Utangulizi: Suluhisho za Asili zenye Kuzingatia Jinsia

Mazingira na Mabadiliko ya TabianchiUsafi na usafi wa mazingira

Backgrounder

Wanawake wa vijijini wanaoshiriki katika Suluhisho za Kiasili (NbS) barani Afrika wanaweza kupata manufaa mengi, kwa ngazi ya mtu binafsi na jamii. Suluhisho za Kiasili, kama zinavyofafanuliwa na Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Asili (IUCN), zinahusisha hatua zinazolenga kulinda, usimamizi endelevu, na urejeshaji wa ikolojia asilia na ikolojia iliyobadilishwa. Njia hizi zimeundwa ili kukabiliana na changamoto za jamii kwa ufanisi na kuhakikisha manufaa kwa ustawi wa binadamu na bioanuwai

Kuelewa NbS 

Suluhisho za Asili (NbS) husaidia watu binafsi na jamii kukabiliana na changamoto mbalimbali kama vile kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi*, usalama wa maji na chakula, kupunguza hatari za maafa na maendeleo ya kijamii na kiuchumi. NbS inachukua faida ya michakato ya asili na mifumo ikolojia kushughulikia changamoto hizi kwa ufanisi, kwa manufaa ya mazingira na wanadamu. Mifano ni pamoja na kurejesha ardhi oevu ili kuchuja vichafuzi vya maji, kupanda miti ili kupunguza mmomonyoko wa udongo na utoaji wa gesi chafuzi, na kutengeneza maeneo ya bustani ya miti katika maeneo ya miji ili kuimarisha ubora wa hewa na kupata maeneo ya burudani.

Umuhimu wa NbS unatokana na utendaji kazi wake mwingi*—hazitatui tu changamoto za jamii bali pia huchangia katika kuhifadhi bayoanuwai na kuimarisha huduma za mfumo ikolojia, * kupitia kutambua muunganiko wa mifumo ya binadamu na mifumo asilia

NbS zenye kuzingatia Jinsia ni nini?

Suluhisho za Asili zinazozingatia jinsia (NbS) sio tu kwamba zinatoa kipaumbele kwa uendelevu wa ikolojia na ustawi wa jamii, lakini pia hutetea usawa wa kijinsia. Zinatambua na kushughulikia mahitaji mbalimbali, changamoto, matarajio na mitazamo ya watu binafsi katika jinsia zote. Kwa kukuza ushirikishwaji mpana na uwakilishi, ikijumuisha sauti za wanawake, wanaume na vijana waliotengwa, NbS zinazozingatia jinsia zinahakikisha kuwa masuluhisho yanajumuisha na yana usawa, huku zikitumia hekima ya pamoja na uzoefu wa jamii mbalimbali.

Wanawake wa vijijini mara nyingi hushiriki majukumu makuu katika kusimamia maliasili na ni muhimu sana katika kuendeleza maisha na kuimarisha ustahimilivu wa jamii za vijijini duniani kote. Maarifa na uzoefu wao wa kipekee ni muhimu katika kuunda NbS bora, endelevu, na zinazozingatia jinsia.

Kimsingi, Suluhisho za asili (NbS) zinazozingatia jinsia hujitahidi kuhakikisha kwamba wanajamii wote, hasa wanawake na watu wa jinsia tofauti, wanashiriki kikamilifu na kufaidika na ubunifu, utekelezaji na tathmini ya masuluhisho haya. Mbinu hii inahitaji kutengeneza nafasi ambapo mitazamo tofauti ya kijinsia inasikika na kuheshimiwa, na ambapo masuluhisho yanaibuka kutokana na maarifa na uzoefu wa jamii.

Kwanini mada hii ni muhimu kwa wasikilizaji? 

Udhaifu kwa mabadiliko ya tabianchi*: Nchi nyingi za Afrika ziko katika mstari wa mbele wa mabadiliko ya hali ya hewa, zinakabiliwa na athari kali kama vile ukame, mafuriko, na mabadiliko ya mifumo ya mvua. NbS zinazozingatia jinsia zinatoa njia zinazoonekana za kukabiliana na mabadiliko haya huku zikihakikisha kwamba mikakati ya kukabiliana na hali hiyo ni sawa na kushughulikia mahitaji ya wanajamii wote, na hasa jinsia zote.

