Kilimo cha aina mpya ya mpunga kwa Afrika: Kampeni Shirikishi ya redio huwasaidia wakulima kuboresha maisha yao

Uzalishaji wa mazao

Ujumbe kwa mtangazaji

Save and edit this resource as a Word document.

Muhtasari kwa mtangazaji

African Radio Research initiative, au AFRRI, ulikuwa mradi wa utafiti uliofanywa na shirika la Farm radio International kwa kushirikiana na vituo 25 vya redio vya Afrika katika nchi tano, kwa msaada wa kifedha kutoka kwa Bill na Malinda Gates Foundation. Ulizinduliwa rasmi Aprili 2007. Malengo ya AFRRI yalikuwa ni kuvumbua, kutengeneza nyaraka na kuweka kwa uwazi zaidi namna ya kutumia redio katika kuboresha suala la usalama wa chakula barani Afrika. AFRRI ilikuwa asasi ya kwanza kutathimini matokeo ya kipindi cha redio cha mkulima juu ya maarifa na mbinu wazitumiazo wakulima katika kilimo.

AFRRI ilianzisha na kutumia mbinu ya Farm radio iliyoitwa “kampeni shirikishi ya redio” au PRC Ikiwa na lengo moja la ‘uboreshaji’ ulioteuliwa na kuchaguliwa na wakulima kutokana na uwezo wao uliothibitishwa kusaidia wakulima kuboresha suala la usalama wa chakula. Vipengele vilivyochaguliwa kuboreshwa, ndio ulikuwa mwelekeo wetu mkuu wa mfululizo wa vipindi vya redio vya kila wiki ambavyo vilidumu kwa muda wa miezi kadhaa.

Katika kila nchi, jumuiya mbalimbali, vituo vya redio vya umma na vyuo vya kibiashara vilitangaza vipindi vya PRC. Vipindi vilitangazwa kwa kawaida, anagalau mara moja kwa wiki katika wakati ambao wakulima wangeweza kusikiliza katika lugha zao. Walizipa umuhimu sauti za wakulima, fikra zao na kujali majibu ya wakulima.

Kwa kila PRC, jumuiya tatu zilichaguliwa kama jumuiya ya wasikilizaji maalumu na jumuiya moja ilichaguliwa kama msikilizaji wa kawaida. Wakulima katika jumuiya ya wasikilizaji maalumu walipewa fursa ya kuwa sehemu ya mradi. Walikuwa wakihojiwa redioni na kutoa majibu kwa njia ya mawasiliano ya simu na walisaidia katika kuchagua maudhui ya kipindi. Wasikilizaji wa kawaida hawakushirikishwa moja kwa moja, lakini waliweza kusikiliza matangazo.

Katika mswada ufuatayo PRC ilihamasisha ukulima wa mpunga wa NERICA. Pamoja na kwamba mswada huu ni wa kubuni na haitumii majina ya watu halisi, umejikita katika mahojiano halisi na katika programu halisi ya PRC iliyofanyika Ghana. Utautumia kama hamasa ya kufanya utafiti na kuandika mswada juu ya mada hiyohiyo katika eneo lako. Au unaweza kuandaa mswada huu katika kituoa chako, kwa kutumia waigizaji ili kuwakilisha wahojiwa. Kama utafanya hivyo, hakikisha unawaambia wasikilizaji wako mwanzoni mwa kipindi, kwamba sauti sio za wahojiwa bali ni za waigizaji.

Script

Wahusika:

  • Alhassan Baaba, afisa wa uenezi wa kilimo, katika manispaa ya Ho.
  • Frank Dzameku, Mtungaji na mratibu wa vipindi vya mkulima katika redio ya Nkomo FM.
  • Halimatu, mkulima wa kike.
  • Efo Osei, mkulima wa kiume.
  • Asigri, mkulima wa kike.
  • Banka, mwanamasoko, mfanyabiashara wa mpunga.
  • Agyyeiwaa mkulima wa kike.
  • Akua, binti wa Asigri.

MTANGAZAJI:
Habari za jioni wasikilizaji, hii ni (jina la kituo cha redio) jina langu ni (jina la mtangazaji) mtangazaji wenu wa (jina la kipindi), mtasikiliza igizo linalohusu wanajamii walionufaika kutokana na kampeni ya redio juu ya uzalishaji wa mpunga wa NERICA.

