Maji ni uhai. Yagawe.

Ujumbe kwa mtangazaji

Watu wengi hushiriki mapambano kwa manufaa ya walio wengi.  Lakini mara kwa mara, matokeo huishia kuwanufaisha watu wachache tu wenye mali katika jamii.  Makala haya yanasimuilia kisa kilichotokea katika kijiji cha Tiopazi nchini Malawi.  Kijiji kiliimbuka na wazo la kumaliza njaa katika jamii yao kwa kuanzisha mradi wa kunyunyizia mimea maji.  Katika miaka ya kwanza ya mradi huu, ni wachache tu walionufaika.  Hata hivyo, kijiji hiki hakikufa moyo.  Walipambana na matatizo hayo na kufua dafu.   Isipokuwa Bw. German na Bw. Bimphi, majina yote katika makala haya ni ya kubuni. Makala haya ni hadithi iliyobuniwa na ambayo ina misingi ya mahojiano kamili na wanakijiji.  Unaweza kutumia makala haya kama msukumo kutafiti na kuandika makala juu ya mada sawia katika eneo lako.  Ama unaweza kuchagua kutoa makala haya katika kituo chako ukitumia waigizaji wa sauti kuwakilisha wazungumzaji.  Endapo utafanya hivyo, tafadhali hakikisha unaiambia hadhira yako mwanzoni mwa kipindi kuwa sauti hizo ni za waigizaji na wala si wazungumzaji asilia walioshiriki katika mahojiano.

Script

Wahusika

German:
Mtu mwenye busara na moyo safi katika kijiji
Mkuu wa Kijiji:
Mwenye busara lakini menye unyonge mara kwa mara.
Eda:
Mwanamke mzee, mjane, anawalea mayatima walioachwa na mwanawe wa kiumealiyefariki aliyefariki njaa.
Bimphi:
Mlevi wa kawaida. Mwenye bidii, lakini anayetumia pesa zake nyingi kulewa pombe.
James:
Mpwa wa Mkuu wa Kijiji, mgumu wa roho na mchoyo
Jacob:
Rafiki mwema wa Bimphi, mwenye bidii na asiyeshiriki pombe

Msimulizi:
Kijiji cha Tiopaizi katika eneo linalosimamiwa na Chifu Msakambewa kilipoteza watu watano kwa ajili ya njaa mnamo 2001. Baada ya mkasa huu, waligundua kuwa kuna hazina fiche ambayo ilkuwa haitumiki: kulikuwa na mto wa kudumu katika kijiji kile. Walikutana baada ya kushinikizwa na mpendwa afisa kilimo wa eneo lao. Walikubaliana kuanzisha mradi wa kunyunyizia maji mashambani ili kuongezea mavuno ya kutokana na maji ya mvua.

Lakini tatizo lilikuwa kuwa sehemu ilifaa zaidi kwa kilimo hiki cha unyunyiziaji maji ilikuwa sehemu ya eneo tengwa la msitu wa serikali. Walihitaji ruhusa kutoka kwa Idara ya Misitu kupitia kwa Mkuu wa Wilaya yao Bwana DC. Mkuu wa Kijiji aliamua kumwona Bwana DC. Je, Bwana DC atawapa ruhusa kutumia ardhi wanayohitaji?

FX:
Umati wa watu katika ua la mkuu wa kijiji.

Bimphi:
(Akiongea kwa sauti ya chini inayosikika chini ya kelele ya umati) Jacob, ona vile mkuu wa kijiji anaoenekana mwenye huzuni…..nilikwambia, Bwana DC hatakubali jambo hili.

Jacob:
Bimphi, hebu tusikilize anachotaka kutwambia….

Bimphi:
Lakini hii ndiyo ilikuwa nafasi yetu ya kupata pesa za kutosha kununulia bia

Jacob:
Wewe hufikiria bia pekee. Marafiki zako wanafikiria chakula.

Bimphi:
Mkuki kwa nguruwe, tamu kwa binadamu. Nazungumzia chakula changu bwana….Si watu walikufa njaa na kuniacha mie – mlevi – hai?

Jacob:
Koma wee! Hilo si jambo la mzaha.