Kilimo na maisha: Katika Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara, sehemu kubwa ya wakazi wanategemea kilimo na maliasili kwa ajili ya maisha yao. Wanawake, haswa, wana jukumu muhimu katika sekta hizi, lakini mara nyingi hawana njia ya kupata rasilimali hizi, taarifa na kufanya maamuzi. Kujadili NbS zinazozingatia jinsia kwenye redio kunaweza kuangazia umuhimu wa kuwajumuisha wanawake katika mijadala na kufanya maamuzi kuhusu masuala endelevu, yanayopelekea jamii kuwa thabiti zaidi na kuwa na maisha bora kwa wote.

Uwezeshaji na usawa: Usawa wa kijinsia ni suala muhimu katika jamii nyingi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. NbS zinazoshughulikia jinsia sio tu zinashughulikia changamoto za kimazingira bali pia zinatoa njia za kuwawezesha wanawake na kukuza usawa kwa kutambua na kuthamini kwa usawa majukumu mahususi na ujuzi wa wanawake katika usimamizi wa mazingira na kukabiliana na hali ya hewa.

Elimu na ufahamu: Redio ni chombo chenye nguvu cha kutoa elimu na kuongeza ufahamu katika maeneo ya vijijini, ambapo ufikaji wa aina nyingine za vyombo vya habari unaweza kuwa mdogo. Kujadili NbS zinazozingatia jinsia kunaweza kuwafahamisha na kuwatia moyo wasikilizaji kuhusu masuluhisho ya kibunifu kwa changamoto za kimazingira ambayo ni ya usawa, yanayozingatia jinsia na yaliyo jumuishi. 

Ushirikishwaji wa jamii: Kushirikisha jamii katika midahalo kuhusu NbS zinazozingatia jinsia kupitia redio kunaweza kukuza hisia ya umiliki na ushiriki katika mipango ya kuhifadhi mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa. Inawahimiza wanajamii wote, wakiwemo wanawake, kubadilishana uzoefu, mawazo njia zao wanazotumia.

Taarifa muhimu kuhusu Suluhisho za Asili zinazojumuisha na zinazozingatia jinsia

Kwa kuhakikisha kwamba wanawake wanashiriki kikamilifu katika awamu mbalimbali za muundo na utekelezaji wa NbS—kutoka kutambua matatizo hadi kupanga mipango hadi utekelezaji na tathmini—miradi na michakato inakuwa jumuishi na yenye ufanisi zaidi. Sehemu zifuatazo zinaangalia jinsi kila hatua ya mradi inaweza kuimarishwa kupitia ushiriki wa kina wa wanawake na uongozi.

  1. Kutambua tatizo

Shirikisha makundi mbalimbali katika jamii, ikiwa ni pamoja na wanawake na makundi yaliyotengwa, tangu mwanzo ili kuhakikisha kwamba mitazamo yao ya kipekee, ufahamu, ujuzi, na uzoefu vinazingatiwa. Kwasababu mara nyingi wanawake ndio wasimamizi wakuu wa maliasili katika maeneo ya vijijini, wanaweza kutoa maarifa muhimu katika masuala ambayo yanaweza yasionekane wazi kwa wengine mara moja, kama vile masuala mahususi ya ubora wa maji au kupungua kwa spishi za mimea muhimu kwa ajili ya chakula cha kila siku cha familia au mahitaji ya matibabu.

  1. Kubuni/Kuunda

Wanawake wanaposhiriki kikamilifu katika kubuni shughuli za NbS, huongeza uwezekano kwamba matokeo yatashughulikia wigo mpana wa mahitaji na mitazamo ya jamii, ikijumuisha nyanja za kijamii, kiuchumi na kimazingira. Ushiriki wa wanawake huhakikisha kuwa masuluhisho yameandaliwa vyema na yananufaisha jamii nzima. Kwamfano, miradi inapohusisha kazi zinazohitaji kutumia nguvu kama vile kupanda miti au kujenga matuta, wanawake wanapaswa kushiriki katika kupanga ili kuhakikisha kwamba shughuli zilizopangwa zinakidhi uwezo na mapungufu ya kimwili ya wanaume na wanawake. Hii ni pamoja na kuzingatia ratiba zao za kila siku, majukumu, na mahitaji maalum, na kuhakikisha kuwa kuna zana na mbinu zinazofaa kwa washiriki wote.

