Wanawake wanajiwezesha: Mchezo kuhusu wanawake kulima na kuuuza maharage — Part 4

Usawa wa kijinsiaUzalishaji wa mazao

Ujumbe kwa mtangazaji

Nukuu kwa Waandishi wa Habari
Wakina dada wanafanya wenyewe haya ni maigizo yenye sehemu-tano inayoongelea kikundi cha wanawake wanaokabiliana na chagamoto za kujikwamua na kupata maendeleo. Wanawake hawa ni wanachama wa vikundi vya kuweka na kukopa au vicoba nchini Tanzania, na wote wanalima maharage. Wanawake wanafanya kazi nyingi zaidi katika shughuli za uzalishaji wa maharage. Lakini kwasababu ya utamaduni wao wa kimajukumu katika jamii, wanaume wanafanya maamuzi yote baada ya mavuno, ikiwemo kuuza maharage na kumiliki kipato.

Baathi ya wahusika katika maigizo, ni mama Farida na Mama Mjuni, ambao wameonekana kuongoza katika kujaribu kufanya tofauti. Wanawahimiza wanawake kufanya kazi pamoja katika mashamba yao, na mwishowe kuzalisha maharage pamoja na kutafuta masoko kama kikundi.

Soma wahusika wakuu

Maigizo yanapinga hali mbaya, ikiwemo ugomvi baina ya mwanamke na mwanaume: unyanyasaji wa nyumbani katika familia moja, na juhudi za jamii kuwatumia wanawake vibaya na kujipatia faida kutokana na shughuli za kijangili.

Kuna utani kidogo katika maigizo, ingawa inaongelea mandhari nzito. Ukitengeneza maigizo na kikundi, hakikisha kuwa sehemu zenye mada nzito zinaoanishwa na sehemu zenye mada nyepesi za kufurahisha, za marafiki wakinongoneza matukio mazuri na wakicheka.

Kila kipengele kina urefu wa kama dakika 20-25, ikiwemo muziki wa kianzia na kumalizia. Kwasababu vipengele ni virefu, unaweza kupanga kurusha vipengele (kipande kimoja wapo katika Igizo) viwili au vitatu tu katika kipindi chako. Kwa mara nyingi vipande viwili au vitatu vinachukua dakiak 6-8.

Unaweza kupata mrejesho wa maigizo kwa kuandaa kipondi kitakacho pokea simu ambazo wasikilizaji watajadili baathi ya mambo waliyoyasikia katika maigizo, waalike wataalamu wa kike na wakiume kujadili mada. Majadiliano yanaweza kujumuisha:

  • jinsi jamii inavyogawanya kazi za kuzalisha na kuuza maharage, au mazao mengine yanayolimwa katika eneo, na jinsi gani mgawanyo huu umetenga mahitaji ya wanawake, na hata inaweza kuathiri familia;
  • unyanyasaji majumbani na utamaduni au tabia za ukimya inayoruhusu hii kuendelea; na
  • aina ya msaada wanaume wanayoweza kuwapatia wanawake ambao wanahangaika kujisaidia wao na famila zao.

Script

1.
Scene 1
2. Sehemu:
Nje. Nyumbani kwa Farida. Asubuhi.
3. Utambulisho wa kipengele:
Mlango unagongwa.

4. Wahusika:
Farida, Jenny.

5. SFX:
MLANGO UNAGONGWA KWA NGUVU.
6. FARIDA:
(AKIKARIBIA MIC) Nakuja!… Nakuja!
7. SFX:
FARIDA ANAFUNGUA MLANGO.
8. FARIDA:
(KWA MSHANGAO) Jenny! Hujaenda gereji leo?
9. SFX:
JENNY ANAINGIA NDANI.
10. JENNY:
(KWA HOFU) Nini kilitokea? Uko sawa? Amekufanya nini?
11. FARIDA:
Mbona sikuelewi….Unaongelea nini?
12. JENNY:
Namuongelea mumeo. Jana usiku amekuja kwangu anakutafuta, kwanza yupo?
13. FARIDA:
Hapana hayupo ameenda kazini.
14. JENNY:
Na watoto je? Wapo?
15. FARIDA:
Wapo shule. Kwani kuna nini?
16. JENNY:
Inabidi nikuulize wewe…uko salama?
17. FARIDA:
(ANACHEKA) Mimi mbona niko poa kabisa. (ANAJARIBU KUBADILISHA MAZUNGUMZO) Subiri nikupe chai; nimetoka kupika chai na viazi sasa hivi.
18. JENNY:
Sisikii njaa Farida. Wewe niambi nini kimetokea?
19. FARIDA:
Hakuna chochote kilichotokea!
20. JENNY:
Hakuna kilichotokea? Mumeo alikuwa kama amechanganyikiwa akikutafuta jana usiku. Kwanza ulikuwa wapi?
21. FARIDA:
Nilikuwa uwanjani pale uhuru.
22. JENNY:
Mimi najua hilo tamasha la Tunu liliisha mapema.
23. FARIDA:
Ni kweli liliisha mapema lakini kulikuwana kikao cha wanawake baada ya tamasha. Kwa hiyo ilibidi niwarudishe watoto nyumbani, nikapika, alafu nikarudi kwenye kikao.
24. JENNY:
Kwanini ulimdanganya sasa? Ukamwambia kwamba upo kwangu. Unajua ulitusababishia wote matatizo…Kwa sababu alifikiri nakutunzia siri.
25. FARIDA:
Jenny, unajua kabisa kwamba nisingeweza kumwambia kwamba naenda kwenye kikao…angekuwa radhi afe kuliko kuniachia nitoke usiku.
26. JENNY:
Ooh! Farida! Ni bora kumwambia ukweli tu.
27. FARIDA:
Nilijua ningewahi kurudi mapema kabla yay eye kurudi kutoka kazini.
28. JENNY:
Kwa hiyo ilikuwaje ulivyorudi?
29. FARIDA:
(AKIJARIBU KUMUAMINISHA) Hakunachochote lilichotokea…zaidi ya kubishana tu kama ilivyo kawaida kwa mume na mke.
30. JENNY:
(AKIONESHA KUTOMUAMINI) Alikupiga?
31. SFX:
UKIMYA.
32. JENNY:
Farida! Alikupiga?
33. FARIDA:
Sikiliza alikuwa amekasirika alafu…alafu…(ANAPATWA NA KIGUGUMIZI)
34. JENNY:
(ANAANZA KUONDOKA KWA HASIRA MABLA NA MIC) Basi! Nimechoka!
35. FARIDA:
(ANAJARIBU KUMSIMAMISHA) Jenny! Unaenda wapi sasa?
36. JENNY:
(KWA HASIRA) Naenda kumwambia ukweli kuhusu tabia yake ya kukupiga kila siku Farida! Imetosha kwa kwa kweli!
37. FARIDA:
Subiri! Subiri kwanza! Sidhani kama ni wazo zuri!
38. JENNY:
Hivi unajisikia kweli? Au ndio umeshatosheka kuwa zigo la mazoezi maisha yako yote?
39. FARIDA:
(KWA HASIRA) Sikiliza yameisha, sawa? Tulikuwa na tofauti zetu lakini tumeyamaliza!
40. JENNY:
(KWA KEJELI) Mmeyamaliza eeh? Kwa yeye kukupa kipigo? Ndio mlivyoyamaliza sio?
41. FARIDA:
Wewe mwenyewe umesema nisingemdanganya. (ANAJARIBU KUJIPA MOYO) Nisingedanganya. Hilo ndio kosa langu, ningejua ningemwambia ukweli tu. Wewe mwenyewe unajua jinsi alivyokuwa na wivu yule mwananume.
42. JENNY:
Na vipi kuhusu mara nyingine ukiacha jana?
43. SFX:
UKIMYA.
44. JENNY:
Farida, nimeshakushauri mara nyingi kwamba inabidi uwe makini sana, lakini mwisho wa siku ni uamuzi wako…Sema itabidi uwaze mwenyewe kwamba ni mfano gani unawaonesha watoto wako wa kike kwa kuwaonesha kwamba mwanaume anaweza akakufanyia vyovyote anavyotaka tu!
45. SFX:
JENNY ANAONDOKA NA KUFUNGA MLANGO.
46. CONTROL:
Jenny.

