Matangazo kuhusu chanjo za COVID-19, uhimizaji wa chanjo, hatua za afya ya umma na usawa wa kijinsia na ushirikishwaji

AfyaAfya

Ujumbe kwa mtangazaji

Vidokezo kwa Watangazaji

COVID-19 inaendelea kuwa tishio kubwa la afya duniani. Kwa kuwa sasa chanjo zinapatikana, una fursa ya kuwahimiza wasikilizaji wako kupata chanjo kwa:

  • Kujibu kwa heshima maswali yao na wasiwasi wao kuhusu chanjo ya COVID-19.
  • Kutoa taarifa sahihi na za kuaminika kuhusu chanjo.
  • Kuhimiza wasikilizaji wako kupata chanjo kwa kushirikisha sauti za watu waliochanjwa katika jamii yako ambao wako tayari kuwa kama mabalozi na kuhimiza chanjo za COVID-19.
  • Kuwahakikishia wasikilizaji wako kwamba chanjo za COVID -19 ni salama na zina ufanisi.

Taarifa na ujumbe kuhusu COVID-19 haupaswi kutolewa tu katika progamu ya kituo chako inayohusiana na masuala ya afya pekee! Unaweza kutangaza chanjo za COVID-19 kwa urahisi na kwa ufanisi kwa kurusha mfululizo huu wa matangazo 24 kwenye programu zako nyingi—pamoja na habari zako, muziki, biashara, michezo na programu za kidini—ili kufikia wasikilizaji wengi iwezekanavyo.

Chukua muda kukagua matangazo haya na ubadilishe kulingana na aina tofauti za programu za kituo chako. Kwa mfano, matangazo fulani hufanyika sokoni, lakini yanaweza kufanyika kwa urahisi kwenye mechi ya michezo au tamasha la muziki, ofisini, katika mashamba ya wakulima, au mahali pa ibada.

Unaweza pia kuhariri matangazo ili kuendana na muktadha wa jamii yako kwa:

  • Kubadilisha majina ya wahusika katika tangazo na kuweka majina ya eneo lako,
  • Kutumia jina la kituo chako cha redio inavyofaa (maandishi yanasomeka: Redio XXX),
  • Kwa kutumia maneno yanayofahamika ambayo yanaeleweka kwa urahisi na wasikilizaji wako (kwa mfano, wasikilizaji wako wanaweza kurejelea COVID-19 kwa jina lingine kama vile “COVID” au “Corona”), na
  • Kuhakikisha kwamba taarifa unayoshirikisha haitofautiani na ushauri unaotolewa kutoka kwa mamlaka za afya za eneo lako.

Ili kuunda matangazo yako mwenyewe, waombe wasikilizaji washirikishe uzoefu wao kuhusu chanjo na kisha uwaombe ruhusa ya kurekodi sauti zao, na kuzitumia kama sehemu ya matangazo yanayoendelea. Katika kurekodi sauti, waulize majina yao, umri, kwa nini walipata chanjo, na jinsi wanavyohisi sasa. Mapendekezo chanya kama haya yanaweza kusaidia sana kuwashawishi wasikilizaji wako kwamba chanjo hizo ni salama na zinafaa.

Tangazo #21 katika safu hii, ni mfano wa “idhinisho la chanjo’.  Unaweza kumwomba mtu mmoja katika jamii ambaye ni maarufu na anayeaminika kurekodi eneo hili, au lingine kama hilo, na kuendelea kulitangaza.

Ili kufikia watu wengi iwezekanavyo, tafsiri matangazo haya katika lugha zinazozungumzwa na wasikilizaji wako. Baada ya muda, Farm Radio International itatafsiri matangazo haya katika lugha kadhaa za Kiafrika kwa matumizi yako. Ili kufikia tafsiri hizi zinapopatikana, nenda kwenye tovuti: https://scripts.farmradio.fm/radio-resource-packs/translations-available/

Script

 

Tangazo 1:
Vaa barakoa na uvae ipasavyo

MSIMULIZI:
Janga la COVID-19 limekuwa la kuchosha-na bado halijaisha. Lakini usikate tamaa! Tunahitaji kuendelea kuwa imara kwa kila mmoja wetu, na kulinda marafiki zetu, familia na jamii.