  1. Utekelezaji

Shughuli na michakato ya NbS inaposonga kutoka kwenye hatua ya muundo hadi hatua ya utekelezaji, kudumisha usawa wa kijinsia katika majukumu ya uongozi na majukumu ya kazi kunaweza kusaidia kuhakikisha upatikanaji sawa wa manufaa, ikiwa ni pamoja na ajira, faida za kiuchumi, manufaa ya mazingira na bioanuwai, na uwezeshaji wa kijamii. Kudumisha usawa huu kunaweza kutoa changamoto kwa majukumu ya kijinsia ambayo yapo kitamaduni kwa kutoa mafunzo na rasilimali kwa wanawake katika maeneo ambayo kwa kawaida yanatawaliwa na wanaume, kama vile kazi za upandaji miti au uhandisi unaohusiana na shughuli za kuhifadhi maji.

  1. Ufuatiliaji na tathmini

Ili shughuli za NbS ziwe zinazozingatia jinsia, wanawake lazima watekeleze majukumu muhimu katika kufanya ufuatiliaji na tathmini. Hii inahusisha sio tu kufuatilia maendeleo dhidi ya malengo ya mazingira, lakini pia kuhakikisha kuwa miradi inaendelea kukidhi mahitaji ya kijamii. Wanawake wanaweza kutoa maoni sio tu kuhusu lengo la mazingira, lakini jinsi miradi inavyoathiri maisha ya kila siku, kupendekeza marekebisho, na kusaidia kupima matokeo yanayohusiana na usawa wa kijinsia na uwezeshaji.

  1. Tathmini ya mafanikio au kutokufanikiwa

Kufafanua mafanikio au kutokufanikiwa kutokana na mtazamo unaozingatia jinsia kunahusisha kuangalia mbali zaidi ya vipimo vya jadi au desturi kama vile idadi ya miti iliyopandwa au hekta za ardhi zilizorejeshwa rutuba. Inajumuisha pia kufuatilia uboreshaji katika viwango vya mapato ya wanawake, kupunguzwa kwa muda unaotumika katika kufanya kazi za matunzo zisizolipwa kutokana na usimamizi bora wa rasilimali, na kuongezeka kwa ushiriki wa wanawake katika michakato ya kufanya maamuzi katika ngazi za mitaa na nyinginezo.

Kutathmini mafanikio au kutokufanikiwa ni fursa ya kufafanua mafunzo tuliyojifunza, na kushirikisha yale tuliyojifunza wanajamii wengine au jamii za jirani. Ni muhimu kuwajumuisha wanawake kwenye fursa zozote za kushiriki, ili waweze kuzingatia kama watakubali au jinsi gani watapata suluhisho zinazofanana.

  1. Mrejesho na Kupitishwa na wanufaika

Shughuli na michakato ya NbS zinapaswa kuwa na mifumo ili kuhakikisha mrejesho na upitishaji endelevu, unaowawezesha kuzoea kikamilifu changamoto na fursa zinazojitokeza. Hatua hii inaweza kuhakikisha kwamba njia hizi zinadumishwa, na hata kuunganishwa katika mifumo ya sera za mitaa, kikanda na kitaifa na mipango ya utekelezaji. Mchango unaoendelea wa wanawake ni muhimu hapa, kwani unaweza kusababisha uboreshaji ili kuendana vyema na mahitaji yanayoendelea ya kila mtu katika jamii pamoja na mazingira.

  1. Kujenga uwezo na kutoa elimu

Kuwawezesha wanawake kupitia elimu na kujenga uwezo katika usimamizi wa mazingira, uongozi, na ujuzi wa kiufundi husaidia kuhakikisha kwamba ujuzi unabaki ndani ya jamii na kurithishwa kwa vizazi vijavyo. Hii ni muhimu katika kudumisha manufaa ya NbS kwa muda mrefu na kukuza ustahimilivu wa jamii.

Kwa muhtasari, kushirikisha wanawake wa vijijini katika NbS sio tu kwamba kunaboresha matokeo ya mradi lakini pia hukuza usawa wa kijinsia, huhakikisha kuwa suluhisho za kimazingira zinaendeleza haki ya kijamii na ustawi wa jamii. Mbinu hii ni muhimu katika kuhakikisha kuwa maendeleo endelevu yanawanufaisha wanajamii wote.