 

47.
Scene 2
48. Sehemu:
Nje. Barabarani. Asubuhi.
49. Utambulisho wa kipengele:
Kelele za magari na pikipiki.

50. Wahusika:
Grace, Mjuni, Adam, Alex.

51. ADAM:
Oya nirushie kiberiti hicho mwanangu!
52. SFX:
KIBERITI KINAWASHWA.
53. MJUNI:
(KWA SAUTI YA CHINI) Oya subiri! Usiwashe kwanza, Sista wako anakuja!
54. ALEX:
(KWA KUTOJALI) Aaah! Mwache aje! Kwani wewe unajali?
55. GRACE:
(AKIKARIBIA MIC) Mjuni, ni wewe?
56. ADAM:
(KWA UTANI) Hapana sio yeye!
57. SFX:
ADAM NA ALEX WANACHEKA.
58. ADAM:
(KWA MAIGIZO) Aaah! Dada Grace karbu sana! Unaelekea wapi asubuhi yote hii?
59. GRACE:
Ebu achana na mimi!
60. ALEX:
Vipi umepika?
61. GRACE:
Labda ndotoni. (ANAMGEUKIA MJUNI) Mjuni, ebu naomba tunongee kidogo.
62. ADAM:
Kwani kuna siri gani mpaka unashindwa kuongea nae hapa?
63. GRACE:
Kwanza hayawahusu!
64. MJUNI:
Oya nakuja sasa hivi.
65. ALEX:
Poa Mjuni, wewe usikonde wala nini!
66. SFX:
GRACE NA MJUNI WANASOGEAPEMBENI KUONGEA HUKU NYUMA YAO, ADAM NA ALEX WAKIGOMBANIA KIBERITI.
67. MJUNI:
Niambie Grace! Unaelekea wapi na hiyo ndoo?
68. GRACE:
Naelekea kisimani kuchota maji. Mjuni mbona haupo shule sasa hivi?
69. MJUNI:
Tuna mapumziko sasa hivi.
70. GRACE:
Asubuhi yote hii? Na hao je unafanya nao nini?
71. MJUNI:
Nani? Adam na Alex? Wako poa! Hawana noma!
72. GRACE:
Nisikilize vizuri Mjuni, nawajua wadogo zangu vizuri. Kazi yao ni kusababisha matatizo tu hapa kijijini. Watu wote wanawachukulia kama wahuni tu. Na wewe ndio unataka watu wakuchukulie hivyo?
73. MJUNI:
Mimi sijali watu wananifikiria vipi.
74. GRACE:
Kweli? Kwanza sigara umeanza kuvuta lini?
75. MJUNI:
Nani mimi? (ANACHEKA KIDOGO) Mbona navuta sigara muda mrefu sana.
76. GRACE:
Hapo unanidanganya. Sijawahi kukuona hata siku moja ukivuta sigara. Hivi itakuwaje wazazi wakipita hapa wakakuona eeh?
77. MJUNI:
(KWA KIBURI) Kwani wao wanajua nini?
78. GRACE:
Mjuni umekuwaje?
79. MJUNI:
Nani mimi? Mbona niko freshi tu!
80. GRACE:
Hapana umebadilika kwa kweli. Nakumbuka zamani ulivyokuwa ukipenda masomo na jinsi ulivyokuwana bidii.
81. SFX:
MJUNI ANACHEKA.
82. GRACE:
Nini kimekuchekesha?
83. MJUNI:
Nakumbuka hata wewe ulikuwa msongo sana. Tena ulikuwaga kiranja. Imekuwaje tena? Mbona haupo shule?
84. GRACE:
Sikuchagua kuachana na shule kwa hiari lakini ni kwa sababu ya matatizo. Nikipata pesa, nitarudi kumalizia masomo hyangu ya A level. Lakini wewe inabidi umalize shule Mjuni!
85. MJUNI:
Sawa, kila la kheri.
86. GRACE:
Kweli Mjuni namaanisha. Usije ukapotea kwa kukaa na hao wapuuzi.
87. MJUNI:
(KWA HASIRA) Aaah! Achana na mimi!
88. SFX:
MJUNI ANARUDI KWA ADAM NA ALEX NA KUMUACHA GRACE.
89. CONTROL:
Grace.

 