Kwa hivyo hata kama umechanjwa kikamilifu, endelea kuvaa barakoa inayofunika pua na mdomo wako. Ili barakoa ikulinde, lazima ikae vizuri dhidi ya mashavu na pua yako, na juu ya kidevu chako. Inapovaliwa vizuri, barakoa yako inapaswa kukaa vizuri.

Vaa barakoa inayofunika vizuri, na upate chanjo.

Kwa pamoja, tunaweza kuishinda COVID-19.

 


 

Tangazo 2:
Barakoa za kimatibabu (zinazotumika hospitalini) zinafaa zaidi kuliko barakoa za kitambaa—lakini barakoa yoyote ni bora kuliko kutokuwa na barakoa.

MSIMULIZI:
Barakoa ni mojawapo ya zana bora zaidi tulizo nazo za kuzuia COVID-19 kuenea. Barakoa za matibabu zenye ubora mzuri na zinazoweza kutumika ni bora zaidi katika kukukinga na maambukizo na kuzuia kuenea zaidi kwa COVID-19 kuliko barakoa vitambaa ambazo zinazoweza kutumika tena.

Lakini kumbuka: Ni lazima barakoa yako ikae vizuri pale inapovaliwa ili kukulinda dhidi ya kuambukizwa na kukuzuia kuwaambukiza wengine.

Iwapo huna uwezo wa kupata barakoa za matibabu zinazoweza kutumika na kisha kutupwa, endelea kuvaa barakoa za kitambaa zinazotoshea vizuri kwenye pua na mdomo wako. Kuvaa barakoa ya kitambaa ni bora zaidi kuliko kutokuwa na barakoa hata kidogo.

Linda watu unaowapenda. Vaa barakoa.

 


 

Tangazo 3:
Bado tunahitaji kuchukua tahadhari dhidi ya COVID-19.

MSIMULIZI:
Janga la COVID-19 limekuwa la muda mrefu na gumu. Na kwa bahati mbaya, bado haijaisha.

Kwa hivyo sote tunahitaji kuendelea kuchukua tahadhari.

Endelea kuvaa barakoa ambayo inafunika pua yako NA mdomo. Kaa umbali kati ya mtu na mtu. Safisha mikono yako mara kwa mara. Hakikisha kunakuwa na mzunguko mzuri wa hewa kwa kufungua madirisha. Kohoa na kupiga chafya kwenye kiwiko chako cha mkono.

Na muhimu zaidi, pata chanjo!

Tuendelee kuwa imara kwa kila mmoja na kulinda jamii zetu.

 


 

Tangazo 4:
COVID-19 inaweza kuwa na athari za kiafya za muda mrefu.

SFX:
SAUTI YA KUNYANYUA KITU KIZITO. KISHA KUKOHOA

MKE:
Kofi, uko sawa? Nini tatizo?

MUME:
(ANAPUMUA KWA NGUVU) Ndiyo, asante mpendwa, niko sawa. Sijahisi hivyo tangu nilipopona COVID-19 … bado nina shida ya kupumua, na shughuli za kutumia nguvu ambazo hapo awali niliziona rahisi sasa ni changamoto.

MKE:
Lakini hilo linawezekana vipi? Ulipimwa na haukuonekana kuwa na COVID-19 wiki iliyopita na wewe ni kijana mwenye afya njema!

MUME:
Hiyo ni kweli, lakini daktari wangu aliniambia kuwa COVID-19 inaweza kusababisha uharibifu wa kudumu kwa mapafu, moyo, na figo—na hata kupoteza harufu na ladha. Unajua sijapata ladha ya chakula chako kwa wiki sasa. Na mimi huhisi uchovu kila wakati …

MKE:
Lo, mpenzi wangu, pole … natumai utajisikia vizuri hivi karibuni. Nashukuru tumechanjwa sasa.

MSIMULIZI:
COVID-19 haina ubaguzi. Ni hatari kwa KILA MTU na inaweza kuwa na athari za kudumu kwa afya na ustawi wako. Chanjo ndiyo njia salama na bora zaidi ya kuzuia kuumwa sana, kulazwa hospitalini na kifo kutokana na COVID-19.

