Boresha samadi ili upate mbolea nzuri

Ujumbe kwa mtangazaji

Muswada huu unawajumuisha wahusika wafuatao Philip (Mtangazaji) na Dokta. Compost (Peter Composter). Philip anatokea mjini. Ana tatizo la tumbo na kwa hali Fulani hajui sana mbinu zinazotumika katika kilimo. Dokta. Compost amekulia kijijini, na ana shahada ya chuo kikuu katika masuala ya elimu ya Kilimo.

Wakulima wanaokusikiliza ni lazima watambue kuwa mazao yao yatakuwa bora kama ardhi waliyotumia kuyalima nayo itakuwa bora. Kuongeza samadi katika ardhi ni sawa na kuweka fedha “katika benki ya udongo.” Kilimo kinachojumisha kuongeza Nitrojeni katika ardhi  na mimea mingine inayorutubisha ardhi ni faida kubwa. Kama benki yako ambayo ni udongo ni tajiri, mazao yatakuwa mazuri. Lakini katika maeneo mengi hapa duniani, udongo umechoka, na mara nyingi unakuwa hautoi mazao mazuri, na mimea inayolimwa katika ardhi hiyo inashambuliwa haraka na magonjwa pamoja na wadudu.

Ushauri mwingine wa kuimarisha ardhi yako ili itoa mazao bora ni pamoja na:

  • Jinsi mazao yanayofunika ardhi yanavyoweza kuboresha udongo
  • Kazi ya minyoo ya ardhini katika kila udongo wa mkulima inavyoweza kusaidia mpango wa kurutubisha ardhi.

Muswada huu ni mchezo mdogo wa kuigiza unaodokeza jinsi ya kutumia kinyesi cha mifugo kujitengenezea mbolea yako mwenyewe. Kuna njia mbili za kuutumia muswada huu, kwanza ni kwa kuuchukua kama ulivyo na kutengeneza mchezo wa kuigiza au kutumia yaliyomo katika muswada huu kutengeneza mchezo wako wa kuigiza utakaoendana na mazingira yako, lakini ukizingati maelezo yaliyotolewa.

Script

Wahusika

Philip:
Mtangazaji kutoka redio ya mjini
Dokta. Compost, Shahada ya Uzamivu.
(Peter Composter): Mtaalamu wa kilimo mwenye umri takribani wa miaka 70, ana tabia ya kushau sahau. Ana uzoefu wa mambo ya shambani na elimu ya chuo kikuu. Shida yake ni kwamba, wakati mwingine unapozungumza naye anachanganya mada. Hata hivyo taarifa anazotoa mara nyingi ni za manufaa, zenye kuvutia na unaweza kuzifanyia kazi.

Philip:
Habari za asubuhi wasikilizaji na karibu katika kipindi chetu cha leo. Kama wewe ni mkulima, bila ya shaka unafahamu kuwa kwa kuongeza mbolea katika udongo wa shamba lako utapata mazao bora. Unaweza kununua mbolea inayotengenezwa kwa kemikali. Lakini pia unaweza kutumia vitu ulivyonavyo nyumbani kwako ama shambani, kujitengenezea mbolea. Kwa mfano unaweza kutumia mabaki ya chakula kutoka jikoni na taka zilizobaki shambani au unaweza kutengeneza mbolea kutokana na samadi ya wanyama kama vile kuku na ng’ombe.

(Kituo) leo katika studio zetu tuna mgeni, ni mtaalamu wa kurutubisha udongo na mboji. Karibu Dokta Compost.

Dokta. Compost:
(anaonyesha woga kidogo na kuzungumza kwa haraka) Ndiyo, kwa hakika kinyesi cha wanyama huwa kinatumiwa kama mbolea. Lakini kinyesi kibichi cha wanyama kinakuwa na wadudu wanaoshambulia mimea na vijidudu vyenye magonjwa, ambayo pia yanaweza kuwa tatizo (Ghaflla ananyamaza na kuanza kutulia, halafu anaanza kuzungumza pole pole) Asante kwa kunikaribisha, Philip. Nafurahi kufika hapa.

Philip:
(Kwa sauti ya mshangao) umesema vijidudu vyenye magonjwa?” Ni magonjwa gani hayo?

Dokta. Compost:
Usiwe na wasiwasi, Peter. Ni magonjwa ya mimea. Leo nitazungumzia jinsi ya kutengeneza vinyesi vya wanyama kuwa mbolea kwa kuyachanganya. Je unajua kwamba, wakulima nchini China wamekuwa wakitumia mbinu hii kwa karne nyingi? Wanachukua samadi ya mbolea ambayo imehifadhiwa kwa muda mrefu, kisha wanachanganya na kinyesi kipya cha wanyama na kuweka tena baadhi ya mimea na udongo na kuufunika mchanganyiko huo kwa udongo. Kutokana na hali hiyo fukuto hutokea ndani ya mchanganyiko huo linalounguza vijidudu vyote na wadudu wengine wanaoleta magonjwa na mwisho kutengeneza mbolea nzuri.