90.
Scene 3
91. Sehemu:
Nje. Shambani kwa Farida. Asubuhi.
92. Utambulisho wa kipengele:
Mazingira ya shambani.

93. Wahusika:
Farida, Mama Mjuni, Grace, Jenny, Mama K.

94. MAMA MJUNI:
Sawa wapendwa! Asanteni kwa kazi nzuri. Leo tumemaliza shambani kwa Farida. Kesho itakuwa zamu ya Grace na mama K.
95. MAMA K:
(ANARUKA JUU KWA FURAHA) Ndioo! Na kesho mje mapema!
96. SFX:
WANAWAKE WANACHEKA.
97. MAMA MJUNI:
Sawa jamani imetosha kwa leo. Tutaonana kesho!
98. GRACE:
Kwaheri Farida! Kwaheri mama Mjuni!
99. MAMA MJUNI, FARIDA:
Kwa heri Grace!
100. FARIDA:
Asanteni jamani na kwa heri!
101. WOTE:
Kwa heri!
102. MAMA MJUNI:
(KWA UCHOVU) Nimechoka hatari!
103. FARIDA:
Yaani we acha tu! Kama ningekuwa na uwezo ningepaa mpaka kitandani.
104. SFX:
WOTE WANACHEKA.
105. MAMA MJUNI:
Sikutegemea kama ingekuwa kazi hivi. Mgongo unauma kweli. Sijui ndio uzee huo!
106. FARIDA:
Pole mama Mjuni, lakini bora tunasaidiana sasa hivi!
107. MAMA MJUNI:
Kweli kabisa. Hili lilikuwa wazo zuri sana na limekuja muda muafaka. Sidhani kama ningeweza kufanya kazi zote hizi peke yangu.
108. FARIDA:
Ina maana ulikuwa unafanya kazi peke yako? Kwani Mjuni huwa akusaidiii?
109. MAMA MJUNI:
(ANATOA KICHEKO) Mjuni? Anisaidie kazi? Hiyo siku mbwa atapiga mswaki. Kwanza nitampata wapi.
110. FARIDA:
Basi afadhali sisi tupo kukusaidia.
111. MAMA MJUNI:
Na kweli, eh na mimi inabidi nianze safari ya kurudi nyumbani.
112. FARIDA:
(KWA GHAFLA) Si ukae kidogo?
113. MAMA MJUNI:
(KWA HOFU) Kwanini? Kwani kuna shida Farida?
114. FARIDA:
Kusema kweli, kuna kitu nataka tuongee.
115. MAMA MJUNI:
Nini?
116. SFX:
UKIMYA.
117. MAMA MJUNI:
Farida….kuna kitu kibaya kimetokea?
118. FARIDA:
Hapana, siwezi kusema ni mbaya kabisa…
119. MAMA MJUNI:
Unamaanisha nini?
120. FARIDA:
(KWA KUSITA) Nipo katika wakati mgumu na ninahitaji msaada wako.
121. MAMA MJUNI:
Sikiliza Farida, usijali. Unaweza ukaniambia chochote na nitafanya kila ambalo lipo ndani ya uwezo wangu kukusaidia.
122. FARIDA:
Mambo sio mazuri sasa hivi na mume wangu….
123. SFX:
FARIDA ANASHINDWA KUMALIZIA SENTENSI YAKE.
124. MAMA MJUNI:
Ndio…
125. FARIDA:
(KWA KUSITA) Alafu…Alafu
126. MAMA MJUNI:
Usijali Farida—Ongea tu.
127. FARIDA:
(GHAFLA) Nahitaji unikope pesa kiasi ili niwalipie ada ya shule watoto kwa sababu mume wangu hana kitu sasa hivi.
128. MAMA MJUNI:
Ndio hicho ulitaka kuniambia?
129. FARIDA:
Ndio…nahitaji msaada wako mama Mjuni. Nisipowalipia ada wanangu, hawataruhusiwa kufanya mtihani. Nakuahidi kukulipa pesa yako.
130. MAMA MJUNI:
Kwa kusema kweli, mimi binafsi sina pesa kwa sasa hivi. Lakini naweza kuongea na mume wangu akusaidie na hiyo ada ya watoto. Kwani ni shingapi?
131. FARIDA:
Laki nne.
132. MAMA MJUNI:
Sawa, usijali mpendwa.
133. FARIDA:
Oh. Asante sana Mama Mjuni!
134. MAMA MJUNI:
Usijali mpenzi.
135. CONTROL:
Mama Mjuni

 

