Mkulima anatumia ushauri wa Mtaalam wa mifugo ili kuokoa kuku kutokana na ugonjwa wa kideri

Ujumbe kwa mtangazaji

Pakua na hariri taarifa hii kwa matumizi yako

Vidokezo kwa Mtangazaji

Katika nchi ya Mali, karibu 70% ya watu wanaishi katika maeneo ya vijijini na kutegemea kilimo cha mazao, kufuga mifugo, na uvuvi. Kufuga kuku ni sehemu ya utaratibu wao wa kila siku. Ndege huzaa haraka, ni rahisi kulisha, na kuleta faida. Kuku ni “benki ya simu” kwa wanakijiji nchini Mali; fedha wanazopata kutokana na kuuza kuku huwasaidia kulipa gharama mbalimbali za familia mara kwa mara.

Katika Wilaya ya Bougouni, ufugaji wa kuku ni shughuli kuu ya vijana. Vijana hawa wameamua kubaki vijijini kwa sababu kuu za ufugaji wa kuku kuwapa faida kubwa, ambayo inawawezesha kufikia mahitaji makubwa ya familia zao.

Ndivyo ilivyo kwa Soumaïla Diakité, mwanamume mwenye umri wa miaka 28 ambaye, baada ya kuishi miaka miwili mjini, aliamua kurudi kijijini kwake ili kufuga kuku. Lakini, kama wafugaji wengi wa kuku katika eneo hilo, alikabiliwa na ugonjwa wa kideri. Ugonjwa huu una athari kubwa kwa wafugaji wa kuku, licha ya juhudi za Serikali na mashirika ya umma yaani NGOs. Ugonjwa wa kideri hauna tiba, lakini kuna chanjo ambayo inaweza kuuzuia. Sehemu ya tatizo ni kwamba wakulima wanapendelea kutunza kuku zao wenyewe badala ya kuuliza ushauri wa wataalam wachache wa mifugo wa jamii kwa msaada.

Katika muongozo huu, tunamtembelea mkulima mdogo wa kuku katika kijiji cha Bougouni, kilomita 160 kutoka mji mkuu wa Mali, Bamako. Siku ya ziara yetu, mtaalam wa mifugo na chanjo ya ndege alikuwa akitoa chanjo dhidi ya ugonjwa wa kideri, ambao uliharibu kundi la mfugaji huyo mwaka uliopita.

Moussa Koné ni mtaalamu mkuu wa mifugo na uzalishaji katika Wilaya ya Bougouni. Anatoa chanjo ya mifugo na kutoa huduma za kuku katika vijiji karibu na Bougouni, na anawashauri wakulima jinsi ya kuzuia magonjwa ya kuku kwa ujumla, na hasa ugonjwa wa kideri, ambao yeye anauita “ugonjwa wa ndege wa hatari zaidi”.  Katika muongozo huu, anamshauri mkulima mdogo ambaye alimwomba kumsaidia kuokoa kuku ake.

Unaweza kuchagua kutumia muundo huu wa kipindi hiki kama sehemu ya kipindi chako cha kawaida cha kilimo, kwa kutumia waigizaji wa sauti kuwakilisha wasemaji. Ikiwa ndio, tafadhali hakikisha unawaambia wasikilizaji wako mwanzoni mwa kipindi kwamba sauti ni ya washiriki, sio watu wa awali waliohusika katika mahojiano.

Unaweza pia kutumia muongozo huu kama nyenzo za utafiti au kama msukumo wa kuunda kipindi chako juu ya kudhibiti magonjwa ya kuku au mada sawa na hii katika nchi yako.

Zungumza na wakulima na wataalamu ambao hufuga kuku au wanajua kuhusu ndege.

Unaweza kuwauliza:

  • Je kaya yako inafuga kuku katika eneo lako?
  • Je, wakulima wanatumia mifumo wa kuwaachia kuku huru, au wanaweka ndege zao katika sehemu au maisha yao yote?
  • Je, ni yapi magonjwa makubwa ya kuku katika eneo lako? Ni ufumbuzi gani ambao wafugaji wa kuku na wataalamu wengine wamepata kwa changamoto hizi?

