Ujumbe kwa mtangazaji
Nukuu kwa Waandishi wa Habari
Wakina dada wanafanya wenyewe haya ni maigizo yenye sehemu-tano inayoongelea kikundi cha wanawake wanaokabiliana na chagamoto za kujikwamua na kupata maendeleo. Wanawake hawa ni wanachama wa vikundi vya kuweka na kukopa au vicoba nchini Tanzania, na wote wanalima maharage. Wanawake wanafanya kazi nyingi zaidi katika shughuli za uzalishaji wa maharage. Lakini kwasababu ya utamaduni wao wa kimajukumu katika jamii, wanaume wanafanya maamuzi yote baada ya mavuno, ikiwemo kuuza maharage na kumiliki kipato.
Baathi ya wahusika katika maigizo, ni mama Farida na Mama Mjuni, ambao wameonekana kuongoza katika kujaribu kufanya tofauti. Wanawahimiza wanawake kufanya kazi pamoja katika mashamba yao, na mwishowe kuzalisha maharage pamoja na kutafuta masoko kama kikundi.
Maigizo yanapinga hali mbaya, ikiwemo ugomvi baina ya mwanamke na mwanaume: unyanyasaji wa nyumbani katika familia moja, na juhudi za jamii kuwatumia wanawake vibaya na kujipatia faida kutokana na shughuli za kijangili.
Kuna utani kidogo katika maigizo, ingawa inaongelea mandhari nzito. Ukitengeneza maigizo na kikundi, hakikisha kuwa sehemu zenye mada nzito zinaoanishwa na sehemu zenye mada nyepesi za kufurahisha, za marafiki wakinongoneza matukio mazuri na wakicheka.
Kila kipengele kina urefu wa kama dakika 20-25, ikiwemo muziki wa kianzia na kumalizia. Kwasababu vipengele ni virefu, unaweza kupanga kurusha vipengele (kipande kimoja wapo katika Igizo) viwili au vitatu tu katika kipindi chako. Kwa mara nyingi vipande viwili au vitatu vinachukua dakiak 6-8.
Unaweza kupata mrejesho wa maigizo kwa kuandaa kipondi kitakacho pokea simu ambazo wasikilizaji watajadili baathi ya mambo waliyoyasikia katika maigizo, waalike wataalamu wa kike na wakiume kujadili mada. Majadiliano yanaweza kujumuisha:
- jinsi jamii inavyogawanya kazi za kuzalisha na kuuza maharage, au mazao mengine yanayolimwa katika eneo, na jinsi gani mgawanyo huu umetenga mahitaji ya wanawake, na hata inaweza kuathiri familia;
- unyanyasaji majumbani na utamaduni au tabia za ukimya inayoruhusu hii kuendelea; na
- aina ya msaada wanaume wanayoweza kuwapatia wanawake ambao wanahangaika kujisaidia wao na famila zao.
Wahusika wakuu
Farida: Mwanamke amaliziaye rika la miaka 20.
Farida ni mama wa nyumbani anayafnay shughuli zote za jumbani, ikiwemo kupika na kufanya usafi wa wasichana wake watatu na mumewe. Farida pia anamajukumu ya shughuli ngumu za shamba katika shamba lao dogo la ekari -moja pasipo kupata msaada wowote kutoka kwa mume wake ambaye mwishoni mume wake ndiye anafanya maamuzi ya kuuza mazao yao.
Ameolewa na mkuu wa polisi wa kijiji, Afande Kaifa, ambaye amezaa naye binti wa tatu warembo Sifa (10), Zuhura (8), na Hafsa (3).
Farida alipata ujauzito wa mwane wa kwanza Sifa wakati bado anasoma shule ya sekondari na alilazimika kuacha shule na kuolewa na mume wake. Kila mara Farida anatamani kuwa angemaliza shule maisha yake yangekuwa tofauti.
Farida amekuwa akinyanyaswa na mumewe kwa miaka mingi, ila mume wake amekuwa akimpiga huku akijihami aije akamuweka majeraha ambayo yataonekana kwa jamii. Manyanayaso haya sana sana yametokana na kutojiamini kwa mume wake, mume wake amekuwa na kinyongo dhidi ya mke wake kwa kuwa hajamzalia mtoto wa kiume. Anategemea Farida awe mke mwenye unyenyekevu, lakini Farida anafikra zake za kipekee. Anapenda kusikiliza muziki wa taarabu akiwa hana kazi.
Farida ni mwanamke mwenye nguvu na ana mawazo mengi mazuri kwa familia yake, lakini vikwazo kutoka kwa mumewe mwenye kujisikia na majidai mara kwa mara vimekuwa vikimkwamisha.
Farida analima maharage, ambayo mume wake anayauza maharage haya kwatika masoko mbalimbali. Nafasi ya Farida- kufanya maamuzi ni ndogo kiasi ya kwamba hawezi kuamua hata nini cha kupika nyumbani.
Mbali na kulima maharage, pia analima mazao mengine kwaajili ya kulisha familia yake.
Farida na mume wake wanamilika mifugo michache, Farida anachanganya kinyesi cha ngombe na vitu vingine na kuuza mbolea, na pia wananunua kuku na kuuza mayai. Anaulewe wa pesa, biashara na uwekezaji.
Muda pekee ambao Farida anajihisi ni wa thamani, mwenye uhuru, na wa dhamani ni pale anapokuwa na binti zake au anapokuwa na wanawake wengine kakita vikundi vya kuweka- na kukopa. Yeye ni wadhamini kubwa sana kwa kikundi chake.
Rafiki mkubwa wa Farida ni Jenny, lakini pia yuko karibu sana na Stella, rafiki yao wazamani pamoja na Jenny ambaye hivi karibuni amehamia kijijini kutoka mjini. Pia yuko karibu na mwenyekiti wa kikundi, Mama Mjuni.
Afanda Kaifa: mwanaume wa miaka 42, mkuu wa polisi kijijini, mume wa Farida.
Amejijengea jina zuri sana hapa kijijini. Kwa wengi, ni mtu mchangamfu sana na mtu mwenye msaada mkubwa kwa watu, na ni wa kuaminika na mtumishi anayepatikana pindi anapohitajika. Lakini ndani ya familia yake, amkuwa akimnyanyasa mke wake kwa miaka mingi.
Amekuwa katika famila ambayo mama yake alikuwa mpole na baba yake alikuwa mkali mwenye kumiliki kila kitu ndani ya familia ambaye pia alikuwa polisi. Amefata nyayo za baba yake na kumuangalia baba yake.
Anaonekana wa kutojiamini kutokana na kuonekana kushindwa kwake kuzaa mtoto wa kiume, na tabia ya baba yake mzazi juu ya hili inazizi kufanya mambo kuwa mabaya. Kwa sababu hii amekuwa akimnyanayasa mke wake kwa miaka mingi. Anatumani kuwa siku moja atakuwa na mtoto wa kiume ambaye atakuwa mridhi wa kila kitu na kufuata nyao zake.
Afanda Kaifa ni mmiliki na mbinafsi, na wivu wake juu ya Farida unajulikana-vizuri kijijini.
Jenny: Mwanamke aliyeolewa anayemalizia rika la miaka ya 30.
Ameolewa na Vumi kwa miaka tangu sasa. Jenny hana uwezo wa kuzaa watoto hii ndiyo sababu ya kuvunjika kwa ndoa yake ya mwanzo.
Jenny anamiliki gereji ya magari ambaye alirithi kutoka kwa marehemu baba yake. Ni mwanakme mchapa kazi aliyefanikiwa kuunda biashara nzuri, na kuwaajiri wanaume kadhaa. Anauelewa mzuri wa magari kwa sababu hii inamfanya atazamwe tofauti na wanawake wengine kijijini ambao wanafikiri kwamba majukumu ya mwanamke ni kazi za jikoni, kufanya usafi nyumbani na kulima shambani.
