Kamati za maji zinasaidia wanavijiji, hususan wanawake na watoto

Ujumbe kwa mtangazaji

Maji ni ya muhimu na ni moja kati ya mahitaji muhimu kwa uhai wa binadamu, na kwa kawaida yanalinganishwa na “uhai.” Hata hivyo, upatikanaji na salama wake ni vitu viwili muhimu kwa ajili ya maisha bora. Unatikanaji wa maji safi ni jambo muhimu sana hasa katika kipindi hiki tunapokabiliana na matatizo ya mabadiliko ya tabia nchi. Katika maeneo mengi, hasa vijijini, maji kidogo yanayopatikana huko, mara nyingi huwa sio safi na yanapatikana umbali mrefu kutoka katika makazi ya wanakijiji. Watoto ndio waathirika wakubwa wa hali hii. Uhaba wa maji, na mazingira machafu, mara nyingi husababisha maradhi na vifo na hata vifo kwa watoto kutokana na magonjwa ya kuharana na magonjwa mengine yanayotokana na uchafu.

Wanawake, na kwa kiasi Fulani watoto, wanawajibu wa kutafuta maji kwa matumizi ya nyumbani, kuyatoa toka pale yanapopatikana hadi nyumbani, kuyatunza hadi pale yatakapotumika, kuyatumia kupikia, kufanyia usafi, na kunyweshea mifugo nyumbani. Kunapokuwa na upungufu wa maji, wanaoteseka ni wanawake na watoto, ambapo inawalazimu kutumia saa sita kwa siku wakitembea kutafuta maji, ambayo yanaweza kuwa sio salama. Ni vema watangazaji wakatambua tatizo hili na kutangaza kuhusu uhifadhi wa maji safi.

Muswada huu kutoka nchini Tanzania unaonyesha juhudi za pamoja za wakulima kijijini katika eneo lenye upungufu wa maji tangu kijiji hicho kilipoanzishwa miaka ya 1960. Hakuna vyanzo vya maji kijijini; wanawake na watoto (hasa wa kike) wanatembea umbali wa kilometa nane kutafuta maji. Maji yanayochotwa si salama, kwa sababu chanzo cha maji ni bwawa tu lililochimbwa ardhini ambalo maji yake hujikusanya wakati wa mvua. Kwa vile bwawa hili linatumiwa na mifugo kunywa maji, mara kadhaa mifugo huingia ndani na kuchafua maji. Magonjwa yanayotokana na uchafu wa maji yamekuwa ni ya kawaida kijijini hapo.

Baada ya kuteseka kwa miaka mingi, wakisubiri serikali kuwapatia maji, wanakijiji kwa pamoja waliamua kutatua tatizo lililokuwa linawakabili. Walichimba bwawa kuvuna maji wakati wa masika. Wanaweza kutumia maji haya ya kwenye bwawa kwa miezi mitatu baada ya msimu wa mvua kumalizika. Pia serikali ya kijiji inakusanya fedha kutoka kwa wanakijiji kulipia gharama za uchimbaji wa visima ili waweze kupata maji safi kijijini kwao.

Muswada huu unaweza kuwekwa katika mazingira ya kijijini, mahali ambapo maji safi na salama ni tatizo, na ambapo wanakijiji hawajapata msaada wowote kutoka serikalini au katika mashirika yasiyo ya kiserikali na ambapo sasa wanalazimika kutumia juhudi binafsi kutatua tatizo la maji kijijini kwao.

Muswada huu unatokana na mahojiano ya kweli, yaliyofanywa kwa kiongozi mmoja wa kijiji nchini Tanzania. Ili kuutumia vizuri muswada huu katika kituo chako cha redio, unaweza kutumia msanii, kuwakilisha mwenyekiti wa kijiji, na kubadilisha maneno katika muswada ili yaende sambamba na mazingira yenu. Kama utafanya hivyo, tafadhali hakikisha umwewaambia wasikilizaji mwanzoni mwa kipindi kuwa sauti hizo ni za waigizaji, na kwamba kipindi hiki kimewekwa katika mazingira maharia, yenye msingi wa mahojiano halisi.

