Wakulima huko Niger wananufaika kwa kuacha miti kukua katika mashamba yao

Ujumbe kwa mtangazaji

Save and edit this resource as a Word document

Vidokezo kwa watangazaji

Katika miaka ya 1970s na 80s, mengi yalikuwa yameandikwa kuhusu shida ya nishati katika nchi za Saheli na katika sehemu zingine kame na zenye ukame. Kulikuwa na pengo kubwa kati ya mahitaji ya nishati pamoja na idadi ya watu – mahitaji ya kuni – na uwezo wa miti na vichaka kukidhi hitaji hilo. Kwa wakati huu, Saheli ilikuwa imekumbwa na miaka mfululizo ya ukame. Ardhi ya kilimo iliongezeka zaidi na zaidi katika maeneo ya pembezoni, ambayo mimea yake iliharibiwa.

Ilionekana kuwa mimea karibu na miji katika Sahel ilikuwa inaenda kuharibiwa kabisa kwa sababu ya kuongezeka haraka kwa mahitaji ya kuni miongoni mwa watu.

Hivi sasa, inadhaniwa kuwa mimea katika Sahel inapungua kutokana na matumizi ya binadamu kupita kiasi. Wakati hili linatokea dhahiri katika baadhi ya maeneo ya Sahel, kuna maeneo mengi ambayo yanakabiliwa na ongezeko la mimea ya miti. Kwa mfano, nchini Niger, ongezeko la mimea ya miti ni katika mikoa ya Tahoua, Maradi na Zinder. Katika mkoa wa Tahoua, upandaji miti umeandaliwa na miradi inayolenga kukarabati ardhi tasa, wakulima pia walianza kulinda miti na vichaka ambavyo ni vya asili. Wakati huo huo, wafugaji wanalinda mimea ya asili kama miti aina ya Acacia raddiana. Katika mkoa wa Maradi, taasisi zisizo za serikali (NGOs), zilisaidia wakulima kulinda na kusimamia miti na vichaka ambavyo viliota tena moja kwa moja katika mashamba yao. Utaratibu huu ulianza katikati ya miaka ya 1980s. Hivi karibuni, mradi katika wilaya ya Aguié unaunga mkono uundaji wa mashirika ya vijijini kulinda, kusimamia na kutumia miti ya mashambani. Katika mkoa wa Zinder, mkulima mkubwa alifanikisha uoto mpya wa asili.

Maandishi haya yanajadili Kisiki Hai (Farmer Managed Natural Regeneration – FMNR).  Kisiki Hai ni shughuli inayofanywa na wakulima ambayo inajumuisha kulinda na kudhibiti ukuaji tena wa miti na vichaka kwenye mashamba. Kisiki Hai inafaidisha wakulima kwa kurudisha mimea ya miti. Wakulima karibu kila wakati hulenga kurudisha miti na vichaka vyenye thamani ya kiuchumi.

Inashangaza kujua kwamba Kisiki Hai katika mashamba ya mazao umepokea umakini mdogo. Watoa maamuzi wachache wa kitaifa na kimataifa wanafahamu kuhusu hili, na kuna machapisho machache tu kuhusiana na mada hii. Lakini utafiti mmoja unasema kwamba, Kisiki Hai, imekuwa na athari chanya kwa angalau hekta milioni tano za ardhi iliyolimwa huko Niger. Ikiwa hii ni sahihi, ni ya kipekee katika Saheli na pengine barani Afrika kwa ujumla.

Maandishi haya ni mahojiano halisi. Unaweza kutumia maandishi haya kama msukumo wa kutafiti na kuandika maandishi kwenye mada kama hii katika eneo lako. Au unaweza kuchagua kuzalisha hati/maandishi haya kwenye kituo chako, ukitumia waigizaji wa sauti kuwakilisha waongeaji walioko katika maandishi haya. Ikiwa ni hivyo, tafadhali hakikisha unawaambia wasikilizaji wako mwanzoni mwa kipindi kwamba sauti ni za waigizaji na sio za watu wa kwanza waliohusika katika mahojiano.

