Ujumbe kwa mtangazaji
Pakua na hariri taarifa hii kwa matumizi yako.
Muhtasari kwa mtangazaji.
Redio imejikita katika utamaduni wa masimulizi ya mdomo. Watangazaji hupenda kujiita kuwa ni wasimiliaji wazuri wa hadithi, na ni kwa kusimulia hadithi ndipo tunaweza kuteka na kushikilia umakini wa wasikilizaji wetu. Vipande vyote vya habari lazima viwe na masimulizi, iwe ni drama, mahojiano, majadiliano au namna nyingine.
Waraka huu wa habari wa mtangazaji unapambanua vipengele vya msingi vya hadithi, huonesha vitu vya kuzingatia juu ya ubora wa hadithi makini, huonesha mfano mmoja wa hadithi, na kumaliza na dondoo chache juu ya usimulizi wa hadithi.
Script
Utangulizi
Mifumo mingi ya redio huweza kutumika kuwasilisha masuala mbalimbali katika kipindi cha mkulima – mahojiano, vipindi vya kupiga simu, vipande vya maandishi, mahojiano na watu mitaani, kutaja kwa uchache. Lakini mifumo hii yote huweza kutengenezwa kwa wingi na kwa umakini endapo itasimulia hadithi.
Neno “hadithi” linatumika kwa namna nyingi katika redio. Kwa upana wa fasili yake, inaweza kuwa kitu chochote na kila kitu unachotangaza (kwa mfano: “Je, una hadithi ya Kombe la Dunia?” au “Hivi tuna hadithi ya mabadiliko ya hali ya hewa wiki hii?” au “Kuna hadithi gani juu ya mwimbaji na waziri?”).
Lakini neno “hadithi” pia hutumika katika redio kuelezea aina mahususi sana ya masimulizi. Aina hii ya hadithi ipo katika moyo wa mashujaa wa Kiafrika na tamthiliya za Ki-shakespear na riwaya za kisasa. Aina hii ya hadithi hutumia muundo mahususi sana kuvuta na kuhabarisha na kuhamsisha hadhira yake. Unapokuwa na ujumbe muhimu wa kuwasilisha, ni vema kuweka hadithi katikati yake, na kuibua nguvu ambayo hadithi huweza kuleta.
Kwa kifupi, hadithi ni masimulizi kuhusu
- mtu mwenye kuhisi hisia za wengine (“mtu mwenye kuhisi hisia za wengine” ni mtu ambaye wasikilizaji huweza kuhusiana naye au wanaweza kushirikiana naye katika hisia zake)
- mtu anayekabiliana na vikwazo au matatizo
- na kuchukua hatua kulitatua
Ni rahisi hivyo tu!
Kurudi katika mifano iliyotajwa hapo juu, hadithi ya Kombe la Dunia huweza kuhusisha mlinda mlango bora au mshambuliaji ambaye anavunjika mguu lakini anaendelea kucheza akiwa katika maumivu hadi anapata ubingwa. Hadithi ya mabadiliko ya hali ya hewa inaweza kuhusu familia ya wakulima ambao hupanda katika msimu mfupi mahindi yanayovumilia ukame baada ya kipindi kirefu cha kiangazi kuharibu mahindi ya msimu mzima. Na hadithi kuhusu mwimbaji na waziri inaweza kumhusisha waziri anayependa makuu akikosa mkutano muhimu kwa sababu amekuwa na mahusiano na mwimbaji, na anajenga upya maisha yake baada ya kufukuzwa serikalini.
Tunachokiweka zaidi katika redio sio katika mfumo wa hadithi. Mifano huhusisha utabiri wa hali ya hewa, taarifa za masoko, taarifa za habari, mazungumzo na mihadhara, orodha, maelekezo, ushauri, sherehe, na matangazo ya serikali. Mifumo hii ya redio ni halali na pia ina dhima katika kipindi cha mkulima.
Lakini habari iliyojengwa katika hadithi ni kitu kikubwa!
Hadithi in nguvu na athari kwa sababu inamvutia msikilizaji. Inamsisimua msikilizaji kuwa hai, kutengeneza picha akilini ambazo zinafafanua hadithi ya mdomo. Na msikilizaji akiwa amevutiwa, anakumbuka hadithi na ujumbe wake, na kwa hiyo anakuwa amehamasishwa vizuri kutenda.
Kwa nini hadithi zinakuwa na nguvu sana? Sababu tatu:
1) Hadithi huteka na hushikilia umakini wa msikilizaji. Hufanya hivi kwa kutumia muundo wa kidrama: ni kuhusu watu na harakati zao. Sisi tunaangalia watu. Hatuangalii sana ukweli. Hadithi
- huvuta umakini wa msikilizaji kupitia uwasilishaji wake wa mhusika anayejali hisia za wengine.
- hushikilia na hujenga mvuto kadri mhusika anavyopambana juu ya nini cha kufanya anapokabiliana na kikwazo au tatizo.
- huleta kujiridhisha wakati mhusika anapata ufumbuzi juu ya hatua ya kuchukua kutatua tatizo.
2) Hadithi humsaidia msikilizaji kukumbuka. Hufanya hivi kwa kutumia maelezo ya kuamsha hisia kutengeneza picha za akilini – za mtu, sehemu na vitendo. (“Maelezo ya kuamsha hisia” ni maelezo ambayo huhamasisha au huvuta au “huamsha” kumbukumbu, taswira na hisia). Haya maelezo ya kuamsha hisia huvuta fikra za msikilizaji, na hicho ni muhimu katika kukumbuka. Maelezo ya kuamsha hisia huweza kutokana sauti moja tu, maneno machache kutoka kwa msimuliaji, au sauti kutoka kwa mhusika mwenyewe.
