Dhuluma dhidi ya wanawake na HIV/UKIMWI

Ujumbe kwa mtangazaji

Dhuluma dhidi ya wanawake inajumuisha ubakaji na ngono ya kulazimishwa, kunyanyaswa kimwili au kimapenzi, na pia mila zenye madhara kama vile ukeketaji wa wanawake na ndoa za mapema. Aina hizi za dhuluma huongeza hatari ya wanawake kupata maambukizi ya HIV ama moja kwa moja kupitia ngono ya kulazimishwa au kwa njia nyinginezo, kwa kuwatia woga jambo ambalo hupunguza uwezo wa wanawake kujadili jinsi ngono inavyofanyika na matumizi ya mipira. Dhuluma ina athari hasi kimwili, kisaikolojia na maendeleo ya kijamii.

Wanawake wengi huripoti tajriba za dhuluma baada ya kutangazwa hali zao za HIV, au hata kufuatia kukiri kuwa upimwaji wa HIV umetafutwa. Dhuluma hii inaweza kutatiza uwezo wa mwanamke kufikia matibabu na huduma au kufuatilia matibabu madawa ya kupunguza makali ya ukimwi (ARV). Baadhi ya wanaume wengine hata hutumia madawa ya ARV ya wenzao.

Dhuluma dhidi ya wanawake inatokea sana katika nchi zinazoendelea na zilizoendelea. Katika maeneo mengi, takriban asilimia 50% ya wanawake wanaripoti kuwa wahathiriwa wa dhuluma.

Kama makala haya yanavyoonyesha, kuna uhusiano wa karibu kati ya dhuluma dhidi ya wanawake na ukosefu wa heshima kwa haki za wanawake kama vile haki ya elimu, haki ya kujieleza, na haki ya uhuru wa kutembea. Dhuluma dhidi ya wanawake inachochewa na kushikiliwa kwa maadili yanayokataa kuwapa wanawake haki hizi.

Ili kuweza kuitayarisha makala haya kwa hadhira ya eneo lako, unaweza kutaka kuwahoji wawakilishi wa vikundi vya mitaani au kitaifa hewani, na labda uongeze sehemu ya kupigiwa simu katika kipindi hiki. Mnamo mwaka 1999, shirika la Umoja wa Mataifa liliitaja Novemba 25 kuwa Siku ya Kimataifa ya Kumaliza Dhuluma Dhidi ya Wanawake. Unaweza ukataka kuwa na msululu wa vipindi unaohusiana na tukio hili.

Script

Dominic Mutua Maweu:
Hujambo msikilizaji mpendwa. Hii ni Radio Mang’elete FM hapa katikati mwa Kenya, na jina langu ni Dominic Mutua Maweu. Leo, nakuletea kipindi cha Imanyiliile ambacho nina uhakika kuwa kimekuwa cha manufaa makubwa kwako na unakipenda! Katika lugha ya kikamba, ‘imanyiliile’humaanisha “Chunga. Kuna hatari!”

Leo hii ningependa tuangazie jinsi dhuluma dhidi ya wanawake inavyoweza kuchochea kusambaa kwa HIV na UKIMWI. Tunapoongea kuhusu dhuluma dhidi ya wanawake, tunamaanisha vita, ubakaji/najisi na uvujaji wa haki za wanawake. Na tunapozungumzia haki za wanawake, tunamaanisha kuwanyima wanawake haki ya kuelimishwa katika wakati unaofaa, na haki ya wanawake kujieleza na kutoa maoni yao juu ya jambo lo lote linalowahusu wao wenyewe, jamii yao na nchi yao.

Mpenzi msikilizaji, unajua kuwa kifaa bora katika vita dhidi ya kirusi hiki ni mapenzi. Wanaume! Kama kweli tunawapenda wanawake wetu, ambao wanajumuisha dada zetu na mama zetu, huoni kuwa tutakoma kuwapiga manyumbani mwetu, kazini na katika masoko yetu? Je, hufikiri kuwa tutaacha kuwabaka na kuwanyima haki zao?

(Sita) Ningependa usikilize hotuba kutoka kwa Rhoda Maende, mwanamke kutoka wilaya yetu ambaye ni mtoaji wa ushauri nasaha na kiongozi wa shirika la wanawake linalojulikana kama Makueni Women’s Regional Assembly. Katika hotuba hii, anawahutubia watu wa Wilaya ya Makueni mjini Makindu ambapo walikuwa wamekusanyika kusherehekea Siku ya Dunia Kuhusu UKIMWI mnamo Januari 12, 2005.

Sauti za umati zinazofifia, na kasha kusikika chini kwa chini kwa muda wote wa hotuba yake.