136.
Scene 4
137. Sehemu:
Ndani. Mgahawa. Mchana.
138. Utambulisho wa kipengele:
Mazingira ya Mgahawa.

139. Wahusika:
Farida, Jenny, Stella.

140. SFX:
FARIDA, JENNY NA STELLA WANAFUNGUA MLANGO NA KUINGIA NDANI YA MGAHAWA.
141. JENNY:
Heeh! Hii sehemu nzuri!
142. FARIDA:
Nina uhakika tungepata sehemu nzuri tu ya kula kule kijijini badala ya kuja kote huku.
143. STELLA:
Farida ebu tulia jamani! Jenny mwambie Farida atulie!
144. FARIDA:
Mimi inabidi niwahi kurudi ujue…Siwezi kuchelewa.
145. STELLA:
Nakumbuka alikuwa anasema maneno hayo hayo tulivyokuwa kwenye gari uliyoiba kwenye gereji ya baba yako!
146. JENNY:
(ANACHEKA) Alafu ni kweli.
147. FARIDA:
(AKIKUMBUKA) Jamani naomba msinkumbushe. Niliogopa sana…Mungu wangu!
148. STELLA:
(ANACHEKA) Wote tuliogopa!
149. JENNY:
Sitaisahau ile siku! Sikuwahi kumuona mzee wangu amekasirika kiasi kile, na kilichomuudhi zaidi ni kwamba ilikuwa gari ya mteja wake.
150. SFX:
WOTE WANACHEKA.
151. FARIDA:
Wewe ulikuwa mjinga sana.
152. JENNY:
Na nyinyi mlikuwa wajinga kwa kunifuatisha.
153. SFX:
WOTE WANACHEKA.
154. STELLA:
Eh, jamani niliwamiss sana. Ni miaka mingi sana tangu tukae kama hivi.
155. JENNY, FARIDA:
Na sisi tulikumiss pia.
156. STELLA:
Kwani hamjafurahi tumekuja huku jamani?…tulihitaji mapumziko kidogo kutoka kwenye maisha yetu ya kila siku.
157. JENNY:
Ni kweli kabisa unavyosema.
158. FARIDA:
Mimi nilihitaji kupumzika sana jamani.
159. STELLA:
Kweli, hata mimi, hasa kwa jinsi mambo yanavyoenda kule kiwanadani.
160. JENNY:
Imekuwaje tena?
161. STELLA:
Oh! We acha tu mpendwa! Tumekuwa tukiingiza mzigo mdogo tofauti na kawaida.
162. FARIDA:
Vipi wauzaji wenu kama akina Sigi? Si nilimuona siku ile pale kiwandani nilivyokuja kukuona.
163. STELLA:
Safari hii hata Sigi amekuwa akituletea mzigo kidogo.
164. JENNY:
Itakuwa kwa sababu ya mavuno mabovu msimu huu. Unajua kijiji kizima kimekuwa kikilalamikia mavuno msimu huu.
165. FARIDA:
Ni kweli, sasa utafanyaje?
166. STELLA:
Sijui kwa kweli. Meneja wetu Mr. Patel ametuambia tujitahidi tutakavyoweza kuhakikisha tunapata mzigo wa kutosha. Tunahitaji kuongeza mzigo kutoka nje.
167. FARIDA:
(ANAROPOKA) Nina wazo! Kwanini kikundi chetu cha vikoba kisianze kuwauzia maharage kiwanda chenu?
168. JENNY:
(ANACHEKA) Farida, ebu acha utani. Wewe si unamuona Stella mwenzio hayuko kwenye utani.
169. FARIDA:
Hata mimi sitanii.
170. JENNY:
Hautanii eh? Haya ebu tuambie itawezekana vipi?
171. FARIDA:
Ebu angalia kama Sigi kwa mfano. Anawauzia maharage kiwanda chenu lakini hayo maharage yanalimwa kwa nguvu na jasho la wanawake wa hapa kijijini.
172. JENNY:
Lakini usisahau kwamba mara nyingi wanaume ndio huwa wanamuuzia maharage Sigi na sio wanawake.
173. STELLA:
Ni kweli.
174. FARIDA:
Ndio najua. Lakini kwanini wanawake tusiamue kupanda maharage yetu na kuuza kwenye kiwanda chenu?
175. JENNY:
Itawezekana vipi wakati asilimia kubwa ya wanawake wanapanda hayo maharage kwenye mashamba ya waume zao?
176. STELLA:
(AKIWAZA) Mmhh! Itabidi wanawake wote waungane kweli na wakubali kufanya kazi kwa pamoja ili muweze kufanikiwa.
177. STELLA:
Kwani hakuna yoyote kwenye vikoba ambaye ana shamba kubwa ambapo mnaweza kulima maharage?
178. FARIDA:
Ukiacha Mama Mjuni, sidhani kama kuna mtu mwingine. Yeye na mumewe mzee Ali wanamiliki shamba kubwa sana.
179. STELLA:
Je mnaweza kumshawishi ili mtumie shamba lake kwa ajili ya kulimia maharage?
180. JENNY:
Unahisi mama Mjuni atakubali?
181. FARIDA:
Anaweza kukubali…kama ni wazo zuri, mama Mjuni huwa hana shida.
182. JENNY:
Na vipi kuhusu mzee Ali?
183. FARIDA:
Anaweza kukubali; mzee Ali ni mtu muelewa sana. Lakini najiuliza je shamba lao linaweza kutosha kulima magunia yote hayo ya maharage?
184. JENNY:
Kwani hapo kiwandani kwenu huwa mnachukua mzigo kiasi gani?
185. STELLA:
Kusema kweli, kwa kila msimu wa mavuno huwa tunaingiza kama gunia elfu moja hivi.
186. JENNY:
Heeeh! Hayo ni mengi!
187. FARIDA:
Kwa namba ya wanachama kwenye vikoba, hatuwezi kuzalisha hata nusu ya hayo magunia elfu moja.
188. STELLA:
(KWA SHAUKU) Lakini sisi hatuhitaji mzalishe hata nusu ya hayo magunia elfu moja. Tayari tunao watu wengi wanaotuuzia, lakini tunaweza kukubaliana labda mkatuletea kati ya gunia tisini mpaka gunia mia.
189. FARIDA:
Ndio, hapo sio mbaya sana. Nahisi tunaweza kuzalisha kiasi hicho. Kwani Jenny unaonaje?
190. JENNY:
(BADO AKIWA NA SHAKA) Sijui Farida, ni kazi ngumu kuzalisha kiasi chote hicho. Alafu pia tusisahau bado hatujaongea na mama Mjuni kuhusu kutumia shamba lake kulimia maharage.
191. STELLA:
Ni kweli, nahisi ingekuwa vizuri kama mtaongea na mama Mjuni kwanza.
192. CONTROL:
Farida

 

193.
Scene 5
194. Sehemu:
Nje. Shambani kwa Mama Mjuni. Mchana.
195. Utambulisho wa kipengele:
Mazingira ya shambani.

196. Wahusika:
Mama Mjuni, Farida, Mama K, Grace, Doris, Monica, Mama Juma, Lydia.

197. SFX:
WANAWAKE WANABISHANA.
198. MAMA MJUNI:
(AKIJARIBU KUWATULIZA) Jamani naomba tusikilizane! Naomba tusikilizane!
199. SFX:
KELELE ZINATULIA.
200. MAMA MJUNI:
Wapendwa wanawake wenzangu, tunaweza kutofautiana lakini naomba tuheshimu maoni ya wengine. Ndio mama Juma unasemaje?
201. MAMA JUMA:
Hapa nilipo nashindwa hata kulima maharage ya kutosha kwa mwaka mzima kwa familia yangu, sasa ebu niambie nitawezaje kuzalisha maharage ya kutosha ambayo nitayauza kiwandani?
202. FARIDA:
Nelewa wasi wasi wako mama Juma lakini kama tutafanya kazi kwa pamoja, tunaweza kufanikisha.
203. MAMA K:
Kwani tunahitaji kuzalisha kiasi gani?
204. JENNY:
Hapo kiwandani huwa wanaingiza gunia elfu moja kwa msimu. Lakini sisi tunatakiwa kuzalisha gunia 90 mpaka gunia 100.
205. SFX:
MIGUNO YA WANAWAKE.
206. MAMA K:
Hayo ni magunia mengi sana!
207. MONICA:
Ndio! Nakubaliana na Mama K.
208. FARIDA:
Hakuna kinachoshindikana chini ya jua! Inawezekana kama tukijitahidi.
209. JENNY:
Mimi nakubaliana na Farida. Nadhani tutanufaika sana zaidi ya kunufaisha watu wanyanyasaji kama Sigi ambaye anahisi anaweza kuwafanyia wanawake kama anavyojisikia.
210. GRACE:
Ni kweli. Mimi mwenyewe ni shahidi. Na nimepitia unyanyasaji mkubwa kwa Sigi, kisa tu nilitaka nimuuzie maharage yangu.
211. SFX:
KELELE ZA HASIRA.
212. MAMA JUMA:
(KWA HASIRA) Mwanaume amekosa haya yule!
213. LYDIA:
Haoni hata aibu mwanaume mzima! Ndio mwanzo na mwisho kumuuzia maharage!
214. MONICA:
(ANAINGILIA KATI) Hiyo ni rahisi kwa nyie wengine hapa. Na sisi je ambao hatuna nguvuya kuamua tutauza wapi kwa sababu waume zetu ndio huwa wanaamua. Tuatafanyaje?
215. FARIDA:
Naelewa mpendwa. Hata mimi ni kama wewe kwa sababu mume wangu ndiye anayeamua tumuuzie nani maharage kila baada ya mavuno. Na ndio maana tunataka tuongee na mama Mjuni kama inawezekana, tutumie shamba lake kulima maharage.
216. SFX:
GHAFLA PANAKUWA KIMYA.
217. MAMA JUMA:
Unadhani itawezekana, Mama Mjuni?
218. MAMA MJUNI:
Ndio inawezekana lakini itabidi niongee kwanza na Mzee Ali.
219. LYDIA:
(ANAINGILIA KATI) Lakini nina wasi wasi itakuwa kazi sana kuzalisha maharage na mazao mengine kwa ajili ya familiza zetu na hapo hapo kuzalisha maharage kwa ajili ya kuuza kiwandani. Na bado tukizijali familia zetu.
220. JENNY:
Na ndio maana tunafanya kazi kwa pamoja, si ndio? Hili wazo limekuja wakati mzuri kwa sababu inabidi tushirikiane kwa pamoja.
221. DORIS:
Lakini magunia tisini mpaka magunia mia sio kazi ndogo.
222. MAM MJUNI:
Hakuna mtu aliyesema ni kazi rahisi. Mafanikio hayaji kirahi rahisi tu. Lakini kama kweli tunayo nia na tukifanya kazi kwa pamoja basi tunaweza.
223. FARIDA:
Mimi nakubaliana na Mama Mjuni! Niko tayari kufanya kazi na nyie wote…Nani mwingine hyuko tayari?
224. JENNY:
Niko tayari.
225. MONICA:
Hata mimi niko tayari!
226. LYDIA:
Mimi pia.
227. MAMA JUMA:
Na mimi pia.
228. GRACE:
Hata mimi niko tayari.
229. MAMA MJUNI:
Mimi pia…Vipi mama K unasemaje?
230. SFX:
MAMA K ANASITA KIDOGO.
231. MAMA K:
Aaah! Bwana eeh! Na mimi nipo tayari!
232. SFX:
WANAWAKE WOTE WANASHANGILIA.
233. CONTROL:
Mama Mjuni

