Ujumbe kwa mtangazaji
Save and edit this resource as a Word document
Maelezo kwa mtangazaji
COVID-19 ni mojawapo ya majanga ya kutisha ya karne hii, kwa kiwango sawa na homa ya Uhispania ya mwaka 1918. Lakini bila ya kuwa na dawa, serikali nyingi ulimwenguni zimeamua kuwazuia watu kutoka majumbani mwao kwa kipindi cha muda ili kudhibiti kuenea kwa janga hili. Hii kwa ujumla imekuwa ikijulikana kama kizuizi. Mkakati huu unatarajiwa kusitisha kuendelea na kuenea kwa virusi. Walakini, kwa jamii ya wakulima kama hiyo ya mashariki mwa Zambia, kuzuiliwa kumeathiri vibaya wakulima, ambao
wanategemea jamii za mijini kununua mazao yao. Imeathiri pia watu wa mijini ambao wanategemea zaidi jamii za wakulima kwa ajili ya kupata mboga mboga.
Maandishi haya yanaelezea njia kadhaa ambazo wakulima wanakabiliana na hali hiyo. Pia inaeleza hatua za kukabiliana na hali hiyo zilizochukuliwa na wakaazi wa mijini kupata mboga kutoka shambani baada ya kukosekana kutoka kwa vyanzo vyao vya kawaida.
Unaweza kuchagua kuwasilisha maandishi haya kama sehemu ya programu yako ya kawaida ya mkulima, ukitumia waigizaji wa sauti kuwakilisha waongeaji. Ikiwa ni hivyo, tafadhali hakikisha unawaambia wasikilizaji wako mwanzoni mwa programu kwamba sauti ni za waigizaji, sio watu halisi ambao walihusika kwenye mahojiano.
Unaweza pia kutumia maandishi haya kama mfano wa kuunda programu yako mwenyewe juu ya jinsi wakulima na wadau wengine wanavyoendelea nchini mwako mbele ya janga la COVID-19. Unaweza kuhoji wakulima wadogo, wataalamu wa lishe, wachumi wa kilimo, wauzaji mbalimbali wa soko la mazao ya kilimo, na vile vile wawakilishi wa mashirika ya afya na waganga wa jadi ili kusimulia hadithi yako. Unaweza kuwauliza:
- Kiwango cha maambukizi katika nchi yako na ni hatua zipi Wizara ya Afya na watendaji wengine wameweka kudhibiti na kuzuia janga hilo.
- Jinsi wakulima wadogo wanavyokabiliana na hatua hizi za kudhibiti.
- Hatua zilizochukuliwa na jamii kufuata hatua hizi (ni pamoja na umuhimu wa wahudumu wa afya wanaoaminiwa kwa kufuata hatua za kukabiliana na janga).
* Tafadhali fahamu kuwa maandishi haya yanaelezea hali ilivyo mashariki mwa Zambia mnamo mwezi Aprili na Mei 2020, na hali imebadilika tangu wakati huo.
Muda wa maandishi haya, ikijumuisha utangulizi na uhitimishaji: Dakika 20-25
Script
KAMBOLE:
Halo, mimi ni Kambole Kanyanta katika Ofisi ya Kilimo ya Wilaya. Naweza kujua ni nani anayepiga simu?
FILIUS:
Jina langu ni Filius Chalo Jere, mtayarishaji wa kipindi cha redio cha Kilimo ni Biashara kutoka Breeze FM. Naweza kufanya mahojiano na wewe kwa njia ya simu?
FILIUS:
Kuhusu athari ya virusi vya corona kwa jamii ya wakulima na washirika wao wa kibiashara.
KAMBOLE:
Unamaanisha janga la virusi vya corona, ambayo inajulikana kama COVID-19?
FILIUS:
Ndio. Pamoja na vizuizi vya hivi karibuni vya watu kutembea, tayari tunaona kupungua kwa wakulima wanaokuja mjini kuuza mboga zao. Hii pia inazuia wafanyabiashara kutoka soko la kijani kutoka kwenda kununua mboga kutoka kwa wakulima. Tafadhali toa muhtasari mfupi wa mnyororo wa usambazaji wa mazao ya chakula kutoka kwa wakulima kupitia kwa watu wa kati (madalali) na watu wa kati ambao ni wanawake mpaka kwa watumiaji.
