Njia kubwa za juu zaidi kutoka “Njia sabini na tano za kuandaa kipindi chako cha redio cha mkulima”

Ujumbe kwa mtangazaji

Pakua na hariri taarifa hii kwa matumizi yako.

Muhtasari kwa mtangazaji

Radio zaidi ya chombo chochote kile cha habari, huzungumza lugha ya wakulima. Wakulima hutegemea redio kuwapa taarifa wanazohitaji, wakati wanapozihitaji. Na wakulima wanataka redio kuwahusisha katika mijadala inayohusu namna bora ya kupanda mazao yanayolisha familia zao, na namna ya kupata pesa katika masoko.

Mara kwa mara, redio huwaangusha wakulima. Wakulima huzima redio zao wakati ambapo taarifa za muhimu sana hazitangazwi au ambapo mihadhara itolewayo na maprofesa, wanasiasa na wadhamini. Hii huhafifisha sauti za wakulima.

Haitakiwi iwe hivi. Watangazaji wa Afrika wanaweza kuzalisha programu nzuri kwa ajili ya wakulima. Wanaweza kukidhi mahitaji ya wakulima, kuwahusisha wakulima, na kufanya matangazo kuwa ya kuvutia zaidi. Kinachotakiwa ni kuweka desturi nzuri na kuishirikisha kwa upana Afrika kote.

Mwaka 2010, Farm Radio International ilikusanya taarifa zihusuzo programu za redio za mkulima kutoka vituo vya redio Cameroon, Ghana, Kenya, Tanzania na Malawi. Tulitembelea vituo ishirini na vyumba viwili vya uzalishaji na tulisikiliza vipindi vyao vya mkulima. Tuliuliza mamia ya maswali kwa watu wanaoviandaa na watu wanao visikiliza. Kulingana na utafiti wetu, tunachapisha orodha ya dondoo kwa watangazaji wanaohiji kuboresha vipindi vyao vya mkulima kuanzia sasa!

Mabadiliko chanya huwa hayaji kwa siku moja, bali huanza na hatua moja mbele. Tumezipanga dondoo hizi katika makundi matatu: suluhisho la muda mfupi, maboresho ya kati, na kitu kikubwa. Tunakutia moyo kufikiria kutekeleza “suluhisho la muda mfupi.” Kama itafanikiwa, songa mbele kwa maboresho makubwa zaidi. Baada ya muda mfupi utakuwa na vipindi vya redio vilivyoboreshwa – makini zaidi na zinazofurahisha zaidi – lakini pia zinazofanya ufurahie kazi yako!

Kwa kifurushi hiki, tumechagua njia zetu “kubwa za juu zaidi,” pamoja na chache kutoka katika kila kipengele cha waraka asilia. Kwa waraka mzima, nenda http://www.farmradio.org/broadcaster-resources/special-resources/.

Maelezo juu ya kichwa: tutafurahi endapo“Njia sabini na tano za kuandaa kipindi chako cha mkulima” inakuwa “Njia tisini na tisa za kuandaa kipindi chako cha mkulima”! Lakini hiyo inategemeana na wewe. Wasiliana nasi na tuambie mawazo yako ili kuboresha vipindi vyako vya mkulima, na vitu vya kuepuka. Tutamtaja kila mtu ambaye atatoa mapendekezo tutakayoyatumia katika toleo lijalo. Wasiliana nasi kwa barua pepe info@farmradio.org na andika “Sabini na tano” katika mstari wa kichwa cha barua pepe.

Kila la heri kwenu nyote!

Script

Suluhisho la muda mfupi: Hivi ni vitu unavyoweza kuvifanya hivi sasa, wiki ijayo, na katika miezi inayokuja, bila nyenzo mpya na huwenda bila kuomba ruhusa kwa mtu yeyote yule.

Tanbihi: Tarakimu katika mabano hurejelea waraka asilia.

1. Andika utangulizi unaowavuta wasikilizaji kuendelea kusikiliza: Unatakiwa kupata utii wa wasikilizaji kwa kila kisa cha kipindi. Wasikilizaji watakupa dakika chache mwanzoni ili uwashawishi kwamba ni lazima waendelee kusikiliza. Kwa sababu hiyo utangulizi wako lazima uwe moja ya vitu unavyoviandaa ulivyovifikiria kwa makini. Na usitoe tu orodha ya vitu vya kununua. Gusa udadisi na matamanio binafsi ya msikilizaji. Mpe msikilizaji sababu inayogusa hisia zake kusikiliza. Kwa mfano, usiseme tu “tutazungumza na mtaalam katika ugonjwa wa x,” bali sema “Mbuzi wa Betty Mumo wanakufa kutokana na ugonjwa x. Tutazungumza na mtaalam wa mifugo ambaye atakueleza namna ya kufanya ili hili lisitokee katika mifugo yako.”