Muziki unaingilia kati kwa muda wa dakika moja hivi

HALIMATU:
Agoo, agoo. (Maelezo ya mhariri: inamaana kubisha hodi katika lugha ya Akan) Nani yupo? Kuna mtu yeyote humu ndani? (Sauti ya mlango ukifunguka) ni wewe Akua? Mama yako yuko wapi?
AKUA:
Ameenda kwenye kikao shuleni.
BI HALIMATU:
Atakaporudi, mwambie nilikuwa hapa (sauti za kutembea kwa miguu na majibizano) oh, Yule anakuja. Habari za asubuhi? Habari rafiki yangu? Ni muda mrefu tangu tuonane.
BI ASIGRI:
Oh, mimi sijambo na ninapatikana! Nilitoka kidogo nyumbani kwenda kwenye kikao cha wazazi na walimu shuleni. Lakini wamesema kikao kimeahirishwa mpaka siku nyingine. Nini kimekuleta hapa asubuhi hii?
Kaa chini; tuzungumze, Vipi hali ya watoto na mume wako?
BI HALIMATU:
Oh, hawajambo, nimepitia hapa mara moja ili tuongee juu ya kitu fulani. Nilikuwa nikisikiliza Nkomo FM usiku wa kuamkia jana, katika kipindi chao mkulima, nilisikia kuhusu aina mpya ya mpunga unaoweza kulimwa katika maeneo ya uwanda wa juu. Pia unaweza kupandwa kwa kuchanganywa na mazao mengine na unakua vizuri hata mbali na vyanzo vya maji. Nilipiga simu kituo cha redio ili kupata taarifa zaidi, na waliniambia kuwa wewe na mume wako mmekuwa mkilima aina hiyo. Hivyo nimekuja kupata taarifa zaidi kuhusu aina hiyo ya mpunga.
BI ASIGRI:
Oh, ni kweli nimekuwa nikilima mpunga huo kwa muda fulani sasa.
Niliusikia kwa afisa uenezi wa kilimo. Alitutembelea nyumbani na kutupatia mbegu za kufaa kwa majaribio. Tulifanyia majaribio katika shamba letu jipya na matokeo yake mpunga huo hukua ukiwa umechanganyika na mazao mengine, kama alivyosema, mihogo, mahindi, migomba, magimbi, mazao yote haya hukua vizuri yanapochanganywa na mpunga huu. Unaitwa mpunga wa NERICA. Rafiki yangu unajua, mpunga wetu wa asili unaweza kulimwa katika maeneo yenye majimaji. Lakini unaweza kulima aina hii ya mpunga mahali popote. Afisa alisema unaitwa mpunga wa nyanda za juu kwa sababu unaweza kukua vizuri mahali popote katika mashamba yetu.
BI HALIMATU:
Sawa kwa hiyo, hii ndio aina waliyokuwa wakiiongelea katika kipindi.
Nilimsikia Afisa uenezi akizungumza kwenye redio kuhusu baadhi yafaida zake. Lakini rafiki yangu ngoja mimi niende sasa, nitakuja jioni kwa taarifa zaidi.
BI ASIGRI:
Sawa, lakini unadhani kuwa tunatakiwa kupata taarifa zaidi kutoka kwa Afisa uenezi? Au tungeenda kwenye kituo cha redio au kwa bwana kilimo. Sawa, ngoja mimi niende, tafadhali nifikishie salamu zangu kwa mumeo na watoto.
BI HALIMATU:
Sawa, hilo ni wazo zuri. Nitakuona jioni.

Sauti za kufungua na kufunga mlango

Mziki unaingilia kati kwa muda wa dakika tano hivi

BI HALIMATU
Habari za jioni rafiki yangu mpendwa?
BI ASIGRI:
Ni nzuri rafiki yangu, vipi wewe hujambo?
BI HALIMATU:
Mimi sijambo. Kama tulivyoongea asubuhi, nimekuja ili kuamua tuwasiliane na nani ili kupata taarifa zaidi juu ya mpunga huo wa NERICA.
BI ASIGRI:
Sawa, rafiki yangu, mimi nadhani itakuwa vyema zaidi kama tukimuona afisa uenezi kwanza aliyeanzisha wazo hilo. Anaishi jirani na soko la zamani. Anaitwa Alhassan.
BI HALIMATU:
Sawa rafiki yangu twende basi.

