Ujumbe kwa mtangazaji
Save and edit this resource as a Word document.
Muhtasari kwa mtangazaji
Kikundi cha wakulima wa mtama kutoka katika kijiji cha Zaare nje kidogo ya manispaa ya Bolgatanga, Mkoa wa Mashariki ya Juu nchini Ghana wanabadilisha desturi zao za kilimo ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa katika kilimo cha mtama ambao ndio zao kuu la asili. Mtama una matumizi mengi katika mkufu wa chakula, kuanzaia sabo – chakula cha asili kinachoandaliwa kutokana na unga wa mtama kwenda tuo zaafi, ugali wa mtama unaoandaliwa na kuliwa pamoja na mbogamboga au mlenda wa bamia, hadi kokoo, uji mwepesi unaoandaliwa kwa ajili ya kifungua kinywa au kama asusa wakati wa mchana ukiwa pamoja na karanga au keki ya maharage.
Wakulima hawa pia wanalima mahindi yanayokua kwa muda mfupi na wanazidisha shughuli zao za ususi wa vikapu kwa ajili ya kukabiliana na njaa na kuhakikisha usalama wa chakula unakuwepo katika nyumaba zao. Katika mswada huu, mwandaaji wa vipindi wa redio ya jamii Lydia Ajono anaangalia katika athari za mabadiliko ya hali ya hewa katika uzalishaji wa mtama na jitihada wanazochukua wakulima kulisha familia zao na kuongeza usalama wa chakula.
Mswada huu unatokana na mahojiano halisi. Utautumia kama hamasa ya kufanya utafiti na kuandika mswada juu ya mada hiyohiyo katika eneo lako. Au unaweza kuandaa mswada huu katika kituoa chako, kwa kutumia waigizaji ili kuwakilisha wahojiwa. Kama utafanya hivyo, hakikisha unawaambia wasikilizaji wako mwanzoni mwa kipindi, kwamba sauti sio za wahojiwa bali ni za waigizaji.
Script
Mtangazaji:
Ndugu wasikilizaji, karibuni katika kipindi cha
Dunia hamisim, ikiwa na maana ya “hali ya hewa ya dunia inabadilika.” Unaweza kuita mabadiliko ya hali ya hewa duniani au ongezeko la joto duniani, hili ni jambo lenye uzito mkubwa sana kwa wakulima wa kaskazini mwa Ghana. Hii ni kweli hasa kwa makazi ya shambani na jamii zinazoishi kandokando mwa mto White Volta unaoanzia Burkina Faso hadi sehemu za kaskazini mwa Ghana.
Nilitembelea kaskazini mwa Ghana katika jamii zinazofahamika kwa kilimo cha mtama. Miongoni mwao ni Binde katika wilaya ya Mamprusi, Mkoa Kaskazini, Zebilla katika wilaya ya Bawku Mashariki, na Zaare karibu na bwawa kubwa la Vea katika wilaya ya Bolgatanga.
Ingawaje zipo katika maeneo tofautitofauti ya mkoa, wakulima katika jamii hizi wana changamoto zinazofanana katika kulima mtama.
Wasikilizaji, mnaelewa nini kuhusu ongezeko la joto duniani au mabadiliko ya hali ya hewa? Endelea kunitegea sikio, mimi ni mtangazaji wako, Lydia Ajono.
Sauti ya kiashirio cha kipindi na kisha iondoe
Mtangazaji:
Kwa lugha ya ki-Manpruli izungumzwayo mashariki mwa wilaya ya Mamprusi wanaita dunia hamisim, ikiwa na maana ya “hali ya hewa ya dunia inabadilika.” Katika lugha ya ki-Gurune izungumzwayo Bolgatanga, wanaita sanga teere, ikiwa na maana ya “mabadiliko katika majira au nyakati.” Na katika lugha ya ki-Kusaal izungumzwayo Bawku Magharibi, huitwa tenlebgre, ikiwa na maana “mabadiliko katika mazingira”
Ungana nami ili kujua kile wanachokifahamu wakulima hawa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa. Kwanza tutamsikiliza mkulima Dimonso kutoka Binde mashariki mwa wilaya ya Mamprusi. Atafuatiwa na wakulima wawili kutoka Zebilla na Zaare. Lakini kwanza nilimuuliza mkulima Dimonso juu ya uzoefu wake kuhusiana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Mkulima Dimonso:
Miaka ya hivi karibuni, tumekuwa tukipitia uzoefu wa matukio ya asili ambayo yanaathiri mashamba yetu na ufugaji wa mifugo. Mavuno ya mazao yamepungua sana kutokana na kukosekana kwa mvua kwa muda mrefu. Mvua inapokuja inazamisha mazao yetu na kufanya iwe vigu kustahimili. Uchomaji wa misitu umesambaa sana na hii imechangia katika tatizo. Tunadhani mabadiliko ya hali ya hewa husababisha ukame na mafuriko kwenye mashamba yetu kila mwaka. Mabadiliko haya ya hali ya hewa pia yamechangia kupotea kwa mazao kutokana na mafuriko.