Mbali na kuzungumza moja kwa moja na wakulima na wadau wengine muhimu katika sekta ya kilimo, unaweza kutumia maswali haya kama msingi wa kipindi kwa ajili ya mawasiliano kwa njia ya simu au ya maandishi.

Inakisiwa muda wa kipengee hiki ni dakika 15-20, ikiwa ni pamoja na kuweka ufunuzi wa kipindi na kufuna kipindi.

Script

WAHUSIKA:

MARIAM KONÉ:
Mwandisi wa habari katika gazeti la Mtangazaji

SOUMAÏLA DIAKITÉ:
Mfugaji wa kuku, kijiji cha Flaboula

MOUSSA KONÉ:
Mtaalam kiufundi wa afya ya mifugo

MARIAM KONÉ:
Mpenzi msikilizaji, habari za wakati huu. Mara nyingine tena, asante kwa kuchagua Radio La voix des paysans [Maelezo ya mhariri: Radio Sauti ya Mkulima.] Karibu katika Maendeleo vijijini, kipindi cha kila wiki. Leo, tunawasilisha hadithi ya mkulima mdogo wa kuku ambaye anakabiliwa na ugonjwa wa kideri.

Jina langu ni Mariam Koné na mimi ni mwandishi wa habari wa Mtangazaji, gazeti linaloongozwa na wanawake. Tutaongozana pamoja kwenda kijiji cha Flaboula, katika Wilaya ya Bougouni, kilomita 160 kutoka Bamako. Katika kipindi hiki tunajifunza jinsi mkulima Soumaïla Diakité alivyoweza kuokoa kuku dhidi ya ugonjwa wa kideri, kwa sababu ya ushauri wa wataalam wa mifugo. Baada ya ugonjwa kuzuka kwenye kuku zake, mkulima huyu mdogo hakuacha ufugaji, lakini alileta kuku wapya. Wakati huu, aliamua kumuita mtaalam wa mifugo. Mtaalamu anampa ushauri na anawapa kuku zake chanjo. Hebu sasa tusikilize hadithi ya mkulima.

SFX:
SAUTI ZA UFUGAJI KWA SEKUNDE CHACHE, KISHA SHUSHA SAUTI CHINI ISIKIKE KWA MBALI

MARIAM KONÉ:
Ni saa 6:30 mchana, na sisi ni shamba la Soumaïla Diakité. Shamba lipo katika eneo la misitu nyuma ya kijiji. Mheshimiwa Diakité alitoa sehemu moja ya msitu kujenga “ngome” yenye kuvutia na matofali yaliyokaushwa kwa jua na majani. Mti wa shea umesimama katikati ya ua, na kuku, ndege aina ya kanga, na ndege wachache wa Uturuki hukaa katika kivuli chake kupunga upepo ili kuepuka jua kali. Mwelekezi wangu na mimi tulitembea kilomita tisa chini ya jua hilo ili kuhoji mkulima mdogo kwenye shamba lake la kuku.

Kelele ya pikipiki yetu iliwazindua ndege, ambao wamesambaa kwenye bustani iliyojaa majani. Kuna mabanda ya kuku mwishoni mwa ua la nyumba, na mkusanyiko wa mahindi, mtama, ulezi, na uwele na mchanganyiko wa nafaka mbalimbali. Dakika chache tu, kuku na ndege na ndege aina ya kanga wametawanya nafaka wakitafuta nafaka ardhini, na mbegu.

Shamba la mahindi linazunguka bustani ya mkulima huyu mdogo. Mtu mrefu aliyevaa suruali ya kijivu na shati nyekundu na vesti yenye matobo madogo madogo anatoka shambani. Ni Soumaïla Diakité, mwanamume aliyeoa mwenye watoto watatu, licha ya umri wake mdogo. Anatembea kuja kwetu akitabasamu na kuweka masikio ya mahindi aliyovuna shambani chini. Anamsalimia mwelekezi wangu kwanza kabla ya kunifikia na kunishika mkono kwa heshima na kunisalimia kwa kumaanisha.

SFX:
SAUTI YA NDEGE WA MWITUNI NA KUKU ZIKICHANGANYIKA NA MAZUNGUMZO YA WATU

SOUMAÏLA DIAKITÉ:
Habari za asubuhi. Bibie! Natumaini hujachoka kwa safari. Barabara zetu haziwezi kupitika wakati wa msimu huu wa mwaka.