Script

Piga kiashirio cha kipindi kwa sauti ya chini

Mtangazaji:
Mpendwa msikilizaji, karibu katika kipindi cha leo. Inafahamika vizuri kuwa maji ni moja kati ya mahitaji muhimu kwa uhai wa maisha ya mwanadamu. Maji ni lazima yawe safi. Uhaba wa maji unasababisha magonjwa ya ngozi kwa vile watu wanakuwa hawaogi. Hali kadhalika, maji yasiyo salama yanaweza kusababisha magonjwa ya milipuko kama vile kuharisha na magonjwa ya matumbo. Maji pia ni muhimu kwa mifugo yetu, umwagiliaji katika mashamba, na hata kutengenezea matofari kwa ajili ya ujenzi wa nyumba zetu. Hata hivyo maji yameanza kuwa adimu katika maeneo mengi ya Tanzania, ni vijiji vichache vyenye maji safi na salama. Kwa hiyo basi ni muhimu kwa kila mmoja wetu kuchukua tahadhari.

Piga muziki wa ala, na upunguze taratibu hadi mwisho

Mtangazaji:
Katika jipindi chetu cha leo, tutazungumza na Bwana Costa Francis, ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya maji kutoka katika kijiji cha Talawanda kata ya Ludiga, wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani. Bwana Francis atatueleza jinsi kamati ya maji ilivyosaidia juhudi za kijiji chao kutatua tatizo la maji ambalo limekuwa likiwakabili wakazi wa kijiji hicho tangu miaka ya 1960 kijiji hicho kilipoanzishwa. Nataraji, kwa kumsikiliza Bwana Francis, tutajifunza mengi, na yatatuhamasisha kufanya juhudi binafsi kutatua matatizo yetu katika maeneo yetu.

Piga muziki wa ala, halafu upunguze taratibu hadi mwisho.

Mtangazaji:
Karibu katika studio zetu Bwana Francis.

Francis:
Asante.

Mtangazaji:
Bwana Francis unaweza kuwaeleza wasikilizaji hali ya maji ilivyo katika kijiji cha Talawanda?

Francis:
Maji yana athari chanya kwa kila mmoja wetu, kwa sababu maji ni uhai. Watoto, wanaume, wanawake na hata wanyama – wote tunaathiriwa na maji kwa njia moja ama nyingine. Naweza kutaja mifano michache. Watoto ambao hawaogi kwa siku kadhaa wanapata magonjwa ya ngozi. Familia nyingi zinachelewa kula, kwa vile kina mama katika familia hizi wanatumia muda mwingi kutafuta maji. Wanawake wanapata shida zaidi kwa vile wanawajibika na shughuli zote za nyumbani.

Mtangazaji:
Kwa nini unasema wanawake wanapata shida zaidi?

Francis:
Wanawake ndio wanaotembea hadi umbali wa kilomita tisa kutoka vijijini kwao kwenda kutafuta maji wanayoyabeba kwenye vyombo vyenye lita 40. Muda ambao wanawake wanatumia kutafuta maji unawafanya washindwe kuziangalia vema familia zao pamoja na mambo mengine.

Mtangazaji:
Francis, ni kwa vipi wakulima wanaathiriwa na tatizo la ukosefu wa maji?

Francis:
Upungufu wa maji unafanya zoezi la umwagiliaji wakati wa kiangazi kuwa gumu, au wakati kunapokuwa na kipindi kirefu cha kiangazi. Mazao kama nyanya na mboga za majani yanakuwa na bei kubwa wakati wa kiangazi, lakini katika kipindi hicho hatuwezi kuyalima kwa vile kunakuwa hakuna maji ya kutosha kuyamwagilia. Mifugo kama vile ng’ombe, kondoo na mbuzi haipati maji ya kutosha kama inavyostahili. Badala yake mifugo hii inapatiwa maji mara mbili kwa wiki.