Mtangazaji:
Wakulima wengi katika eneo la Zebilla wanategemea mto Volta Mweusi, ambao hutoa riziki kwa jamii nyingi ziishizo kandokando mwa kingo zake. Hebu tumsikilize mkulima Kugre akizungumzia jinsi baadhi ya wakulima kutoka Zebilla wanavyo kabiliana na baadhi ya athari zinazohusishwa na mabadiliko ya hali ya hewa.
Mkulima Kugre:
Sasa hivi tuanishi kwa hofu ya kuogopa kusombwa na mafuriko wakati wa msimu wa mvua, na mashamba yetu na mali zetu kuteketezwa na moto wa misitu wakati wa kiangazi. Hii sasa imekuwa sehemu ya maisha yetu hapa vijijini. Haikuwa hivi miaka 10 au 15 iliyopita. Kwa miaka ya hivi karibuni kilimo kimekuwa sio kazi ya kuvutia ya kujipatia riziki kwa sababu ya mvua hafifu. Hii ndio sababu vijana wengi wanakimbilia sehemu za kusini mwa nchi kutafuta kazi mijini.
Mtangazaji:
Kutoka Zebilla, tumesikia kile alichosema mkulima Kugre kuhusu hali ya hewa inayobadilika na jinsi upepo wa kiangazi unavyoweza kusababisha moto. Sasa tumsikilize mkulima Ayamga, kutoka Zaare wilaya ya Bolgatanga.
Mkulima Ayamga:
Takribani miaka 20 iliyopita, uzalishaji wa mazao hapa ulikuwa mzuri sana, hasa ule mtama wa zamani. Lakini siku hizi unaweza kuweka juhudi nyingi shambani lakini mwishoni unapata kidogo au usipate kabisa. Hii ndio sababu tunafikiri kitu fulani angani kimebadilika.
Kinaathiri kalenda yetu ya kilimo. Sielewi jinsi ya kukielezea lakini utanielewa….(Anasita). Tulikuwa tumezoea kuona aina fulani ya wadudu au chungu. Baba zetu walituambia kwamba wadudu hawa walilikuwa wanatupatia taarifa juu ya aina ya msimu na rutuba ya udongo. Lakini sasa hatuwaoni hawa wadudu rafiki. Badala yake tunawaona wadudu waharibifu wengi zadi kwenye mashamba yetu.
Mtangazaji:
Baada ya kuwasikiliza wakulima hawa, tulifanya majadiliano na kikundi cha wakulima kutoka Zaare. Lakini hebu kwanza tuburudike na wimbo kutoka kwa wanawake wa Zaare. Tutakaporejea, tutasikiliza mahojiano na wakulima wawili kutoka katika kikundi cha wakulima cha Zaare. Mahojiano yalifanyika chini ya mbuyu mkubwa karibu na shule.
Weka wimbo wa jumuia ya wanawake
Mtangazaji:
Karibu tena. Unasikiliza kipindi cha Dunia hamisim au Sanga teere. Sasa ungana nami nikiwa Zaare na mkulima Ayamga pamoja na mkulima Nsoh. Tutawasikiliza wakizungumza juu ya athari halisi za ongezeko la joto duniani na namna tunavyoweza kukabiliana na athari zake katika kilimo cha mtama, hasa katika upande huu wa Ghana. Tunapokuwa tunaendelea kusikiliza mjadala, tafadhali kumbuka kutushirikisha kisa chako juu ya kile unachokifanya wewe na jamii yako ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa. Tutamsikiliza kwanza mkulima Nsoh.
