Zuia malaria wakati wa ujauzito!

Ujumbe kwa mtangazaji

Pakua na hariri taarifa hii kwa matumizi yako

Tatizo la Malaria wakati wa ujauzito na katika watoto linaendelea kuwepo nchini Zambia na kote barani Afrika. Ugonjwa huu umesabababisha vifo vingi, hasa kwa wanawake wajawazito na watoto wa umri wa chini ya miaka mitano.

Kulingana na Kituo cha Udhibiti wa Malaria nchini Zambia (The National Malaria Control Center), malaria huua zaidi ya watu milioni moja duniani kila mwaka, wengi wao wakiwa wanaishi Afrika, kusini mwa Sahara. Zaidi ya vituko milioni tatu za malaria huripotiwa katika vituo vya afya duniani kila mwaka.  Hii ni mara tano ya maambukizi ya kifua kikuu, UKIMWI, surua na ukoma kwa pamoja.  Malaria husababisha kifo kimoja kwa kila vifo vinne vya utotoni barani Afrika.  Ugonjwa huu huua mtoto wa Kiafrika kila sekunde 30. Wale wanaonusurika maradhi kali ya malaria huweza kuwa na ulemavu mkuu wa kimwili na kiakili.

Ni jambo la kusitikisha kuwa wanawake wana uwezekano mara nne wa kuugua na mara mbili wa kufariki kutokana na malaria endapo ni wajawazito. Nchini Zambia, asilimia ishirini ya vifo vya wakati wa ujauzito vinatokana na malaria. Wanawake wajawazito na watoto wanaougua malaria huchukua asilimia kubwa ya vitanda hospitalini.

Wataalam wa kiafya hupendekeza mambo kadhaa kuzuia uzambazaji wa malaria. Pendekezo mojawapo ni kutumia nyavu za vitandani zilizotibiwa kwa dawa ya mbu manyumbani.  Pendekezo lingine ni kuhakikisha boma na maeneo ya karibu nazo yamepuliziwa dawa.  Wanawake wanaoishi katika maeneo yenye malaria wanapaswa kunywa madawa ya kuzuia malaria kila mara wanapokuwa wajawazito ili kujikinga wenyewe na pia mtoto aliye tumboni.

Makala haya yanaangazia tajriba ya Bi. Mirriam Chawila, mwanamke Mzambia ambaye ana mimba ya miezi saba. Yanaonyesha mambo aliyokumbana nayo wakati malaria yalimvamia vikali.

Makala haya ni igizo ndogo lenye misingi ya mahojiano halisi na mwanamke mjamzito na maofisa wa afya. Unaweza kutumia makala haya kama msukumo kutafiti na kuandika makala juu ya mada sawia katika eneo lako. Ama unaweza kuchagua kutoa makala haya katika kituo chako ukitumia waigizaji wa sauti kuwakilisha wazungumzaji. Endapo utafanya hivyo, tafadhali hakikisha unaiambia hadhira yako mwanzoni mwa kipindi kuwa sauti hizo ni za waigizaji na wala si wazungumzaji asilia.

Script

Fifiisha sauti za nyumbani … sufuria, maji yakimiminika, na kukifagiliwa

Bi. Chawila:
Nancy, unaweza kuja kunisaidia kumaliza kusafisha madirisha tafadhali? Karibu nimalize. Lililobakia ni moja tu hili ya jikoni.

Nancy:
Shangazi, naomba nimalize kusafisha vyombo vya jikoni – naja sasa hivi.

Bi. Chawila:
EEEEEEhhhhyeeeee! Na Na Nanc …!

Nancy:
(Akipiga mayowe kwa hofu) Shangazi! Shangazi! Shangazi, kuna nini? Shangazi … Shangazi … Ongea! Saidieni! Saidieni jamani, … Shangazi yangu ameanguka kutoka juu ya stuli na kuzirai!

Bi. Bwalya:
(Sauti za miguu ya watu wakikimbia kwenye mic) (Kwa hofu) Mungu wangu! Bi Chawila … Bi. Chawila, jirani, amka, jamani! Unanisikia Bi. Chawila? Tafadhali niambie! (Kimya kidogo, halafu sauti za watu wakiongea na kunong’onezana chini kwa chini kuhusu kilichosababisha Bi Chawila kudondoka kutoka juu ya stuli. Sauti zinaendelea chini ya
Bi. Bwalya:
Hakikisheni anapata hewa nyingi ili apatefahamu haraka.

