah! Ni gauni!
353. SIGI:
Ndio na la bei mbaya kweli kweli. Sio mtumba huo.
354. SFX:
GRACE ANAGUNA.
355. SIGI:
Vipi tena?
356. GRACE:
Zawadi ni nzuri sana lakini sidhani kama nitaweza kuipokea, si unaelewa lakini?
357. SIGI:
Aaah Grace ebu acha utoto bwana- hii ni zawadi, sio kitu kibaya.
358. GRACE:
Najua lakini sitajisikia huru kama tutaendelea kufanya biashara nikijua fika nimepokea zawadi kwako. Alafu pia haitakuwa vizuri Doris akijua.
359. SFX:
SIGI ANACHEKA.
360. GRACE:
Unacheka nini?
361. SIGI:
Kwa hiyo unataka kusema mimi na Doris ni wapenzi?
362. GRACE:
Ndio, na yeye inaonekana nakupenda sana kwa sababu huwa anakuongelea sana.
363. SIGI:
Hapana, usijali hawezi kukasirika. Ebu lijaribu hilo gauni basi.
364. GRACE:
(KWA MSHANGAO) Unamaanisha kweli?
365. SIGI:
Ndio. Sikiliza, sikujua vipimo vyako kwa hiyo ilibidi nikisie tu. Jaribu basi tuone.
366. GRACE:
(ANACHEKA KWA UOGA) Siwezi kuvaa hili gauni hapa mbele yako.
367. SIGI:
Aaah! Acha kuwa mshamba bwana. Si unajaribu tu gauni.
368. GRACE:
Nitalijaribu nikifika nyumbani.
369. SIGI:
Acha mambo yako bwana. Mimi nataka nikuone ndani ya hilo gauni.
370. GRACE:
(KWA UKALI) Nilidhani tumekuja hapa kuongea biashara.
371. SFX:
SIGI ANASIMAMA KUTOKA KWENYE KITI CHAKE NA KUMFUATA GRACE.
372. SIGI:
(AKIONEKANA KUNOGEWA) Kwa nini unataka kuondoka na ndio kwanza umefika?
373. GRACE:
(KWA UKALI) Usiponiachia, nitapiga kelele kiasi kwamba kijiji kizima kitasikia.
374. SIGI:
Usiwe hivyo. Nakuahidi nitanunua maharage yako kwa bei ya juu kuliko watu wote hapa kijijini.
375. GRACE:
(WASIWASI UNAONGEZEKA) Tafadhali nakuomba uachie mkono wangu.
376. SFX:
GRACE ANAPIGA KELELE KWA MAUMIVU.
377. GRACE:
(ANAPIGA KELELE) Unaniumiza mkono!
378. SIGI:
(KWA SAUTI YA KUBEMBELEZA) Usiwe hivyo bwana. Usijali.
379. GRACE:
(AKITETEMEKA) Hapana, nataka kuondoka.
380. SIGI:
(AKIONEKANA KUNOGEWA) Unataka kuondoka mapema yote hii na ndio kwanza tumefika?
381. GRACE:
(KWA UKALI) Sikiliza, usiponiachia nitapiga kelele kiasi cha kwamba kijiji kizima kitanisikia.
382. SIGI:
(ANABADILIKA GHAFLA) Sawa nenda Malaya mkubwa! Kwanza huna shukrani! Nimekununulia zawadi nzuri na haya ndio malipo yake?
383. GRACE:
(KWA HASIRA) Ndio, sijali! Kwa sababu mimi sio msichana wa aina hiyo!
384. SFX:
GRACE ANAMRUSHIA GAUNI SIGI NA KUTOKA NJE KWA HASIRA.
385. CONTROL:
Grace

 