Kwa hiyo usisubiri. Pata chanjo leo.

 


 

Tangazo 5:
Unasitasita kuhusu chanjo za COVID-19? Pata maelezo unayohitaji

MWANAUME 1:
Siamini kuwa tunaambiwa tupate chanjo dhidi ya COVID-19. Hii inakiuka haki na uhuru wangu!

MWANAUME 2:
Ndugu yangu, ninaelewa jinsi unavyohisi. Nilisitasita kuhusu chanjo za COVID-19 pia. Nilitaka kujifunza zaidi kuhusu chanjo hizi na jinsi zinavyofanya kazi, kwa hivyo nilisikiliza Redio XXX na kuuliza maswali yangu yote. Baada ya hapo, nilibadili mawazo yangu. Sasa ninadhani kwamba lazima tupate chanjo ili kuwalinda wengine katika jamii yetu, pamoja na sisi wenyewe.

MWANAUME 1:
Hmmm … kama umefanya utafiti wote huo, labda upo sahihi … itabidi nifikirie kuhusu hilo…

MWANAUME 2:
Asante! Sasa vipi kuhusu hiyo mechi ya soka! (SAUTI YA KUFIFIA)

MSIMULIZI:
Watu wengi wanasitasita, wana hasira, au wanaogopa kuchukua chanjo za COVID-19.

Kuwa balozi wa chanjo kwa kuchukua muda wa kujifunza kuhusu chanjo na kuzungumza na familia yako na marafiki kuhusu chanjo.

Pata ukweli. Pata chanjo.

 


 

Tangazo 6:
Kuambukizwa baada ya chanjo

SFX:
SIMU INAITA

MWANAMKE:
Haloo, hii ni Radio XXX. Uko hewani!

MWANAUME:
Haloo! Nina swali kuhusu chanjo za COVID-19, tafadhali. Kwa nini nipate chanjo? Nasikia kwamba hata watu waliochanjwa wanaweza kuugua COVID-19.

MWANAMKE:
Ndiyo, inawezekana kuugua COVID-19 na hata kuisambaza kwa wengine baada ya kuchanjwa. Lakini kupata chanjo hupunguza sana hatari hiyo.

Chanjo hiyo hukukinga vyema kutokuumwa sana, kulazwa hospitalini, na hata kifo. Ndiyo maana ni muhimu kupata chanjo-ni kwa ajili ya afya yako mwenyewe.

MWANAUME:
Je, unasema kwamba nikipata COVID-19 baada ya kuchanjwa, nitakuwa na afya bora kuliko kama sikuchanjwa?

MWANAMKE:
Hasa!

MSIMULIZI:
Kirusi cha omicron inaambukiza na kusambaa. Ndio maana watu wengi wanaugua COVID-19 baada ya kuchanjwa.

Lakini chanjo ni nzuri sana katika kuzuia kuumwa sana, kulazwa hospitalini, na kifo.

Kwa hiyo usisubiri. Chanja.

 


 

Tangazo 7:
Pata chanjo ili kuwalinda walio hatarini zaidi.

BINTOU:
Fatou! Mbona sijakuona sokoni hivi majuzi?

FATOU:
Halo, Bintou. Ninaogopa sitatoka sana nje tena. Siwezi kupata chanjo dhidi ya COVID-19, kwa hivyo sina budi kuchukua tahadhari zaidi ili kuwa na afya njema.

BINTOU:
Oh hapana! Kwanini usichanje?

FATOU:
Nilitaka, rafiki yangu. Lakini kwa sababu ninatibiwa

saratani, siwezi. Chanjo ni salama na ni nzuri, najua, lakini mfumo wangu wa kinga ni dhaifu sana kwa chanjo kwa sababu ya matibabu yangu.

BINTOU:
Hiyo ni mbaya, pole Fatou. Je, kuna chochote ninachoweza kufanya?

