Jinsia na Vipindi vya redio vya mkulima

Ujumbe kwa mtangazaji

Pakua na hariri taarifa hii kwa matumizi yako.

Muhtasari kwa Mtangazaji

Waraka huu wa habari huwapa mwogozo watangazaji wa redio juu ya mada ya jinsia na usawa wa kijinsia. Utakupa baadhi ya fasili za msingi, na kweli kadhaa na takwimu juu ya hali ya kutokuwa sawa kati ya wanaume na wanawake. Unatoa mwongozo juu ya jinsi ya kuwafikia wanaume na wanawake kwa pamoja, kuwahusisha kwenye kipindi chako na kuwapatia taarifa wanazohitaji. Pia unaonesha mambo ya kuzingatia ili kuhakisha kipindi chako kinaheshimika kwa wasikilizaji wote, wanaume kwa wanawake. Mwisho, waraka huu wa habari unakuhimiza kuzingatia usawa wa kjinsia katika kituo chako.

Script

Utangulizi.
Wanawake katika eneo la Afrika kusini mwa jangwa la sahara wana jukumu la kusimamia nusu ya kazi za shambani. Kwa hiyo wanawake watakuwa sehemu muhimu ya hadhira yako.

Kuna masuala sugu na yaliyokita mizizi ambayo huwaathiri wakulima wanawake yanayohusiana na hali ya kutokuwa sawa kati ya wanaume na wanawake. Kwa mfano, wanawake wanaweza wasiwe na haki ya kumiliki ardhi, au waume zao wanaweza wakawa ndio wanapangilia namna mapato ya shambani yanavyopaswa kutumika, licha ya wanawake ndio wanaofanya kazi kubwa za shambani. Ili kuwahudumia vizuri wasikilizaji, utatakiwa kuelezea masuala muhimu sana ambayo wakulima wa kike hukabiliana nayo, pia vilevile ambayo wakulima wa kiume hukabiliana nayo.

Hebu tuanze na baadhi ya fasili.

Fasili muhimu

Mara nyingi mtangazaji analazimika kutafsiri na kutumia maneno na vifungu vya maneno katika lugha mama. Ili kufanya vizuri, ni muhimu kuzielewa istilahi hizi kabla hujazitumia hewani. Kuna maneno na vifungu vya maneno vichache ambavyo hujitokeza sana amabapo suala la jinsia linapozungumziwa. Tutatoa fasili kwa baadhi ya maneno hayo na vifungu vya maneno.

Jinsi: Ni tofauti majumui na ya kibiolojia kati ya wanaume na wanawake. Jinsi ni kitu unachozaliwa nacho.

Jinsia: Ni mgawanyiko wa majukumu ya kijamii ya wanaume na wanawake, tabia na mitazamo yao inayotazamiwa na jamii. Kwa mfano, karibu ulimwenguni kote, wanawake hufanya kazi za ndani zaidi kuliko wanaume. Tofauti na jinsi, hiki ni kitu kinachobadilika kulingana na wakati na tofauti za tamaduni.

Mgawanyo wa majkumu: Hii hurejelea jinsi kazi zinavyogawanywa kwa wanaume na wanawake katika utamaduni au jamii mahususi, na jinsi kazi za wanaume na wanawake zinavyothaminiwa. Kwa ujumla kazi za wanaume hulipwa vizuri, huchukuliwa kuwa ni za muhimu zaidi, imechukuliwa kuwa ni kawaida na inahesabiwa katika takwimu za taifa. Kinyume chake, kazi za wanawake hazilipwi vizuri au hazilipwi kabisa, zina Chukuliwa kuwa zina umuhimu mdogo, ni za msimu, za muda mfupi, na “zisizoonekana.”