Mkuu wa Kijiji:
Kimya tafadhali! Kimya! Nimewaita hapa nyote ili niwaeleze matokeo ya mazungumzo yangu na Bwana DC.

Bimphi:
(Kwa sauti ya kilevi) Mkuu wa kijiji, wewe tuambie moja kwa moja ulilotuitia.

James:
(Akimkemea Bimphi) Nyamaza wewe! Tunataka kusikia anachosema mkuu wa kijiji.

Bimphi:
Nani hataki kusikia sasa…? Wewe James hujiona mwelevu sana.

Umati:
(Kelele) Aaaa wewe!

Sauti:
Bimphi daima huwa mlevi – yeye hupata wapi pesa?

Sauti nyingine:
Ni kweli. Kinachomnonesha nguruwe hakijulikani, au siyo?

Mkuu wa Kijiji:
Keti wewe Bimphi, na unyamaze… Bwana DC…. amekubali ombi letu

Wote:
Ndio, ndio.

Wanakijiji wanaimba wimbo wa kumsifu mkuu wa kijiji kwa ujasiri wake.

Kongwe:
Tiopaizi Ni samba ….iiiii.

Wote:
Yeye ni simba.

Kongwe:
Yeye ni simba.

Wote:
Yeye ni simba ii…ii…ndio, yeye ni simba ii…ii…ndio. Yeye ni simba

Mkuu wa kijiji:
Asanteni, asanteni. Ketini. Bwana DC atatuma masoroveya kuweka mipaka mipya kesho.

Wote: (
Wengine wakipiga mbinja Ndio, mkuu wa kijiji.

Mkuu wa kijiji:
Yeye ana furaha kuwa hatujawahi kunyakua sehemu ya msitu. Hii ndiyo zawadi yetu.

Eda:
(Analia kwa kwikwi) Oh, mkuu wa kijiji, tazama. Haya yanafanyika wakati tayari nimepoteza mwanangu mpendwa kwa ajili ya njaa. Asante, mkuu wa kijiji!

Bimphi
: Eda bibi yetu, hii si siku ya matanga bibie… tunaserehekea hapa. Usituharibie shangwe, mama. Tutakuwa na pesa za kutosha kulewa sasa.

Eda:
(Akiongea pole pole) Bimphi, inasitikisha kuwa mradi huu wa unyunyiziaji maji mashambani unakuja baada yangu kupotesha mtoto wa miaka ishirini na mitano kwa sababu ya njaa…. Hebu angalia mayatima na mama yao alioniachia.

Mkuu wa kijiji:
Ama kwa kweli ni jambo la kusikitisha kuwa tulifiwa na watu watano kutokana na njaa mwaka uliopita…Mungu na awarehemu.

Bimphi:
Ndio, mkuu wa kijiji. Ama kwa kweli Mungu awarehemu.

Mkuu wa kijiji:
Nina tangazo moja. Yule afisa wa ardhi atakuja kesho asubuhi kuhamisha mpaka wa eneo tengwa na kutuachia bonde…Tukutane pale na tutie bidii kulima ardhi ile.

Wote:
Ndio.

James:
Huu utakuwa mwisho wa njaa kijijini mwetu.

Mpito wa jukwaa

Msimulizi:
TWatu wa kijiji cha Tiopaizi walifanya kazi kwa bidii sana kulima ardhi waliopewa. Walifanikiwa kugeuza mto na kuuelekeza kwenye ardhi hii huku wakisaidiwa na afisa kilimo wa eneo lao. Watu walipanda mahindi ili kuongezea chakula chao. Mahindi yalistawi. Lakini jambo fulani likatokea. Ni jambo gani hili? Je, njaa itasahaulika katika kijiji hiki?

FX:
Jogoo anawika. Mlango unabishwa.

James:
Nani?

German:
Fungua mlango, James. Ni mimi.

James:
(Akiwa na usingizi) Nani?
German:
German…. Amka. Kuja twende tukanyunyizie maji mimea yetu kabla yaw engine kuamka.

James:
Kwani ni saa ngapi hizi?

German:
Ni saa kumi asubuhi…. Si tuliagana tuamke saa hizi?

FX:
Mlango unafunguliwa. James anaenda miayo.

