Jumuiya zinazoishi karibu na misitu zinajipatia kipato huku zikitunza mazingira

Ujumbe kwa mtangazaji

Idadi ya wanyama na mimea mingi ya porini inazidi kupungua. Kwa mfano inakadiriwa, kulikuwa na tembo Milioni tano barani Afrika katika miaka ya 1930 na 1940. Hivi sasa idadi yao ni chini ya Laki tano. Hapo awali, biashara haramu ya pembe za ndovu, ilikuwa ni tishio kubwa kwa wanyama hawa. Lakini tangu mwaka 1989 biashara hii ilipopigwa marufuku, tatizo sasa limekuwa kwa binadamu, wanaoendelea kupanua makazi yao na kilimo hadi katika makazi ya wanyama. Jamii nyingine ya wanyama inashambuliwa na watu wanaotafuta vitoweo porini.

Baadhi ya jamii zinakabiliwa na uharibifu wa mazao na wakati mwingine watu kupoteza maisha kutokana na wanyama waharibifu. Hali hii imesababishwa na binadamu anayepanua makazi yake hadi katika makazi ya wanyama wa mwituni. Hata hivyo wanavijiji ni lazima wajitafutie chakula na kujiingizia kipato. Ni kwa vipi wanyama wa porini na binadamu wanaweza kuishi pamoja kwa amani?

Katika matukio mengi, mashirika yasiyo ya kiserikali yanafanya kazi na jamii mbalimbali kutafuta njia madhubuti za kuishi karibu na wanyama, lakini wakati huo huo jamii hizi zilikilinda mazingira ya asili. Wakati mwingine, jamii hizi zimepata njia ya kulinda mazingira, huku zikitarazaki na kujipatia chakula.

Muswada huu ni wa mradi ulioko Kusini magharibi mwa Cameroon. Shirika kubwa lisilo la kiserikali la – World Wide Fund for Nature (WWF) – linazisaidia jumuiya zinazoishi karibu na misitu vikundi vidogo vya kibiashara kujipatia kipato kwa kutumia aina mbalimbali za wanyama wa msituni bila kuharibu misitu. Kama utatafiti kwa uangalia katika maeneo unayoishi, huenda ukabaini miradi kama ile inayoendesha na asasi hii ya WWF.

Muswada huu ni kuhusiana na mahojiano ya kweli. Unaweza kutumia muswada huu kukuhamasisha kufanya utafiti katika eneo lako kutokana na mada inayofanana na hii. Au unaweza kuutumia muswada huu katika kituo chako cha redio, kwa kutumia sauti za waigizaji kuwawakilisha wazungumzaji katika muswada. Endapo utaamua kufanya hivyo, tafadhali wafahamishe wasikilizaji mwanzo wa kipindi kuwa sauti zinazosikika ni za waigizaji na wala sio wahusika halisi.

Script

Mtangazaji:
Habari za asubuhi msikilizaji. Je, unahabari kuwa unaweza kusaidia kulinda mazingira? Vizuri, kipindi cha leo kitakusaidia kuelewa ni kwa vipi unaweza kutunza vitu vya asili. Kipindi hiki ni kuhusu uzoefu wa wanavijiji watatu katika eneo moja la misitu lililoko Kusini Magharibi mwa nchi ya Cameroon, na jinsi walivyosaidiwa na shirika moja lisolo la kiserikali la World Wild Fund for Nature or WWF, linalojihusisha na uhifadhi wa wanyama pori na mimea.

Muziki

Mtangazaji:
Mahali popote pale ambapo watu wanaishi, wanakuwa wakitegemea mazingira yaliyo karibu kwa ajili ya uzalishaji wa chakula na kujipatia kipato. Katika maeneo yenye misitu, watu hukata miti, ili wapate mbao au miti kwa matumizi mbalimbali, au kwa ajili ya uvunaji wa asali. Watu hawa wanawinda wanyama kwa ajili ya chakula na biashara. Mazao ya misitu ni maarufu sana. Lakini, hata kama ikiwa ni kwa matumizi ya mimea yenye tiba au wanyama, mara nyingi watu wanawaangamiza wanyama na mimea ya msituni ili kujipatia kipato na kukidhi mahitaji yao ya kila siku.