KAMBOLE:
Uchumi wa Chipata unategemea kilimo na karibu kila mtu katika wilaya ana jukumu katika mnyororo wa thamani. Kusimama kwa sehemu yoyote katika mnyororo huu wa thamani utaathiri vibaya maeneo mengine yaliyobaki.
FILIUS:
Tafadhali fafanua haswa jinsi hii ilivyo.
KAMBOLE:
Ni rahisi. Wakulima vijijini wanazalisha chakula lakini hawana mahitaji ya msingi kama chumvi, sukari, na sabuni. Wakazi wa miji wanapata mahitaji ya kimsingi lakini wanakosa chakula kutoka shambani. Kama matokeo, lazima kuwe na kubadilishana kwa bidhaa kati ya hizo mbili. Walakini kwa mkulima kuzalisha chakula chochote, lazima kwanza apate pembejeo kama mbegu, mbolea, na kemikali za shamba kutoka mjini.
Mwishowe, mkulima lazima aende mjini kuuza mazao. Kwa njia hii, mkulima hupata pesa na anaweza kupata mahitaji muhimu ya nyumbani, pamoja na pembejeo za kuzalisha mboga zaidi. Mnyororo huu wa thamani umefanya kazi vizuri kwa kila mtu hadi ugonjwa wa virusi ya corona ulipotokea.
FILIUS:
Je! Hii iliathirije mlolongo wa thamani? Je! Ni kwasababu watu walianza kuugua na kufa?
KAMBOLE:
Sio kivile. Shida ni kufungwa/vizuizi ambavyo vilitangazwa ghafla nchi nzima.
FILIUS:
Tafadhali elezea maana ya kizuizi kwa maneno rahisi.
KAMBOLE:
Kuhusiana na hali ya sasa, kufungwa kunamaanisha vizuizi ambavyo serikali imeweka ili kuangalia kuenea kwa virusi. Polisi na vyombo vingine vya kutekeleza sheria wapo maeneo yote ya mjini na kwenye maboma kufanya doria ili kuhakikisha kuwa watu muhimu tu ndio wako nnje.
FILIUS:
Ni nani wanaochukuliwa kuwa watu muhimu? Nilidhani watu wote walikuwa muhimu.
KAMBOLE:
Ndio, kila mtu ni muhimu. Walakini, chini ya hali zilizopo, ikiwa kila mtu anaruhusiwa kuzurura na kuchanganyika kwa uhuru, virusi vitakuwa na siku nzuri na kuruka kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine na watu wengi wangeugua na kufa. Kwa hivyo, serikali haitaruhusu mtu yeyote kuzurura- wafanyakazi tu wa hospitalini na watu wengine wachache ambao kazi yao ni ya lazima ndio huruhusiwa. Hii ni pamoja na polisi na maafisa wengine wa kutekeleza sheria. Wengine wanatarajiwa kukaa ndani ya mipaka ya nyumba zao hadi kufungwa/vizuizi vitakapoondolewa.
FILIUS:
Wakulima sio muhimu? Hatuwezi kula pasipo vyakula wanavyopanda.
KAMBOLE:
Hakika, wakulima ni muhimu. Lakini katika hali ya kuishi na kifo kama hii, wao pia, lazima wazuiliwe. Vinginevyo, jambo hili linaweza kukua na kusambaa kama mafua ya Uhispania ya mwaka 1918 ambayo yaliua zaidi ya watu milioni 50 ulimwenguni.
FILIUS: Ikiwa wakulima hawawezi tena kuja mjini kuuza mazao yao, inamaanisha kuwa, kwa sasa, hakutakuwa na duka la mazao yao na wataenda tu kupoteza, wakibaki hawana kipato.
