Kutoka kwa umasikini wa wakati wa hedhi hadi usawa wakati wa hedhi: Kuwaweka wasichana salama na wenye furaha

Ujumbe kwa mtangazaji

Maelezo kwa watangazaji:

Hedhi ni sehemu ya asili ya mzunguko wa uzazi wa wanawake na msichana ambapo damu ya hedhi hutoka kupitia uke. Utokaji huu wa damu hutokea, kwa wastani, kwa siku mbili hadi saba wakati wa mzunguko wa hedhi. Mzunguko wa hedhi unaweza kutokea kila baada ya siku 21-35 wakati wa umri wa uzazi. Katika sehemu nyingi za ulimwengu, hedhi ni jambo la mwiko, na, kwa sababu ya imani za kidini na za kimapokeo, huenda likaonwa kuwa jambo la kuaibisha, la aibu, na “chafu.”

Unyanyapaa kama huo unamaanisha kuwa wasichana wengi waliobalehe wanaweza kutokuwa tayari wamejiandaa kukabiliana na hedhi zao au kuelewa jinsi ya kudhibiti. Kulingana na Benki ya Dunia, takriban wanawake na wasichana milioni 500 duniani kote wanakosa nyenzo za kutosha za kuhakikisha usafi wakati wa hedhi, ikiwa ni pamoja na taulo za kike au pedi, sabuni na maji, na pia hawana vifaa vya kubadilisha, kusafisha, na kutupa bidhaa ambazo tayari wameshazitumia. Ni muhimu sana wasichana wadogo kujua jinsi ya kudhibiti mzunguko wao wa hedhi kabla ya kipindi chao cha kwanza. Hii inahitaji kwamba wasichana wawe na uwezo wa kupata taarifa zinazolingana na umri na kwa wakati. Kwa bahati mbaya, hawapati taarifa nzuri kuhusu usafi wakati wa hedhi kutokana na ukosefu wa rasilimali na vikwazo vya kijamii vinavyofanya kuzungumza juu ya masuala haya kuwa ni vigumu.

Taarifa zisizo sahihi au ukosefu wa taarifa za jinsi ya kusimamia vyema hedhi inaweza kusababisha kushindwa kuzingatia swala la usafi wakati wa hedhi, ambayo inaweza kusababisha ugonjwa na kukosa shule. Kulingana na ripoti ya mwaka 2014 kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, msichana mmoja kati ya 10 katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara hukosa shule wakati wa mzunguko wao wa hedhi. Watafiti wa UNESCO pia waligundua kuwa huduma bora za usafi na elimu ya afya ya uzazi kwa wasichana huboresha mahudhurio shuleni.

Katika program hii, tunasikia hatua zinazochukuliwa nchini Kenya na Uganda kuhusu afya ya hedhi na usafi. Tunazungumza na Florence Kamaitha wa Pad Heaven na Geoffrey Businge wa AFRIpads kuhusu pedi zao zinazoweza kuoshwa na kutumika tena, na pia jinsi wanavyowapa wasichana habari kuhusu hedhi. Pia tunasikia kutoka kwa wasichana wawili wa Kikenya wanaoitwa Quinter na Lucy, ambao hawawezi kufurahia shughuli za shule kwa sababu hawana pedi za zinazofaa kuwaweka safi wakati wa hedhi.

Iwapo ungependa kuandaa programu sawa nah ii kuhusu masuala ya afya ya hedhi kama vile “umaskini wa kipindi” ulioonyeshwa katika mwongozo huu wa utangazaji, unaweza kutumia mwongozo huu kukuongoza. Ukiamua kuwasilisha mwongozo kwenye kipindi chako cha kawaida, unaweza kutumia waigizaji wa sauti au watangazaji wa redio kuwakilisha wahojiwa.

Ikiwa ungependa kuunda programu kuhusu masuala ya hedhi, zungumza na daktari wa afya ya uzazi au mfanyakazi wa kijamii. Kwa mfano, unaweza kuwauliza maswali yafuatayo:

  • Kwa nini ni muhimu kuzungumza waziwazi kuhusu hedhi?
  • Mbali na taulo zinazoweza kutupwa, ni njia gani nyingine mbadala za pedi salama zipo?
  • Je, ni baadhi ya taratibu gani nzuri za kuzingatia usafi wakati wa hedhi kwa maeneo ya vijijini na mijini?
  • Unawezaje kuhimiza jamii kujihusisha na afya ya hedhi (shuleni na nyumbani)?