Mtangazaji:
Je kijiji chenu kina njia gani mbadala ya kutatua tatizo hili?

Francis:
Kijiji kiko katikati ya milima yenye vijito, mabondeni kuna mabwawa mawili ambayo hujaa maji yanayotoka katika vijito hivyo wakati wa mvua. Mabwawa haya yako katika maeneo ya watu. Sina hakika na ukubwa wake kwa sababu hatujayapima. Lakini nadhani yana ukubwa wa mita 200 upana na urefu nadhani ni mita kumi. Huwa tunatumia maji haya ya kwenye mabwawa mvua zinapokuwa zimekatika kuanzia mwezi Mei hadi mwezi wa nane. Baada ya muda huo kupita, wanakijiji hulazimika kutafuta maji katika maeneo mengine.

Mtangazaji:
Mnachotaje maji katika mabwawa hayo?

Francis:
Kwa ndoo.

Mtangazaji:
Je wanyama wanaruhusiwa kunywa maji moja kwa moja toka kwenye mabwawa?

Francis:
Ndiyo, na hali hii inasababisha maji kuchafuka.

Mtangazaji:
Hadi sasa mkiwa ni kamati ya maji katika kijiji chenu, mmefanya nini kutatua tatizo hili la maji kijijini?

Francis:
Kazi ya kamati ya maji kijijini ni kuratibu shughuli zinazohusiana na maji kijijini. kwanza, tunawaelekeza wanakijiji kuchimba visima vidogo. Kwa kawaida vinakuwa na ukubwa wa mita 20 kwenda chini, na upana mita tano. Tungeweza kufanya zaidi, lakini tuna uhaba wa vifaa. Kwa bahati, visima hivi vinatusaidia kupata maji, ingawa sio mengi. Hata hivyo visima hivi huwa havikauki hadi pale dalili za msimu wa mvua zinapoanza.

Mtangazaji:
Visima hivyo vinakuwa wapi? Je kila mtu anaweza kutumia maji ya visima hivyo?

Francis:
Visima hivyo viko karibu na shule ya msingi, na yeyote anayehitaji maji anaweza kwenda kuchota kisimani.

Mtangazaji:
Wanakijiji wanachotaje maji kutoka kisimani?

Francis:
Kwa kawaida maji yanayotochwa kisimani ni kwa ajili ya matumizi ya nyumbani. Wanawake hutumia vyombo vidogo au ndoo zenye ujazo wa lita tano, ambazo hufungwa kwenye kamba kubwa.

Mtangazaji:
Je kisiwa hufunikwa na kitu chochote?

Francis:
Hapana, na kuna hatari kuwa maji hayo yanaweza kuchafuliwa, au watoto wanaweza kuanguka ndani ya kisima.

Mtangazaji:
Je kamati yenu ya maji ina mpango wa kuboresha hali hii?

Francis:
Ndiyo. Tumeamua kupanua kisima na kikufunika kwa zege ili tuweze kupata maji mengi zaidi ambayo pia ni salama na ambayo yanaweza kutumika wakati wa kiangazi. Kama ikiwezekana tungependa kupata pampu ya kusukumia maji.

Mtangazaji:
Nani atafadhili maendeleo yenu hayo?

Francis:
Serikali yetu imekuwa ikituhamasisha kuwa na maendeleo yanayotokana na nguvu zetu wenyewe. Kwa hiyo kamati ya maji imeagiza kila kaya kijijini kutoa mchango wa shilingi elfu kumi, na kijiji chetu kina kaya 640 ili tupate shilingi milioni sita. Kwa hiyo tutakapokamilisha michango, tutaiomba serikali ya wilaya kutupatia msaada wa kiufundi na kifedha kukamilisha mradi wetu.

Mtangazaji:
Kwa hiyo kuna kisima kimoja tu cha kuaminika kijijini kwenu. Je mna mpango wa kuongeza visima zaidi?

