Backgrounder
Save and edit this resource as a Word document
Utangulizi
Rwanda ni moja ya nchi ndogo kabisa barani Afrika ikiwa na zaidi ya kilomita za mraba 26,000. Kwa kulinganisha na nnchi ya jirani yake, Tanzania, ni kubwa mara 35. Rwanda inapakana na Uganda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na Tanzania. Nchi ina vilima na udongo wenye rutuba nyingi, na uchumi wake unategemea sana kilimo cha kujikimu. Inakadiriwa 90% ya idadi ya watu wanaofanya kazi wanahusika katika shughuli zinazohusiana na kilimo, na kilimo kilihesabu asilimia 42 ya pato la Taifa mnamo 2010 na asilimia 29 mnamo 2019.
Mauaji ya kimbari ya mwaka1994 dhidi ya Watutsi yalifanya nchi hiyo kuwa na mkwamo wa kimaendeleo, na hakuna mtu aliyetarajia muujiza kutoka kwa nchi hii isiyo na bandari. Lakini tangu wakati huo, Rwanda imekuwa ikiendelea kuwekeza katika huduma, miundombinu, elimu, na huduma za kiafya na utawala. Hii imewezesha nchi karibu kufikia kiwango cha Upatikanaji wa huduma ya Afya kwa Wote (Universal Health Coverage – UHC) *. Asilimia themanini na tano ya idadi ya watu wanapata mtandao mkubwa wa huduma bora za afya. Mamlaka za mitaa na viongozi wa mitaa ni muhimu kwa mpango wa mawasiliano wa serikali kwa vitisho vya kiafya kama vile COVID-19, kwani wao ndio wanajua eneo la watu walio katika mazingira magumu katika jamii.
Ikilinganishwa na mifumo mingine duni ya afya ya Kiafrika, Rwanda ina afadhali — mfumo wake wa rufaa uliogawanywa. Vitisho vya kiafya kama magonjwa ya milipuko vinasimamiwa katika ngazi za chini kabisa katika mfumo, katika ngazi za mitaa na jamii — katika maeneo yote ya mjini na vijijini. Kuanzia kituo kidogo kabisa cha afya (kinachoitwa”seli”) ambapo kuna wahudumu wa afya wa jamii ambao jamii zote za vijijini na wakulima wanaweza kuwafikia, watu katika maeneo ya vijijini na maeneo ya kilimo ambao wanahitaji uangalizi wa haraka wanapata huduma ya matibabu ndani ya maili moja kutoka kwenye nyumba zao. Na seli kama sehemu ya kwanza ya kuingia, zaidi ya vituo vya afya 2,500 hupokea wagonjwa katika maeneo ya vijijini na kutoka maeneo ya ndani kabisa. Vituo vya afya vinalenga maeneo yenye watu wengi. Kutoka kwa vituo vya afya vyenye vifaa vya matibabu, wagonjwa wanaweza kupewa rufaa na kupelekwa hospitali ya wilaya.
Rwanda imepiga hatua nzuri katika kukabiliana na kudhibiti janga la COVID-19. Mafanikio yake katika kushughulikia COVID-19 yanahusiana sana na mfumo wake wa afya uliogawanywa, ukijumuisha na shughuli za ufuatiliaji wa serikali, na ushirikiano kati ya taasisi za kitaifa (kwa mfano, Wizara ya Afya, Kituo cha Biomedical cha Rwanda, Jeshi la Polisi, Vikosi vya Ulinzi) na serikali za mitaa. Wafanyakazi wa afya ya jamii katika ngazi za kitaifa na ngazi zilizogawanywa za vijiji wenye uzoefu katika kutoa huduma za msingi za afya walihamasishwa kutibu COVID-19. Jambo lingine lililochangia kufanikiwa ni kwamba Wanyarwanda tayari walikuwa na uzoefu wa kuripoti kwa kufuata utaratibu na kunawa mikono kama sehemu ya makabiliano ya kitaifa yanayoendelea kutokana na virusi vya Ebola.
