Epuka hasara baada ya mavuno, kwa kutunza mazao yako vizuri: Kidokezo cha nane cha redio

Shughuli za baada ya mavuno

Ujumbe kwa mtangazaji

Baadhi ya wakulima wanafikiri kuwa ni vigumu kuepuka hasara baada ya mavuno, na wanashindwa kuchukua hatua madhubuti kuepuka hasara hizo. Unaweza ukapoteza asilimia ishirini ya mazao yako baada ya mavuno na asilimia hiyo ikaongezeka zaidi pale unapovuma matunda na mboga. Ukiwa ni mtangazaji, una uwezo wa kuwaeleza wakulima kuhusu faida ya kupunguza hasara zinazoweza kupatikana baada ya mavuno. Vidokezo hivi vya redio vitawasaidia wakulima kuelewa kwamba kuna njia madhubuti za kupunguza uharibifu wa mazao na bado wakajiongezea kipato.

Kidokezo hicho kinaweza kurudiwa mara kadhaa ili kusisitiza ujumbe wa kutunza vema mazao. Kidokezo hicho ni vema kikawa kifupi ili kitumike katikati ya kipindi au mara baada ya tangazo la washitiri. Kwa kurudia utangulizi kwa kila kidokezo, wasikilizaji watabaini kuwa hivi punde jambo fulani muhimu litaanza kuelezwa katika kipindi.

Unaweza pia ukatengeneza matangazo ama vidokezo vinavyoelezea jinsi ya kuepuka hasara mara baada ya mavuno kwa kutunza vema matunda ama mboga zako. Unapotengeneza unaweza kuzingatia yafuatayo:

  • Jinsi ya kutengeneza jokofu la bei nafuu ili kuhifadhi matunda na mboga mboga
  • Njia za jadi za kutunza nafaka!
  • Ukaushaji kwa kutumia jua unaweza kuongeza kipato cha mkulima.
  • Kulima matunda na mboga kwa ajili ya soko la mjini
  • Kulima matunda na mboga kwa ajili ya soko la nje ya nchi
  • Njia bora ya kuvuna na kusafirisha maembe (na matunda mengine)

Kuongeza thamani katika shamba lako kwa kusindika chakula

Script

Kidokezo #1:
Kuvuna maembe kwa uangalifu

(Zingatia: Chagua tunda linalofaa katika eneo lako.)

Mazao yanapojeruhiwa wakati wa kuvuna au mara baada ya mavuno, yanaharibika kwa haraka. Unaweza kushindwa kuuza mazao yaliyoharibika au kujeruhiwa na wakati mwingine ukalazimika kuyauza kwa bei ndogo. Kwa upande mwingine, kama utafanikiwa kupunguza hasara, unaweza pia kuongeza kipato chako. Ifuatayo ni njia mojawapo ya kupunguza hasara.

  • Ni muda wa mavuno, je unachuma matunda au unayapiga ili yaanguke?
  • Unapokuwa ukichuma matunda, kuwa mwangalifu, usiyagonge kwenye mti au kuyaacha yakaanguka ardhini.
  • Kama tunda likianguka chini, linaweza kupata michubuko au majeraha.
  • Halafu magonjwa na vijidudu vinalishambulia, kwa hali hiyo, mara moja tunda huharibika.
  • Wakati mwingine inaweza kuwa vigumu kuzuia tunda lisianguke kutoka kwenye mti, lakini kama utaweza kuzuia idadi ya matunda yanayoanguka chini, utakuwa na bidhaa bora sokoni.

Kidokezo #2:
Mavuno ya matunda na mbonga asubuhi

Matunda yanapokuwa yamejeruhiwa wakati wa kuvuna ama baada ya kuvuna, huharibika kwa haraka. Unaweza hata ukashindwa kuyauza, au unaweza kulazimika kuyauza kwa bei ya chini. Kwa maana nyingine, kama utaweza kupunguza uharibifu wa matunda yako, utaongeza pia kipato chako. Hapa kuna njia mojawapo ya kupunguza hasara.