 

234.
Scene 6
235. Sehemu:
Nje. Nyumbani kwa Mama Mjuni. Usiku.
236. Utambulisho wa kipengele:
Mazingira ya kwa Mama Mjuni.

237. Wahusika:
Mama Mjuni, Mzee Ali, Mjuni.

238. MZEE ALI:
(HUKU AKITAFUNA CHAKULA) Mama Mjuni huyu samaki wa leo umemtengeneza kama ninavyompenda. Ndimu hujaweka nyingi sana- kiasi tu.
239. MAMA MJUNI:
Na mimi nimefurahi kwamba umempenda. Subiri nikuongeze.
240. MZEE ALI:
Hapana anatosha; kwanza hapa nilipo nimeshashiba.
241. MAMA MJUNI:
Una uhakika?
242. MZEE ALI:
Ndio. Mbona hujaniambia siku yako ilivyoenda leo?
243. MAMA MJUNI:
(KWA SHAUKU) Siku ya leo ilikuwa nzuri sana!
244. MZEE ALI:
Oh! Inaonekana una furaha sana leo!
245. MAMA MJUNI:
Yaani huwezi kuamini! Leo kwenye kikao tumeamua tuanze biashara ya kuzalisha maharage na kuuza kiwandani. Yaani nimefurahi sana!
246. MZEE ALI:
Kweli? Nani amebuni hilo wazo?
247. MAMA MJUNI:
(KWA FURAHA) Farida!
248. MZEE ALI:
Hilo ni wazo zuri sana. Ametumia akili sana.
249. MAMA MJUNI:
Ndio, ana akili sana yule binti. Saa nyingine namuonea huruma sana na maisha yake na yule mwanaume.
250. MZEE ALI:
(ANABADILISHA MAZUNGUMZO) Ni wazo zuri lakini bora niwe muwazi kabisa…Inaonekana itakuwa kazi ngumu sana. Haitakuwa rahisi.
251. MAMA MJUNI:
Hakuna mtu anayesema itakuwa rahisi na ndio maana tutahitaji kila aina ya msaada ili kufanikisha.
252. MZEE ALI:
Ndio. Mimi nipo kama mtahitaji msaada wa aina yoyote.
253. MAMA MJUNI:
Wnawake wameniomba nikuulize kama wanaweza kutumia shamba letu kulima maharage.
254. MZEE ALI:
Unahisi ni wazo zuri?
255. MAMA MJUNI:
Kwanini? Mwaka jana tulipanda mazao lakini mwaka bado hatujaamua tutapanda nini kwa hiyo lipo tu. Mimi naona si vibaya kama tukilitumia.
256. MZEE ALI:
Kama mmekubaliana basi unaweza ukawaambia kwamba hakuna shida.
257. MAMA MJUNI:
Asante mpenzi. Kabla sijasahau, Naomba pesa kidogo nimpe Farida. Ningeweza kumpa mimi mwenyewe lakini sina kitu sasa hivi.
258. MZEE ALI:
Anahitaji shingapi?
259. MAMA MJUNI:
Laki nne.
260. MZEE ALI:
Mbona nyingi hivyo? Au unaonaje?
261. MAMA MJUNI:
Anahitaji kuwalipia ada wanae.
262. MZEE ALI:
Sawa, nikumbushe asubuhi nikupe hiyo pesa.
263. MAMA MJUNI:
Amesema atatulipa pindi tu mumewe atakapopata pesa.
264. MZEE ALI:
Sawa hakuna shida!
265. MAMA MJUNI:
Alafu na kitu kingine mume wangu, nilikuwa nafikiria kwamba ungeweza kuongea na wanaume wenzio waweze kuwapa msaada wa hali na mali wake zao kipindi hiki ambacho tuataanza huu mradi.
266. MZEE ALI:
Mama Mjuni unajua kabisa jinsi wanaume wa kijiji hiki walivyo vichwa ngumu. Haitakuwa kazi rahisi!
267. MAMA MJUNI:
Najua lakini wewe ni mwenyekiti wa serikali za mtaa hapa kijijini, hawa wanaume wanakuheshimu sana. Najua watakusikiliza tu.
268. MZEE ALI:
Nitajitahidi kuongea nao.
269. MAMA MJUNI:
MLANGO UNAFUNGULIWA NA MJUNI ANAINGIA NDANI. ANAWASALIMIA WAZAZI WAKE NA KUANZA KUELEKEA CHUMBANI KWAKE.
270. MJUNI:
Shikamoo!
271. MZEE ALI:
Marahaba!
272. MAMA MJUNI:
Mjuni! Huu ndio muda unaorudi nyumbani kutoka shuleni?….Mimi nilijua tayari umerudi?
273. MZEE ALI:
Hata mimi nilijua hivyo.
274. MAMA MJUNI:
Si naongea na wewe! Huu ndio muda unaorudi nyumbani?
275. SFX:
MJUNI ANABAKI KIMYA.
276. MAMA MJUNI:
Oh! Umekuwa bubu ghafla eh? Saa ngapi saa hizi?
277. MJUNI:
(KWA SAUTI YA CHINI) Saa mbili usiku.
278. MAMA MJUNI:
Ulikuwa wapi?
279. MJUNI:
Nilikuwa na rafiki zangu.
280. MAMA MJUNI:
Marafiki? Marafiki wanaokuacha ukae nje mpaka usiku huu? Hao ni marafiki gani?
281. MZEE ALI:
Hao ni marafiki zako wa shuleni?
282. MJUNI:
Ndio.
283. MAMA MJUNI:
La kukutokea lingekutokea huko nje ingekuwaje?
284. MJUNI:
Mimi nimechoka mnavyonifanya kama mtoto mdogo.
285. MAMA MJUNI:
Nini?
286. MZEE ALI:
(KWA UKALI) Wewe Mjuni! Usimjibu mama yako hivyo!
287. MJUNI:
(KWA HASIRA) Na wewe nimechoka unavyojifanya baba yangu!
288. SFX:
MJUNI ANAONDOKA NA KUINGIA CHUMBANI KWAKE NA KUFUNGA MLANGO KWA HASIRA.
289. MAMA MJUNI:
(AKILIA) Sijui nifanyaje! Siku zinavyozidi kuenda ndio anazidi kuharibikiwa.
290. MZEE ALI:
(ANAM’BEMBELEZA) Usijali, kila kitu kitakuwa sawa.
291. CONTROL:
Mama Mjuni