Utumiaji wa NbS zinazozingatia jinsia katika maeneo mbalimbali:

Kilimo mseto: Wakati wa kutekeleza kanuni za kilimo mseto, ni muhimu kuzingatia jinsi kazi mbalimbali zinavyozingatia swala la usawa wa jinsia. Kwa mfano, wanawake wanaweza kuhusika hasa katika kuvuna matunda na karanga, wakati wanaume wanaweza kujikita katika upasuaji wa mbao. NbS zinazozingatia jinsia zinaweza kutoa mafunzo na nyenzo zilizolengwa kwa wanawake ili kuongeza ujuzi na maarifa yao katika mikakati endelevu ya uvunaji na uuzaji, kuhakikisha shughuli zao zinakuwa na faida na endelevu kama shughuli za wanaume.

Upandaji miti: Suluhisho ya asili ya upandaji miti inayozingatia swala la jinsia itahakikisha kwamba spishi zilizochaguliwa kwa ajili ya kupanda zinaakisi mifumo ya matumizi na mapendekezo ya wanaume na wanawake. Kwa mfano, wanawake wanaweza kupendelea spishi zinazotoa matunda, njugu, au mimea ya dawa ambayo wao kawaida hutumia, wakati wanaume wanaweza kupendekeza miti ambayo inaweza kutumika kupasua mbao. Kuwashirikisha wanaume na wanawake katika kupanga na kufanya maamuzi hakutahakikisha tu kunakuwa na aina mbalimbali za mimea (kuimarisha bayoanuwai), lakini pia kutaongeza manufaa ya kiikolojia na kiuchumi kwa kila mtu katika jamii.

Urejeshaji wa misitu ya mikoko: Suluhisho ya asili ya urejeshaji wa miti ya mikoko inayozingatia swala la jinsia itajumuisha mashauriano na wanaume na wanawake kutoka jamii za maeneo husika wakati wa awamy ya kuunda mpango/mradi. Wanawake, ambao kwa kawaida wanaweza kukusanya magamba ya viumbe wa baharini kutoka kwenye mikoko, na wanaume, ambao kwa kawaida wanaweza kuvua samaki katika maeneo ya karibu ya bahari, wangekuwa na maarifa tofauti kuhusu afya ya mfumo wa ikolojia na jinsi urejesho wake ungeweza kuboresha maisha yao. Mchakato wa NbS unaozingatia jinsia utahakikisha kwamba mitazamo ya wanawake na wanaume inaunda malengo na mbinu za suluhisho, na kusababisha matokeo ambayo ni ya manufaa na ya usawa kwa jamii nzima. Wanawake na wanaume pia wanaweza kushirikishwa katika shughuli tofauti za ufuatiliaji na tathmini, kutokana na shughuli zao tofauti katika misitu ya mikoko.

Mifumo ya usimamizi wa maji: Katika maeneo mengi ya vijijini, wanawake wanawajibika hasa katika swala la ukusanyaji na usimamizi wa maji. NbS inayozingatia jinsia ambayo ililenga kurejesha maeneo ya maji au ardhi oevu ingehusisha wanawake katika hatua za kubuni au kuunda mpango ili kuhakikisha kwamba maeneo ya kupata maji yanapatikana kwa urahisi na kwamba ubora wa maji unakidhi mahitaji ya nyumbani. Pia itaelimisha wanaume na wanawake juu ya matumizi endelevu ya maji na kuwashirikisha katika usimamizi wa maji, kusaidia kuboresha ustahimilivu wa jumla wa jamii kwa changamoto zinazohusiana na maji.

Mifano ya suluhisho za Asili zenye Kuzingatia Jinsia

Upandaji miti huko Nepal

Tatizo lililotatuliwa: Ukataji miti na ukosefu wa ushiriki wa wanawake katika kufanya maamuzi.

Suluhisho lililotekelezwa: Nchini Nepal, mradi wa kijamii wa upandaji miti unaofadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Asili (IUCN) uliwashirikisha kikamilifu wanawake katika majukumu ya kufanya maamuzi. Hii ni pamoja na kuwapa mafunzo ya usimamizi wa kitalu cha miti na mbinu za upandaji miti.

Matokeo: Mpango huu sio tu uliboresha eneo la misitu bali pia uliwawezesha wanawake kwa kuwapa udhibiti wa rasilimali na maamuzi, na hivyo kushughulikia masuala yote mawili ya mazingira na usawa wa kijinsia.