COVID-19 nchini Rwanda: Nyakati
Baada ya mgonjwa wa kwanza kupimwa na kukutwa na maambukizi tarehe 14 Machi 2020, serikali ya Rwanda ilianzisha hatua za kuzuia, ikiwa ni pamoja na kutafuta wale waliokutana na wenye maambukizi *na hatua za kujitenga*. Mamlaka za afya waliwasiliana na umma kupitia mitandao ya kijamii na kupitia wavuti za taasisi za umma kama vile Wizara ya Afya, na walitumia drones na sinema za nje, runinga, maigizo ya redio, tahadhari za maandishi kwa njia ya simu, na maigizo ya tamthiliya ili kuongeza uelewa miongoni mwa wanajamii. Njia hizi mara kwa mara ziliwaarifu Wanyarwanda juu ya maendeleo ya hivi karibuni ya COVID-19 na kuelezea tahadhari za usalama zinazohusiana na kunawa mikono, kuepuka mikusanyiko mikubwa, kukaa umbali kati ya mtu na mtu, kuhamasisha malipo bila pesa taslim, na watu kupiga simu katika namba ya bure na kuripoti kuhusu dalili za ugonjwa pale mtu anapozipata. Kwa muda mfupi tu, bomba za kunawa mikono ziliwekwa katika vituo vya mabasi, masoko, maeneo ya biashara, na majengo katika mji mkuu wa Kigali na vile vile katika maeneo ya vijijini.
Siku saba baadaye, kizuizi cha wiki mbili nchini kote kilianza kutumika kuzuia kuenea kwa COVID-19. Wakati huo, kulikuwa na visa 17 nchini. Matembezi yasiyo ya lazima yalipigwa marufuku, shule na vyuo vilifungwa, na marufuku ya mikusanyiko ya umma ilifuata. Umma ulionywa kutoa habari sahihi kwa ajili ya kufuatilia wale wote waliokutana na wenye maambukizi au adhabu ya hatari. Polisi wa Rwanda walilazimisha kufuata amri za kutotoka nje na hatua zingine za kuzuia kwa kutoza faini na kukamatwa kwa muda. Pia kuna ufuatiliaji ulioenea, pamoja na watu kuripotiana kwa mamlaka kwa tuhuma za kukiuka maagizo ya serikali.
Kwa kuongezea, serikali iliagiza maduka ya dawa na biashara zingine kuepuka kuongeza bei ya vitakatishi (dawa za kusafisha) na paracetamol (acetaminophen) ili kuhakikisha upatikanaji wa vifaa vya matibabu la sivyo watakabiliwa na adhabu.
Wakati bei za chakula muhimu zilipanda barani Afrika, na wanunuzi walipokuwa wameweka hifadhi ya vitu muhimu na wauzaji walitaka kupata faida wakati wa hofu ya virusi vya corona, Rwanda ilikuwa ni serikali ya kwanza ya Kiafrika kuweka kizuizi cha jumla mnamo mwezi Machi na kufunga mipaka yake. Serikali ilisambaza chakula kwa kaya zilizo katika mazingira magumu kote nchini. Kabla ya mwisho wa mwezi Machi, wizara ya biashara ilisaidia familia kwa kupanga bei ya vyakula 17 muhimu, ikiwa ni pamoja na mchele, tambi, unga wa mahindi, maharagwe, sabuni, mafuta ya kupikia, na unga wa uji. Utaratibu huu uliongozwa na viongozi wa mitaa katika ngazi za seli na vijiji. Serikali pia ilipanga bei za vyakula vilivyosindikwa, ambazo vingi vinaagizwa kutoka China.
Wale waliofaidika kimsingi na juhudi za serikali kusambaza chakula na kupanga bei walikuwa vikundi vilivyo hatarini zaidi, pamoja na wale waliopoteza kazi na mapato ya kila siku, na watu wanaofanya kazi katika sekta isiyo rasmi kama waashi wa kawaida, wafanyikazi wa saluni za nywele, madereva wa teksi, wale wanaofanya kazi katika baa, na wafanyikazi wa kawaida.
Kukomesha kuenea kwa janga la COVID-19, muda wa kizuizi kwa nchi nzima uliongezwa hadi zaidi ya tarehe 21 mwezi Machi. Lakini kwasababu ya kuendelea kwa vizuizi, wakulima wengi walikabiliwa na changamoto, haswa wale wanaojishughulisha na ufugaji wa mifugo na kuku. Mnamo mwezi Mei 2020, njia za usambazaji wa mazao yao zilikuwa zimevurugwa na hatua za kufungwa kwa nnchi kutokana na virusi vya corona.
