Utangulizi katika mikufu ya thamani

Kilimo

Backgrounder

Utangulizi.

Mkufu wa thamani sio kitu unachoweza kukiona. Bali, mkufu wa thamani ni njia nzuri ya kuelewa namna ulimwengu wa uzalishaji, ununuaji na uuzaji vitu unavyofanya kazi.

Sisi sote ni sehemu ya mkufu wa thamani kwa namna moja ama nyingine kama wazalishaji, walaji wa bidhaa na huduma, wasindikaji, wauzaji wa rejareja, wafadhili, nk. Kama walaji sote tunakula na kuvaa nguo, na kwa hiyo tumeunganishwa kwenye mikufu mingi ya thamani – mikufu ya mazao ya nafaka, mizizi, matunda na mbogamboga, kunde, mafuta, na nguo. Mkufu huu huanzia kwa wakulima kuja jikoni kwetu, meza za chakula, mavazi na kuendelea zaidi.

Katika upande mmoja wa mkufu huu kuna wazalishaji – wakulima wanaopanda mazao na kufuga mifugo. Katika upande mwingine kuna walaji ambao wanakula, kunywa, kuvaa na kutumia bidhaa za mwisho. Na katikati kuna maelfu mengi ya wanaume na wanawake, na bishara ndogo na kubwa. Kila mtu na kila biashara hupiga hatua moja ndogo katika mkufu, na kila mtu huongeza thamani kadri unavyosonga mbele kwa kupanda, kununua, kuuza, kusindika, kusafirisha, kuhifadhi, kukagua na kufungasha.

Watu wengine na biashara nyingine zina jukumu muhimu katika kusaidia mkufu. Benki hutoa mikopo, serikali huanzisha sheria na sera, na mashirika ya utafiti wa kilimo huweka njia kwa ajili ya wakulima kushiriki kwa ukamulifu katika mkufu wa thamani.

Vituo vya redio pia vina jukumu muhimu la kusaidia. Redio huweza kutoa taarifa kwa wakulima juu ya bei, ubunifu na mafanikio ya mikufu ya thamani, fursa kwa wakulima katika kuhusihwa kwenye mikufu ya thamani, na kuwadaidia wakulima kufahamu namna mkufu wa thamani unavyofanya kazi. Pia redio huweza kuwasaidia wakulima kushiriki kikamilifu katika mikufu ya thamani.

Mkufu wa thamani wa kilimo ni watu na shughuli zinazozalisha bidhaa muhimu za kilimo kama vile mahindi au mbogamboga au pamba kutoka mashambani hadi kwa walaji, kupitia hatua kama vile kusindika, kufungasha na kusamabaza.

Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa linafasili mkufu wa thamani kuwa ni “shuguli zote zinazohitajika kuleta bidhaa au huduma kutoka katika hatua yake ya awali ya uzalishaji hadi katika hatua yake ya mwisho ya matumizi, ikiwa ni pamoja na njia zote za masoko zilizopo katika biashara.”

Hata wakulima wadogo nao ni sehemu ya mikufu ya thamani. Idadi kubwa ya wakulima wadogo hulima baadhi ya mazao au hufuga baadhi ya mifugo kwa ajili ya kuuza. Hata katika maeneo ya ndani sana, wakulima wengi wadogo wameunganishwa na masoko, na huuza kiasi kidogo cha mazao yao kwenye masoko ya palepale au kwa wafanya bishara wanaokwenda mashambani kwao.

Kwa kweli, mikufu ya thamani inahusu maingiliano ya binadamu. Inahusu miunganiko kati ya watu na wafanyabiashara wanaosafirisha au kubadilishana bidhaa, fedha, maarifa na habari.

Katika mkufu wa thamani imara, watu katika hatua tofauti tofauti za mkufu husaidiana. Ambapo kila mmoja katika mkufu humsaidia kila mtu, kila mtu hufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi, na maisha ya kila mmoja huimarika. Kila mtu katika mkufu hushiriki katika lengo moja la kutosheleza mahitaji ya walaji kwa kusudi la kongeza faida zao wenyewe.

Mifano ya mikufu ya thamani.