Fursa na udhibiti: Dhana hizi mbili zina tofauti kubwa. Kwa mfano, mkulima anaweza kuwa na fursa ya ardhi (hii ina maana kwamba, anaweza kulima kwenye ardhi ambayo inamilikiwa na mtu mwingine), lakini hana udhibiti wa ardhi (hii ina maana kwamba hamiliki ardhi na hana uwezo wa kuamua jinsi gani ardhi hiyo itumike). Hivyo, wanawake wanaweza kuwa na fursa katika rasilimali muhimu, lakini bila udhibiti wa rasilimali hizo, wana machache ya kusema katika maamuzi juu ya rasilimali hizo.

Usawa wa kjinsia: Katika usawa wa kijinsia, wanawake na wanaume wote wana haki sawa, na matamanio yao na mahitaji huchukuliwa sawa. Katika kusisitiza usawa wa kijinsia huhusisha:

  • kuhamasisha ushiriki sawa wa wanawake na wanaume katika kufanya maamuzi.
  • kuwasadia wanawake na wasichana ili kutumia haki zao kikamilifu.
  • kupunguza pengo la fursa, udhibiti na faida zitokananzo na rasilimali kati ya wanaume na wanawake.

Sasa ni baadhi ya kweli kuhusu hali ya kutokuwa na usawa wa kijinsia.

Baadhi ya kweli.
Kweli na takwimu hapa chini huchora picha halisi ya hali ya kutokuwepo na usawa kati ya wanawake na wanaume katika kilimo na vyombo vya habari Afrika na ulimwenguni kote. Huonesha hitaji kubwa kwa vipindi vya redio vya mkulima vinavyohamasisha usawa wa kijinsia.

Jinsia na kilimo.
Wanawake katika kilimo na wanawake katika maeneo ya vijijini wana fursa ndogo na udhibiti mdogo katika rasilimali zinazohitajika kuzalisha mazao na mifugo, na fursa ndogo katika kuboresha maisha yao. Pengo la kijinsia linapatikana maeneo mengi: ardhi, mifugo, na teknolojia. Pengo hili haliwaumizi wanawake peke yao tu, lakini pia sekta ya kilimo, uchumi, na jamii kwa ujumla. Kuziba pengo la kijinsia katika kilimo itaweza kusaidia sekta ya kilimo na jamii kwa ujumla. Kwa mfano, kama wanawake wangekuwa na fursa sawa katika rasilimali kama wanaume wangeweza kuongeza mavuno ya mashamba yao kwa asilimi 20 – 30.

Vyombo vya habari na wanawake.
Mradi wa utafiti wa hivi karibuni ulipata tofauti zifuatazo za kijinsia katika taarifa za habari:

    Aslimia 24 tu ya wahusika katika magazeti, redio na televisheni walikuwa wanawake; asilimia 76 walikuwa wanaume.
  • Mwanamke mtaalam mmoja tu kati ya wataalamu watano waliohojiwa katika vyombo vya habari.
  • Asilimia 37 ya habari zilizoripotiwa kwenye televisheni, redio na katika magazeti zilitolewa na waandishi wanawake.
  • Takribani nusu (asilimia 46) ya habari ziliendeleza mawazo mgando juu ya masuala ya kijinsia, wakati asilimia 6 tu zilikosoa mawazo hayo.
  • Wanawake walikuwa ni mara nne zaidi ya wanaume kurejelewa kwa kigezo cha mahusiano, mfano; kama mke, mama, nk.

Wanawake na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
TEHAMA mpya kama vile wavuti huweza kutoa fursa kwa wanawake, lakini wanawake katika nchi zinazoendelea wanafursa ndogo katika kupata mifumo yote ya teknolojia. Baadhi ya wanawake ni wajuzi katika kutumia TEHAMA lakini wengi wao sio wajuzi. Kuna mgawanyiko wa pekee wa “kidijiti” kati ya wanaume na wanawake. Na matokeo yake, mazingira ya mtandaoni kwa kiwango kikubwa yamekuwa yakitengenezwa na wanaume na kwa ajili ya wanaume. Suala hili limeongeza mgawanyiko wa kidijiti na mawazo mgando hasi juu ya wanawake. Ni muhimu kutambua na kuondoa huu mgawanyiko wa kidijiti kwa kuhakikisha kwamba wanawake wanapata mafunzo stadi, na kuwafundisha wanawake wengine kwa ujuzi stadi.