Suti za kufungua na kufunga milango na watu wanatoka nje

Muziki unaingilia kati kwa muda wa sekunde 10

BI ASIGRI:
Agoo, nani yupo hapa?
ALHASSAN BAABA:
Karibu ndani – o!

Oh, Mama Halimatu, woezor! (Maelezo ya Mhariri: “woezor” ina maana ya “Karibu” kwa lugha ya Ewe, lugha kuu katika Mkoa wa Volta nchini Ghana) natumaini kila kitu kiko sawa. Habari za nyumbani? Mmenishitukiza sana, kuja kwangu wakati huu na rafiki yako. Mimi kwanza ndio nafika kutoka shambani. Tafadhali kaeni chini ili tuzungumze. Nini kimewaleta hapa jioni hii? Karibuni sana!

BI ASIGRI NA HALIMATU:
Asante.
BI ASIGRI:
Sawa, huyu ni rafiki yangu Halimatu. Alikuja kwangu asubuhi ili kuelewa zaidi kuhusu mpunga wa NERICA. Nikaona kuwa ni vyema tukaja kukuona wewe kwa sababu wewe ndio ulinipatia hizo mbegu kiasi za kupanda. Aliniambia kuwa amesikia kuhusu aina ya mpunga wa NERICA katika redio ya Nkomo FM wakati wa kipindi chao cha mwisho cha kilimo. Na ana shauku kubwa ya kupata taarifa za kina juu ya huo mpunga.
ALHASSAN BAABA:
Oh sawa, ni vyema. Nilikuwa kwenye kituo cha redio walipokuwa wakifanya hicho kipindi.
BI HALIMATU:
Oh, we ndiye ulikuwa afisa uenezi pale?
ALHASSAN BAABA:
Ndiyo, nilikuwa mimi. Wizara ya chakula na kilimo inahamasisha uzalishaji wa NERICA kama sehemu ya juhudi za kuboresha ubora wa mpunga unaozalishwa ndani ya eneo hili.
BI HALIMATU:
Kwa hiyo Nkomo FM inahamasisha aina hiyo ya mpunga ?
ALHASSAN BAABA:
Ndiyo ninaiwakilisha wizara ya chakula na kilimo katika huo mradi wao. Mradi unaitwa African Farm Radio Research Initiative, au AFRRI. Nkomo FM hutangaza vipindi vya mpunga wa NERICA kwa wakulima wadogo wadogo katika maeneo yao wanayosikilizia. Hutangaza hicho kipindi kila jumatano saa 2 usiku na kurudia saa 11 jioni siku za jumapili. Kama unahitaji taarifa zaidi, ninakusihi uwasiliane na mratibu wa mradi, Frank Dzameku. Tafadhali njoo unione baadaye ili tuweze kutembelea kituo cha redio pamoja.
BI HALIMATU:
Sawa, Efo Alhassan, asante sana. (Maelezo ya mhariri: “efo” inamaanisha “mzee”)

Muziki unaingilia kati kwa sekunde 10

Sauti za salamu na redio zikisika kwa mbali

WATU WATATU
Habari za jioni bwana Dzameku!
FRANK DZAMEKU:
Ni nzuri! Habari zenu?
WATU WATATU:
Sisi hatujambo.
LHASSAN BAABA:
Tumekuja hapa ili kupata taarifa zaidi kuhusu mradi wa mpunga wa NERICA.
FRANK DZAMEKU:
Oh Alhassan, lakini wewe ndiye kiongozi wa mkoa wa mradi wa mpunga wa NERICA.