Pamoja na kwamba anashughuli nyingi Gereji, Jenny huwa anatenga muda wa kusaidia shambani, ijapo kuwa namuachia mume wake kutafuta masoko ya mazao yake. Jenny pia ni mwanachama wa kikundi cha wanawake cha kuweka – kukopa.
Amevumilia miaka na miaka ya manyanyaso kutoka kwa wakwe zake, hasa hasa mama mkwe, kutokana na kutoweza kuzaa, mbali na kuwa yeye ndiye analisha familia.
Jenny hana marafiki wengi kijijini, lakini yuko karibu sana Farida, na alikuwa rafiki wa Stella wakiwa shuleni. Kwa kiasi fulani, anaweza kulinganisha hali yake na Farida kutoka na kutoweza kupata watoto na Farida kushindwa kuzaa watoto wa kiume.
Jenny na Farida wako karinu sana ingawa wako tofauti kabisa. Kwa namna kwamba, Jenny anataka Farida alichokuwa nacho—watoto—na Farida anataka alichokuwa nacho Jenny —uhuru wa kifedha.
Grace: Binti wa miaka 19 wa Mama K.
Grace ni msichana mwenye akili aliye na misimamo yake. Uzuri wake unampa kipaombele kijijini; ukweli, huwa yeye ni mada inayojadiliwa na wanaume wengi.
Miaka miwili iliyopita, Grace alimaliza shule ya sekondari na alitamani kuendelea na elimu ya juu, ingawa mama yake hamsaidii sana katika suala la elimu.
Grace sio kipenzi cha mama yake, ijapokuwa yeye ndiye anayesaidia shughuli za nyumbani na kuwalea mapacha wawili wadogo zake wa kiume, Alex na Adam, ambao wamekuwa wakidekezwa na mama yao.
Grace ni mchapa kazi: analima mahindi na mazao mengine katika kibustani kidogo nyuma ya nyumba yao. Mama yake na wadogo zake hawatilii maanani shamba lake ingawa analisha familia na baathi ya mazao anauza sokoni.
Mara chache anasaidia shughuli katiaka baa ya mama yake, kuwafurahisha walevi wanao shinda baa.
Grace ni mwanachama katika kikundi cha wanawake cha kuweka na kukopa, na ni rafiki mzuri wa Doris. Alikuwa rafiki mzuri wa Mjuni kabla hajabadilisha tabia.
Mama Mjuni: Mwanamke mwenye rika la miaka 40, mke wa mtumishi wa halmashauri ya wilaya, Mzee Ali.
Ndoa yake ni ndoa inayo tamaniwa na wanawake wengi hapa kijijini kwani yeye ndiye mwanamke pekee anayefanya maamuzi katika shughuli za kilimo akishirikiana na mume wake, kwanzia zao la kupanda, kuvuna na kulima mpaka kwenye kuuza mazao. Mume wake pia anamchango katika shughuli za nyumbani na za shambani. Kwa muda mrefu, imekuwa ikiaminika kuwa Mama Mujuni amemloga mume wake na kumshikilia kwa uchawi.
Mama Mjuni mwanamke mwenye fikra za mbali na mwenye roho nzuri. Yeye ndiye mwanzilishi wa kikundi cha kuweka na kukopa cha wanawake na yeye ndiye mwnyekiti.
Ana mtoto mmoja aliyezaa katika ndoa yake ya kwanza, na kijana aitwaye Mjuni. Anaumia sana na tabia ya Mujuni kutembea na kikundi kibaya cha vijana. Hajazaa watoto wowote na Mzee Ali.
Mzee Ali: mtumishi wa halmashauri ya wilaya mweye rika la miaka 60. Mume wa Mama Mjuni na Baba wa kambo wa Mjuni.
Ijapokuwa Mjuni ni mtoto wake wa Kambo, Mzee Ali anamjali na kumpenda kama vile ni mwanae.
Mzee Ali anaamini katika usawa katika kufanya maamuzi baina ya mke na mume. Ni kawaida kumkuta yeye na mke wake shambani kipindi cha kulima au kumkuta nyumbani akiosha vyombo wakati mke waki akifanya usafi.
Tabia ya mzee Ali imemfanya adharaulike kijijini, na watu wakisema kwamba mkwe wake ndiye anayevaa suruali katika familia na kwamba mzee Ali amelogwa.
Sigi: Mmiliki wa kampuni ya mauzo ya jumla na mmiliki wa ghala akiwa na miaka 40.
Kampuni ya Sigi ni wasambazaji wakubwa wa maharage kwenye kiwanda cha Tikka. Ni mfanyabiashara mnyongaji asiye jali chochote zaidi ya hela tu; ni aina ya watu ambao wanaweza kumtoa hata mama yake mzazi kafara kupata hela.
Mbali na biashara ya uuzaji wa jumla, anaendesha biashara za kimagendo katika ghala lake akiwatumia Adam na Alex kwa kazi zake chafu na biashara zake za giza.
Ni muovu, anapenda kuwa na wanawake wazuri, na anajulikana kwa kuwa honga kwa kuwapa zawadi.
Pia anapenda kupata kinywaji na mara nyingi anaenda baa ya Mama K akiwa na wafuasi wake na vijana wake waalifu.
Stella: Rafiki wa utotoni wa Jenny na Farida mwenye umri wa rika la miaka 30 ya awali.
Baada ya kupata matokeo mazuri shule ya sekondari, alijiunga na chuo mjni.
Aliishi mjini kwa miaka kadhaa baada ya kumaliza chuo, na baada ya kurudi kijijini, alipata kazi kijijini kusimamia usambazaji wa maharage.
Mama K: Katika miaka ya 50. Mama yake Grace na Vijana wawili wahuni, Adam na Alex.
Mama K ni mmiliki wa baa inayojulikana kijijini, na inaitwa, Mama K. Baa hii ni kituo cha walevi wengi katika kijiji hiki.
Mama K ni mlevi, ni mwoga na ni mchoko, anapokuwa amelewa hasa hasa kwa Grace, ambaye amekuwa akimnyanyasa kwa muda mrefu kwa imani kuwa yeye ndiye sababu ya mume wake wa kwanza kumuacha. Mama K amewalea Grace na vijana wawili na kuwapendelea vijana pamoja na kuwa siku zote wamekuwa wakijiingiza katika matatizo.
Adam and Alex: Wapacha wa Mama, miaka 17.
Vijana wawili hawa huwezi kuwatenga, siku zote wanakuwa pamoja. Wameunda “kikundi” na wakakiita: viroboto (kiroboto), jina hili linawafaa sana kwani siku zote wamekuwa wakiiba vitu na kuanzisha ugomvi.
Wamedekezwa na wameoza na wanajua siku zote wanamtegemea mama yao kulipa dhamana wakikamatwa.
Hawaendi shuleni, wanatumia muda wao mwingi kuvuta madawa na kutafuta kitu cha kuiba. Kijiji kimechoshwa na wizi wao maovu yao madogo madogo.
Mjuni: Kijana wa miaka kumi na sitawa Mama Mjuni na mtoto wa kambo wa mtumishi wa halamashauri, Mzee Ali.
Ni kijana aliye na matatizo na kugombana na wazazi wake. Tabia yake inapelekea kuumia kwa familia yake, hasa hasa mama yake. Anapenda kuwa na Adam na Alex, na anatoroka shuleni na kujiingiza katika matatizo, pamoja na kwamba ameonywa vikali ina wazazi wake.
Kabala hajabadilika tabia Mjuni alikuwa rafiki wa karibu wa Grace.
Doris: Mwanamke wa miaka ishirini na mwanachama wa vyama wa kuweka na kukopa.
Doris ni msichana anayependa vitu vizuri katika maisha, lakini hapendi kujituma. Yuko tayari kuwa na mwanaume tajiri ambaye anaweza kumuhudumia. Ni binti aliye dekezwa, na amekuwa mmoja kati ya wanawake wengi wa Sigi.
