Matangazo ya redio kuhusu COVID-19 – Sehemu ya kwanza

Afya

Script

Tangazo 1

SFX:
MAKELELE YA KUKU
MSIMULIAJI:
Kwenu wakulima!

Kuna uvumi wa uwongo unaozunguka kwamba kuku na wanyama wengine wanaweza kuambukiza wanadamu ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19). Hii sio kweli! Hakuna ushahidi wowote kwamba mnyama wa aina yoyote anaweza kuambukiza binadamu ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19).

Maambukizi ya binadamu husababishwa na mgusano kati ya mtu na mtu au kugusa nyuso za vitu vyenye maambukizi.

Unaweza kukaa salama kwa kuzingatia suala la usafi kwenye shamba lako na suala la kukaa mbali kati ya mtu na mtu, ambayo inamaanisha kukaa angalau mita moja kutoka kwa mtu yeyote ambaye sio wa kutoka katika kaya yako au shamba.


Tangazo 2

MSIMULIAJI:
Kunywa pombe HAKUKUKINGI dhidi ya COVID-19!

Ndio, Shirika la Afya Ulimwenguni linapendekeza kutumia visafisha au vifuta mikono vyenye kileo/pombe ili kupambana na COVID-19. Lakini hapana – KUNYWA pombe HAKUKUKINGI au kutibu COVID-19.

Kwa kweli, kunywa pombe mara kwa mara au kupita kiasi kunaweza kukuongezea hatari ya matatizo ya kiafya kama vile saratani hadi uharibifu wa ini.


Tangazo 3
MUME:
Nilienda kwenye duka la dawa leo na hautaamini nilichokiona!
MKE:
Nini?
MUME:
Hakukuwa na dawa za kuua vimelea (antibiotics)! Makabati yote ya kuweka dawa hayakuwa na kitu! Kwa kweli, hakuna mahali ambapo dawa hizi za kuua vimelea zinapatikana katika mkoa wote. Lazima watu watakuwa wanafikiri dawa hizi zinazuia COVID-19!
MKE:
(TWETA) Hii ni hatari. Ikiwa watu wengi wananunua kwa sababu zisizo sawa, nini kitatokea kwa watu ambao wanazihitaji dawa hizi?
MSIMULIAJI:
Dawa za kuua vimelea SIO fanisi kuzuia au kutibu COVID-19. Dawa za kuua vimelea hazifanyi kazi dhidi ya virusi, ni kwa ajili tu ya vimelea (antibiotics). COVID-19 ni Kirusi.

Usinunue dawa ambazo hazijathibitishwa kisayansi kwamba zinatibu COVID-19. Kama utafanya hivyo, watu wengine ambao watakuwa wanazihitaji kwasababu nyingine za matatizo ya kiafya watashindwa kuzipata.


Tangazo 4

MTU #1:
Shangazi yangu anafanya vitu vya tofauti siku hizi. Unapaswa kuona vitu ambavyo anafanya.
MTU #2:
Kama nini?
MTU #1:
Anaendelea kufanya mambo mbalimbali kujikinga na ugonjwa wa virusi vya coronana. Anakunywa limau na baking soda, vitunguu saumu, kuchemsha machungwa na kupumua kwenye mvuke (kujifukiza)… anasema inamuweka salama.
MTU #2:
Hiyo inakuwa kama habari ya kughushi kwangu. Kama ingekuwa rahisi hivyo kuzuia virusi vya corona, hakika isingekuwa tatizo kubwa hivyo.
MSIMULIAJI:
Kuna uvumi wa uwongo kwamba baadhi ya vitu vingine vinaweza kuponya au kuzuia kuambukizwa COVID-19. Lakini kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni, hakuna matibabu au chanjo ya ugonjwa huo.

Njia bora ya kuzuia virusi kuenea ni kuosha mikono yako mara kwa mara, kudumisha angalau umbali wa mita moja kati yako na mtu anayepiga chafya au kukohoa, epuka kugusa uso wako, na kufunika mdomo wako na pua na kiwiko chako au tishu wakati wa kukohoa au kupiga chafya.


