Wanawake wanajiwezesha: Mchezo kuhusu wanawake kulima na kuuuza maharage — Part 3

Usawa wa kijinsiaUzalishaji wa mazao

Ujumbe kwa mtangazaji

Nukuu kwa Waandishi wa Habari
Wakina dada wanafanya wenyewe haya ni maigizo yenye sehemu-tano inayoongelea kikundi cha wanawake wanaokabiliana na chagamoto za kujikwamua na kupata maendeleo. Wanawake hawa ni wanachama wa vikundi vya kuweka na kukopa au vicoba nchini Tanzania, na wote wanalima maharage. Wanawake wanafanya kazi nyingi zaidi katika shughuli za uzalishaji wa maharage. Lakini kwasababu ya utamaduni wao wa kimajukumu katika jamii, wanaume wanafanya maamuzi yote baada ya mavuno, ikiwemo kuuza maharage na kumiliki kipato.

Baathi ya wahusika katika maigizo, ni mama Farida na Mama Mjuni, ambao wameonekana kuongoza katika kujaribu kufanya tofauti. Wanawahimiza wanawake kufanya kazi pamoja katika mashamba yao, na mwishowe kuzalisha maharage pamoja na kutafuta masoko kama kikundi.

Soma wahusika wakuu

Maigizo yanapinga hali mbaya, ikiwemo ugomvi baina ya mwanamke na mwanaume: unyanyasaji wa nyumbani katika familia moja, na juhudi za jamii kuwatumia wanawake vibaya na kujipatia faida kutokana na shughuli za kijangili.

Kuna utani kidogo katika maigizo, ingawa inaongelea mandhari nzito. Ukitengeneza maigizo na kikundi, hakikisha kuwa sehemu zenye mada nzito zinaoanishwa na sehemu zenye mada nyepesi za kufurahisha, za marafiki wakinongoneza matukio mazuri na wakicheka.

Kila kipengele kina urefu wa kama dakika 20-25, ikiwemo muziki wa kianzia na kumalizia. Kwasababu vipengele ni virefu, unaweza kupanga kurusha vipengele (kipande kimoja wapo katika Igizo) viwili au vitatu tu katika kipindi chako. Kwa mara nyingi vipande viwili au vitatu vinachukua dakiak 6-8.

Unaweza kupata mrejesho wa maigizo kwa kuandaa kipondi kitakacho pokea simu ambazo wasikilizaji watajadili baathi ya mambo waliyoyasikia katika maigizo, waalike wataalamu wa kike na wakiume kujadili mada. Majadiliano yanaweza kujumuisha:

  • jinsi jamii inavyogawanya kazi za kuzalisha na kuuza maharage, au mazao mengine yanayolimwa katika eneo, na jinsi gani mgawanyo huu umetenga mahitaji ya wanawake, na hata inaweza kuathiri familia;
  • unyanyasaji majumbani na utamaduni au tabia za ukimya inayoruhusu hii kuendelea; na
  • aina ya msaada wanaume wanayoweza kuwapatia wanawake ambao wanahangaika kujisaidia wao na famila zao.

Script

1.
Scene 1
2. Sehemu:
Nje. Kiwanda. Asubuhi.
3. Utambulisho wa kipengele:
Kelele za honi ya lori.

4. Wahusika:
Farida, Stella, Sigi, Mlinzi.

5. SFX:
KELELE ZA HONI YA LORI.
6. SIGI:
(ANAPIGA KELELE MBALI NA MIC) Oya fungua mlango bwana! Alaa!
7. MLINZI:
(KWA HARAKA) Nakuja kiongozi!
8. SFX:
MLINZI ANAFUNGUA GETI NA LORI LINAINGIA NDANI.
9. SFX:
INJINI YA LORI INAZIMWA.
10. STELLA:
Sababu yako ya kuchelewa leo nini?
11. SIGI:
Eiish! Acha kukuza mambo! Siku mbili tu?
12. STELLA:
Siku mbili zinaweza zisiwe kitu kwako lakini kwetu sisi ni kitu kikubwa sana. Hii ni biashara, au umesahau?
13. SIGI:
Unajua unaongea sana wakati umeanza kazi juzi juzi tu!
14. STELLA:
Kwanza naomba ujiangalie sana. Inawezekana umeshasahau kwa hiyo inabidi nikukumbushe. Mimi ndio msimamizi hapa kiwandani kwa hiyo nafanya kazi yangu. Ningekushauri na wewe uanze kufanya kazi yako na usije ukadhani wewe ni muhimu sana.
15. SIGI:
Unanitisha au?
16. STELLA:
Nimeshasema ninachohitaji kusema kwa hiyo naona ni bora turudi kwenye biashara iliyotuleta hapa.
17. FARIDA:
(ANAKARIBIA MIC) Stella!…Stella!
18. STELLA:
(KWA MSHANGAO) Farida!? Sitaki kuamini! (ANAMGEUKIA SIGI) Samahani kidogo.
19. SIGI:
(KWA HASIRA) Unaenda wapi sasa?
20. SFX:
FARIDA NA STELLA WANAKUMBATIANA KWA FURAHA.
21. STELLA:
(KWA FURAHA) Farida, siamini kama ni wewe. Eheee niambie za kwako?
22. FARIDA:
(ANACHEKA) Mimi naendelea vizuri tu! Kwanza nimekuja muda m’baya au?
23. STELLA:
Kusema kweli ndio nilikuwa namalizana na mteja yule pale.
24. FARIDA:
Basi acha nirudi baadae au?
25. STELLA:
Hapana! Wala usijali…Kwanza nina muda mrefu sijakuona.
26. FARIDA:
Mungu wangu! Ni muda mrefu sana. Kwanza Jenny ndiye aliyeniambia kuwa umerudi kijijini.
27. STELLA:
Kwanza kabla hujaanza kulalamika naomba nijielezeee.
28. FARIDA:
(ANAMKATISHA KWA UTANI) Naomba ujielezee kabisa, kwanini Jenny unamtembelea lakini mimi hunitembelei…inaonekana yeye ndiye rafiki yako pekee hapa kijijini.
29. STELLA:
(ANACHEKA) Nilipanga kuja kukuona wikiendi hii. Lakini unajua tangu nimerudi sijapata muda wa kupumzika hata kidogo. Mambo yamekuwa mengi sana…si unajua tena kazi na nini.
30. FARIDA:
Huna haja ya kunielezea mpendwa, naelewa. Mimi nimefurahi tu umerudi.
31. STELLA:
Nimefurahi pia. Naona hujabadilika sana wala nini!
32. FARIDA:
Hata wewe hujabadilika.
33. SFX:
STELLA NA FARIDA WANACHEKA.
34. SIGI:
(ANAKARIBIA MIC) Oya! Oya! Hivi unatuchukulia sisi ni masanamu au? Tumekuwa tukikususbiri muda wote huu.
35. STELLA:
Sawa (ANAMGEUKIA FARIDA) Farida samahani kidogo mpendwa.
36. FARIDA:
Wala usijali.
37. SFX:
STELLA NA SIGI WANASOGEA PEMBENI.
38. SIGI:
Hiyo ndio shida ya kuajiri wanawake. Wewe badala ya kumaliza biashara huku, uko na mwenzio pale mnapiga domo tu.
39. STELLA:
Yaani wewe ndio wa kuongea? Mzee wa kuwahi. Unatudai shingapi?
40. SIGI:
(KWA HASIRA) Hii hapa, nimeandika kwenye karatasi.
41. STELLA:
Sawa unaweza kuenda kwa keshia na atakulipa.
42. SIGI:
(KWA KEJELI) Asante sana.
43. SFX:
SIGI ANAONDOKA NA STELLA ANARUDI KUONGEA NA FARIDA.
44. FARIDA:
Pole sana rafiki yangu.
45. STELLA:
Yaani! Anahisi anaweza kuongeana wanawake jinsi anavyojisikia. Hana heshima hata kidogo.
46. FARIDA:
Sigi na heshima?! Hivi vitu viwili ni kama maji na mafuta. Unajua siku chache zilizopita amejaribu kumlazimisha msichana kulala nae kisa tu alikuwa anajaribu kumuuzia maharage.
47. STELLA:
(KWA MSHANGAO) Acha bwana! Unasema kweli?
48. FARIDA:
Sikutanii hata kidogo. Sigi ni mtu m’baya sana. Yaani kama ningekuwa na uwezo nisingemuuzia hata punje ya moja ya maharage.
49. STELLA:
Sasa kwanini unaendelea kufanya nae biashara?
50. FARIDA:
(ANAGUNA) Mume wangu. Yeye ndiye mwenye maamuzi ya kuamua tunamuuzia nani.
51. STELLA:
Huyo msichana alienda polisi?
52. FARIDA:
Nani?
53. STELLA:
Huyo msichana ambaye Sigi alijaribu kum’baka. Je alienda polisi?
54. FARIDA:
Sidhani kama polisi wangefanya lolote. Labda kama angebakwa kweli…mume wangu ndio alivyoniambia.
55. STELLA:
Mbona haileti maana sasa?
56. FARIDA:
Mwenyewe nilisema hivyo hivyo.
57. STELLA:
Inasikitisha sana….(ANABADILISHA MAONGEZI) Nasikia una watoto watatu.
58. FARIDA:
(ANACHEKA) Ndio, mweneyezi Mungu kanibariki na wasichana watatu.
59. STELLA:
(KWA SHAUKU) Yaani nitafurahi nikiwaona kama nini! Hongera sana kipenzi!
60. FARIDA:
Asante. Ehee na wewe ndoa lini? Au ndio umeshapata mtu huko mjini?
61. STELLA:
(ANACHEKA) Yaaniushaanza kuwa kama mama yangu! (ANAGUNA) Bado nasubiri mpendwa.
62. FARIDA:
Sasa unasubiria nini? Kwani unafikiri atashuka kutoka mbinguni?
63. STELLA:
(ANACHEKA) Eeeh inavyoonekana ndoa ya mtu Fulani ni moto moto!
64. FARIDA:
(KWA UPOLE) Tunajitahidi hivyo hivyo! (ANABADILISHA MAZUNGUMZO GHAFLA) Alafu kabla sijasahau, nimekuletea maziwa haya.
65. STELLA:
Hee! Haya yote umeninunulia mimi? Farida na wewe kulikuwa hakuna haja.
66. FARIDA:
Hapana sijayanunua. Ninamiliki ng’ombe na mbuzi, huwa nauza maziwa na mbolea.
67. STELLA:
(KWA FURAHA) Farida mfanyabiashara! Ni vizuri kuona hujabadilika hata kidogo.
68. FARIDA:
Najitahidi lakini usijali wala sitakudai hayo maziwa.
69. STELLA:
Yaani kama umejua vile kwa sababu na mimi nilikuwa sina mpango wa kukulipa.
70. SFX:
FARIDA NA STELLA WANACHEKA.
71. CONTROL:
Stella