386.
Scene 8
387. Sehemu:
Nje. Nyumbani kwa mama K. Jioni.
388. Utambulisho wa kipengele:
Grace analia.

389. Wahusika:
Grace, Farida.

390. SFX:
GRACE ANALIA.
391. SFX:
MZIKI UNASIKIKA KWA MBALI KWENYE BAR YA MAMA K.
392. SFX:
GRACE ANAENDELEA KULIA.
393. FARIDA:
(ANAKARIBIA MIC) Grace! Vipi?
394. SFX:
GRACE ANAENDELEA KULIA.
395. FARIDA:
Grace imekuwaje tena?
396. GRACE:
(ANAJARIBU KUACHA KULIA) Hapana.
397. FARIDA:
Kwa nini unalia?
398. SFX:
GRACE ANABAKI KIMYA.
399. FARIDA:
Nini kimekusibu mpendwa?
400. GRACE:
Hakuna shida.
401. FARIDA:
Lakini naona kabisa kuna kitu kinakusumbua. Nini shida? Ni mama k?
402. GRACE:
Hapana.
403. FARIDA:
Sasa tatizo nini?
404. GRACE:
Sijisikii kuongea.
405. FARIDA:
Grace, unajua kabisa mimi na wewe tunajuana kkabla ya hata vikoba…mimi ni kama dada yako. Kwa hiyo kama kuna tatizo unaweza kunieleza kwa sababu naweza kukusaidia.
406. GRACE:
Sikiliza, huwezi kufanya chochote kama ambavyo mimi siwezi kufanya chocote, sawa? Kwa hiyo hata nikikwambia haitasaidia kitu.
407. FARIDA:
Unaongelea nini?
408. GRACE:
(BAADA YA MUDA) Sigi!
409. FARIDA:
Amefanyaje tena?
410. GRACE:
Alinialika ofisini kwake ili tuongee biashara. Nilikuwa nataka nimuuzie maharage lakini nilipofika huko akaanza kunilazimisha kufanya mapenzi.
411. FARIDA:
(ANAKOSA CHA KUSEMA) Oh!
412. GRACE:
Nilijua tu utakosa cha kusema.
413. FARIDA:
Umeenda polisi kuripoti?
414. GRACE:
Sidhani kama polisi watweza kunisaidia.
415. FARIDA:
Kwa nini?
416. GRACE:
Sigi ana pesa nyingi na ushawishi mkubwa hapa kijijini. Unafikiri polisi wataniamini mimi?
417. FARIDA:
Sidhani kama ni hivyo unavyofikiria. Kama amefanya kosa inabidi apewe adhabu ili asirudie tena kufanya kosa kwa mtu mwingine.
418. GRACE:
(ANACHEKA KIDOGO) Weweumenizidi kiumri lakini sikutegemea kama una mawazo ya kitoto kama hayo.
419. FARIDA:
(KWA UKALI) Nisikilize mimi; Mume wangu ni polisi na nitamwambia kila kitu. Lazima hatua ya kisheria ichukuliwe ili kuhakikisha tunamaliza mambo kama haya.
420. GRACE:
Asante kwa kunisikiliza na kwa uelewa wako.
421. CONTROL:
Grace

 