 

Muda wa programu nzima ikijumuisha utangulizi na ufungaji: dakika 20-25.

Script

SAINI TUNE

MTANGAZAJI:
Wasichana wengi barani Afrika hukosa shule wakati wa hedhi kwa sababu hawawezi kumudu taulo za kujisitiri. Utafiti wa hivi majuzi wa Benki ya Dunia unaripoti kwamba, kwa wastani, wasichana hukosa shule kwa siku nne kila baada ya wiki nne.

Katika program ya leo, tunasikia kutoka kwa wasichana ambao wanaathiriwa na hili, na pia tunajifunza kuhusu pedi za bei nafuu na zinazoweza kutumika tena ambazo zinaweza kuwa suluhisho mojawapo kwa tatizo la upatikanaji wa bidhaa za hedhi. Karibu kwenye programu

Zingatia wanawake na wasichana. Mimi ni _____.

SFX
KENGELE INALIA, SAUTI ZA WATOTO WAKICHEZA. SAUTI JUU KISHA CHINI.

MTANGAZAJI:
Ni saa tatu alasiri katika shule ya msingi ya Soda katikati mwa kitongoji duni cha Kibera jijini Nairobi. Quinter mwenye umri wa miaka kumi na nne na rafiki yake Lucy huketi ndani ya darasa lao na kutazama wanafunzi wenzao wakielekea kwenye uwanja wa michezo wa karibu kwa ajili ya michezo. Leo, Lucy hawezi kucheza na Quinter yuko hapa kumuunga mkono rafiki yake.

LUCY:
Inanihuzunisha kwa sababu siwezi kucheza kama wengine. Mwalimu akija na kuniuliza kwa nini siko nje, nitatoa kisingizio … naona aibu kumwambia ukweli.

QUINTER:
Wakati mwingine, ni bora kukaa nyumbani wakati uko kwenye siku zako. Tatizo pekee ni kwamba unapaswa kuwaeleza wazazi wako. Inatia aibu sana na wakati mwingine baba yangu hataki hata kuelewa.

MTANGAZAJI:
Lucy na Quinter ni wasichana wawili tu kati ya wengi barani Afrika ambao hupata aibu wakati wa siku zao kwa angalau siku mbili hadi saba kwa mwezi. Niliketi na wasichana na tulizungumza zaidi kuhusu kile wanachotumia wakati wa siku zao za hedhi na jinsi inavyowafanya wahisi. Nilimuuliza Lucy anatumia nini wakati wa siku zake.

LUCY:
Mama yangu hana uwezo wa kununua pedi kutoka kwenye maduka makubwa, kwa hivyo wakati mwingine mimi hutumia tishu au blanketi.

MTANGAZAJI:
Huogopi kwamba zinaweza kuanguka?

LUCY:
(ANACHEKA) Wakati mwingine zinadondoka na wavulana wanatucheka.

QUINTER:
(ANACHEKA) Ndio maana tunakaa hapa badala ya kucheza na wengine.

MTANGAZAJI:
Je, unaziosha baada ya kutumia

LUCY:
Wakati mwingine, lakini kuna nyakati ambapo hakuna maji hivyo ni lazima kusubiri hadi nipate maji. Lakini kuna vipande vya nguo ambavyo ni vichafu na vinaweza kukuathiri.

MTANGAZAJI:
Vipi kuhusu wewe, Quinter, unatumia nini?

QUINTER:
Mimi hutumia vipande vya nguo kama Lucy, au nakata kipande cha sponji kutoka kwa godoro

MTANGAZAJI:
Na unazihifadhije?

QUINTER:
Chini ya kitanda, kwa sababu sitaki dada yangu mdogo na kaka kuiona. Hii inamaanisha kuwa inaweza kuwa chafu ninapotaka kuitumia tena na huwa naogopa inaweza kuniathiri.