Anajiona kuwa ni mwenye akili, lakini ameweza kudanganywa kiurahisi na Sigi. Ni rafiki wa Grace.
Script
2. Sehemu:
Nje. Barabarani. Asubuhi.
3. Utambulisho wa kipengele:
Gari na mziki ndani ya gari.
4. Wahusika:
Jenny, Mr. Patel, Mvulana.
5. SFX:
INJINI YA GARI HUKU MZIKI UKISIKIKA NDANI YA GARI.
6. SFX:
MR. PATEL ANAIMBA KUFUATISHA MZIKI.
7. SFX:
GHAFLA KELELE KAMA ZA PANCHA ZINASIKIKA.
8. MR. PATEL:
(ANASHTUKA) Ohoo! (ANAONGEA PEKE YAKE) Sijui nini tena?
9. SFX:
GARI INAPUNGUZA MWENDO NA KUZIMA GHAFLA.
10. MR. PATEL:
(ANAONGEA PEKE YAKE KWA HASIRA) Nimeshaichoka hii gari! Kila siku mambo yale yale!
11. SFX:
MR. PATEL ANAJARIBU KUIWASHA GARI.
12. SFX:
GARI INAWAKA NA KUZIMA.
13. SFX:
MR. PATEL ANASHUKA KUTOKA KWENYE GARI NA KUBAMIZA MLANGO KWA HASIRA.
14. MR. PATEL:
(KWA HASIRA) Nakumbuka niliwaambia kabisa kwamba kila mwezi wakumbuke kuangalia kama gari ina matatizo yoyote! Lakini hakuna chochote walichofanya!
15. SFX:
MR. PATEL ANAJARIBU KUIKAGUA INJINI YA GARI.
16. MR. PATEL:
Hata sijui kwanini nawalipa hawa wazembe?
17. SFX:
MR. PATEL GHAFLA ANAPIGWA NA SHOTI.
18. MR. PATEL:
(ANAPIGA KELELE KWA MAUMIVU) Aaargh!
19. MVULANA:
(ANAKARIBIA MIC) Mzee, uko sawa?
20. MR. PATEL:
(KWA MAUMIVU) Nenda ukanitafutie fundi! Fanya haraka!
21. MVULANA:
Sawa, Nakuja sasa hivi.
22. SFX:
MR. PATEL ANALIA KWA MAUMIVU.
23. MVULANA:
(ANAKARIBIA MIC AKIKIMBIA) Huyu hapa!
24. JENNY:
Vipi mheshimiwa una tatizo gani?
25. MR. PATEL:
(KWA MAUMIVU) Niko sawa.
26. JENNY:
Ebu subiri nikusaidie.
27. MR. PATEL:
Hakuna shida; Naweza kusimama mwenyewe. (ANAMGEUKIA MVULANA) Wewe si nilikwambia uende ukanitafutie fundi?
28. MVULANA:
Lakini huyu ni fundi.
29. JENNY:
Mimi ni fundi.
30. MR. PATEL:
(KWA MSHANGAO) Oh!
31. JENNY:
Bado unataka nitengeneze gari yako?
32. PETER:
(ANAPATA KIGUGUMIZI CHA GHAFLA) Ah … Ah …
33. JENNY:
(ANAMKATISHA) Sikiliza, kama unaona itakusaidia naweza kuenda kumchukua mmoja wa wanaume pale gereji aje kutengeneza gari yako.
34. PATEL:
Hapana sio hivyo …. Basi endelea tu hakuna shida.
35. SFX:
JENNY ANAANZA KUITENGENEZA GARI.
36. PATEL:
Samahani, lakini sijawahi kukutana na mwanamke ambaye ni fundi wa magari hapa kijijini.
37. JENNY:
Usijali. Hii sio mara ya kwanza nasikia hayo maneno. Nimeshazoea.
38. MR. PATEL:
Kwa hiyo umekuwa ukitengeneza magari kwa muda gani?
39. JENNY:
(ANACHEKA) Mheshimiwa, kama ni ujuzi wangu wa magari ndio unakupa hofu, usijali. Nimekuwa nikifanya kazi ya ufundi kwa miaka kumi na tano sasa.
40. MR. PATEL:
Ulianzaje kufanya hii kazi?
41. JENNY:
Baba yangu alikuwa mmiliki wa gereji na yeye ndiye aliyenifundisha mambo yote kuhusu magari…Samahani, naomba hiyo spana hapo pembeni.
42. MR. PATEL:
(ANAMPA SPANA) Hii hapa.
44. MR. PATEL:
Kwa hiyo bado unamfanyia kazi baba yako?
45. JENNY:
Hapana, kwa bahati mbaya alifariki.
46. MR. PATEL:
Oh! Pole sana.
47. JENNY:
Asante; miaka mingi imepita sasa.
48. MR. PATEL:
Kwa hiyo unamfanyia kazi nani sasa hivi?
49. JENNY:
Simfanyi kazi mtu yoyote. Mimi ndio bosi kwenye gereji yangu na nimeajiri baadhi ya watu.
50. SFX:
MR. PATEL ANACHEKA.
51. JENNY:
Mbona unacheka?
52. MR. PATEL:
Ni kwamba sijawahi kukutana na mwanamke kama wewe hapa kijijini. Unanishangaza. Kumbe wewe sio fundi tu lakini ni mmiliki wa gereji na umeajiri watu pia.
53. JENNY:
Baada ya mzee wangu kufariki, ilibidi niendelee kufanya kazi. Nilirithi gereji yake na kuiendeleza….Unaweza kujaribu kuiwasha gari?
55. SFX:
MR. PATEL ANAWASHA GARI NA GARI INAANZA KUUNGRUMA.
56. MR. PATEL:
Umenishangaza kwa mara nyingine tena!
57. JENNY:
Nimefurahi nimeweza kuwa msaada kwako.
58. MR. PATEL:
Kwa hiyo unanidai shingapi? (ANAMKABIDHI JENNY PESA) Sikiliza—shika hii.
59. JENNY:
Hizi ni pesa nyingi sana.
60. MR. PATEL:
Usijali, hiyo ni kwa kuiokoa siku yangu. Labda siku moja utaamua kuajiriwa na kiwanda chetu ili uwe unatutengezea magari yetu.
61. JENNY:
Ni bora utoe hiyo tenda kwa gereji yangu.
62. MR. PATEL:
(ANACHEKA) Wewe sio fundi mzuri tu lakini ni mfanyabiashara pia dada?
63. JENNY:
Jenny… Naitwa Jenny.
64. MR. PATEL:
Kwa kweli umeokoa siku yangu Jenny. Mimi naitwa Mr. Patel, na ni meneja wa Tikka common beans factory.
65. JENNY:
Ooh! Basi karibu gereji yetu siku yoyote ukipata shida.
66. MR. PATEL:
Asante sana na siku njema.
68. SFX:
MR. PATEL ANAINGIA NDANI YA GARI YAKE NA KUIWASHA NA KUONDOKA.
71. Sehemu:
Ndani. Hospitalini. Asubuhi.
72. Utambulisho wa kipengele:
73. Wahusika:
Farida, Mama Mjuni, Daktari, Nesi.
75. NESI:
(NEAR MIC) Farida Kaifa! Farida Kaifa yupo?
76. FARIDA:
(FAR FROM MIC) Ndio nipo!
78. FARIDA:
(ANAKARIBIA MIC) Mimi ni Farida Kaifa.
79. NESI:
Sawa, daktari yupo tayari kukuona.
80. SFX:
MLANGO UNAFUNGULIWA NA FARIDA ANAINGIA.
81. DAKTARI:
(KARIBU NA MIC) Tafadhali karibu kiti.
82. FARIDA:
(ANAKARIBIA MIC) Asante.
83. SFX:
FARIDA ANAVUTA KITI NA KUKAA.
84. DAKTARI:
(ANAFUNGUA MAFAILI YAKE) Unaitwa Farida Kaifa na una miaka ishirini na nane. Haya niambie, nini kinakusumbua?