KAMBOLE:
Hasa! Hakutakuwa na mapato kwa wakulima na hakuna mboga kutoka shambani zitafika kwako na kwangu hapa mjini. Kwa kweli, mboga zinazoagizwa zinapatikana kwenye maduka makubwa, lakini ni ghali sana na sio halisi kutoka shambani. Kwa kuongezea, zinanyanyapaliwa kama GMOs, ambapo watu wengi wanaziona kuwa mbaya kwa afya. Ndio sababu watu wengi wanapendelea kupata mboga halsi kutoka kwa wakulima. Maduka makubwa sasa yako wazi, lakini kwa kiwango kidogo na wateja wachache wanazitumia.
FILIUS:
Ningependa kujua jinsi wakulima na wateja wao walioko mijini wanakabiliana vipi wakati huu wa kufungwa/vizuizi. Tafadhali niunganishe na watu wengine ninaoweza kuzungumza nao.
KAMBOLE:
Sawa, kuna Bwana Grevazio Banda, ambaye amekuwa akifanya vizuri sana kwenye bustani yake. Kawaida hupanda mboga nyingi, nyanya, na mazao mengine, ambayo huyauza kwenye soko kuu. Nashangaa sijui anaendeleaje chini ya hali hii kwasababu sioni tena akija mjini kuuza mazao yake.
FILIUS:
Hakika, itakuwa ya kupendeza zaidi kujua jinsi ufungaji huu unavyoathiri biashara ya kilimo ya Grevazio. Vipi kuhusu mteja wa mboga, mmoja au wawili wanaokaa mjini? Je! Una mtu yeyote unamfahamu unaweza kuniunganisha nikazungumza naye?
KAMBOLE:
(KICHEKO) Ndio, ninaweza kukuunganisha wewe mwenyewe. Wewe ni mkaazi wa mjini ambaye pia unategemea wakulima kupata mboga kutoka shambani. Unaweza ukajihoji wewe mwenyewe.
FILIUS:
(ANACHEKA PIA) Labda uko sawa. Walakini, wewe pia ni mkazi wa mjini ambaye umekuwa akinunua mboga halisi kutoka kwa wakulima. Kwa hivyo, nitakuhoji badala yake.
KAMBOLE:
Mimi sistahiki kwasababu ya taaluma yangu kama mchumi wa kilimo. Walakini kwa mawazo ya pili, labda hii ni fursa ya kuwaonyesha watu umuhimu wa bustani za mboga za nyuma ya nyumba ambazo tumekuwa tukipendekeza kwa miaka mingi. Watu wengi wamepuuza ushauri wetu kwa kuogopa kupata bili kubwa za maji. Hiyo ni sababu isiyo na mashiko.
KAMBOLE:
Bustani za nyuma ya nyumba hazipelekei kupoteza maji kwasababu sio lazima iwe kubwa sana. Kwa mfano, nina tuta moja la nyanya, lingine la vitunguu, na mawili ya mboga. Ninatumia maji machafu kuwamwagilia. Hii ni sawa maadamu haina sabuni au mabaki ya mafuta. Hiyo ni kuchakata, kitu ambacho kinashauriwa sana. Kila mtu anapaswa kufanya!
KAMBOLE:
Lazima wafanye hivyo sasa kwasababu hakuna njia mbadala. Tayari, watu wachache wamekuja kwangu kujifunza jinsi ya kutengeneza vitalu vya mboga na mbolea. Ninafundisha pia watu ambao hukaa katika vyumba vya juu katika magorofa jinsi ya kupanda mboga kwenye ndoo kwenye balconi zao.
FILIUS:
Hiyo inavutia sana. Sasa, tafadhali nipe na mbari za simu. Ninahitaji kuzungumza na Bwana Grevazio Banda mtunza bustani, na labda mtu mmoja au watu wengine wawili kwenye mnyororo wa thamani wa mboga.
KAMBOLE:
Sawa, namba za Grevazio ni ____________.
FILIUS:
Nimeipata. Asante, rafiki yangu. Nitakushukuru katika programu yangu kwa kuifanya iwezekane.
SFX:
MZIKI KWA UFUPI UNAFIFIA NA SIMU INAITA
FILIUS:
Filius Chalo Jere kutoka Breeze FM. Je! Unayo muda wa kuzungumza nami juu ya kilimo chako kipindi hichi cha hali ya sasa ya COVID-19?