MARIAM KONÉ:
Habari za asubuhi, Soumaïla. Ninaendelea vizuri, shukrani. Mimi ni Mariam Koné kutoka gazeti Mtangazaji. Nimekuja hapa kuzungumza na wewe kuhusu ugonjwa wa kideri. Nilichagua shamba lako kwa sababu wanakijiji waliniambia kuwa unapenda ufugaji wa kuku, lakini ugonjwa huu umekuwa kikwazo kuzuia maendeleo yako. Soumaïla, ugonjwa huu ni nini na kwa nini wanakijiji wote huita “ugonjwa mkubwa wa mlipuko”?

SOUMAÏLA DIAKITÉ:
Pia tunauita “tingatinga la banda la kuku.” Wakati ugonjwa unaingia ndani ya banda la kuku, manyoya pekee ndiyo yanakubakia. Watu wengine huita “uti wa mgongo wa kuku” kwa sababu baadhi ya kuku wanapooza na hata kuwa vipofu, baada ya kuteswa kwa kuhara. Kuku zingine huwa kama vichaa.

MARIAM KONÉ:
Vichaa?

SOUMAÏLA DIAKITÉ:
Ndio, wanayumba wakati wanatembea na kufanya sauti za ajabu ajabu. Wanafanya kama vile watu wenye kichaa waliopotea porini.

MARIAM KONÉ:
Ulikutana nao wakati gani na ugonjwa huu wa kideri?

SOUMAÏLA DIAKITÉ:
Nilipoanza ufugaji wa kuku. Ugonjwa huu ni wa zamani ambao tumeweza kuudibiti kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Wafugaji wote wa kuku ambao wana mabanda ya kuku wanakabiliwa na ugonjwa huu, hata kama si wafugaji wakuu. Ndiyo sababu, kila mwaka, watu wanatafuta kizazi kipya cha vifaranga kujaza nyumba zao kabla ya ugonjwa huo kurudi tena.

MARIAM KONÉ:
Je ni wakati gani katika mwaka ugonjwa huu hutokea?

SOUMAÏLA DIAKITÉ:
Inatokea wakati wa baridi, kati ya Novemba na Februari. Ndio wakati kuku wa jirani zangu huugua.

MARIAM KONÉ:
Je! umewahi kujiuliza kwa nini wakati huu ni hatari kubwa sana kwa kuku zako?

SOUMAÏLA DIAKITÉ:
Kulingana na wazee, ni upepo ndio huleta ugonjwa huo. Lakini tangu nilipopoteza kuku wengi, nilikwenda Bougouni kumwomba mtaalam wa mifugo kama angeweza kutembelea kuku zangu na kufanya kitu hivyo ugonjwa huu haukuwashika kuku zangu kwa mwaka huu.

MARIAM KONÉ:
Je! Ugonjwa huo uliathiri kiasi gani wakati wa mwisho ulipovamia kuku zako?

SOUMAÏLA DIAKITÉ:
Miezi nane iliyopita, kulikuwa na kuku zaidi ya 80 katika banda langu la kuku. “Ugonjwa mkubwa wa mlipuko” uliharibu kizazi chote. Sasa, nina kuku 50 tu walioachwa. Habari njema ni kwamba kuku zangu watano wametotoa vifaranga wiki mbili zilizopita.

MARIAM KONÉ:
Kwa nini umengojea muda huu wote kabla ya kumwomba bwana mifugo akusaidie?

SOUMAÏLA DIAKITÉ:
Nilikuwa nawapa chanjo kuku zangu mwenyewe mapema kabla ya msimu, kabla ya ugonjwa huo. Lakini, mara nyingi, kuku waliugua siku chache baadaye, na wengi walikufa.

MARIAM KONÉ:
Je! Unakumbuka uliwapoteza kuku wangapi baada ya kuwapa chanjo kuku zako?

SOUMAÏLA DIAKITÉ:
Nilipoteza karibu thelathini. Ilikuwa Februari iliyopita.

MARIAM KONÉ:
Je, mtaalam wa mifugo alikupa ushauri kabla ya kuidhinisha chanjo?