85. FARIDA:
Nimekuwa nikisikia maumivu.
86. DAKTARI:
Maumivu?…Sehemu gani ya mwili?
87. SFX:
FARIDA ANATOA KICHEKO CHA UOGA.
88. DAKTARI:
(ANACHEKA KIDOGO) Sikiliza mpendwa, nina uhakika chochote kinachokusumbua nimeshawahi kukiona. Kwa hiyo nakuhakikishia hakuna haja ya kuogopa.
89. FARIDA:
Unaweza ukaniandikia dawa ya kupunguza maumivu?
90. DAKTARI:
Siwezi kukuandikia dawa bila ya kujua tatizo kwanza. Nitakuwa sifuati miiko na sheria ya kazi yangu.
91. SFX:
FARIDA ANAKAA KIMYA.
92. DAKTARI:
Nakuomba uje kukaa hapa kwenye hiki kitanda cha wagonjwa mara moja.
93. SFX:
FARIDA ANAINUKA NA KUKAA KWENYE KITANDA.
94. DAKTARI:
Sawa, naomba unioneshe ni wapi unaposikia hayo maumivu.
95. FARIDA:
(AKIONESHA) Ni hapa na hapa.
96. DAKTARI:
Sawa…kwa hiyo kwenye tumbo na mapaja.
98. DAKTARI:
Sawa, nitakuomba utoe huo mtandio ili nikufanyie vipimo.
100. DAKTARI:
(ANAMTIA MOYO) Usiogope.
101. SFX:
FARIDA ANATOA MTANDIO WAKE.
102. DAKTARI:
(KWA MSHANGAO) Heeh! Nini kilikutokea? Uliporwa na majambazi au?
103. FARIDA:
(KWA SAUTI YA CHINI) Ndio.
104. DAKTARI:
Ulienda polisi?
105. FARIDA:
(GHAFLA) Sikiliza daktari, sikuporwa.
106. DAKTARI:
Nini kilikutokea sasa? Nani amefanya hivi?
107. SFX:
FARIDA ANAKUWA KIMYA TENA.
108. DAKTARI:
Sikiliza dada yangu, itabidi uende polisi; hii ni hatari sana. Ebu angalia haya makovu.
109. FARIDA:
Lakini sasa hivi najisikia nafuu kidogo. Sio mbaya sana.
110. DAKTARI:
Sikiliza dada yangu nimeshaona kesi kama yako mara nnyingi sana. Wanawake kama wewe wanakuja hapa -wamepigwa na kuumizwa vibaya lakini wanaogopa kuongea. Kama utaniruhusu nitakusaidia kuandika polisi ripoti.
111. FARIDA:
(KWA HASIRA) Lakini nimekuja hapa kupa matibabu, sio kupata msaada wa kisheria.
112. DAKTARI:
(ANAGUNA) Sawa. Nitakuandikia dawa za kutuliza maumivu na sindano ya tetanus.
113. FARIDA:
Asante daktari.
114.
PUNGUZA SAUTI HATUA KWA HATUA
115.
ONGEZA SAUTI HATUA KWA HATUA
116. MAMA MJUNI:
(MBALI NA MIC) Wewe Farida! Farida!
117. FARIDA:
(KARIBU NA MIC) Mama Mjuni.
118. MAMA MJUNI:
(ANAKARIBIA MIC) Nilihisi tu ni wewe. Ehee! Kulikoni mwenzangu unaumwa?
119. FARIDA:
Malaria imekuwa inanisumbua sana.
120. MAMA MJUNI:
Oh! Pole sana —Si unajua tena hiki kipindi cha mwaka, watu huwa wanaumwa sana malaria.
121. FARIDA:
Asante. Na wewe nini kimekuleta hapa hospitali?
122. MAMA MJUNI:
Nimekuwa najisikia ovyo mpaka nikaanza kuhisi labda mzee Ali kanipa ujauzito (ANACHEKA MWENYEWE)— Umri huu jamani?! Si kitakuwa kituko!
123. SFX:
FARIDA ANATOA KICHEKO KWA MBALI.
124. MAMA MJUNI:
Farida, Upo sawa kweli?
125. FARIDA:
Hapana niko sawa, ni hii malaria tu imekuwa inifanye nijisikie ovyo. Acha mimi niende tu, tutaonana baadae kwenye kikao cha vikoba.
126. MAMA MJUNI:
Farida, subiri …
127. SFX:
FARIDA ANAONDOKA HARAKA.
130. Sehemu:
Nje. Nyumbani kwa mama K. Asubuhi.
131. Utambulisho wa kipengele:
Grace anachambua maharage.
133. SFX:
MAHARAGE YANAPEPETWA.
134. SFX:
GRACE ANAANZA KUIMBA HUKU AKIPEPETA MAHARAGE.
135. DORIS:
(ANAKARIBIA MIC) Grace, unafanya nini? Mimi nilijua utakuwa tayari sasa hivi.
136. GRACE:
(KWA UTANI) Mimi mzima; asante sana kwa kunijulia hali.
137. DORIS:
Ebu acha utani bwana. Unajua ukiendelea hivi tutachelewa kuonana na Sigi.
138. GRACE:
Wewe unajua kabisa kwamba siwezi kuondoka bila ya kuwapikia hapa nyumbani. Wakirudi na kukuta hakuna chakula, kijiji chote kitajua.
139. DORIS:
Kwani Alex na Adam hawawezi kupika wenyewe?
140. GRACE:
Adam na Alex wapike?! (ANACHEKA) Nasubiri hiyo siku ifike.
141. DORIS:
(KWA MSISISTIZO) Lakini unajua hauwezi kupika na kuwahi kukutana na Sigi.
142. GRACE:
Heeh! Mama ebu tulia. Kwanza mimi nilijua tunaenda huko kwa ajili ya biashara, mbona umevaa kama tunaenda disco?
143. DORIS:
(ANACHEKA) Umependa gauni langu eh?
144. GRACE:
Ni zuri na limekupendeza kwa kweli.
145. DORIS:
Kweli? Na viatu je?
146. GRACE:
Vinaoenekana vya gharama kama nini.
147. DORIS:
(ANACHEKA) Unajua leo ilibidi nivunje kabati kwa sababu inabidi ujipange pale unapoenda kukutana na mtu kama Sigi.
149. DORIS:
Unaguna nini sasa?
150. GRACE:
Hapana, ila kuwa makini tu kwa sababu nimesikia stori nyingi sana kuhusu huyo Sigi hapa kijijini.
151. DORIS:
Stori gani hizo?
152. GRACE:
Nasikia ni kiwembe ile mbaya. Kazi yake ni kubadilisha wanawake tu kama bodaboda.
153. DORIS:
Wewe unajua jinsi watu walivyo hapa kijijini, kazi yao ni umbea tu na kuongelea watu wengine.
154. GRACE:
Haya shauri yako, sema unajua lisemwalo lipo.
155. DORIS:
Watu wanaona wivu tu kwa sababu Sigi ni mfanyabiashara mkubwa hapa kijijini. Anafanya biashara mpaka na kile kiwanda cha maharage.
156. GRACE:
(ANAGUNA) …Sijui kuhusu yote hayo lakini najua kwamba nakuonea wivu na hivyo viatu. Nimebaki navitamani tu.
157. DORIS:
(ANACHEKA) Unavipenda eeh? Yaani ungejua pesa ilivyonitoka hapa, we acha tu.
158. GRACE:
Vinaonekana tu ni vya bei mbaya. Na sijui kama bado unaweka akiba ili tuje kununua ng’ombe kwa ajili ya ile biashara yetu ya kuuza maziwa.
159. DORIS:
Yaani wala usijali Grace mimi bado naweka akiba.
160. GRACE:
Hmmm! Mimi nina wasiwasi.
161. DORIS:
Grace, unajua tunazidi kuchelewa wakati bado tunaongea hapa. Ebu twende bwana.
162. GRACE:
Sawa twende basi lakini tusikae muda mrefu kwa sababu inabidi nirudi kupika.