 

72.
Scene 2
73. Sehemu:
Nje. Shambani kwa Farida. Asubuhi.
74. Utambulisho wa kipengele:
Farida analima huku akiimba.

75. Wahusika:
Farida, Mama Mjuni, Zuhura, Sifa, Hafsa.

76. SFX:
FARIDA ANALIMA HUKU AKIIMBA.
77. ZUHURA:
(KWA SHAUKU) Mama! Mama! Angalia! Jongoo!
78. FARIDA:
Wewe Zuhura ebu acha! Usije ukaanza kuwashwa mwili mzima hapa sasa hivi!
79. ZUHURA:
Simshiki na mkono, natumia fimbo.
80. SIFA:
(KWA UOGA) Mama!…Zuhura ananigusa na fimbo aliyoshikia jongoo!
81. SFX:
ZUHURA NA SIFA WANAKIMBIZANA.
82. FARIDA:
Wewe Zuhura ebu mwache mwenzio amwangalie mdogo wenu.
83. ZUHURA:
(KWA KUDEKA) Mimi sijafanya kitu!
84. FARIDA:
Mimi nilijua mmekuja hapa kunisadia na kazi lakini mnafanya utundu tu! Tunakazi nyingi za kufanaya na inabidi tumalize kabla giza halijaingia.
85. ZUHURA:
Mimi nafanya kazi.
86. FARIDA:
Haya nisaidie kung’oa majani na mizizi ya maharage lakini angalia miiba. Sawa?
87. ZUHURA:
Sawa.
88. MAMA MJUNI:
(AKIKARIBIA MIC) Eeeh! Wacha weee! Mama na wanae wazuri!
89. FARIDA:
(ANACHEKA) Eeeh! Mama Mjuni karibu! Umetukuta kwenye kazi kidogo!
90. MAMA MJUNI:
Naona!
91. ZUHURA, SIFA:
Shikamoo!
92. MAMA MJUNI:
Marahaba watoto wazuri mnamsaidia mama yenu au mmekaa tu?
93. FARIDA:
Wao kazi yao kucheza tu!
94. ZUHURA:
(KWA SHAUKU) Tunamsaidia!
95. SIFA:
Muongo; anacheza tu!
96. ZUHURA:
(KWA HASIRA) Hapana!
97. SIFA:
(KWA SAUTI) Ndio!
98. FARIDA:
(ANAINGILIA KATI) Haya acheni kugombana.
99. MAMA MJUNI:
(ANACHEKA) Hawa watoto wa siku hizi bwana!
100. FARIDA:
(ANAGUNA) Wanaweza kukufanya ukachanganyikiwa!
101. MAMA MJUNI:
Nimefurahi lakini kukuona umerudi katika hali yako kawaida tangu tulipoonana mara ya mwisho plae hospitalini. Unafanya nini?
102. FARIDA:
Nimeona bora niandae shamba kwa ajili ya kilimo kwa kulisafisha na kukata majani na mizizi ya maharage ambayo tumetoka kuvuna.
103. MAMA MJUNI:
Hapana Farida! Usiondoe mizizi ya maharage iliyobaki.
104. FARIDA:
Kwanini? Si nimeshavuna maharage….Haina haja ya kuendelea kuiacha hapa inamaliza nafasi tu!
105. MAMA MJUNI:
Unaona! Watu wengi wanashindwa kuelewa kwamba pale unapoiacha mizizi ya maharage kwenye ardhi, unaongeza kiwango cha gesi ya naitrojeni kwenye ardhi yako na itasiaidia baadae kwenye mavuno yako.
106. FARIDA:
(KWA MSHANGAO) Kweli?
107. MAMA MJUNI:
Niamini mimi. Watu wengi hawajui hili lakini inasaidia kweli yaani.
108. FARIDA:
Heeh! Wewe unapata wapi mambo yote haya?
109. MAMA MJUNI:
Kuna mtaalamu aliniambia alipokuja kupima rutuba ya ardhi yangu.
110. FARIDA:
(ANAGUNA) Eeeh bora ya wewe, mimi sina uwezo huo wa kumlipa mtaalamu kuangalia ardhi yangu.
111. MAMA MJUNI:
(ANACHEKA) Ebu lete nikusaidie!
112. FARIDA:
Asante.
113. SFX:
MAMA MJUNI ANAMSAIDIA FARIDA KUNG’OA MAJANI.
114. MAMA MJUNI:
Unajua saa nyingine huwa nakuhurumia sana… Itakuwa vigumu sana kuangalia watoto huku ukifanya kazi shambani.
115. FARIDA:
Kusema kweli sio rahisi lakini wakati mwingine hawa watoto wanasaidia kunitia nguvu…Bila ya wao nahisi ningekuwa nimeshakata tama siku nyingi.
116. MAMA MJUNI:
Sikiliza Farida, nataka ujue muda wowote ukihitaji msaada nipo hapa kwa ajili yako sawa?
117. FARIDA:
Sawa… asante mama Mjuni. Nashukuru sana.
118. MAMA MJUNI:
Usijali kipenzi…Unajua nimekuwa nikifikiria.
119. FARIDA:
Kuhusu nini?
120. MAMA MJUNI:
Sikiliza Farida, nadhani nina wazo ambalo linaweza kutusaidia. Kwanini wanawake tusiungane pamoja na kusaidiana kufanya kazi za shambani uku tukipanga zamu za kusaidiana kutazama watoto.
121. FARIDA:
(ANACHEKA) Ebu usinitanie mama Mjuni. Unatania au?
122. MAMA MJUNI:
Kwani inashindikana? Itasaidia kwapunguzia mzigo wanawake wengi. Itakusaidia hata wewe…
123. FARIDA:
Najua. Lakini sidhani kama wanawake wengi watakubaliana na hilo wazo. Vipi kuhusu wanawake wengine wasio na watoto?
124. MAMA MJUNI:
Nao watasaidiwa na wanawake wengine kufanya kazi mashambani mwao pale itakapofika muda wao. Haijalishi kama wana watoto au la, ikiwa tu kama nao watasaidia wanawake wengine.
125. FARIDA:
(KWA MASHAKA) Sijui Mama Mjuni…nahisi itakuwa vigumu sana kwa kila mwanamke hapa kijiini kukufanya hivyo.
126. MAMA MJUNI:
Tunaweza kuanza kidogo kidogo. Kwanini tusipeleke ili wazo kwenye kikundi chetu cha vikoba ili tuone.
127. FARIDA:
Lakini watasikiliza?
128. MAMA MJUNI:
Ndio tutajua.
129. CONTROL:
Farida.