Kwa habari zaidi kuhusu umuhimu wa ushiriki wa wanawake katika urejeshaji wa mandhari ya misitu, angalia makala kutoka Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Asili (IUCN): https://www.iucn.org/news/forests/202108/strategies-help-rural-women-protect-forests 

Usimamizi wa maji huko Jordan

Tatizo lililotatuliwa: Usambazaji usio sawa wa maji na ukosefu wa ushiriki wa wanawake katika usimamizi wa maji.

Suluhisho lililotekelezwa: Nchini Jordan, mradi uliofadhiliwa na shirika la wanawake la umoja wa mataifa (UN Women) ulizingatia hatua endelevu za usimamizi wa maji. Hii ni pamoja na kuunda vyama vya watumiaji maji ambapo wanawake walihimizwa kushiriki kama wanachama na viongozi.

Matokeo: Ushirikishwaji wa wanawake ulihakikisha kuwa taratibu za usambazaji maji zinazingatia mahitaji ya wanakaya wote, wakiwemo wanawake, kukuza usawa na uendelevu katika usimamizi wa maji. 

Kwa habari zaidi kuhusu mikakati ya kuwasaidia wanawake wa vijijini kulinda misitu na michango yao katika uhifadhi wa misitu, angalia andiko fupi la shirika la wanawake la umoja wa mataifa (UN Women):

https://wrd.unwomen.org/sites/default/files/2021-11/UNWomen-RuralWOmenJordan-Brief-WEB.pdf 

Mashujaa wa kike wa upandaji miti nchini Uganda 

Tatizo lililotatuliwa: Uharibifu wa ardhi, ukataji miti, na ukosefu wa usawa wa kijinsia katika usimamizi wa ardhi.

Suluhisho Lililitekelezwa: Mradi wa Uwezeshaji Wanawake katika Usimamizi Endelevu wa Ardhi (WESLAM) katika wilaya za Bugiri na Mayuge mashariki mwa Uganda unalenga kupunguza uharibifu wa ardhi na ukataji miti kupitia kilimo endelevu na upandaji miti upya. Ikifadhiliwa na Bahati Nasibu ya Postikodi ya Uswidi, WESLAM inashughulikia upotevu mkubwa wa misitu, ambao umesababisha uharibifu wa udongo na kuongezeka kwa umaskini, hasa unaoathiri wanawake.

Matokeo: Mradi unawajengea uwezo wanawake kwa kuwashirikisha katika vitendo endelevu kama vile ufugaji wa nyuki na kulima uyoga ambapo ni vyanzo mbadala vya mapato vinavyopunguza utegemezi wa shughuli zinazochangia ukataji miti. Kupitia mbinu shirikishi ya usimamizi wa misitu, wakulima wa maeneo hayo wanapata ufikiaji endelevu wa hifadhi za misitu, kuboresha maisha yao na mazingira.

Kwa taarifa zaidi kuhusu mradi wa WESLAM na athari zake, tembelea tovuti ya Vi Agroforestry:

 https://viagroforestry.org/projects/weslam/ 

Changamoto 

Wanawake wa vijijini wanakabiliwa na changamoto kadhaa za kipekee ambazo zinaweza kuwazuia kushiriki kikamilifu katika kubuni na utekelezaji wa Suluhisho za Asili. Vikwazo hivi mara nyingi hutokana na ukosefu wa usawa wa kijamii na kiuchumi, kitamaduni na kimuundo ambao huzuia ushiriki na manufaa yao. Kukabiliana na changamoto hizi ni muhimu ili kuhakikisha kuwa NbS zinazingatia jinsia na manufaa kwa jamii nzima. Hizi ni baadhi ya changamoto kuu zinazowakabili wanawake wa vijijini:

Upatikanaji mdogo wa rasilimali: Wanawake wa vijijini mara nyingi wanapata fursa duni zaidi kuliko wanaume kwenye rasilimali muhimu kama vile ardhi, maji, fedha na teknolojia. Hii inaweza kuzuia uwezo wao wa kushiriki na kufaidika na mipango ya NbS katika maeneo kama vile kilimo mseto au kilimo endelevu, ambacho mara nyingi kinahitaji umiliki wa ardhi na uwezo wa kuwekeza katika teknolojia mpya.

Kanuni za kitamaduni na kijamii: Katika jamii nyingi, majukumu ya kijinsia ya jadi yanazuia ushiriki wa wanawake katika michakato ya kufanya maamuzi katika kaya zao na ndani ya jumii zao, pamoja na kuwapa wanawake wajibu wa kazi zote za nyumbani. Majukumu haya yanaweza kuzuia wanawake kushiriki katika mikutano ya jamii, kuchangia katika michakato ya kupanga, au kuchukua majukumu ya uongozi katika NbS.