422.
Scene 9
423. Sehemu:
Nje. Bar ya mama K. Usiku.
424. Utambulisho wa kipengele:
Mazingira ya bar ya mama K.

425. Wahusika:
Grace, Mama K, Doris, Adam, Alex, Mlevi, Monica.

426. SFX:
GRACE ANAOSHA VYOMBO.
427. ADAM:
Umepika?
428. GRACE:
Hapana.
429. ALEX:
Kwa nini?
430. GRACE:
Sijisikii vizuri.
431. ADAM:
Kwa hiyo hujapika kwa sababu hujisikii vizuri?
432. GRACE:
Mmeshakuwa watu wazima- kwanini msijipikie hata mara moja?
433. ADAM:
Lakini wewe ndio mwanamke; wewe ndio unatakiwa kupika.
434. ALEX:
Alafu tuko bize sana kupika.
435. GRACE:
(ANACHEKA) Mko bize? Mko bize mnafanya nini? Ukiacha kuzurura kijijini siku nzima.
436. ADAM:
Tutamwambia mama hujapikia.
437. GRACE:
Nendeni mkamwambie.
438. MAMA K:
(ANAINGILIA KATI) Haya makelele yote ya nini?
439. ADAM:
Si huyu Grace, hajapika chochote!
440. MAMA K:
Wewe Grace kwa nini usiwapikie wadogo zako?
441. SFX:
DORIS ANAWASILI.
442. DORIS:
(ANAKARIBIA MIC, AKIFOKA) Yuko wapi? Malaya mkubwa.
443. SFX:
DORIS ANATELEZA NA KUDONDOKA.
444. SFX:
GRACE ANAJARIBU KUMSAIDIA KUMUINUA DORIS.
445. GRACE:
Wee Doris- kuwa makini! Sidhani hivyo viatu vinafaa kutembea umbali mrefu.
446. DORIS:
(KWA HASIRA) Niache! Wewe inakuhusu nini?
447. GRACE:
Doris umelewa?
448. DORIS:
Haikuhusu!
449. GRACE:
Una nini leo?
450. DORIS:
Mimi nina nini? Hivi ulifikiri sitagundua?
451. GRACE:
Unaongea kuhusu nini?
452. DORIS:
Oh! Usijifanye kama hujui naongelea nini. Najua sana kuhusu mipango yako ya kumuiba Sigi wangu!
453. GRACE:
(ANACHEKA) Unatania au?
454. DORIS:
Unacheka? Unajua Sigi kaniambia kila kitu; ameniambia jinsi ulivyoenda ofisini kwake na kuanza kujipendekeza kwake.
455. GRACE:
(KWA MSHANGAO) Oh ndio kakuambia hivyo?
456. DORIS:
Ndio.
457. GRACE:
Je amekuambia pia jinsi alivyojaribu kunirubuni kwa zawadi na nikamkatalia lakini akajaribu kunilazimisha kulala nae?
458. DORIS:
Huo ni uongo. Huoni hata aibu?
459. GRACE:
Huniamini? Ebu angalia hizi alama kwenye mikono yangu (GRACE ANAMUONESHA DORIS ALAMA ZA MAKOVU) Unafikri nimezipata vipi? Amejaribu kunikama kwa kutumia nguvu.
460. DORIS:
(ANAPAZA SAUTI) Wewe ni muongo!
461. GRACE:
Doris umelewa!
462. DORIS:
(ANAPIGA KELELE) Nakuchukia!
463. SFX:
DORIS ANAJARIBU KUMRUKIA GRACE.
464. MAMA K:
(ANAINGILIA KATI) Hakuna kupigana katika sehemu yangu ya biashara!
465. ADAM:
(ANASHANGILIA) Ngumi! Ngumi! Ngumi!
466. ALEX:
Mama waache wapigane tuone!
467. MAMA K:
Hapana, nimesema hakuna kupigana hapa. Kwanza amelewa sehemu nyingine huko. Bora angekuwa amekunywa hapa, kidogo ningevumilia.
468. DORIS:
(ANAMGEUKIA GRACE) Najua ulikuwa unanionea wivu. Kila nilipokuonesha zawadi Sigi alizoninunulia ulinionena wivu. Ulitamani ungekuwa mimi.
469. GRACE:
Wala! Sitaki chochote kutoka kwa huyi bwana wako. Kwanza yeye ndiye aliyetaka kunipa mimi zawadi lakini nikamtolea nje.
470. DORIS:
Acha uongo! Najua Sigi wangu hawezi kufanya hivyo.
471. GRACE:
Nakuonea huruma sana rafiki yangu! Umepigwa upofu kiasi cha kushindwa kugundua Sigi ni mtu wa aina gani.
472. DORIS:
(ANAJARIBU KUMRUKIA GRACE) Nakuchukia sana!
473. MAMA K:
(ANAINGILIA KATI TENA) Nyie nimesemaje? Hakuna kupigana hapa. Kama mnataka kupigana naomba muondoke kwa sababu mnanisababishia vurugu hapa. Ebu ona wagtu wamehsaanza kujaa kwa sababu yenu.
474. DORIS:
Sawa, mimi naondoka lakini hayajaisha!
475. SFX:
MLEVI ANACHEKA.
476. DORIS:
Na wewe unacheka nini?
477. MLEVI:
Nakucheka wewe kwa sababu unagombana na rafiki yako kisa Sigi.
478. DORIS:
Wewe unajua nini? Wewe si mlevi tu!
479. MONICA:
Anakuambia ukweli ndugu yangu. Sigi sio mtu mzuri na ndio kawaidayake kutumia wanawake hapa kijijini kama bidhaa. Alinifanyia hivyo hivyo mimi na rafiki yangu; Alituchezea wote.
480. DORIS:
Nyie wote waongo.
481. SFX:
DORIS ANAONDOKA.
482. CONTROL:
Doris

 

483.
Scene 10
484. Sehemu:
Ndani. Nyumbani kwa Farida- chumbani. Usiku.
485. Wahusika:
Farida, Afade Kaifa
486. Utambulisho wa kipengele:
Afande Kaifa anakoroma.