2. Warejelee wageni wanawake kwa hadhi sawa kama wanaume: (7) Hivi ni kwa nini mtangazaji aseme “Ninazungumza na Dkt. Stanley Lubo wa chuo cha kilimo,” lakini anapokwenda shambani anasema “Habari mama?” Kwanini asiseme “Ninazungumza na mkulima Maria Smith katika kijiji cha Luganda?” “Na kwa nini aseme ninazungumza na mwanamke mrembo katika soko la Zomba?” Wakati hata hakuweza kufikiria kusema “Ninazungumza na mwanaume mtanashati sana katika soko la Zomba?”

3. Yapambe maneno yanayojenga taswira: (26) Unapokwenda kijijini kuzungumza juu ya ugonjwa wa mahindi, awali ya yote, unatakiwa uwe macho ya msikilizaji. Fafanua “picha kubwa” unapokuwa unaingia kijijini – watoto wanacheza, wazee wamekaa nje, na kitu chochote kinachokitofautisha kijiji hiki husika – jengo, mto, duka, hekalu. Kisha “ikuze” na pamba maneno yanayojenga taswira ya shamba husika, mkulima na mahindi yaliyoathirika. Hii inawafanya waskilizaji wako wawe pamoja nawe na huamsha shauku yao.

4. Hadithi, hadithi, hadithi: (29) Kila mtu anapenda hadithi, na redio ina kuwa bora zaidi inapokuwa inazisimulia. Hadithi huwa inahusisha mtu wa kuvutia ambaye anakabiliana na tatizo na hatimaye Jifunze namna ya kutumia hadithi kuteka na kuwashikilia wasikilizaji wako. Hadithi zinaweza kuwa “za kweli” kama katika habari ya mtoa habari au zinaweza kuwa ni za “uwakilisho” kama katika nusu – drama. Zote hufanya vizuri.

5. Tumia njia nyingine za mawasiliano: (44) Redio inaweza kufanya vingi lakini haiwezi kufanya kila kitu! Kama suala la kilimo linaweza kuwasilishwa vizuri kupitia picha pekee, tafuta namna ya kupata picha kwa ajili ya kuwapa wakulima. Picha hizi huweza kutumika kama marejeleo kwa wakulima wakati wote, tofauti na kipindi cha redio, ambacho hurushwa hewani mara moja au mara mbili. Pengine Idara ya Uenezi huweza kutoa picha kwa ajili ya shule kuwapa wanafunzi ili wazipeleke nyumbani. Pengine picha zinaweza kuwekwa sokoni, na programu yako inaweza kuwaongoza watu kwenda kwenye picha hizo. Pengine kituo chako kina maktaba ambayo wakulima wanaweza kuitembelea ili kuangalia picha za kazi za kilimo ulizozizungumzia redioni.

Maboresho ya kati: Mabadiliko haya huenda yakawa yanahitaji nyenzo mpya na uhusikaji wa uongozi wa kituo. Fikiria kuyatekeleza katika miezi michache ijayo.

6. Toka nenda kwa wakulima vijijini mwao: (46) Vipindi vingi sana vya mkulima ni vya studioni na husumbuliwa na hilo tatizo. Simu za mkononi huweza kuwa daraja kati ya mkulima na mtangazaji, lakini hiyo haitoshi. Usafiri ni gharama, lakini ni lazima uende katika mashamba ya wakulima. Wakulima watakuheshimu sana kama watajua umeona upepo unapeperusha udongo mkavu, umesubiri kivuko kwa muda mrefu, umekwama kwenye tope barabarani wakati unakwenda sokoni, na umesikia kilio cha mbuzi mgonjwa. Inawezekana ukawa huwezi kusafiri kila wiki, lakini huenda watangazaji wengine wanaweza – kwa mfano waandishi na wafanyakazi wa uenezi kwa hakika. Tulipokuwa tukitathimini vipindi ishirini na mbili katika utafiti wa ARRPA, tulibaini kwamba vipindi vilivyotembelea mashamba vilikuwa na ubora wa juu kuliko vile ambavyo havikutembelea. Tafuta nyenzo ya kukufikisha hapo. Na kwa wakati huohuo tembelea soko lililopo karibu nawe na wahoji wakulima.