 

130.
Scene 3
131. Sehemu:
Nje. Kwa mama Mjuni. Asubuhi.
132. Utambulisho wa kipengele:
Mazungumzo ya wanawake.

133. Wahusika:
Farida, Mama Mjuni, Doris, Grace, Jenny, Mama K, Monica, Mama Juma.
134. SFX:
MAZUNGUMZO BAINA YA WANAWAKE.
135. MAMA MJUNI:
Mnisamehe kwa kuchelewa wapendwa lakini nadhani tunaweza tukaanza mkutano wetu sasa.
136.SFX:
MAZUNGUMZO YANAENDELEA.
137. MAMA MJUNI:
(KWA UKALI) Sawa, naomba utulivu wenu tafadhali!
138. SFX:
KELELE ZINAISHA.
139. MAMA MJUNI:
Sawa kabla hatujaendelea kuzungumzia mambo mengine, nadhani tungejadili jambo ambalo ni la msingi sana na lenye manufaa kwetu sote hapa. (ANAJIWEKA SAWA KIDOGO) Hivi karibuni nilikuwa na mazungumzo mazuri sana na Farida na sote tulikubaliana kwamba ingekuwa vizuri kama wanawake wote tungefanya kazi kwa pamoja kwa manufaa ya wanawake wote. Kwa sababu wanawake wengi hapa kijijini wanapata shida kulea wanao huku wakifanya kazi mashambani.
140. SFX:
MLIPUKO WA KELELE HEWANI.
141. MAMA K:
(ANARUKA JUU) Mnamaanisha nini?
142. JENNY:
(KWA SHAUKU) Hilo ni wazo zuri!
143. MONICA:
(KWA SAUTI YA JUU) Hapana! Hapana! Haiwezekani mimi nipoteze muda wangu kulea mtoto wa mtu mwingine wakati ni mambo yangu kibao.
144. SFX:
MAMA MJUNI ANAWATULIZA KWA KUGONGA KWENYE MEZA.
145. MAMA MJUNI:
Sawa, naomba tuwe waelewa basi tafadhali! Mimi binafsi nadhani ni wazo zuri kwa sababu litawasaidia wanawake wengi. Kwa sababu kama tunavyojua wanawake wengi wana mzigo wa kuangalia familia zao na kufanya kazi mashambani.
146. FARIDA:
(KWA MSISITIZO) Ndio! Na wengine tuna mzigo wa kulea watoto pamoja na kufanya kazi mashambani…
147. MAMA K:
(ANAMKATISHA) Kwa hiyo? Inanihusu nini mimi? Mimi sina watoto; watoto wangu wote ni watu wazima sasa kwanini nikusaidie wewe kulea watoto wako?
148. JENNY:
Mama K, nadhani ungewafikiria na wanawake wengine sio unajifikiria peke yako tu.
149. MAMA K:
Yaani wewe bora hata usiongee! Kwanza kwenye vikao tu unakuja mara moja moja muda wote upo kwenye gereji yako. Haya niambie huo muda wa kusaidia hao wanawake wengine utaupata wapi?
150. JENNY:
Nina uhakika nitaupata tu.
151. FARIDA:
Mimi nahisi nyie wengine mnashindwa kuelewa. Hii haitawasaidia wanawake wenye watoto tu bali kila mtu- kwa sababu nina uhakika wote tuna mambo mengi ya kufanya majumbani mwetu. Lakini kwa kutengeana zamu, tunaweza kusaidiana sana.
152. MONICA:
Samahani, lakini mimi nakubaliana na mama K! Mimi nilidhani sababu kubwa ya vikoba ni kuweka akiba ya pesa kwa ajili ya upatu, sasa haya mambo mengine yote yanatokea wapi?
153. DORIS:
Mimi nakubaliana na wazo lakini kuna watu nitashindwa kufanya nao kazi humu.
154. MAMA MJUNI:
Una maana gani?
155. GRACE:
Najua ananizungumzia mimi… Hata mimi sitaki kufanya kazi na wewe!
156. DORIS:
Kwani nani aliyekuuliza?
157. GRACE:
Siongei na wewe.
158. SFX:
MAMA MJUNI ANAWATULIZA KWA MARA NYINGINE TENA.
159. MAMA MJUNI:
Jamani! Jamani! Sidhani kama tutafika mbali kama tutaendelea kubishana. Mimi naona bora tupige kura tu.
160. MAMA JUMA:
Hapo nakubaliana na wewe.
161. MAMA MJUNI:
Kwa hiyo kura ya wengi ndio itaamua…Kwa hiyo wanawake mnaokubaliana na wazo hili naomba mnyoshe mikono yenu juu!
162. JENNY:
(ANANYOSHA MKONO JUU) Huku! Huku!
163. SFX:
BAADHI YA WANAWAKE WANANYOSHA MIKONO YAO JUU.
164. MAMA MJUNI:
Na wanawake wangapi hawakubaliani na wazo hili?
165. MAMA K:
(KWA SAUTI) Tupo hapa! Kazi zangu zenyewe tu zinanishinda, nitaanzaje kulea mtoto wa mtu!
166. SFX:
MAKELELE YA WANAWAKE HUKU WENGINE WAKISHANGILIA.
167. MAMA MJUNI:
Sawa, kwa hiyo tumepata kura nyingi za wanaokubaliana na hili wazo. Kwa hiyo wazo limepitishwa.
168. SFX:
WANAWAKE WANASHANGILIA.
169. MAMA MJUNI:
Nadhani hii inaoenesha wengine wenu mnawajali wanawake wenzenu- ambacho ni kitu kizuri. Huu uamuzi wa kufanya kazi kwa pamoja hautawasaidia wanawake wenye watoto tu bali hata wanawake wasio na watoto. Naamini kwa kufanya kazi kwa pamoja tutafanikisha mambo mengi.
170. SFX:
WANAWAKE WANASHANGILIA.
171. CONTROL:
Mama Mjuni