GREVAZIO:
Ndio, tunaweza kuzungumza. Ninasikiliza programu yako. Daima unasema kuwa programu ya Kilimo ni Biashara ndio nafasi ambayo sisi wakulima tunaweza kujieleza na kusikilizwa. Biashara ya kilimo imekuwa changamoto katika wakati huu wa janga hili. Serikali inatarajia tuishije?
FILIUS: Kabla hatujaingia katika hilo, tafadhali niambie jinsi mambo yalivyokuwa hapo awali.
GREVAZIO:
Mambo yalikuwa mazuri sana. Unajua, bustani yangu iko ukingoni mwa Mto wenye kutiririsha maji mwaka mzima wa Lutembwe, na nina pampu ya kusukuma maji kwa kukanyaga. Kwahivyo basi, nina maji mengi katika kipindi cha mwaka mzima, tofauti na marafiki zangu wengine ambao vyanzo vyao vya maji hukauka ndani ya mwaka. Kwa hivyo, nina bustani kubwa sana na mboga nyingi.
FILIUS:
Kwa kawaida unauzaje mboga zako?
GREVAZIO:
Kwa kawaida, mimi huchukua mboga zangu hadi kwenye soko la kijani kibichi (Green market) katika mji ambapo wafanyabiashara wa kati na wanawake wafanyabiashara wa kati hununua kwa wingi. Lakini njia hii sio nzuri kwasababu wanawake wanasumbua hadi wajadili bei hadi kiwango ambacho mkulima yuko ukingoni mwa kutoa tu mazao yake. Kwa hivyo wakati mwingine mimi hufanya ushawishi ili kupata mikataba ya kusambaza mboga hospitalini na shule za bweni. Wakati mwingine, mimi huzunguka kwa baiskeli yangu na kuuza moja kwa moja kwa watumiaji.
FILIUS:
Je! Unakabiliwa na changamoto gani sasa kwa kuwa kuna vizuizi kwenye kutembea?
GREVAZIO:
Kwanza, vizuizi au kufungiwa huku kulikuja ghafla sana, na nilikuwa na mboga nyingi ambazo zilikuwa tayari kuvunwa. Mwanzoni, sikujua jinsi ya kuzisambaza. Nilijaribu kuzunguka mjini mara kadhaa kwasababu tulihitaji pesa ya chumvi na sabuni na mboga zinaweza kupotea ikiwa hazikuvunwa.
FILIUS:
Je! Hukuenda mjini bila kujali?
GREVAZIO:
Hakika, ilikuwa ni tabu. Polisi walikuwa maeneo yote kuhakikisha kuwa kila mtu ambaye yupo barabarani ni mfanyakazi muhimu na amevaa barakoa. Kwa kuongeza, lazima uweke angalau umbali wa mita moja kutoka kwa mtu anayefuata, ambayo ni ngumu sana wakati wa kuuza mboga. Lazima pia kunawa mikono kwa kutumia kitakatishi chenye kemikali ya kusafisha kabla ya kuingia kwenye duka lolote kununua sabuni au sukari na vitu vingine muhimu.
FILIUS:
Hiyo lazima ilikuwa shida sana kwako.
GREVAZIO:
Ndio, ilikuwa hivyo. Niligundua pia kuwa kile nilichokuwa nikifanya ni hatari kwasababu ikiwa nitaambukizwa nitachukua virusi na kurudi navyo kijijini na watu wengi wanaweza kufa kwasababu yangu.
FILIUS:
Hicho kitakuwa ni kitu cha kusikitisha sana. Lakini basi, mboga zako ziko katika hatari ya kwenda kupotea. Utafanya nini?
GREVAZIO:
Nimewasiliana na hospitali na watatumia usafiri wao kuja kuchukua mboga. Wafanyakazi wa hospitali wanaonekana kuwa wafanyakazi muhimu, kwa hivyo wanaweza kutembea kwa uhuru. Shida pekee katika kufanya biashara nao ni kwamba hawalipi pesa taslimu mara moja, na sisi tunahitaji pesa sana.
GREVAZIO:
Nina bahati kwasababu watu kutoka katika vijiji vinavyozunguka wanakuja kununua mboga zangu.
