Mazao yenye ubora wa hali ya juu yanainua kipato na kupunguza umaskini

Shughuli za baada ya mavunoUzalishaji wa mazao

Ujumbe kwa mtangazaji

Ukulima wa mazao yenye ubora ni jambo linaloendelea kuwa la muhimu kwa wakulima wanaotaka kuuza bidhaa zao katika maeneo yao kitaifa na kimataifa na hasa katika soko la kimataifa. Ubora wa bidhaa ni jambo la muhimu katika kupata bei nzuri ya mazao.

Ubora wa chakula huanzia tangu pale kinapolimwa na kuandaliwa kwa uangalifu mkubwa katika hatua zake zote za usindikaji. Uangalifu huu unajumuisha aina ya vitu anavyotumia mkulima kukuzia mazao yake, hatua zinazotakiwa kuchukuliwa wakati wa uvunaji, uhifadhi hasa kwa mazao yanayosafirishwa nje ya nchi na ni jinsi gani mazao hayo yanafungashwa na kusafirishwa.

Wakulima binafsi wanahitaji msaada ili wazalishe bidhaa zenye ubora. Moja kati ya njia wanazoweza kutumika ili kupata msaada huo ni kupitia jumuiya za wakulima na ushirika wa masoko. Jumuiya hizi zinatakiwa kuwa karibu na kufuatilia mahitaji ya soko, ikiwa ni pamoja na bei mpya za mazao na mahali ambapo kuna soko zuri.

Ufuatao ni muswada wa mkulima bora wa pilipili hoho zilizoongezewa virutubisho nchini Zambia, Bibi. Nancy Kondolo. Kutokana na kisa chake, umoja wa kitaifa wa wakulima nchini Zambia ulitoa mafunzo na taarifa zilizomsaidia kuweza kufikia viwango vinavyotakiwa vya kusafirisha pilipili hoho barani Ulaya.

Watangazaji wanaweza kuwasaidia wakulima wadogo kupanda mazao yenye ubora kwa kutangaza habari zenye mafanikio za ukulima kama hizi. Wanaweza pia wakawafanyia mahojiano wawakilishi wa wakulima kutoka katika vyama vya ushirika vya wakulima ambavyo vimefanya vizuri katika eneo lao, na kuwauliza maswali je ni mazao gani yanayoweza kuwa na soko zuri zaidi la ndani na nje ya nchi?

Muswada huu ni kuhusiana na mahojiano ya kweli. Unaweza kutumia muswada huu kukuhamasisha kufanya utafiti katika eneo lako kutokana na mada inayofanana na hii. Au unaweza kuutumia muswada huu katika kituo chako cha redio, kwa kutumia sauti za waigizaji kuwawakilisha wazungumzaji katika muswada. Endapo utaamua kufanya hivyo, tafadhali wafahamishe wasikilizaji mwanzo wa kipindi kuwa sauti zinazosikika ni za waigizaji na wala sio wahusika halisi.

Script

Ingiza kiashirio cha kipindi na punguza sauti, mruhusu mtangazaji aanze kipindi

Mtangazaji:
Hujambo? Karibu katika kipindi cha leo kisemacho Sauti ya mkulima, kinacholetwa kwako kwa ridhaa ya Umoja wa wakulima nchini Zambia. Mimi ni mtangazaji wako, Alice Lungu Banda. Tuwe sote.

Ondoa taratibu kiashirio cha kipindi

Mtangazaji:
Wakulima nchini Zambia wamefanikiwa kulima kilimo mchanganyiko na kujipatia mavuno makubwa katika juhudi zao za kupambana na umaskini. Hata hivyo bado wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kuuza bidhaa zao!

Ni furaha ilioje kujua kuwa kuna habari njema: wakulima wote wanaweza kuzalisha mazao yenye virutubisho vingi. Na mazao yenye virutubisho vingi yanamfungulia mlango mkulima katika masoko ya kimataifa.

Wakulima! Ngoja niwakumbushe kuwa, jambo la muhimu ni kile mteja anachotaka sokoni na wala sio kile muuzaji anachouza. Mafanikio katika soko lenye ushindani yanategemea udhibiti wa mazao bora tangu upandaji hadi wakati wa kuvuna. Kwa mfano pilipili hoho zilizolimwa kwa kuongezewa virutubisho zinaweza kumuongezea fedha nyingi mkulima katika soko la ndani na nje ya nchi na kumsaidia kupambana na umaskini.

Katika kipindi chetu cha leo tunaye Bibi. Nancy Kondolo, mwenye umri wa miaka 59-ambaye ni mkulima kutoka kijiji cha Mwanamwemba kilichoko katika jimbo la Kusini mwa Zambia. Bibi Kondolo analima pilipili hoho kama zao la biashara na kuliuza katika soko la ndani na kimataifa. Ungana nami, ninapokuwa nikizungumza naye.