Sasa ni muda wa kuanza kufikiri juu ya jinsia na kipindi chako cha mkulima.

Jinsia na kipindi chako cha mkulima.

Mgawanyo huu hapa chini umeandaliwa ili kukusaidia kuandaa kipindi kinachoelezea masuala ya kijinsia na kinacho wahudumia wakulima wanawake, pia wakulima wanaume.

Mahitaji tofauti
Wakulima wanawake na wanaume huwa wanakuwa na mahitaji tofauti ya taarifa na mawasiiano. Wanapatikana kusikiliza redio kwa nyakati tofautitofauti za siku, na wanaweza wakawa na upendeleo tofauti katika habari, muundo na maudhui.

Unapotembelea jamii ya wasikilizaji kufanya utafiti wa hadhira, hakikisha unazungumza na wasiklizaji wote wanaume kwa wanawake na chukua tofauti yoyote unayoiona katika upendeleo wao. Hizi hapa ni baadhi ya hatua unazoweza kuchukua kuhakikisha kuwa kipindi chako cha mkulima kinakidhi mahitaji ya wanawake na wanaume kwa pamoja:

  • Simulia habari zako kwa zamu. Kwa mfano, wakati fulani unaweza ukajikita katika masuala yenye umuhimu kwa wakulima wanawake, na wakati mwingine unaweza ukajikita katika masuala yenye umuhimu kwa wakulima wanaume.
  • Vipindi vya mkulima virudiwe angalau mara moja kwa wiki. Hakikisha kuwa moja au zaidi ya marudio ya kipindi yanatangazwa katika muda ambao ni muafaka kwa wanawake kusikiliza.
  • Fikiri juu ya hadhira yako yote wakati unapokuwa unatangaza. Kwa mfano, hata kama sehemu za kipindi chako kinawagusa zaidi wanaume, hakikisha kuwa maudhui hayo yanawaheshimu wanawake. Na sio kinyume chake.
  • Kipindi chako kinapokuwa kimelenga masuala yenye umuhimu mkubwa kwa wote, wanawake kwa wanaume, chukua muda kujifunza namna tofauti ambazo wanaume na wanawake wanaathiriwa na suala hilo, na jinsi wanavyoweza kukabiliana nalo. Kwa mfano kama suala ni kupungua kwa rutuba ya udongo, wanaume na wanawake wanaweza wakawa na mahitaji tofauti na suluhisho tofauti: wakulima wanaume wanaweza wakawa na uwezo wa kununua mbolea za viwandani wakati wakulima wanawake wakachagua njia ya kupanda kunde kwenye mazao mengine.

Utafiti juu ya wanawake na jamii ya redio nchini Liberia, Sierra Leone na Guinea ulibaini kuwa ni wanawake wachache sana wanaofanya kazi redioni. Katika baadhi ya vituo, hata vipindi vya wanawake vilikuwa vinaendeshwa na wanaume. Wanawake waliokuwa wanahojiwa katika utafiti walisema kuwa hata mwanaume aliyepata mafunzo bora zaidi asingeweza “kutoa ujumbe kwa namna ambayo wanawake wangeweza kuupokea vizuri.” Utafiti ulibainisha kuwa wanawake wanavutiwa sana na uchumi na siasa, lakini huwa hawasikilizi au kushiriki katika vipindi vya redio vinavyo zungumzia masuala hayo kwa sababu vipindi hivyo vimetekwa na wataalamu wanaume na mitazamo ya wanaume.

Utafiti ulibainisha kwamba wanawake wanataka kushiriki katika redio jamii lakini vituo vya redio haviwahusishi kikamilifu wakati wa vipindi, na kwa sababu sauti za wanawake hazisikiki hewani. Mara nyingi sana hata wakati ambapo kituo kinaendesha kipindi cha wanawake, huelezea kwa ufinyu sana masuala yanayohusu wanawake, hujikita tu katika ndoa, uangalizi wa mtoto au majukumu ya kifamilia.