Nancy:
tafadhali fanya haraka ulete teksi tumpeleke kliniki mara moja. Inachukua muda kuleta teksi katika sehemu hii ya mtaa huu wa vibanda

Sauti za miguu ya Nancy zinafifia kwenye mic. Kimya kwa sekunde mbili. Sauti ya gari ikikaribia na kisha kusimama.

Bi. Bwalya:
(Kwa sauti ya chini) Haya Nancy, na tumwinue shangazi yako tumuweke ndani ya teksi. Lazima tumpeleke kwenye kliniki sasa hivi! Hali yake inaonekana kuwa baya sana.

Sauti za Nancy na Bi. Bwalya wakijaribu kumuweka Bi. Chawila ndani ya teksi, kisha mlango wa gari ukifungwa. Kimya, kisha sauti ya gari likiondoka, fifiisha kisha uihimili. Sauti ya gari likisimama katika chumba cha dharura, na mlango kufunguliwa. Sauti za wauguzi na daktari wakija kwa haraka ili kumchukua Bi. Chawila kwa machela.

Daktari Kamanga:
Alifanya nini?

Nancy:
(Akieleza kwa hofu na woga) Mimi sijui, daktari. Alikuwa akisafisha dirisha nje ya nyumba, halafu nikasikia akipiga mayowe na kuanguka chini kutoka kwenye stuli. Nilipofika pale nje, niliona kuwa amezirai na hangeweza kuzungumza name.

Daktari Kamanga:
Wewe unaitwaje na una uhusiano gani na mama huyu? Anaitwa nani?

Nancy:
Jina langu ni Nancy na mimi ni mpwa wake. Jina lake ni Bi. Mirriam Chawila.

Daktari Kamanga:
Mimba yake ni ya miezi mingapi? Amekuwa mgonjwa? Una habari kama amekuwa akiumwa na kichwa, homa au kizunguzungu?

Nancy:
Sina uhakika, lakini nafikiri mimba ni ya kama miezi saba hivi. Kwa ujumla, amekuwa na hali baya katika ujauzito huu. Ama kwa kweli, tunafikiri kuna mtu aliyemtupia jicho baya kwa vile amekuwa akipatwa na maumivu makali ya kichwa ya ghafla na pia kizunguzungu.

Daktari Kamanga:
Sawa, asante Nancy. Naomba mtoke msubiri hapo nje. Tutaona tutakavyosaidia.

Fifiisha sauit, kisha upaandishe sauti za chumba cha matibabu ya dharura, sauti za vyombo vya matibabu vikiwekelewa mezani, watu wakiongea kwa sauti za chini na kadhalika. Simamisha kidogo chini ya onyesho hili.

Msimulizi:
Nancy anatoka kwenye chumba cha matibabu ambamo daktari na muuguzi wanamshughulikia Bi. Chawila. Daktari anampa vitu maji maji kupitia mishipa yaani IV, na kisha madawa ya kunusa ili arejeshe fahamu, huku naye muuguzi akipima malaria na kuangalia hali ya mtoto tumboni na kugundua kuwa mtoto yuatoka.

Daktari Kamanga:
Muuguzi, mama huyu ana malaria +++ na ukosefu mbaya wa damu. Yuko katika hali ya kujifungua sasa.(Ujumbe wa mhariri. Nchini Zambia, wafanyikazi wa kiafya hutumia maelezo “ malaria +++” kuelezea malaria iliyokithiri).Tunapaswa kumsaidia kujifungua.

Mwuguzi:
Naam daktari, nakubaliana nawe. Mpigo wa moyo wa mtoto tumboni pia unasikika kuwa hafifu. Angalia, nafikiri anarejeresha fahamu sasa. Bi Chawila, unanisikia?

Daktari Kamanga:
(Akikatisha) Ona, ana fahamu zake sasa, lakini hata usifikirie upasuaji wa ‘caesarean’! Hebu tuone.(kimya kidogo anapomkagua)…Sawa, nafikiri anaweza kustahimili uchungu wa uzazi na pia kusukuma mtoto. Tusiwe na pupa kumtuma kwa mpasuaji. Tunaweza kumpoteza yeye au mtoto au hata wote wawili hasa kama yuko na upungufu wa damu. Bi. Chawila… Bi. Chawila, unanisikia?