Philip:
Nimeshawahi kuona wakulima wanaoongeza mbolea ya mavi ya wanyama katika mashamba yao. Kwa nini uhangaike kuweka michanganyiko yote hiyo ya kinyesi cha wanyama uliyoieleza?

Dokta. Compost:
Nimefurahi kwa kuuliza swali hilo, Philip. (Kituo) Samahani, swali lenyewe linasemaje tena? … (baada ya sekunde mbili za ukimya, anakumbuka tena) Usijali, nakumbuka. Sawa, nilisema, rundo la mchanganyiko huo wa kinyesi cha wanyama na majani unasaidia kuua mbegu za magugu na magonjwa kwa mimea yanayoweza kutokana na kinyesi cha ng’ombe ambacho bado hakijaoza. Faida nyingine ya kutengeneza mbolea ya aina hii ni kwamba, unaweza ukaiweka moja kwa moja kwenye mashimo, unamotaka kupanda mbegu, kwa sababu haiwezi kuunguza mazao yako kama kinavyofanya kinyesi cha wanyama ambacho bado ni kibichi.

Philip:
Asante, Dr. Compost. Kwa hiyo mkulima anawezaje kutengeneza jeruba la mbolea hiyo? (akionyesha wasiwasi) Je ni lazima ashike kwa mikono samadi ya wanyama?

Dokta. Compost:
(Bila kujali wasiwasi wa Philip) Kama unataka kutengeneza jaruba la mbolea inayotokana na wanyama, zifuatazo ni hatua za kufuata. Ni kama ifuatavyo.

Kwa kuanzia, unahitaji mita chache za eneo la mraba ambalo ni tambarare katibu na eneo unalotaka kulima mazao yako. Ondoa fimbo zote, mawe na takataka nyingine zilizoko karibu na eneo ulilochagua. Unaweza kutengeneza jeruba lako la mbolea katika ngazi nne.

Katika safu ya kwanza ya ngazi yako unaweza kuweka magugu na majani mengine au kitu chochote kinachotokana na mimea ambavyo unataka vioze pamoja na kwa wakati. Hii safu inatakiwa kuwa na urefu wa mita ishirini kwenda juu na iwe tambarare. Mita ushirini ni sawa na urefu wa kiwiko cha kiganja hadi kwenye kidole chako kirefu kuliko vyote cha mkononi.

Baada ya hapo tengeneza safu ya pili. Sambaza kinyesi kibichi cha mavi ya ng’ombe au kuku juu ya yale majani uliyowekwa kwanza. Urefu wa kinyesi hiki cha wanyama inabidi ulingane na ule wa majani ambao ni sentimita ishirini kwenda juu. Baada ya hapo ongeza safu ya tatu ambayo itajumuisha udongo mbichi.

Philip:
Subiri kidogo. Hebu turudie tena. Hizi safu tatu za mbolea yetu zinakuwa zimetengenezwa kwa kutumia … (anasubiri Dokta. Compost kumalizia sentesi yake)

Dokta. Compost:
(Taratibu na kwa uvumilivu) safu ya kwanza inatengenezwa na magugu na majani. Safu ya pili inatengenezwa kwa kinyesi kibichi cha ng’ombe ama kuku. Na safu ya tatu inatengenezwa kwa udongo wenye unyevu. Unalazimia kutumia mara tatu zaidi ya udongo uliouweka na kinyesi ama majani. Kwa hiyo safu ya tatu inatakiwa kuwa na urefu wa sentimeta sitini kwenda juu. Sentimeta sitini ni sawa na urefu kutoka kwenye bega lako hadi kwenye mkono. Kama huna udongo wenye unyevu, tumia udongo mkavu halafu umwagie maji. Lakini hakikisha kuwa umeumwagia maji ya kutosha ili urowane – na sio vinginevyo.

Lipo jambo linguine la kufanya ili kutengeneza mbolea bora. Unaweza kuniuliza, “Je ni nini umuhimu wa vitu hivi Dokta Compost?” (Kituo,baada ya sekunde chache Dokta Compost anakohoa na kurudia tena alichokisema kwa sauti kubwa.) Unaweza kuniuliza, “Je ni nini umuhimu wa vitu hivi Dokta Compost?”

Philip:
(kama vile mtu aliyetoka usingizini) Oh! Um … je ni nini umuhimu wa vitu hivi, Dokta. Compost?