Kila mkufu wa thanmani ni wa pekee, na unajumuisha mchanganyiko wa pekee wa “miunganiko.” Kwa mfano nchini Tanzania mkufu wa thamani wa muhogo, (tazama jedwali hapa chini), unaweza kusema kuwa wakulima wanaolima muhogo na mashirika humilikiwa na au huuzwa kwa wafanyabiashara, makampuni ya usindikaji, na washirika mbalimbali wa masoko, hivi ni viungo muhimu katika mkufu wa thamani kwa walaji. Lakini kuna viungo vingine muhimu. Hii huhusisha maduka, na watu wanaouza pembejeo za kilimo kama vile mbolea na dawa za kilimo kwa ajili ya kulima muhogo. Pia kuna wauzaji wa jumla wa mhogo ghafi, wasafirishaji, na washirika wengine. Hata hivyo miunganiko yote huathiriwa na mazingira ya sera za kitaifa na za kimataifa.
value chain diagram SW

Mchoro hapa chini huonyesha namna thamani inavyoongezwa katika kila kiungo kwenye mikufu ya thamani mitatu tofauti. Kwa mfano, katika mkufu wa thamani wa kiazi kitamu nchini Ghana, kazi anayoifanya mchuuzi inaongeza thamani, kiasi kwamba bei anayoitoza mfanyabiashara kwa kilo (au tani) ya kiazi kitamu ni asilimia 50 zaidi ya bei anayomlipa mkulima kununua viazi vitamu.

Anayefuata ni muuzaji wa jumla, naye huongeza thamani kiasi kwamba bei anayomtoza muuzaji wa rejareja ni asilimia 13 zaidi ya bei anayomlipa mchuuzi. Na bei ambayo muuzaji wa rejareja anamtoza mlaji ni asilimia 18 zaidi ya bei ambayo muuzaji wa rejareja anamlipa muuzaji wa jumla. Kwa lugha ya mkufu wa thamani, kila mtu katika mkufu hutoza “faida ya ziada” kwenye hatua yake ya mkufu.

value chain diagram 2 SW

Kwa nini tuzungumze juu ya mkufu wa thamani?
Wakulima wadogo wadogo Afrika na kwingineko ulimwenguni huwa wanasema kuwa kupata bei ya chini kwa mavuno yao ni changamoto kubwa. Kwa uhalisia, mkulima humsubiri mchuuzi kumtembelea shambani kwake. Mchuuzi ananunua kwa bei ya chini na hatanunua mazao yote. Mkulima anakuwa hana furaha, muda wake na juhudi zake hazikulipwa vizuri. Anaweza kumlaumu mchuuzi juu ya matatizo yake.

Wakulima na mchuuzi mara nyingi hugombana juu ya bei. Mkulima anaweza kumdanganya mfanyabiashara kwa kuweka bidhaa hafifu chini ya gunia, na mchuuzi anaweza kumdanganya mkulima kwa kutumia uzito na vipimo visivyofaa. Siku zote kunakuwa hakuna imani kati ya hawa watu wawili. Hii inasababisha mkufu wa thamani usifanye kazi kama ambavyo ungetakiwa kufanya, na hivyo kumaanisha matokeo mabaya kwa kila mmoja.

Mchuuzi huuza mazao ya mkulima kwa msindikaji, naye husambaza kwa muuzaji wa jumla, anaye sambaza kwa muuzaji wa rejareja, ambaye naye husambaza kwa mlaji kwa usafiri na viungo vingine katikati. Kila mshirika katika mkufu huu huongeza thamani, na baadae hupata faida, ambayo huitwa “faida ya ziada.” Kiasi apatacho kila mshirika katika mkufu huzidiana kati ya aina ya bidhaa na mikufu ya thamani. Lakini bei anayopata mkulina ni kijisehemu tu cha bei inayolipwa na mlaji.

Kama mtu mmoja mmoja, wakulima wadogo wadogo siku zote wanapata hasara katika aina hii ya mikufu ya thamani. Kwa sababu wakulima wengi hulima mazao au hufuga mifugo kama mtu mmoja mmoja, wana nguvu ndogo ya kujadili bei. Wana ushawishi mdogo au hawana kabisa juu ya bei ambazo mchuuzi huwalipa kununua mazao yao, au bei wanayolipa kuwalipa wasamabazaji wa pembejeo kwa ajili ya kununua mbegu, mbolea, viuatilifu, nk.