Bi. Chawila:
Eeeesh! Eeeesh! Ndio, nakusikia. Lakini wewe ni nani? Niko wapi?

Daktari Kamanga:
Mimi ni daktari Kamanga, na uko katika kliniki ya dharura. Umepoteza fahamu kwa kuwa una maradhi ya malaria yaliyokithiri, na ambayo imekuletea ukosefu wa damu unaojulikana na baadhi ya watu kama ‘damu hafifu’

Sikiza, hakuna muda wa kujibu maswali zaidi kwa sasa. Uko katika hali ya kujifungua na mtoto yuko njiani. Nataka ufuate maagizo yangu kwa makini… Nikisema sukuma, unasukuma, sawa?

Bi. Chawila:
Sawa.

Daktari Kamanga:
Sawa sasa! Sukuma! Tena! Sawa ng…ngoja..ngoja…ngoja! Sawa, sasa utasukuma mara nyingine moja kwa nguvu na tutamaliza mara moja. Sukuuuma! Daa (Kimya)Ndiyo huyo hapo mtoto, ni msichana. Lakini kwa vile mtoto hakulia wala kupiga kelele yo yote, itabidi tumfanyie majaribio ya malaria pia. Muuguzi. Fanya majaribio hayo na kisha umweke mtoto kwenye oksinjeni mara moja. Pia unganisha mpira kwa ajiri ya chakula cha mtoto. Naja sasa hivi.

Mwuguzi:
Sawa daktari, mtoto atakuwa kwenye kitanda nambari 37.

Fifiisha sauti za kliniki. Sekunde mbili za kimya, kasha upaaze taratibu sauti za kliniki. Sauti za nyayo za daktari akikaribia

Daktari Kamanga:
Bi Chawila, itabidi ulazwe hapa katika kliniki kwa muda kwa kuwa mtoto wako ana malaria pia. Itabidi tuwape matibabu nyote wawili hadi pale tutakapokuwa na uhakika kuwa mko wazima. Hapo ndipo tutawaachilia wewe na mtoto mwende nyumbani.

Bi. Chawila:
Sawa, naweza kumuona mtoto sasa?

Daktari Kamanga:
Hata! Unahitaji kupumzika ili uwezeshe damu na sukari zilizo kwenye mipira kuisha. Hapo ndipo utaweza kutembea. Utajisikia nafuu sana, na mwenye nguvu. Wauguzi watashughulikia mtoto, usitie shaka.

Kimya, kisha ufifiishe sauti za watu wakitembea na kuzungumza katika kliniki.

Msimulizi:
Imekuwa majuma mawili tangu Bi. Chawila alipokuja kwenye kliniki. Leo anaachiliwa kwenda nyumbani pamoja na mtoto wake msichana. Wote wawili ni wazima. Nancy amefika kumsaidia mizigo yake. Anaona kuwa shangaziye anaingia kwa daktari na hivyo anamsubiri nje. Daktari anamweleza Bi. Chawila kuwa imebidi ampe ushauri kuhusu jinsi ya kujikinga na kutibu malaria katika ujauzito kwa ajili ya usalama wake na wa mtoto ambaye hajazaliwa. Hebu tusikilize kwa maakini daktari anapoongea na Bi. Chawila ofisini mwake.

Daktari Kamanga:
Bi. Chawila, kulingana na kadi yako ya kliniki kabla ya kujifungua, naona kuwa ulitembelea kliniki hiyo mara tatu. Kuna wakati ulipatiwa madawa ya kuzuia malaria au kushauriwa ulale chini ya neti iliyotibiwa?

Bi. Chawila:
Ndiyo daktari, nilipewa madawa yale, lakini ni lazima nikiri kuwa sikuyatumia…(Kimya)

Daktari Kamanga:
Naam, endelea.

Bi. Chawila:
Nyanyangu daima aliniambia kuwa mwanamke akiwa mjamzito, hapaswi kamwe kutumia madawa ya Kizungu kwa kuwa yanaweza kusababisha mimba kutoka au kuleta madhara kwa mtoto tumboni. Kuna jirani yangu ambaye amejifungua mtoto aliye na kasoro, jambo lililonitia wasiwasi. Kwa hivyo niliyatupa madawa yale.