165. Sehemu:
Nje. Gala la Sigi. Mchana.
166. Utambulisho wa kipengele:
167. Wahusika:
Grace, Doris, Sigi, Mjane, Mudi.
168. MJANE:
(ANAMSIHI SIGI HUKU AKIPIGA MAGOTI) Nakuomba mwanangu, nahitaji hizo pesa sana. Nakuomba mwanangu, niko chini ya miguu yako.
169. SIGI:
Mama, nimeshakwambia kwamba nitakupa pesa zako za maharage pale nitakapolipwa na kiwanda. Mbona hatuelewani lakini?
170. MJANE:
Mwanangu unajua kabisa mimi ni mjane. Mume wangu ameshafariki.
171. SIGI:
Na mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Lakini hayo yote yananihusu nini mimi?
172. MJANE:
Nitawalisha nini wanangu bila ya pesa? eeh? Ebu niambie, umeme nitalipia nini mimi?
173. SIGI:
Mimi sijui yote hayo. Ninachojua ni kwamba tulihaidiana kuwa nitakulipa pesa yako baada na mimi kulipwa na kiwanda.
174. MJANE:
Najua mwanangu lakini nakuomba unisaidie tu hii mara moja.
175. SIGI:
Samahani lakini hili suala liko nje ya mikono yangu. Biashara ni biashara na ahadi ni ahadi. Mudi ebu nisaidie kumuondoa.
176. MUDI:
Haya mama twende.
177. SFX:
MUDI ANAMUONDOA MJANE.
178. SFX:
MJANE BADO ANALIA.
179. GRACE:
(ANALALAMIKA) Wewee! Haina haja ya kumvuta hivyo!
180. SIGI:
(ANAKARIBIA MIC) Samahani kwa kuwaweka lakini kuna watu wengine hawajui biashara ni nini.
182. SIGI:
Samahani, lakini ulisema unaitwa nani?
183. DORIS:
Mimi naitwa Doris na huyu anaitwa Grace.
184. SIGI:
Huyu namjua; nishamuona mara nyingi pale kwa mama k. Wewe ni mtoto wake mama K eeh?
185. GRACE:
Ndio. Samahani naomba niongee na rafiki yangu mara moja.
186. SIGI:
Sawa haina shida.
187. SFX:
GRACE ANAMVUTA DORIS PEMBENI.
188. DORIS:
(KWA SAUTI YA CHINI) Vipi?
189. GRACE:
(KWA SAUTI YA CHINI) Mimi Sijiskii poa kuhusu hii ishu yote.
190. DORIS:
Una maana gani?
191. GRACE:
Siwezi kufanya biashara na huyo jamaa.
192. DORIS:
Usiniambie unataka kubadilisha mawazo. Sikiliza- Sigi atatupa dili poa.
193. GRACE:
Na tukija kutimuliwa kama huyo mama tuliomkuta hapa?
194. DORIS:
Hiyo haiwezi kutokea bwana.
195. GRACE:
Una uhakika gani? Tunaweza kupata watu wengine wa kununua maharage yetu bwana.
196. DORIS:
Sikiliza- Sigi ndiye mwenye pesa ya maana hapa kijijini. Wewe unafikiri kwa nini kila mtu anamuuzia maharage yeye?
197. GRACE:
Mbona ameshindwa kumlipa huyo mama sasa?
198. DORIS:
Mimi sijui; labda huyo mama ameshindwa kufuata makubaliano yao. Sikiliza wewe jipange turudi kuongea nae.
199. SFX:
DORIS NA GRACE WANARUDI KUONGEA NA SIGI.
200. DORIS:
(ANACHEKA) Haya tumerudi.
201. SIGI:
Sawa. Kwa hiyo tulikuwa tumeishia wapi?
202. DORIS:
Tulikuwa tunakaribia kupendekeza bei ya maharage yetu.
203. SIGI:
Sawa, basi tuingie ofisini kwangu ili tujadili.
204. SFX:
GRACE NA DORIS WANAANZA KUINGIA OFISINI KWA SIGI.
205. SIGI:
Samahani, lakini naweza kumruhusu mmoja wenu tu kuingia ofisini kwangu.
206. GRACE:
(ANACHEKA) Kwanini? Ofisi yako ni ndogo sana au?
209. SIGI:
Hapana sikutanii hata kidogo.
210. GRACE:
Mbona hueleweki? Tumekuja hapa kuongea biashara na wewe, sasa inakuaje unataka kumruhusu mmoja wetu tu kuingia ofisini kwako?
211. SIGI:
Ndio ilivyo. Hii ni sehemu yangu ya biashara na nina sheria zangu.
212. GRACE:
Samahani lakini huu ni upuuzi; siwezi kuingia ofisini kwako bila Doris.
213. SIGI:
Basi tufanye hakuna biashara.
214. GRACE:
Poa. Haina shida (ANAMGEUKIA DORIS) Twende Doris.
215. DORIS:
Basi acha mimi niingie ofisini na Sigi.
216. GRACE:
(KWA MSHANGAO) Doris, unatania au? Samahani mara moja.
217. SFX:
GRACE ANAMVUTA DORIS PEMBENI.
218. GRACE:
(SAUTIYA CHINI MPAKA MWISHO WA SCENE) Hivi unawaza nini?
219. DORIS:
Hatukuja kote huku kuangalia dili letu likienda na maji. Na mimi sijapendeza hivi bure.
220. GRACE:
Tunaweza kufanya biashara na mtu mwingine.
221. DORIS:
Mimi nakwambia hatuwezi kupata dili la ukweli kama hili.
222. GRACE:
Mimi sidhani kama ni wazo zuri.
223. DORIS:
Shauri yako, mimi naenda.
224. GRACE:
Doris, usivunje heshima yako kisa tu unataka kuuza maharage.
225. DORIS:
Una maana gani?
226. GRACE:
Mimi naona kama umechanganyikiwa.
227. DORIS:
Sikiliza — kisa tu unasikia tetesi hapa kijijini, haimaanishi kwamba ni za kweli. Mimi naenda, kama watu wakitaka kuongea waache waongee.
228. SFX:
DORIS ANAMUACHA GRACE NA KUINGIA OFISINI KWA SIGI.
229. GRACE:
(KWA SAUTI) Doris! Doris! Doris!
232. Sehemu:
Ofisi ya mwenyekiti wa serikali za mtaa. Mchana.
233. Utambulisho wa kipengele:
234. Wahusika:
Mama Mjuni, Mama K, Lydia, Rehema, Monica, wanawake wengine.
235. REHEMA:
Na wewe je? Unahisi utapata gunia ngapi za maharage mwaka huu?
236. LYDIA:
(ANAGUNA) Sina uhakika, lakini nahisi nitapata chache zaidi ukifananisha na mwaka jana, kwa jinsi mambo yanavyoonekana.
237. MONICA:
Yaani sijawahi kuona mwaka m’baya kama mwaka huu.
238. MAMA K:
(KWA SAUTI YA ULEVI) Hakuna jipya hapo! Kila mwaka m’baya kwako inavyoonekana. (ANACHEKA)
239. MONICA:
Mama K, nilikuwa siongei na wewe kwa hiyo jiangalie. Ohoo!
240. REHEMA:
Monica, hivi kwanini unajisumbua? Wewe huoni kashalewa huyo?
241. LYDIA:
Eeeh! Mama K—asubuhi yote hii?
242. MAMA K:
Aaah, Achana na mimi. Mimi ninachotaka pesa yangu tu, niondoke saa hizi. Na huyo mama Mjuni na Farida wako wapi tuanze kikao sasa hivi!
243. REHEMA:
Huyo hapo anakuja.
244. MAMA MJUNI:
(ANAKARIBIA MIC) Jamani wanachama wenzangu mnisamehe kwa usumbufu wa kunisubiria. Nadhani tunaweza tukaanza kikao sasa. Mnaendeleaje lakini?
