Ukatili Majumbani: Sababu na matokeo yake

Ujumbe kwa mtangazaji

Maelezo kwa Watangazaji

Kulingana na ripoti ya mwaka 2021 kuhusu ukatili wa kijinsia (GBV) nchini Mali, 38% ya kesi zinahusisha ukatili wa kijinsia. Asilimia 23 ilihusisha ubakaji. Ukatili huu karibu kila mara unafanywa dhidi ya wanawake, aidha walioko ndani au nnje ya ndoa.

Ukatili wa majumbani ni matokeo ya tabia, vitendo na mitazamo ya mmoja wa wapenzi au wapenzi wa zamani. Vitendo hivi vinakusudiwa kumdhibiti, kumlazimisha, au kumtawala mwenza. Ukatili wa majumbani ni aina ya ukatili wa kijinsia na unahusisha ukatili kwa njia ya matusi, kimwili, kingono na kiuchumi, vitisho au kulazimishwa. Pia huathiri wazazi na ndugu wa mwathiriwa na mhalifu hasa watoto.

Kwa mtazamo wa kisheria, ukatili wa nyumbani ni uhalifu. Lakini, kutokana na vikwazo vya kijamii na kitamaduni nchini Mali, waathiriwa hawaanzishi kesi za jinai dhidi ya wahusika wa uhalifu huu. Vyama kadhaa vya Mali na NGOs sasa zinahamasisha kupiga kura juu ya sheria ya ukatili wa kijinsia.

Mwongozo huu wa redio utakusaidia kuelewa sababu za ukatili wa majumbani na matokeo yake kwa mwathiriwa na wanafamilia wengine. Mwongozo huu unatokana na mahojiano halisi na watu watatu: mwathirika wa ukatili wa nyumbani, mwanasheria aliyebobea katika maswala ya ukatili wa kijinsia, na mfanyakazi wa NGO.

Ili kutumia mwongozo huu kuzalisha kipindi kituo chako, unaweza kuchagua kutumia waigizaji wa sauti ili kucheza nafasi ya watu ambao wamefanyiwa mahojiano. Katika hali hii, hakikisha kuwafahamisha wasikilizaji wako mwanzoni mwa kipindi kwamba sauti zinazotumiwa ni za waigizaji, sio wahojiwa halisi.

Vile vile, unaweza kuboresha mwongozo huu ili kuzalisha kipindi chenye mada sawa katika eneo lako na kuandika mwongozo wako mwenyewe. Kwa mfano, unaweza kuwauliza waliohojiwa maswali yafuatayo:

  • Ukatili wa majumbani ni nini?
  • Je, ukatili wa majumbani unasababishwa na nini?
  • Je, ukatili wa majumbani hujidhihirishaje?
  • Ni nini matokeo ya ukatili wa majumbani na waathirika wanawezaje kusaidiwa?

Muda uliokadiriwa wa mwongozo huu wa redio pamoja na muziki, utangulizi na ufungaji: dakika 30.

Script

MTANGAZAJI:
Hamjambo wapenzi wasikilizaji, karibuni katika kipindi chetu.

Leo, pamoja na wageni wetu, tutazungumzia ukatili wa majumbani, aina ya ukatili wa kijinsia, unaojulikana pia kama GBV. Watazungumza kuhusu sababu na matokeo ya ukatili wa majumbani, pamoja na hatua zinazochukuliwa na mashirika na watu binafsi kukabiliana nayo. Pia watajadili hatua zinazochukuliwa na vyama na mashirika yasiyo ya kiserikali kuondokana na vikwazo vya utekelezaji wa sheria dhidi ya aina hii ya ukatili.

Tutazungumza na watu watatu wa muhimu sana. Wa kwanza, Bi. Aminata Traoré, ni mwathirika wa ukatili wa nyumbani na mwalimu wa shule ya binafsi huko Djoro, katika eneo la Segou. Ataeleza jinsi alivyonusurika na ukatili huu.