Uharibifu wa misitu umekuwa na athari nyingi mbaya, athari hizo ni za mazingira moja kwa moja au ardhi kwa ujumla. Kwa mfano, uharibifu wa misitu unachangia ongezeko la joto ambalo linaambatana na mabadiliko ya tabia nchi. Uharibifu wa misitu pia unasababisha vifo vya aina mbalimbali za wanyama na mimea.

Asasi nyingi zinafanya kazi ya kutunza misitu. Moja kati ya hizo ni World Wide Fund for Nature au WWF, ambayo ni asasi ya kimataifa iliyoanzishwa mwaka 1961. Lengo la asasi hii ni kudhibiti uharibifu wa mazingira ya asili na kujenga mazingira ya baadaye ambapo binadamu anaishi kwa amani na mazingira kwa kulinda maisha ya viumbe mbalimbali vya dunia, kupunguza uchafuzi wa hali ya hewa na taka, na kuhakikisha anatumia rasilimali za asili zilizoendelevu.

WWF imekuwa kifanya kazi nchini Cameroon tangu mwaka 1989 na kufanikiwa kuendesha programu nne, ikiwa ni pamoja na programu ya WWF ya misitu katika ukanda wa pwani huko kusini magharibi na mikoa iliyoko karibu na pwani huko Cameroon. Mahojiano utakayoyasikia hivi sasa yalifanyika katika moja kati ya programu hizo iliyoko katika kata ya Kupe Muanenguba katika mkoa wa Magharibi mwa Cameroon. Eneo hili ni moja kati maeneo yenye baianuai yenye joto huko kusini Magharibi ambapo WWF inafanya kazi, eneo la Kupe Muanenguba ambalo ni eneo maalum lililochaguliwa.

Sauti ya msituni – ndege wakiimba na sauti za wanyama wengine

Mtangazaji:
Kupe ni eneo la milima lenye urefu wa mita 2,000 kutoka usawa wa bahari. Sehemu kubwa ya milima hii ni misitu, na misitu yake ni moja kati ya misitu ya siku nyingi sana barani Afrika. Katika msitu huu kuna mimea inayopatikana eneo hilo tu duniani, kuna wanyama wengine wengi walioko katika hatari ya kupotea duniani, pamoja na mimea mingine: wanyama jamii ya mamalia wanaopenda kufukua chini kama kinyonga, na zaidi ya aina 300 za ndege.

WWF imekuwa ikifanya kazi tangu mwaka 1990 huku ikikabiliwa na tishio la uharibifu wa mazingira katika eneo hilo. WWF inaridhia na kuimarisha kazi zilizoanzishwa na mashirika mengine kama vile shirika la kimataifa linalojishughulisha na maisha ya ndege na wizara ya Misitu na wanayamapori ya Cameroon iliyoandaa kampeni maalum ya kuwasisitiza watu kutowaua wanyama walioko katika hatari ya kutoweka duniani au kukata miti kinyume cha sheria msituni.

WWF inafanya kazi na jamii mbalimbali zinazoishi katika bara hili. Inaelimisha na kutoa mafunzo kwa jamii hizi jinsi ya kujipatia kipato bila kuharibu misitu, inazipatia jamii hizi misaada, nyenzo na mafunzo ya kuendesha shughuli zake na kuzitafutia wanunuzi kwa ajili ya bidhaa zinazozalishwa na jamii hizi. Kwa njia hii, WWF inasaidia kupunguza umaskini katika jamii hizi na kuzisaidia kuendeleza usimamizi endelevu wa misitu.