SOUMAÏLA DIAKITÉ:
Hapana.

MARIAM KONÉ:
Na wewe hakumwuliza ushauri wowote? Una uhakika yeye ni mtaalam wa mifugo halisi?

SOUMAÏLA DIAKITÉ:
(AKICHEKA) Uko sawa. Mimi tu nilinunua dawa ya chanjo. Ananiuzia bila ushauri wowote. Kwa sababu anauza bidhaa za wanyama, kila mtu anamwita mtaalam wa mifugo.

MARIAM KONÉ:
Je! Unanunua wapi tena chanjo au bidhaa za kutibu kuku zako?

SOUMAÏLA DIAKITÉ:
Mara nyingi ninanunua kutoka kwa muuzaji wa mitaani ambaye anakuja kwenye soko la kijiji chetu kila wiki.

MARIAM KONÉ:
Je, yeye huuza bidhaa gani?

SOUMAÏLA DIAKITÉ:
Anauza madawa ya kutibu magonjwa mengine.

MARIAM KONÉ:
Kama vile…?

SOUMAÏLA DIAKITÉ:
Kuna chupa ndogo za dawa ya kuua chawa, vimelea, na hasa ugonjwa wa malale, inayoitwa buganw ka sumayia katika lugha ya Bambara.

MARIAM KONÉ:
SAWA. Nadhani mtaalamu wa mifugo atakuja na kutupa maelezo.

SFX:
SAUTI ZA PIKIPIKI IKIKARIBIA

MARIAM KONÉ:
Kwa hiyo, hebu eleza kumhusu mtaalam wa mifugo …

SOUMAÏLA DIAKITÉ:
Na ninao uhakika atakuja!

MARIAM KONÉ:
(AKICHEKA). (Maelezo ya Mhariri: mwandishi hutaja msemo na kusema: “Ongea juu ya shetani na ana hakika kuonekana.”)

SFX:
SAUTI YA PIKIPIKI POLEPOLE IKIWASILI, KISHA PANDISA SAUTI ZA KUKU NA NDEGE WAKIKIMBIAKIMBIA, KISHA UTULIVU.

MARIAM KONÉ:
(HADHIRA) Mtu mfupi anaegesha pikipiki yake nyekundu aina ya skuta chini ya mti wa shea katikati ya bustani. Anavua kofia yake ya pikipiki na anasema hello.

MOUSSA KONÉ:
Habari ya asubuhi!

MARIAM AND

SOUMAÏLA:
Salama. Habari ya asubuhi.

SOUMAÏLA DIAKITÉ:
Mariam, huyu ni Moussa Koné, ni fundi na mtaalam wa mifugo kutoka Bougouni ambaye nimesema habari zake.

MARIAM KONÉ:
Habari za asubuhi. Imekuwa vema kukutana nawe. Mimi ni Mariam Koné, mwandishi wa habari wa gazeti la Mtangazaji. Inaonekana kwamba idadi kubwa ya kuku hufa hapa. Nimekuja hapa kuona mambo mwenyewe. Napenda kuhojiana nawe ili uweze kutuambia zaidi kuhusu ugonjwa huu wa kuku?

MOUSSA KONÉ:
Itakuwa ni furaha yangu kufanya hivyo. Lakini napenda kuchunguza ndege wachache na kukagua mabanda ya Soumaïla kwanza. Ungependa kuwa msaidizi wangu?

MARIAM KONÉ:
Sawa. Nifanye nini kwanza? Je! Unanitaka mimi nibebe mkoba wako?

MOUSSA KONÉ:
La hasha. Kwanza kabisa, angalia kile ninachokifanya.

MARIAM KONÉ:
(AKICHEKA) Hilo alina tatizo!

MARIAM KONÉ:
(HADHIRA) Mtaalamu wa mifugo anainama kidogo, na kuingia ndani ya banda la nyumba ya kuku ya kwanza, na kuzungusha macho kukagua banda kwa kifupi. Anafanya jambo lile lile kwa nyumba ya pili ya kuku. Nami ninasimama ndani ya banda la kuku. Ni joto sana. Sakafu imefunikwa na vitu vyeupe na vyeusi na harufu mbaya. Baada ya kuchukua hatua chache ndani, Moussa Koné akakimbia hadi mlangoni na akatoka kuelekea kwenye mti wa shea ambapo kuku na ndege aina ya kanga wamepumzika wakifurahia kivuli cha mti kukwepa joto la jua kali.