  • Je ni muda gani mzuri wa kuvuna matunda na mboga?
  • Jibu ni, wakati wa asubuhi!
  • Kama utavuna matunda yako na mboga wakati wa asubuhi, yataonekana kuwa ni mazuri na hayataharibika upesi.
  • Subiri mpaka utakapoona umande umekauka, halafu vuna kabla jua halijawa kali.
  • Unapovuna wakati wa jua kali, matunda na mboga zako zinaweza kusinyaa au kunyauka. Pia zitashambuliwa na magonjwa au wadudu.
  • Kwa hiyo vuna asubuhi ili uweze kupata mazao ambayo bado yanavutia na imara.

Kidokezo #3:
Matunda huharibika yanapokuwa juani

Zingatia: Muswada huu unahitaji sauti tatu tofauti –mtangazaji atakayetoa utangulizi na sauti mbili za kike ambapo moja itakuwa ya mama na ya pili ya binti.)

Mtangazaji:
Mazao yanapokuwa yamejeruhiwa mara baada ya mavuno au wakati wa kuvuna, yanaharibika kwa haraka. Unaweza kushindwa kuuza mazao yako ambayo yamejeruhiwa, au ukalazimika kuyauza kwa bei ya chini. Kwa maana nyingine, kama unaweza kuepuka hasara, unaweza kuongeza kipato chako. Hapa kuna njia mojawapo ya kupunguza hasara.

Ingiza sauti ya shamba kwa sekunde tano –ndege wakiimba, sauti ya ng’ombe au mbuzi, kuku – baada ya hapo changanya sauti ya magari katika barabara za vijijini

Mama:
Seema, tafadhali chukua hiki kikapu cha matunda ukiweke chini ya ule mti, tunapokuwa tukisubiri.

Binti:
Lakini mama, kikapu chenyewe ni kizito sana. Je siwezi kukiacha mahali kilipo?

Mama:
Hapana. Hapa kituoni hakuna kivuli. Jua litayapiga moja kwa moja matunda yetu mazuri ambayo tayari yameiva.

Binti:
Je jua linaweza kuharibu matunda?

Mama:
Ndiyo. Jua linapoyapiga matunda, litayafanya yakose maji na kunyauka, hivyo yataharibika haraka.

Binti:
Haya. Nitakwenda kukiweka kikapu kivulini.

Mama:
Asante. Endapo tutayaweka matunda kivulini, yataendelea kuwa imara na ya kuvutia hadi tutakapofika sokoni ambapo yatapelekea tupate fedha zaidi.

Binti:
Ndio – huenda tukapata fedha za ziada za kununulia pipi nyumbani!

Mama:
(Kicheko) Ndio, labda!

Kidokezo #4:
Kutoa tunda kwenye kikonyo

Matunda yanapokuwa yamejeruhiwa wakati wa mavuno au mara baada ya mavuno, yanaharibika kwa haraka. Unaweza ukashindwa kuuza mazao ambayo yameharibika au ukalazimika kuyauza kwa bei ya chini. Kwa lugha nyingine, endapo utazuia mazao yako yasiharibike, utajiongezea kipato. Hapa kuna njia mojawapo ya kupunguza hasara.

Wakulima wanajua kuwa mazao yaliyoharibika yanauzwa kwa bei ndogo. Lakini unawezaje kuchuma tunda kutoka kwenye kikonyo bila kulijeruhi?

Matunda mengi mabivu kama vile, matufaa, mapasheni na nyanya huwa yana tabia ya kujeruhiwa. Hii humaanisha kuwa baadhi ya vikonyo huendelea kubaki kwenye haya matunda.