 

292.
Scene 7
293. Sehemu:
Ndani. Shambani kwa mama Mjuni. Asubuhi.
294. Utambulisho wa kipengele:
Mazingira ya shambani kwa Mama Mjuni.

295. Wahusika:
Farida, Mama Mjuni, Jenny, Grace, Mama K, Stella.

296. MAMA MJUNI:
Karibuni wanawake wenzangu kwenye shamba lenu jipya.
297. SFX:
MISHANGAO YA WANAWAKE.
298. GRACE:
(KWA MSHAGANO) Eh! Ni kubwa sana!
299. JENNY:
Kabisa! Sio kama nilivyokuwa nikifikiria.
300. MAMA K:
Samahani mama Mjuni, hili shamba lina ukubwa gani?
301. MAMA MJUNI:
Lina ukubwa wa heka kumi na moja!
302. MAMA K:
(ANAGUNA) Hiyo ni kazi sasa!
303. MAMA MJUNI:
Ndio! Itabidi tukaze kamba za viatu veytu kwa sababu hii safari iliyo mbele yetu si rahisi.
304. JENNY:
Kuna majani kibao!
305. FARIDA:
Ndio. Na kazi yetu ya kwanza ni kukata haya majani yote kwa sababu kama mnavyoona, sasa hivi ni kichaka tu.
306. MAMA MJUNI:
Ndio. Basi tuwahi kesho asubuhi na mapema ili tuanze hiyo kazi. Lakini kabla sijaendelea najua mmegundua kuna sura mpya, naomba nimkaribishe mwanachama wetu mpya…dada Stella.
307. SFX:
WANAWAKE WANASHANGILIA KWA MAKOFI NA VIGEREGERE.
308. MAMA MJUNI:
Stella anafanya kazi kwenye kiwanda ambacho tutakuwa tunawauzia maharage.
309. SFX:
WANAWAKE WANASHANGILIA TENA KWA MARA NYINGINE.
310. MAMA MJUNI:
Basi acha nimkaribishe ili aongee maneno machache.
311. STELLA:
Asanteni sana kwa ukarimu wenu. Nina furaha sana kuwa hapa kwenye familia yangu mpya. Nataka niseme kwamba niliguswa sana na uamuzi wenu wa kujiendeleza na nikasema lazima nijiunge na kikundi hiki cha wanawake majasiri kwa sababu nilihamasishwa sana. Niko tayari kufanya kazi na nyie wote.
312. MAMA K:
(ANAMKATISHA) Samahani, lakini una cheo gani hapo kiwandani?
313. FARIDA:
Heeh! Mama K, si umuache aongee jamani?
314. MAMA K:
Nadhani wote tuna haki ya kujua.
315. STELLA:
(ANACHEKA) Hapana usijali. Mimi ni msimamizi wa operesheni zote za maharage.
316. MAMA K:
Kwa hiyo wewe ni kama bosi?
317. STELLA:
(ANACHEKA) Ndio, unaweza kusema mimi ni kama bosi.
318. MAMA K:
(ANASHANGILIA) Weweee! Tupo na bosi wa kiwandani!
319. SFX:
KILA MTU ANACHEKA.
320. MAMA K:
Sawa, naomba nikuulize tena. Utatupa tenda nzuri?
321. STELLA:
Jamani itabidi niwe muwazi na nyinyi….Kwa sababu tu nimejiunga na kikundi hiki cha vikoba, haina maana kwamba nitapendelea kikundi hiki. Nitafanya kazi yangu kwa bidii na ninategemea na nyie mfanye kazi yenu kwa bidii. Lengo ni kuzalisha magunia 90 mpaka 100 ya maharage. Nadhani kama tukiwekeza akili zetu na mioyo yetu tutafanikiwa tu. Namchukulia kila mtu hapa kama dada yangu na nasubirikwa hamu kufanya kazi nanyi wote.
322. SFX:
WANAWAKE WANAMPIGIA MAKOFI NA KUMSHANGILIA.
323. MAMA MJUNI:
Na kwa maneno hayo mazuri, sina cha kuongezea, bali nawaomba wote muwe hapa ili tuanze kazi.
324. CONTROL:
Mama Mjuni

 