Ukosefu wa elimu na mafunzo: Wanawake wa vijijini mara nyingi wana fursa chache za elimu rasmi na mafunzo ya ufundi stadi. Hii inaweza kupunguza uelewa wao wa NbS, kupunguza uwezo wao wa kushiriki kwa ufanisi.

Vikwazo vya kiuchumi: Utegemezi wa kiuchumi huathiri wanawake kwa njia isiyo sawa, na hivyo kupunguza muda wanaoweza kujitolea kufanya shughuli za NbS. Kwa sababu wanawake kwa kawaida huwajibika kwa malezi ya watoto na kazi zote za nyumbani, mara nyingi huwategemea wenzi wao kwa usaidizi wa kifedha. Bila uhuru wa kifedha, inaweza kuwa changamoto kwa wanawake kushiriki katika miradi ya muda mrefu ambayo haitoi mapato ya haraka ya kiuchumi.

Uwakilishi na ushiriki usiotosheleza: Hata wakati wanawake wanashiriki katika mipango ya NbS, ushiriki wao mara nyingi ni mdogo, mara nyingi wanashiriki katika kutoa nguvu kazi badala ya kushiriki katika kupanga na katika uongozi. Uwakilishi huu mdogo katika upangaji, usimamizi, na ufanyaji maamuzi unamaanisha kuwa mahitaji na maarifa mahususi ya wanawake yanaweza yasionyeshwe ipasavyo katika miradi.

Ukosefu wa upatikanaji wa masoko: Wanawake katika maeneo ya vijijini mara nyingi wanakabiliwa na vikwazo vikubwa vya kupata na kunufaika na masoko. Hii inaweza kuwa kutokana na ukosefu wa usafiri, ukosefu wa taarifa za soko, au kwa sababu ya kanuni za kijamii zinazozuia harakati zao au shughuli za kiuchumi. Bila upatikanaji wa soko, ni vigumu kwa wanawake kuuza bidhaa kutoka kwenye shughuli za NbS au kupata nyenzo muhimu.

Ukosefu wa mitandao ya usaidizi: Mara nyingi wanawake hukosa mitandao ambayo inaweza kutoa usaidizi, ushauri na upatikanaji wa fursa katika miradi ya mazingira. Hii inaweza kuzuia maendeleo yao kama viongozi na wavumbuzi katika NbS. 

Ukosefu wa takwimu: Ukosefu wa takwimu zilizogawanywa kwa jinsia hufanya iwe vigumu kuelewa udhaifu na mahitaji maalum ya jamii. Hii inaweza kufanya iwe vigumu kufanya maamuzi katika kuunda NbS ambazo zinanufaisha kila mtu. 

Kuingiliana: Ni muhimu kutambua kwamba watu hupitia vikwazo mbalimbali vya usawa vinavyohusiana na jinsia, rangi, kabila, umri, uwezo, lugha, mwelekeo wa kijinsia, hali ya kijamii na kiuchumi na mambo mengine. Wale walio na ulemavu au wasio na makazi mara nyingi hawajumuishwi katika michakato ya kufanya maamuzi, na kwa hivyo wanawake wanaokumbwa na haya yote, pamoja na wale wanaotoka katika makabila madogo, wanaweza kuwa na uwezekano mdogo wa kushiriki katika michakato ya NbS.

Manufaa ya wanawake wa vijijini wanaojihusisha na NbS zinazozingatia jinsia barani Afrika 

Uzalishaji wa kipato: Suluhisho za Asili mara nyingi huhusisha kilimo endelevu, kilimo mseto, na shughuli nyinginezo za maisha ambazo ni rafiki kwa mazingira. Kwa kushiriki katika mipango hii, wanawake wa vijijini wanaweza kujipatia kipato wao na familia zao.

Usalama wa chakula: Mbinu za NbS kama vile kilimo endelevu au kilimo ikolojia zinaweza kuimarisha usalama wa chakula na lishe kwa kukuza mchanganyiko mbalimbali wa mazao ya chakula yanayostahimili hali ya hewa. Wanawake wa vijijini wana jukumu muhimu katika shughuli hizi, na hivyo kuchangia katika kuboresha uzalishaji wa chakula na lishe ya familia.