FILIUS:
Ina maana kwamba vizuizi vya kutembea havijaleta athari katika vijiji?
GREVAZIO:
Sio sana. Lakini hakuna vizuizi vikali kabisa hapa. Tunaweza kuzunguka kwa muda mrefu ikiwa tumevaa barakoa na wala hatukusanyiki katika vikundi vya zaidi ya watu hamsini.
FILIUS:
Lakini umesema una mboga nyingi. Nina hakika kuwa uuzaji wa mara moja tu kwa hospitali na kuuza kwa ujanja kwa wanakijiji wenzako haitoshi kuepusha kupoteza mboga zako ambazo zimeshakuwa. Una mpango gani wa kuepuka kupoteza mazao yako?
GREVAZIO:
Mke wangu ni mbunifu sana. Ameanza kuvuna mboga na kupika kidogo kabla ya kuzikausha kwenye kichanja kwenye kivuli. Tunaziita mufutsa na ana mpango wa kuuza mufutsa kwa watu wa mjini mara tu jambo hili litakapomalizika. Mboga kavu zina bei ya juu sana jijini, na haziharibiki na kuwa mbaya kama zile ambazo ni mbichi kutoka shambani. Kwakweli, kadri zinavyokaa zaidi, ndivyo zinavyokuwa tamu zaidi.
FILIUS:
Hakika, huo ni ubunifu sana kwake.
GREVAZIO:
Mke wangu anafikiria hata kutengeneza jam kwasababu tuna nyanya nyingi. Walakini, kiungo muhimu zaidi ni sukari, ambayo hatuwezi kupata kwa urahisi kwasababu ya vizuizi vya kutembea. Pia si rahisi kupata mitungi kwa ajili ya kuweka jam. Pamoja na yote, hivi vizuizi ni vizuri kwasababu imetufanya tufikirie kuhusu kuongeza thamani kwa mazao yetu.
FILIUS:
Asante kwa kuzungumza nami, Bwana Banda. Ulisema mwanzoni kwamba wakati mwingine uliuza mboga zako moja kwa moja kwa watu kwenye maboma. Je! Unaweza kunipa namba ya simu ya mteja wako mmoja au wawili ili niweze kuwapigia?
GREVAZIO:
Labda unaweza kuzungumza na Bi Miriam Mwale. Alikuwa mteja wangu wa mara kwa mara na nina hakika kupata mboga kwa sasa imekuwa changamoto kubwa kwake sasa. Nambari yake ni _____________.
FILIUS:
Kwa ushirikiano wako. Baada ya kukoma kwa vizuizi vya kutembea, hakika nitakuwa mmoja wa wateja wako wa mara kwa mara wa mboga.
SFX:
MZIKI KWA UFUPI UNAFIFIA NA SIMU INAITA
FILIUS:
Jina langu ni Filius Chalo Jere. Mimi …
MIRIAM:
(MAONGEZI YANAINGILIWA) Oh, wew ni rafiki wa wakulima kutoka Breeze FM. Ni ajabu sana kupata simu yako! Lakini . . . Mimi sio mkulima. Uhusiano wangu pekee na wakulima na kilimo ni kwamba mimi hununua mboga zao. Kwa hivyo, siwezi kuwa mdau muhimu wa programu ya Kilimo ni Biashara, je naweza kuwa!
FILIUS:
Kweli wewe ni mdau haswa. Ninataka kuzungumza na wewe kama mtu ambaye hununua mboga kutoka kwa wakulima. Nina hakika una changamoto katika kipindi hiki cha kufungwa au vizuizi vya kutokutembea.
MIRIAM:
Bila shaka ninayo changamoto. Vizuizi vya kutokutembea vinaweza kuwa vizuri kama kinga dhidi ya COVID-19. Lakini ni kama gereza kwa sababu hatuwezi kwenda sokoni au dukani. Hatuwezi kwenda hata kanisani na shule zimefungwa. Kwa hivyo, kila mtu yuko nyumbani kama mbuzi kwenye zizi.
FILIUS:
Lazima iwe nzuri kwako, kuwa na kila mtu karibu kwa mara moja.