245. REHEMA:
Mimi sipo vizuri mama Mjuni. Mavunoi mabaya sana msimu huu.
246. MONICA:
Kweli kabisa; hapa nilipo sidhani kama nitapata zaidi ya gunia tano au sita za maharage.
247. MAMA MJUNI:
Watu wengi wanalalamika mavuno ya msimu huu. Nyie mnahisi tatizo ni nini?
248. REHEMA:
Tunafahamu basi; Inawezekana kwa sababu ya mvua chache.
249. LYDIA:
Au labda ardhi ya hapa kijijini nayo imepoteza rutuba yake.
250. MAMA K:
(ANAWAKATISHA) Basi imetosha! Mavuno! Mavuno! Mimi ninachotaka kujua Farida yuko wapi ili anipe pesa zangu.
251. MAMA MJUNI:
Sidhani kama Farida atakuja leo.
252. MAMA K:
Una maana gani? Yeye ndio mweka hazina- anatakiwa kuwepo hapa kwa sababu leo ni mwisho wa mwezi.
253. MAMA MJUNI:
Najua ni mwisho wa mwezi mama K, lakini nahisi Farida anaumwa.
254. MAMA K:
Kwa hiyo inapofika zamu yangu kulipwa, ghafla mweka hazina ndio anapata ugonjwa eeh?
255. MAMA MJUNI:
Hapana, ni kweli anaumwa. Nimemuona hospitali leo na hakuwa vizuri.
256. MAMA K:
(ANAGUNA) Nilijua tu.
257. MAMA MJUNI:
Una maana gani?
258. MAMA K:
Hivi unadhani mimi ni mjinga? Najua hii ni njama yenu wewe na Farida kuchukua pesa zangu.
259. LYDIA:
(ANAINGILIA) Mama K, ebu kuwa na busara. Unamshutumu vipi mama Mjuni kuwa mwizi?
260. MAMA K:
Ebu kaa kimya na wewe! Sikuwa naongea na wewe!
261. MONICA:
Ameshalewa huyo; hamuwezi kuelewana nae.
262. REHEMA:
Ndio! Kwanza ameingia hapa ananuka pombe hatari.
263. SFX:
MAMA MJUNI ANAWATULIZA.
264. MAMA MJUNI:
Sawa basi, naomba tuelewane. Mama K kama utakubali, mimi nitakupa pesa yangu alafu Farida akirudi atanirudishia pesa yangu.
265. MAMA K:
Sawa, hiyo imekaa vizuri.
268. Sehemu:
Nje. Nyumbani kwa Farida. Mchana.
269. Utambulisho wa kipengele:
Keleleza watoto wakicheza.
270. Wahusika:
Farida, Jenny, Sifa, Zuhura.
271. SFX:
WATOTO WANACHEZA.
272. ZUHURA:
(ANAONGEAS KWA SHAUKU) Angalia! Mama mdogo Jenny!
273. SFX:
SIFA NA ZUHURA WANAKIMBIA KUMKUMBATIA JENNY.
274. JENNY:
(KWA FURAHA) Mambo yenu! Mko poa?
275. SIFA, ZUHURA:
Ndio. Shikamoo?
276. JENNY:
Marahabaa! Hafsa yuko wapi?
278. JENNY:
Na kwanini nyie hamjalala?
279. ZUHURA:
Sisi wakubwa.
280. JENNY:
(ANACHEKA) Nani kawaambia nyie wakubwa?
281. SIFA:
Hajatuambia mtu. Ni kweli.
282. JENNY:
(ANACHEKA) Inabidi mlale kama Hafsa ili muendelee kukua! Haya nimewaletea machungwa. (ANAWAPA MACHUNGWA) Haya shikeni.
283. SIFA, ZUHURA:
Asante.
284. JENNY:
Msisahau kumpa na Hafsa chungwa lake. Mama yenu yuko wapi?
285. ZUHURA:
Yuko kwenye banda anawalisha mbuzi lakini amesema mtu akiuliza tumwambie amelala.
286. JENNY:
(ANACHEKA) Ndio alivyowaambia eh?
287. SFX:
JENNY ANAELEKEA KWENYE BANDA LA MBUZI.
288. JENNY:
(ANAITA KWA SAUTI) Farida! Farida!
289. FARIDA:
(MBALI NA MIC) Niko huku!
290. JENNY:
Naona unawafundisha wanao kuwa waongo eh?
291. FARIDA:
(KWA UTANI) Nimesikia unacheka toka mbali uko- nikajua tu biashara itakuwa ilikuwa nzuri leo.
292. JENNY:
(ANACHEKA) Biashara sio mbaya .Lakini kuna kitu cha ajabu kimetokea leo we acha tu!
294. JENNY:
Si nimekutana na yule meneja wa kiwanda cha maharage.
295. FARIDA:
(KWA MSHANGAO) Kweli? Alikuja gereji au?
296. JENNY:
Hapana nimekutana nae barabarani – gari yake iliharibika.
297. FARIDA:
Kwa hiyo ulitengeneza gari yake? Atakuwa amekulipa pesa nzuri tu.
298. JENNY:
Kanilipa vizuri, sio mbaya (ANACHEKA) Farida natamani ungekuwepo kuona pesa aliyonipa! Mwili mzima ulinisisimuka kwa kuziangalia tu. Basi nikajifanya kama amenipa pesa nyingi wakati nilikuwa nikifurahia kimoyo moyo.
299. SFX:
JENNY NA FARIDA WANACHEKA HAWANA MBAVU.
300. FARIDA:
Unaona?Nilijua tu biashara itakuwa nzuri. Kwa hiyo kwa sababu leo umejaa na umesema mwenyewe…ni bora ununue mbolea kama ulivyoahidi.
301. JENNY:
Umeshaanza mambo yako. Nilijua tu, kila nikija hapa lazima ujaribu kuniuzia kitu.
302. FARIDA:
Hapana. Ahadi ni ahadi. Nimekutunzia mbolea nzuri kabisa kwa ajili yako hapa. Hii hapa.
303. SFX:
FARIDA ANAJARIBU KUINUA GUNIA LA MBOLEA LAKINI ANADONDOKA CHINI AKILIA KWA MAUMIVU.
304. JENNY:
(KWA WASI WASI, ANAMSOGELE FARIDA KUMSAIDIA) Farida! Uko sawa?
305. FARIDA:
(KWA MAUMIVU) Niko poa; Nimeteleza tu.
306. JENNY:
Acha niukusaidie.
307. FARIDA:
Hapana, hakuna shida.
308. SFX:
JENNY ANAJARIBU KUMSAIDIA FARIDA LAKINI FARIDA ANALIA KWA MAUMIVU NA JENNY ANAGUNDUA MAKOVU YA FARIDA.
309. JENNY:
(KWA HOFU) Farida, hayo sio makovu kwenye mkono wako?
310. FARIDA:
(ANAJARIBU KUPOTEZEA) Hapana sio kitu.
311. JENNY:
Sio kitu? Una maana gani sio kitu wakati nayaona kabisa kwenye mkono wako?
312. FARIDA:
Niliteleza bwana nikadondoka bafuni.
313. JENNY:
Amekupiga tena? Nijibu amekupiga tena?
314. SFX:
KUNA UKIMYA KATI YA FARIDA NA JENNY NA GHAFLA ZUHURA ANAKUJA AKILIA.
315. ZUHURA:
(ANALIA AKIKARIBIA MIC) Mama! Sifa amechukua chungwa langu alilonipa mama mdogo Jenny.
316. SIFA:
(ANAPAZA SAUTI) Muongo! Muongo! Sijachukua chungwa lake!
317. FARIDA:
Sifa! Kwanini unapenda kumsumbua mdogo wako lakini?
318. SIFA:
(KWA KUDEKA) Lakini sijachukua chungwa lake. Mimi ninalo langu.
319. FARIDA:
(ANAJARIBU KUMTULIZA ZUHURA) Acha kulia mwanangu! Nitakununulia chungwa lingine sawa?