Tangazo 5

MTU #1:
Wow, jua leo linawaka hasa!
MTU #2:
Ndio, msimu wa kiangazi mwaka huu hauhimiliki.
MTU #3:
(KICHEKO) Lakini unajua jambo zuri kuhusu joto hili ni kwamba litaua virusi vya corona.
MTU #1:
(KICHEKO) Rafiki yangu, kama hiyo ingekuwa ni kweli, kungekuwa hakuna kabisa virusi vya corona Afrika!
MSIMULIAJI:
Kujiweka kwenye jua au kwenye joto zaidi ya nyuzi joto 25 HAKUZUII COVID-19. Nchi zilizo na hali ya hewa ya moto zimeripoti visa vingi vya COVID-19. Unaweza kupata maambukizi ya COVID-19, haijalishi hali ya jua au joto iko vipi.

Ili kujikinga, hakikisha unasafisha kabisa mikono yako mara kwa mara na epuka kugusa macho yako, mdomo na pua.


Tangazo 6

MSIMULIAJI:
Kuoga maji ya moto au kutumia vikausha mikono HAKUTAKUKINGA kupata maambukizi ya COVID-19.

Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni, tiba zingine zinaweza kusaidia kupunguza dalili za COVID-19. Lakini hakuna ushahidi kwamba dawa YOYOTE ya sasa au shughuli zinaweza kuzuia au kuponya ugonjwa huo.

Tangazo 7

MTOTO:
Yummmm … Mama, hii supu leo ina ladha nzuri! Umefanya nini?
MAMA:
Nimeongeza vitunguu saumu vya ziada. Nilisikia kwamba kula vitunguu saumu kutatuzuia kupata virusi vya corona. Ninaiweka katika kila kitu, pamoja na chai yako!
MTOTO:
(ANAKUNYWA CHAI KIDOGO NA KUITEMA) Yuck!
MSIMULIAJI:
Kula vitunguu saumu HAKUSAIDII kuzuia kuambukizwa COVID-19. Vitunguu saumu ni chakula cha afya ambacho kinaweza kusaidia kupambana na magonjwa kadhaa. Lakini hakuna ushahidi kwamba kula vitunguu saumu kunaweza kulinda watu dhidi ya COVID-19.


Tangazo 8

SFX:
SAUTI YA MMBU. SAUTI YA KUPIGWA KIBAO NA MKONO.
MTU:
Aha! Kama vile malaria haitoshi, sasa inabidi nihofie kuhusu mmbu kunipa virusi vya corona.
MSIMULIAJI:
COVID-19 HAIWEZI kuambukizwa kupitia kung’atwa na mmbu.

COVID-19 huenea kupitia matone yanayotoka wakati mtu aliyeambukizwa anakohoa au kupiga chafya, au kupitia matone ya mate au matone yanayotoka kwenye pua wakati wa kupumua.


Tangazo 9

MTU #1:
Hey tazama! Naweza kuzuia pumzi yangu kwa zaidi ya sekunde 10. Madaktari wanasema hii inamaanisha kwamba sina COVID-19.
MTU #2:
Kweli? Ngoja nijaribu! (ANAVUTA SANA HEWA NDANI NA BAADA YA HAPO ANAANZA KUKOHOA)
MTU #3:
Rafiki yangu! Unajaribu kujiua? Unajua kuwa kipimo cha maabara ndiyo njia pekee ya uhakika ya kujua ikiwa una COVID-19!
MSIMULIAJI:
Usidanganyike. Kuwa na uwezo wa kushikilia pumzi yako kwa sekunde 10 au zaidi bila kukohoa au kuhisi usumbufu HAINA maana unakuwa huru dhidi ya COVID-19.

Shirika la Afya Ulimwenguni linawashauri watu ambao wanafikiria wanaweza kuwa na maambukizi ya COVID-19 kukaa nyumbani na kutafuta matibabu kwa kupiga simu mamlaka zao za afya.

Njia PEKEE ya kuthibitisha kama una virusi vya COVID – 19 ni vipimo vya maabara. Hauwezi kuthibitisha hili kwa kutumia zoezi hili la kupumua – ambalo linaweza kuwa hatari!


Tangazo10

MSIMULIAJI:
Virusi vya corona SIYO hukumu ya kifo!

Karibu 80% ya watu ambao wameambukizwa wana magonjwa tu dhaifu na hupona kabisa. Lakini wanaweza kukumbana na changamoto tofauti – unyanyapaa. Watu wanaweza kuwaepuka wale ambao wamewahi kuambukizwa, au kusema vitu vibaya juu yao au kuwatendea vibaya.

Unyanyapaa wa aina hii unaweza hata kuzuia watu kwenda kupimwa! Kubagua watu waliopona kunapaswa kuachwa. Tuangiliane na tulinde kila mtu wakati wa nyakati hizi ngumu. Sote tuko pamoja katika janga hili.