Kisha tutazungumza na Bi. Mariam Traoré, mwanasheria na mtaalamu wa maswala ya ukatili wa majumbani. Atatushirikisha uzoefu wake na mbinu zinazotumiwa kuwasaidia wanawake walionusurika. Mwisho, tutamkaribisha Bw. Ségné Sangaré. Yeye ni mwanasaikolojia, mshauri wa afya na mwanachama wa chama cha wanasaikolojia wa Mali. Atazungumza juu ya mada hii lakini katika kona ya mtazamo wa athari za kisaikolojia za ukatili wa majumbani kwa wanawake na watoto.

MTANGAZAJI:
Karibu, Bi. Aminata Traore!
AMINATA TRAORE:
Asante kwa kuwa nami.
MTANGAZAJI
:
Kama mnusurika wa ukatili wa nyumbani, tuambie ilivyokuwa kwako.

AMINATA TRAORE:
Nilimjua mume wangu wa zamani karibu miaka ishirini iliyopita. Wakati huo tulikuwa wanafunzi. Nilioana naye bila ridhaa ya wazazi wangu ambao walimwona hana adabu sana. Tangu mwanzo, alikuwa na wivu pale aliponiona nikizungumza na wanaume wengine ikiwa ni pamoja na marafiki zangu. Hakuzungumza nami kwa siku kadhaa. Hali ilizidi kuwa mbaya tulipooana. Ili kuonyesha kutofurahishwa kwake, alinipiga kwa mkanda wake. Sikuweza kuinua sauti yangu alipozungumza, vinginevyo angenipiga. Ilikuwa ngumu zaidi alipopoteza kazi yake. Ilinibidi kuvumilia kwa sababu nilikuwa nimejifungua mtoto wa kiume aliyekuwa na umri wa miaka mitano wakati huo. Lakini sikuweza kuzungumzia jambo hilo na familia yangu, kwa kuwa tayari walikuwa wakipinga ndoa yetu.

Siku moja alinipiga na kiti kidogo cha mbao kilichokuwa ndani ya nyumba. Nilikuwa na damu kila mahali na majeraha kichwani. Lakini licha ya majeraha yangu, hakuniruhusu nilale bila kukidhi hamu yake ya ngono. Nilihisi kwamba kuniona ninalia ilikuwa furaha yake. Nilipoteza mimba mara mbili kwa sababu ya ukatili huu. Nilitarajia angebadilika, lakini hali ilikuwa inazidi kuwa mbaya.

Miaka michache baadaye, nilipata mimba ya binti yangu. Lakini hali haikuwa bora. Kwa miaka mingi, niliteseka kwa kila aina ya ukatili nyumbani kutoka kwa mume wangu. Hakunisaidia kifedha. Kwa mshahara wangu kama mwalimu, nililazimika kulipia dawa na chakula kwa ajili ya watoto wangu na yeye. Kwa ufupi, nilitekeleza jukumu ambalo sheria ya ndoa nchini Mali inamtaka yeye kufanya. Sheria inasema kwamba mwanamume lazima amlishe na kumlinda mke wake.

Wakati huu, hakujaribu kufanya kazi. Na niliposhindwa kubeba mizigo hiyo, alininyanyasa kimwili na kunitukana. Ukatili wa kingono, wa matusi na kimwili ambao nilivumilia ulidhorotesha afya yangu ya akili na kuniacha katika hali ya mfadhaiko, huzuni, hasira, na chuki dhidi ya wanaume kwa ujumla.

MTANGAZAJI
:
Kwa nini ulivumilia mateso haya kwa muda mrefu?

AMINATA TRAORE:
Nilijilaumu kwa sehemu kwa sababu ya maonyo ya familia yangu kuhusu mume wangu wa zamani. Kwa hiyo, sikuweza kulalamika kwa wazazi wangu. Pia, nchini Mali, si rahisi kwa mwanamke kumwacha mume mwenye jeuri, hasa kwa uzito wa utamaduni unaopendekeza wanawake kuwa na subira na kuvumilia.

MTANGAZAJI:
Je! watoto wako walipitiaje kipindi hiki?

AMINATA TRAORE:
Kabla ya talaka, mwanangu mwenye umri wa miaka 16 alihisi matatizo yangu. Angesimama kati ya baba yake na mimi, akijaribu kumzuia asinitusi. Hili lilinitia hofu kwa sababu mwanangu alikuwa na uwezo wa kumpiga baba yake ili kunilinda, ingawa ni marufuku kabisa katika jamii yetu. Huku machozi yakinitoka, niliendelea kumwambia amruhusu baba yake anipige. Binti yangu angelia na kuingia chumbani. Shuleni, mwanangu angeshambulia marafiki zake. Alikuwa na hasira kila wakati juu ya vitu vidogo, na binti yangu alikuwa akiogopa kila wakati.