Hapa kuna habari za Ngol’epie, Pa Atabe, na Mbonteh, watu watatu kutoka kata ya Kupe Muanenguba ambao wataisaidia WWF, katika kuimarisha udhibiti wa misitu.

Muziki
Mtangazaji:
Kwanza tutamsikiliza Ngol’epie, anayeishi katika kijiji kijiji kidogo cha Nyasoso, kilichoko karibu na msitu wa Kupe.

Mtangazaji:
Habari gani Bwana. Ngol’epie, hujambo?

Ngol’epie:
Nzuri. Sijambo.

Mtangazaji:
Unaweza kuwaeleza wasikilizaji, kwa nini umeamua kubadilisha kazi,kutoka kwenye uwindaji na sasa umekuwa mkulima?

Ngol’epie:
Bila ya shaka. Naishi huko Nyasoso na familia yangu. Kama mwindaji, nawajibika kwenda msituni kila siku kuwinda wanyama ili niwauze, na kuvuna magome ya miti kwa ajili ya matumizi ya dawa za asili.

Nimekuwa pia nikifanya kazi kama msimamizi katika shirika moja lisilo la kiserikali, ambalo linafanya shughuli zake msituni. Lakini kutokana na uhusiano nilionao na WWF, nimegundua kuwa shughuli zangu za uwindaji, zimekuwa zikichangia katika kuteketeza misitu.

Siku moja, nilipokuwa msituni, nikitafuta mimea kwa ajili ya dawa, nilimuona panya akitokea kwenye shimo. Nikamkamata, kwa msaada wa mbwa wangu, aliyefukua zaidi shimo alimokuwa amejificha. Ndani ya lile shimo nilikamata panya wengi zaidi waliokuwa wamejificha na kuwatia katika mfuko wangu. Nikiwa na mke wangu, tulijaribu kuwafuga hawa panya. Kwanza, nilitengeneza kitundu cha mbao cha kuwahifadhia, lakini kwa bahati mbaya panya hawa walikitafuna chote. Lakini nashukuru kwa ushauri na msaada kutoka WWF, nitatengeneza kidundu kingine na kuendelea kufuga panya. Niliwalisha samaki wakavu, ndizi, viazi, karanga, majani ya porini kama vile sissongo au mabingubingu, pamoja na majani ya viazi mbatata au mviringo.

Ili kunihamasisha, WWF ilininunulia riksho au kitita cha majani maalum ya mifugo yaliyonisaidia kuwalisha panya. WWF inanipa ushauri endelevu unaonisaidia kupunguza msongo wa kufikiria kutarazaki kupitia wanyama wa msituni au mazao ya misitu kwa ujumla.

Baada ya mwaka mmoja wa kuwafuga panya, sasa wamekomaa na ninafurahi kusema kuwa naweza kuwauza na kujipatia faida kubwa.

Kutokana na hili, nashawishika kwamba ufugaji utanisaidia kujipatia kipato. Pesa za mauzo ya kwanza niliyopata nilitumia kununua nguruwe.

Mtangazaji:
Bwana Ngol’epie, ni kitu gani ulichofanya ili wengine pia wafaidike na uzoefu wako?

Ngol’epie:
Kutokana na ushauri niliopata kutoka WWF, nilitengeneza kikundi cha watu saba ambao kwa pamoja tulishiriki kufuga. Kikundi hicho kinajulikana kama Bakossi kwa kikwetu kinaitwa “Dion de Dienge.” Biashara hii ina faida kubwa kiasi kwamba hivi sasa tunajenga kitundu kikubwa cha mabati kufugia mifugo yetu. Sasa nimetambua kuwa naweza kuishi karibu na msitu na nikajipatia fedha bila kuua wanyama ndani ya msitu.

Mtangazaji:
Asante Bwana Ngol’epie.

Muziki

Mtangazaji:
Baada ya kusikiliza uzoefu wa Bwana Ngol’epie, hebu sasa tumsikilize Pa Atabe. Ni mfanyakazi mstaafu wa umma anayeishi huko Tombel, kijiji ambacho kinapakana na msitu wa Kupe. Anajishirikisha na uvunaji wa asali.