Daktari Kamanga:
Na neti za kuzuia mbu je? Umekuwa ukitumia neti iliyotibiwa?

Bi. Chawila:
Sijawahi kulala chini ya neti ya kuzuia mbu kwa kuwa kuna rafiki yangu aliyenieleza kuwa dawa inayotumiwa kutibu neti husabababisha mizio
.

Daktari Kamanga:
Naona. Je ulijisikia mgonjwa wakati wa ujauzito? Mpwao alitaja kuwa ulikuwa na maumivu makali ya kichwa na kizungunguzungu.

Bi. Chawila:
Ndiyo, wakati nilikuwa mjamzito kwa muda wa miezi sita, nilianza kupata maumivu hayo makali ya kichwa, homa kali, na nikapoteza hamu ya chakula. Hali hii ilikuwa ikinijia jioni jioni, kwa hivyo nikaipuuza. Nilifikiria kuwa ni hali ya ujauzito tu. Lakini kadri siku zilivyoendelea, ilikuwa wazi kwangu kuwa haukuwa ugonjwa wa ujauzito pekee, hatimaye, nilikuwa nyumbani kwangu nikisafisha madirisha, na punde si punde, nikaona kizunguzungu. Ninachokumbuka tangu hapo ni kuwa nilianguka.

Daktari Kamanga:
Bi. Chawila, kwanza nataka ujue kuwa malaria ndiyo muuaji nambari moja nchini Zambia, na hata kote barani Afrika. Watu walio na uwezekano mkubwa zaidi wa kuugua malaria ni wanawake wajawazito, watoto wa umri wa chini ya miaka mitano, na watu wanoishi na virusi vya ukimwi au wenye ukimwi. Ama kwa kweli, malaria ni hatari kuliko ukimwi. Malaria huweza kuua kwa muda wa masaa au siku chache. Ukimwi huchukua miezi au miaka kujitokeza au kuua mtu.

Bi. Chawila:
Kwa hivyo ugonjwa wa malaria ndio umenipelekea kujifungua mtoto kabla ya wakati uliofaa? Au kuna matatizo mengine ninayopaswa kujua?

Daktari Kamanga:
La hasha, hamkuwa na matatizo mengine. Malaria ndiyo umekupelekea kujifungua katika mwezi wa saba badala ya ule wa tisa. Unajua, wakati mbu jike anakuuma ukiwa mjamzito, anakuletea viini vya malaria. Viini hivi ndivyo vinasababisha malaria. Viini hivi huenda mara moja hadi kwenye chungu cha uzazi ambapo huzaana kwa kasi kuliko vikiwa ndani ya mwili wa mtu ambaye hana mimba. Chungu cha uzazi ni mahala pazuri sana kwa viini vya malaria kuzaana. Kwa hivyo, mtoto aliye mle anaambukizwa. Virusi huendelea kuzaana mtoto akiwa mchanga na huku akiwa hana nguvu za kutosha kustahimili maambukizi. Mwanamke mjamzito akiwa na malaria pia yuko katika hatari ya kujifungua mapema, hii ikiwa na maana kuwa unaweza kujifungua katika mwezi wa saba badala ya ule wa tisa. Mtoto anayezaliwa katika mwezi wa saba akiwa na malaria huweza kuwa mnyonge na mwenye mwili mdogo sana. Wengi hawaponi kwa kuwa hawana nguvu za kupigana na maambukizi.

Bi.Chawila:
(Akimkatiza daktari)Hivyo ndivyo mbu jike anaweza kuwa hatari. (Kwa mshangao) Mungu wangu! Lakini niulize, tunawezaje kutambua mbu kuwa jike au dume?