Script

Mwenyeji:
Karibu, wasikilizaji. Leo tutazungumza juu ya shughuli ya kilimo inayoitwa Kisiki Hai (Farmer Managed Natural Regeneration) au FMNR, ambayo hufanywa na wakulima wengi kusini mwa Niger. Katika FMNR, wakulima wanalinda na kusimamia kikamilifu aina ya miti katika mashamba yao ili kurudisha mimea kwenye eneo lenye ukame na kuboresha mazao yao na mapato yao. Aina ya mimea wanayotumia kila wakati ni ile yenye thamani ya kiuchumi – kwa maneno mengine, ni ile aina ya mimea inayozalisha matunda au kuni za moto na bidhaa zingine. Shughuli hii ya kilimo inaitwa Kisiki Hai ili kuitofautisha na upandaji wa miti na usimamizi wa miti ya asili. Kipindi hichi kinazungumzia juu ya sababu ambazo wakulima katika mkoa wa Maradi kusini mwa Niger walianza kulinda uoto wa asili wa miti na vichaka katika mashamba yao, jinsi wanavyosimamia miti hii na vichaka, na athari za Kisiki Hai kwenye maisha yao ya kila siku.

Kisiki Hai katika mkoa wa Maradi kusini mwa Niger ilianza na kazi iliyofanywa na NGO inayoitwa Serving-In-Mission au SIM miaka ya 1980 kupitia Mradi wa Maendeleo wa Maradi (Maradi Development project). Kufuatia hayo, kulikuwa na mradi uliofadhiliwa na IFAD katika wilaya ya Aguié ambao ulijikita zaidi katika Kisiki Hai. Mnamo mwaka 1999, 88% ya watu waliohojiwa katika vijiji vya mradi na katika vijiji vilivyokuwa nje ya mradi walikuwa wanatekeleza mpango wa Kisiki Hai kwa kiwango fulani katika mashamba yao. Matokeo yalikuwa kwamba miti takribani milioni moja na robo iliongezwa kwenye ukanda wa mradi kila mwaka.

Ninahojia na na Bwana Ali Micko, ambaye amehusika na mradi huo katika wilaya ya Aguié mkoa wa Maradi.

Habari, Bwana Micko. Jina langu ni Lawali Mamane Nassourou kutoka taasisi isiyo ya serikali (NGO) inayoitwa Le Micro Vert. Mahojiano yetu leo yatajikita katika programu ya Kisiki Hai. Unaweza kuanza kwa kujitambulisha?

Ali:
Jina langu ni Ali Micko, mimi ni mkulima na Raisi wa kikundi cha wanakijiji huko Dan Saga.

Mwenyeji:
Ulianza lini kuona kuzorota kwa mimea kwenye mashamba yako?

Ali:
Mimea ilianza kupungua miaka ya 1960s, na ilifikia kilele chake katika miaka ya 1970s. Kupungua huku kulisababishwa sana na kuharibu miti yote na kwa kuacha tabia ya kupumzisha mashamba ili yapate rutuba.

Mwenyeji:
Ni nini kilichosababisha ubadilishe mazoea yako ya kilimo?

Ali:
Hali imekuwa ya changamoto kwa wakulima wote. Ardhi ilikuwa hailimiki, mchanga ulifunika mazao yetu, na kuni au miti yenye matumizi mengi ilikuwa ni nadra. Tulibadilisha mazoea yetu ya kilimo kwa kuacha miti michanga mashambani. Mawazo haya yaliungwa mkono na mradi ulioratibiwa na CARE International.

Mwenyeji:
Ulibadilishaje aina yako au mazoea yako ya kilimo?

Ali:
Kwa wakati fulani, kila mtu alitambua umuhimu wa kuacha miti midogo au sampuli katika mashamba. Wakulima walianza kutumia njia za kusafisha mashamba zilizoboreshwa kwa kusaidiwa na mradi. Pia tunatunza mimea midogo inayochipua na kukua katika mizizi ya miti mikubwa. Tofauti na hili, tumetengeneza kitalu chenye aina ya miti ya asili kama vile Hyphaene thebaica, Acacia albida, na Parkia biglobosa (Taarifa ya Mhariri: Angalia majina ya kawaida mwishoni mwa maandishi haya). Tulianza pia kutumia takataka za miti– majani yaliyokauka, magome na matawi ambayo yameanguka ardhini – kama matandazo.

Mwenyeji:
Lini uliona kuwa jitihada hizi zina athari chanya kwa mimea katika mashamba yako?

Ali:
Jitihada zetu ni za kipindi cha miaka 25 nyuma lakini zilifatishwa kwa kiwango kikubwa takribani miaka 18 iliyopita.

Mwenyeji:
Athari gani zimekuwepo katika mazao yako?

Ali:
Katika kipindi ambacho mimea ilikuwa imeharibiwa kabisa, mavuno ya Mtama kwa ekari moja ilikuwa ni kilo 90-120 tu au takribani mafungu 13-17. Lakini sasa kutokana na kuongezeka kwa mimea, tunaweza kupata kilo 315 mpaka 455 kwa ekari. Kama tukitumia mbolea ya madini, mavuno yanaweza kufikia kilo 700 kwa ekari.