MOUSSA KONÉ:
(AKIONGEA NA SOUMAÏLA) Nilitathmini nyumba za kuku zako. Jambo la kwanza unalopaswa kufanya ni kuweka dawa ya kuua wadudu kabisa kabisa. Banda lako la kuku halitunzwi vizuri. Kuna uchafu uliogandamana, sakafu imejaa unyevunyevu na ni baridi, na pananuka vibaya.

SOUMAÏLA DIAKITÉ:
Kweli! Kwa jinsi gani?

MOUSSA KONÉ:
Lazima uangalie sakafu, choma vinyesi vya kuku, na kisha pia nyunyiza nyumba yako na dawa ya kuua wadudu. Pia, mimi nakushauri kuanzia sasa usiwachukulie kuku zako kwa urahisi. Unasema unawapa chanjo kuku na kanga zako peke yako. Lakini kuna mchakato maalum unapaswa kufuata ili kuzuia ugonjwa wa kideri. Utahitaji kuchukua mafunzo na kupata chanjo zinazozingatia viwango. Ili kuzuia kuku zako kuambukizwa na ugonjwa wa kideri, lazima uzingatie ratiba ya chanjo na matibabu sahihi.

SOUMAÏLA DIAKITÉ:
Sawa. Masikio yangu yote yanasikia.

MOUSSA KONÉ:
Kwanza, tunapaswa kuwachanja vifaranga mara tu wanapokuwa wameanguliwa na kisha kuwapa kipimo cha kuwakuza wiki moja au siku 15 baadaye. Baada ya kila chanjo, lazima tuwape dawa kuwaondolea mfadhaiko. Hii imetengenezwa kwa kiuavijasumu na vitamini. Kiuavijasumu na vitamini huondoa haraka ndege kutokana na matatizo ambayo husababishwa na chanjo na inapunguza kushindwa kwa chanjo. Kwanza, tutaenda kutoa chanjo kwa vifaranga vyenye siku 15 au zaidi.

MARIAM KONÉ:
(KWA HADHIRA) Bila kusema neno, mkulima mdogo alielekea katika banda ambapo alikusanya vikapu vitatu vilivyotengenezwa na vichaka vya mashina ya mitende. Kuna kuku na ndege ya kanga katika vikapu hivi.

MARIAM KONÉ:
(KWA MKULIMA) Je kuku zako tayari wameshaandaliwa?

SOUMAÏLA DIAKITÉ:
Ndiyo.

MOUSSA KONÉ:
Hebu nione. (SAUTI YA CHUMBA NDOO IKISHIKWA MKONONI) Ndiyo, naona chanjo ya ugonjwa wa kideri, lakini nyingine ni dawa ya wanyama, kama ng’ombe na mbuzi. Hii sio mzuri kwa kuku!

SOUMAÏLA DIAKITÉ:
(AKISISTIZA) Lakini mmoja wa marafiki zangu katika kijiji kingine alinipa. Anatoa kwa kuku na ndege ya kanga, na wana afya nzuri.

MOUSSA KONÉ:
Unaweza kunipa jina lake?

SOUMAÏLA DIAKITÉ:
Jina lake ni Amadou Coulibaly.

MOUSSA KONÉ:
Je! Tunazungumzia kuhusu Amadou huyo aliye na Djakarta ya bluu? (Maelezo ya Mhariri: “Djakarta” ni aina ya pikipiki inayotumiwa na watu nchini Mali.) Ikiwa ndiye huyo, nilikwenda kwake juma la jana ili kutoa chanjo kwa kuku na ndege ya kanga. Kuku zake hufanya vizuri si kwa sababu anawapa madawa haya, lakini kwa sababu anatumia ushauri niliyompa ili kuzuia ugonjwa wa kideri.

SOUMAÏLA DIAKITÉ:
Kweli?