Sauti za vicheko

BI ASIGRI:
Tafadhali, Bwana Dzameku, rafiki yangu tunahitaji taarifa zaidi juu ya mpunga wa NERICA. Tumetaarifiwa kuwa ulikuwa ukijishughulisha na mradi wa mpunga wa NERICA kwa wakulima wadogo wadogo. Ulianzaje anzaje?
FRANK DZAMEKU:
Mpunga wa NERICA ulikuwa ukihamasishwa kama sehemu ya mradi ulioitwa The African Farm Radio Initiative, ulioanzishwa mwaka 2007 na Farm Radio International na baadhi ya vituo vya redio vilivyopo Afrika. Haukupita muda mrefu, kituo cha Nkomo FM kikahusishwa.
Lengo kuu la kampeni ya ushirikishaji wa Redio ilikuwa ni kuanzisha aina mpya ya mpunga Afrika unaoitwa NERICA. Ulichaguliwa kwa sababu mpunga ni mojawapo ya zao kuu katika mkoa huu. Mpunga wa NERICA unaweza kukua mahali popote pale katika maeneo haya. Hutoa mavuno mazuri na kukua kwa muda mfupi tu. Mpunga wa NERICA ni stahimilivu kwa ukame na magonjwa. Huitwa mpunga wa uwanda wa juu kwa sababu unaweza kukua mahali popote shambani. Pia unaweza kupandwa kwa kuchanganywa na mazao mengine.
Ni vizuri kulima mpunga wa NERICA katika mkoa huu kwa sababu kuna hali ya hewa nzuri inayowezesha zao hili kukua vizuri. Kuna upatikanaji wa ardhi, msaada kutoka kwa maafisa waenezaji, na hali ya hewa nzuri ya kukaushia baada ya mavuno. Pia kuna soko la uhakika.
BI HALIMATU:
Ndiyo nimekuwa nikiwasikia watu wengi wakiongelea juu ya NERICA kuwa ni aina ya mpunga mtamu. Wakulima wanahusishwaje katika mradi huo?
FRANK DZAMEKU:
Kampeni shirikishi ya redio ya AFRRI katika kile tunachokiita “uboreshaji” kwa maneno mengine ililenga katika utendaji mzuri unaoweza kutumiwa na wakulima. Kwa mfano, wanaweza kulenga katika mazao mapya na ya aina tofauti tofauti, namna nzuri za kutumia udongo, namna ya kuzuia upotevu wa mazao baada ya kuvuna, au namna za kutafuta soko la mazao hayo.
Baada ya kuchagua NERICA kama zao la kuboreshwa, AFRRI ilitusaidia kufanya utafiti. Tulikusanya taarifa za kimaarifa, mtazamo, na utendaji wa wakulima juu ya zao la NERICA.
Tulitumia kila namna ya ushirikishaji katika program hii. Tulishughulika na jamii tatu zilizoitwa “jamii za wasikilizaji hai” ambapo tuliwahusisha wanajamii moja kwa moja, timu ya uenezaji na wafanyakazi wengine wa mradi katika mchakato mzima wa mpango wa program. Jamii hizi zilikuwa Yamfo, Susuanso, na Afrispa.
Tulihusisha hizi jamii ili tuweze kubaini kama kungekuwa na mabadiliko yoyote baada ya jamii hizo kusikiliza vipindi hivyo redioni. Jamii za wasikilizaji hai walitoa mrejesho wakati wote wa muda wa kipindi. Sauti zao zilisikika kwenye kipindi, na wakati mwingine sauti zao zilitumika kama kiashirio cha kipindi.