MTANGAZAJI:
Wanawake na wasichana katika nchi mbalimbali duniani ambao hawana uwezo wa kununua bidhaa za hedhi au hawana uwezo wa kuzipata wanalazimika kutumia nguo kuukuu, karatasi, na hata majani ili kudhibiti kutokwa na damu wakati wa hedhi. Hali hii ni mbaya zaidi kwa wasichana wa shule kama Lucy na Quinter kwa sababu sio tu kwamba hukosa shule siku za hedhi, lakini nyenzo hizi hazina usafi na zinaweza kusababisha matatizo kama vile maambukizi ya njia ya uzazi. Lakini taulo zilizopo ni ghali sana kwa wazazi wao. Ili kujua jinsi taulo za usafi zilivyo nafuu au ghali, nilienda kwenye maduka makubwa ya karibu.

SFX:
SAUTI ZA MADUKA MAKUBWA (MASHINE YA TELA, KOINI, NA SAUTI ZA WATU WANANUNUA)

MTANGAZAJI:
Nimesimama nnje ya maduka makubwa na ninaweza kuhesabu angalau 2, 3, 4 …. Chapa/aina 7 tofauti za taulo za usafi au pedi za kuanzia dola moja hadi dola sita za kimarekani kwa pakiti ya pedi nane zinazoweza kutumika. Hiyo ni gharama ya robo kilo ya nyama katika kaya ya Kenya, na ni kaya chache sana ambazo zinakuwa na nyama kwenye menyu yao. Hii ina maana kwamba taulo za usafi ni jambo la mwisho ambalo familia nyingi zingepanga bajeti.

Kwa hivyo, kuna njia mbadala za bei nafuu za taulo za usafi zinazoweza kutumika? Nilizungumza na Florence Kamaitha, mwanzilishi wa shirika, Pad Heaven, na mtengenezaji wa pedi za kuosha za Malkia nchini Kenya kuhusu kazi yake ya kuhimiza usafi wakati wa hedhi. Nilianza kwa kuuliza kwa nini anavutiwa na afya ya hedhi.

FLORENCE KAMAITHA:
Nilianza jitihada hizi mwaka wa 2012 baada ya kutembelea shule iliyopo kijijini na kugundua kuwa ni wavulana pekee waliokuwa uwanjani. Nilipouliza, niliambiwa kuwa wasichana wengi walikuwa nyumbani kwa sababu walikuwa wapo kwenye siku zao na hawawezi kumudu kununua taulo za kujisitiri. Kuanzia hapo, niliamua kwamba nitawapa wasichana wengi iwezekanavyo njia ya kufanya kipindi wanapokuwa kwenye siku zao.

MTANGAZAJI:
Kwa nini usafi wakati wa hedhi ni muhimu kwa wasichana na wanawake

FLORENCE KAMAITHA:
Wanawake na wasichana nchini Kenya wanakosa vifaa vya kutosha vya kusimamia usafi wakati wa hedhi. Hii ni pamoja na kupata maji safi ya kujisafisha wakati wa hedhi, vyoo safi vinavyofungika au vyoo vya shimo ambapo wanaweza kubadilisha, njia sahihi ya kutupa pedi zao zilizotumika, na bidhaa za bei nafuu na bora kudhibiti mtiririko wao wa damu. Usafi mzuri wa hedhi huzuia maambukizi ya bakteria na kuwasha ngozi pamoja na ugonjwa wa mshtuko wa sumu. Wasichana na wanawake pia wanakosa taarifa muhimu kuhusiana na usafi na afya ya hedhi.

 

MTANGAZAJI:
Je, Taarifa kuhusu afya ya hedhi huwasaidiaje?

FLORENCE KAMAITHA:
Taarifa za afya ya hedhi zinaweza kuwaongoza wanawake na wasichana kuhusu idadi ya saa za kukaa na pedi, aina sahihi za bidhaa za kutumia, na njia za kuzitupa. Wanapokuwa na taarifa sahihi kuhusu hedhi, wasichana na wanawake wanaweza kufanya maamuzi yenye afya na maarifa kuhusu mwili wake. Wasichana kutoweza kusimamia usafi wa hedhi shuleni kunasababisha utoro shuleni, ambao una gharama kubwa za kiuchumi kwa maisha yake na kwa nchi.

MTANGAZAJI:
Kwa hivyo Pad Heaven inafanya nini kubadilisha hali hiyo?