 

172.
Scene 4
173. Sehemu:
Nje. Gala la Sigi. Mchana.
174. Utambulisho wa kipengele:
Mazingira ya Gala.

175. Wahusika:
Sigi, Adam, Alex, Mkulima.

176. SFX:
MLANGO UNAFUNGULIWA NA SIGI NA MKULIMA WANATOKA NJE.
177. MKULIMA:
Kwa hiyo utanilipa kiasi kile kile kwa maharage yangu au?
178. SIGI:
Kwani tumekuwa tukifanya biashara tangu lini ndugu yangu?
179. MKULIMA:
Nilitaka nihakikishe kwamba tunakubaliana tu!
180. SIGI:
Wewe usiwe na wasiwasi. Kwanza naweza kukulipa hata mara mbili yake vile vile!
181. MKULIMA:
Wewe?! Sigi unilipe mara mbili? Siku hiyo ndio mbwa atapiga mswaki!
182. SFX:
SIGI NA MKULIMA WANACHEKA.
183. ALEX:
(ANAKARIBIA MIC) Samahani Sigi, tunaweza tukaongea kidogo.
184. SIGI:
Tukaonge?! Kwani wewe huoni nipo katikati ya mazungumzo hapa?
185. ADAM:
Tunaona, lakini ni muhimu sana.
186. SIGI:
(ANACHEKA) Muhimu eeh? (ANAMGEUKIA MKULIMA) Watoto wa siku hizi bwana…hawana adabu hata kidogo.
187. MKULIMA:
Usijali wewe endelea tu, mimi na wewe nahisi tumeshamaliza.
188. SIGI:
Sawa basi nitakuja jumatano kuchukua mzigo wangu.
189. MKULIMA:
Sawa.
190. SFX:
MKULIMA ANAONDOKA. SIGI ANAWAVUTA ADAM NA ALEX PEMBENI.
191. SIGI:
(KWA SAUTI YA CHINI) Kwanini hamkunipigia kabla ya kuja hapa?
192. ALEX:
Hatukuwa na pesa kwenye simu.
193. SIGI:
Kwa hiyo mkaamua kuja kwenye sehemu yangu ya biashara bila taarifa?
194. ADAM:
Sikiliza, tulisahau Sigi na hata kama tungetaka kukupigia tusingeweza kwa sababu hatukuwa na dakika kwenye simu.
195. ALEX:
Alafu sio kama tunakuja tu! Kuna biashara tunataka tuongee.
196. SIGI:
(ANAGUNA) Hivi wewe una akili kweli? Mnaniuzia vitu vya wizi wewe mpuuzi! Itakuwaje kama mtu akiwaona?
197. ADAM:
Kusema kweli hatukufikira hilo!
198. SIGI:
Ndio siku nyingine mfikirie…tumieni akili bwana! Wateja wangu kila siku wapo hapa; hii ni sehemu yangu ya biashara. Haiwezekani mkawa mnaonekana kila siku mnaingia na kutoka kama mnavyojisikia tu. Watu watashtukia.
199. ADAM:
Tusamehe Sigi, hatutarudia tena.
200. SIGI:
Kwa kuomba msamaha tu hamjambo! Hakikisheni siku nyingine mnanipigia kabla!
201. ADAM, ALEX:
Sawa.
202. SIGI:
Sawa, kwa hiyo mna ishu gani leo?
203. ADAM:
Leo tuna vifaa vya magari…Muoneshe Alex.
204. SFX:
ALEX ANAFUNGUA MFUKO NA KUMUONESHA MZIGO.
205. ADAM:
Wewe subiri uone- ni bonge moja la mzigo yaani. Lakini kwa wewe tutakufanyia bei poa, tupe kilo tu!
206. SIGI:
Ebu leta nione….taa za magari? Sasa mimi nitafanyia nini hivi?
207. ALEX:
Acha hizo Sigi, sisi tunajua unajuana na watu. Utapata tu mteja!
208. SIGI:
(KWA DHARAU) Samahani lakini hivi vyote havina mpango kwangu!
209. ADAM:
(KWA KUBEMBELEZA) Usifanye hivyo Sigi…sawa basi tutakupunguzia. Tupe hamsini basi!
210. SIGI:
Hayo ndio maneno sasa, sawa nitavichukua! (ANACHEKA) Kumbe nyie sio wapuuzi kama nilivyokuwa nafikiria.
211. SFX:
SIGI ANACHUKUA MFUKO WENYE VIFAA NA KUANZA KUONDOKA.
212. ALEX:
Subiri Sigi, vipi kuhusu pesa?
213. SIGI:
Utapata pesa baadae. Oh! Alafu siku nyingine mniletee vitu vya maana kidogo na mnipigie simu kabla ya kuja.
214. SFX:
SIGI ANAINGIA OFISINI KWAKE NA KUFUNGA MLANGO.
215. CONTROL:
Sigi

 