Dokta. Compost:
Swali zuri, Philip. (Anakuwa kama mvivu kidogo, lakini mwenye ari) Asante kwa kuniuliza. Jambo lingine muhimu ni kulifunika eneo lote kwa safu nyembamba ya udongo. (Kituo) Haswa – funika eneo lote kwa matope. Hiyo itakuwa safu ya nne na ya mwisho. Funika eneo la juu la jaruba lako kwa matope hadi yakutane na ardhi. Kama eneo lina udongo wa kijivu basi linakuwa na matope mengi ambayo ni mazuri zaidi. Udongo wenye tope unaweza kutengenezwa kwa vitu vidogo vidogo vinavyoweza kuchanganyika. (Angalizo kwa mhariri: kama mkulima anaweza kupata mifuko mikubwa ya plastiki anaweza kuitumia badala ya matope hasa katika maeneo yenye mchanga mwingi ambako inakuwa vigumu kutengeneza tope).

Philip:
Matope? Lakini kwa nini ufunike jeruba lako la kutengenezea mbolea kwa matope? Nimeshaona majeruba mengi ya mbolea ambayo hayajafunikwa kwa matope na bado yakaonekana kufanya kazi vizuri.

Dokta. Compost:
Vizuri, sio lazima kufunika rundo lako lote la mbolea kwa matope unapotengeneza mboji. Lakini kuna faida mbili zinazopatikana unapofunika jaruba lako kwa matope. Kwanza, inaruhusu kuwepo kwa fukuto ndani ya jaruba. Kadiri rundo lako la jeruba linavyopata joto ndivyo mbolea yako inavyotengenezeka kwa haraka. Jambo la pili, matope yanafanya virutubisho vilivyoko ndani ya mbolea yako visipotelee hewani.

Sasa, baada ya kufunika jeruba lako kwa matope, liache jinsi lilivyo kwa siku kumi, au kwa siku zaidi kama ni kipindi cha baridi. Unaweza usione kinachoendelea kwa nje, lakini kwa ndani kuna aina Fulani ya wadudu wanaokula na kuvunja mchanganyiko uliouweka katika vipande vidogovidogo …

Philip:
(Kwa wasiwasi) Ewwww …

Dokta. Compost:
(Kwa mara nyingine, anadharau hofu na mshangao wa Philip na kuendelea kuzungumza kwa uchangamfu) Shughuli za wadudu hawa ndani ya jaruba zinasababisha kuwepo kwa joto jingi. Joto hili linaua mbegu za magugu na wadudu wengine ndani ya jeruba.

Baada ya siku kumi, bomoa jaruba lako na kuchanganya kila kitu kilichokuwepo pamoja na kwa uangalifu. Mbolea yako ambayo pia inajulikana kama mboji, inakuwa tayari kwa matumizi. Unaweza kuitimia haraka iwezekanavyo.

Philip:
Kwa nini uitumie haraka kiasi hicho?

Dokta. Compost:
Kuna sababu. Kama ukiiacha mbolea yakokuendelea kuwa ndani ya jeruba, itaanza kupoteza virutubisho. Baadhi ya virutubisho vinaweza kupotelea hewani. Vingine vinaweza kuzolewa na maji mara mvua inaponyesha. Kama unaona huwezi kutumia mbolea yako mara moja, basi funika jaruba lako kwa majani ya mgomba au majani mengine makubwa yanayoweza kufunika jaruba vizuri.

Philip:
Naomba nielewe jambo hili vizuri Dokta. (Kituo) unamaanisha kuwa baadhi ya virutubisho vinaweza kupotelea hewani au katika udongo kama jaruba halitafunikwa?

Dokta. Compost:
Sawa sawa.

Philip:
Je jambo kama hili haliwezi kutokea kwa samadi ya wanyama ambayo haikujumuishwa kwenye jeruba? Kama ng’ombe wako na mbuzi pamoja na wanyama wengine wata … (anasita kidogo) , je na hizi nazo virutubisho vyake havitaondoka kama visipofunikwa kama ulivyofunika jeruba?

Dokta. Compost:
(Kwa ari) Hilo ni swali zuri sana, Philip. Zote, kinyesi cha wanyama na mikojo yao ni vizuri inaongezewa kwenye jaruba letu. Bila ya shaka ni vigumu kuchanganya mavi ya wanyama pamoja na mikojo yao kwenye jaruba. Lakini kuna njia rahisi ya kuvipata vitu hivyo kwa kadiri unavyotaka. Njia mojawapo ni kutumia mkojo wa wanyama uliouhifadhi kuongezea kwenye jaruba lako. Mara nyingi wakati wa mvua jaribu kulisha mifugo yako katika eneo ambalo unaweza kuhifadhi mikojo yao wanapokuwa wakila, hivyo itakuwa rahisi kuitumia kwenye jaruba.