BI HALIMATU:
Kama ulifanya haya yote inaonekana kipindi kilikuwa kimepangiliwa kwa umakini sana.
FRANK DZAMEKU:
Ni kweli. Mimi binafsi nilijifunza zaidi juu ya umuhimu wa kupangilia kipindi kwa ushirikiano wa karibu na wasikilizaji, na hasa wakulima. Kama wakulima wakijiona wenyewe kuwa wa muhimu katika vyombo vya habari na kushiriki ipasavyo katika kupangilia vipindi, watasikiliza na kuitikia ujumbe.
BI ASIGRI:
Nimelima mpunga wa NERICA, Lakini nilipata mbegu kutoka kwa Efo Alhassan, ambaye tuko naye hapa. Na nimekuwa nikisikiliza hicho kipindi kwa muda fulani sasa. Hiyo kampeni ya redio ilichukua muda gani?
FRANK DZAMEKU:
Kipindi kilitangazwa kwa muda wa miezi mitano. Kituo kilitangaza kipindi kwa lugha ya wakulima kwa muda ambao wangeweza kusikiliza. Tulijikita zaidi katika mpunga wa NERICA.
Kipindi kiliendeshwa na mtangazaji aliyeielewa hali ya wakulima na alipendwa na wakulima. Tulifanya mahojiano tukiwa studioni na mashambani. Pia tuliwasiliana na wakulima na wafanyakazi wa uenezaji kwa njia ya simu. Waliwaeleza wasikilizaji uzoefu wao juu ya NERICA. Pia kulikuwa na mawasiliano ya simu ambapo wakulima waliweza kuchangia mawazo yao juu ya matukio muhimu katika kilimo cha mpunga wa NERICA. Wakati mwingine wasikilizaji wa kudumu walizawadiwa kuchagua muziki kwa ajili ya wapendwa wao.
BI HALIMATU:
Kama wakulima walikuwa wakizawadiwa, kweli uliwapatia fursa ya kuzifanya sauti zao zisikike! Kuna yeyote kati yao alikwambia uzoefu wao na changamoto juu ya mradi?
FRANK DZAMEKU:
Ndiyo, walituambia baadaye kuwa mazao yao yaliongezeka Walivutiwa sana na kipindi. Lakini uanzishwaji wa NERICA ulidhihirisha baadhi ya changamoto. Kwanza kabisa, mtazamo wa awali wa wakulima juu ya kuanzishwa kwa aina mpya ya mpunga wa NERICA, kwa kiasi fulani ilionekana kuwa na uwalakini. Hii ni kwa sababu wakati wizara ya kilimo ilipokuwa ikihamasisha kilimo cha NERICA, Maafisa uenezaji hawakuwatembelea wakulima kwa wakati kuwaelezea ushiriki wao. Pili; wakulima walizoea kulima mpunga katika maeneo yenye majimaji kwa miaka mingi. Hivyo ilikuwa vigumu kwao kuhamia kilimo cha aina mpya ya mpunga wa nyanda za juu. Hawakutaka kuendelea na kujishughulisha na aina mpya ya mpunga bila msaada madhubuti na wa mara kwa mara kutoka kwa maafisa uenezi. Kulikuwa na changamoto zingine kama upataji na utumiaji sahihi wa mbolea, kudhibiti magugu na katika uvunaji.