Serikali ilitumia ubunifu wa teknolojia kujaribu na kufuatilia ufuataji wa maagizo ya serikali miongoni mwa wananchi. Huko Kigali, roboti zilipeleka dawa na chakula kwa watu waliotengwa, zilifanya vipimo vya awali vya uchunguzi wa COVID-19, na kuwasilisha taarifa hiyo kwa wafanyikazi wa afya. Drones zilitumika kufuatilia na kuwabainisha watu ambao hawakutii hatua za vizuizi vya kutembea. Mnamo mwezi Julai, Wizara ya Afya ya Rwanda ilizindua mpango wa upimaji wa jumla ulioundwa kuwapima madereva 5,000, watembea kwa miguu, na madereva wa teksi kwa siku katika jiji la Kigali na katika vituo vya mpakani mwa nnchi.
Idadi ya visa vya COVID-19
Mpaka tarehe 2 Oktoba, 2020, Rwanda ilikuwa ipo nafasi ya 136 miongoni mwa nchi zenye visa vingi zaidi ulimwenguni, ikiwa na visa 5,060 vilivyorekodiwa, 4,806 kati ya hao wamepona kabisa, na kati ya visa 220, hakuna mgonjwa ambaye yupo katika hali mbaya na kuhitaji uangalizi maalumu. Watu thelathini na wanne wamekufa tangu kisa cha kwanza cha maambukizi kiliposajiliwa mnamo mwezi Machi 2020.
Hadi mwanzoni mwa mwezi Juni, wastani wa kila wiki wa kesi mpya ulikuwa 36. Tangu wakati huo, wastani wa kila wiki umeongezeka hadi 284. Jumla ya vifo vilifuata mtindo kama huo-kutoka tatu katika kipindi kabla ya kilele hadi 34 ya sasa.
Mara ya kwanza kuona, hali hii inaweza kutazamwa kuwa ya kutisha au kama kushindwa kudhibiti janga hilo. Lakini ukiangalia kwa undani unaonyesha kuwa Rwanda ni kati ya nchi ambazo zimefanikiwa kudhibiti janga hilo.
Kwa kila watu milioni, Rwanda ina visa 388 na vifo 3, vyote vikiwa chini sana kwa viwango vya ulimwengu. Idadi ndogo ya vifo na kiwango cha juu cha kupona jumla huonyesha jibu bora kwa janga hilo na inaonyesha mafanikio ya kiwango cha juu ya chanjo ya afya nchini Rwanda.
Ongezeko la hivi majuzi la visa vilivyothibitishwa hakika ni kwasababu ya kuongezeka kwa idadi ya upimaji uliofanywa nchini. Nchi ilianza kufanya vipimo hata kabla kisa cha kwanza hakijathibitishwa na kupanua uwezo wake wa upimaji kutoka 891 kwa siku mnamo mwezi Aprili hadi 2,421 kwa sasa. Mwisho wa mwezi Agosti, upimaji wa kila siku ulikuwa umeongezeka hadi 5,382, kabla ya kushuka kwa kiwango cha sasa kwasababu ya utambuzi mdogo wa kesi mpya kupitia utaftaji wa wale waliokutana na wenye maambukizi. Kwa kulinganisha, serikali ya Uingereza inapima zaidi ya watu 270,000 kwa siku, Korea Kusini zaidi ya 9,000 kwa siku, na Ujerumani inafanya vipimo milioni moja kwa wiki kama njia thabiti la “kupima, kufuatilia, kutenga.” Kufikia tarehe 25 Oktoba, 2020, Rwanda imefanya vipimo zaidi ya nusu milioni, ikiwakilisha zaidi ya vipimo 41,000 kwa kila watu milioni moja, na kuiweka nchi hiyo katika nafasi ya 12 barani Afrika.
Sababu zingine zinazowezekana za kuongezeka kwa kesi ya maambukizi zinaweza kujumuisha kumalizika kwa kizuizi na kufunguliwa kwa biashara na mipaka, lakini hizi zinahitaji uchunguzi zaidi.