Tangazo 11

SFX:
KUKUHOA NA KUPIGA CHAFYA
MSIMULIAJI:
COVID-19 inaambukiza sana! Je! Unajua jinsi inavyoenea?

Watu wanapata maambukizi ya COVID-19 kutoka kwa watu wengine ambao wana virusi vya ugonjwa wa corona. Unasambaa kupitia matone madogo yanayozalishwa wakati mtu mwenye maambukizi anakohoa, anapiga chafya au anatoa hewa nnje wakati wa kupumua. Matone haya yanaweza kuvutwa na watu walio karibu au yanaweza kutua katika nyuso za vitu vilivyo karibu. Watu wanapovuta matone haya wakati wa kupumua au kugusa nyuso ya vitu vyenye matone haya, na kugusa macho yao, pua au mdomo, wanaweza kuambukizwa.

Kwahiyo jilinde na uwalinde pia wenzako. Vaa barakoa uwapo maeneo ya umma, weka umbali wa mita 1 kutoka kwa watu wengine, na osha mikono yako kadri inavyowezekana.


Tangazo 12

SFX:
KUKUHOA NA KUPIGA CHAFYA
MSIMULIAJI:
Sikia hiyo? Kikohozi cha kawaida kinaweza kuwa ishara ya kitu hatari zaidi. COVID-19 ni ugonjwa wa kuambukiza unaoathiri mapafu. Unaenea wakati mtu mwenye afya anapogusana na matone kutoka kwa macho, pua au mdomo wa mtu aliyeambukizwa.

Kuzuia kusambaa kwa COVID-19, kila mara funika mdomo na pua yako kwa kiwiko cha mkono wako au tishu pale unapopiga chafya au kukohoa. Tupa tishu iliyotumika punde tu baada ya kumaliza.

Kwa kufuata kanuni hizi, unaweza kuwakinga watu wanaokuzunguka dhidi ya COVID-19 na virusi vingine kama vile homa na mafua.


Tangazo 13

MSIMULIAJI:
Wewe ni mfanyabiashara anayefanya kazi katika soko?

Ikiwa ndio, nafasi ni kwamba unakutana sana na pesa za karatasi na sarafu siku nzima. Lakini pesa ni chafu na inaweza kubeba virusi kama COVID-19.

Kwahiyo kipi unachoweza kufanya? Vaa glavu wakati unaposhika pesa na mara tu baada ya hapo osha mikono yako kwa maji na sabuni kwa muda usiopungua sekunde 20 baada ya kugusa pesa na bidhaa. Kama inawezekana, jaribu kutumia njia za kielektroniki kuhamisha pesa ili kuepuka kugusa pesa.


Tangazo 14

MSIMULIAJI:
Nani yupo hatarini zaidi kupata virusi vya corona?

Ni wana familia za watu walioambukizwa na wafanyakazi wa afya.

Kwanini?

Kwasababu wanakutana sana na watu wenye maambukizi. Lakini wakati mwingine watu wenye maambukizi hawana dalili zozote.

Ndio maana ni muhimu sana kujikinga na kuwakinga wengine kwa kuvaa barakoa, kuosha mikono yako mara kwa mara kwa maji na sabuni, na kukaa umbaki wa angalau mita 1 kutoka kwa watu wengine kuepuka kusambaa kwa maambukizi.


Tangazo 15

BINTI:
Mama, inabidi niende sokoni leo kuuza mavuno ya nanasi.
MAMA:
(AKIWA NA HOFU) Oh! Sipendi wazo la wewe kuwa karibu na watu wengine wengi wakati wa janga hili la virusi vya corona.
BINTI:
Sipendi pia, lakini tunaweza kufanya nini? Ukulima ni riziki yetu na soko ndio mahali pekee pa kupata pesa kwa ajili ya chakula na vitu vingine.
MAMA:
Lakini utajikinga vipi? Sitaki wewe uumwe!
BINTI:
Nitavaa barakoa siku nzima. Basi linachukua tu abiria wachache ili kuruhusu abiria kukaa kwa mbali na kuachiana nafasi. Nawaomba pia wateja walipe kwa njia ya simu ili nisiguse fedha za karatasi au sarafu.
MAMA:
Vipi kuhusu kuosha mikono yako?
BINTI:
Nitaosha mikono yangu kila mara kwa kutumia bomba lililopo sokoni. Nimesikia kuna muuzaji mpya ambaye anauza sabuni na vitakatishi kwahiyo nitanunua kiasi fulani na kuleta nyumbani kwa ajili yako na baba.
MAMA:
Kuwa mwangalifu sana na uwe salama ili uweze kurudi nyumbani kwa ajili yangu, binti yangu.