FLORENCE KAMAITHA:
Wakati wa programu zangu za kufika shuleni, niliona kile wasichana wanatumia pale wanapokuwa kwenye siku zao. Wengi walikuwa wakitumia vipande vya nguo vilivyokunjwa. Kwa kuwa wasichana wengine tayari walikuwa wakitumia nguo na kuzifua baada ya kuzitumia, niliamua kutengeneza pedi isiyoweza kuvuja, salama na inayoweza kutumika tena kwa bei nafuu. Pedi hizo zinagharimu shilingi za Kenya 650, ambazo ni takriban dola sita za Kimarekani na zinaweza kutumika tena kwa mwaka mmoja.

Pia nilitambua kwamba wasichana wengi hubalehe wakiwa hawana taarifa nyingi kuhusu hedhi, kwa hiyo nilifanya dhamira yangu kuzungumza juu ya mada ya “mwiko” ambayo wengi hawazungumzii. Nilichapisha kitabu juu ya usafi wakati wa hedhi kwa wasichana. Kitabu kinaelezea taarifa kuhusu kubalehe, hedhi, matumizi na utupaji wa pedi, usafi, lishe, udhibiti wa maumivu, pamoja na hadithi zinazohusiana na masuala ya hedhi.

MTANGAZAJI:
Je, umesambaza pedi ngapi hadi sasa?

FLORENCE KAMAITHA:
Nimeajiri wanawake nane na kwa pamoja tumezalisha zaidi ya pedi 50,000 zinazoweza kufuliwa na kutumika tena.

MTANGAZAJI:
Tunazungumzia afya ya hedhi na usafi katika kipindi chetu cha leo. Hapo awali katika programu, tulisikia kutoka kwa wasichana wawili wa shule ya msingi jijini Nairobi kuhusu vifaa wanavyotumia wakati wanapokuwa kwenye siku zao. Pia tulisikia kutoka kwa Florence wa Pad Heaven kuhusu pedi inayoweza kufuliwa na kutumika tena ambayo anatengeneza na kazi yake ya kutoa taarifa kuhusu afya ya hedhi na usafi kwa wanawake na wasichana. Kisha, tutavuka hadi Uganda na kusikia kuhusu mipango mingine kuhusu afya ya hedhi na usafi. Lakini kwanza muziki tupate kidogo.

MUZIKI

MTANGAZAJI:
Karibu Katika kipindi cha Kuangazia Wanawake na Wasichana. Katika program ya leo, tunazungumzia afya ya hedhi na usafi. Nchini Uganda, kufikia mwaka 2016, ni asilimia 21 pekee ya wasichana walioandikishwa katika shule za sekondari na asilimia 7 katika shule za upili, ikilinganishwa na asilimia 91 katika shule za msingi. Watafiti wanaamini kuwa gharama ya bidhaa za usafi na ugumu wa kudhibiti vipindi vya hedhi vina mchango mkubwa katika kuwazuia wasichana wasiende shule za sekondari.

AFRIpads ni shirika moja nchini Uganda ambalo linatoa taulo za nguo zinazoweza kufuliwa, zinazoweza kutumika tena kwa wanawake na wasichana na pia kufanya kazi na wauguzi wa afya ya jamii waliopatiwa mafunzo ili kuzungumza na wasichana kuhusu afya ya hedhi na usafi. Nilizungumza na Geoffrey Businge, meneja wa AFRIpads kuhusu kile ambacho shirika linafanya.

MTANGAZAJI:
Ni vizuri kuzungumza na mwanamume ambaye anahusika katika afya ya hedhi na usafi. Ni nini kinakuchochea kujihusisha na masuala haya?

GEOFFREY BUSINGE:
Katika kazi yangu, nimeona wanawake wakiteseka wakati wa hedhi kwa sababu wanaume hawaelewi mchakato unaotokea kwa mwanamke kila mwezi. Nilijitwika jukumu la kuwasaidia wanaume na wavulana daima kuelewa kwa nini wanawake na wasichana wanahitaji usaidizi wao katika kipindi hiki, na pia kuwasaidia wasichana kuelewa mchakato wa hedhi.

MTANGAZAJI:
Nipe mfano wa jinsi ulivyoona wanawake na wasichana wakitendewa wakati wa hedhi.