Nchi imepanga kutekeleza mfumo wa kutafuta waliokutana na wenye maambukizi ambao umeajiri wafuatiliaji 1,900 wanaofanya kazi katika maeneo ya vijijini nchini na inajumuisha pia ushirikiano na nchi jirani.
Kwa muhtasari, Rwanda ni miongoni mwa nchi za mfano linapokuja suala la kukabiliana na janga la virusi vya corona.
Jinsi wakulima wa Rwanda walisaidiwa kukabiliana na COVID, mvua kubwa, na mafuriko
Kwasababu wakulima wameruhusiwa kuendelea kufanya kazi katika mashamba yao, maeneo ya vijijini hayakuathiriwa sana na janga la COVID-19 kwa upande wa athari za kiuchumi na upatikanaji wa chakula. Hatahivyo, mvua iliyonyesha mnamo mwezi Aprili na Mei ilisababisha maporomoko ya ardhi na mafuriko. Hii iliathiri maisha, kilimo, makazi, miundombinu sekta za mazingira, na pia upatikanaji wa shughuli za kujiongezea kipato. Maeneo hatarishi zaidi yapo kaskazini, ambayo ni Nyabihu, Rubavu, na Gakenke.
Hadi mafuriko, wakulima walikuwa wakitarajia kuongezeka kwa upatikanaji wa chakula kutokana na uzalishaji wao wenyewe, kutokana na mavuno ya wastani hapo juu ambayo yalimalizika mwezi Machi 2020, na mavuno ya kawaida yaliyotarajiwa mwezi Mei-Julai.
Kufikia tarehe 9 Oktoba, 2020, Shirika la Chakula na Kilimo la umoja wa Mataifa (FAO) lilikuwa limeanza kutoa pembejeo na zana za kilimo kwa wahanga wa mafuriko, kwa kushirikiana na washirika mbalimbali, pamoja na Shirika la Uhamiaji la Kimataifa (IOM). IOM ilitoa makazi kwa familia zilizo katika mazingira magumu ambazo nyumba zao ziliharibiwa na mvua. Kaya zilizofaidika na msaada huu ni pamoja na zile zinazoongozwa na wanawake, wazee, wanawake wajawazito na wanaonyonyesha, na ni pamoja na watoto na watu wenye ulemavu. Watu walio hatarini na waliokuwa na ardhi ya kilimo iliyopandwa mazao mbalimbali ambayo yaliharibiwa na mafuriko walipokea vifurushi vyenye maharagwe yenye madini ya chuma, mahindi mseto, mbolea, na zana za kilimo.
Ugumu katika hatua za kukaa umbali kati ya mtu na mtu na hatua zingine za tahadhari
Wilaya ya Nyagatare katika mkoa wa Mashariki wa Rwanda ni wilaya kubwa na ya pili yenye idadi kubwa ya watu nchini Rwanda. Wilaya ina idadi kubwa ya ng’ombe, na ardhi hailimwi sana kama katika maeneo mengine ya nchi, hali ambayo inaweza kupunguza hatari ya kuambukizwa COVID-19 na hitaji la mazingatio ya utengamano wa kijamii.
Mwangalizi kutoka shirika la UN aliyetembelea eneo hilo mwishoni mwa mwezi Agosti 2020 kuzungumza na wakulima wa mboga aliripoti juu ya kuchukua kwa wakulima hatua za tahadhari dhidi ya COVID-19. Kuhusiana na kukaa umbali kati ya mtu na mtu, kuvaa barakoa, na kuzingatia usafi wa mikono, pamoja na hali ambayo ni ngumu kufuata hatua hizi, wakulima wanafanya usafi na kunawa mikono mara kwa mara wakati wowote inapowezekana, ingawa haijulikani ikiwa wanaosha nyumbani au kwa bomba za kunawa mikono zilizowekwa na serikali za mitaa. Wakulima pia wanaripoti kwamba wanazingatia kabisa amri ya kutotoka nnje kuanzia saa 10 jioni hadi saa 11 asubuhi.