FATOU:
Ndio—wahimize marafiki zako na familia kupata chanjo! Hatakama siwezi kupata chanjo, inasaidia kama kila mmoja anayenizunguka amechanja. Wakati ambapo kila mtu atakuwa amechanja, basi labda nitajisikia salama kurudi sokoni.

MSIMULIZI:
Watu walio na kinga dhaifu wana uwezekano mkubwa wa kuugua au kufa kwa sababu ya COVID-19. Na kwa sababu hawawezi kupata chanjo, hatari ni kubwa zaidi.

Linda jamii yako, ikiwa ni pamoja na wale walio katika hatari zaidi. Pata chanjo.

 


 

Tangazo 8:
Ndiyo, wanawake wajawazito wanaweza kupata chanjo kwa usalama dhidi ya COVID-19.

MWANAMKE 1:
Hongera kwa ujauzito wako, dada yangu! Lazima utakuwa na hamu ya kumkaribisha mtoto mwingine kwenye familia yako.

MWANAMKE 2:
Tumefurahi sana! Na ninahisi salama zaidi sasa kwa kuwa nimechanjwa dhidi ya COVID-19!

MWANAMKE 1:
(KWA MSHANGAO) Umechanjwa?? Lakini unawezaje kupata chanjo wakati una ujauzito?

MWANAMKE 2:
Hujasikia? Wanasayansi wanasema kuwa chanjo hiyo ni salama kabisa kwa wanawake wajawazito na watoto waliowabeba tumboni. Lakini kuugua COVID-19 itakuwa hatari kubwa kwangu na kwa mtoto. Chanjo itatulinda!

MWANAMKE 1:
Hiyo ni habari nzuri, basi! Kwa hivyo … unafikiri mtoto atafanana na wewe au mume wako? (KICHEKO NA SAUTI KUFIFIA CHINI)

MSIMULIZI:
Wanawake, mnaweza kupata chanjo ya COVID-19 salama kabisa ikiwa wewe ni mjamzito. Wanasayansi ambao wanaendelea kutafiti chanjo ya COVID-19 wanasema kwamba wanawake wajawazito wanaweza na wanapaswa kupata chanjo.

Kwa hivyo usisubiri! Jilinde mwenyewe na mtoto wako. Pata chanjo.

 


 

Tangazo 9:
Chanjo ya COVID-19 HAISABABISHI utasa au kutokuwa na nguvu za kiume.

MSIMULIZI:
Huenda umesikia uvumi kwamba chanjo za COVID-19 hukufanya kuwa tasa au kutokuwa na uwezo wa kuzaa! Hii SI kweli. HAKUNA ushahidi kwamba chanjo za COVID-19 huathiri uzazi au kutokuwa na nguvu za kiume.

Usiamini uvumi wa uwongo. Pata chanjo.

 


 

Tangazo 10:
Chanjo za COVID-19 HAZISABABISHI utasa kwa wanaume

MWANAUME 1:
Rafiki yangu, nilisikia kuwa hujachanjwa dhidi ya COVID-19. Kwa nini usichanje?

MWANAUME 2:
Siwezi kupata chanjo—huenda bado nataka kuwa na watoto!

MWANAUME 1:
Lo, huu ni uvumi mbaya. Na sio kweli. Chanjo za COVID-19 hazikufanyi kuwa tasa! Chanjo hizo ni salama na zinafaa. Zinakulinda dhidi ya kuugua sana, kulazwa hospitalini, au kufa kwa sababu ya COVID-19.

MWANAUME 2:
Kwa hivyo unasema. Lakini unawezaje kuwa na uhakika hivyo?

MWANAUME 1:
Nilisikiliza Redio XXX. Waliwahoji maafisa wa afya ya umma, madaktari wa eneo hilo, na watu ambao wamechanjwa. Na wote wakasema kitu kimoja. Chanjo za COVID-19 HAZIFANYI wanaume au wanawake kuwa wagumba.

Kwa hivyo tafadhali pata chanjo. Ni kwa ajili ya afya yako mwenyewe, na manufaa ya kila mtu katika jamii.

MWANAUME 2:
(AKIFIKIRIA) Vema … inaleta tofauti kwangu kwamba watu hao wote walisema kitu kimoja. Na kila mara nimekuwa nikiamini Redio XXX … lakini bado nina maswali machache. Nitapiga simu kwenye redio usiku wa leo.