Pia, mara nyingi wakulima wanakosa taarifa juu ya masoko ya mazao yao. Kwa mfano, wanaweza wasijue mazao yao yana thamani kiasi gani, na kiasi gani zaidi wangepata endapo, kwa mfano, wangesafirisha kwenda katika soko la jirani kuliko kuuza kwa mchuuzi. Wanaweza wasijue wadau wengine katika soko ni akina nani; wanaweza wasijue nini kinatokea katika mazao yao baada ya kuyauza; na wanaweza wasijue ni aina gani ya bidhaa wanayohitaji walaji. Katika mifano mingi, mkulima analima zao lisilofaa sokoni. Kwa sababu hizi zote, ni vigumu kwa mkulima wa kiafrika kufaidika katika mkufu wa thamani ambao amekwisha jihusisha nao.

Kwa kiwango fulani, wakulima kwa kutojua wanachangia katika matatizo yao wenyewe. Kwa mfano, mkulima naweza kulima maembe ya aina zote. Baadhi ni makubwa na yenye afya na mengine ni madogo na yenye madoa doa. Mkulima anafungasha maembe yote katika gunia. Mchuuzi hajui yatakuwa na ubora gani, kwa hiyo anatoa bei ya chini.

Ili kuongeza kipato na kupata faida zaidi (“faida ya ziada”) katika mkufu wa thamani, wakulima wanatakiwa kuongeza uhusika wao katika mkufu wa thamani. Kuna njia nyingi za kufanya hili. Hatua moja wanayopaswa kuchukua ni kuwa “wakulima wa zao maalum.” Mkulima wa zao maalum ni mkulima ambaye ameboresha njia zake za kilimo na anazalisha bidhaa kwa ajili ya soko kwa njia ya ufanisi na yenye tija. Kwa mfano, kwa kutumia njia bora za kilimo, mkulima anaweza kuzalisha maembe mengi na yenye ubora wa juu. Hii huwaridhisha wanunuaji na walaji. Tutaangalia baadae njia nyingine za kuboeresha katika waraka huu.

Kuna faida gani katika kutumia njia ya mkufu wa thamani?
Njia ya mkufu wa thamani huangalia kazi za wadau wa mkufu waliopo, wafadhili, na mazingira ya sera. Inatusaidia kushughulikia changamoto zilizopo katika mkufu wa thamani, na vilevile fursa ya kuboresha ufanisi wa mkufu wa thamani na maslahi ya kila mtu anayehusika. Kwa mtazamo wa kumwangalia mkulima, kuwa sehemu ya mkufu wa thamani unaofanya kazi vizuri kunaweza kuleta kipato kikubwa zaidi.

Kuchanganua mkufu wa thamani – kutambua changamoto zake, udhaifu, na faida kunaweza kusaidia kutambua fursa mpya za kuongeza kipato.

Wakati mwingine, kushiriki katika mkufu wa thamani unaofanya kazi vizuri, hakuwapi wakulima kipato cha juu tu au bei za juu tu, bali kipato imara zaidi na kinachoweza kutabirika.

Masoko na mikufu ya thamani inayofanya kazi vizuri huweza kuwavutia vijana katika shughuli za kilimo au kuwashawishi ili wasiondoke vijijini kwa kuwapatia njia bora za kupata pesa.

Kushiriki katika mkufu wa thamani kunaweza kumsaidia mkulima kujifunza mbinu mpya na kutumia njia zilizoboreshwa. Badala ya kurundika mboga mboga kwenye gunia na kuzipakia kwenda kwa mchuuzi au sokoni, wakulima wanaweza kupata pesa kwa kufanya njia za awali za usidikaji wakiwa shambani. Hata kusafisha na kutenganisha mazao kwa viwago vyake huweza kuleta tofauti. Kuosha na kufungasha saladi au nyanya na kuzipeleka katika soko la palepale au katika maduka makubwa wanaweza kupata bei ya juu. Kumenya na kukatakata matunda kunaweza kuwa ni njia rahisi ya kuingia katika soko linalokua karibu na maeneo ya mijini la bidhaa za vyakula vilivyotayari kwa ajili ya kula.