216.
Scene 5
217. Sehemu:
Nje. Shambani kwa Mama Mjuni. Mchana.
218. Utambulisho wa kipengele:
Mazingira ya shambani.

219. Wahusika:
Mama Mjuni, Farida, Mama K, Grace, Doris, Monica, Mama Juma.

220. SFX:
WANAWAKE WANASHANGILIA NA KUPIGA MAKOFI.
221. MAMA MJUNI:
Nataka niwashukuru wote mlioweza kufika hapa leo kuanza siku ya kwanza ya kufanya kazi pamoja na kusaidiana. Inaonesha umoja ni nguvu, uwepo wenu umenipa motisha na kunihamasisha sana. Naona hata mama K amekuja leo!
222. SFX:
WOTE WANACHEKA.
223. MAMA MJUNI:
Inaonesha kwamba tunaweza kuweka tofauti zetu pembeni na kufanya kazi kwa pamoja.
224. MAMA K:
Lakini mimi nina swali!
225. MAMA MJUNI:
Ndio mama K!
226. MAMA K:
Kwanini tuanze kufanya kazi kwako?
227. MAMA JUMA:
Kwa sababu yeye ndio mwenyekiti wetu na ndio maana amepata huo upendeleo.
228. FARIDA:
Ndio na kwa wote tuliobaki tumetengeneza ratiba nzuri yenye tarehe zinazoonesha zamu ya kila mtu.
229. GRACE:
Na sisi tunaweza kupata hiyo ratiba?
230. FARIDA:
Ndio, nitampa kila mmoja baadae Grace.
231. MAMA MJUNI:
Sawa tunaweza kuanza na kazi iliyotuleta hapa leo – maandalizi ykwa ajili ya msimu wa kilimo ambao hauko mbali. Lakini kwanza nimtambulishe mgeni…tafadhali karibu mtaalamu wa kilimo, dada Lydia.
232. SFX:
WANAWAKE WENGINE WANAMKARIBISHA KA KUMPIGIA MAKOFI.
233. LYDIA:
Asanteni sana wanawake wenzangu, na labda kwa kumsahisha mama Mjuni. Mimi sio mtaalamu wa kilimo kwa sababu kilimo ni neon pan asana, lakini nimebobea kwenye kilimo cha maharag ambacho najua wengine wenu hapan mnatumia kama mboga ya nyumbani na kuuza pia.
Labda niseme pia, Mama Mjuni alivyoniomba nije kuongea na nyinyi leo, nilikuwa nimefurahi sana. Nyie wote ni mfano wa kuigwa na wanawake sehemu nyingine kwa kufanya kazi kwa pamoja.
234. SFX:
WANAWAKE WANASHINGILIA KWA KUPIGA VIGEREGERE.
235. LYDIA:
Kwa hiyo kama mnavyojua msimu wa kulima haupo mbali. Kwa hiyo leo nitaanza kwa kuwaonesha mbinu sahihi ambazo kama mtazifuta zitawapa mavuno mazuri kwenye kiilimo cha maharage.
236. SFX:
WANAWAKE WANASHINGILIA KWA VIGEREGERE NA MAKOFI.
237. LYDIA:
Kitu cha kwanza ambacho huwa tunafanya kabla ya msimu wa kulima ni kusafisha mashamba yetu kwa kuondoa uchafu wote na kwa kukata majani kabla hatujaanza kupanda mbegu. Na sio ndio maana wote tupo hapa leo?
238. ALL:
(KWA SAUTI) Ndio.
239. LYDIA:
Kitcu cha kwanza kabisa ambacho inabidi tuelewe- na ni muhimu sana – ni kwamba tusiondoe mabaki kama mizizi na mashina yaliyobaki ya maharage.
240. SFX:
MSHANGAO KUTOKA KWA WANAWAKE.
241. LYDIA:
Najua wengine wenu mtakuwa mnajiuliza kwanini na mimi nitawaambia kwanini. Ni kwa sababu mizizi na mashina yataongeza kilo 5 mpaka 20 za gesi ya naitrojeni kwa heka moja ambayo itakuwatayari kwa mimea inayofuata. Pia itasaidia kuboresha na kusaidia usafirishaji wa maji na hewa ndani ya ardhi ambayo pia ni nzuri kwa maharage yetu.
242. DORIS:
Samahani lakini kazi ya hiyo naitrojeni ni nini?
243. LYDIA:
Ndio ninapoelekea huko mpendwa…Hii gesi ya naitrojeni itasaidia kwenye uboreshaji mazao mapya mtakayopanda ambayo ukiunganisha na mbinu bora za ulimaji itasaidia uzalishaji wa zaidi ya kilo 800 pale unapobadilisha mazao kama mahindi.
244. SFX:
MSHANGAO KUTOKA KWA WANAWAKE.
245. MAMA K:
Kusema kweli mimi sikujua hayo yote!
246. MONICA:
Yaani muda wote huo mimi nilikuwa natoa mizizi. Kumbe ningeacha ningeweza kupata magunia mengi zaidi.
247. LYDIA:
Ndio lakini tusisahau kwamba hiyo peke yake haitoshi kukupa mavuno mazuri. Inabidi pia utumie mbinu sahihi za kilimo. Kitu kingine inabidi mtoe majani na mimea isiyohitajika kwa sababu itakuwa inashindana tu na mimea yako kupata jua na maji na virutubisho vingine. Lakini pia ni muhimu kuangalia rutuba ya ardhi yako. Kama unahisi ardhi yako haina rutuba ya kutosha, jaribu kupata vipimo kabla ya kupanda maharage yako. Sasa hivi tunaanzisha vituo mbali mbali kwa ajili ya kusaidia watu lakini haina maana vitakuwa kila sehemu. Kwa hiyo unaweza ukamtafuta mtaalamu wa kijiji kukusaidia kupima ardhi.
248. MAMA JUMA:
Haitakuwa gharama sana?
249. LYDIA:
Hapana kusema kweli ni bei ya kawaida sana.
250. MAMA MJUNI:
Ni kweli kabisa. Mimi kabla ya kuanza kulima lazima nimtafute Lydia aje kupima ardhi yangu.
251. MAMA K:
Lakini sio kila mtu mwenye huo uwezo.
252. LYDIA:
Kama mnaona gharama ni kubwa sana kwa mtu mmoja mmoja, mnaweza kuungana pamoja na nitawafanyia kwa bei nzuri tu.
253. GRACE:
(KWA SHAUKU) Ndio! Hiyo itakuwa vizuri zaidi!
254. MONICA:
Hayo ndio maneno sasa!
255. LYDIA:
Sababu kubwaya kupima ardhi ni kwa sababu maharage yanahitaji ardhi yenye virutubisho. Pia hayawezi kukua vizuri kwenye ardhi yenye tindikali na alkali. Kwa hiyo utaongeza uwezekano wa kupatya mavuno mazurio kwa kupanda kwenye ardhi nzuri.
256. FARIDA:
Samahani lakini je kuna suluhisho kwa tatizo kama hilo?
257. LYDIA:
Kikubwa ambacho unaweza kufanya kama ardhi yako ina vipimo vikubwa vya tindikali, ni kuweka chokaa ili kupunguza tindikali.
Kitu kingine ni kupanda mbegu za aina bora. Hapa Tanzania mbegu za aina bora ni pamoja na Njano Uyole, Lyamungu 90, na Rozi koko/ kitenge. Kwa sababu mbegu bora zitaongezauwezekano wa kupata mavuno mazuri, na pia ni ngumu kupatwa na magonjwa na pia zina thamani kubwa kwenye masoko. Muepukane na mbegu zenye kasoro na mbovu zilizotokana na mimea yenye magonjwa kwa sababu nazo zinaweza kuwa na magonjwa.
258. GRACE:
Unatushauri tutumie aina gani ya mbegu?
259. LYDIA:
Kuna aina mbili za mbegu za maharage, zile zinazokuwa kwa muda mfupi ambazo ni nzuri kwenye sehemu kavu. Zinakuwa kwa muda mfupi lakini mavuno yake sio makubwa. Pia zipo ambazo zinakuwa kwa muda mrefu ambazo ni nzuri kwenye sehemu za maji maji na zinatoa mavuno mazuri sana na pia huchangia katika kuongeza virutubisho kwenye ardhi yako.
260. GRACE:
Mimi naona hizo zinazokua kwa muda mrefu ni nzuri sana.
261. FARIDA:
Nakubalina na wewe.
262. MAMA JUMA:
Kweli kabisa.
263. LYDIA:
Itabidi mtumie mbegu zinazoendana na hali yenu ya hewa pamoja na ardhi.
264. MAMA MJUNI:
Wapendwa mimi naona ni bora tuanze kazi sasa kwa sababu muda nao umetutupa mkono. Tutahakikisha Lydia anarudi siku nyingine ili aendelee kutupa elimu hii ya kilimo cha maharage iliyo nzuri kabisa.
265. GRACE:
(KWA SHAUKU) Itakuwa vizuri sana!
266. MAMA MJUNI:
Sawa jamani, ebu tumpigie makofi dada Lydia kwa mchango wake mkubwa leo!
267. SFX:
WANAWAKE WANAPIGA MAKOFI.
268. FARIDA:
Sawa jamani tutaanza kuuondoa uchafu na majani na mimea yote isiyo hitajika.
269. MAMA MJUNI:
Ndio lakini naomba tukumbuke mafunzo ya Lydia. Tukumbuke tunatoa mimea isiyohitajika na sio mizizi ya maharage.
270. FARIDA:
(KWA SHAUKU) Sawa tuanze kazi jamani!
271. MONICA:
Lakini ebu ngojeni kwanza! Tutafanya vipi kazi bila ya wimbo wa kutupa motisha eeh?
272. GRACE:
Kweli.
273. MAMA MJUNI:
Wewe kuna nyimbo yoyote unaifahamu?
274. MONICA:
Mimi nyimbo ninayo lakini sauti yangu mbaya!
275. SFX:
WANWAKE WANACHEKA.
276. MAMA MJUNI:
Nani sasa atuongoze na nyimbo? Basi mama K.
277. MAMA K:
Hapana. Mtu mwingine aanzishe nyimbo!
278. GRACE:
Inabidi Farida atuongoze; ana sauti nzuri sana. Nishamsikia anaimba taarab siku moja.
279. FARIDA:
(ANACHEKA KWA AIBU) Sawa mimi nitaanzisha.
280. SFX:
FARIDA ANAANZISHA NYIMB HUKU WANWAKE WENGINE WAKIITIKIA KWA NYUMA.
281. FARIDA:
(AKIIMBA) Wanawake wenzangu tubebe majembe yetu kwani mafanikio yapo mikononi mwetu; tuamke sasa kwani muda ndio huu!
282. MZEE ALI:
(ANAWAKATISHA) Samahani akina mama lakini naomba na mimi nijiunge.
283. SFX:
WANWAKE WANAMSHANGILIA MZEE ALI ANAYEJIUNGA KWENYE KAZI.
284. SFX:
FARIDA ANAENDELEA KUIMBA HUKU WAKIFANYA KAZI.
285. CONTROL:
Mama Mjuni