Uhifadhi wa mazingira: Wanawake wa vijijini mara nyingi ndio wasimamizi wa maliasili katika jamii zao. Kushiriki kwao kikamilifu katika Suluhisho za Asili kunaweza kusababisha uhifadhi na usimamizi bora wa maliasili, ikijumuisha udongo, maji, na bayoanuwai. 

Kupunguza na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi: Suluhisho za Asili mara nyingi hutengenezwa ili kuongeza uwezo wa kustahimili mabadiliko ya tabianchi. Kwa kutumia mbinu za kilimo zinazozingatia hali ya hewa na kusimamia rasilimali kwa njia endelevu, wanawake wa vijijini wanaweza kusaidia jamii zao kukabiliana vyema na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Ustawi wa jamii: Suluhisho za Asili kwa kawaida huwa na athari chanya kwa ustawi wa jamii kwa ujumla. Kwa mfano, upatikanaji wa maeneo ya kijani kibichi katika maeneo ya mijini, usimamizi endelevu wa maji, uhifadhi wa misitu, na uboreshaji wa hali ya hewa huchangia afya bora ya kimwili na kiakili. Kwa kuhusika katika mipango kama hii, wanawake wanaweza kuchangia kwa ujumla afya na ustawi wa jamii zao.

Uwezeshaji na usawa wa kijinsia: Katika jamii nyingi, wanawake wa vijijini kimila wanakabiliwa na vikwazo vya kupata rasilimali na michakato ya kufanya maamuzi. Kushiriki katika Suluhisho za Asili zinazozingatia jinsia kunaweza kuwawezesha wanawake kwa kutoa fursa za kukuza ujuzi, kuchukua majukumu ya uongozi, na kuhusika kikamilifu katika kufanya maamuzi ya jamii. 

Uhifadhi wa bioanuwai: Suluhisho za Asili zinasisitiza umuhimu wa bioanuwai. Kupitia ushiriki wao katika shughuli endelevu za kilimo na uhifadhi wa makazi ya viumbe, wanawake wanaweza kuchukua jukumu muhimu katika kuhifadhi bioanuwai.

Uhifadhi wa kitamaduni: Suluhisho za Asili zinatokana na maarifa ya kitamaduni na maarifa asilia. Kama walinzi wa maarifa ya kitamaduni, wanawake wa vijijini wanaweza kuchangia katika kuhifadhi na kukuza mila na tamaduni ambazo ni endelevu kiikolojia.

Uwiano wa kijamii: Kushiriki katika Suluhisho za Asili kunaweza kuimarisha uhusiano wa kijamii kadiri watu wanavyofanya kazi pamoja kufikia malengo yanayofanana. Kupitia ushirikiano na ushirikishwaji wa jamii, wanawake wa vijijini wanaweza kuchangia katika kujenga mshikamano wa kijamii na ustahimilivu.

Elimu na kujenga uwezo: Ushiriki katika Suluhisho za Asili mara nyingi huhitaji elimu na kujengewa uwezo. Kwa kupata maarifa na ujuzi katika utendaji endelevu, wanawake wa vijijini wanaweza kuwa mawakala wa mabadiliko katika jamii zao kwa kutoa taarifa muhimu kwa wengine katika jamii, na kwa vizazi vijavyo.

Wanawake kama mawakala wa kuleta mabadiliko

Kuwawezesha wanawake wa vijijini kisiasa na kiuchumi, kupitia ushiriki wao katika shughuli za NbS zinazozingatia jinsia na vinginevyo, kunaweza kusababisha mabadiliko ya kimapinduzi, kupunguza umaskini, kuimarisha usalama wa chakula, na kuimarisha ustahimilivu kwa mabadiliko ya tabianchi. Kulingana na Umoja wa Mataifa, imekadiriwa kuwa kuwapa wanawake katika maeneo ya vijijini fursa sawa ya rasilimali, elimu, na masoko kama wanaume kunaweza kusababisha kuongezeka kwa uzalishaji wa kilimo na kupunguza njaa kwa hadi watu milioni 150.

Kushirikisha wanawake wa vijijini katika Suluhisho za Asili katika Afrika kunaweza kuleta athari chanya na endelevu katika nyanja mbalimbali za maisha ya jamii, kuanzia maendeleo ya kiuchumi hadi uhifadhi wa mazingira na ustawi wa jamii.