MOUSSA KONÉ:
Ndiyo. Dawa hii inapendekezwa kwa magonjwa ya wanyama, na inatumiwa kwa ng’ombe kwa kipimo cha kilogram 100 au zaidi. Kwa hivyo nakushauri kuacha kuchanja kuku zako kwa dawa hii.

SOUMAÏLA DIAKITÉ:
Ninakuelewa.

MARIAM KONÉ:
Soumaïla, kwa nini umeweka vifaranga katika kikapu?

SOUMAÏLA DIAKITÉ:
Si rahisi kushika vifaranga. Ndio maana mimi nimewaweka katika vikapu ili kupata chanjo.

MOUSSA KONÉ:
Msaidizi wangu, unaweza kuniletea chupa tupu imefungwa kwenye pikipiki?

MARIAM KONÉ:
Ndiyo, bwana!

SOUMAÏLA DIAKITÉ:
Mafunzo yenye nguvu sana hii! (KICHEKO)

MARIAM KONÉ:
(KWA HADHIRA) Nina chupa tupu, ambayo ndani yake ni ina rangi nyeupe.

MOUSSA KONÉ:
Asante.

MARIAM KONÉ:
(KWA HADHIRA, POLE POLE) Mtaalamu wa ufugaji wa mifugo hufungua chupa tupu na kuondoa kifuniko kama vile Soumaïla anayeshikilia. Anajaza sindano. Soumaïla anachukua vifaranga mmoja mmoja, na mtaalam wa mifugo huinua mbawa zao tete. Vifaranga vinapigana na kuruka vibaya.

SFX:
SAUTI YA VIFARANA WAKIKIMBIA NA KULIA SANA KWA SEKUNDE 10, KISHA PUNUZA SAUTI NA ACHA KWA SAUTI YA CHINI.

MARIAM KONÉ:
Hatua kwa hatua, kikapu kinaisha wakati Soumaïla akitoa vifaranga ili awape dozi ya chanjo. Kwa kelele ya kusikia iliyofanywa na kuku, bata wa Uturuki, na ndege aina ya kanga, Soumaïla, kwa msaada wa mkewe na ndugu yake mdogo, huleta ndege kupewa chanjo. Operesheni yote inakaribia dakika arobaini.

MARIAM KONÉ:
Lakini daktari, kuna chanjo iliyoachwa.

MOUSSA KONÉ:
Ndiyo. Chupa hiki kina kutosha kwa ndege 100 na dozi inapaswa kutolewa kwa kila ndege na ni nusu mililita.

SOUMAÏLA DIAKITÉ:
Nilikuwa natumia chupa mbili kwa kuku 60. Nadhani nilikuwa nikifanya makosa.

MARIAM KONÉ:
(KWA MOUSSA KONÉ) Ninaona kwamba unaweka chanjo yako kwenye baridi, tofauti na chanjo za Soumaïla, zilizo kwenye meza katika chumba chake cha kulala. Je! Hii inashauriwa?

MOUSSA KONÉ:
(KWA MOUSSA KONÉ) Siyo jinsi Soumaïla anavyotumia kulinda chanjo, wala dozi aliyowapa kuku wake iliyozingatia viwango vya huduma za mifugo. Chanjo hii lazima ihifadhiwe katika nyuzi nane Celsius za baridi. Ikiwa haihifadhiwi kwenye joto hili, inakuwa sumu kwa kuku. Badala ya kuwalinda, huwafanya wagonjwa.

Wakulima wengi wa kuku hukataa kufuga kuku kwa sababu wanaamini kwamba ni chanjo inayowaua. Lakini chanjo haiwezi kuua; ni mfumo mbaya wa kuhifadhi na kushindwa kutoa dozi sahihi ambayo ni tishio kubwa kwa ndege.

Ninamshauri Soumaïla na wakulima wengine wasiisikilize kile ambacho wasio wataalam wanasema. Huduma za mifugo zinapatikana kwa wakulima wote. Wanahitaji tu kujiandaa na watujulishe siku ambayo inawafaa, ili tuweze kuja na kutibu kuku zao. Na sisi tu radhi.

MARIAM KONÉ:
Niambie zaidi kuhusu ugonjwa wa kideri.