 

286.
Scene 6
287. Sehemu:
Nje. Nyumbani kwa Farida. Mchana.
288. Utambulisho wa kipengele:
Mazingira ya kwa Farida.

289. Wahusika:
Farida, Jenny.

290. JENNY:
(KWA MSHANGAO) Kweli?….Unatania au?
291. FARIDA:
Hapana sikutanii. Mzee Ali nae alianza kuimba na kufanya kazi pamoja na sisi.
292. JENNY:
Mungu am’bariki kwa kweli, yuko tofauti sana.
293. FARIDA:
Kwa kweli! Kama wanaume wote hapa kijijni wangekuwa kama mzee Ali, mambo yangekuwa tofauti sana.
294. JENNY:
Wewe endelea kuota tu. Haitatokea ohoo!
295. SFX:
FARIDA NA JENNY WANACHEKA.
296. JENNY:
Natamani na mimi ningekuwepo. Inaonekana mlienjoy sana.
297. FARIDA:
Tatizo lako wewe bwana muda wote uko busy na gereji yako. Inabidi ujipe muda kwa ajili ya mambo mengine. Unajua siku hizi hata kwenye vikao huonekani.
298. JENNY:
Ndio najua, basi nitajitahidi nitapate muda wa kuja kwenye vikao japo hata kufanya kazi na wanawake wenzangu.
299. FARIDA:
Ndio, bora uje tu. Hutaki habari zianze kusamabaa kwamba hausaidii kazi za mashambani kwa sababu muda wako ukifika, kila mtu atakugeuka.
300. JENNY:
Ni kweli kabisa unachosema.
301. FARIDA:
Unajua nimemshauri hata Stella ajiunge na vikoba.
302. JENNY:
Kweli? Amesemaje?
303. FARIDA:
Amesema atajiunga. Anahitaji muda tu wa kupangilia mambo yake vizuri.
304. JENNY:
Na kweli bora afanye hivyo.
305. FARIDA:
Ehee mambo mengine vipi? Unajua ni mud asana tangu tumekaa chini tukaongea.
306. JENNY:
Mambo yamekuwa mengi alafu unajua Vumi alipata malaria, kwa hiyo ilibidi nimuuguze.
307. FARIDA:
Eh! Masikini ya Mungu! Poleni sana. Anaendeleaje sasa hivi?
308. JENNY:
Anaendelea vizuri kidogo sasa hivi. Ilibidi mama yake aje kukaa nasi kwa siku chache kusaidia kumuuguza.
309. FARIDA:
Jamani? Mama mkwe hajambo?
310. JENNY:
Yaani Farida ilikuwa kama jehanamu! Sijui nimfanyie nini ili huyu mwanamke aridhike; muda wote yeye ni kulalamika tu.
311. FARIDA:
(ANACHEKA) Mimi na wewe hatuchekani kipenzi.
312. JENNY:
Kusema kweli Farida sijui mwenzangu unaweza vipi kuwavumilia hao wakwe zako.
313. FARIDA:
Sio rahisi. Hujui mara ngapi nimefikiria kumuacha yule mwanaume. Lakini nikifikiria watoto zangu, nani atawalea?
314. JENNY:
Na kweli kipenzi, watoto wako wanakutegemea mama yao.
315. FARIDA:
Jenny hujui tu jinsi gani nimemvumilia yule mwanaume na familia yake.
316. JENNY:
Najua umepitia mengi shoga yangu.
317. FARIDA:
Yaani haikuwa rahisi. Na bkama sio hawa wanangu, sijui ningekuwa wapi leo hii.
318. JENNY:
Farida, mimi nakusifu kwa ujasiri wako kwa ajili ya wanao. Lakini na wewe inabidi ujifikirie pia. Inaweza ikafikia kipindi akasababisha matatizo makubwa sana kwako.
319. FARIDA:
Jenny, kwa sasa hivi mimi nawafikira wanangu tu. Sijali kitakachotokea!
320. JENNY:
Farida, inabidi uwe mwangalifu sana. Niahidi utakuwa mwangalifu.
321. FARIDA:
Nakuahidi nitakuwa mwangalifu.
322. CONTROL:
Farida

 

323.
Scene 7
324. Sehemu:
Ndani. Nyumbani kwa Farida. Mchana.
325. Utambulisho wa kipengele:
Tangazo kwenye redio.

326. Wahusika:
Farida, Afande Kaifa, Sifa, Zuhura.

327. SFX:
TANGAZO REDIONI.
328. MTU KWENYE REDIO:
Karibuni! Karibuni wote siku ya leo kuanzia saa saba mchana katika kiwanja Uhuru kwenye tamasha la la kilimo lililoandaliwa na shirika la Tunu. Hakutakuwa na kiingilio na watu wa rika lote mnakaribishwa kujifunza kilimo bora kabisa. Pia kutakuwa na michezo kwa ajili ya watoto! Mnakaribishwa!
329. ZUHURA:
Mama, tutaenda eeh?
330. FARIDA:
Tutaenda wapi?
331. ZUHURA:
Hiyo sehemu kwenye redio!
332. FARIDA:
Sawa tutaenda lakini maliza kwanza chai yako basi.
333. SIFA:
Mama hata mimi nataka kuenda!
334. AFANDE KAIFA:
(AKIKARIBIA MIC) Hizo kelele zote za nini?
335. FARIDA:
Watoto wako wanataka kuenda kwenye hilo tamasha wanalotangaza kwenye redio.
336. AFANDE KAIFA:
Tamasha gani?
337. FARIDA:
Kuna tamasha linafanyika leo katika viwanja vya Uhuru limeandaliwa na shirika linaitwa Tunu kwa ajili ya kuwaelimisha watu juu ya kilimo bora.
338. AFANDE KAIFA:
Sasa inakuwaje hawa nao wanataka kuenda?
339. FARIDA:
Wamesikia kuna michezo kwa ajili ya watoto.
340. AFANDE KAIFA:
Na shule je?
341. FARIDA:
Hilo tamasha linafanyika mchana huu. Kwa hiyo wakitoka shule naweza kuwapeleka na kuwarudisha nyumbani.
342. AFANDE KAIFA:
Mbona kama nahisi wewe ndio unataka kuenda kuliko hawa watoto?
343. FARIDA:
Ndio nataka niende pia- kwani nani asiyetaka kuenda jamani? Nahisi itakuwa vizuri kwangu na kwa watoto pia. Nitajifunza mengi kwenye tamasha hilo ju ya kilimo cha maharage.
344. AFANDE KAIFA:
Sawa unaweza kuenda lakini hakikisha unanipikia kwanza kabla hujaondoka.
345. FARIDA:
Sawa mume wangu.
346. AFANDE KAIFA:
Na uhakikishe unawahi kurudi. Usichelewe.
347. CONTROL:
Farida