Sauti ya kufungua mlango na watu wanaingia ndani

ADANE NA EFO OSEI:
Habari za jioni mabibi na mabwana!

WOTE:
Ni nzuri!

FRANK DZAMEKU:
Ah Kofi, habari yako? Umemleta mtu muhimu sana hapa jioni hii. Efo Osei, muda mrefu hatujaonana. Habari yako?

KOFI ADANE NA EFO OSEI:
Hatujambo. Tunatumaini kuwa kila kitu kiko sawa.

KOFI ADANE:
Nimemleta Efo Osei hapa ili atuambie wakulima gani wanaweza kuelezea juu ya kilimo cha NERICA na kuhusu kampeni ya redio.
FRANK DZAMEKU:
Sawa. Asigri na Halimatu, tafadhari onaneni na Adane, mwendesha kipindi cha program ya kilimo kwenye studio ya Nkomo FM. Efo Osei alikuwepo pia kwenye program. Ni mkulima kutoka Susuanso, jamii iliyohusika katika mradi. Efo Osei alikuwa akilima aina nyingine ya mpunga kabla ya kuanzishwa kwa kilimo cha NERICA. Tafadhali unaweza kuwambia wasikilizaji wangu uzoefu wako juu ya zao la NERICA?
EFO OSEI:
Ni kweli. Kabla ya kusikia mradi huu kwenye redio ya Nkomo FM, ni wakulima wachache sana katika mkoa na mimi mwenyewe nikiwemo, tulikuwa na uelewa kiasi juu ya mpunga wa NERICA.
Kabla ya kampeni ya redio, wakulima hawakutaka kufikiria juu ya kulima NERICA kutokana na mtazamo hasi juu ya miradi na programu za serikali. Serikali huleta miradi, lakini wakulima wanapojihusisha nayo na baadaye kuhitaji taarifa na pembejeo kama vile mbegu na madawa, mara nyingi huwa hatujaliwi. Hivyo kabla ya mradi wa redio, Hapakuwa na mkulima yeyote aliyekuwa akilima NERICA katika eneo hili.
BI HALIMATU:
Unafikiri ni kwanini wakulima waliitikia kwa kukubali baada ya kusikia kampeni ya NERICA?
EFO OSEI:
Kwa sababu mradi wa Nkomo FM uliweka wazi aina mpya kwa kutumiaa sauti za wakulima, Maafisa uenezaji kama rafiki yangu Alhassan, maafisa masoko wanawake, na watumiaji wa mpunga wa ndani. Pia kituo kilitangaza taarifa za namna ya kulima mpunga wa NERICA. Kwa kuhusisha mbinu za uzalishaji, taarifa za baada ya mavuno na masoko.
Kwa sasa NERICA ni moja ya mazao yanayopandwa sana hapa ukifuatiwa na aina tofauti tofauti za mpunga. Kama mkulima kiongozi katika jamii yangu, ninaweza kusema kuwa asilimia 50 ya wakazi kwa sasa wanalima NERICA. Hapo mwanzo kiasi hicho kilikuwa kikubwa, mpaka asilimia 90. Lakini kwa sasa wakulima wengi wanalima mpunga uliopuliziwa madawa.
ALHASSAN BAABA:
Ni kweli, tofauti na miradi mingine ya serikali, mradi wa NERICA uligawa mbegu kwa wakulima.
Kabla ya mradi kutangazwa, hakukuwa na mkazi yeyote wa jamii ya wasikilizaji mahususi waliokuwa wamesajiliwa kwa ajili ya kupokea, au kupanda mpunga wa NERICA. Lakini baada ya kutangazwa kiasi cha asilimia 75 ya wakazi katika jamii walijisajili kununua mbegu na kulima mpunga wa NERICA. Kama asilimia 50 katika jamii za wasikilizaji wa kawaida walinunua na kulima mpunga wa NERICA. Pia watu kutoka maeneo mengine walikuja kuchukua taarifa juu ya mpunga wa NERICA au mbegu zake. Hivyo matokeo ya utangazaji yalikuwa makubwa katika maeneo ilikosikika redio ya Nkomo FM.
BI HALIMATU:
Nimevutiwa sana. Nadhani tunaweza kuendelea kutumia redio kubadilisha mitazamo na kuboresha maisha ya wakulima.
KOFI ADANE:
Ndiyo, kipindi hiki kilikuwa miongoni mwa miradi iliyofanikiwa iliyowahi kufanywa na Nkomo FM. Nilichukua kumbukumbu katika soko, ambapo niliongea na baadhi ya maafisa masoko wanawake kuhusu mpunga wa NERICA. Unaweza kusikiliza mahojiano yangu na Bi Banka, bibi masoko na mfanyabiashara wa mpunga. Nina rekodi yake hapa. Nilimuuliza endapo mpunga wa NERICA unauzika vizuri sokoni. Hebu tusikilize.

Pumziko fupi kabla ya sauti iliyorekodiwa

Kipengele cha sauti iliyorekodiwa ya Bi Banka:
Ndio mpunga wa NERICA unauzika vizuri. Watu wengi hununua NERICA ama kwa mara ya kwanza au kama wanunuzi wa mara kwa mara. Uuzaji wa NERICA kwa kweli uliongezeka. Niliuza takribani magunia 30 kwa mwezi ukilinganisha na wastani wa magunia 3 kwa kipindi cha nyuma. Kwa ujumla faida ya mpunga wa aina tofauti tofauti nchini iliongezeka. Mara nyingi watu huulizia mpunga unaozalishwa ndani ya nchi na mara nyingi tulisema ni mpunga wa NERICA. Kumekuwa na hitaji maalumu la mpunga wa NERICA na watu wengi, wengi zaidi wanatumia mpunga huo. (Mwisho wa kusikika kwa sauti iliyorekodiwa)
FRANK DZAMEKU:
Nimepokea maoni kama hayohayo kutoka kwa wakulima, Maafisa masoko wanawake, na jumuiya kwa ujumla kwa njia ya simu-kutoka kwa jamii husika, barua, na simu kutoka nje ya jamii ya wasikilizaji hai na jamii nyingine. Nina rekodi ya sauti iliyorekodiwa ya bi Agyeiwaa, mwanamke mkulima kutoka Yamfo. Aliongelea juu ya program hiyo na uzoefu wake.