Rhoda Maende:
Hamjambo, Hamjambo tena? Jina langu ni Rhoda Maende kutoka Makueni. Mimi nafanya kazi na shirika linalojulikana kama Makueni Women’s Regional Assembly. Mojawapo ya majukumu yangu muhimu ni kuhakikisha kuwa wanawake wanapewa haki zao, kwamba watoto wanapewa haki zao, na kwamba wanaume wanapewa heshima. Leo, ningependa kuzungumza kidogo kuhusu kirusi hiki cha mkurupuko cha UKIMWI. Ningependa kuongea kuhusu vile kilivyoshikamana na dhuluma dhidi ya wanawake ama aina yo yote ya unyanyasaji wa mwanamke awe ameolewa au hajaolewa. Vita katika maboma yetu na ubakaji wa wanawake wetu huchochea kuenea kwa kirusi hiki.

Dhuluma ya wanawake lazima ikome. Ama sivyo akina mama?

Kuna wanawake wanaofanya kazi katika baa zetu. Kazi ni kazi na mwanamke ana haki ya kufanya kazi mahali po pote. Ukweli kwamba anafanya kazi katika baa haumaanishi kuwa anaweza kudhulimiwa na mteja ye yote afikae pale. Na nikisikia visa vya wanaume wakiwadhulumu wanawake hawa ama kuwachukua kwa nguvu, nitawapeleka kortini na watafungwa. Hii ni kwa sababu hili ni kosa la jinai.

Kila mwanamke anapaswa kuheshimiwa katika jambo analolifanya. Ana haki ya kujitafutia riziki, kwani atakula nini kama hafanyi kazi? Tunasema kuwa dhuluma hii lazima ikome na kila mwanamke apewe heshima. Kama mwanamke anakubali kutembea na wewe, hiyo ni sawa! Lakini dhuluma hii lazima ikome.

Sauti za umati zififie kwa muda wa nukta tano, kisha uzime.

Dominic Mutua Maweu:
Natumai umesikia alivyosema kiongozi huyu. Lakini nigependa wewe ufikirie hivi. Uvujaji wa haki za wanawake, na hasa haki ya elimu, ndio mtuhumiwa mbaya zaidi katika kueneza virusi hivi. Hii ni kwa sababu ni kupitia masomo peke yake ambapo mtu hujua kuhusu virusi na athari zake. Na ni kwa kupitia kuwa na uhuru ambapo mwanamke anaweza kusema, “Nataka kutumia mpira” hata kama anaongea na bwana yake.

Katika kumalizia, hii hapa ni njia ambayo jamii inapaswa kushughulika kunapotokea dhuluma dhidi ya wanawake. Kwanza, jaribu kuchukua hatua ukiona vitendo ambavyo unaviona kuwa ni dhuluma. Pili, sikiliza na utende bila kulaumu watu walioathirika. Tatu, ambia watu wengine kuhusu dhuluma dhidi ya wanawake. Nne, kumbuka kuwa usiri ni muhimu sana unapoongea kuhusu dhuluma yo yote. Tano, panga mikutano ya jamii na polisi na serikali na usisitize kuhusu huduma bora kwa wanawake waliodhulumiwa. Na juu ya yote, unga mkono haki ya wanawake kuishi kwa usalama na uaminifu katika jamii yako.

Asante na naomba tukomee hapo kwa leo. Jina langu ni Dominic Mutua Maweu, na mimi ndiye mtayarishaji na mtangazaji wa kipindi hiki. Hadi wakati mwingine, kwaheri na chunga!

Acknowledgements

Imechangiwa na: Dominic M. Maweu, mtayarishaji na mtangazaji, Kipindi cha HIV/AIDS, Radio Mang’elete, Mtito Andei, Kenya.
Imehaririwa na: Rebecca Hodes, D.Phil mwanafunzi wa Historia ya Matibabu, Oxford University, lengo: HIV/UIMWI katika vyombo vya habari; na Mawethu Zita, Msimamizi na Mwelekezi wa Sanaa wa Driven Force, Na Mwanachama wa Timu, Ikhwezi Lokusa Wellness Centre, East London, South Africa

Information sources

Rosemarie Muganda, undated. Violence and the threat of HIV/AIDS. African Women and Child Feature Service. http://www.awcfs.org/new/features/health/hivaids/128-violence-and-the-threat-of-hivaids
Harvard School of Public Health, 2006. HIV/AIDS and Gender-Based Violence (GBV)
Literature Review. http://www.hsph.harvard.edu/pihhr/files/resources_and_publications/literature_reviews/Final_Literature_Review.pdf
UNAIDS, undated. Stop Violence Against Women – Fight AIDS.
http://data.unaids.org/Publications/IRC-pub07/jc1184-stopviolence_en.pdf Human Rights Watch, 2003. Policy Paralysis: A Call for Action on HIV/AIDS-Related Human Rights Abuses Against Women and Girls in Africa. http://www.hrw.org/reports/2003/africa1203/