Asali ya msituni ina radha ya peke yake na inauzwa kwa bei kubwa sana mijini. Ili kuvuna asali ya porini, watu hulazimika kukata miti yenye mizinga ya nyuki ili kuvuna asali hali inayosababisha uharibifu wa miti.

Hebu tusikilize uzoefu wa Pa Atabe’s.

Mtangazaji:
Habari, Pa Atabe.

Pa Atabe:
Nzuri, hamjambo wasikilizaji?

Mtangazaji:
Unaweza kutueleza kuhusu uzoefu wako wa kurina asali na WWF?

Pa Atabe:
Asante! Kwa msaada wa WWF, nimehudhuria mafunzo ya kurina asali nchini UINGEREZA na Cameroon. Hapa Tombel, nitawafundisha wengine na kwa pamoja tutaanzisha kikundi cha uhamasishaji. Kitaitwa jumuiya ya warina asali wa Tombel-Bangem. Kwa msaada wa WWF, tutajifunza kutengeneza mizinga ya nyuki ya mbao na tutapatiwa nguo za kujikinga, meza, chupa, nta, nguo za kujaza ndani ya mizinga na sehemu ya kukuzia nyuki.

Kuwavuta nyuki mwezi Julai, Agosti na Septemba, wanachama wa jumuiya hiyo wanachoma masega ya asali kwa moto ili wapate kuingia kwenye mizinga na kurina asali. Harufu ya moshi wa masega ya asali yanayoungua inawavutia nyuki. Pia tutapanda miti aina ya Cariandra karibu na sehemu za kukuzia nyuki ambapo pia itakuwa karibu na mizinga ya nyuki. Hii ni kwa sababu miti hii ya Cariandra inapendwa sana na nyuki. Mara nyuki watavutiwa kuja kwenye miti hii ya caliandra, na yumkini wataanza kutengeneza makazi yao katika mizinga ya nyuki. Miezi kadhaa baadaye – katika mwezi Machi, April na Mei – asali huvunwa na kila mwanachama huleta mavuno katika makao makuu ya jumuiya yetu. Mauzo ni ya kudumu na wale wanunuzi wa ndani ya eneo letu ikiwa ni pamoja na wanunuzi kutoka miji jirani watakuja kununua asali.

Mtangazaji:
Ni faida gani unazoweza kupata kwa kurina asali?

Pa Atabe:
Kuna faida mbalimbali. Kwanza jumuiya yetu inazalisha lita 2,000 za asali kwa mwaka, ambazo hutuingizia takribani dola 9,000 za Marekani. Mapato ya jumuiya yetu yameongezeka na tunatoa ajira kwa vijana. Shinikizo la kutumia msitu kukata miti ili turine asali limekwisha.
Mtangazaji:
Mwishowe, ni habari za Mbonteh, anayeishi huko Tombel.

Mtangazaji:
Habari Bwana Mbonteh. Unajisikiaje leo?

Mbonteh:
Nzuri. Mi mzima.

Mtangazaji:
Unawajibika na jumuiya inayotoa mchango wake katika uhifadhi wa msitu kwa ufugaji wa konokono. Nyama ya konokono inauzwa kwa bei kubwa katika maeneo ya mijini. Tuambie kuhusu uzoefu wako.

Mbonteh:
Watu wa Bakossi wanaoishi katika maeneo mengine ya misitu wanawinda konokono msituni. Halafu wanauza hao konokono. Lakini walikuwa wakiangamiza jamii nyingine za viumbe msituni. Kwa mfano, kama sungura atapita katika maeneo yao wa uwindaji, basi watampiga risasi. Ingawa watu hawa wa Bakossi walikuwa wakienda porini kuokota konokono, endapo wakikutana na wanyama wengine wadogo, basi hao nao huchukuliwa.