MSIMULIZI:
Chanjo za COVID-19 HAZIKUFANYI kuwa tasa.

Usiamini uvumi wa uwongo. Pata chanjo.

 


 

Tangazo 11:
Chanjo za COVID-19 HAZISABABISHI utasa kwa wanawake.

SFX:
SAUTI ZA SOKONI. SAUTI INAFIFIA CHINI.

MWANAUME 1:
Ahmed, nilisikia kwamba mke wako alipata chanjo ya COVID-19. Kwa nini alifanya hivyo? Nilidhani unataka mtoto mwingine.

MWANAUME 2:
Ndiyo, Abdoul, alichanjwa na nimefurahi. Chanjo ya COVID-19 haitamfanya kuwa tasa. Itamlinda asiugue sana na kifo.

MWANAUME 1:
Umejuaje?

MWANAUME 2:
Kweli, mabilioni ya watu wamechanjwa salama dhidi ya COVID-19, kwa hivyo nina imani kuwa atakuwa sawa.

MSIMULIZI:
Chanjo za COVID-19 HAZIFANYI wanawake au wanaume kuwa wagumba.

Usiamini uvumi wa uwongo. Pata chanjo.

 


 

Tangazo 12:
Wanawake wanaonyonyesha wanaweza kupata chanjo ya COVID-19

SFX:
MTOTO ANALIA. SAUTI INAFIFIA CHINI.

ASSATA:
Oh, Mariama, ni mtoto mzuri wa kike! Hongera sana.

MARIAMA:
Asante, Assata, tumebarikiwa sana. Na wiki iliyopita tu nilichanjwa dhidi ya COVID-19 ili niwe na afya nzuri kadri mtoto wangu anavyokua.

ASSATA:
(KWA MSHANGAO) Umechanjwa?? Hiyo inawezaje? Kweli unamnyonyesha mtoto wako?? Hutaki kupitisha chanjo na maziwa yako ya mama!

MARIAMA:
Rafiki yangu, bila shaka ninamnyonyesha msichana wangu mzuri. Chanjo za COVID-19 ni salama kabisa kwa akina mama wanaonyonyesha na watoto wao, na chanjo hiyo inaweza hata kupitisha kinga fulani dhidi ya COVID-19.

ASSATA:
Naam, hiyo ni ahueni! Ninafurahi kuwa unajitunza vizuri wewe na mtoto wako.

MARIAMA:
Mimi ni mama sasa—siwezi kuhatarisha afya yangu.

MSIMULIZI:
Wanawake, mnaweza kupata chanjo ya COVID-19 kwa usalama ikiwa unanyonyesha. Wanasayansi wanaochunguza chanjo za COVID-19 wanasema kuwa wanawake wanaonyonyesha wanaweza na wanapaswa kupata chanjo.

Kwa hivyo usisubiri! Jilinde wewe NA mtoto wako. Pata chanjo.

 


 

Tangazo 13:
Wanaume! Wasaidieni wanawake wakati wa janga la COVID-19.

MSIMULIZI:
Wanaume! Wakati wa janga la COVID-19, wanawake wengi wamekuwa wakifanya kazi kwa bidii na kwa muda mrefu zaidi kuliko hapo awali. Watoto wamekosa shule, wanafamilia wameugua, na wanawake wamekuwa na mahitaji mengi zaidi kwa wakati wao—juu ya majukumu yao mengine yote shambani, kazini, na nyumbani!

Usiruhusu wanawake katika maisha yako wakateseka.

Wanaume, wasaidieni dada zenu, wake, binti na mama zenu katika wakati huu wa mahitaji kwa kutoa msaada wenu katika malezi ya watoto na majukumu mengine ya nyumbani.

Na kuna njia nyingine muhimu unaweza kuinua na kusaidia wanawake na kuwaweka salama. Pata chanjo dhidi ya COVID-19.

 


 

Tangazo 14:
Kuna msaada kwa wanawake ambao wanapitia unyanyasaji na unyanyasaji wa kijinsia wakati wa janga la COVID-19.