325.
Scene 8
326. Sehemu:
Ndani. Duka la nguo. Mchana.
327. Utambulisho wa kipengele:
Mazingira ya dukani.

328. Wahusika:
Doris, Sigi.

329. DORIS:
(KWA SHAUKU) Mpenzi! Ebu angalia hili gauni! Zuri eh?
330. SIGI:
(KWA MBWEMBWE) Aah! Zuri sana! Lichukue, nataka uchukue nguo yoyote ndani ya duka hili kwa sababu nitalipia!
331. DORIS:
Oh! Asante sana mpenzi wangu! Ndio maana nakupenda!
332. SIGI:
Nakupenda pia mpenzi wangu, ebu nichumu!
333. SFX:
DORIS ANAMBUSU SIGI.
334. DORIS:
Unajua Sigi….nina bahati sana kuwa na wewe (KWA KUJIDAI) Na ndio maana wasichana wengine kama akina Grace wananionea wivu sana.
335. SIGI:
Wewe hata wasikuumize kichwa. Wewe ndio umekamata moyo wangu.
336. DORIS:
Grace ananionea wivu sana. Hivi unajua anavaaa mitumba tu? Nina uhakika hajawahi kuingia kwenye duka kama hili.
337. SIGI:
Anaonekana amezoea kuvaa mitumba.
338. SFX:
DORIS NA SIGI WANACHEKA.
339. DORIS:
Angalia hili! Litanipendeza eh?
340. SIGI:
Litakupendeza sana!
341. DORIS:
(AKITEMBEA KWA MADOIDO NDANI YA GAUNI LAKE) Kama namuona Grace anavyoniangalia kwa wivu nitakavyoingia kwenye kikao cha vikoba.
342. SIGI:
Eh! Utawamaliza na hilo gauni, mpenzi!
343. DORIS:
(KWA MAJIGAMBO) Ndio maanake! Yaani hujui tu nilivyomchoka Grace na kuiona sura yake kwenye vikao. Lakini sina cha kufanya, na hivi sasa tumeanza mradi wa kuuza maharage kiwandani. (ANAGUNA)
344. SIGI:
(KWA MSHANGAO) Nani? Nyie? Una maana gani mnauza maharage kiwandani?
345. DORIS:
Oh! Hivi sikukuambia? Tuna mpango wa kuanza kuuza maharage kiwandani.
346. SIGI:
Nani?
347. DORIS:
Si kikundi chetu cha vikoba.
348. SIGI:
(AKIWA HAAMINI) Unataka kuniambia wanawake wote wa vikoba wana mpango wa kuuza maharage kiwandani?
349. DORIS:
Ndio.
350. SIGI:
(ANACHEKA) Haiwezekani! Kikundi chenu cha vikoba?! Hamuwezi, mtapata wapi hiyo pesa ya kufanya hivyo?
351. DORIS:
Kumbe wewe ndio hujui…sasa mbona mambo yamechachamaa. Na tumeshaanza kulima hayo maharage shambani kwa mama Mjuni.
352. SIGI:
UKIMYA.
353. DORIS:
Kuna nini mpenzi? Uko sawa? Mbona umekuwa kimya ghafla?
354. SIGI:
Hapana hakuna kitu…Ebu tuondoke mara moja.
355. DORIS:
Una maana gani? Na wakati mimi ndio kwanza nimeanza kuangalia nguo.
356. SIGI:
(KWA UKALI) Sikiliza sitaki kubishana na wewe – ebu twende! (ANAMKAMATA MKONO)
357. DORIS:
(ANALIA KWA MAUMIVU) Aaah! Unaiumiza mkono wangu. Naomba uniachie.
358. SIGI:
Sawa twende.
359. SFX:
SIGI NA DORIS WANATOKA DUKANI.
360. DORIS:
Mbona unanifanyia hivi jamani?
361. SIGI:
Unafikiri sielewi unafanya nini?
362. DORIS:
(AKIONEKANA KUCHANGANYIKIWA) Mbona sikuelewi? Una maana gani?
363. SIGI:
Wewe na hao wenzio mna mpango wa kuniibia biashara sio.
364. DORIS:
Nini? Unajua siwezi hata siku moja kukufanyia hivyo mpenzi wangu!
365. SIGI:
Wamekutuma ili uje kunichunguza vizuri ili mje kuniibia vizuri sio?
366. DORIS:
Mpenzi unajua hayo yote sio kweli. Kama ningekuwa na nia mbaya kweli, je ningekwambia kama tumeanza biashara?
367. SIGI:
Sikiliza, sitaki kusikia huo upuuzi. (ANACHEKA) Yaani siamini nimekuwa nikitumia pesa zangu juu yako wakati wote huo wakati unapanga mipango na wale vikaragosi wenzio.
368. DORIS:
(AKIOMBA) Sigi, unajua nakupenda mpenzi wangu na siwezi hata siku moja kukufanyia hivyo.
369. SIGI:
(KWA HASIRA) Sikiliza, usinishike sawa? Nakuanzia sasa uniache na wala sitaki kukuona tena!
370. DORIS:
(AKILIA) Sigi unaenda wapi?
371. SFX:
SIGI ANAINGIA KWENYE GARI YAKE NA KUONDOKA.
372. DORIS:
(AKILIA KWA UCHUNGU) Sigi, subiri kwanza! Usiende!
373. CONTROL:
Doris.

 

374.
Scene 9
375. Sehemu:
Nje. Shambani. Usiku.
376. Utambulisho wa kipengele:
Mazingira ya shambani.

377. Wahusika:
Mama Mjuni, Farida, Grace, Doris.

378. MAMA MJUNI:
Wapendwa wanawake wenzangu, tumekutana hapa leo ili tuanze kazi rasmi. Lakini kabla hatujaanza, nataka muelewe ya kwamba sisi wote ni kama familia hapa. Kwa hiyo inabidi tumalize tofauti ili tuweze kufanye kazi kama timu moja. Kwa hiyo ningependa kuomba yoyote yule mwenye ugomvi na mtu, tukate mzizi wa fitina ili tuanze kazi.
379. SFX:
UKIMYA.
380. MAMA MJUNI:
Kama una ugomvi na mtu yoyote yule ni bora kuumaliza sasa. Kwa sababu hatutaki ugomvi uharibu kazi yetu.
381. SFX:
MINONG’ONO YA WANAWAKE.
382. SFX:
KILIO KINASIKIKA.
383. MAMA MJUNI:
Kumetokea nini tena?
384. FARIDA:
Ni Doris.
385. MAMA MJUNI:
Kimemtokea nini?
386. FARIDA:
Hata hatujui.
387. SFX:
DORIS ANAENDELEA KULIA HUKU MINONG’ONO YA WANAWAKE IKIENNDELEA.
388. MAMA MJUNI:
Doris una nini?
389. DORIS:
(AKILIA) Mimi ni mjinga sana Mama Mjuni.
390. MAMA MJUNI:
Kwanini unasema hivyo? Wewe sio mjinga Doris.
391. DORIS:
Ndio mimi ni mjinga. Nimesababisha mpaka Sigi atagombanishe mimi na rafiki yangu Grace. (ANAENDELEA KULIA)
392. MAMA MJUNI:
Oh! Jamani! Grace, tafadhali ebu njoo mara moja.
393. SFX:
GRACE ANASOGEA MBELE WALIPO DORIS NA MAMA MJUNI.
394. MAMA MJUNI:
Grace, nadhani Doris kuna kitu anataka kukuambia.
395. DORIS:
Grace anaomba unisamehe kwa jinsi nilivyokufanyia.
396. GRACE:
Usijali nimekusamehe kipenzi!
397. DORIS:
Siamini kama nilikuwa kipofu kiasi kile nikashindwa kugundua jinsi Sigi alivyokuwa kinitumia muda wote. Kanitumia na kunitupa kama tambara bovu.
398. GRACE:
Usijali kipenzi…wala usijali. Nimefurahi kwamba umetambua thamani yako kwa sababu hicho ndio kitu muhimu zaidi. Sigi astahili kuwa na msichana kama wewe.
399. SFX:
GRACE NA DORIS WANAKUMBATIANA HUKU WANAWAKE WENGINE WAKIWASHANGILIA.
400. MAMA MJUNI:
Jamani si inapendeza au sio?
401. WOTE:
Ndio.
402. GRACE:
Doris, nakubali nimekusamehe lakini lazima nikuuliza…hivyo viatu vipi? Utafanya vipi kazi?
403. DORIS:
(KWA SHAUKU) Vipi umevipenda?
404. GRACE:
Ndio, lakini sidhani kama vinafaa kufanyia kazi.
405. DORIS:
Kwanini? Mwananamke anatakiwa kupendeza babu, hata wakati wa kazi.
406. SFX:
WOTE WANACHEKA.
407. CONTROL:
Doris

 

408.
Scene 10
409. Sehemu:
Nje. Kijiweni/ Shambani kwa mama Mjuni. Jioni.
410. Utambulisho wa kipengele:
Mziki unasikika.