Nani ananufaika katika mkufu wa thamani?
Kila mtu anayeshiriki katika mkufu wa thamani anaongeza thamani kadri bidhaa inavyosonga mbele kutoka mwanzoni mwa mkufu kuelekea kwa mlaji. Na matokeo ya kuongeza thamani hii, washirika wote hupata faida ya ziada. Hii ndio faida kubwa au kifuta jasho katika kushiriki katika mkufu wa thamani.

Watu wengi wanaofaidika katika mkufu wa thamani wana silka ya kiujasiriamali, yuko radhi kuwasiliana na watu katika sehemu mbalimbali za mkufu wa thamani, na wana shamba na rasilimali fedha na maarifa kutengeneza masoko mapya au kushiriki kikamilifu zaidi katika masoko yaliyopo.

Wakulima ambao wana ardhi ndogo, ambao wako mbali na masoko, ambao wana vitega uchumi vichache, ambao wana vikwazo vya lugha, na ambao hawajihusishi katika vyama vya wakulima wataono ni vigumu sana kufaidika katika mkufa wa thamani.

Umuhimu wa vikundi vya wakulima.
Wakulima wanatakiwa wawe wamejipanga vizuri ili kushindana katika soko linalokua sana. Kama vile kuwa wakulima wa zao maalum, kujiunga katika vikundi vya wakulim ni hatua muhimu kwa wakulima wadogo wadogo wanaohitaji kuongeza kipato chao na kupata faida zaidi katika mkufu wa thamani. Tofauti na mkulima mmoja mmoja, vikundi vya wakulima vina rasilimali kwa kuwavutia na kujenga uhusiano na miunganiko mbalimbali katika mkufu wa thamani, kitaifa na kimataifa.

Vikundi vya wakulima husaidia mkulima mmojammoja kwa kukusanya pamoja mazao ya wakulima wengi, kununua pembejeo nyingi kwa bei ya chinini kwa niaba ya mkulima, na kuwawezesha wakulima kupata huduma za shamba. Kwa ukubwa wake, vikundi vina nguvu ya kutosha ya masoko, kupandisha bei zinatolewa kwa mkulima mmojammoja na kuhakikisha kuwa wakulima wanapata kipato cha uhakika. Vikundi vingi vya wakulima pia huhusisha utaratibu wa kuweka na kukopa kwa wanachama wao. Utaratibu huu huwasaidia wakulima kutumia vizuri pesa zao, kutunza kumbukumbu, na kujifunza mbinu za kifedha ambazo ni muhimu sana kukuza biashara zao.

Mtangazaji wa redio ana wajibu gani katika mkufu wa thamani?
Kimsingi kuna mtiririko wa vitu vitatu katika mkufu wa thamani: bidhaa hutoka kwa wazalishaji kwenda kwa walaji, pesa hutoka kwa walaji kwenda kwa wazalishaji, na mtiriko wa habari huenda sehemu zote.

Redio huweza kutenda kama wakala wa habari na maarifa. Hii ina maana kwamba vituo vya redio huweza kupeleka habari juu ya mkufu wa thamani kwa wasikilizaji wake. Redio pia huweza kupeleka habari juu njia mpya na makini katika kuhusishwa kwenye mkufu wa thamani.

Redio huweza kutangaza fursa za masoko au fursa za kufanya mkataba ambazo huweza kuwasaidia wakulima wadogowadogo.

Redio inaweza kutangaza habari za mafanikio, na kuwasaidia wakulima kuelewa faida ya kuunganishwa na biahara nyingine katika mkufu wa thamani.

Ni muhimu watangazaji kutumia lugha inayostahili pale wanapozungumzia mikufu ya thamani. Zungumza na wakulima wacahche katika hadhira yako. Tafuta maneno mazuri zaidi katika lugha izungumzwayo katika eneo lako yanayoweza kufafanua zaidi istilahi “mkufu wa thamani” na “muunganiko” na istilahi nyingine zinazohusika na mkufu wa thamani. Chagua maneno yanayotoa maana kwa usahihi na ambayo hadhira yako inayaelewa.