Daktari Kamanga:
Ni mbu jike anayeleta matatizo haya yote. Lakini kwa vile hatuwezi kwa macho yetu pekee kutambua aliye jike au dume, lazima tujikinge kutokana na aina yo yote ya mbu kwa kutumia mbinu ambazo nitazungumzia sasa hivi. Kama nilivyokuwa nasema, dalili za kwanza za malaria ni kuhisi homa, maumivu ya kichwa, na dalili nyinginezo. Katika hali hii, ‘wanajeshi’ walio mwilini mwako – na kwa hii nina maana chembechembe za damu zinazopigana na maambukizi – huwa wamevamiwa. Viini huanza kuwapiga na kuwaua, hivyo kuacha mtoto kuwa katika hali mbaya ya unyonge. Endapo wanawake wajawazito wenye malaria hawatatibiwa, ugonjwa huu huweza kusababisha kutoka mimba, kujifungua mapema, na ukosefu wa damu. Hapa nchini Zambia, tumechagua mikakati miwili ya kuzuia malaria katika ujauzito na hivyo kulinda maisha ya mtoto tumboni. Wa kwanza ni kutumia neti zilizotibiwa. Pili ni kuhakikisha wanawake wajawazito wanatumia madawa ya malaria. Kwa kawaida, madawa haya hugawa kupitia kliniki za kabla ya kujifungua.

Bi. Chawila:
Daktari, mambo hayo ni mengi sana kwangu. Huenda nisikumbuke maelezo haya yote, ingawa najua ni mambo muhimu sana. Ningependa wanawake kijijini mwangu waelewe mambo haya.

DaktariKamanga:
Sawa! Lakini tafadhali sikiliza hapa – ni muhimu sana endapo utakuwa mjamzito tena. Kliniki za kabla ya kujifungua ni muhimu sana. Kila nipatapo nafasi ya kuzungumza na akina mama katika kliniki, mimi huwasinikisha kuendelea kutembelea vituo vya afya vilivyo karibu nao wanapokuwa wajawazito. Hii si kwa ajili tu ya kumwona mkunga. Hii inahusiana na afya ya jumla kwa mama na mtoto anayekuwa tumboni. Unapokosa kuhudhuria kliniki hizi, unayaweka maisha yako na ya mtoto katika hatari kubwa kwa kuwa unaweza kukosa kugundua dalili za awali za malaria. Aidha, unaweza kupuuza dalili za maambukizi. Kama ulivyofanya Bi. Chawila.
.

Bi. Chawila:
Lakini nikuulize daktari, madawa ya malaria hayawezi kumfanya mtoto wangu azaliwe na kilema?

Daktari Kamanga:
Naelewa. Una wasiwasi kuwa dawa ya malaria inaweza kuwa na madhara kwa mtoto aliye tumboni. Madawa yanayozuia malaria wakati wa ujauzito ndiyo yale yale tunayowapa watu ambao hawana mimba. Tunapeana madawa hayo wakati tu ni salama kwa mama na mtoto – hivyo ni kusema baada miezi 16 ya ujauzito. Huu ndio wakati viungo vya mwili wa mtoto tayari vimekomaa, na hakuna hatari yo yote kwa mtoto. Kwa wingi, madawa ya kuzuia malaria hutolewa mara tatu kwa mama wakati wote wa ujauzito.

Bi. Chawila:
Naona daktari. Kwa hivyo unasema kuwa wanawake wasianze kutumia madawa ya malaria mara tu wagunduapo kuwa ni wajawazito?

Daktari Kamanga:
Hapana. Kama nilivyosema, tunaepuka kuwapa wajawazito dawa hii wakati viungo vya mtoto vinajitunga tumboni au katika muda wa mienzi mitatu ya mwanzo wa ujauzito. Katika kipindi hiki, tunawashauri wanawake kulala chini ya neti iliyotibiwa na kuhakikisha mazingira ya karibu yamesafishwa na kupuliziwa dawa. Dawa inayotumiwa kutibu neti za kuzuia mbu haina madhara kwa mama na mtoto aliye tumboni. Neti iliyotibiwa hugharimu takriban Kwacha za Zambia 3000 (Maelezo ya mhariri: chini ya dola moja ya Kimarekani), na huwaweka mama na mtoto aliye tumboni salama kutokana na malaria.

Bi. Chawila:
(Akitabasamu kwa kutosheka na kwa shukrani) Daktari, asante sana kwa habari hii. Sikujua haya yote. Haya mambo yana uzito sana na yapaswa kujulikana na watu wengine. Wanawake wengi katika jamii hii hawajui mambo haya. Nafikiri napaswa kuandaa mkutano na wanawake wenzangu niwaambie yaliyonipata. Unaonaje daktari?

Daktari Kamanga:
Naam! Hilo ni wazo la busara. Bi.Chawila. Napendekeza ualike wale wanawake ambao hukataa kwenda hospitali na kliniki wakati wa ujauzito.