MSIMULIZI:
COVID-19 imeumiza kila mtu—lakini hasa wanawake.

Wakati wa janga la COVID-19, wanawake wengi wameshindwa kuondoka nyumbani, na wamenyanyaswa na waume zao. Iwapo wewe au mtu fulani unayemjua anahitaji usaidizi wa kihisia, matibabu, kisheria au kisaikolojia, piga simu kwa [WEKA NAMBA YA SIMU AU HUDUMA ZA MSAADA KWA UKATILI WA MAJUMBANI KATIKA UKANDA WAKO].

Kumbuka, hauko peke yako.

 


Tangazo 15:
Zuia na uripoti unyanyasaji wa kijinsia wakati wa janga la COVID-19.

MSIMULIZI:
Baba, kaka, dada, na akina mama—sote tuna jukumu muhimu la kutekeleza katika kuzuia na kuripoti unyanyasaji dhidi ya wanawake. Ikiwa ni pamoja na wakati wa janga la COVID-19.

Iwapo wewe au mtu fulani unayemjua anahitaji usaidizi wa kihisia, matibabu, kisheria au kisaikolojia, piga simu kwa [WEKA NAMBA YA SIMU AU HUDUMA ZA MSAADA KWA UKATILI WA MAJUMBANI KATIKA UKANDA WAKO].

Sema hapana kwa ukatili dhidi ya wanawake.

 


 

Tangazo 16:
Wazazi! Zungumzeni na watoto wenu kuhusu chanjo za COVID-19.

MUME:
Mpendwa wangu, nadhani tunapaswa kuzungumza juu ya chanjo za COVID-19. Watoto wetu wakubwa sasa wanaweza kupata chanjo, kwa hivyo tunahitaji kuamua la kufanya.

MKE:
Ndiyo, uko sahihi … ninajisikia vizuri sana baada ya chanjo yangu. Na daktari alituambia kwamba chanjo hutoa ulinzi mzuri dhidi ya kuugua sana, kulazwa hospitalini, na kifo.

MUME:
Hiyo ni kweli … Hebu tuketi na watoto usiku wa leo na tuzungumze kama familia. Nadhani ni wakati wa watoto wetu kupata chanjo.

MSIMULIZI:
Wazazi! Fanyeni kazi pamoja kufanya maamuzi kuhusu afya na ustawi wa familia yenu. Zungumza na watoto wako kuhusu chanjo za COVID-19, na ufanye chaguo sahihi ili kulinda familia na jamii yako.

Usisubiri. Ni wakati wa kupata chanjo.

 


 

Tangazo 17:
Chanjo sio tu kwa wazee!

MWANAMKE 1:
Karibuni wote kwenye mkutano wetu wa ushirika usiku wa leo. Nina furaha sana kurudi na kukutana na nyie ana kwa ana na ninajisikia vizuri baada ya kupokea dozi yangu ya pili ya chanjo ya COVID-19.

MWANAMKE 2:
Lakini kwa nini upate chanjo, bibie? Chanjo hizo za COVID-19 ni za wazee pekee, na wewe ni kijana na u mzima wa afya.

MWANAMKE 1:
Sawa, asante, lakini … chanjo hizi ni za kila mtu—wazee NA vijana! Wanawake wajawazito pia.

MWANAMKE 2:
Hata wanawake wajawazito?

MWANAMKE 1:
Ndiyo, ni salama kabisa kwa wanawake wajawazito kuchanjwa dhidi ya COVID-19. Maafisa wa afya ya umma wanasema chanjo ndiyo njia bora ya kujikinga wewe, familia yako na jamii yako.

Sasa, turudi kwenye mkutano wetu … (SAUTI INAFIFIA CHINI)

MSIMULIZI:
COVID-19 haina ubaguzi. Inaweza kuathiri mtu yeyote wa umri wowote.

Chanjo za COVID-19 ni njia salama na madhubuti ya kulinda watu wa rika zote.

Ni wakati wa kupata chanjo.

 


 

Tangazo 18:
Usiruhusu COVID-19 ikuweke mbali na marafiki, familia na kazi.