Mkulima Nsoh:
Kwa miaka ya hivi karibuni, wakulima wachache sana ndio wanaolima mtama, hii ni kwa sababu ya ukame. Mtama unahitaji mvua baada ya kuwa umeupanda. Pia unahitaji mvua baada ya kuwa umeanza kuchanua, na unahitaji mvua ya mwisho kabla ya mavuno. Lakini hilo halipo tena karibu kwa miaka 10 au 20. Majira ya mvua yamebadilika sana.
Mhojaji:
Ni kipindi gani ambapo kilimo cha mtama kilikuwa kizuri?
Mkulima Nsoh:
Naweza kusema ni takribani miaka 50 iliyopita, wakati nilipokuwa bado kijana mdogo nikilima na baba yangu. Tulikuwa tunavuna mtama mwingi hususani mtama wa lulu ambao unakomaa baada ya miezi miwili au mitatu. Lakini kwa miaka mingi sasa mambo yamebadilika na mtama unaokomaa mapema haufanyi vizuri.
Mhojaji:
Umekuwa unafanya nini ili kuendana na mabadiliko haya? Mkulima Ayamga?
Mkulima Ayamga:
Wakulima hapa Zaare sasa wameunda vikundi vya watu 20 ili kusaidiana katika misimu yote ya mvua na kiangazi. Mtama wa mapema unapandwa sana katika maeneo ya umwagiliaji. Haya ni maeneo yaliyoanzishwa na serikali miaka ya 1970, yanapita katika jumii zaidi ya 20 wilayani Bolgatanga. Eneo hili lina mifereji ambayo hutumiwa wakati wa kiangazi. Wakati wa mvua kila mkulima analima shamba analolimiliki katika eneo hili kwa ajili ya mazao ya asili na mazao mengine.
Katika maeneo haya, siku zote kunakuwa na unyevunyevu, hata kama mvua zisiponyesha wakati wa msimu wa mvua. Wakati wa kiangazi tunapanda soya, nyanya na mbogamboga nyingine. Mtama unapenda mbolea ya asili kuliko mbolea za kemikali. Badala hizo mbolea, tunasambaza mbolea ya wanyama ardhini. Baada ya mvua za kwanza, ardhi inalimwa kwa plau na mtama unapandwa.
Mhojaji:
Kwa hiyo, hiyo humaanisha umehama kutoka katika kilimo cha kutegemea mvua na kwenda katika kilimo cha umwagiliaji?
Mkulima Ayamga:
Tunafanya vyote, lakini mtama unapandwa sana katika msimu wa mvua, kwa sababu kunakuwa hakuna mvua za kutosha kwa wakati muafaka wa kupanda mtama wa mapema. Ndege wanakula mtama wa mapema nao pia ni tatizo.
Mhojaji:
Unalima mazao ya aina ngapi?
Mkulima Ayamga:
Tunalima mpunga, mtama au mawele, karanga, maharage na aina tofauti tofauti za mbogamboga. Watu wachache hulima mahindi, lakini yale yanayokomaa ndani ya miezi mitatu. Mahindi haya husaidia wakati wa upungufu wa chakula katika kipindi cha msimu wa mvua tunapokuwa tunapalilia shamba. Hata wakati mwingine tunayauza ili kuwasadia watoto kwenda shule.
Mhojaji:
Ngoja nikuulize Nsoh … Kama ungeambiwa kuacha kulima mtama na kujikita tu katika kulima soya ili upate pesa zaidi za kukusaidia wewe pamoja na familia yako, ungesemaje?
Mkulima Nsoh:
Kama ningeacha kulima mtama, hasa mtama wa unaokomaa mapema ingekuwa inamaanisha kuwa sitambuliki kama mkulima. Sisi watu wa mashariki ya juu hasahasa jamii ya Frafra tunatambulika kwa kulima mtama unaokomaa mapema. Ingawaje hatupati mavuno mazuri, bado tunaendelea kufanya kila jitihada kuendelea kuupanda.
Mhojaji:
Umepanda mtama ekari ngapi mwaka huu?
Mkulima Nsoh:
Nina takribani ekari mbili katika eneo la umwagiliaji. Nilitumia ekari moja kupanda mtama unaokomaa mapema na ule wa kawaida. Na ekari nyingine nilipanda mchele.
Mhojaji:
Kwa nini ulipanda pamoja mtama wa kawaida na ule unaokomaa mapema?