Kutokana na kampeni iliyoandaliwa na WWF mwaka 2001, ikishirikiana na mradi wa mlima KUPE, mimi na wakulima wenzangu tulihamasika kufuga konokono nyumbani.
WWF ilisaidia kutuunganisha katika vikundi ili tuweze kufuga konokono. Hivyo ndivyo kikundi cha Jumuiya ya utekelezaji wa maendeleo kilivyoanzishwa. WWF ilitupatia mafunzo ya uongozi na kuandika usanifu wa mradi.

Ufugaji wa konokono ni kazi inayotaka uangalifu mkubwa. Inachukua kati ya miezi mitatu hadi minne tangu mayai ya konokono yanapoanguliwa hadi kutotolewa. Wafuga konokono wanalazimika kubadilisha vizimba vya konokono mara tatu katika kipindi hiki. Vizimba hivi ni lazima viangaliwe na kuratibiwa kwa uangalifu ili kudhibiti unyevu na hewa inayoingia ndani. Chakula cha konokono kinatengenezwa kutokana na mapapai, mapapai, baadhi ya mboga za majani na ndizi.

Kwa kupitia hatua hizi, WWF ilikisaidia kikundi kwa vifaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na ushauri na mafunzo yaliyoendeshwa nchini Cameroon na katika maeneo mengine. Nilipata bahati ya kushiriki katika mafunzo nchini Nigeria, Chile na Afrika Kusini. WWF inakisaidia kikundi chetu kusafirisha konokono hadi katika maduka ya jumla na hata kufanya makubaliano ya kibiashara ya kimataifa na kupata thamani ya nyama ya konokono. Nchi zinazoagiza kwa wingi bidhaa hii ni Nigeria na Italia.
Ushirikiano kati yetu na WWF kwa hakika umeongeza kipato cha wanachama wetu. Biashara ya kikundi chetu kwa mwezi inakiletea kikundi faida ya Dola za Marekani 210. Kutokana na mafunzo hayo nilikuwa mtaalamu na nikaweza kuwafundisha wanachama wengine katika kikundi chetu. Familia kadhaa zinafuga konokono na zimeweza kuinua kipato cha familia na maisha kwa ujumla. Kwa vile konokono hawavunwi tena msituni, na badala yake wanapatikana katika mashamba ya kufugia konokono, shinikizo la kwenda kutarazaki msituni limepungua.

Muziki

Mtangazaji:
Mpendwa msikilizaji, mwisho, kwa kuzisaidia jamii mbalimbali kuwa na usimamizi endelevu wa mali asili katika mikoa ya Kusini magharibi mwa Cameroon, WWF imeweza kuzisaidia jumuiya zipatazo 33 zinazojishughulisha na shughuli mbalimbali za kijipatia kipato kama vile ufugaji wa nyuki, ufugaji wa konokono, ufugaji wa nguruwe, ufugaji wa panya na panya buku. Vikundi hivi vimekuwa vikiendelea na shughuli zao bila kuharibu mazingira na kuinua maisha ya wanavikundi.

Acknowledgements

Washiriki: Serge Kuate, PROTEGE QV, Cameroon,mshirika wa redio ya kimataifa ya Farm.
Imepitiwa na: Janet Molisa, Afisa mawasiliano, WWF mpango wa misitu ya pwani, Cameroon na Peter Ngea, Meneja wa mawasiliano, WWF ofisi ya kanda ya Africa ya Kati (CARPO), Yaounde, Cameroon.
Shukrani pia zimwendee Ngwene Theophilus, Afisa wa mambo ya uchumi jamii, WWF mpango wa misitu ya pwani, Cameroon; Dokta. Atanga Ekobo, mratibu wa mpango, WWF mpango wa misitu ya pwani Cameroon; na Sylvie Siyam, Rais wa PROTEGE QV.

Information sources

Mahojiano haya yalifanyika Februari 11, 2009.