MTANGAZAJI:
Uliwezaje kupata talaka?

AMINATA TRAORE:
Kama tunavyosema mara nyingi, inatosha. Hatimaye, alianza kulala na wahudumu wa nyumba yangu na binti za majirani zetu. Nilipomtaka aache, alinipiga kofi na kunipiga na fimbo hadi akanivunja mkono. Wakati huo, nilichukua vitu vyangu vyote na kwenda nyumbani kwa wazazi wangu. Hapo ndipo nilipoamua kuachana naye kwa sababu nilimchukia. Nilizungumza kuhusu hilo na marafiki, ambao walinishauri kuwasiliana na vyama vya utetezi wa waathiriwa wa dhuluma ili kuwasilisha malalamiko na kuomba talaka. Haikuwa rahisi kwa sababu sikujua taratibu za kufuata mahakamani. Lakini kwa msaada wa NGOs kama vile WiLDAF na marafiki zangu, nilifanikiwa kupata talaka. Sasa ninaishi nyumbani kwa wazazi wangu na watoto wangu, nikingoja kupata mahali pangu mwenyewe.

MTANGAZAJI:
Una ushauri gani kwa wanawake?

AMINATA TRAORE:
Ningependa kuwaambia wanawake kwamba watu wote ni sawa mbele ya sheria na kwamba hakuna mtu ana haki ya kumdhuru mwingine. Mtu anaoelewa ili kuwa na furaha, na si kuwa mtumwa wa mwenzi wake. Mwanamke anapopoteza maisha, watoto wake ndio wa kwanza kuteseka. Inabidi ufanye uamuzi kabla hujachelewa. Nilikuwa na bahati ya kutoka ndani yake. Lakini ni wanawake wangapi wamekufa? Fanya uamuzi haraka, au unaweza kuwa mwathirika mwingine.

MTANGAZAJI:
Asante, Aminata Traoré. Hebu tumsikie sasa Bi. Mariam Traoré, mwanasheria na mtaalamu wa masuala ya ukatili majumbani wa WiLDAF. WiLDAF Mali ni mtandao wa takriban vyama ishirini na wanachama hamsini binafsi. Inalenga kulinda na kukuza haki za wanawake na watoto.

Asante kwa kukubali mwaliko wetu. Hivi Mariam, ukatili wa majumbani ni nini?

MARIAMTRAORE:
Ukatili wa majumbani ni aina ya tabia, vitendo, na mitazamo ya mwenza au mwenza wa zamani ambayo inalenga kumdhibiti na kumtawala mwenza wake. Ukatili huu naweza kuchukua sura ya vitisho vya maneno, kimwili, kingono, au kiuchumi au kumlazimisha mwenza mwingine.

MTANGAZAJI:
Je, hali ikoje na aina hii ya ukatili nchini Mali?

MARIAM TRAORE:
Nchini Mali, kama sehemu nyingine yoyote, ukatili wa majumbani unaendelea kuwa suala la kutia wasiwasi. Tunaishi katika jamii yenye mfumo dume sana. Mume anaonekana kama mkuu wa kaya. Mzigo wa kaya unamwangukia yeye. Ama mke anatarajiwa kumtii mumewe. Ukosefu huu wa usawa mara nyingi husababisha ukatili wa ndani ya nyumba.

Kwa mfano, tumeona kwamba baadhi ya wanawake wanaona vigumu kuendelea na masomo au taaluma zao baada ya kuolewa kwa sababu ya upinzani kutoka kwa waume zao. Kulingana na takwimu, mwanamke mmoja kati ya kila wanawake wawili wenye umri wa miaka 15 hadi 49 nchini Mali amekumbana na ukatili wa kimwili, kihisia, au kingono angalau mara moja katika maisha yake. Idadi sawa ya wanawake pia wanakabiliwa na ukatili wa kihisia au kimwili wakati wa kutengana.