GEOFFREY BUSINGE:
Nimeiona shuleni: wavulana wakati mwingine huwadhihaki wasichana kwa sababu hawaelewi kabisa kile ambacho wasichana wanapitia. Nimeiona pia nyumbani: baadhi ya wanaume wanaamini kuwa damu ya hedhi ni chafu na wanajitenga na mwanamke wakati wa hedhi. Katika hali ambapo mwanamke ana uchungu na hawezi kutekeleza majukumu yake ya nyumbani kama inavyotarajiwa, anaweza kukabiliana na unyanyasaji wa kimwili na matusi, ambayo ni aina zote mbili za unyanyasaji wa kijinsia.

MTANGAZAJI:
Je, unashughulikiaje hili kama mwanamume anayefanya kazi katika eneo la Afya ya hedhi?

GEOFFREY BUSINGE:
Kwanza, tunazungumza na wasichana na kuwasaidia kuelewa kile wanachopitia na jinsi ya kujisaidia wao wenyewe wakati wakiwa kwenye siku zao. Kisha tunazungumza na wavulana na wanaume na kuwasaidia kuelewa kwamba hedhi ni ya kawaida na ya asili na si chafu—na hivyo wanawake na wasichana hawapaswi kutendewa tofauti wanapokuwa kwenye siku zao.

MTANGAZAJI:
Je, umeona mabadiliko yoyote?

GEOFFREY BUSINGE:
Naam, imechukua muda mrefu, lakini sasa tunaona tofauti kidogo, hasa shuleni. Tunawahimiza walimu kuwa makini katika kuwaambia wavulana kuwa huu ni mchakato wa asili. Pia tumezihimiza shule kuwasaidia wasichana ili wasiachwe nje ya masomo na shughuli za ziada wanapokuwa katika hedhi. Na tumeona mabadiliko. Tumewaona wavulana wakiketi kwenye mazungumzo ya hedhi na kujitolea kuwasaidia wasichana inapobidi. Hilo lilikuwa halijasikika miaka kadhaa nyuma. Nyumbani, sasa tunaona baadhi ya akina baba wakiwapa binti zao pesa za kununulia taulo za kujisitiri, lakini hili si jambo la kawaida sana.

MTANGAZAJI:
Je, AFRIpadi zinazoweza kufuliwa na kutumika tena zinawasaidia wasichana?

GEOFFREY BUSINGE:
Ndiyo. Katika suala la kuwasaidia wasichana kuendelea na maisha yao ya kawaida wakati wa kupata hedhi, zinafanya kazi. Hii ni kweli hasa katika maeneo ambayo kuna umaskini uliokithiri na familia haiwezi kutoa taulo za usafi.

MTANGAZAJI:
Huenda wasichana wakawa na pedi zinazoweza kutumika tena, lakini bado wanahitaji kupata maji, vyoo, na vifaa vya usafi—na katika hali fulani, njia ya kutupa taka za hedhi. Je, hili linashughulikiwaje?

GEOFFREY BUSINGE:
Masuala ya afya ya hedhi na usafi yanaweza tu kushughulikiwa kwa ufanisi kupitia mbinu ya kujumuisha sekta mbalimbali. Tutatoa pedi zinazoweza kutumika tena, lakini pia tunahitaji washirika katika sekta ya maji, usafi wa mazingira, na usafi na serikali ili kutoa maji safi na usafi wa mazingira. Kwa sasa, tunaweza tu kusambaza pedi zinazoweza kutumika tena katika maeneo ambayo wasichana na wanawake wanaweza kupata maji. Ikiwa sote tutafanya bidii yetu, tunaweza kutatua maswala yote ya umasikini na aibu wakati wa hedhi.

MTANGAZAJI:
Mengi yanahitajika kufanywa kuwasaidia wasichana na wanawake katika kipindi chao cha hedhi, lakini kumekuwa na maendeleo katika sehemu mbalimbali za bara. Nchi nyingi katika Afŕika Kusini mwa Jangwa la Sahaŕa zimeanza mipango ya kutoa pedi kwa wanawake. Kenya ilikuwa ya kwanza kupunguza gharama ya bidhaa za usafi kwa wasichana wa vijijini na kuondoa ushuru wa ongezeko la thamani kwa bidhaa za usafi wa hedhi. Florence kutoka Pad Heaven anaelezea baadhi ya hatua zilizopigwa na Kenya.