3) Kwa sababu ya hadithi, msikilizaji pia hukumbuka masuala ambayo hadithi hufafanua. Mkulima anaweza akawa anasikiliza drama ya hadithi, lakini wakati huohuo anapata habari muhimu juu ya suala muhimu. Kwa kuwavuta wasikilizaji katika jambo kupitia kushikamana kwao na haiba, mapambano, maamuzi na vitendo vya mhusika anayehisi hisia za wengine, hadithi inaweza kuwasaidia
- kuelewa na kukumbuka kiini cha suala gumu.
- kuona ni kwa jinsi gani ujumbe katika hadithi unaweza kufanya kazi katika maisha yao.
- kujenga ujasiri, moyo na nguvu ili kufanya mabadiliko.
Vitu muhimu vya kuangalia: ubora wa hadithi makini.
Hadithi inakuwa na
1) mhusika mkuu ambaye
- yupo sawa na wakulima (asiwe juu yao)
- ana haiba ambayo huvuta usikivu na ragba ya msikilizaji, ambayo msikilizaji huona inamvutia sana
- huzungumza kuhusu jinsi alivyoshughulika na tatizo alilokabiliana nalo
- huzungumza kuhusu jinsi alivyoweza kupata suluhisho juu ya tatizo
2) msimuliaji ambaye
- kwa maneno machache, hujenga taswira sahihi ya hali ambayo kwayo mkulima hujikuta akiwamo
- kwa maneno machache, huunganisha pamoja vipande mbalimbali vya sauti ya mhusika mkuu ili kuunda mpangilio na mwelekeo wa hadithi
- hufunga hadithi kwa namna ambayo huhusiana na tatizo na suluhisho
3) uonyeshaji ambao
- husisitiza ubayana na drama na hufika kwenye kiini haraka
- hutumia sauti na lugha ya ufafanuzi ili kumsisimua msikilizaji ili kujenga taswira akilini
Mfano wa hadithi (fadhila ya Bob Carty, CBC (Shirika la Utangazaji la Kanada) Redio)
MWISHO
Dondoo chache za kusimulia hadithi
Andika kauli ya jumla inayoelezea kiini cha jambo: Unapokuwa na wazo juu ya hadithi unayoitafuta na kuamua yule utakayemhoji, unda kauli ya jumla inayoeleza kiini cha jambo kwa ajili ya hadithi yako. Hii itasaidia kuweka mahojiano katika mwelekeo maalum. Utakapokuwa umaemaliza mahojiano yako, unaweza kupitia tena kauli ya jumla inayoelezea kiini cha jambo kama inavyohitajika.
Kuunda kauli ya jumla inayoelezea kiini cha jambo, tumia sentensi moja kufafanua umuhimu wa hadithi. Jiulize: “Hadithi hii inamhusu nani?” “Mhusika mkuu ni nani?” “Tatizo ni nini?” “Mhusika mkuu anafanya nini katika kujaribu kutatua tatizo?” “Matokeo yake ni nini?”
Kauli ya jumla inayoelezea kiini cha jambo ni lazima iwe na muundo: “Mtu fulani anafanya kitu fulani kwa sababu.” Katika hadithi kuhusu Benjamin kauli ya jumla inayoelezea kiini cha jambo inaweza kuwa: “Benjamin anapanda kunde pamoja na mahindi ili kurejesha mbolea ya udongo wake na kulisha familia yake.”
Tumia ala za usimulizi wa hadithi katika kipengele cha maandishi cha habari yako. Ingawa sehemu kubwa ya hadithi yako itakuwa inasimuliwa (na lazima isimuliwe) katika sauti za wahojiwa wako, lazima utengeneze mswada ulioandikwa kwa ajili ya sehemu mbalimbali za habari yako. Hii inaweza kuhusisha utangulizi wa kipindi na mahojiano, mwachano baina ya mahojiano, maswali ya mahojiano, na hitimisho.
Sehemu hizi ni vipengele muhimu sana katika haditi yako, na hutoa fursa ya kutumia ala za usimulizi wa hadithi.
Urudiaji wa kimkakati, ucheshi, mshangao, na tofauti katika ridhimu na mpangilio zote ni ala muhimu za msimuliaji wa hadithi. Unaweza kutumia ala hizi katika kipengele kifupi cha maandishi ili kuleta burudani na kuteka au kushikilia mvuto wa msikilizaji kadri hadithi inavyosonga mbele.
Kwa mfano, wasikilizaji wanaposikia ucheshi redioni, wanasitisha kile wanachofanya na kusikiliza kwa makini zaidi. Ndio hivyohivyo hutokea kwenye hisia yoyote ile – hasira, huzuni, kulia, mshangao, mshituko, n.k. hisia ni kitu ambacho siku zote hukumbukwa, kwa hiyo tumia faida ya fursa hizi kuibua hisia.
Acknowledgements
Imechangiwa na: Vijay Cuddeford, Mhariri mtendaji, Farm Radio International, katika maandishi imechangiwa na Doug Ward, Rais, Farm Radio International
Imepitiwa upya na: David Mowbray, Meneja, Mafunzo na Viwango, Farm Radio International.
Mradi umefanywa kwa msaada wa Serikali ya Kanada kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Kanada (CIDA)