Kufanya ubia na mashirika ya ndani yanayojikita katika masuala ya kijinsia
Kunaweza kukawa na shirika lisilo la kiserikali au asasi ya kiraia inayofanya kazi na jamii za vijijini ili kuboresha maisha ya wanawake wa vijijini. Kama ndio hivyo, itakuwa ni tija kufanya nao kazi. Shirika lisilo la kiserikali linaweza kukuelezea shughuli zake na kukukusaida kuelewa masuala ya kijinsia na masuala ya kilimo katika jamii, na ukapata mawazo juu ya namna ya kuingiza vitu vinvyogusa masuala ya kijinsia katika kipindi chako.

Mashirika haya yanaweza yakawa yanazijua jamii za vijijini ambazo zimefanikiwa kuelezea masuala ya usawa wa kijinsia na kuboresha maisha ya wakulima wanawake na wanaume. Mifano kama hii inaweza kutengeneza habari ya redio ya kuvutia. Wasikilizaji kutoka katika sehemu nyingine wanaweza kuhamasika kuiga mbinu yao.

Kupanga kukutana na wanawake
Wanawake wanashughulika sana. Hii inasaidia kujua mahali ambapo wakulima wanawake hukusanyika na muda ambao wanaweza kuzungumza. Unaweza usikutane nao kwa muda mrefu, na unaweza kupanga muda wa kukutana nao kama huna muda wa kuuliza maswali yako yote. Unatakiwa kuwahimiza wanawake kuja na watoto wao kwenye mkutano. Hii itafanya wasichana wengi kuhudhuria.

Kuwahoji wanawake
Inashauriwa kwa nguvu zote kwamba ufanye mkutano unao jumuisha wanawake wote. Pengine wanaume hawatapenda kuhudhuria mkutano huo, na hivyo wanawake watahamasika kuzungumza kwa kusikia wanawake wengine wakifanya hivyo. Hii inaweza kupelekea mjadala mzito na wa kina.

Kwa kutegemeana na desturi za kiutamaduni na kidini, kuwahoji wanawake kunaweza kukawa tofati kuliko unavyowahoji wakulima wanaume.

Mambo muhimu ya kuzingatia endapo wewe ni mwanaume ukimhoji mwanamke:

  • Ni lazima mume awepo kwa ajili ya mahojiano?
  • Je unahitaji mtu wa kuambatana naye wakati unapofanya mahojiano?
  • Je, mume atakuwa anamruhusu mwanamke kujibu maswali badala ya kujibu yeye mwenyewe?

Mambo muhimu ya kuzingatia endapo wewe ni mwanamke ukimhoji mwanamke mwingine:

  • Je, inatakiwa mume awepo kwa ajili ya mahojiano?
  • Je, mwanamke anaweza kujibu maswali bila kuomba maoni ya mume wake?

Uandaaji wa kipindi.
Farm Radio International imeandaa mambo ya kuzingatia yafuatayo ili kusaidia kipindi chako kiwe kinajali masuala ya kijinsia.

Masuala ya kuzingatia ya jinsia kwa ajili ya kipindi chako.
Zingatia hoja zifuatazo unapokuwa unaandaa kipindi chako. Unaweza kushindwa kukidhi hoja hizi zote kila wakati, kwa kuzisisitiza wakati utakapoweza, utasaidia kuhakikisha kwamba sauti na mitazamo ya wanaume na wanawake imewasilishwa vizuri.

Wanaume na wanawake wamewakilishwa?