FLORENCE KAMAITHA:
Kenya ilizindua sera ya usafi wa hedhi mwaka 2019. Inaeleza kile kinachofaa kufanywa ili kuhakikisha kuwa wasichana na wanawake wanapata kile wanachohitaji ili kujihifadhi wakati wa hedhi. Serikali pia ilianzisha mpango wa pedi za bure shuleni, ambazo zilihudumia idadi kubwa ya wasichana wa shule kwa miaka michache. Hata hivyo, katika bajeti ya 2021-2022, hakuna fedha zilizotengwa kwa ajili ya usimamizi wa masuala ya hedhi. Ninaamini mengi zaidi yanaweza kufanywa shuleni na sehemu za kazi kwa kutoa bidhaa na vifaa vya hedhi ili kuhakikisha kwamba wasichana na wanawake wanashughulikia siku zao kwa usafi, uhuru, heshima, na bila unyanyapaa au miiko.

MTANGAZAJI:
Kwa Lucy na Quinter, wasichana wenye umri wa miaka 14 kutoka Kibera, wanachotaka tu ni kuweza kusalia darasani na kucheza kama wanafunzi wenzao wengine. Lakini wanaweza tu kufanya hivyo ikiwa wanaweza kupata pedi, maji, na usafi wa mazingira, na sahihi juu ya afya ya hedhi na usafi.

Je, ungependa kutumia pedi kama wasichana wengine, Quinter?

QUINTER:
Ndio, hivyo tutaweza kukaa shuleni, kucheza na marafiki zetu, na tusiwe na wasiwasi kuhusu pedi kuanguka.

MTANGAZAJI:
Na hivyo ndivyo tunatarajia kila msichana barani Afrika ataweza kufanya anapokuwa kwenye siku zake. Maneno hayo ya Quinter, msichana mdogo kutoka vitongoji duni vya Kibera ambaye anatarajia kutumia pedi siku moja, yanatufikisha mwisho wa programu yetu.

Leo, tulikuwa tunazungumza juu ya afya ya hedhi na usafi. Tulisikia kutoka kwa Florence Kamaitha wa Pad Heaven na Geoffrey Businge wa AFRIpads kuhusiana na pedi zao zinazoweza kufuliwa na kutumika tena na jinsi wanavyowapa wasichana taarifa zinazohitajika sana kuhusiana na hedhi. Pia tulisikia kutoka kwa wasichana wawili wadogo, Quinter na Lucy, ambao hawana huduma ya afya ya hedhi na bidhaa za usafi na vifaa. Jiunge nasi tena wiki ijayo kwa habari zaidi na hadithi kuhusu Angazia Wanawake na Wasichana. Mimi ni…

Acknowledgements

Shukrani

Imechangiwa na: Winnie Onyimbo, Trans World Radio, Nairobi, Kenya

Imehaririwa na: Florence Kamaitha, Mwanzilishi wa PadHeaven Initiative; Diana Nelson na Elena Steinhaus, Days for Girls
 

Rasilimali hii imeandaliwa kwa  msaada wa ruzuku kutoka kwa M. L. Geyer

Information sources

Mahojiani:

Mr. Geoffrey Businge, Maneja biashara na ushirikiano wa kanda, Afripads, mahojiano yaliyofanyika December 15, 2021

Florence Kamaitha, Mwanzilishi wa PadHeaven Initiative, mahojiano yaliyofanyika December 8, 2021

Mahojiano na Lucy pamoja na Quinter yaliyofanyika November 18, 2021

Chanzo cha taarifa

Tovuti ya AFRIpads: https://www.afripads.com/

Tovuti ya Pad Heaven Initiative: https://padheaven.org/

Tofaris, E., 2020. Keeping African girls in school with better sanitary care. The Impact Initiative. https://opendocs.ids.ac.uk/opendocs/bitstream/handle/20.500.12413/13575/KeepingAfricanGirlsInSchool.pdf?sequence=1&isAllowed=y

UNESCO, 2014. Puberty education & menstrual hygiene management. Good policy and practice in health education, Booklet 9. https://unesdoc.unesco.org/ark:/48223/pf0000226792

Verma, R., 2019. Menstrual hygiene in Africa: No pad or no way to dispose it. Down to earth.  https://www.downtoearth.org.in/news/waste/menstrual-hygiene-in-africa-no-pad-or-no-way-to-dispose-it-63788

World Bank, 2018. Menstrual Hygiene Management Enables Women and Girls to Reach Their Full Potential. https://www.worldbank.org/en/news/feature/2018/05/25/menstrual-hygiene-management