MIRIAM:
Ndio, ni nzuri kwasababu tunakuwa karibu kama familia na tunajuana vizuri. Mume wangu pia hawezi kwenda nje kunywa bia yake na kurudi akipiga kelele kama banshee na kunuka kama kitu kutoka kwenye dampo la takataka.
Watoto pia wanasoma zaidi, kuandika zaidi, na kutazama Runinga na kucheza zaidi. Lakini wanaposhiba, wanaanza kupigana na lazima niamulie pigano moja baada ya lingine.
FILIUS:
(ANACHEKA TARATIBU) Ni jambo la kushangaza kwamba kila wakati kuna kitu kisichoweza kupendeza katika kila kitu, bila kujali ni Kizuri vipi.
MIRIAM:
Ndio, ni bahati mbaya. Lakini haujasikia yote. Kufungiwa huku kumepunguza ufikiaji wetu wa chakula. Hata hivyo imeongeza matumizi ya chakula nyumbani. Je! Nitahudumiaje vinywa hivi vyote vyenye njaa wakati siwezi kwenda kwenye soko la kijani (green market) na wakulima hawawezi kuja mjini na mboga zao? Nina amini, watu wengi watakonda na kuwa mifupa tu wakati vizuizi vitakapokoma.
FILIUS:
Kwa hivyo unapataje mahitaji ya kila siku ya familia yako?
MIRIAM:
Ni vita ya kupanda kama kupanda mlima. Kwa bahati nzuri, nina unga kidogo ndani ya nyumba na ninaandaa vitafunywa kwa ajili ya kiamsha kinywa chetu. Pia nina chakula kikavu kama maharagwe na mufutsa ambazo nilinunua kwa wingi kabla ya uwekwaji wa vizuizi.
FILIUS:
Inafurahisha kuwa unazungumza juu ya mufutsa kwasababu nilikuwa nikiongea na mkulima mmoja aliyeitwa Grevazio Banda. Alisema mkewe yuko bize kusindika mboga zake kuwa mufutsa za kuuza. Je! Mufutsa zina faida yoyote zaidi ya mboga mbichi za kawaida kutoka shambani?
MIRIAM:
Binafsi, ningesema mufutsa zina faida nyingi. Kwanza kabisa, ni aina ya kuhifadhi mboga kwa matumizi wakati wa miezi migumu. Ina ladha nzuri kwasababu kawaida hukaushwa kwenye kivuli.
Kama matokeo ya ukaushaji huu, ni kama ukusanyanyikaji wa virutubisho kwasababu virutubisho vingi vya kwenye mboga mbichi kutoka shambani huhifadhiwa kwa muda mrefu sana. Tofauti na mboga mbichi ambazo wingi wa virutubisho hupungua wakati wa kupika, mufutsa huongezeka kwa kiasi wakati majani makavu ya mboga yanaponyonya maji na kujaa.
FILIUS:
Unamaanisha mufutsa inaweza kuchukua nafasi ya mboga mbichi kutoka shambani?
MIRIAM:
Sio kweli. Bado tunahitaji mboga mbichi kutoka shambani, vinginevyo tutapata ugonjwa wa kiseyeye na magonjwa mengine kama wale mabaharia maskini wa siku za zamani.
FILIUS:
Kwa hivyo unawezaje kuhakikisha una mboga mbichi kutoka shambani wakati wakulima hawawezi tena kuzileta mjini kwasababu ya janga hilo?
MIRIAM:
Kwa kweli, inawezekana kwasababu Bwana Kambole ambaye ni afisa kilimo amekuwa akituhimiza kuanzisha bustani za nyuma ya nyumba.
FILIUS:
Nilikuwa nikiongea naye hivi karibuni na amekubali kuzungumza kwenye programu yangu juu ya bustani za nyuma ya nyumba.
MIRIAM:
Hiyo itakuwa nzuri sana. Nilikuwa nikifikiri bustani ya nyuma ya nyumba itasababisha upotezaji wa maji kwa mazao. Lakini sasa ninagundua kuwa bustani za nyuma ya nyumba zinaweza kusababisha utumiaji mzuri wa maji machafu kwasababu tungeyatumia kwenye mboga badala ya kuyatupa tu.