7. Mpango, mpango, mpango: (49) Kipindi cha mkulima lazima kisikike kama kimeanza chenyewe na chenye kuburudisha. Lakini nyuma ya utulivu huo, usikivu usio rasmi, lazima kuwe na mpango makini. Je, tukio hili litatimiza kusudi lako la jumla la kipindi chako cha mkulima? Je, litapeleka mbele mjadala na utatuzi wa suala lililokita mizizi? Je, linahusisha wakulima wakijadili masuala muhimu ya kilimo? Je, ripoti yetu ya masoko hujumuisha soko ambalo wakulima wanatumia? Haya ni maswali ambayo mwandaaji wa kipindi anapaswa kujiuliza kila wiki, alafu ni lazima afanye kazi inayotakiwa kuwasilisha maudhui – na fanya yasikike hewani kana kwamba jitihada kubwa haikufanyika.

Kitu kikubwa: Mabadiliko haya yatachukua muda lakini yanafaa sana! Yatahitaji kupanga na uhusikaji wa uongozi wa kituo – na pengine baadhi ya nyezo za kutumia mara moja au hata nyongeza ya zinaoendelea. Lenga kutimiza zile unazoona ni muhimu kwako kwa kipindi cha miezi mitatu au kumi na mbili ijayo.

8. Unda kauli ya jumla inayoonesha kusudi: (58) Kituo kinapoamua kufanya kipindi cha mkulima, mara nyingi kazi hiyo hupewa mwandaaji wa kipindi na ni juu yake kuamua nini cha kufanya. Hiyo sio haki kwa mwandaaji au kwa wasikilizaji! Shirikiana na meneja wako kuunda kauli ya jumla inayoonesha kusudi iliyo wazi na yenye manufaa. Mfano mzuri huu hapa:
“Wakulima Kwanza” husaidia wakulima wa mkoa wa Tembe kupanda chakula kinachofaa kwa ajili ya familia yao na kuuza na kujenga jumuiya ya wanakijijini inayoeandelea. “Wakulima Kwanza” ni kipindi cha kila wiki kinachoburudisha, kinachotoa taarifa wanazohitaji wakulima na wakati wanapozihitaji kutoka katika vyanzo vya kuaminika. Pia kinatoa fursa kwa wakulima kujadili masuala ambayo yana umuhimu kwao.

9. Fanya ubia na watoa huduma za uenezi: (59) Redio kwa kiwango kikubwa huwa hudumia wakulima kutoka katika kituo maalum. Mawakala wa uenezi mara kwa mara husafiri kwenda vijijini. Wote wanaweza kuboresha huduma zao endapo watafanya kazi pamoja. (Hili huenda litahitaji mkataba rasmi au MOU inayoonyesha nani anafanya nini).

10. Watafute wakulima wajadili masuala muhimu hewani: (63) Hakutakuwa na maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika eneo lako kama wakulima hawatakuwa sehemu ya mjadala huo wa maendeleo. Kipindi chako kinaweza kutoa “nafasi” nzuri ambapo majadiliano hayo huweza kuanza, na ambapo yanaweza kujadiliwa kwa kina na ambapo yanaweza kujumuisha wakulima wengi na wengi zaidi wa jinsi zote.

Mwisho, vitu vichache vya kuepuka!

Kupitia matokeo ya utafiti wa ARRPA (na vipindi vingine vya vituo vya nje), tumekuja na baadhi ya desturi za redio ambazo tunadhani hazina nafasi katika kipindi cha mkulima. Desturi hizo ni hizi hapa. Kuonywa mapena ni kuchukua hatua mapema!