Licha ya idadi kubwa ya watu huko Nyagatare, kunawa mikono na kuheshimu amri ya kutotoka nje inaweza kuwa imelipa, kwani hakuna visa vya COVID-19 vilivyorekodiwa na hakuna watu waliotengwa katika vituo vya COVID kwasababu ya dalili zinazohusiana na COVID. Rwanda haikutumia vituo vilivyopo kama vile vituo vya matibabu ya Ebola lakini iliunda vituo vya matibabu na kutengwa haswa kwa ajili ya COVID-19.
Vizuizi vya kutembea na mikusanyiko na hatua zingine zimekuwa na athari mbalimbali kwa wakulima. Wakulima wengine wamehitaji kugeuza matumizi ya pesa ambazo wangewekeza katika shughuli za kilimo kusaidia familia zao kukidhi mahitaji ya haraka zaidi na kupata afya ya msingi.
Kusafirisha bidhaa na kukutana na wateja wa kawaida ni changamoto, na kupata wateja wapya inakuwa haiwezekani. Mkulima mmoja alibainisha kuwa anasafiri kwenda Kigali kuuza mazao yake badala ya kutegemea wateja wa kudumu. Lakini mkulima huyo ameshindwa kusafiri kwenda Kigali, na hakuweza kusafirisha mazao yake kwa wateja waliopo. Kwa kawaida, karibu tani tano za matunda na mboga huvunwa kwa hekta katika mkoa huu, lakini hii imeshuka hadi tani tatu, na mazao yaliyosalia yataharibika.
Wakulima wa Rwanda wanaungwa mkono sio tu na serikali na mipango mbalimbali ya UN, lakini pia wanaweza kutegemea Ubudehe. Ubudehe ni utamaduni wa mababu, mazoea ya muda mrefu ya Wanyarwanda ya hatua za pamoja, utunzaji, na kusaidiana ili kutatua shida za jamii. Vyama vya ushirika vingi vya wakulima na wanachama mmoja mmoja wametoa msaada wa chakula kwa wanajumuiya wenzao walioathiriwa na COVID-19 na vizuizi. Kwa mfano, Ushirika wa Shamba la Kabiyaki na Ushirika wa karibu wa Tuzamurane-Cyeza Mashariki mwa Rwanda walitoa karibu tani moja ya mahindi yaliyozalishwa na ushirika, pamoja na bidhaa zingine za chakula, kwa karibu watu 200 kutoka kwa familia 42. Kila familia ilipokea kifurushi cha chakula kilicho na mahindi kilo 20, mchele kilo tano, kilo mbili za uji wenye lishe kwa watoto wadogo, lita moja ya mafuta ya kula, na sabuni.
Wanawake wa vijijini nchini Rwanda wanajishughulisha kikamilifu na kilimo — kama wazalishaji, wasindikaji, wauzaji, na wafanyabiashara wasio rasmi – lakini ushiriki wao katika shughuli hizi umepunguzwa sana na shida hiyo ya COVID -19. Kupungua kwa fursa za wanawake kupata riziki kutokana na vizuizi vya kusafiri na kuongezeka kwa ukosefu wa ajira kunaathiri nguvu zao za kufanya maamuzi nyumbani, na kuathiri upatikanaji wa lishe bora katika kaya na uthabiti.
Ukatili wa kijinsia umetajwa kama “janga kivuli” la COVID-19. UN Women inabainisha kuwa, barani Afrika na kwingineko ulimwenguni, simu za mkononi kwa ajili ya kuripoti ukatili na masuala ya makazi zimekuwa zikiongezeka wakiomba msaada. Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni, mafadhaiko yanayosababishwa na vizuizi kutokana na COVID-19 na kutokuwa na uhakika wa kiuchumi huzidisha mashambulio ya vurugu. Janga hilo limewalazimisha wanawake wengi walio katika uhusiano wa dhuluma kubakia nyumbani na wanyanyasaji wao, na kuzidisha hatari kwao.