Kwa bahati mbaya, muktadha wa kijamii mara nyingi humlazimisha mwanamke kumvumilia na hata kumsamehe mwenzi wake kwa ukatili huu. Wale wanaoacha nyumba zao wananyanyapaliwa na jamii. Lakini jeuri, mateso anayowekewa mwenzi mwingine, huharibu upatano wa maisha ya ndoa na kuleta changamoto katika hatima ya watoto wa wanandoa hao.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini Mali yanakashifu ukatili wa majumbani kwa namna zote. Lakini pamoja na wito wa mara kwa mara wa mageuzi, maendeleo kidogo yanafanywa katika kushughulikia aina hii ya ukatili kwa utaratibu na ufanisi.

MTANGAZAJI:
Je, ni sababu gani zinasababisha ukatili wa majumbani nchini Mali?

MARIAMTRAORE:
Ukatili wa nyumbani una sababu nyingi. Kuna sababu ya elimu. Watoto huiga tabia hii wanapolelewa katika mazingira ambayo matatizo yote hutatuliwa kwa nguvu, iwe shuleni au katika familia.

Katika jamii ya Mali, dhana nyingi potofu zinahusishwa na mke ambazo si halali kwa mama, dada, na binti. Kwa mfano, nampenda mama yangu, nampenda dada yangu, nampenda binti yangu, lakini sipaswi kumuamini mke wangu.

Hivi karibuni, ukatili hutokea wakati kuna upendeleo dhidi ya wanawake. Katika jamii ya Mali, kijadi mwanamume anachukuliwa kuwa muhimu zaidi kwa sababu ndiye anayeoa mwanamke, kulisha familia, na kuitunza. Hata katika kugawana mali ya familia, kwa mujibu wa desturi zetu, mwanamume hupokea sehemu mara mbili ya mwanamke. Kwa hivyo, ikiwa wanaume wanadhani kuwa wanawake wana hadhi ya chini, au kwamba wanawake hawana mamlaka sawa na wanaume, wanawake watatendewa kwa ukatili. Kimsingi, ukatili wa nyumbani ni matokeo ya ukosefu wa usawa wa kijamii.

MTANGAZAJI
:
Je, shirika lako linafanya nini kuwasaidia wanawake walionusurika na ukatili?

MARIAMTRAORE:
Mashirika kadhaa ya haki za wanawake hutoa msaada wa kisheria na kijamii kwa wanawake walionusurika na ukatili wa majumbani. Sisi wenyewe tuna makazi ya wanawake na watoto walio katika dhiki. Wakati huo huo, kuna warsha za kisheria kusaidia wanawake kuwasilisha malalamiko. Waathirika wanaweza pia kufaidika na usaidizi wa wanasaikolojia, ambao huwasikiliza na kuwahakikishia usalama wao. Kisha tunapanga warsha kwa ajili ya mafunzo, uhamasishaji, na taarifa juu ya haki za wanawake na juu ya sheria zinazowalinda wanawake dhidi ya ukatili wa majumbani.

MTANGAZAJI:
Ni nini kinafanya iwe vigumu kutekeleza sheria dhidi ya ukatili wa majumbani nchini Mali?

MARIAMTRAORE:
Wahalifu wengi wa ukatili wa majumbani wanaamini kwamba sheria haipaswi kuingilia maisha yao ya ndoa. Waathiriwa wa ukatili wa majumbani huhisi hatia kwa sababu wanasadiki kwamba wamefanya jambo baya. Kwa hiyo, wale wanaokumbana na ukatili kila siku huficha, hupunguza, au hufikiri kwamba ukatili huo ni wa muda tu kwa sababu wanaamini kwamba mtendaji atabadilika punde au baadaye.

Manusura wa ukatili wa majumbani wanataka ukatili huo ukomeshwe, lakini mara nyingi hawataki kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mhusika. Pia, shinikizo la kijamii kutoka kwa watoto au familia zote mbili linaweza kumzuia muathiriwa kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mwenzi anayemwacha, kumtukana, au kumpiga. Wanawake wa Mali wanashikamana sana na maisha yao ya ndoa na mustakabali wa watoto wao na wanaweza kusadikishwa kwamba wanapaswa kuwavumilia kupita kiasi wenzi wao kwa muda mrefu kabla ya kuamua kuvunja ndoa zao.