MIRIAM:
Hakika nitaangalia kile atakachosema kwenye programu hiyo. Nina hakika ninaweza kuanza bustani yangu mwenyewe ya nyuma ya nyumba mara tu baada ya kumsikiliza. Jambo hili la COVID-19 na vizuizi vya kutokutembea kumetufundisha masomo muhimu juu ya jinsi ya kukabiliana na hali hii.
FILIUS:
Kwa kweli, imekuwa hivyo Bi Mwale. Nimejifunza pia mengi kutokana na hali hii. Kwanza, lazima nipanue programu yangu kwasababu sasa ninatambua kuwa biashara ya kilimo haimaanishi wakulima tu bali hata wafanyabiashara wa kati na wanawake ambao hununua kutoka kwa wakulima na kuuza kwa watumiaji kama wewe.
Inamaanisha pia kuwashirikisha watu kama wewe kwenye njia ndogo za kuzalisha mboga kwenye bustani zako za nyuma ya nyumba. Kwa hivyo, angalia sehemu yangu inayofuata ya Kilimo ni Biashara kwenye Breeze FM, Bibi Mwale, kwa sababu hivi karibuni utakuwa mmoja wa nyota wangu wa kipindi!
FILIUS:
Msikilizaji, janga la COVID-19 kwa kweli limeleta mateso mengi, na tumefika mwisho wa programu hii bila kuwa na majibu. Kwa kweli, tumekuwa na maoni kadhaa juu ya jinsi wakulima, wafanyabiashara wa kilimo, na watumiaji wanavyokabiliana. Lakini zaidi ni dhiki.
Ili kushughulikia maswala kadhaa yaliyoibuliwa katika programu hii, labda wakulima na wakaazi wa mijini wanapaswa kukutana katika eneo la mnada ambalo limetakaswa na linalodhibitiwa na Wizara ya Afya na wadau wengine. Mamlaka ya afya ingekuwa na kipima joto kwa ajili ya kupima na kutafuta wale waliokutana na wenye maambukizi.
Wasiwasi mwingine muhimu ni maji. Wakulima wengi katika maeneo ya vijijini hawana huduma ya kupata maji kwa ajili ya kunawa mikono ili kuepuka kupata virusi. Kwa kweli, hawajui hata umuhimu wa kunawa mikono mara kwa mara na suala la kukaa umbali kati ya mtu na mtu.
Walakini wakulima ni muhimu sana. Ni muhimu katika kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa kuhusu kumaliza umaskini na njaa na kuhakikisha usalama wa chakula. Kwa hivyo ni lazima sote tuunge mkono mchango wa wakulima katika kuboresha lishe na kufanya kilimo kuwa endelevu zaidi.
Kumbuka kwamba COVID-19 ni ya kweli. Kwasababu hii, tafadhali zingatia hatua zote za kudhibiti maambukizi ili kuwa salama. Kwa kuongeza, tafadhali fanya kila linalowezekana kukabiliana na hali hiyo. Kama nilivyosema, wakulima wanaweza kuwa funguo za kumaliza umaskini na njaa na kufikia kuwa na usalama wa chakula.
Acknowledgements
Shukrani:
Imechangiwa na: Filius Chalo Jere, Muandaaji wa kipindi cha Kilimo ni Biashara, Breeze FM, Chipata, Zambia
Imeoitiwa na kuhakikiwa na: Elisabeth Wilson, mwandishi wa habari na mtaalamu wa mawasiliano
Information sources
Vyanzo vya habari
Mahojiano:
Kambole Kanyanta, Mchumi wa kilimo, Wizara ya Kilimo Chipata, Zambia, Aprili 2020.
Grevazio Banda, mkulima wa mboga, Eneo la Makazi ya Kauzu, Chipata, Zambia, Aprili 2020.
Bibi. Miriam Mwale, mama wa nyumbani, CS 19, Old Jim Compound, Chipata, Zambia, Mei 2020
Rasilimali hii imeandaliwa kwa msaada wa kifedha kutoka kwa serikali ya Canada uliotolewa kupitia Global Affairs Canada.