  • Je, majukumu muhimu ya uandaaji na ya kurusha kipindi, yako wazi kwa wanaume na wanawake?
  • Kama mwandaaji wa kipindi ni mwanaume, je, kuna wanawake wanaosaidiana naye ambao wanaweza kuchangia mawazo yao katika masuala ya uandaaji? (Na kinyume chake).
  • Kama mtangazaji ni mwanaume, kuna majukumu mengine muhimu ya kurusha kipindi yanayofanywa na wanawake? (Na kinyume chake).
  • Kipindi chako kinatoa muda sawa kwa masuala na sauti za wanaume na wanawake?
  • Je, wanawake unaowahoji wanawakilisha tamaduni na matabaka tofaotitofauti? Kwa mfano, kama unamhoji mwanamke kutoka kundi moja la kikabila katika eneo lako, fikiria kusisitiza mitazamo ya wanawake wengine kutoka makudi mengine ya kikabila.
  • Baadhi ya wanawake (na wanaume) ni vigumu kuwafikia kwa sababu wanaishi katika maeneo ya mbali sana. Je, umefanya utaratibu wowote ili kuwafikia watu hawa ili kusudi visa vyao visimuliwe?

Uchoraji wa wanaume na wanawake.

  • Je, kipindi chako kinaakisi mwonekano halisi wa wanawake na wanaume, je, wanaume na wanawake wanajitokeza kikamilifu katika shughuli (kwa mfano sio tu katika kazi za nyumbani kama ni wanawake)?
  • Je, watu wote wanachukuliwa katika hali ya utu katika habari unazoziandaa?
  • Je, habari zako na kipindi kizima kinakosoa mawazo mgando juu ya jinsia? Kwa mfano, je, unawawakilisha wanawake kama watu wenye majukumu mengi katika jamii, kuliko majukumu ya msingi kama mama, mke, au binti?
  • Je, uzoefu na masuala yanayowahusu wanawake yanachukuliwa kwa umakini? Je, yanawasilishwa kuwa sawa na uzoefu na masuala yanayo wahusu wanaume?

Lugha

  • Je, unatumia lugha inayowajumuisha wanaume na wanawake? Kwa mfano katika kiingereza, badala ya “mankind” tumia “humankind.” Badala ya “man-made” tumia “manufactured.” Badala ya “policeman” tumia “police officer”. Je, umepata au umeunda maneno katika lugha yako ambayo hujumuisha wanawake na wanaume?
  • Je, unaepuka kutumia vivumishi ambavyo haviendani au vinaendeleza mawazo mgando juu ya jinsia? Wakati mwingine waandishi au watangazaji wa redio wanampambanua mwanamke kama “mrembo” au “anayevutia” wakati ambapo mwonekano wa mwanamke hauna uhusiano wowote na habari. Wanaume zaidi, hupambanuliwa kama “wachapakazi” au “waliofanikiwa.” Mtazamo wa namna hiyo huthamini tu kile ambacho wanaume hukifanya na huthamini wanawake kama chombo cha starehe tu. Wote kwa pamoja wanawake na wanaume wanastahili kitu bora zaidi ya hicho katika kipindi chako cha redio.

Kabla hatujamaliza ni wakati wako sasa kufikiria juu ya usawa wa kijinsia katika kituo chako.

Kwenye kituo chako.
Tulikuwa tumejikita zaidi katika namna kipindi chako cha redio kinavyoweza kuhudumia wanaume na wanawake kwa namna ambayo huheshimu jinsia na mahitaji yao. Ni muhimu pia kuangalia ni kwa jinsi gani masuala ya kijinsia yanavyoweza kuzungumziwa katika kituoa chako cha redio.

Baadhi ya maswali unayoweza kuyafikiria:

  • Wanaume wangapi na wanawake wangapi wanafanya kazi katika kituo chako cha redio? Kwa nini pawepo na wanaume wengi au wanawake wengi?
  • Je kuna nafasi ambayo hupenda kukaliwa zaidi na wanaume au wanawake? Kwa nini? Je, iendelee kuwa hivi?
  • Je, wanawake wana fursa ya kufanya kazi muhimu na zinazovutia katika kituo chako? kama sio, kwa nini, na hatua gani zinaweza kuchukuliwa kufanya kituo chako kiwe na usawa wa kijinsia?
  • Je, kituo chako kina sera inayounga mkono usawa wa kijinsia, katika ufanyaji kazi na katika uandaaji wa vipindi? Kama sio, kwa nini, na hatua gani zinaweza kuchukuliwa kuboresha suala hili?
  • Je, mtafanyaje wewe na mwenzako kufanya mazingira yenu ya kila siku ya kazi yawe sehemu ya usawa kwa wanaume na wanawake?