Pumziko fupi kabla yan sauti iliyorekodiwa

Kipengele cha sauti iliyorekodiwa ya Bi Agyeiwaa:
Siku moja nilisikia tangazo na kuvutiwa nalo tokea hapo na kuendelea. Sauti yangu ilikuwa ikirekodiwa mara nyingi na kurushwa hewani ili kusikilizwa. Ilinifanya nijisikie sehemu ya mradi. Pia wanawake wakulima wengine wengi walipewa fursa hiyohiyo. Kampeni ya redio ilitusaidia kuongeza faida kubwa kutokana na kulima mpunga wa NERICA. Lakini ni vigumu kwa jamii nyingi kupata mbegu. Wakulima wengi hawakuweza kupata mbegu walizokuwa wakizisikia sana redioni kwa urahisi. Hiki kilikuwa kikwazo kwetu. (Mwisho wa kusikika kwa sauti iliyorekodiwa)
FRANK DZAMEKU:
Mabibi na mabwana, hiyo ilikuwa sauti ya Bi Agyeiwaa. Binafsi nimeelewa baadhi ya changamoto alizokumbana nazo. Wakulima wengi walikuja kituoni kwetu kununua mbegu na pembejeo nyingine. Tuliona kuwa kushindwa kutoa utaratibu mzuri wa ugawaji ulisababisha wakulima kuhisi kukata tamaa au kutokuwa na imani na mradi na kituo chetu cha redio. Lakini kiasi kikubwa cha changamoto hizi ndogo kilitatuliwa na kituo chetu kwa kushirikiana na wizara ya kilimo. Mradi ulitufundisha masomo tutakayoyatumia katika miradi kama hiyo kwa kipindi kijacho.

Kufifia kwa majadiliano kati ya Frank Dzameku na wahusika wengine, na kufifia kwa sauti ya redio) kisha anasikika mtangazaji.

MTANGAZAJI:
Wasikilizaji tumekuwa tukizungumzia kampeni ya redio juu ya mpunga wa NERICA, au aina mpya ya mpunga kwa Afrika. Nkomo FM hutangaza kampeni shirikishi ya redio kuhusu NERICA iliyohusisha wakulima kupanga na kutangaza mradi huo. Mwishoni mwa kampeni wakulima wengi waliamua kulima mpunga wa NERICA. Sawa, hayo ndiyo yaliyojadiliwa kwa leo. Mpaka tutakapoonana wakati mwingine, Kwa sasa nawaaga. Jina langu ni (jina la mtangazaji).

Mziki unasikika

Acknowledgements

Kimechangiwa na: Kwabena Agyei, Meneja wa spectacle Media Consult, Techiman, Ghana
Mswada huu ni tabaruku kwa Bwana Koku Asuo Dzigbordi, ambaye alikuwa Afisa Uenezaji aliyehusishwa kwenye mradi na alifariki mwaka 2011.
Imepitiwa upya na: Benjamin Kudjoe Fiafor, Meneja wa Eneo, Farm Radio International.

Information sources

• Anane Gbadago, Mratibu wa AFFRI, mtayarishaji / msimamizi wa kipindi cha mkulima cha Volta Star Radio, Ho, Oktoba 20, 2011
• Kofi Nkrabea, msimamizi wa kipindi cha mkulima cha Volta Star, Oktoba 20, 2011
• Jonny Dumahasi Wodui, afisa uenezaji kilimo wa manispaa ya Ho, Novemba 21, 2011
• EFO Dovlo Asabi, mkulima wa kiume, Pampawie, Novemba 21, 2011
• Maria Djanmah, mkulima wa kike, Novemba 21, 2011
• Dina Boateng, bibi masoko, muuza mchele, Oktoba 20, 2011
• Lande Dake, mkulima wa kike, Hlefi, Novemba 21, 2011

gac-logoMradi umefanywa kwa msaada wa Serikali ya Kanada kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Kanada (CIDA)