323. Sehemu:
Nje. Nyumbani kwa mama Mjuni. Mchana.
324. Utambulisho wa kipengele:
Mzee Ali anachota maharage na koleo.
326. SFX:
MZEE ALI ANACHOTA MAHARAGE NA CHEPEO NA KUWEKA KWENYE GUNIA.
327. MZEE ALI:
Hee! Mbona umewahi kurudi? Ilikuwaje?
328. MAMA MJUNI:
Hawajakuta chochote zaidi ya BP kuwa juu.
329. MZEE ALI:
Kwa maana hiyo unaumwa. Unahitaji kupumzika. Njoo ukae hapa.
330. MAMA MJUNI:
Ah na wewe ushaanza! Unapenda kukuza mambo kama nini. Mbona unafanya kazi peke yako? Mjuni yuko wapi?
331. MZEE ALI:
Usiwe na wasi. Hili nalo ni zoezi zuri.
332. MAMA MJUNI:
Acha nikusaidie basi.
333. MZEE ALI:
Hapana wewe pumzika. Kwanza inaonekana siku yako ilikuwa ndefu sana.
334. MAMA MJUNI:
Nishazoea siku zangu kuwa ndefu na akina mama wenzangu kwenye kikoba.
335. MZEE ALI:
Vipi kikao kimeendaje lakini?
336. MAMA MJUNI:
Kila kitu kilienda sawa mpaka mama K alipoanzisha varangati katikati ya kikao.
337. MZEE ALI:
Heeh! Shida nini?
338. MAMA MJUNI:
Ilikuwa zamu yake kupata pesa lakini Farida hakutokea leo, ndipo shida ilipoanzia hapo.
339. MZEE ALI:
(ANACHEKA) Mimi mama K simshangai lakini kwanini Farida naye hakutokea leo?
340. MAMA MJUNI:
Nadhani atakuwa anaumwa. Nilimuona leo nilivyoenda hospitali.
341. MZEE ALI:
Uliongea nae?
342. MAMA MJUNI:
Ndio lakini alikuwa tofauti leo.
343. MZEE ALI:
Una maana gani?
344. MAMA MJUNI:
Sijui….Ni kama kuna kitu alikuwa ananificha. Aliondoka ghafla hata kabla ya kuagana vizuri.
345. MZEE ALI:
Hmm! Mbona si kawaida yake!
346. MAMA MJUNI:
Na mimi ndio nilkuwa najiuliza. (GHAFLA) Hivi unadhani mume wake anaweza akawa anampiga kweli?
347. MZEE ALI:
(BILA YA KUTEGEMEA) Sijui. Wewe ndio unatumia muda mwingi nae. Kitu gani kinakupelekea kufikiri mumewe anampiga?
348. MAMA MJUNI:
Kuna kitu hakipo sawa.
349. MZEE ALI:
Inawezekana ni kitu kingine kabisa- umesema mwenyewe alionekana kama kuna kitu anaficha.
350. MAMA MJUNI:
Sijui lakini kuna kitu nahisi. Huwezi kuelewa najua.
352. MAMA MJUNI:
Unadhani unaweza ukaingilia kati kama diwani na kumsaidia?
353. MZEE ALI:
Sikiliza mama Mjuni, hata kama nikitaka kuingilia kati siwezi kwa sababu Farida inabidi aamue mwenyewe na kuweka wazi kama ni kweli anapigwa na mumewe.
354. MAMA MJUNI:
Naomba isiwe kweli lakini kuna kitu kinaniambia kwamba kuna tatizo.
357. Sehemu:
Ndani. Nyumbani kwa Jenny. Jioni.
358. Utambulisho wa kipengele:
360. SFX:
KELELE ZA MPIRA KWENYE T.V.
361. VUMI:
(ANASHINGILIA) Safi! Toa pasi! Toa pasi! Toa pasi! (KWA HASIRA) Aaaah! Unakosa vipi goli pale? Nafasi ya wazi kabisa! Hata mimi nafunga hapo!
362. SFX:
JENNY ANAFUNGUA MLANGO NA KUINGIA.
363. JENNY:
Heeh! Mume wangu, unajua nimekuwa nakusikia kutoka mtaa wa pili hayo makelele yako.
364. VUMI:
Aaah! Si hawa Yanga nao wananiumiza kichwa tu. Wanakosa magoli ya wazi kabisa leo.
365. JENNY:
Watu wanaweza kufikiri kuna mtu kichaa anaishi hapa.
366. VUMI:
Wewe unajua mtu pekee ambaye ananipa uchizi zaidi ya yanga ni wewe!
367. SFX:
VUMI ANAMKUMBATIA JENNY.
368. JENNY:
(KWA UTANI) Mhhh! Mbona kama sio kweli? Mbona hukunishangilia nilivyoingia hapa sasa hivi?
369. VUMI:
(ANACHEKA) Ni kwa sababu nimekuwa shabiki wa yanga tangu mtoto lakini wewe tuna miaka sita tu, tangu tumefunga ndoa.
371. VUMI:
(ANACHEKA) Unajua nilikuwa nakutania tu. Ehee niambie, siku yako ilikuwaje?
372. JENNY:
Nilikuwa nimetingwa na kazi kama nini leo- na wewe?
373. VUMI:
Mimi nilikuwa shambani nasimamia mavuno.
374. JENNY:
Natamani ningekuwepo kusaidia lakini leo nilikuwa nimebanwa sana gereji. (KWA SHAUKU) Unajua leo nimetengeneza gari ya meneja wa kile kiwanda cha maharage.
375. SFX:
VUMI GHAFLA ANARUKA JUU KUSHANGILIA TIMU YAKE KUFUNGA LAKINI SIO GOLI.
376. JENNY:
Hivi umesikia hata nilichosema?
377. VUMI:
Nilikuwa nakusikiliza mpenzi lakini hii timu inanichanganya tu wanakosa sana magoli leo.
378. JENNY:
Pia nilipita kumuona Farida leo, na hakuwa katika hali nzuri.
379. VUMI:
(AKILI YAKE IKIWA KWENYE MPIRA) Toa pasi! Toa pasi! Toa pasi haraka!
380. JENNY:
(KWA SAUTI) Vumi!
382. JENNY:
Naongea na wewe kuhusu mambo ya msingi lakini wewe unawaza mpira tu?
383. VUMI:
Macho yangu yapo kwenye mpira lakini masikio yangu yapo kwako. Mimi nakusikiliza kwa umakini- niamini.
384. JENNY:
Kama ni kweli, niambie nimetoka kusema nini sasa hivi hapa?
385. VUMI:
Si umesema umetoka kumuona Farida na alikuwa kwenye hali nzuri.
386. JENNY:
(KWA MSISITIZO) Hakuwa katika hali nzuri! Nimesema hakuwa katika hali nzuri. Nahisi Kaifa amekuwa akimpiga tena.
387. VUMI:
Hapana. Kwanini unafikiria hivyo?
388. JENNY:
Si kwa sababu nilikuwa nae na nikaona makovu kwenye mikono yake. Yaani siamini kama anamfanyia hivi tena rafiki yangu. Inabidi mtu aingilie kati siku moja.
389. VUMI:
Mimi ningekushauri uachane na mambo yasiyo kuhusu.
390. JENNY:
Samahani, lakini siwezi nikakaa tu wakati rafiki yangu anateseka.
393. Sehemu:
Ndani. Nyumbani kwa Farida. Usiku.
394. Utambulisho wa kipengele:
Kelele za mlango ukigongwa.
395. Wahusika:
Farida, Afande Kaifa, Sifa.
396. SFX:
AFANDE KAIFA ANAFUNGUA MLANGO NA KUINGIA NDANI.
397. FARIDA:
(ANAKARIBIA MIC) Za kwako? Siku yako ilikuwaje?
398. SFX:
SIFA ANAMKIMBILIA BABA YAKE.