Baadhi ya wanawake wanafanya kazi katika vyombo vya habari lakini wachache ndio huchukua nafasi za kutolea maamuzi au nafasi zinazohitaji ufundi stadi. Wanawake pia wanapaswa kuwakilishwa katika suala la umiliki na katika vyombo vya kutolea maamuzi kama vile bodi au kamati za ushauri vilevile kuhakikisha wanakuwa na sauti katika kuunda sera za kituo.

Mambo yafuatayo yatasaidia kuongeza ushiriki wa wanawake katika vituo vya redio:

  • Anzisha programu ya uangalizi wa watoto, masaa mazuri ya kazi na ratiba za utangazaji ambazo hazitaathiri majukumu mengine ya wanawake.
  • Tengeneza mazingira mazuri ndani na nje ya kituo, ikiwa ni pamoja na njia za kumlinda mwanamke dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia na kero nyinginezo, na kutokuwa na uvumilivu kabisa kwa ukiukwaji wa utu wa mwanamke.
  • Hakikisha kuna mwanga na ulinzi wa kutosha kwenye kituo wakati wa mikutano na nyakati za matangazo, na usafiri salama kwa wanawake ambao inawalazimu kusafiri kwenda na kutoka kituoni, hasahasa nyakati za usiku au siku za sikukuu.

Ili kuhimiza usawa wa kijinsia katika kituo na kuhakikisha wanawake wanasikika hewani, ni muhimu kwamba wanawake wapatiwe mafunzo stadi na wapewe fursa ya kuandaa vipindi.

Kwa ujumla, redio ina nafasi katika:

  • kuchangia kutatua hali ya kutokuwepo usawa wa kijinsia.
  • huongeza uhusishwaji wa wanawake katika nyanja zote za uandaaji na kutoa maamuz.
  • kuhakikisha kwamba sauti za wanawake na mambo yanayowahusu yanakuwa ajenda ya habari za kila siku.
  • wasaidie wanawake kupata ustadi na uhakika wa kuendesha mawasiliano yao wenyewe.
  • Utajikuta kwamba kwa kuongelea masuala ya usawa wa kijinsia kila siku katika kituo chako, inakuwa kawaida kwako kuyaingiza katika vipindi vyako vya redio bila tatizo, mara kwa mara na kwa ufanisi.

Acknowledgements

Imechangiwa na: Vijay Cuddeford, Mhariri mtendaji, Farm Radio International, katika maandishi imetengenezwa na Blythe McKay, Meneja, Nyenzo kwa Watangazaji, Farm Radio International.
Imepitiwa upya na: Doug Ward, Mwenyekiti, Farm Radio International; Kevin Perkins, Mkurugenzi Mtendaji, Farm Radio International; Jessica Tomlin, Mkurugenzi Mtendaji, Match International; Katherine Im-Jenkins, Meneja Mkuu, Kipindi na Maendeleo ya Vipindi, World University Services Canada.

Information sources

Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO), hakuna tarehe. Men and women in agriculture: closing the gap. http://www.fao.org/sofa/gender/key-facts/en/
Shirika la Mawasiliano la Kimataifa (WACC), 2010. Who makes the news?http://www.medinstgenderstudies.org/wp-content/uploads/highlights_en.pdf
Search for Common Ground, 2011. Community Radio, Gender and ICTs in West Africa. http://www.radiopeaceafrica.org/assets/texts/pdf/2012-Community-Radio-Gender-ICT_SFCG.pdf

gac-logoMradi umefanywa kwa msaada wa Serikali ya Kanada kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Kanada (CIDA)