Moja ya athari chanya za janga la COVID-19 nchini Rwanda ni kwamba nchi hiyo imezingatia na kuanza kutetea usawa wa kijinsia na mapambano dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia katika maeneo ya vijijini. Kituo cha Kutoa Huduma Zote Mahali Pamoja cha Isange (Isange One Stop Center) ambacho kipo ndani ya Hospitali ya Polisi ya Kacyiru jijini Kigali, kimekuwa kitovu cha waathirika wa unyanyasaji wa kijinsia. Katika kituo hicho, manusura wanaweza kupata huduma zote zinazohitajika mahali pamoja na bure. Kituo hicho kinaendeshwa na Wizara ya Jinsia na Familia, Afya na Usawa pamoja na Jeshi la Polisi la Rwanda. Mpango huu ulianza mnamo mwaka 2009 kama kituo cha mfano na umepanuka kote nchini. Rwanda sasa ina Kituo cha Kutoa Huduma Zote Mahali Pamoja katika kila wilaya. Kila siku, hadi waathirika makumi hupokelewa katika kituo hicho.
Kupungua kwa fursa za kujipatia riziki kwa wanawake kuna athari zingine, kwani mapato ya wanawake kwa ujumla yanaelekezwa kwenye elimu, huduma za afya, na uwekezaji tena katika kilimo cha wanawake au shughuli za ujasiriamali. Kwa Rwanda, kuchunguza tena athari maalum za kijinsia za COVID-19 na kujumuisha uwezeshaji wa wanawake bado ni muhimu kwa mikakati ya kuendelea na maisha baada ya COVID-19.
Mafanikio ya Rwanda katika kudhibiti janga la ulimwengu lilianza kwa kutekeleza sera na teknolojia za sayansi. Rwanda imeonyesha mfano kwa nchi zingine kufuata, haswa barani Afrika. Swali sasa ni ikiwa nchi hiyo itaweza kuhakikisha kuwa watu wanaoingia nnchini kutoka katika mataifa ya Afrika Mashariki hawana COVID-19 kufuatia kufunguliwa tena kwa uwanja wa ndege tarehe 1 Agosti 2020.
Kama nchi nyingine za Kiafrika, Rwanda inaomba cheti cha majibu ya kipimo cha COVID-19 kutoka kwa wasafiri wanaowasili. Kwa kuongezea, wasafiri hupimwa wakati wa kuwasili na lazima wajitenge katika makazi yao hadi hapo watakapopokea majibu ya vipimo vyao, angalau masaa 24. Bado haijafahamika ni kwa kiwango gani hatua hizi zitafanikiwa, lakini kiashiria kimoja cha mafanikio ni ukweli kwamba Rwanda ni nchi pekee ya Kiafrika iliyoorodheshwa na Baraza la Umoja wa Ulaya kuwa miongoni mwa nchi 11 zilizo salama na magonjwa ulimwenguni.
Ufafanuzi muhimu
Karantini (Quarantining): Kutenganisha na kuzuia kutembea nnje watu ambao walikuwa wamekutana na ugonjwa wa maambukizi ili kuchunguza ikiwa wataugua.
Kutengwa (Isolation): Kutenganisha watu walio na ugonjwa wa kuambukiza kutoka kwa watu ambao sio wagonjwa.
Ufuatiliaji wa walikutana na wenye maambukizi (contact tracing): Mchakato wa ufuatiliaji unaojumuisha hatua tatu za msingi: kubainisha waliokutana na mwenye maambukizi, orodha ya walikutana, na ufuatiliaji wa wote waliokutana.
Upatikanaji wa Afya kwa Wote (Universal Health Coverage – UHC): Hali ambayo watu wote wanapata huduma za afya zinazohitajika (ikijumuisha kuzuia, kuchochea, matibabu, uponyaji, na upunguzaji wa maumivu) za ubora wa kutosha na zenye ufanisi mzuri na pia kuhakikisha kuwa kutumia huduma hizi hakuleti ugumu wa kifedha kwa watumiaji.
Acknowledgements
Shukrani
Imechangiwa na: Elisabeth Wilson, Mwanahabari na Mtaalam wa Mawasiliano.
Rasilimali hii imeandaliwa kwa msaada wa kifedha kutoka kwa serikali ya Canada uliotolewa kupitia Global Affairs Canada.