MSIMULIZI:
Walio na visa vikali vya COVID-19 wanaweza kuchukua wiki sita au zaidi kupona, na COVID-19 inaweza kuwa na madhara ya kudumu kwa afya zao. Hii inamaanisha kuwa mbali na marafiki, familia na kazini.

Lakini watu ambao wamechanjwa dhidi ya COVID-19 wana uwezekano mdogo wa kuugua sana, kulazwa hospitalini, au kufa. Wanaweza kuwa na afya njema na kuendelea kutunza na kufurahia familia zao.

Kwa hiyo usisubiri. Pata chanjo.

 


 

Tangazo 19:
Usipoteze maisha yako kwa COVID-19.

MSIMULIZI:
Takriban watu milioni sita ulimwenguni wamekufa kwa sababu ya COVID-19. Huu ni msiba mbaya sana.

Lakini kuna njia rahisi ya kujilinda. Chanjo za COVID-19 ni salama na zinafaa. Kupata chanjo hukupa ulinzi mzuri dhidi ya kuugua sana, kulazwa hospitalini, au kufa kwa sababu ya COVID-19.

Usipoteze maisha yako. Pata chanjo.

 


 

Tangazo 20:
Je, unasitasita kuhusu chanjo za COVID-19? Pata ukweli.

AMMA:
Habari za asubuhi, Sita! Nimefurahi kukuona kwenye duka langu. Unaonekana upo vizuri!

SITA:
Asante, Amma. Najisikia vizuri! Nimechanjwa kikamilifu dhidi ya COVID-19. Ni ahueni iliyoje!

AMMA:
Lo, Sita … sina uhakika kuwa ninaziamini chanjo hizo.

SITA:
Ninaelewa wasiwasi wako. Lakini unaweza kutaka kujifunza zaidi kuhusu chanjo hizi. Familia yangu yote na marafiki wa karibu wamechanjwa, na wote ni wazima, kama mimi.

AMMA:
Kweli?

SITA:
Ndiyo. Mabilioni ya watu wamepokea chanjo za COVID-19 salama. Wao wapo salama na wanazuia kuugua sana, kulazwa hospitalini, na kifo.

AMMA:
Naam, asante kwa kuniambia. Lakini nina maswali zaidi. Unaweza kuniambia zaidi kuhusu … (SAUTI INAFIFIA CHINI)

MSIMULIZI:
Kuzungumza na marafiki na familia yako kuhusu wasiwasi wao kunaweza kusaidia kuwahakikishia kuwa chanjo za COVID-19 ni salama na zinafaa.

Pata ukweli, pata chanjo, na uwe balozi wa chanjo kwa kuzungumza na marafiki na familia yako kuhusu chanjo za COVID-19.

 


 

Tangazo 21:
Uidhinishaji binafsi wa chanjo

MSIMULIZI:
Maisha ni baraka. Kila mmoja wetu ana jukumu la kulinda familia na jamii zetu dhidi ya COVID-19.

Mimi ni (jina, cheo) hapa kukuambia kuwa chanjo za COVID-19 ni salama na zinafaa. Ninawahimiza ninyi nyote kupata chanjo haraka iwezekanavyo—ili muweze kuendelea kupokea baraka za maisha.

 


 

Tangazo 22:
Madhara ya kawaida, madogo ya chanjo za COVID-19

SFX:
SIMU INAITA

MWANA:
Halo, ni Benjamin hapa.

BABA:
Ben! Halo, mwanangu!

MWANA:
Habari yako baba?

BABA:
Niko sawa, lakini nilisikia kwamba umepata mojawapo ya chanjo hizo za COVID-19. Je, hujui mambo hayo yatakufanya uwe mgonjwa?

MWANA:
Lo, huo ni uvumi mbaya tu, baba. Nilipata madhara ya kawaida, madogo baada ya kupata chanjo. Mkono wangu ulikuwa unauma, na nilikuwa nimechoka kidogo, lakini hilo lilitoweka baada ya siku moja au mbili. Kama chanjo nyingine yoyote.

Na sasa ninahisi afya na ninajisikia vizuri. Chanjo hazifanyi watu kuwa wagonjwa-huweka watu salama. Natumai wewe na mama mtapata chanjo hivi karibuni.