399. SIFA:
(ANAKARIBIA MIC) Baba amerudi! Baba amerudi!
400. FARIDA:
Sifa, ebu acha kelele! Usiku sasa hivi, watu wamelala.
402. AFANDE KAIFA:
Marahaba. Mbona bado hujalala?
403. SIFA:
Kwa sababu nilikuwa nakusubiria unisaidie na kazi ya shule.
404. AFANDE KAIFA:
Kwa nini usimwambie mama yako?
405. SIFA:
Kwa sababu kila nikumuomba anasema ana kazi.
406. AFANDE KAIFA:
Mimi nimechoka sana leo.
407. SIFA:
Lakini mwalimu kasema atanipa adhabu kama kesho sijamaliza kazi yake.
408. FARIDA:
Sifa, hivi huoni baba yako amechoka? Ebu nenda chumbani, nitakuja kukusaidia baadae.
409. SFX:
SIFA ANAENDA CHUMBANI.
410. FARIDA:
(ANAMWAMBIA AFANDE KAIFA) Inabidi ule.
411. AFANDE KAIFA:
Umepika nini?
412. FARIDA:
Nimepika ndizi na maharage kwa ajili yako.
413. SFX:
FARIDA ANAMTAYARISHIA CHAKULA AFANDE KAIFA.
414. FARIDA:
Ndizi za leo nzuri sana. Nimezinunua kutoka kwa mama Juma sokoni leo.
415. SFX:
AFANDE KAIFA ANAANZA KULA.
416. FARIDA:
Basi leo wakati niko sokoni, kidogo tu Grace mtoto wa mama K nae huyo. Basi sio miluzi hiyo kutoka kwa wanaume pale sokoni. Mara huyu kamuita huku mara mwingine kwamwita huku mpaka nikamuonea huruma jamani. Kumbe uzuri unaweza kuwa kero saa nyingine.
417. SFX:
AFANDE KAIFA ANAENDELEA KULA.
418. FARIDA:
Hivi nimekwambia Jenny alikuja leo akaniambia jinsi alivyotengeneza gari ya meneja wa kiwanda cha maharage. Nilifurahi sana alivyoiambia!
419. AFANDE KAIFA:
Nini kilikufurahisha?
420. FARIDA:
Jamani sio kila siku unaona mwanamke anatengeneza gari ya mtu mkubwa hapa kijijini kama yule.
421. AFANDE KAIFA:
Mimi namuonea huruma mume wake tu.
423. AFANDE KAIFA:
Kwa sababu mwanamke sehemu yake ni jikoni na sio kwenye gereji akifanya kazi za wanaume.
424. SFX:
GHAFLA TUNASIKIA MZIKI UKISIKIKA KUTOKA NJE.
425. AFANDE KAIFA:
(KWA HASIRA) Aaah! Kelele zimeshaanza tena usiku wote huu!
426. FARIDA:
Zitakuwa zinatokea kwenye bar ya mama K.
427. AFANDE KAIFA:
Nilishamuonya aache hizo kelele la sivyo nitamuweka ndani lakini hasikii! We muache tu!
430. Sehemu:
Nje. Bar ya mama K. Usiku.
431. Utambulisho wa kipengele:
433. MAMA K:
(KWA SAUTI YA ULEVI, MBALI NA MIC) Jamani kuna kitu nataka niseme! Ebu zima ziki kwanza!
434. GRACE:
(KWA AIBU, KARIBU NA MIC) Anafanya nini tena?
435. DORIS:
(ANACHEKA, KARIBU NA MIC) Hata sijui! Mungu wangu! Amelewa sana!
436. MAMA K:
(ANAENDELEA, MBALI NA MIC) Nimesema, zima mziki!
437. GRACE:
Basi kila siku ndio hivi hivi! Baada ya hapo kazi yangu ni kuenda kumlaza kitandani baada ya kuzima!
438. MAMA K:
(ANAENDELEA, MBALI NA MIC) Nimesema zima mziki Dj! Zima mziki!
439. SFX:
MUSIC UNAZIMWA.
440. MAMA K:
Leo ni siku nzuri sana kwa sababu nimejaa sana!
441. SFX:
WATU WANASHANGILIA.
442. MAMA K:
Narudia tena: Leo nimelipwa pesa yangu ya vikoba! Kwa hiyo nataka kila mtu anywe anachotaka! Mimi nitalipa!
443. SFX:
WATU WANASHANGILIA KWA NGUVU ZAIDI.
444. GRACE:
(KWA HASIRA) Yaani naichukia sana tabia yake ya kulewa ovyo!
445. DORIS:
Mimi naona bora umwachie mama yako ale bata! Yeye anafurahia kama nini. (ANACHEKA) Ebu muone anavyocheza!
446. GRACE:
Ni rahisi wewe kusema hivyo kwa sababu sio mama y yako.Yaani nimeyachoka haya maisha we acha tu. Natamani ningekuwa na pesa za kuendelea na masomo. Siku moja nikija kupata kazi hatoendelea na biashara. Nachukia kumuona hivi kama nini!
447. DORIS:
Sidhani kama mama K atakubali kuiachia bar yake.
448. GRACE:
We subiri tu! Nitaongeza bidiii na kukazana na kilimo cha maharage ili nitengeneze pesa nyingi ambazo zitanisaidia kulipia ada ya shule.
449. DORIS:
(KWA KEJELI) Kwa hilo rafiki yangu unatakiwa ukomae kweli na biashara na sio kudhani kila anayekukaribisha katika ofisi yake anakutaka.
450. GRACE:
Ahaa! Naona biashara yako na Sigi itakuwa ilienda vizuri sana- kwa sababu huachi kumuongelea.
451. DORIS:
(KWA AIBU) Ehee! Iliikuwa poa sana Grace, na wiki ijayo amenihaidi atanipeleka sehemu (ANACHEKA) Sijui anataka kunipeleka wapi.
452. GRACE:
(ANACHEKA) Doris! Doris! Lakini sishangai kwa kweli!
453. DORIS:
Ona! Mama yako anapanda juu ya meza.
454. GRACE:
Nini tena? Mwisho ataumia huyu!
455. MAMA K:
(MBALI NA MIC) Kunywa bia! Nasema kunywa bia! Nitalipa mimi!
456. GRACE:
(ANASIMAMA) Acha nimpeleke akalale bwana.
457. SFX:
GRACE ANAMFUATA MAMA YAKE.
458. GRACE:
Mama ebu shuka basi kwenye hiyo meza, utaumia!
459. MAMA K:
(KWA SAUTI YA ULEVI) Ebu achana na mimi! Mimi bado najitambua! Au unafikiri nimelewa? Mimi sijalewa!
460. GRACE:
Sijasema umelewa, haya njoo basi; twende ukalale.
461. SFX:
GRACE ANAMSAIDIA MAMA YAKE KUSHUKA KUTOKA KWENYE MEZA.
462. MAMA K:
Ebu niache; Naweza kutembea mwenyewe. Mimi sijalewa!
463. GRACE:
Sawa. Angalia usidondoke hapo mbele kuna shimo!
464. MAMA K:
Mimi sijalewa. Nakuambia mimi sijalewa!
465. SFX:
GRACE NA MAMA K WANAISHIA NDANI YA NYUMBA YAO.
Acknowledgements
Imechangiwa na: Kheri Mkali, mwandishi wa muongozo, Dar es Salaam, Tanzania.
Imepitiwa na: Frederick Baijukya, mtaalamu wa kilimo na mratibu wa shirika la N2Africa Tanzania, Shirika la kilimo kwa nchi kitropiki (IITA), East Africa Hub, Dar es Salaam, Tanzania.
Kazi hii imewezeshwa kwa masaada wa Shirika la utafiti, lililopo Ottawa, Kanada (International Development Research Centre, Ottawa, Canada) www.idrc.ca, na msaada wa kifedha kutoka serikali ya Kanada, kupitia idara ya masuala ya kimataifa, (Global Affairs Canada) www.international.gc.ca.