Kama kawaida, ni muhimu kutozungumza na wakulima kwa dharau, ama kwa toni ya sauti yako au kwa kutumia lugha ambayo wachache katika ahadhira yako ndio wanaifahamu. Kabla hujafanya kipindi juu ya mikufu ya thamani, hakikisha kwamba unajua kwa undani mikufu ya thamani ni nini na jinsi gani inaweza kuwasaidia wakulima. Kama huelewi vizuri, ongea na wakala wa uenezi, wawakilishi wa viwanda vya vyakula au mwingine anayeweza kukusaidia kujua mikufu ya thamani ni nini na jinsi inavyofanya kazi katika eneo la wasikilizaji wako.

Watangazaji wanatakiwa kufanya wawezalo kuelewa juu ya mkufu wa thamani mahali. Kutafuta kujua washirika wanaohusika katika mkufu wa thamani unaofahamika sana katika jumuia yako ya wasikilizaji. Zungumza na wakulima, wasindikaji na wauzaji wa rejareja na wengine katika mkufu wa thamani. Fahamu mipangilio inayofanikiwa zaidi na ile isiyofanikiwa. Watangazaji wanaweza kutoa taarifa sahihi juu ya mikufu hii kwa kuwahoji watu hewani wanaohusika katika mkufu mahususi.

Kuna faida kwa watangazaji katika kuchangamana na miunganiko tofauti tofauti katika mkufu. Utajiunganisha na wasindikaji, wauzaji wa rejereje, wasambazaji, vilevile mkulima anaweza kukusaidia kupanua vyanzo vyako vya utangazaji, na kugundua fursa mpya za kibiashara kwa ajili ya kituo chako.

Kupanda daraja
Kwa mkulima, kupanda daraja kunamaanisha kuboresha ujuzi wake wa kilimo na biashara kwa namna ambayo humwezesha kupata faida zaidi katika mkufu wa thamani. Kupanda daraja kunaweza kuwasaidia wakulima kupata njia mpya, wabia wapya na mawazo mapya ya kupeleka biadhaa kwenye soko. Au kunaweza kusaidia kuboresha shughuli zao katika mkufu wa thamani uliopo. Kupanda daraja kunaweza kuzidisha faida na kunaweza kupunguza hasara, au vyote.

Kuna njia nyingi kwa mkulima kustawisha uhusika wake katika mkufu wa thamani. Zifuatazo ni mbinu kuu nne za kupanda daraja.

Kupanda daraja kimkakati: Kwa wakulima, kupanda daraja kimkakati humaanisha kuongeza mavuno au kupunuza gharama za kuzalisha kiwango fulani cha mazao, kwa mfano kupunguza gharama ya jumla iliyohusika katika kupanda na kuvuna kilo 100 za muhogo. Kupanda daraja kimkakati kunahusisha njia bora za kilimo – mbinu bora za upandaji au mbegu za kupanda, umwagiliaji, udhibiti bora wa wadudu na ufungashaji. Njia hizi huweza kusababisha mavuno mengi, mauzo zaidi, au chakula cha kutosha kwenye meza ya familia.

Kupanda daraja kimkakati ni kubadili pembejeo za kilimo (wafanyakazi, mbolea, mbegu za kupanda, viuatilifu, nk.) kuwa mavuno yenye ufanisi zaidi. Kwa mlimaji, hatua hii inaitwa “kuwa mkulima wa zao maalumu.” Ili kupata faida zaidi katika mkufu wa thamani, wakulima ni lazima wawe wakulima wa zao maalumu.

Uratibu mlalo: Aina ya pili ya kupanda daraja ni uratibu mlalo. Uratibu mlalo ni kwamba unaratibu shughuli zako pamoja na wengine ambao wapo katika hatua sawa katika mkufu, kwa mfano, wakulima kushirikiana na wakulima wengine katika vikundi vya wazalishaji au ushirika. Kununua pembejeo kwa pamoja na kuuza mazao yao kwa pamoja, gharama zao za uzalishaji hupungua na wanakuwa na uwezo wa kufikia masoko.