BABA:
Nimefurahi kuwa unajisikia vizuri! Kuhusu mimi na mama yako, tutafikiria juu ya chanjo, ninaahidi. Kwaheri, mwanangu, nitakupigia tena hivi karibuni … (SAUTI INAFIFIA CHINI)

MSIMULIZI:
Madhara madogo kama vile kidonda, uchovu, maumivu ya kichwa, na homa kidogo ni ya kawaida katika siku chache za kwanza baada ya kupata chanjo ya COVID-19. Hizi ni za kawaida, na zinamaanisha kuwa chanjo inafanya kazi.

Chanjo ya COVID-19 ni salama na zina ufanisi.

Pata ukweli. Pata chanjo.

 


 

Tangazo 23:
Saidia watoto wako kupata chanjo.

SFX:
MLANGO UNAGONGWA. SAUTI YA MLANGO KUFUNGULIWA.

MKE:
Andrade, Niko nyumbani!

MUME:
Habari Mpenzi wangu.

MKE:
Kwa nini unaonekana kuwa na wasiwasi sana, mpenzi wangu?

MUME:
Nimesikia kutoka kwa Aziz … alisema atapata chanjo dhidi ya COVID-19. Najua watu wanasema chanjo hizo ni salama, lakini nina wasiwasi …

MKE:
Ni kawaida tu kuwa na wasiwasi juu ya mtoto wako, mpenzi. Lakini ninajua watu wengi ambao wamepata chanjo, na wote ni wazima na wanaendelea vizuri. Daktari wangu aliniambia itanilinda dhidi ya COVID-19. Labda tunapaswa kujifunza zaidi kuhusu chanjo hizi?

MUME:
Labda unasema kweli … Na yeye ni mtoto wetu. Tumemlea vizuri na ninamwamini.

MSIMULIZI:
Chanjo za COVID-19 ni salama na zina ufanisi. Wasaidie watoto wako kwa kujadili nao suala la chanjo.

Ni wakati wa kupata chanjo.

 


 

Tangazo 24:
Chanjo hizo ni salama na zina ufanisi.

MSIMULIZI:
Baadhi ya watu wana wasiwasi kwamba chanjo za COVID-19 zilitengenezwa haraka sana na si salama. Lakini chanjo za COVID-19 ni salama na zina ufanisi.

Hapa kuna sababu tatu kwa nini zilipatikana haraka sana:

Kwanza, watafiti wamekuwa wakitafiti virusi vya corona kwa miongo kadhaa. COVID-19 inafanana na virusi vingine vya corona, na kwa hivyo wanasayansi waliweza kujua haraka ni aina gani ya chanjo ingefanya kazi dhidi ya COVID-19.

Pili, kwa sababu COVID-19 ni janga la kimataifa, mashirika mengi, makampuni, na serikali ziliwekeza pesa nyingi katika kuunda chanjo ya kuwaweka watu salama. Fedha hizi ziliruhusu wazalishaji wa chanjo kufanya kazi kwa haraka na kwa ufanisi zaidi kuliko wanavyopata chanjo zingine.

Tatu, chanjo za COVID-19 zimejaribiwa ili kujiridhisha na usalama wake, na majaribio haya yanaendelea, hata sasa. Kwa sababu athari za COVID-19 zinaweza kuwa kubwa sana, wanasayansi walisoma data za majaribio mara tu ilipopatikana. Hii ilisaidia makampuni kutengeneza chanjo kwa haraka zaidi.

Chanjo za COVID-19 ni salama na zina ufanisi.

Kwa hiyo usisubiri. Pata chanjo.

 


 

Acknowledgements

Shukrani

Imechangiwa na: Vijay Cuddeford, Mhariri Mtendaji, Farm Radio International na Hannah Tellier, Mratibu wa Rasilimali, Farm Radio International

Chanzo hichi kimefadhiliwa na Serikali ya Canada kupitia Global Affairs Canada kama sehemu ya mradi wa Kuokoa Maisha na Afya ya Umma na Mawasiliano kuhusu Chanjo katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara (au VACS).