Ni vizuri kuyavuna matunda haya kwa njia zifuatazo:

  • Kwa makini shika tunda halafu uliinue juu, kisha lizungushe likiwa kwenye kikonyo na halafu livute kutoka kwenye mti wake au shina.
  • Barabara! – inua tunda, lizungushe likiwa kwenye kikonyo, kisha livute kutoka kwenye mti au shina lake.

Hatua hii itafanya matufaa, mapasheni na nyanya visiharibike wakati wa kuvuna.

Kidokezo #5:
Jinsi ya kuvuna matunda ambayo hayajaiva

Mazao yanapojeruhiwa wakati wa kuvuna ama baada ya kuvunwa huharibika kwa haraka. Unaweza ukashindwa kuuza mazao yako yaliyoharibika au ukalazimika kuyauza kwa bei ya chini. Kwa lugha nyingine, unapopunguza hasara wakati wa kuvuna unaweza kujiongezea kipato. Hapa kuna njia mojawapo ya kupunguza hasara.

Wakati mwingine tunavuna matunda kama vile maembe, maparachichi, mapapai na hata malimao kabla hayajaiva sawasawa.

Matunda ya namna hii yanatakiwa kuvunwa kwa njia maalum ili vikonyo vyake visivunjike. Kama vikonyo vyake vikivunjika wadudu wanaweza kulishambulia.

Zifuatazo ni njia zitakazokifanya kikonyo kuendelea kubaki kwenye tunda:

  • Tumia kisu au kitu cha kukatia kukata kikonyo na sio shina.
  • Unapokuwa ukikata, hakikisha umeacha kipande cha kikonyo kwenye tunda.
  • Kama ukitumia kisu, hutalazimika kuvuta tunda kutoka kwenye kikonyo.

Hiyo ndiyo njia bora ya kuvuna mazao ambayo hayajaiva.

Kidokezo #6:

Mazao yanapojeruhiwa wakati wa kuvuna ama baada ya kuvunwa huharibika kwa haraka. Unaweza ukashindwa kuuza mazao yako yaliyoharibika au ukalazimika kuyauza kwa bei ya chini. Kwa lugha nyingine, unapopunguza hasara wakati wa kuvuna unaweza kujiongezea kipato. Hapa kuna njia mojawapo ya kupunguza hasara.

  • Unapowasili sokoni, je matunda na mazao yako yanakuwa katika hali gani?
  • Je unaweza kuuza kila ulichopakia kwenye gari?
  • Hii inategemea jinsi ulivyosafirisha mazao yako.
  • Jaribu kusafirisha mazao yako katika matenga yaliyotengenezwa kwa mbao. Matenga ya mbao yanazuia matunda kuharibika, kuliko ukiyasafirisha yakiwa ndani ya magunia makubwa.
  • Tumia matenga ambayo yahawezi kuharibika kwa urahisi yanapowekwa pamoja. Hali hii itapunguza michubuko kwenye matunda.
  • Uwe makini unapotumia matenga yaliyotengenezwa kwa mianzi – mara nyingi yanakuwa na ncha kali zinazoweza kujeruhi mazao.
  • Usisahau pia kutumia matenga ambayo ni masafi. Endapo utatumia maboksi au matenga yaliyotengenezwa kwa udongo, basi mazao yako yatakuwa katika hali mbaya. Hali kadhalika utapata fedha kidogo!

 

Kidokezo #7:
Epuka kuacha utomvu kwenye maembe

Mazao yanapojeruhiwa wakati wa kuvuna ama baada ya kuvunwa huharibika kwa haraka. Unaweza ukashindwa kuuza mazao yako yaliyoharibika au ukalazimika kuyauza kwa bei ya chini. Kwa lugha nyingine, unapopunguza hasara wakati wa kuvuna unaweza kujiongezea kipato. Hapa kuna njia mojawapo ya kupunguza hasara.