Francis:
Tunafahamu kuwa hatuna maji ya kutosha. Tunafikiria kuchimba visima vingine zaidi kuzunguka kijiji. Tungependa kuwa na kisima kwa kila kitongoji na kijiji chetu kina vitongoji vitatu. Tuna mpango pia wa kupanua visima tulivyonavyo.

Mtangazaji:
Mnahifadhi vipi pesa zenu?

Francis:
Ili kujenga uaminifu katika jamii, ni lazima fedha zihifadhiwe vizuri na kutumia kwa makusudi yaliyotarajiwa. Wote wanaotoa michango hupewa risiti. Tumefungua akaunti benki ili kuhakikisha fedha zinakuwa salama.

Mtangazaji:
Mnafanya nini pale mabwawa yanapokuwa yamekauka maji baada ya ile miezi mitatu ya neema?

Francis:
Tuna pesa tulizopokea kutoka serikalini zilizoko kwenye akaunti yetu benki. Tunatumia fedha hizo kununulia maboma yanayosukuma maji kutoka kwenye mabwawa hadi katika matenki karibu na kila mitaa midogo iliyoko kijijini kwetu.Idara ya maji ya serikali itatandaza mabomba na maji hayo yatatiririka kutokana na nguvu za uvutano. Kazi hiyo itafanyika kwa miezi mitano. Kwa hivi sasa tutalazimika kuchimba visima zaidi.

Mtangazaji:
Kwa nini msichimbe mabwawa makubwa ili mpate maji mengi zaidi?

Francis:
Endapo bwawa linakuwa refu kwenda chini, linakuwa sio salama. Watu na wanyama wanaweza kutumbukia ndani yake. Kama bwana litakuwa refu sana, itakuwa ni vigumu mtu kujiokoa mara anapokuwa ametumbukia ndani. Kwa hiyo tunaogopa visitokee vifo.

Mtangazaji:
Ni vifaa gani vitatumika kujengea visima?

Francis:
Tutatumia matofari ya saruji kujengea visima. Matofari hayo yanatengenezwa kwa saruji na mchanga. Tutakapotumia vifaa hivi, maji hukaa salama kwa muda mrefu.

Mtangazaji:
Mtarudishaje gharama zitakazotumika katika wa ujenzi wa visima?

Francis:
Tutaitisha mkutano wa kijiji na kuelezea mpango mzima, ikiwa ni pamoja na faida zake na jinsi wanakijiji wanavyoweza kusaidia. Tunataraji watakuwa tayari kwa sababu wazo hili lilitoka kwao.

Mtangazaji:
Ni lini mnapotarajia kuanza mradi huu?

Francis:
Wakati wa mavuno, kwa sababu kipindi hicho wanakijiji watakuwa na pesa. Hiyo itakuwa ni mwezi Juni hadi Oktoba mwakani. Mradi huo unaweza kukamilika katika kipindi cha miezi mitano.

Ingiza muziki wa ala taratibu, halafu uumalizie kwa nguvu

Mtangazaji:
Wapendwa wasikilizaji, natumai mmemsikiliza kikamilifu Costa Francis, mwenyekiti wa kamati ya maji katika kijiji cha Talawanda, na mmejifunza njia nyingine ya kuhifadhi maji katika maeneo yenye upungufu wa maji. Tafadhali usikose kipingi kingine kama hiki.

Piga kiashirio cha kipindi

Acknowledgements

Washiriki: Emmanuel na Lillian Manyuka, Radio Maria, Tanzania, washirika wa redio ya Farm Radio International.
Imepitiwa na: Alan Etherington, mshauri binafsi wa maji, na uhamasishaji usafi na aliyekuwa mfanyakazi wa shirika la misaada la maji.

Information sources

Mahojiano na viongozi wa kamati ya maji
Shukrani za dhati kwa taasisi ya Harbinger kwa kutoa muswada huu unaohusiana na maji salama.