James:
Usingizi ulikuwa mtamu huo. Unajua wakati wa baridi ya asubuhi, usingizi unakuwa mtamu.

German:
Mashamba yetu yako mbali na kitovu cha maji, hivyo hatuna bahati. Hii ndiyo maana lazima tuamke mapema namna hii.

James:
Najua. Hebu tuanzie shamba langu kwa sababu liko mbali zaidi. Tutaenda kwenye shamba lako baadaye.

German:
Hamna shida rafiki yangu.

Mpito wa jukwaa

FX:
Maji yakitiririka na kufanya makelele chini kwa chini

James:
German, Angalia! Maji yanavunja mkondo huo. Funga mtaro huo.

German:
Huoni kuwa najaribu kuufunga? Lakini maji bado yanavunja… …

James:
Sawa, fungua mtaro wa kuelekea unakotaka yaende kwanza ili upunguze nguvu zake. Kisha ufunge ile ya usikotaka yaende.

Wanacheka wote.

German:
Na kweli imefaa … ndio …

FX:
Kelele za maji zinaisha.

German:
Kuna nini sasa? Hebu ona, ni kiasi kidogo tu cha maji kinachokuja. Ni kitu gani kimetokea?…Kweli tutamaliza kunyunyizia maji leo kwa kutumia kiasi hiki kidogo kinachokuja? Dakika kumi kumaliza kijisehemu kimoja – haya mambo yamezidi!

James:
Nafikiri kuna kitu kilichozimba ule mtaro mkuu

German:
Nafikiri hayo ni kweli. Huenda hiyo ndiyo sababu….Tufanye nini?

James:
Hebu niende nikaone kinachoendelea…Wewe endelea kuweka maji – naja..
German:
Twende wote. Endapo ni jiwe kubwa lililozimba mtaro, huenda ikabidi watu wawili washirikiane kuliondoa.

Mpito wa jukwaa

FX:
Sauti ya maji

German:
Hakuna kitu kilichozimba mto hapa. Kila kitu ni sawa.

James:
Sawa, sasa ninajua. Naona kuwa Bimphi, Jacob na bibi Eda pia wanatumia maji, na mashamba yao yako karibu na kiini cha maji.

German:
Naam. Kwa hivyo tutafanya nini?

Bimphi:
(Tayari amelewa) Habari ya asubuhi German na James. Kwa nini mnaonekana wenye wasiwasi. Kuna nini?

James:
Bimphi, mlianza lini kunyunyizia maji?

Jacob:
James, hilo ni swali la aina gani? Una maana kuwa huoni kwamba tumeanza sasa hivi?

Bimphi:
Jacob, huwa sijibu maswali ya kijinga. Jibu langu kwa swali hilo litaleta tofauti gani?

James:
Bimphi, tayari unanifahamu, na naomba tusigombane. Sisi ndio tulitangulia kufika hapa. Mlitupata hapa na mnaweza kunyunyizia pindi tukimaliza.

Bimphi:
Kwa nini tusubiri mmalize kwanza? Mradi huu ni wetu sote.

German:
Shinda ni kuwa maji yameacha kuenda kwenye mashamba yetu kwa kuwa mnayatumia. Yanayofika kule ni kidogo no.

Jacob:
Je, hilo ni tatizo letu? Fanyeni mtakalo, lakini kamwe hatuachi kunyunyizia mimea yetu maji.

James:
Hivi ndivyo mambo yanavyofanyika: aliyetangulia anaanza yeye. Natoa amri uache. Kama huachi, nitakugonga.

Bimphi:
Sawa! sawa, Jacob, na tuyaache hayo. Mpwa wa mkuu wa kijiji anastahili kunyunyizia kabla ya wengine…huyu ni mtu anayeweza kumchapa ye yote yule akitaka.

James:
Usiongee, acha tu. Enda nyumbani urejee baadaye, kwa kuwa hatutaki utuingilie tena.

Bimphi:
Ndiyo, Chifu.

James:
Bi kizee, koma kunyunyizia na uende nyumbani.

German:
Anaweza kunyunyizia. Mwache anyunyizie.

James:
Kuna tofauti gani? (Kwa Eda) Koma, nenda nyumbani, kisha urejee baadaye.