Uratibu mlalo hufanya watu kuheshimika zaidi. Hii huimarisha hali ya kiuchumi ya mkulima, humwezesha kuwekeza katika vifaa na vitu vingine, na humpatia uwezo wa kupata pesa za kununulia kile anacho kihitaji wakati anapokihitaji. Hii huongeza kipato cha mtu na familia, na huongeza usalama wa chakula kwa sababu ya matumizi makubwa ya mazao kwa ajili ya chakula.

Uratibu mlalo pia huweza kuwasaidia wakulima kuingia katika masoko yanayohitaji cheti cha uthibitisho, kama vile masoko huria, na huweza kuwapa wakulima nguvu kubwa ya kujadiliana bei katika mkufu wa thamani.

Uratibu wima: Aina ya tatu ya kupanda daraja inaitwa uratibu wima. Uratibu wima huhusisha kusonga mbele muingiliano wa mara moja tu wa mnunuzi-muuzaji na kwenda mahusiano ya muda mrefu ya kibiashara. Uratibu wima humaanisha kuratibu shughuli zake pamoja na watu na biashara katika hatua tofauti tofauti za mkufu wa thamani, kwa mfano, wasindikaji au maduka makubwa.

Aina mojawapo ya uratibu mlalo ni kilimo cha mkataba, ambacho kwao msindikaji, muuzaji wa rejareja au msafirishaji husaini mkataba na wakulima kuzalisha kiwango fulani cha mazao cha ubora mahususi na kwa kipindi mahususi.

Uratibu wima mara nyingi huhusisha makampuni makubwa – mara nyingi ni wanunuzi wakubwa au maduka makubwa ambao huratibu vitendo vyote katika mkufu wa thamani. Katika uhusiano wima, makampuni makubwa mara nyingi huwapa wakulima pembejeo kwa punguzo la bei, uwezo wa kupata mikopo, msaada wa kiufundi na vifaa.

Uratibu mlalo huweza kuwapa wakulima uhakika na usalama juu ya mauzo na mapato ya baadae. Lakini uratibu mlalo huhusisha kujenga imani katika ya wauzaji na wanunuzi, hatua ambayo inaweza kuwa ya taratibu na ngumu. Imani inaweza kukua pale ambapo kila mmoja ana imani kwamba atafaidika.

Upandaji daraja wa kiutendaji: Upandaji daraja wa kiutendaji hutokea pale ambapo wakulima hufanya kazi nyingi katika mkufu, kwa mfano, kusindika, kufungasha au hata kufanya mauzo. Hii huweza kuwasaidia wakulima kupata faida zaidi ya ziada, kitu kinachomaanisha kupata kipato zaidi. Mfano huhusisha wakulima wanaozalisha unga wa muhogo au vipande vya muhogo na wakulima wanaouza kumbwe za muhogo.

Hili linaweza kuonekana kuwa wazo zuri. Lakini ili kufanikiwa kufanya mazoezi haya mapya, wakulima lazima wawe na vitendea kazi na lazima wajue jinsi ya kuyafanikisha, vilevile wawe na rasilimali nzuri ya kifedha na wawe na ujuzi mzuri wa kupangilia mambo.

Kwa mfano, mikufu ya thamani inapokuwa mifupi ambapo uratibu wima unapohusisha kusaga mahidi na kuyaweke kwenye kiroba, njia hii inaweza kuwa thabiti. Lakini kadri mkufu unavyozidi kuwa mrefu ndivyo hasara inavyozidi kuongezeka, hasa kwa wale wenye uzoefu mdogo.

Aina nyingine za kupanda daraja: Mifumo mingine ya kupanda daraja ambayo haikujadiliwa hapa kwa kina ni pamoja na:
Upandishaji daraja wa bidhaa: kwenda katika bidhaa chanagamani na zenye ubora wa juu.
Upandishaji daraja ndani ya mkufu: kutumia ujuzi ulioupata kutoka katika kiungo kimoja cha mkufu na kuutumia katika mkufu mwingine
Kukidhi viwango na vyeti vya uthibitisho (kwa mfano, katika soko huria). Huu unaweza kuwa upandishaji daraja wa bidhaa, na huendeshwa na ubadilikaji wa soko unaohusishwa na uchaguzi wa walaji.