Tangazo 16

MTU #1:
(GUMIA) Jiji limefungwa kwa kipindi cha muda mrefu.
MTU #2:
Ndio, watu wanapata shida kabisa.
MTU #1:
Nafikiria kurudi kijijini kwangu. Naweza pia kutumia muda na familia yangu. Bibi yangu anazeeka sana sasa.
MTU #2:
Sidhani kama hilo ni wazo zuri. Unaweza kupeleka virusi vya corona kijijini bila hata kujua! Virusi vinaweza kuishi juu ya nyuso- fikiria jinsi basi linaweza kuwa chafu. Na unajua baadhi ya watu wanaweza kuwa na virusi bila kuwa na dalili zozote. Itakuwa vibaya kueneza virusi vya corona kwa familia yako bila kufahamu. Fikiria kuhusu bibi yako!
MTU #1:
Ah, Nadhani uko sahihi. Sisi sote ni salama ikiwa tutakaa nyumbani. Badala yake labda ninapaswa kuwapigia simu.
MTU #2:
Nina hakika wataelewa na kuthamini hilo.


Tangazo 17

BABA:
Mwanangu, wakati ukiwa mtoto mdogo, ugonjwa mbaya unaoitwa Ebola ulienea Afrika Magharibi. Watu wengi walipoteza maisha. Sasa, kuna ugonjwa mwingine mbaya ambao unaenea, lakini wakati huu ugonjwa huu ni mbaya zaidi.
MWANA:
Ugonjwa huo ni nini?
BABA:
Unaitwa virusi vya corona au COVID-19. Unasambaa kwa haraka sana kote ulimwenguni.
MWANA:
(ANAOGOPA) Sisi wote tutaumwa?
BABA:
Njia nzuri ya kuzuia kuugua ni kukaa nyumbani na kupunguza kukutana na watu wengine. Hii ni kwa sababu virusi huenea miongoni mwa watu pale wanapokohoa au kupiga chafya. Kwa hivyo lazima kila wakati tuvae barakoa, kuosha mikono yetu mara kwa mara kwa maji na sabuni, na kuepuka kugusa macho yetu, pua na mdomo.
MWANA:
Tunapaswa kufanya hivyo kwa muda gani?
BABA:
Ni ngumu kusema. Lakini lazima tuzingatie habari kutoka kwa mamlaka zetu za afya na Shirika la Afya Ulimwenguni. Watu watavyochukua tahadhari zaidi za usalama, maisha yetu yatarudi katika hali ya kawaida mapema.


Tangazo 18

MTU 1:
Wazee katika jamii yetu wana busara sana.
MTU 2:
Nakubali. Tunapaswa kupewa heshima zote!
MTU 1:
Vizuri, njia moja ya kuwaheshimu ni kuchukua hatua za ziada za kuwaweka salama dhidi ya virusi vya corona, ambavyo vinaathiri watu wazee kuliko vijana!
MSIMULIAJI:
Ni muhimu tuwalinde dhidi ya virusi vya corona watu ambao ni wazee na kila mtu aliye na hali ya kiafya kama ugonjwa wa kisukari, matatizo ya moyo, na saratani.

Virusi vya corona vinaweza kuwa hatari zaidi, kwa hivyo ongeza ufahamu na fanya kila uwezavyo kuzuia usisambaze. Ikiwa wewe au mtu yeyote katika kaya yako ana kikohozi, anapata ugumu wakati wa kupumua, au homa ya ghafla, hata ikiwa dalili zako ni ndogo, kaa nyumbani.

Usiende sokoni. Usiende mjini. Na usiwatembelee ndugu wengine. Ikiwa dalili zako zinazidi kuwa mbaya, nenda hospitalini kwa ajili ya matibabu.

Jilinde na uwalinde wengine kwa kuvaa barakoa, kaa umbali wa angalau mita moja kutoka kwa watu wengine, na kuosha mikono yako mara kwa mara.

Acknowledgements

Shukrani

Imechangiwa na: Maxine Betteridge-Moes, mwanahabari huru na mshauri wa zamani wa rasilimali Utangazaji wa FRI Ghana.

Rasilimali hii imeandaliwa kwa msaada wa kifedha wa Serikali ya Canada iliyotolewa kupitia Global Affairs Canada