Mpito wa jukwaa

Msimulizi:
Mzozano kuhusu maji umeanza. Je, tatizo hili litafika kikomo. Je, wanakijiji hawa watafikia malengo yao?

FX:
Sauti za kimaumbile za usiku vichakani.

James:
Tazama uzuri wa mahindi tuliyo nayo mwaka huu. Hayakauki kwa ukosefu wa maji kama mashamba haya mengine.

German:
Ama kwa kweli ni mahindi mazuri sana. Lakini hii ni kwa sababu tunaamka mapema ili kunyunyizia mimea yetu.

James:
Si ndio! Unajua kuwa mgaagaa na upwa hali wali mkavu?

German:
Najua. Lakini watu wanahoji kwamba hatuwapi nafasi kumwagia mimea yao maji..

James:
Je, unakubaliana nao? German, unakubaliana nao?

German:
Nimekuwa nikifikiria kuhusu suluhisho la kudumu kwa tatizo hili. Sipendi lile wazo la kuwahi huku tukiwa na watoto na wazee kati ya wanachama.

James:
Usiongee kama mhubiri. Sote tunafanya inavyostahili. Je, tunawasimamisha wale tunaowakuta mashambani….? Wewe fikiria, maji yameacha kutufikia. Hii ni haki? Wamekuja tena. Unayataka haya, German?

German:
Utafanya nini? Ni yule mama mzee, Bimphi na Jacob. Tufanye nini?

James:
Nitawakataza. Hawakutuelewa vizuri tulipowakataza jana.

German:
Hapana, mwache yule mama mzee amwagie maji. Yule bwana anaweza kuacha.

James:
Mnafanya nini leo tena Bimphi, Jacob, na wewe bibi?

Bimphi:
Kwa nini unauliza swali kama hilo wakati unaona kuwa tunamwagia maji mimea? Na kwa nini unauliza ni lini tunamwagia maji? Hukutuuliza maswali kama hayo tulipokuwa tunatengeneza mitaro na kufyeka vichaka.

FX:
Sauti ya kibao

Bimphi:
(Kwa hasira)Umenichapa kibao! Umenichapa kibao!…kwa nini? Kwa nini?…Siendi ng’o.
James:
(Kwa hasira) Kwa nini wewe daima unakuwa mkorofi? Ndiyo sababu ya kukuzaba kibao…. Sasa ondoka shambani.

Jacob:
Hapana James, usituchape – tutaondoka mara moja. Tunajua wewe ni hodari kwa vita.

Bimphi:
Mimi siondoki.

FX:
Sauti ya vibao zaidi.

Bimphi:
Basi! Basi! Tunaondoka.

James:
Muna hiari kwenda kuripoti haya kwa mkuu wa kijiji – mimi sijali. Kama tunatangulia kufika hapa, na mpate tunamwagia mimea maji, kamwe msianze kumwagia yenu. La sivyo, nitawatia adabu.

German:
Kuna nini, James?

James:
Kimya, German … Huenda nikasahau kuwa wewe ni rafiki yangu. (Kwa Eda) Eda, ondoka. (Kimya)Unafikiri ni mzaha? Ondokeni mrejee baadaye. Ama kunaye anayetaka kibao?

Eda:
Tafadhali niruhusu nimwagie maji mahindi yangu angalau kwa leo tu. Si unaona yanakauka?

James:
Tuliwaambia jana kuwa inategemea anayetangulia. Ulikuwa wapi? Ama ulizidisha usingizi kwa kuwa wewe ni mchawi?

Eda:
(Akilia) Msiongee hivyo wanangu.

James:
Mimi si mwanao..

Eda:
Wewe si wa rika langu. Unastahili kunipa heshima. Wewe ni rika la mjukuu wangu.

James:
Sisemi usirudi. Nasema ungojee nimalize. Nina haki pia.

Eda:
(Kwa kwikwi) Jana ulinikataza, leo vile vile. Hata umempiga Bimphi leo. Ah, mwanangu, usifanye hivyo.

German:
James, mwache tu amwagie. Tutaendelea baadaye.

Eda:
Eee, mwanangu. Tafadhali msihi rafiki yako. Unajua kuwa nachelewa kuamka kwa kuwa mwili huniuma; si unaelewa kuwa mimi ni mzee?.