Kutunza kumbukumbu na kupata taarifa za masoko.
Hatua moja muhimu ya kuwa mkulima fanisi au “mkulima wa zao maalum” ni kutunza kumbukumbu nzuri. Kwa kufuatilia wafanyakazi na pembejeo shambani, mkulima anaweza kujua gharama zilizohusika katika kuzalisha mazao yake. Anapojua gharama ya uzalishaji, anaweza kufanya maamuzi mazuri yaliyojikita katika taarifa kama vile kukukotoa gharama za kuuza kwa ufanisi zaidi.

Taarifa za masoko ni muhimu pia. Endapo wakulima watafahamishwa vizuri juu ya bei zilizopo na mwelekeo wa soko, wanaweza wakajadiliana vizuri juu ya bei na wanunuzi.

Mkufu wenye maono.
Ili kufanya kazi na viungo vingine katika mkufu wa thamani, wakulima wanatakiwa kuendeleza “mkufu wenye maono.” Hii inamaanisha kuwa wanaona jinsi mkufu wao wa thamani unavyofanya kazi, kadri mtandao wa makampuni unavyochangiana kila mmoja katika kutengeneza faida.

Wakulima wanatakiwa watambue nafasi ya viungo vingine katika mkufu, na kuheshimu kuwa nia zao pia ni halali. Miunganiko tofauti tofauti katika mkufu lazima waelewe ulazima wa kushirikiana kuliko kugombana wao kwa wao. Wanatakiwa kuelewa kuwa ingawa wauzaji na wanunuaji siku zote watakuwa na matamanio yanayopingana – bei ya juu na bei ya chini mtawalia – lakini wana lengo sawa la kumridhisha mlaji. Mlaji anaporidhika biashara ya wote, wauzaji na wanunuzi itakaua. Ili mkufu wa thamani ufanikiwe, kila mtu katika mkufu lazima afaidike na ahisi kwamba wote wanachukuliwa sawa.

Kumbuka: Mikufu ya thamani sio tu juu ya kusafirisha mazao.
Ambapo wakulima wa kiafrika (na watu wengine) wanaposikia juu ya mikufu ya thamani, mara nyingi hufikiri juu ya kusafirisha mazao kama vile maua, kahawa, kakao, na matunda na mboga mboga kwenda ulaya na masoko mengine ya kimataifa.

Ila sio wazo zuri siku zote kuwaunganisha wakulima wadogo na wasafirishaji wakubwa. Wakulima wadogo wadogo Afrika na kwingineko kwa ujumla wanajaribu kupunguza hatari ya kushindwa kupanada mazao mengi na kufuga mifugo wengi. Kujikita katika zao moja tu ni hatari zaidi. Inaweza kuwa vema zaidi kwa wakulima kuangalia soko la kikanda na la ndani vilevile, kama njia mbadala ya masoko ya kimataifa. Kwa sababu ya ongezeko la makazi ya mjini na ukuaji wa tabaka la kati Afrika, masoko ya kikanda na ya ndani yanakuwa muhimu sana kwa wakulima.

Jinsia na mikufu ya thamani.
Katika mikufu mingi ya kilimo, wanawake wanaweza kukabiliana na hali ngumu kuliko wanaume. Kwa mfano, katika mikufu wa thamani wa kusafirisha matunda na mboga mboga, wanawake mara nyingi wanaajiriwa kama wafanyakazi wa muda, ambapo wafanyakazi wa kudumu huwa ni wanaume. Kwa mfano, katika biashara ya kusafirisha matunda na na mbogamboga nchini Kenya, wanawake wanachukua asilimia 80 ya nafasi katika kufungasha, kuweka nembo na kutengene karatasi za msimbo. Wafanyakazi wa kike siku zote wanapewa malipo ya chini kuliko wanaume.