MOUSSA KONÉ:
Ugonjwa huja kwa aina tatu: aina ambayo ni kali kidogo tu na ni ya kawaida sana, aina ambayo ni ya kawaida kali kiasi, na aina ambayo ni kali sana.

MARIAM KONÉ:
Je “ukali” maana yake nini?

MOUSSA KONÉ:
Ina maana kwamba ina uwezo wa kusababisha dalili kali za ugonjwa huo. Inategemea aina ya virusi, ugonjwa unaosababisha, jinsi inavyobadilika, na matokeo yake, kwa mfano, idadi ya kuku wagonjwa, idadi ya kuku waliokufa, na wakati wa kuingizwa.

Katika baadhi ya matukio, shinikizo lenye virusi linaweza kuua ndege wengi, ingawa ndege huonyesha ishara chache za ugonjwa huo.

Pamoja na aina kidogo ya virusi, kuku pia wanaweza kufa bila kuonyesha dalili yoyote, isipokuwa manyoya kusimama, mabawa kulegea, na ukosefu wa nishati na hamu ya kula.

MARIAM KONÉ:
Nini kuhusu ugonjwa wa kawaida au wenye nguvu? Je! Ndege wana aina hizi za ugonjwa huangalia na sauti yake kama ya nini?

MOUSSA KONÉ:
Kuku wenye virusi ya kawaida wana matatizo ya kupumua kama vile kukohoa, kupiga chafya, na sauti ndogo za kukoroma wakati wanapumua. Ishara nyingine ni uvimbe wa kichwa na shingo. Kuku zinaweza kuharisha kijani, na uzalishaji wa mayai unaweza kushuka kwa kasi. Wakati mwingine mayai husababishwa kukosa sura nzuri.

Ndege zilizo na ugonjwa zinaweza kutetemeka au kuchanganyikiwa. Wanaweza pia kuwa na shida ya kutembea na katika mbawa na miguu yao, kutembea kwa mzunguko, kiarusi, kupepesuka, au kupooza. Kunaweza kuwa na kuhara kinyesi cha kijani, uzalishaji wa mayai unaweza kuacha au kupunguzwa, na mayai yanaweza kuwa na rangi isiyo ya kawaida, sura, au ganda.

Vifo vinaweza kufikia 100%. Aina hii ya ugonjwa wa kideri unaweza kuwa kama mafua ya ndege. Mafua ya ndege yanaambukiza sana. Unaenea kwa haraka na wanadamu wanaweza kuharibiwa na ndege wagonjwa au kwa kutumia vifaa vichafu. Wanadamu wanaweza kufa kutokana na homa ya ndege. Ndiyo sababu unapaswa kutoa ripoti pale ambapo kuna vifo vingi vya ndege wa kufugwa ndani na a mwitu kwenye mamlaka husika.

MARIAM KONÉ:
Je ugonjwa huu unaeneaje?

MOUSSA KONÉ:
Ugonjwa wa Kideri mara nyingi huenea kwa kukaribiana na ndege wagonjwa – ama kwa njia ya kugusa kinyesi au kupitia hewa kama makamasi, mate, au kwa njia ya chakula kilichoathirika, maji, vifaa, au nguo za kibinadamu.

MARIAM KONÉ:
Je unapendekeza njia zipi za matibabu?

MOUSSA KONÉ:
Hakuna tiba ya ugonjwa wa Kideri. Njia pekee ya kuzuia ni kwa kuwapa kuku chanjo.

Wakulima wanapaswa kuhakikisha kuwa kuku wanachanjwa mara tu wanapokuwa wameanguliwa na kuwapa chakula cha kukuzia kwa wiki moja baadaye, au siku kumi na tano na zaidi. Hii inaweza kusaidia kuzuia ndege kwa miezi mitano au sita dhidi ya ugonjwa wa Kideri. Chakula cha kukuzia kinaponya chanjo ambazo zilishindwa.

Pia, wafugaji wa kuku wanapaswa kuweka taratibu za ufanisi kuzuia ugonjwa wa kuingia kwenye shamba lao au kuku zake. Wakati virusi vitakavyoonekana katika kundi lisilo na afya njema, wafugaji wanaweza kuhakikisha kwamba ndege zao zote zitaambukizwa ndani ya siku mbili hadi sita.