James:
Hata, nina kazi nyingine, German…. Kwa hivyo Eda, unajua kuwa nikisema acha, nina maana kuwa uache! Sitaki fujo yo yote hapa..

Eda:
(Analia kwa kwikwi) Mwanangu, kwa nini ulikufa mapema hivi na kuniacha hai? Kwa nini ulinipa chakula ukajinyima na kufa wewe, badala ya kuniacha mie mzee, nife njaa.

German:
Bibi, enda. Nitamwaga maji shambani mwako nikimaliza kwangu.

Eda:
Asante mwanangu.

Mpito wa jukwaa

FX:
Eda analia kwa kwikwi

Mkuu wa kijiji:
Eda, kwa nini unalia?

Eda:
Chifu, mpwao James alinikataza kumwagia maji mimea yangu, jana na hata leo. Hata amechapa Bimphi vibao.

Village headman:
James? Kwa nini?

Eda:
Anasema alitangulia kufika. Tunapomwaga maji sote, hayafiki shambani mwake.

Mkuu wa kijiji:
Usiwe na wasiwasi. Mpwa wangu huyo ni kichaa. Wewe rejea baadaye umwagie mimea yako maji….German hakukusaidia?

Eda:
Tayari amenisaidia. Aliahidi kumwaga maji shamabani mwangu

Chief:
Sawa.

Mpito wa jukwaa

Bimphi:
Mkuu wa kijiji, hebu tuambie ni kwa nini watu fulani pekee ndio wanamwagia maji mimea yao kila siku, ilhali sote tulishiriki kuchimba mitaro and kufyeka vichaka?

Mkuu wa kijiji:
Naomba usimulie yote. Nini kilitendeka?

Bimphi:
James anadai kuwa yeye huamka mapema na hivyo huwahi kufika shambani kila siku. Hii ndiyo sababu anataka tusubiri amalize kabla hatujamwaga maji kwetu.

Mkuu wa kijiji:
Ah, kumbe. Kama ni hivyo, ana haki. Kwa nini usiamke mapema, hata kabla yake?

Bimphi:
Mimi naweza, lakini Eda je, mwanamke mzee ambaye anakatazwa kumwaga maji kwa sababu hiyo hiyo ya aliyetangulia anufaike kwanza?

Mkuu wa kijiji:
Nifanye nini kama wanaamka mapema kila asubuhi?

Bimphi:
Kwa nini wanahitaji kumwagia mahindi kila siku? Hawawezi kutuachia nafasi na sisi tukamwagia mara kwa mara?

Mkuu wa kijiji:
Mbona usimuulize?

Bimphi:
Kwa nini usimuulize kwa niaba yetu? Tayari tumeshazambwa vibao na unasema…. (kwa hasira hivi kwamba anashindwa kusema vizuri)ni… mm ..wuu..lize? Kumbuka tulishiriki wote kuchimba mtaro na kufyeka vichaka. Haya mambo ya aliyetangulia anufaike kwanza yametokea lini?

Mkuu wa kijiji:
Huwa sijibu maswali ya kijinga mimi.

Bimphi:
(Kwa hasira)Kama hakutakuwa na suluhisho ifikapo mwisho wa juma hili, nitatenda kitendo. Nitaharibu mtaro na itabidi uanze upya. Nilikuwa mshiriki katika mradi wote huo. Ukiwahi, utatangulia kitu gani?

Mkuu wa kijiji:
Usithubutu kuharibu mtaro. Ukifanya hivyo nitakufukuza kutoka kijijini mwangu.

Bimphi:
Hautathubutu. Nitakushtaki wewe kwa Mkuu wa Wilaya aliyetupatia ardhi ile.

Mkuu wa kijiji:
Wewe, usijaribu kufika huko. Unafikiri ninaweza kufanya nini kumkomesha James asiyakalie maji kwa kuwa yeye huwahi kuamka?

Bimphi:
Ita baraza ya kijiji kizima. Ulituita wakati wa kuanzisha mradi wa unyunyiziaji maji. Kwa nini usiite watu wote tena? Bwana DC atafikiwa na haya bila shaka.