  • Kama unataka maembe yako yawe na bei ya juu, usiache yaharibiwe na utomvu unaotapakaa juu yake baada ya kuvuna.
  • Utomvu wa maembe ni kitu gani?
  • Unapokata kikonyo cha embe, utomvu hutiririka na kuharibu embe. Embe la namna hii huitwa embe lililounguzwa na utomvu.
  • Wateja hutoa fedha kidogo kwa ajili ya maembe yenye makovu ya kuungua, lakini unaweza kukwepa hali hii.
  • Unapokuwa ukivuna maembe yako, acha kikonyo kikining’inia kwenye tunda.
  • Halafu. Ligeuze embe chini juu, ndipo utoe kikonyo ukiwa karibu kabisa na tunda. Ni vizuri kulishikilia embe ukiwa umeligeuza chini juu, ili utomvu utiririke. Hakikisha utomvu haugusi embe.
  • Likandamize embe hilo chini juu kwa dakika thelathini hadi pale utomvu utakapokua umekwisha. Utomvu unapokuwa umekauka, basi embe lako linakuwa tayari kusafirishwa.

Kidokezo #8:
Barabara zenye makorongo zinaharibu mazao

Matunda yanapokuwa yamejeruhiwa wakati wa mavuno au mara baada ya mavuno, yanaharibika kwa haraka. Unaweza ukashindwa kuuza mazao ambayo yameharibika au ukalazimika kuyauza kwa bei ya chini. Kwa lugha nyingine, endapo utazuia mazao yako yasiharibike, utajiongezea kipato. Hapa kuna njia mojawapo ya kupunguza hasara.

Je baada ya safari ndefu ukipita kwenye barabara yenye makorongo kuelekea sokoni, huwa unafurahia ubora wa mazao yako?

Kama jibu ni hapana, sikiliza ushauri jinsi ya kusafirisha matunda yako na mboga katika barabara zenye makorongo.

  • Bananisha matenga yako unapopakia kwenye gari. Hii inasaidia unaposafirisha mazao yako kwenye barabara mbaya na hata kama gari lenyewe pia sio zuri sana. Barabara zenye makorongo na magari mabovu vinaweza kuharibu matunda na mboga zako na kusababisha hasara kubwa. Kwa kubananisha matenga, unapunguza matunda yasichezecheze na hivyo kupunguza hasara.
  • Je huna mazao ya kutosha kujaza tenga lako? Jaribu kulijazia kwa makaratasi yaliyochanika au vitu vingine vinavyofanana na hivyo. Lakini usishindilie sana, hiyo pia inaweza kuharibu. Jaribu kubananisha, lakini sio sana. Hali hiyo itafanya mzigo wako wa chakula kwa ajili ya mauzo kukaa vizuri!

Acknowledgements

Washiriki : Vijay Cuddeford, Vancouver kaskazini, Canada.

Imepitiwa na : François Mazaud, Afisa wa ngazi ya juu, katika kikundi cha udhibiti baada mavuno, FAO, Rome, Italia.

Information sources

  • Udhibiti wa mazao yanayoharibika haraka. FAO huduma ya kilimo, kijarida namba 43, 1981. Shirika la Chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO). http://www.fao.org/docrep/s8620e/S8620E00.htm#Contents
  • Udhibiti wa mazao yanayoharibika haraka : matundas,mboga na mazo ya mizizi, 1989. FAO mfululizo wa mafunzo: namba 17/2. Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO). http://www.fao.org/docrep/T0073E/T0073E00.htm
  • Soko la Mazao mchanganyiko – zana za kufundishia kwa maafisa wa Nje. FAO Kijarida cha kilimo namba 76, 1989. Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO). http://www.fao.org/docrep/S8270E/S8270E00.htm .
  • Compendium on Post-Harvest Operations. Ray Lantin. Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO). http://www.fao.org/inpho/inpho-post-harvest-compendium/en/
  • Ufungashaji wa matunda, mboga na mazao yatokanayo na mizizi, Cornelis C.M Schuur, 1988. Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO). http://www.fao.org/docrep/x5016e/x5016e00.htm