Mkulima Nsoh:
Ni wazo zuri kufanya hivyo. Mtama unaokomaa mapema utavunwa kwanza. Ndani ya mwezi au miezi miwili ule mwingine utakuwa tayari kwa ajili ya mavuno katika kipande kilekile cha ardhi ambacho nilitumia mbolea.
Mhojaji:
Hii itakuwa ni kazi ngumu. Unalishughulikiaje shamba?
Mkulima Ayamga:
Oo, sio kazi ya mtu mmoja. Na hiyo ndio sababu tuliunda vikundi vya wakulima ili kusaidiana kupalilia na kuandaa shamba kwa ajili ya hatua nyingine ya kulima inayofuatia.
Mhojaji:
Vipi kuhusu familia yako? Je, wake zako wanakusaidia?
Mkulima Ayamga:
Ndio, wananisaidia wakati wa kupanda kwa kufukuza ndege. Lakini pia nao wana mashamba yoa na tunawasaidia.
Mhojaji:
Licha ya kusisitiza kilimo cha mtama ili kulinda aina ya mtama ya asili, shughuli gani nyingine unazozifanya wewe na wenzako ili kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa?
Mkulima Ayamga:
Kwa kweli, takribani kila familia katika Zaare, wanajamii – wote wanaume na wanawake sasa hivi wanasuka vikapu. Ni vikapu hivi ndivyo kwa kweli vinavyowalisha wana jamii kuliko ulimaji wa mazao. Hii ni kwa sababu mabadiliko haya ya hali ya hewa, sasa inafanya kilimo kiwe ni shughuli ya kupoteza pesa.
Mhojaji:
Unaona nini katika kilimo cha mtama miaka 10 ijayo kuanzia sasa?
Mkulima Ayamga:
Kusema kweli, kama watu wa ofisi ya kilimo hawatakuja na msaada wa kitaalam au kutoa fedha kwa wakulima wa hapa, sioni kama utaendelea kulimwa kwa kiwango kikubwa kama tulivyokuwa tukilima miaka ya 50. Tutaendelea kuulima katika maeneo haya madogo kwa ajili ya kulisha familia zetu. Lakini hicho hakitoshi kulisha watu wote katika eneo la Bolgatanga. Kwa hiyo tunahitaji msaada kutoka serikalini na kutoka kwa wadau wengine wanopenda kilimo.
Mhojaji :
Unadhani kupata taarifa za mara kwa mara juu ya mabadiliko ya hali ya hewa na athari zake, na mapendekezo juu ya mbinu za kilimo, kutakufanya uendelee kulima mtama?
Mkulima Ayamga:
Kukutana na watu wa redio kama wewe kumetupatia mawazo kadhaa ambayo tutayatumia wakati wa mikutano yetu ya wakulima. Pia kunatusaidia kujadili changamoto zetu na wadau wengine wanaoweza kututembelea.
Mhojaji:
Asante sana kwa kushirikiana nami. Tutaendelea kukuletea taarifa zaidi kupitia redio juu ya mabadiliko ya hali ya hewa.
Mkulima Ayamga:
Nasi pia tunakushukuru.
Mtangazaji:
Dunia hamisim au Sanga teere kilikuwa kipindi cha kwanza katika mfululizo wa vipindi vyetu juu ya mabadiliko ya hali ya hewa. Mjadala wa leo ulikuwa juu ya athari za mabadiliko ya hali ya hewa katika zao la mtama, na jamii yetu ya kwanza ilikuwa Zaare katika eneo la Bolgatanga Mkoa wa Mashariki ya Juu nchini Ghana.
Hadi wakati mwingine, napenda kuwashukuru wanajamii wote na timu ya ufundi ambao wamenisaidia katika kuandaa kipindi.
Acknowledgements
Imechangiwa na: Lydia Ajono, Redio Gurune, Ghana
Imepitiwa na: John FitzSimons, Profesa Mshiriki, Shule kuu ya Usanifu wa Mazingira na Maendeleo ya Vijijini, Chuo kikuu cha Guelph, Canada
Information sources
Mahojiano na:
Dinmoso Dagansa, Binde, Wilaya ya Mamprusi Mashariki, Oktoba 10, 2011
Kugre Ben, Wilaya ya Zebilla, Oktoba 12, 2011
Abaa Ayamba na Nsoh Joseph, Zaare, Wilaya ya Bolgatanga, Desemba 23, 2011
Mradi umefanywa kwa msaada wa Serikali ya Kanada kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Kanada (CIDA)