Wimbo wa mpito wa jukwaa

Msimulizi:
Mkuu wa kijiji anajua kuwa Bwana DC atamtimua kama mkuu wa kijiji. Mkuu wa kijiji atafanya nini kuzuia Bimphi kuharibu mitaro na kumshtaki kwa Bwana DC?

FX:
Sauti ya kengele.

Boy:
(Kwa sauti iliyopaazwa) Mkuu wa kijiji anawaita nyote. Tukutane kwenye mradi wa kunyunyizia maji mashambani kesho asubuhi. Kaeni kwa utulivu.

Sauti ya kengele

Wimbo wa mpito wa jukwaa.

Msimulizi:
Mkuu wa kijiji atawaambiaje watu wale? Atawaambia vipi? Je, kuna suluhisho rahisi hapa?

FX:
Umati wa watu ukiongea

German:
Kimya tafadhali! Kimya! Naomba tumsikilize mkuu wa kijiji Bwana Tiopazi, shujaa wetu.

Mkuu wa kijiji:
Jamani watu wetu. Naomba mwenyekiti wa mradi huu wa kunyunyizia maji aje asimame na mimi hapa.

Bimphi:
Tulidhani wewe ndiye mwenyekiti.

Mkuu wa kijiji:
Mimi! Nimeshawahi kusema hivyo?

Umati:
Hapana, hapana!

Mkuu wa kijiji:
Kwa hivyo, namtaka kiongozi wa mradi huu wa kunyunyizia maji. German, ni nani mwenyekiti?

German:
Hamna bwana.

Mkuu wa kijiji:
Itakuwaje kitu kisicho na kichwa kisonge mbele? Nitakuwa msimamizi. Hebu tumchague mwenyekiti leo. Nipeni majina manne, tafadhalini, ya watu wanaoweza kuwa mwenyekiti.

Umati:
German. German Banda, tafadhalini.

Mkuu wa kijiji:
Mnakubaliana nyote?

Umati:
Ndio.

Mkuu wa kijiji:
German, wewe sasa ndiye kiongozi wa mradi huu wa unyunyiziaji maji mashambani. Kabla hatujachagua maofisa wengine katika mradi huu, niambie jinsi utakavyogawa maji kwa njia ya haki kwa wote, wakiwemo watoto na wazee.

German:
Nitatoa tu mapendekezo, lakini mnaweza kunipa ushauri tofauti. Ikiwa hampendezwi na mapendekezo yangu, mniambie.

Umati:
Ndio.

Bimphi:
German, tunajua kuwa unatupenda sote, na huwezi kutudhuru. Unaonaje?

German:
Mwanzo, naomba msamaha kwa yote ambaye huenda nilimwuudhi.

Bimphi:
Wewe tuambie tu suluhisho ni nini.

German:
Suala la bibi yetu Eda linanisumbua… Lakini nafikiri tunapaswa kujigawa katika makundi na kutumia maji katika siku tofauti kulingana na makundi hayo.

Umati:
Ndio! German! German!
Mkuu wa kijiji:
Naam mwanangu. Sasa natuchague maofisa wengine ambao watakusaidia kutekeleza mpango huo.

Mpito wa jukwaa

Msimulizi:
Je, unadhani matatizo ya ulafi katika matumizi ya maji yaliendelea? La, tatizo la ugavi wa maji lilifika hapo. Kila mtu alinufaika na akawa na usalama wa chakula. Umoja ni nguvu. Usingojee walevi kukushtua ili utekeleze yanayotakikana na kugawa maji kwa usawa. Maji ni uhai.

Acknowledgements

  • Imechangiwa na: Mwandishi mkuu Gladson Makowa, The Story Workshop, Malawi, mshiriki wa utangazaji wa Farm Radio International.
  • Yamehaririwa na: Erik Nielsen, Manager Country Based Programmes, Water Integrity Network na Alexandra Malmqvist, Assistant Communications Coordinator, Water Integrity Network.

Information sources

  • Mahojiano na Bw. Erick Bimphi na mkuu wa kijiji, Tiopazi.

Shukrani za dhati kwa Water Integrity Network kwa kufadhili makala haya ya uadilifu katika maji.

Canadian Flag Kipindi hiki kimekufikia kwa ufadhili wa serikali ya Canada kupitia Shirika lake la misaada la CIDA