Philip:
Kwa hali hiyo nitajitahidi kukusanya kiasi cha kutosha cha kinyesi cha wanyama na mikojo yao hasa katika lile eneo lililoandaliwa ambapo huwa wanajisaidia, na kisha nikaviongezea kwenye jeruba letu. Sawa?

Dokta. Compost:
Haswa! Njia nyingine bora ya kupata kwa urahisi vitu hivi ni kutumia sakafu iliyosakafiwa vizuri kuwalazia wanyama. Wanyama wanapojisaidia kwenye sakafu iliyosakafiwa vizuri ni virutubisho vichache sana vinavyopotea kutoka kwenye kinyesi chao. Jambo la mwisho ni kuhakikisha eneo ambalo mifugo yako inalia chakula na kulala liwe limefunikwa. Ni virutubisho vichache sana vinavyopotea katika eneo ambalo limefunikwa vizuri kuliko eneo linalopigwa moja kwa moja na jua.

Philip:
Wow, hizo ni taarifa nyingi sansa kwa kipindi kimoja, Dokta. Compost. Unashangaza.

Dokta. Compost:
(Akiwa amechanganyikiwa, na kugugumia kidogo) A-a- asante, Philip.

Philip:
Je kwa haraka tunaweza kurudia hatua tulizozungumzia katika kutengeneza jeruba la mbolea ya mboji, Dokta?

Dokta. Compost:
Bila shaka. Kumbuka kutengeneza jeruba lako la mboji katika safu nne – (akizungumza taratibu) kwanza ni mimea, halafu kinyesi cha wanyama, kisha udongo wenye unyevu, na mwisho funika kwa matope. Acha mchanganyiko huo ukiwa umefunikwa kwa siku kumi. Kisha ufukue na kuanza kuuchanganya kwa uangalifu. Sasa mbolea yako inakuwa iko tayari kwa matumizi.

Philip:
Je kuna wakati ambao ni mzuri zaidi wa kutengeneza mbolea hii?

Dokta. Compost:
Swali zuri, Philip. Takribani siku kumi mara baada ya kutengeneza mbolea yako, inakuwa tayari kwa matumizi. Unaweza kuongeza siku kidogo kama msimu huo ni wa baridi. Kwa hiyo kama unajua ni lini unataka kuitumia mbolea yako, basi anza matayarisho ya kutengeneza jaruba siku kumi kabla.

Philip:
Na je unaitumiaje mbolea uliyoitengeneza?

Dokta. Compost:
Unaweza kuisambaza shambani kati ya mazao yako. Au unaweza kuiweka kwenye mashimo maalum ya miche unayotaka irutubishwe. Utakuja kugundua, kama vile wakulima wa kichina walivyogundua kuwa mbolea hii ya samadi unayotengeneza mwenyewe inafanya mazao yako kuwa bora na yenye afya.

Philip:
Asante sana kwa utangulizi wako mzuri wa kutengeneza samadi inayotokana na kinyesi cha wanyama, Dokta. Compost. Nawashukuru pia wasikilizaji wetu kwa kutusikiliza. Tukutane tena wiki ijayo muda na wakati kama huu. Kwaheri kwa muda.

Shukrani

Muswada huu umeasiliwa kutoka redio ya kimataifa ya Farm iliyochapiswa kama makala namba 8, muswada wa 3, uitwao “Improving manure.”

Acknowledgements

Ukapitiwa na: Jibrim M. Jibrim, Profesa mshiriki wa Idara ya Udongo na Sayansi wa chuo kikuu cha, Bayero huko, Kano, Nigeria.

Information sources

George Kuepper, 2003. Manures for Organic Crop Production. Appropriate Technology Transfer for Rural Areas (ATTRA). http://attra.ncat.org/attra-pub/PDF/manures.pdf.
Muswada wa redio ya kimataifa ya Farm kuhusiana na matengenezo ya mboji na samadi kwa ajili ya kurutubisha ardhi: http://frrp.wpengine.com/english/radio-scripts/fertilization.asp. Kwa ajili ya masuala ya kurutubisha udongo angalia makala namba 89, muswada wa 2 katika http://frrp.wpengine.com/english/radio-scripts/89-2script_en.asp.
Madeleine Inckel, Peter de Smet, Tim Tersmette and Agromisa Foundation Tom Veldkamp, 2005. Agrodok 8: Matayarisho na matumizi ya mbolea ya samadi. Wageningen:. http://www.agromisa.org/agrodoks/Agromisa-AD-8-E.pdf

Shukrani za dhati kwa taasisi ya McLean kwa kufadhili muswada huu wa afya ya ardhi