MARIAM KONÉ:
Moussa Koné, umejibu maswali yangu yote. Je, una maneno yoyote ya mwisho?

MOUSSA KONÉ:
Kitu cha mwisho nataka kuwaambia wafugaji wa kuku ni kuheshimu mpango wa chanjo. Vifaranga vinapaswa kupatiwa chanjo mara tu wanapokwisha kuanguliwa. Kisha, wanapaswa kupata kipimo cha nyongeza siku saba baada ya chanjo ya kwanza na siku 15 baada, na wanapaswa kupata dozi ya mwisho ya chanjo ya nyongeza siku ya 21.

Baada ya kuku kuchanjwa kuku siku ya kwanza, tunatoa vitamini kwa wakulima ili wachanganye na maji ya kunywa ya vifaranga. Wakulima wanapaswa kutoa vitamini kwa vifaranga wakati wa kipindi kizima cha chanjo.

Hivyo vifaranga vinapaswa kupata kipimo cha nyongeza cha chakula cha kukuzia mara moja kwa wiki kwa wiki tatu zifuatazo chanjo ya kwanza ikiwa unataka kuwa chanjo kabisa dhidi ya ugonjwa wa Kideri. Wakulima hawapaswi kusubiri kipindi cha baridi kabla ya kuandaa ndege. Ugonjwa wa Kideri ni kila mahali, na unaweza kutokea wakati wowote kama kuku hawakupokea chanjo.”

MARIAM KONÉ:
Ni nini kinachotokea na chanjo nyingine katika chupa? Je! Utaenda kutupa mbali, au …?

MOUSSA KONÉ:
Hapana. Nitakwenda kijiji kilicho karibu na kuchanja kuku za wafugaji watatu. Ninaenda sasa. Asante kwa msaada wako. Wewe ni msaidizi mzuri! (KICHEKO)

SFX:
SAUTI YA PIKIPIKI IKIPUNGUZWA IKIPOTEA MBALI. SAUTI YA KUKU WAKILIA NA KUOGOPA NA KUSHUSHA CHINI POLE POLE.

MARIAM KONÉ:
Msikilizaji Mpendwa, tulikuwa na Flaboula na mkulima wetu wa kuku. Ili kuokoa kuku zako na ugonjwa wa Kideri, unapaswa kuchanja vifaranga tangu siku ya kwanza ya kuanguliwa hadi siku ya 21. Lazima pia uwape vitamini katika kipindi hicho cha chanjo. Usisahau kuwapa kipimo cha chakula cha kukuzia kila wiki, na kusafisha na kufuta nyumba zao mara kwa mara.

Ni muhimu sana kuuliza daima toka mtaalam wa mifugo ili kuchanja kuku, na kutumia ushauri kila ushauri wa mtaalam wa mifugo. Hii ni muhimu ikiwa unataka kuokoa kuku zako kutoka katika ugonjwa wa Kideri.

Asante kwa tahadhari yako ya aina hii Natumaini ulikuwa na wakati mzuri wa kusikiliza Sauti ya Mkulima. Tutaonana wiki ijayo.

Acknowledgements

Shukrani

Kutolewa na: Mariam Koné, mwandishi wa habari katika gazeti la Mtangazaji

Iliyotathminiwa na: Moussa Koné, Mkurugenzi wa Idara ya Viwanda ya Mifugo, Huduma za Mitaa za Wanyama (SLPIA), Bougouni, Mali

Tovuti ya Wizara ya Mali ya Maendeleo Vijijini: www.developpementrural.gouv.ml

Mahojiano:

Soumaïla Diakité, mkulima wa kuku katika kijiji cha Flaboula

Moussa Koné, mtaalamu wa mifugo

Tarehe ya mahojiano: Septemba 11, 2015

 

Tafsiri ya hati hii inafadhiliwa na ELANCO ANIMAL HEALTH

Information sources

Vyanzo vya habari

Tovuti ya Wizara ya Mali ya Maendeleo Vijijini: www.developpementrural.gouv.ml

Mahojiano:

Soumaïla Diakité, mfugaji wa kuku katika kijiji cha Flaboula

Moussa Koné, mtaalamu wa mifugo

Tarehe ya mahojiano: Septemba 11, 2015