Alice:
Habari za asubuhi Bibi. Kondolo. Ni lini ulipoanza kulima pilipili hoho?

Bibi Kondolo:
Nilianza kuwa mkulima wa pilipili hoho mwaka 1997 mara baada ya kustaafu kazi serikalini kama katibu muhtasi. Nilichagua zao la pilipili hoho kwa vile nilibahatika kusafiri hadi Ulaya. Niligundua kuwa pilipili hoho na mazao mengine mengi yanayolimwa hapa Zambia yanathamani kubwa huko Ulaya na yanauzwa kama njugu.

Alice:
Una maana gani unaposema “yanauzwa kama njugu”?

Mrs. Kondolo:
Namaanisha kuwa mazao hayo yana soko zuri sana. Lakini, naomba nitoe tahadhari kwa wakulima wenzangu. Bidhaa ni lazima zizalishwe chini ya usimamizi mzuri na kufungashwa vema. Ni lazima pia ziwe na virutubisho vya hali ya juu, na zisiwe na chembechembe zozote za mbolea za kukuzia. Mwisho, ni lazima ziwe na mvuto, ili zikidhi viwango vya Ulaya.

Alice:
Unawezaje kufikia viwango vya Ulaya?

Mrs. Kondolo:
Mimi ni mwanachama wa kikundi cha Mwanamwemba, ambacho ni mwanachama wa Umoja wa taifa wa wakulima wa Zambia. Ilikuwa rahisi kwetu kufikia viwango vile, kwa sababu umoja huo ulitufundisha jinsi ya kusimamia zoezi hilo vizuri tnagu maandalizi ya shamba hadi mavuno. Umoja huo pia ulihakikisha kuwa tunauganishwa na masoko ya ndani na yale ya kimataifa.

Alice:
Unawezaje kulinganisha maisha yako ya sasa na wakati ule ulipokuwa katibu muhtasi?

Mrs. Kondolo:
Nina amani. Hivi sasa wakati wote nina pesa mfukoni na ninaweza kuwasaidia watoto wangu wanaosoma. Nawasaidia wanafamilia wengine kijijini kwetu wakati wowote wanapohitaji msaada.

Alice:
Ni hekari ngapi za ardhi unazomiliki? Je unalima mazao mengine?

Mrs. Kondolo:
Nina hekari 60 za ardhi. Kwa sababu ninajua kuwa mazao mchanganyiko ni muhimu, basi huwa ninalima mahindi, soya, karanga na alizeti.

Alice:
Ni njia gani za kilimo unazotumia na ni kwa muda gani umekuwa ukitumia njia hizo?

Mrs. Kondolo:
Ni muda mrefu uliopita, nilikuwa nikitumia mtindo wa kizamani wa kilimo na sikupata mavuno mazuri. Lakini, kutokana na Umoja wa kitaifa wa wakulima wa Zambia, hivi sasa natumia kilimo cha uhifadhi, kilimo cha kuongeza virutubisho na mazao mzunguko. Sipendi utaratibu wa kutumia kemikali.

Alice:
Kwa nini?

Mrs. Kondolo:
Sitaki thamani ya ardhi yangu ishuke kiwango. Na umoja wa Ulaya, ambako ndio nalenga kupeleka mazao yangu, unataka bidhaa zenye virutubisho vya hali ya juu. Nimetambua kuwa kilimo ni biashara na ni lazima nikidhi mahitaji ya wateja wangu ili niweze kuendelea kubaki kwenye biashara.

Alice:
Asante kwa kuzungumza nasi kupitia Sauti ya mkulima. Natumai utapata wasaa wa kuzungumza nasi wakati mwingine.

Mrs Kondolo:
Asante, unakaribishwa tena wakati mwingine.

Presenter:
Asanteni wakulima na wasikilizaji wengine, kwa kutenga muda wenu, licha ya shughuli nyingi mlizonazo kusikiliza Sauti ya mkulima. Tafadhali tuwe sote wiki ijayo, muda kama huu. Shukrani za dhati zimwendee msimamizi wa kipindi, Annie Sampa. Mimi ni Alice Lungu Banda nakutakia siku njema yenye uzalishaji wa kutosha.

Cheza kiashirio cha kumaliza kipindi

Acknowledgements

Mshiriki: Alice Lungu Banda.

Msimamizi: Umoja wa taifa wa wakulima nchini Zambia.
Mkulima: Bibi. Nancy Kondolo. Mwanamwemba Village, Farm no. 1977/M, Mazabuka, Zambia.

Mtangazaji: Shirika la habari la Palesa, P.O.Box 314 FW, Lusaka.

Mtangazaji na muuliza maswali: Alice Lungu Banda.
Muswada huu ni marekebisho ya kipindi kilichotangazwa tarehe 15th mwezi Oktoba, mwaka 2005 na shirika la Utangazaji la Zambia (ZNBC) saa 7.30 mchana.