MTANGAZAJI:
Je, itakuwaje kama sheria dhidi ya ukatili wa majumbani ikitekelezwa?

MARIAM TRAORE:
Katiba yetu imeweka fursa sawa kati ya wanaume na wanawake. Baadhi ya aina za ukatili wa kimwili na kingono zinaadhibiwa na sheria. Kuna haja ya kutekeleza sheria kwa kuongeza shughuli zinazoongeza ufahamu kuhusu matokeo ya ukatili wa majumbani. Ni lazima pia tuunde mfumo wa kitaifa wa kuwalinda walionusurika na kuadhibu vikali ukatili wa majumbani.

Kwa mfano, kuboreshwa kwa upatikanaji wa elimu kwa wasichana, fursa zaidi za kuzalisha kipato kwa wanawake, na uwakilishi bora wa wanawake katika maeneo yote ya sekta ya umma na binafsi, ikiwa ni pamoja na katika nafasi za uongozi, inaweza kuwa na manufaa. Chochote ambacho wanaume wanaweza kufanya, wanawake wanaweza pia kufanya mahali pa kazi. Wanawake na wanaume lazima washirikiane kwa maendeleo ya taifa.

MTANGAZAJI:
Asante sana, Mariam. Sasa tunamgeukia Ségné Sangaré, mwanasaikolojia, mshauri wa afya, na mwanachama wa Chama cha Wanasaikolojia wa Mali.

Bwana Sangaré, ni nini huwafanya baadhi ya wanaume kuwa wakatili dhidi ya wapenzi wao?

SANGARESEGNE:
Wanaume wengine kwa asili wana hasira kali na wana uwezekano mkubwa wa kuwa na ukatili. Katika utamaduni wa Mali, mwanamume anaweza kufikiri kuwa ni “kawaida” kumtawala mke wake. Ikiwa hana utulivu, anamrudisha kwenye mstari. Wanaume hawa wanapowapiga wake zao, lengo ni kumfanya anyenyekee. Ikiwa mwanamke anakataa, inaweza kuwa ngumu, na hata mbaya kwa ajili yake. Lakini sababu za ukatili wa majumbani ni tofauti. Zinaweza kutokana na malezi yetu, kutokana na chuki za jamii dhidi ya wanawake, na kutokana na faida wanazopewa wanaume dhidi ya wanawake katika jamii yetu.

MTANGAZAJI:
Kwa nini wanawake waliofanyiwa ukatili wanakataa kuwaacha wapenzi wao?

SANGARESEGNE:
Kuna sababu kadhaa kwa nini wanawake walionusurika wanakataa kuondoka. Kwanza, jamii inaamini kwamba wanawake lazima wateseke ili watoto wao wafanikiwe katika maisha yao. Kuna sababu nyingine kadhaa. Waathirika mara nyingi huhisi aibu, hatia, na hawana nguvu. Wanaogopa kwamba wengine watawahukumu na wasiamini hadithi yao. Wanafikiri kwamba mtu huyo anaweza kubadilika, kwa sababu ameahidi.

Wanaogopa vitisho vyake na mustakabali wa watoto wao. Wanaogopa matokeo ikiwa wangemwacha. Wanaogopa kupoteza kile ambacho wametumia miaka mingi kujenga. Wanaamini kuwa hawawezi kufanya hivyo peke yao. Wanahisi kuwajibika kwa “kuvunja” familia. Wanapuuza sheria zinazowalinda au wanaamini kwamba sheria haziwezi kuwalinda. Wanawapenda waume zao, lakini si tabia zao za ukatili.

Kwa sababu hiyo, wananaswa, si kwa sababu ya imani yao tu bali pia kwa sababu ya mitazamo yao.

MTANGAZAJI:
Je, ni matokeo gani kwa wanawake walionusurika na ukatili wa majumbani na watoto wao?

SANGARESEGNE:
Ukatili wa majumbani unaweza kudhoofisha uwezo wa baadhi ya wanawake kujiamini. Wanawake hawa hawawezi tena kufanya chochote peke yao, na lazima waongozwe kila wakati. Wanahisi kudhalilishwa na kuchanganyikiwa. Wanateseka kwa kukosa usingizi na kuteseka sana kijamii kwa sababu ya shinikizo la waume zao.