Ufafanuzi: 

Kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi: Mchakato wa kuzoea mabadiliko halisi ya tabianchi au yanayotarajiwa na athari zake. Kwa binadamu, kukabiliana huku kujumuisha kufanya athari ziwe kiasi au kuepuka madhara, au kutumia fursa. Kwa mazingira, jitihada za binadamu zinaweza kusaidia kurekebisha na ustawi wa mfumo wa ikolojia licha ya athari za mabadiliko ya tabianchi zinazotarajiwa.

Kupunguza mabadiliko ya tabianchi: Hatua zinazochukuliwa kupunguza au kuzuia utoaji wa gesi chafuzi kwenye angahewa ili kupunguza kiwango cha mabadiliko ya tabianchi. Mikakati ya kupunguza inaweza kujumuisha matumizi ya nishati safi, kuongeza ufanisi wa nishati, na kulinda au kurejesha misitu ambayo inachukua kaboni dioksidi.

Huduma za mfumo ikolojia: Hizi ndizo faida ambazo wanadamu hupokea kutoka kwenye mifumo asilia. Hizi ni pamoja na upatikanaji wa huduma kama vile chakula, maji, na malighafi; kudhibiti huduma kama vile udhibiti wa mabaadiliko ya tabianchi, udhibiti wa mafuriko, na kusafisha maji; kusaidia huduma kama vile urutubishaji wa ardhi na uundaji wa udongo; na huduma za kitamaduni ambazo hutoa burudani, uzuri na manufaa ya kiimani.

Uwezo wa kufanya kazi nyingi: Inarejelea uwezo wa kitu kutumikia mara nyingi au kufanya kazi nyingi. Katika kilimo, mfano wa utendakazi mwingi ni shamba ambalo huzalisha chakula, huweza kutumika kutoa mafunzo kwa ziara za kielimu, na hutumika pia kama makazi ya wanyamapori. 

Udhaifu: Kiwango ambacho mfumo, jamii, au mtu binafsi anaweza kuathiriwa na kushindwa kukabiliana na athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi. Udhaifu unachochewa na mambo kama vile kukabiliwa na hatari, unyeti wa athari, na uwezo wa kuzoea au kukabili.

Acknowledgements

Imechangiwa na: Stephanie Coucopoulos, Mratibu wa rasilimali za Redio, Farm Radio International.

Imehaririwa na: Sareme Gebre, Mtaalamu wa suluhisho za Asili, Farm Radio International, na Michele Sona Koundouno, Mtaalamu wa maswala ya Jinsia, Farm Radio International.

Information sources

Angula, M. N. et al, 2021. Strengthening Gender Responsiveness of the Green Climate Fund Ecosystem-Based Adaptation Programme in Namibia. Sustainability, 13(18). https://doi.org/10.3390/su131810162

IUCN, 2021. Forest landscape restoration needs women. https://www.iucn.org/news/forests/202103/forest-landscape-restoration-needs-women

IUCN, 2021. Strategies to Help Rural Women Protect Forests. https://www.iucn.org/news/forests/202108/strategies-help-rural-women-protect-forests

IUCN, 2020. Global Standard for Nature-based Solutions: A user-friendly framework for the verification, design, and scaling up of NbS. (1st ed.). Downloadable at: https://portals.iucn.org/library/node/49070

United Nations, 2011. Women in rural areas have potential to be ‘a powerful force’ against hunger. Women could feed millions more people if given access to means of production – UN | UN News

Salcedo-La Viña, C., Trivedi, A., and Grace, K., 2023. Enabling Rural Women as Key Actors in Nature-Based Solutions. World Resources Institute Working Paper, June 2023. https://files.wri.org/d8/s3fs-public/2023-07/enabling-rural-women-key-actors-nature-based-solutions.pdf

UNEP-WCMC, 2020. Empowering Rural Women and Girls as a Solution to Environmental Sustainability and Food Security. https://www.unep-wcmc.org/en/news/empowering-rural-women-and-girls-as-a-solution-to-environmental-sustainability-and-food-security

United Nations Environment Programme, 2022. Nature-based Solutions: Opportunities and Challenges for Scaling Up. https://wedocs.unep.org/handle/20.500.11822/40783

UN Women, 2021. Rural women and climate change in Jordan. Available at: https://wrd.unwomen.org/sites/default/files/2021-11/UNWomen-RuralWOmenJordan-Brief-WEB.pdf

Vi Agroforestry, undated. WESLAM. https://viagroforestry.org/projects/weslam/