Kausha mbegu za mpunga bila kuziweka ardhini ili upate mazao yenye ubora

Shughuli za baada ya mavunoUzalishaji wa mazao

Ujumbe kwa mtangazaji

Wakati wa mavuno, huwa tunawaona wakulima wengi wakianika mazao yao ardhini au kando ya barabara. Lakini, tabia ya kuanika mazao kwenye ardhi inaweza kusababisha mazao hao yakaroa na kuharibika kwa haraka. Muswada ufuatao unaelezea njia rahisi ya kukausha mbegu bila kuziweka ardhini. Njia hii imetumiwa kwa mafanikio makubwa na wanawake wakulima kutoka nchini Bangladesh.

Script

Piga kiashirio cha kipindi na kiashirikio cha kituo chako cha redio

Mtangazaji:
Karibu katika kipindi chetu cha leo. Wote tunafahamu kuwa majira ya mvua yanapokuja, mavuno nayo yako njiani yanayoambatana na ukaushaji wa mbegu za mpunga. Ni vigumu kukausha kitu chochote wakati wa masika, hususan mbegu. Ndio maana kipindi chetu kimelenga katika mada ya njia bora za ukaushaji wa mbegu.

Kwanza, kabla ya kuendelea mbele, pata burudani hii ya muziki [mtaje mwanamuziki].

Muziki wa ala

Mtangazaji:
tumerejea tena, na kama nilivyosema hapo awali, leo tunazungumzia jinsi unavyoweza kukausha mbegu zako za mpunga wakati wa masika na kuzihifadhi zikiendelea kuwa na ubora wake.

Nadhani niko sahihi, pale ninaposema kuwa wakulima wengi wanaosikiliza kipindi hiki, kwa kawaida wanaanika mazao yao nje ya uwanja, mashambani au kando ya barabara. Lakini, mara mvua inapoanza kunyesha unakimbia haraka na kuanza kuanua kila kitu kwa kuhofia kuwa mazao yako yanaweza kuroa, sawa? Na zaidi ya hayo, unafanya kazi kutwa nzima kuhakikisha kuwa mazao yako hayachezewi na watoto au kuku wanaotaka kuyadonoa.

Lakini, tatizo kubwa kuliko yote katika kuanika nafaka kwenye ardhi ni kwamba zinaweza kuharibika haraka sana mara baada ya kuvunwa. Hii ni kwa sababu mbegu zinafyonza unyevu kutoka ardhini. Zaidi ya hayo, mchanga, magugu, na uchafu unaochanganyika na mbegu, unapunguza ubora wa mazao. Ni rahisi pia kwa vitu mbalimbali kuchanganyika pamoja. Je kuna njia mbadala ya kuanika mbegu ardhini, je wewe unafanyaje?

Kwa mara nyingine tena sikiliza muziki, halafu nitakupatia majibu ya maswali hayo.

Muziki wa ala

Mtangazaji:
Karibu tena. Nimesema kuwa, kuanika mbegu ardhini kunapunguza ubora wake. Mazao yanaharibika. Kwa hiyo ni muhimu kuhakikisha kuwa mazao hayagusani na udongo. Kwa bahati kuna njia nyingine unazoweza kutumia kukausha mbegu zako.

Moja kati ya njia hizo tumeipata kutoka nchini Bangladesh. Wanawake nchini Bangladesh wanatumia mikeka, majamvi, na hata meza kuanika mbegu zao. Mazao yanayoanikwa kwenye meza yanakauka haraka kutokana na hewa inayopatikana katika eneo hilo. Kwa kuanika mbegu kwenye meza, wanawake hawa walikuwa na uhakika kuwa mbegu zao hazichafuki. Na mara mvua inapoanza kunyesha wanawake hawa hunyanyua meza zao haraka na kuziingiza ndani, hivyo mbegu zao haziroi.

Awali wanawake hawa walikuwa wakipata shida sana kukausha mazao yao wakati wa kipindi cha masika. Na mara walipogundua kuwa mazao yao yanaweza kukaushwa kwenye kivuli, na kwamba upepo ndio unaowasaidia kukausha, wameshatatua tatizo hili.

Hili ni jambo ambalo hata wewe unaweza kujaribu – kukausha mazao kwenye meza. Haitakugharibu sana kufanya hivi. Unachohitaji ni misumari, mbao, mianzi au miti. Kwa kifupi kazi hii haiwezi kukugharimu chochote – kila kitu unaweza kutoa shambani, labda tu hiyo misumari. Kama utatengeneza meza ya mianzi, hiyo ndiyo itakuwa rahisi zaidi kwani pia ni rahisi kubeba. Na mara unapoona dalili ya mvua ni rahisi kuinyanyua.

Meza pia inaweza kutumika kwa matumizi mengine. Unaweza kuitumia kukaushia samaki, unga, bizari, pilipili na vitu vingine. Meza ni imara na wala haina gharama kubwa, inaweza pia ikatumika kama kitanda au sehemu ya kuhifadhia vitu vingine.

Punguza muziki na weka sauti ya mtangazaji

Mtangazaji:
Huo ndio mwisho wa kipindi chetu kwa leo. Kwa wale ambao ndio kwanza wamejiunga nasi, tunapenda kuwataarifu kuwa tumekuwa tukizungumzia faida ya kuanika mbegu ama nafaka zako kwenye mikeka, majamvi au hata kwenye meza.

Mpendwa mkulima wa mpunga, kama unahitaji nakala ya vipindi vya televisheni kuhusu usafishaji wa mbegu, ukaushaji na uhifadhi wa mazao, unaweza kuwasiliana na [mtangazaji wa redio anaweza kutoa namba za mawasiliano au mahali vipindi hivyo vinapoweza kupatikana kwa wasikilizaji.].

Acknowledgements

Washiriki : Felix S. Houinsou, mshauri wa redio za vijijini /kituo cha ukulima wa mpunga barani Africa (WARDA)
Imepitiwa na : Paul Van Mele, kiongozi wa programu, mafunzo, na mfumo wa ubunifu / kituo cha ukulima wa mpunga barani Africa (WARDA)

Information sources

Mtangazaji anaweza kujiunga na: http://www.warda.org/warda/guide-video.asp kuona maeneo yaliyoelekezwa ili aweze kujua ni wapi mikanda ya video inapouzwa. Au anaweza kuangalia orodha iliyojumuishwa katika muswada huu.

Shirika la kimataifa la misaada ya kilimo (IFAD) kwa kusaidia utafiti shirikishi kwa wanawake wakulima wa mpunga katika maeneo ya nchini na kwa kutafsiri mkanda wa video wa kilimo cha mpunga kwa lugha yao.

The Bill & mfuko wa Melinda Gates na IFAD kwa kusaidia kutayarisha muswada