Mambo ni magumu zaidi kwa watoto. Wanaishi katika muktadha unaotegemea utawala na uchokozi. Wanakabiliwa na chaguo kati ya wazazi wao na wanaishi kwa uchungu. Pia, ukatili haizungumzwi sana ndani ya familia. Ukimya na mwiko unaozingira hali hizi kwa ujumla unamaanisha kwamba watoto hawapati maelezo ya vitendo wanavyoviona na kufanyiwa. Hivyo, hawana fursa ya kueleza hisia zao, au kuhakikishiwa. Wakiachwa katika hali ya dhiki na mshtuko, watoto hawa wanaweza kuendeleza matatizo ya kihisia na kitabia ambayo yataathiri ukuaji wao.

MTANGAZAJI:
Je, Waathirika wa ukatili wanaotafuta huduma zako wana umri gani?

SANGARE SEGNE:
Ni wanawake wa rika zote. Lakini kwa kawaida ni wanawake ambao wamekuwa kwenye uhusiano kwa zaidi ya miaka mitano. Mwanamke mkubwa zaidi niliyewahi kumsaidia alikuwa na umri wa miaka 63 na alikuwa katika uhusiano kwa miaka 45. Alikuwa mwathirika wa ukatili wa kimwili.

MTANGAZAJI:
Je, unaweza kusema nini kuhitimisha mahojiano haya?

SANGARE SEGNE:
Ningesema kwa wanawake ambao ni waathiriwa wa ukatili wa majumbani kwamba tuko pamoja nao mchana na usiku. Ingawa ni vigumu kutekeleza sheria nchini Mali, ingawa jamii tunamoishi haiwapendezi sana, bado kuna matumaini kwa sababu ya vyama na mashirika yasiyo ya kiserikali. Daima husikiliza na kufanya kila wawezalo kwa ajili ya wanawake na watoto.

MTANGAZAJI:
Asante kwa maelezo yako, Bw. Sangaré. Asante pia Bi. Aminata Traoré na Bi. Mariam Traoré kwa michango yao.

Ukatili dhidi ya wanawake ni pamoja na ukatili wa kimwili, lakini pia ukatili wa kiuchumi, kingono na kisaikolojia. Inaathiri jamii zote, zilizoendelea au zinazoendelea, na tabaka zote za kijamii. Matokeo yake ni mabaya kwa jamii kwa ujumla.

Tumefika mwisho wa programu ya leo. Asante kwa wageni wetu wote na kwa kila mtu anayesikiliza. Tutarudi hivi karibuni kwa programu nyingine.

Acknowledgements

Rejea

 

Kulingana na ripoti ya Taasisi ya Mafunzo ya Usalama (https://issafrica.org/fr), mmoja kati ya kila wanawake wawili wa Mali walio na umri wa kati ya miaka 15 na 49 tayari walikuwa wamepitia ukatili wa kimwili au kingono.

This resource was produced through the “HÉRÈ – Women’s Well-Being in Mali” initiative, which aims to improve the sexual and reproductive health well-being of women and girls and to strengthen the prevention of and response to gender-based violence in Sikasso, Ségou, Mopti, and the district of Bamako in Mali. The project is implemented by the HÉRÈ – MSI Mali Consortium, in partnership with Farm Radio International (RRI) and Women in Law and Development in Africa (WiLDAF) with funding from Global Affairs Canada.

 

Translation for this resource was made possible thanks to Farm Radio International donors.

Information sources

Mahojiano: 

 

Bi. Aminata Traoré, mwathiriwa wa ukatili wa kijinsia na mwalimu wa shule ya kibinafsi huko Djoro, eneo la Segou. Mahojiano yaliyofanywa Mei 26, 2022.

 

 

Bi. Mariam Traoré, mwanasheria aliyebobea katika maswala ya ukatili wa kijinsia (GBV) kutoka shirika la WiLDAF. Mahojiano yaliyofanywa tarehe 15 Juni, 2022.

 

 

Bw. Ségné Sangaré, mwanasaikolojia, mshauri katika maswala ya afya na mwanachama wa Chama cha Wanasaikolojia wa Mali. Mahojiano yaliyofanywa tarehe 13 Juni, 2022.