411. Wahusika:
Sigi, Adam, Alex, Mjuni.

412. SFX:
MZIKI KWENYE REDIO.
413. ADAM:
(AKIIMBA KUFUATISHA MZIKI) Kababaaaye! Kababaaye! (ANAACHA KUIMBA NA KUONGEA) Oya Chini Beez ni noma mwanangu!
414. ALEX:
Ndio maanake! Anajua sana! Anajua sana!
415. MJUNI:
Nakubali sana ngoma yake mpya pia.
416. SFX:
GARI INAWASILI.
417. SIGI:
Aaah, madogo! Mnafanya nini?
418. ALEX:
(KWA UKALI) Oya hakuna madogo hapa sawa?
419. ADAM:
We unaona madogo hapa?
420. SIGI:
(ANACHEKA) Sawa, nilikuwa nawazingua tu. Vipi mnataka tukatembee kidogo.
421. ADAM:
Tukafanye nini wakati tunakula vitu hapa.
422. SFX:
ALEX NA MJUNI WANACHEKA.
423. SIGI:
Sawa, kwa hiyo kipi bora? Kula vitu au kutengeneza pesa?
424. ALEX:
(KWA SHAUKU) Sasa hayo ndio mambo.
425. ADAM:
Tunaenda wapi?
426. SIGI:
(BILA PAPARA) Sikiliza – punguza maswali. Kama unataka kujua tunaenda wapi, wewe twende.
427. SFX:
ADAM, ALEX NA MJUNI WANAPANDA KWENYE GARI.
428. SIGI:
(KWA UKALI) Ebu subiri kwanza! Huyu dogo ni nani?
429. ALEX:
Ah! Huyo Mjuni! Mshikaji wetu!
430. SIGI:
Anafanya nini kwenye gari yangu?
431. ADAM:
Usijali Sigi! Mjuni hana noma! Yuko na sisi!
432. SIGI:
(KWA SAUTI) Kwa hiyo kama yupo na nyie? Mimi sitaki watoto wasiojua kazi ambao watakimbia mambo yakiwa magumu. Kwanza anaonekana tu mtoto wa mama.
433. MJUNI:
(KWA HASIRA) Mimi sio mtoto wa mama.
434. SIGI:
(KWA UKALI) Kwani nani kakuuliza?
435. ADAM:
(KWA MJUNI) Sikiliza Mjuni, we kaa kimya tu. (ANAMGEUKIA SIGI) Oya Sigi, unweza ukamuamini Mjuni hana noma. Yuko poa sana.
436. SIGI:
(KWA SAUTI KALI) Ndio akaze buti. Hii kazi ni ya Muhimu sana.
437. SIGI:
SIGI ANAWASHA GARI NA WANAONDOKA.
438.
PUNGUZA SAUTI HATUA KWA HATUA
439.
ONGEZA SAUTI HATUA KWA HATUA
440. SFX:
GARI INAKARIBIA MIC. GARI INAZIMWA.
441. SIGI:
Haya tumefika.
442. ALEX:
Kwa hiyo tunafanya nini hapa?
443. SIGI:
Acha ujinga! Kwani wewe unaona nini mbele yako?
444. ALEX:
(ANATOA KICHEKOCHA UOGA) Naona…naona shamba.
445. SIGI:
Sio shamba tu, bali shamba la wanawake wa vikoba.
446. ADAM:
Kwani unataka tufanye nini hapa?
447. SIGI:
(KWA MAJIGAMBO) Nataka msababishe uharibifu!
448. ADAM:
(ANACHEKA KIDOGO) Unatania au?
449. MJUNI:
(KWA HISIA) Kwanini unataka tuharibu shamba lao?
450. SIGI:
(KWA UKALI) Kaa kimya wewe! Unajua huyu mshikaji wenu ana kiherehere sana! (ANAMGEUKIA MJUNI) Nimeshakwambia unaongea endapo tu nikikupa ruhusa.
451. ALEX:
(AKIMTULIZA SIGI) Sawa Sigi amekuelewa.
(ANAMGEUKIA MJUNI) Oya Mjuni, fanya kama unavyoambiwa mwanangu.
452. ADAM:
Tunatakiwa kufanya nini kingine?
453. SIGI:
(KWA SAUTI YA UKALI) Nimeshakwambia! Nataka mliharibu kabisa ili shamba na mazao yake.
454. ADAM:
Na vipi kuhusu malipo?
455. SIGI:
Nyie fanyeni kama nilivyowaambia. Malipo mtapata mkimaliza kazi.
456. ALEX:
Sawa.
457. SIGI:
Sawa tumemaliza hapa. Haya shukeni.
458. SFX:
SIGI, ADAM NA ALEX WANASHUKA KUTOKA KWENYE GARI NA SIGI ANAONDOKA MARA MOJA.
459. MJUNI:
Huyo jamaa wenu vipi? Mbona anazingua sana.
460. ADAM:
Kweli mtu wangu! Mwenyewe nimemchoka kinoma! (ANAMGEUKIA ALEX) Oya kwani nilikuambiaje? Inabidi tuanze kupiga michongo yetu mwanangu!
461. ALEX:
Hii kazi yetu ya mwisho! Baada ya hapa, tunaachana nae. Kwa hiyo tumalizane nae tu.
462. ADAM:
Hapana, mimi nina wazo zuri zaidi.
463. MJUNI:
(KWA HOFU) Una maana gani?
464. ALEX:
Mbona sikuelewi?
465. ADAM:
Nyie nifuateni mimi.
466. CONTROL:
Sigi

Acknowledgements

Imechangiwa na: Kheri Mkali, mwandishi wa muongozo, Dar es Salaam, Tanzania.
Imepitiwa na: Frederick Baijukya, mtaalamu wa kilimo na mratibu wa shirika la N2Africa Tanzania, Shirika la kilimo kwa nchi kitropiki (IITA), East Africa Hub, Dar es Salaam, Tanzania.

Kazi hii imewezeshwa kwa masaada wa Shirika la utafiti, lililopo Ottawa, Kanada (International Development Research Centre, Ottawa, Canada) www.idrc.ca, na msaada wa kifedha kutoka serikali ya Kanada, kupitia idara ya masuala ya kimataifa, (Global Affairs Canada) www.international.gc.ca.
gaclogoidrc