Sauti za mlango ukibishwa

Daktari Kamanga:
Ingia.

Mwuguzi:
Daktari! Kuna mama ambaye ameingia katika chumba cha dharura na inaonekana kama anajifungua. Tafadhali njoo haraka.

Daktari Kamanga:
Naja, mwuguzi! Bi. Chawila, ikiwa una maswali zaidi kuhusu malaria au jinsi ya kujitunza, tafadhali zungumza na mwuguzi huyu. Anaweza kueleza kila kitu vizuri kama mimi tu.

Bi. Chawila:
Ndio daktari. Nitafanya hivyo. Lakini daktari, ngoja! Unaweza kufika mkutanoni ili unisaidie kujibu maswali yatakayonishinda katika mkutano wa wanawake?

Daktari Kamanga:
Bila shaka Bi. Chawila. Nitakuwa rai kufanya hivyo, na hata wafanyi kazi wenzangu wote. Tunachukua malaria kwa uzito mwingi hasa inapowahusu wanawake wajawazito. Naomba urejee na uniambie siku na saa za mkutano huo wa jamii, na mmoja wetu akuwa tayari kukusaidia.
.
Msimulizi:
Daktari anatoka chumba cha ushauri kwa haraka. Bi. Chawila anamwita Nancy ili ambembee mikoba waende nyumbani. Kabla hawajaondoka, Bi. Chawila anamwomba mpwae Nancy amsaidie.

Bi. Chawila:
Nancy, Nancy! Nitambeba mtoto. Twende zetu nyumbani. Utanisaidia kuandikia mwenyekiti wa chama cha wanawake barua? Ningependa kuandaa mkutano na wanawake ili niwaeleze hatari za malaria.

Nancy:
(Akimkatiza) Hatari za nini? Shangazi! … Unapaswa kuwa nyumbani ukimwangalia huyu mtoto mchanga na kupumzika. Unajua uliyoyapitia wakati wa ugonjwa huu. Hata hujui adui yako ni nani. Ni aina gani ya ambukizo la malaria, ehh?

Bi. Chawila:
Unataka kusema nini, Nancy? Kwamba nimeumwa kwa sababu ya uchawi? Hapana mpwa wangu. Nimekuja kuelewa kwamba ilikuwa malaria. Ninahitajika kuwaeleza wanawake vile ugonjwa malaria ulivyo hatari, na vile wanaweza kukingwa kwa kutumia neti zilizotibiwa na madawa ya kukinga malaria. Na jinsi ya kuutibu wapougua.

Nancy:
Shangazi, ni kama vile umetoka shuleni wala si kliniki. Utawezaje kumudu kuandaa mkutano na pia kuongea mbele ya umati wa watu?

Bi. Chawila:
(Kwa utulivu)Ndio maana nakuomba unisaidie kuandika barua kwa mwenyekiti wa kundi letu kuwaalika wanawake wote wasikose kuhudhuria. Daktari Kamanga amesema kuwa atakuja kusaidia kujibu maswali nikilemewa. Lakini nafikiri kuwa kisa cha tuliyoyapata mimi na mwanangu kwa sababu ya malaria kitatosha kabisa kukinga ugonjwa huu hatari katika jamii yetu.(Kimya)Haya, na tuondoke. Muda umeyoyoma.

Acknowledgements

  • Yamechangiwa na: Senior Writer Alice Lungu Banda
  • Yamehaririwa na: Ellen Brazier, Senior Technical Advisor, Community Engagement, EngenderHealth

Information sources

  • National Malaria Control Centre (Zambia): http://www.nmcc.org.zm/
  • Mahojiano na:Daktari Elizabeth Chizema. National Malaria Control Center. Deputy Director in the Directorate of Health and Research-Malaria, July 3, 2009.
  • Daktari Ameck Kamanga, a gynecologist and programme manager with Marie Stopes
    International Zambia, May 25, 2009 and March 10, 2010.
  • Mheshimiwa Kapembwa Simbao, Minister Of Health for the Republic of Zambia.
    Bi. Mirriam Chawila, March 9, 2010.
Canadian Flag Kipindi hiki kimekufikia kwa ufadhili wa serikali ya Canada kupitia Shirika lake la misaada la CIDA