11. Kamwe usizungumze na wakulima kwa dharau: (69) Tumesikiliza vipindi ambapo waandaaji wanawachukulia wakulima kama watoto wenye utovu wa nidhamu. Tumesikia wafanyakazi wa uenezi wanawalaumu wakulima kwa kutotekeleza njia mpya wanazohamasisha. Tumewasikia waandaaji ambao wanaongeza chumvi kwa kuwasifia wakulima na kufanya ionekane ni uongo na bandia. Wakati mwingine watangazaji wanahisi kwamba wako “juu” ya wakulima, na kwa hiyo kwa kutambua ama kwa kutotambua wanazungumza nao kwa “dharau.” Watangazaji wazuri wa kipindi cha mkulima wanatambua kwamba wakulima hufanya kazi kwa muda mrefu na kwa bidii ili kuboresha afya za familia zao. Watangazaji hawa wanatambua kwamba wana jukumu kubwa kutumia redio ili kuwahudumia wakulima, na kufanya hivyo kwa heshima.

12. Usirundike! (75) Baadhi ya watangazaji wanafikiri kuwa vipindi vyao ni kama toroli: kadri wapakiavyo ndivyo inavyokuwa bora zaidi. Si kweli! Kipindi ni uhusiano wa sauti kati ya mtangazaji na msikilizaji. Wasikilizaji hawamotishwi na mzigo wa taarifa uliowatupia. Wanamotishwa wanapokuwa wamevutwa na kuongozwa katika taarifa kwa kipimo na ujazo wanaoweza kuelewa. Kama unarundika taarifa na kuwa nyingi, wakulima wengi watajiona kama watu wasioweza, (ingawa sio kosa lao), na wataondoka.

Acknowledgements

Kimeandalia na: Marvin Hanke (Blantyre, Malawi) na Doug Ward (Ottawa, Canada)

Kuhusu watunzi

Marvin Hanke, alifanya kazi katika Shirika la Utangazaji la Malawi kama mwandaaji wa vipindi kwa muda wa miaka 24 (1975 – 1999) na alijulikana sana kwa uandaaji wa mchezo wa redio ulioshinda tuzo ujulikanao kama “Theatre of the Air.” Mwaka 1999 alianzisha “Story Workshop,” akiwa na Pamela Brooke, ni shirika lisilo la kiserikali linalojihusha na maendeleo ya vyombo vya habari msisitizo ukiwa katika mawasiliano ya redio, ambapo ailfanya kazi kama Mkurugenzi wa vyombo vya habari na baadae Mkurugenzi Mtendaji. Uandaaji wake wa kipindi kizuri cha redio kinachoitwa Zimachikita kilishinda tuzo ya Jumuiya ya Madola juu ya hatua dhidi ya VVU na UKIMWI. Alikuwa ni mtayarishaji mkuu wa vipindi viwili vya redio vya maendeleo ya vijijini (ni drama ya mfululizo iliyokuwa inahusu njia bora za kilimo na programu ya gazeti iliyokuwa inahusu usalama wa chakula ambazo ziliendeshwa kwa miaka sita). Alistaafu kwa hiyari mwaka 2008 na sasa anaendesha kampuni yake binafsi ya kurekodi, anarekodi na kutoa ushauri juu ya ujuzi wa uandaaji wa vipindi vya redio. Anakalia nafasi ya Makamu Mwenekiti na Mwenyekiti wa Kamati ya Vipindi katika Bodi ya Farm Radio Malawi. Unaweza kuwasiliana naye kupitia marvinhanke54@yahoo.com.

Doug Ward, ni Mwenyekiti wa Farm Radio International. Kama Makamu wa Rais wa Shirika la Utangazaji la Kanada Doug alisimamia vituo vya uzalishaji zaidi ya sabini vya redio na Televisheni vya Shirika la utangazaji la Kanada. Mwanzoni, Doug alikuwa Mkurugenzi wa CBC eneo la Kaskazini, akiandaa vipindi vya redio katika lugha tisa, kwa ajili ya wazawa wa Kanada ya kaskazini. Alikuwa Mwandaaji Mkuu katika timu iliyounda kama kilivyotokea kipindi maarufu cha redio cha kupiga simu cha CBC – sasa kikiwa katika mwaka wake wa arobaini na tatu. Katika Farm Redio International, Doug alibuni njia ya Kampeni Shirikshi ya Redio (PRC), ambayo ilisaidia kuhamasisha wakulima wadogowadogo kutumia njia bora za kilimo wanazoona ni muhimu kwa ajili ya usalama wa chakula wa familia. Doug pia ni Jaji wa umma katika Baraza la Viwango vya Utangazaji la Kanada, ambalo ndilo hushugulikia malalamiko yote ya matangazo ya kibiashara nchini Kanada.

gac-logoMradi umefanywa kwa msaada wa Serikali ya Kanada kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Kanada (CIDA)