 

348.
Scene 8
349. Sehemu:
Nje. Viwanja vya Uhuru. Mchana.
350.Utambulisho wa kipengele:
Mazingira ya viwanja vya Uhuru.

351. Wahusika:
Grace, Farida, Mama Mjuni, Mama K, Mzee Ali, Vumi, Mjuni, Zuhura.

352. SFX:
MZIKI UNASIKIKA KWA MBALI.
353. MAMA MJUNI:
(KWA SHAUKU) Heeh! Farida naona umekuja na mabaunsa wako!
354. FARIDA:
(ANACHEKA) Yaani hawakutaka kuachwa nyuma. Walitaka kuja kucheza na watoto wenzao.
355. ZUHURA, SIFA:
Shikamoo.
356. MAMA MJUNI:
Marahaba! Mwenzangu nikaanza kuhisi hutokuja tena.
357. FARIDA:
Eh! Nisingeweza kukosa! Vipi tamasha lenyewe linaanza saa ngapi?
358. MAMA MJUNI:
Nadhani litaanza baada ya dakika chache.
359. FARIDA:
Naona watu wengi wamekuja!
360. MAMA MJUNI:
Ndio. Ebu twende na sisi tukajichanganye.
361. SFX:
MAMA MJUNI NA FARIDA WANAANZA KUTEMBEA KUELEKEA WALIPO MZEE ALI NA VUMI AMBAO WAMEKAA WAKIONGEA.
362. VUMI:
(KWA HISIA) Mimi nakwambia huu mwaka wetu! Wewe subiri uone. Tunachukua kombe mwaka huu!
363. MZEE ALI:
Mtashinda vipi wakati timu yangu na mimi iko vizuri mwaka huu? Haiwezekani; sisi ndio tuna timu bora kabisa kwenye ligi.
364. VUMI:
Nani kasema?
365. MZEE ALI:
Mimi ndio nakwambia sasa!
366. MAMA MJUNI:
(AKIKARIBIA MIC) Nilijua tu! Kazi kubishana mpira tu?
367. FARIDA:
(UNACHEKA) Wewe unategemea nini?
368. MZEE ALI:
Sasa mke wangu tutaongelea nini?
369. MAMA MJUNI:
Kuna mambo kibao ya msingi ya kuongelea kuliko kupoteza muda kuongelea mpira.
370. VUMI:
Bora ya sisi tunaoongelea mpira kuliko nyie mnaopoteza muda mkiongelea mitindo ya nywele.
371. SFX:
WOTE WANACHEKA.
372. SFX:
MSHEHERESHAJI ANAJARIBU KUPATA USIKIVU WA WATU
373. MSHEREHESHAJI:
Naomba utulivu wenu watu wangu wa nguvu! Nadhani wote mnaenjoy kuwa hapa katika tamasha la Tunu. Si mnaenjoy jamani?
374. WOTE:
(KWA FURAHA) Ndioo!
375. MSHEREHESHAJI:
Basi ni vizuri. Najua wengi wenu mtakuwa mnajiuliza shirika la Tunu ni nini na tunafanya nini…kwa ufupi tu, sisi tunawasaidia wakulima wadogo wadogo.
376. MAMA K:
(ANAMKATISHA) Je huwa mnagawa pesa kwa wakulima wadogo wadogo?
377. SFX:
WATU WANACHEKA.
378. MSHEREHESHAJI:
Hapana, huwa hatugawi pesa mama yangu.

379. MAMA K:
Sasa mna faida gani?
380. MSHEREHESHAJI:
Mimi nadhani tunatoa kitu chenye faida zaidi ya pesa. Tunawasaidia wakulima wadogo kupata elimu juu ya kilimo bora ambayo wakiitumia vizuri inaweza kuwasaidia hapo baadae kwa sababu itawawezesha kutengeneza pesa kwa kuuza mazao yao mazuri kwenye masoko tofauti. Je kuna wakulima wadogo wadogo ambao wanafanya kazi kwa vikundi hapa leo?
381. SFX:
MAMA MJUNI ANASOGEA MBELE.
382. MAMA MJUNI:
Samahani mpendwa lakini sisi tuna kikundi cha akina mama cha Vikoba na mimi ni mwenyekiti. Na hivi karibuni tumeanza kufanya kazi za kilimo kwa pamoja kwa kusaidiana katika kipindi cha kulima na kwenye kipindi cha mavuno.
383. MSHEREHESHAJI:
Vizuri sana! Wanachama wengine wako wapi?

384. SFX:
MAMA MJUNI ANAWAITA WANACHAMA WA KIKUNDI CHAKE.
385. MAMA MJUNI:
Farida, Grace, Mama K njoeni huku mbele.
386. MSHEREHESHAJI:
Hawa ndio wanachama wote?

387. FARIDA:
Hapana, tuko wengi lakini wengine wameshindwa kutokea leo.
388. MSHEREHESHAJI:
Wengine wako wapi?

389. MTU:
(KWA SAUTI) Wapo majumbani wanapika kama wanawake wanavyotakiwa kufanya.
390. SFX:
WATU WANACHEKA.
391. MAMA MJUNI:
Kwa bahati mbaya, watu wanacheka lakini ndio ukweli. Wanawake wengine wanalazimika kubaki nyumbani na kuangalia waume zao na watoto na saa nyibgine wanakosa matamasha muhimu kama hili la leo.
392. FARIDA:
Ni kweli, wanwake wengi wanakataliwa kuja kwenye matamasha kama haya japo wao ndio wanafanya kazi kubwa mashambani.
393. MSHEREHESHAJI:
Hiyo ni mbaya sana. Lakini leo nategemea mtawafundisha wanachama wenzenu ambao hawapo hapa, yote ambayo mtajifunza hapa.
394. MAMA MJUNI:
Ndio.
395. MSHEREHESHAJI:
Nitawaomba nikutane na nyie wote baada ya kumalizika kwa tamasha hili, kabla hamjarudi majumbani kwenu.
396. MAMA MJUNI:
Sawa.
397. MSHEREHESHAJI:
Sawa, sasa tutaendelea na tamasha letu na tutaanza na maswali ya chemsha bongo. Swali la kwanza ni kwa watoto tu, atakayepatia swali hili atajishindia fulana ya Tunu. Mpo tayari watoto?
398. WATOTO:
(KWA FURAHA) Ndio!
399. MSHEREHESHAJI:
Haya swali la kwanza….Nitajie zao kuu la kijijini hapa?

400. SFX:
WATOTO WANASHINDANA KILA MMOJA AKIJARIBU KUJIBU SWALI.
401. MSHEREHESHAJI:
Haya we binti hapo nyuma uliyem’beba mdogo wako, nipe jibu.

402. ZUHURA:
(KWA UOGA) Mimi?
403. MSHEREHESHAJI:
Ndio wewe.

404. ZUHURA:
Ni maharage.
405. MSHEREHESHAJI:
Vizuri sana – hilo ni jibu sahihi! Unaitwa nani mtoto mzuri?

406. ZUHURA:
Naitwa Zuhura!
407. MSHEREHESHAJI:
Sawa Zuhura, umejishindia zawadi ya fulana. Haya njoo mara moja uchukue zawadi yako.
408. SFX:
WATU WANAMSHANGILIA ZUHURA ANAYEENDA KUCHUKUA FULANA YAKE.
409. MSHEREHESHAJI:
Haya shika fulana yako.