487. SFX:
AFANDE KAIFA ANAKOROMA.
488. FARIDA:
(ANAJARIBU KUMUAMSHA) Baba Kaifa! Baba Kaifa!
489.
AFANDE KAIFA (ANAJIBU AKIWA USINGIZINI) Hmm!
490. FARIDA:
Nakuomba uamke; kuna kitu nataka tuongee.
491. AFANDE KAIFA:
(KWA SAUTI YA USINGIZI) Nini gtena saa hizi?
492. FARIDA:
Kuna kitu kimekuwa kikinisumbua leo siku zima!
493. AFANDE KAIFA:
Kwani hatuwezi kuongea kesho?
494. FARIDA:
Kesho tunaweza tusipate mudawa kuongea kwa hiyo bora nikuambie tu sasa hivi.
495. AFANDE KAIFA:
Ni nini?
496. FARIDA:
Unajua leo wakati naenda kununua mafuta ya taa Nilimkuta Grace analia peke yake. Nilivyomuuliza Nini kimemsibu, aliniambia kwamba Sigi alimkaribisha Ofisini kwake na kumlazimisha kufanya nae mapenzi.
497. AFANDE KAIFA:
Na wewe umemuamini?
498. FARIDA:
Ndio, kwanini adanganye sasa?
499. AFANDE KAIFA:
Umeniambia kwamba hii ilitokea ofisini kwake?
500. FARIDA:
Ndio.
501. AFANDE KAIFA:
Na huyo msichana alikuwa anafanya nini ofisini?
502. FARIDA:
Aliniambia alienda kuongea biashara. Na wakati akiwa Huko ndio Sigi akataka kumlazimisha kufanya nae Mapenzi.
503. SFX:
AFANDE KAIFA ANACHEKA.
504. FARIDA:
Unacheka nini?
505. AFANDE KAIFA:
Sikujua kama tuna mpelelezi nyumba hii. Ningejua mapema ningekupa kazi.
506. FARIDA:
Hili sio suala la mchezo. Ingekuwaje kama msichana wa watu angebakwa?
507. AFANDE KAIFA:
Lakini hakubakwa sio?
508. FARIDA:
Kama alibakwa je na labda anajaribu kuficha? Au kama ikimtokea mwanamke mwingine je? Itabidi uchukue hatua.
509. AFANDE KAIFA:
Nichukue hatua kwa ushahidi gani? Kutokana na Maelezo ya Grace? Kisa tu anasema kwamba Sigi Alikuwa akimlazimisha haimaanishi kwamba ni kweli Asilimia mia. Kama anadanganya je?
510. FARIDA:
Mimi namjua, hawezi kudanganya. Ni msichana Mtaratibu sana.
511. AFANDE KAIFA:
Je ana mashahidi wowote?
512. FARIDA:
Sijajua, sina uhakika. Sikumuuliza.
513. AFANDE KAIFA:
Kama hakum’baka basi ina maanisha hakuna kesi.
514. FARIDA:
Itakuwaje kama siku atamfanyia kweli mtu mwingine? Mimi naona bora umchukulie hatua kabla Hujachelewa sana.
515. AFANDE KAIFA:
Sikiliza, mimi narudi kulala. Nakushauri uachane Kujihusisha na mambo ya watu.
516. FARIDA:
Mimi nilikuwa nahisi tu siku zote kuwa Sigi sio Mtu mzuri. Sitaki tumuuzie maharage yetu tena.
517. AFANDE KAIFA:
Mimi ndio naamu nani tutamuuzia maharage yetu. Na pia huwezi kuacha kumuuzia mtu maharage kisa tu uvumi.
518. CONTROL:
Farida.

Acknowledgements

Imechangiwa na: Kheri Mkali, mwandishi wa muongozo, Dar es Salaam, Tanzania.
Imepitiwa na: Frederick Baijukya, mtaalamu wa kilimo na mratibu wa shirika la N2Africa Tanzania, Shirika la kilimo kwa nchi kitropiki (IITA), East Africa Hub, Dar es Salaam, Tanzania.

Kazi hii imewezeshwa kwa masaada wa Shirika la utafiti, lililopo Ottawa, Kanada (International Development Research Centre, Ottawa, Canada) www.idrc.ca, na msaada wa kifedha kutoka serikali ya Kanada, kupitia idara ya masuala ya kimataifa, (Global Affairs Canada) www.international.gc.ca.
gaclogoidrc