Information sources
Chanzo cha taarifa:
- Adepoju, P., 2020. Gender-based violence – the “Shadow Pandemic” of COVID-19. Health Policy Watch. https://healthpolicy-watch.news/75409-2/
- Baryio, N., 2020. Rwanda’s aggressive approach to Covid wins plaudit – and warnings. The Wall Street Journal. https://www.wsj.com/articles/rwandas-aggressive-approach-to-covid-wins-plauditsand-warnings-11601372482
- Beaubien, J., 2020. Why Rwanda is doing better than Ohio when it comes to controlling COVID-19. NPR. https://www.npr.org/sections/goatsandsoda/2020/07/15/889802561/a-covid-19-success-story-in-rwanda-free-testing-robot-
- Bishumba N., 2020. 8 things you need to know about gov’t food distribution programme. New Times. https://www.newtimes.co.rw/news/8-things-you-need-know-about-govt-food-distribution-programme
- Dayton, K., and Williamson, J., 2020. Women’s empowerment in agriculture is essential to COVID-19 survival and recovery. Agrilinks. https://www.agrilinks.org/post/womens-empowerment-agriculture-essential-covid-19-survival-and-recovery
- Devlin, H., 2020. Is 100.000 tests a day an effective strategy against coronavirus? The Guardian. https://www.theguardian.com/world/2020/may/01/is-100000-tests-a-day-an-effective-strategy-coronavirus
- Isaac, K, 2020. How Rwanda plans to save farmers from effects of COVID-19. Taarifa. https://taarifa.rw/how-rwanda-plans-to-save-farmers-from-effects-of-covid-19/
- Kagire, E., 2020. Rwanda: How COVID-19 relief distribution will work. KT Press https://www.ktpress.rw/2020/03/rwanda-how-covid-19-relief-distribution-will-work/
- Kripahl, C., 2020. Price hikes in Africa aggravate the coronavirus crisis. Deutsche Welle. https://www.dw.com/en/price-hikes-in-africa-aggravate-the-coronavirus-crisis/a-52820553
- Kuteesa, H., 2020. Rwanda: Govt extends lockdown until April 30. https://allafrica.com/stories/202004200427.html
- Maema, C., 2020. Rwanda to conduct street testing survey of COVID-19 in capital city. CGTN Africa. https://africa.cgtn.com/2020/07/02/rwanda-to-conduct-street-testing-survey-of-covid-19-in-capital-city/
- Nohana online journal, 2020. FAO has provided emergency agricultural support to disaster victims in Rwanda. http://nonaha.com/fao-has-provided-emergency-agriculture-support-to-disaster-victims-in-rwanda
- Nshiyimana, P., 2020. Rwanda controls COVID-19, but its farmers still struggle. Cornell Alliance For Science. https://allianceforscience.cornell.edu/blog/2020/08/rwanda-controls-covid-19-but-its-farmers-still-struggle/
- Our World in Data, 2020. Rwanda: Coronavirus Pandemic Country Profile. https://ourworldindata.org/coronavirus/country/rwanda?country=~RWA
- Rwibasira E., 2020. Effects of COVID-19 on farming in Rwanda: the fate of poultry farming. The New Times. https://www.msn.com/en-za/news/other/effects-of-covid-19-on-farming-in-rwanda-the-fate-of-poultry-farming/ar-BB13u99Q
- Schengen Visa Info, 2020. EU’s list of epidemiologically safe countries amid Covid-19.
https://www.schengenvisainfo.com/eu-list-of-epidemiologically-safe-countries-amid-covid-19/ - Ssebwami, J., 2020. COVID19 crisis: Rwanda begins distribution of essential goods to citizens affected by coronavirus lockdown. PML Daily. https://www.pmldaily.com/news/2020/03/covid19-crisis-rwanda-begins-distribution-of-essential-goods-to-citizens-affected-by-coronavirus-lockdown.html
- Ssuna, I., 2020. Limited COVID-19 testing? Researchers in Rwanda have an idea. Daily Herald. https://www.dailyherald.com/article/20200813/news/308139976
- World Food Program, 2020. Farmers in Rwanda provide food to those affected by coronavirus. https://insight.wfp.org/farmers-in-rwanda-provide-food-to-those-affected-by-coronavirus-ef4e0bf156e8
- World Health Organization, AFRO, 2020. Rwanda’s response to COVID 19 brings out the need to prepare and learn from practice. https://www.afro.who.int/news/rwandas-response-covid-19-brings-out-need-prepare-and-learn-practice