Mwenyeji:
Ni kwa namna gani mpango wa Kisiki Hai umeathiri kipato chako?

Ali:
Kwa sasa kilimo kina faida. Miti inatoa chakula kwa wanyama, kuni kwa ajili ya kuuza, na kwa ajili ya ujenzi. Wakati wa kipindi cha upungufu wa chakula kuanzia mwaka 1999-2000, kaya nyingi hapa ziliweza kuishi, shukrani kwa kuuza mazao yatokanayo na miti.

Mwenyeji:
Kumekuwa na athari gani kwa kazi ambazo zimefanywa na wanawake?

Ali:
Kutokana na kuongezeka kwa mimea, wanaume wanakata kuni katika mashamba yao na kubeba kupeleka nyumbani kwao kwa kutumia mikokoteni inayovutwa na wanyama ambayo wameinunua kutokana na kipato kinachotokana na kilimo, upandaji na usimamizi wa misitu na ufugaji wa wanyama. Kwa hiyo wanawake hawana kazi kubwa ya kutafuta, kukata na kubeba kuni. Pia, sehemu ya mapato kutokana na kuuza bidhaa zinazotokana na miti kinatumika kununua maji na kusaga nafaka. Hapo awali, wanawake wangelifanya kazi hii.

Mwenyeji:
Je! Unasimamiaje utajiri huu mpya?

Ali:
Tangu mwanzo wa njia hii mpya, tumekuwa na kamati ya usimamizi inayoundwa na wanaume na wanawake. Kamati hiyo inasimamia kuangalia juhudi zinazofanywa na wakulima na kutoa taarifa kwa wakuu wa vijiji pale ambapo watu wanakiuka sheria za jamii juu ya jinsi ya kutunza mashamba. Wakati miti ilipokua mirefu, tuliunda kamati ya usimamizi, ambayo ilileta vijiji vichache katika eneo la Dan Saga. Kwa msaada kutoka shirika la IFAD na huduma za mazingira za serikali, kamati ilifungua soko la kijiji la kuuza kuni lililosimamiwa na jamii. Mapato kutoka katika soko hili yamegawanywa katika hisa ambazo zimewekezwa katika Kisiki Hai, kwa jamii, huduma za mazingira za serikali na kamati. Soko hili linasaidiwa na uwepo wa kuni zinazonunuliwa kutoka kwa wanakijiji ambao huuza miti kwenye mashamba yao.

Mwenyeji:
Asante Ali kwa kufanya mahojiano haya, na kwa kutushirikisha uzoefu wako.

Ali:
Tunakushukuru kwa kuja hapa na kuonyesha nia katika njia yetu ya maisha.

Acknowledgements

Shukrani

Imechangiwa na: Sanoussi Mayana, Raisi wa de lONG RDD Le Micro Vert, mshirika wa utangazaji wa Farm Radio International.

Imehakikiwa na: Chris Reij, Kituo cha ushirikiano wa Kimataifa, Chuo kikuu cha VU, Amsterdam.

Majina ya kawaida ya aina ya miti yaliyotajwa kwenye maandishi

Acacia raddiana, pia unajulikana kama Acacia tortilis:

Kiingereza: umbrella thorn

Kiswahili: munga

Hyphaene thebaica:

Kiingereza: gingerbread tree. doum palm

Kiswahili: Mkoma

Acacia albida, pia unajulikana kama Faidherbia albida:

Kiingereza: winter thorn, apple ring thorn tree, apple ring acacia, ana tree, white thorn,

Kiswahili: mgunga, mkababu

Parkia biglobosa:

Kiingereza: African locust bean tree, nitta nut, monkey cutlass tree
Kiswahili: mkunde, mnienze

Information sources

Chanzo cha Habari

Mr. Ali Miko, raisi wa la grappe de Dan Saga, Idara ya Aguié, Mkoa wa Maradi, Jamhuri Niger.

 

Mpango uliotelekezwa kwa msaada wa kifedha kutoka serikali ya Canada uliotolewa kupitia Wakala wa Kimataifa wa Maendeleo wa Canada (CIDA)

 

 

Toleo la Kiswahili la jarida hili limeandaliwa kwa ufadhili wa Justdiggit kupitia mradi wake wa Kisiki Hai (Farmer Managed Natural Regeneration – FMNR) ulioko mjini Dodoma.