410. ZUHURA:
(KWA FURAHA) Asante.
411. MSHEREHESHAJI:
Jamani ebu mpigieni makofi Zuhura kwa mara nyingine.

412. SFX:
WATU WANAPIGA MAKOFI.
413. MSHEREHESHAJI:
Sawa, sasa naanza maswali magumu kidogo kwa sababu nina zawadi chache zimebaki na watu wachache tu ndio wanaweza kuondoka na zawadi hizo. Swali linalofuata….Nitajie vipimo sahihi vya kupanda maharage?
414. SFX:
KIMYA.
415. MSHEREHESHAJI:
Vipi jamani? Kuna mtu anataka kujibu? Sawa, nitawasaidia na hili. Kwanza kabisa kuna aina mbili za kuweka vipimo. Kwanza kabisa ukipanda maharage kama zao pekee, kipimo sahihi ni sentimeta 50 baada ya kila mstari. Katikati ya mistari, inabidi upande mbegu mbili baada yakila sentimita 20 au mbegu moja baada ya kila sentimita 10. Na kipimo kingine ni pale unapopanda maharage na mazao mengine kama mahindi. Tuseme unapanda maharage na mahindi…unahitaji kupanda mahindi kwa sentimita 75 baada ya kila mstari na kupanda maharage katikati ya mahindi.
416. GRACE:
Nina swali.
417. MSHEREHESHAJI:
Ndio.

418. GRACE:
Utatumia nini kupimia?
419. MSHEREHESHAJI:
Kama hauna utepe wa kupimia, unaweza kutunga visoda kwenye kamba kwa kufuatisha vipimo. Na sasa kwa swali la mwisho kabla ya mapumziko, mtu anitajie manufaa ya hivi vipimo?
420. GRACE:
Inasaidia maharage kustawi kwa uhuru bila ya kushikamana kwa pamoja na pia inasaidia kuokoa muda katika kuondoa majani na kwenye mavuno. Pia wakulima huwa hawapandi kwa wingi kwa hiyo inasaidia kuongeza mimea ambayo itaongeza mavuno.
421. MSHEREHESHAJI:
Safi sana, lakini kabla hujachukua zawadi yak, nina swali moja….Ni wakati gani mzuri wa kuondoa majani na mimea isiyohitajika?
422. SFX:
GRACE ANABAKI KIMYA.
423. MSHEREHESHAJI:
Hujui jibu?

424. GRACE:
Hapana sijui.
425. MSHEREHESHAJI:
Sawa acha nikusaidie na hilo kwa sababu ulishajibu swali nililokuuliza…Muda muafaka wa kuondoa majani na mimea isiyohitajika ni wiki mbili baada ya kupanda mbegu ya maharage yako na kwa mara ya pili ni kati ya wiki tano au sita baada ya kupanda. Sawa mpigieni makofi dada hapa jamani!
426. SFX:
WATU WANAMPIGIA MAKOFI GRACE.
427. CONTROL:
Mshereheshaji.

 

428.
Scene 9
429. Sehemu:
Nje. Nyumbani kwa Farida. Usiku.
430. Utambulisho wa kipengele:
Mlango unagongwa.

431. Wahusika
: Afande Kaifa, Zuhura, Sifa, Hafsa, Farida, Jenny, Vumi.

432. SFX:
MLANGO UNAGONGWA.
433. AFANDE KAIFA:
Faridaaaaa!
434. SFX:
AFANDE KAIFA ANAENDELEA KUGONGA MLANGO.
435. AFANDE KAIFA:
Faridaa!
436. SFX:
MLANGO UNAFUNGULIWA.
437. SIFA:
Shikamoo baba!
438. ZUHURA:
Shikamoo baba!
439. AFANDE KAIFA:
Marahaba! Kwanini mmefunga mlango na mama yenu yuko wapi?
440. SIFA:
Ametoka.
441. AFANDE KAIFA:
Ametoka kivipi?
442. ZUHURA:
Ametuambia kama ukimuulizia yupo kwa mama mdogo Jenny.
443. AFANDE KAIFA:
Kwa mama mdogo Jenny? Huyu mwanamke amechanganyikiwa? Mmekula?
444. SIFA:
Ndio.
445. AFANDE KAIFA:
Mlienda na mama yenu kwenye hilo tamasha?
446. ZUHURA:
Ndio!
447. AFANDE KAIFA:
Na mlirudi saa ngapi?
448. ZUHURA:
Sio muda mrefu. Tulivyorudi alitupa chakula, akabadilisha nguo alafu akatoka.
449. SFX:
KAIFA ANATUPA VITU NDANI YA NYUMBA KWA HASIRA.
450. AFANDE KAIFA:
(KWA HASIRA) Huyu mwanamke mpuuzi! Leo ndio atajuta siku yake ya kuzaliwa!
451. SFX:
HASIRA ZA AFANDE KAIFA ZINAMSABABISHA HAFSA AANZE KULIA.
452. AFANDE KAIFA:
Haya muangalieni mdogo wenu. Naenda kumtafuta mama yenu.
453.
PUNGUZA SAUTI HATUA KWA HATUA
454.
ONGEZA SAUTI HATUA KWA HATUA
455. SFX:
AFANDE KAIFA ANAGONGA MLANGO KWA HASIRA.
456. SFX:
VUMI ANAFUNGUA MLANGO.
457. VUMI:
(KWA MSHANGAO) Oh! Bwana Kaifa! Imekuwaje tena?
458. AFANDE KAIFA:
Mke wako yupo?
459. VUMI:
Ndio.
460. JENNY:
(AKIKARIBIA MIC) Eh! Kaifa! Kuna nini tena?
461. AFANDE KAIFA:
Mke wangu yupo hapa?
462. JENNY:
Hapana. Kwanini?
463. AFANDE KAIFA:
Alikuwepo hapa?
464. JENNY:
(HAJUI CHA KUSEMA) Kwa kweli…kusema kweli…aliku…ali…
465. VUMI:
(ANAINGILIA KATI) Sikiliza, hakuwepo hapa kwa sbabu nilikuwepo hapa siku nzima.
466. AFANDE KAIFA:
Sawa basi mkimuona mwambieni atafute sehemu nyingine ya kulala kwa sababu sitaki kumuona tena.
467. JENNY:
(AMECHANGANYIKIWA) Nini?….nini…nini kimetokea?
468. AFANDE KAIFA:
Amewaacha watoto wangu peke yao nyumbani kwao na alipoenda yeye na Mungu wake ndio wanajua. Alafu bila ya haya akawaambia wanangu kwamba yuko hapa.
469. JENNY:
Subiri Kaifa… labda kuna sababu.
470. SFX:
KIFA ANAANZA KUONDOKA.
471. AFANDE KAIFA:
Sitaki kusikia! Mwambie akae mbali na mimi na wanangu! Na kama anajijali na kwa usalama wake basi ni bora asirudi kabisa.
472. JENNY:
Subiri! Kaifa! Kaifa! Kaifa!
473. SFX:
KAIFA ANABAKI KIMYA HUKU AKIISHIA KWENYE USIKU WA GIZA.
474. CONTROL:
Afande Kaifa

Acknowledgements

Imechangiwa na: Kheri Mkali, mwandishi wa muongozo, Dar es Salaam, Tanzania.
Imepitiwa na: Frederick Baijukya, mtaalamu wa kilimo na mratibu wa shirika la N2Africa Tanzania, Shirika la kilimo kwa nchi kitropiki (IITA), East Africa Hub, Dar es Salaam, Tanzania.

Kazi hii imewezeshwa kwa masaada wa Shirika la utafiti, lililopo Ottawa, Kanada (International Development Research Centre, Ottawa, Canada) www.idrc.ca, na msaada wa kifedha kutoka serikali ya Kanada, kupitia idara ya masuala ya kimataifa, (Global Affairs Canada) www.international.gc.ca.
gaclogoidrc