Kujiunga na vikundi vya wakulima kunaweza kuwasaidia wanawake. Wanapokuwa wanasaidiwa na nguvu ya kikundi, wanaweza kufanikiwa zaidi katika kujadili biashara kubwa.

Ni muhimu kuchukua tahadhari katika athari zisizotarajiwa za kupandisha ngazi mikufu ya thamani. Hii hapa ni mifano mitatu: kwanza, kama familia hutumia nguvu zake zaidi na ardhi katika mazao ya thamani zaidi yanayopandwa na wanaume, wanaume watakuwa na udhibiti mkubwa juu ya rasilimali zinazohusika na mazao hayo, kama vile ardhi na maji. Mazo ya wanawake na usalama wa chakula unaweza ukapata shida.

Pili, endapo fursa za masoko zikiongezeka kwa mazao ya wanawake, wanaume wanaweza kuanza kuingilia kazi za wanawake kwa kuwazuia wasitumie ardhi.

Tatu, endapo familia itashiriki katika kilimo cha mkataba, itahitaji kufungua akaunti ya benki. Akaunti za benki siku zote huwa zinafunguliwa kwa jina la mwanaume. Hii inamaanisha kwamba ili mwanamke apate pesa itamlazimu kupitia kwa mume wake. Katika jamii ambazo wanawake hupata pesa kwa kuuza mazao, wakati mwingine huzificha kwa matumizi ya nyumbani, hii inaweza kudhuru usalama wa chakula wa familia.

Kwa ujumla, ni muhimu kuangangalia sio tu jinsi wanaume na wanawake wanavyojihusisha katika mikufu ya thamani kwa namna tufauti tofauti, bali jinsi ambavyo kupandisha kiwango shuguli zao kunaweza kuwanufaisha (au kutowanufaisha) wanawake na wanaume kwa pamoja.

Hitimisho.
Kama tulivyoeleza hapo juu, katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Farm Radio International itasambaza maandishi mengi na taarifa nyingine juu ya mikufu ya thamani. Kwa taarifa zaidi juu ya mikufu ya thamani, ongea na watu katika wizara ya kilimo, mashirika yasiyo ya kiserikali, na wakulima wanaohusika katika mikufu ya thamani. Kwa taarifa za jumla juu ya mikufu ya thamani angalia orodha ya nyaraka mbalimbali za mtandaoni.

Acknowledgements

Imechangiwa na: Vijay Cuddeford, Mhariri mtendaji, Farm Radio International
Imepitiwa upya na: Yogesh Ghore, Msimamizi mkuu wa kipindi, Taasisi ya Kimataifa ya Coady, Chuo kikuu cha Mtakatifu Francis Xavier, Antigonish, Nova Scotia, Canada; Blythe McKay, Meneja, Nyenzo kwa Watangazaji, Farm Radio International; Rex Chapota, Mkurugenzi mtendaji, Farm Radio Malawi.

Information sources

Making the connection: The rise of agricultural value chains. Spore, Julai 2012, toleo maalum. http://spore.cta.int/hs/pdf/spore-hs-2012-en.pdf
KIT, Faida MaLi na IIRR. 2006. Chain empowerment: Supporting African farmers to develop markets. Royal Tropical Institute, Amsterdam; Faida Market Link, Arusha; na International Institute of Rural Reconstruction, Nairobi. http://www.mamud.com/Docs/chains.pdf
Mary McVay na Alexandra Snelgrove, 2007. Program Design for Value Chain Initiatives. Mennonite Economic Development Associates. http://www.meda.org/images/stories/ML/Program_Design_Toolkit.pdf
Jonathan Mitchell, Jodie Keane, na Christoper Coles, 2009. Trading up: How a value chain approach can benefit the rural poor. COPLA Global: Overseas Development Institute. http://www.odi.org.uk/resources/docs/5656.pdf
Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, Mguko wa kimataifa kwa ajili ya maendeleo ya kilimo, na Shirika la Kazi Duniani, 2010. Gender and Rural Employment Policy Brief #4: Agricultural value chain development: Threat or opportunity for women’s employment?

gac-logoMradi umefanywa kwa msaada wa Serikali ya Kanada kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Kanada (CIDA)